"Mwanangu cha muhimu ni kumuomba
Mungu tu, nakuombea sana; halafu father Filbert alikuwa anakuulizia, na yeye
amewekwa karantini hapohapo airport nimempa namba zako anasema atakufuata ulipo
kesho," alisema baba yake Neema, loh!
"sawa, lakini sidhani kama
ataruhusiwa kuniona, mimi nipo huku geti jingine maana nimetokea Italia, yeye
si ametokea ufaransa?" alisema Neema akipanga uongo mtakatifu maana
alishajua kama huyo Father Filbert atagundua kuwa hayupo airport atamwambia
baba yake.
"Ndiyo mwanangu, ametokea ufaransa,
aya sawa, hakikisha unakaa mbali na watu wenye mafua mwanangu," alisema
Mzee wake Neema; akimlinda mno mwananaye maana yeye ndiye baba na mama kwa
Neema tangu mke wake afariki kwenye ajali ya moto, wakati huo Neema akiwa
kichanga.
Neema mwenyewe aliishiaga kutazama picha
tu za mama yake enzi zake, watu wakamuona na kumwambia amefanana mno na mama
yake na hilo lilimpa simanzi mno.
"wewe ulipona tu kimiujiza, ndiyo
maana nilitaka umtumikie Mungu maisha yako yote kama mtawa," ilikuwa ni
kauli ya baba yake Neema miaka mingi iliyopita na alifurahia kuiona imetimia
kwa Neema kurudi akiwa amepitia hatua ya mwisho kabisa ya kuwa mtawa na
angelikuwa ameishaanza kazi yake huko Roma kama si Corona.
***
Father Filbert pamoja na kuwa padri wa
muda mrefu mkoani Arusha, alikuwa na historia ndefu na familia ya kina Neema.
Tangu ajali ya moto iikute familia hii amekuwa akitoa msaada wa hali na mali
kwao.
Alikuwa kama baba wa pili wa Neema,
alimlea kiimani na kumsaidia baba yake aliyekuwa amekwisha kata tamaa kurudi
kwenye mstari wa matumiani mapya ya maisha katika Kristu.
kwa macho ya kidunia unaweza kusema bila
huyu Father FIlbert, baba yake Neema asingekuwa mtu wa dini kupitiliza, wala
Neema asingekuwa mtawa kilazima. Maana alichungwa, akafungwa na hata bakora
alichapwa ili mradi asiwe kama wasichana wengine wa umri wake bali mtumishi wa
bwana.
Ilikuwa ni mateso na safari ya miiba kwa
Neema na ndiyo iliyomfanya hata kwenye ukubwa wa umri wake wa miaka 26 alionao,
aendelee kumuogopa mno baba yake, lakini zaidi Father Filbert.
Sasa akatulia chumbani mwake akisikilizia
simu yake na cha kudanganya kwa father FIlbert ikiwa tu atamtaka amuelekeze
alipo, na kama tu atakua amekosea kuwa huenda huko karantini ya airport watu
hutembeleana na siyo kutengwa vyumbani kama hapo hotelini.
Loh akakumbuka jambo, TAARIFA ZA HABARI!
Kwanini hakuwaza hili muda mrefu kabla? Ni kweli ili kujua yote hayo lazima
asome habari na kusikiliza hali ya ugonjwa huu wa corona unaendeleaje duniani;
basi akawasha televisheni ya hoteli, akawasha redio kwenye simu yake ya kitochi
akaweka laudispika kisha akafungua smartphone yake na kuanza kugoogle.
TANZANIA YARIPOTI KISA CHA SITA CHA
CORONA, akasoma vizuri habari ile na kugundua visa vinne vya wagonjwa wa corona
ikiwa ndani ya hoteli aliyofikia, huku viwili vikiwa ni Zanzibar na Dar.
Macho yake yakashuka kwenye kichwa cha
habari kilichoandikwa; "WATANZANIA KUJIGHARAMIA WENYEWE KARANTINI"
habari ya pili ikawa "HOTELI ARUSHA KUWA KARANTINI YA CORONA, KANDA YA
KASKAZINI" loh akaingia kusoma habari hii kwa undani akagundua ni hoteli
yao hii ndiyo aliyochaguliwa kurundikwa washukiwa wote wa ugonjwa wa Corona
kuanzia kesho maana yake wasafiri wote wa kanda ya kaskazini wataletwa hapo
hotelini.
Hii sasa ilikuwa na maana mbaya na nzuri,
mbaya ni kwamba Father Filbert naye ataletwa hapo hotelini na kuharibu mipango
yote ya yeye na Cliff; nzuri ni kwamba; ile ya yeye kukutwa hotelini haitakuwa
skendo tena maana, hoteli sasa imefanywa karantini na hata father Gilbert
atakuwepo, yeye ni nani basi hata aogope.
Lakini ndani kabisa ya moyo wake Neema
akawa na hofu kuu zaidi iliyoletwa taswira ya ujio wa Father Gilbert hapo
hotelini alipokuwa. je, ni hofu ipi hiyo nyingine?! mimi na wewe hatuijui;
tusonge.
Mnamo saa sita za usiku, simu ya Neema
iliita namba hii ndiyo aliyokuwa akiisubiria mno na kuitarajia; japo ilikuwa ni
namba ngeni lakini muito wake ulimchezesha machale kuwa huyo si mwingine bali
ni Father Gilbert.
"Tumsifu Yesu Kristu,"ilikuwa
sauti ya nzito ya mwanaume umri sawa na ya baba yake, ilikuwa ni miaka kadhaa
imepita lakini sauti ya Father Gilbert haikubadilika hata kidogo.
"Milele amina," aliitikia Neema
akijifanya anasikilizia huyo mtu wa upande mwingine ajitambulishe kwanza
ingawaje alimfahamu fika.
"Unaongea na Father Gilbert
hapa,"
"Aagh Father,shikamoo; za
masiku,"
"marhaba tu, mwanangu, niliongea na
baba jana akaniambia na wewe upo karantini hapa airport,na mimi nipo hapa mbona
sijakuona!"
"nipo Father, watu ni wengi kidogo
ila natumai nitakuona kesho tu asubuhi!"
"Watu ni wengi? mbona tupo kumi na
mbili tu!" alisema Father Gilbert.
"halloow! haloow .. Father sikusikii
vizuri," alizuga Neema na kukata simu yake.
Haraka akamtumia meseji Cliff. ikasomeka
hivi:
"Angalia habari,kesho hoteli
inageuzwa karantini ya Corona kanda ya Kaskazini. Father Gilbert naye mmoja wao
anakuja! tughairishe ule mpango kwanza."
Loh meseji hiyo ikamshtua pia Cliff,
maana naye alimfahamu vyema Father Filbert, kuwa ni mmoja kati ya madingi
waliombania kwa Neema tangu enzi zile sekondari wakati alipokuwa akimvizia
Neema mafundisho kanisani; hivyo basi ujio wa Father Gilbert ukawa pigo jingine
kwa Cliff.
Tena akakumbuka simu moja wakati Father
Gilbert na baba yake Neema walipomkamataga huko kwenye vyoo vya kanisa na
Neema; baada ya kumchapa bakora, Cliff aliondoka kwa hasira huku akisema:"
Hata mnizuie vipi, Neema nitampata tu, atakuwa wangu!"
Cliff alikumbuka maneno hayo vizuri kama
vile aliyasema jana yake tu. Akakumbuka hata sura ya Father Gilbert na baba
yake Neema ikimkemea Cliff wa enzi zile kama pepo mchafu anayetaka kukwamisha
uongofu wa mtoto wao Neema katika kuifuata njia ya bwana.
Na kama haitoshi alikuwa na uhakika hata
sababu ya Neema kupelekwa kusomea utawa huko nchi za nje ilikuwa ni yeye.Hivyo
basi,Cliff alijua lazima tu Father Gilbert akimuona atamkumbuka tu kwa sababu
walikuwa na kisasi cha wazi kabisa, japo kuwa imepita miaka takribani kumi na
moja tangu tukio lile na miaka saba na ushehe tangu waonane mara ya mwisho.
****
Basi kweli bwana asubuhi ilipofikia,
magari ya ambulance kwa msululu yalikuwa yakitiririka kuingia ndani ya hoteli
ile waliyokuwemo akina Neema na Cliff, pilika za watu zikasikika tu huko
koridoni na sehemu nyinginezo kuonesha kuwa ugeni ulikuwa ikiingia humo ndani.
Ikawa mchana ikawa jioni na hatimaye
usiku mwingine. Safari hii saa tatu kamili ilipotimu, hodi ikagongwa chumbani
kwa Neema aliyekuwa mlangoni ni Father Gilbert akiwa na meneja wa hoteli.
"mwanangu, habari yako!"
alisalimia Father Gilbert kwa tabasamu pana lakini akitunza mipaka ya mita moja
kati yao ili asisababishe Corona.
"Salama tu father, nafurahi
kukuona," aliitikia Neema kwa adabu na hofu kubwa ya kipi kifuatacho;
wakati huo Meneja akadandia.
"Father tunashukuru sista Anne hapa
amekuwa akifanya novena na maombi mazito kuombea wagonjwa wa corona. Na leo
umefika wakati muafaka,"
"Kweli sista Anne!?" alisema
kwa furaha Father Gilbert akionekana yupo tayari kujiunga na hiyo sala hata
dakika hiyohiyo.
"Sista Anne,kamanda ameenda kumleta
dereva wako, mimi kwa leo nitaomba udhuru, nyie kaendeleeni tu na
sala,"alisema Meneja akimtazama Neema, loh Neema akatamani akae chini kwa
maana mchango ulimkamata.
Ikawa basi kila hatua aliyopiga Neema
kuelekea huko kwenye chumba cha sala ilikuwa ni maumivu makubwa kwake. Akajutia
hata ujanja wake wa kujifanya anaanzisha sala kwa ajili ya kukutana kimapenzi
na Cliff, akaona wazi Mungu anamuadhibu kwa mara nyingine kwasababu kama si
Mungu ni nani mwenye nguvu ya kupangua kila wanachokuwa wakikipanga?
Dhima na tashwishwi zikawa hofu na
wasiwasi kichwani mwa Neema, mavazi yake ya usista yakawa hayamtoshi, mbele
akiwa meneja wa hoteli na pembeni yake akiwa Father Filbert aliyepiga hatua
sambamba naye kuelekea kwenye safari ya kuumbuka.
"Ee Mungu naomba mfanye Cliff asije
leo huku," alisema sista Anne ikawa ni sala yake ya mwisho kusali kwa
imani kubwa mno, tena kama sala ile angeliuomba mlima uhame basi hakika andiko
la Nabii Issa lingetimilika katika karne hii ya kizazi cha nyoka, majoka na
manyoka.
Loh chumba kilikuwa kitupu na kamanda
alifika na ujumbe kuwa hali ya dereva si nzuri jioni hiyo, hivyo pia alikuwa na
udhuru ya kutofika ibadani. Kauli hiyo ikawa imemsuuza moyo Neema, akajifuta
kijasho cha hofu kilichokuwa kikimtiririka usoni mwake.
Kwa mara ya kwanza akamshukuru Mungu
kumnusuru maana yajayo yangefurahisha. Akamtazama kamanda na meneja waliokuwa
wakijifanya kutaka kuondoka akasema: "Basi kwakuwa tupo wachache leo
sidhani kama kuna kitu cha muhimu kuliko kumuomba Mungu, naomba kwa dakika kumi
na tano tu tujitolee kwake kuwaombea ndugu zetu wanaopata tabu duniani na
akhera."
"Oh sawa kama ni dakika kumi na
tano, tafadhali tuanze," alisema Kamanda akikazia dakika kumi na tano huku
suraye ikawa surambi maana alikumbuka sana jaramba la jana yake kwa kupigishwa
sala kwa masaa mawili taslimu na hakutaka tena litokee.tena ukute hapo walikaa
kitako kabisa na meneja kuwa wasingethubutu tena kusogelea sala za sista Neema,
wangemuachia yeye na dereva wake.sasa vuta picha Cliff angevyojinoma.
Basi bwana, Sista Anne akapata nguvu
akasalisha kwa ustadi mkubwa siku hiyo mbele ya Father Filbert,hata dakika kumi
hazikufika,ikawa tayari sala imeisha. Kila mmoja alikuwa na nguvu na ikawa kama
vile roho mtakatifu aliwaingia maana mzuka ulikuwa umewapanda hatari.
Sasa katika kuagana kila mmoja akipanga
kurudishwa chumba chake ndipo, Father Filbert akakumbuka jambo.
"Samahani kamanda huyo mwenzetu
ambaye anaumwa, vipi ni kwema kabisa?"
"aah huyo dereva wa parokia!?"
aliuliza meneja.
"kwani ni dereva wa parokia!?"
alihamaki Father akimtazama sista Anne.
"ndiyo," alisema sista Anne
akijua kabisa anaongopea lakini akauongea uongo wake kwa kujiamini maana
alihisi angetetema tu angedabwa kama si sasa basi ni punde maana hata hicho
cheo cha udereva wa parokia alikitunga na hajui kama kipo au lah! na hapo akajiandaa
kujibu swali la; dereva wa parokia ipi.
"Aisee, tatizo ni nini?"
alisema Father Filbert akitoka kwenye mawazo ya sista Anne.
"Hatujui anaumwa nini, ila ameonesha
ana homa hivyo tumempeleka haraka kile chumba cha wagonjwa anafanyiwa vipimo
kwa uangalizi wa karibu sana, hatuwezi kuwa na uhakika zaidi ila ametengwa kwa
muda," alisema kamanda.
"kwa hiyo kama atakutwa na Corona
nini kitatokea!" aliuliza Neema.
"hapo lazima watakuchukua na wewe,
mtatengwa. na najua mimi na Kamanda hatutasalia," aliongeza kamanda
akitweta mno, lakini katika maneno hayo Neema akagundua kitu, na yeye saa
ileile akapiga chafya ya kwanza, ya pili loh! kamanda, Father na meneja
wakakimbia hali wakivaa vimaski zao mara kundi la madaktari wakambeba Neema
kumpeleka chumba alichomo Cliff.
MWISHOOOOO

0 Comments