Jumapili moja baada ya kula chakula cha usiku, baba mzazi wa kijana Abdallah ambaye wengi walipenda kukatisha jina lake na kumwita Dullah , Mzee Reli ya Uhuru akiwa ameketi sebuleni na kijana wake huyo aliyehitimu kidato cha nne, alimweleza kwamba kwa wakati ule hakuwa na fedha za kuweza kumuendeleza kielimu hivyo ajichanganye mjini kujitafutia maisha.
Wakati mzee huyo aliyepewa jina la utani la Reli ya Uhuru kufuatia kuwa mmoja wa watu waliojenga reli hiyo, akimweleza hivyo, mkewe alikuwa akimsikiliza ambapo alimuunga mkono mumewe kwani hali yao kiuchumi aliielewa vizuri.
“Dullah , ni kweli kabisa kwa hivi sasa baba yako hana fedha na unaona jinsi familia yetu ilivyo kubwa na wote tunamtegemea yeye, mimi nakubaliana na ushauri wake wa wewe kujichanganya mjini kufanya vibarua ambavyo vitakuwezesha kupata riziki yako na yetu,” mama huyo alimwambia kijana wake.
Dullah kijana ambaye tangu udogo wake ni handsome boy kiasi cha kuwavutia wasichana wengi wakiwemo watu wazima, aliposikia kauli hiyo ya wazazi wake aliinamisha kichwa na kuanza kufikiria hatima ya maisha yake ingekuwaje.
“Hivi baba, huwezi kuuza lile shamba la Kimanzichana ili fedha zitakazopatikana niweze kuendelea na masomo nitimize ndoto zangu za kuwa mhasibu?” Dullah alimwuliza baba yake.
Baba yake alimfahamisha kwamba baada ya mambo yake kuanza kumwendea kombo, aliuza nusu ya shamba hilo na nusu iliyobaki asingeweza kuiuza kwani alipanga ije iwasaidie wadogo zake ambao walikuwa wadogo.
Kwa kuwa Dullah alikuwa akielewa ukubwa wa familia yao na jinsi mzazi wake alivyokuwa akihangaika kuitunza, akawa hana jinsi zaidi ya kuingia mitaani kusaka kibarua chochote ambacho kingemuwezesha kupata fedha.
“Oke baba na mama, kwa kuwa naielewa hali halisi ya maisha yetu hapa nyumbani, nitazungumza na fundi Yassin ili niongozane naye kwenye shughuli zake za ujenzi,” Dullah aliwaambia wazazi wake.
Alipotoa kauli hiyo, baba yake licha ya kujiuliza moyoni kama kweli Dullah aliyemlea kimayai angeweza kufanya kazi ya uwashi lakini hakutaka kumuonesha wasiwasi wake, akamwambia sawa.
Baada ya mazungumzo hayo, Dullah aliwaaga wazazi wake na kwenda kwenye chumba alichokuwa akilala na wadogo zake wawili kilichokuwa uani, akawa anatafakari ugumu wa maisha uliokuwa ukiwakabili.
Chumbani kwa wazazi wake, baba na mama yake walimjadili sana kijana wao kama angeweza kufanya kazi ya ujenzi lakini baadaye walikubaliana wasubiri kuona matokeo.
Alfajiri na mapema Dullah alikwenda kumgongea fundi Yassin ambaye alikuwa fundi washi aliyekuwa akisifika sana kwa umahiri wake wa kujenga nyumba maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar.
“Niambie Dullah , naona leo umenivamia alfajiri yote hii, umekwama nini?” fundi Yassin aliyekuwa akimpa fedha Dullah siku moja moja alipokwama alimwuliza.
“Ukiacha kukwama, leo nataka tuongozane huko site unakokwenda kujenga japo nikakusaidie kazi yoyote maana mtoto wa kiume kumtegemea baba kila kitu haipendezi,” Dullah alimwambia fundi Yassin.
“Yaani Dullah na huo usharobaro wako unataka kwenda kufanya kazi ya kukoroga zege au kuranda mbao, utaweza kweli?” fundi Yassin alimwuliza.
Kufuatia kuambiwa hivyo, kijana huyo mweupe, mrefu wa wastani na mwenye vidimponsi vinavyoonekana kila akiongea au kucheka alimjibu fundi Yassin kwamba kwa kuwa alikuwa mtoto wa kiume alikuwa tayari kufanya kazi yoyote.
Licha ya Dullah kupewa ushauri wa kutafuta kazi yoyote ya kufanya, aliumia sana kufuatia bro mmoja ambaye ni mambo safi kumchukua demu wake Careen kwa vile hakuwa na hela.
Msichana huyo aliyeingizwa kwenye ulimwengu wa kimapenzi na Dullah , alikuwa akimpenda sana Dullah lakini alishindwa kudumu naye kwa sababu kila alipohitaji sapoti ya fedha kutoka kwa mpenzi wake huyo ilikuwa zii.
Kila Dullah alipokuwa akikumbuka tukio hilo la kuporwa demu wake na yule bro anayemiliki kampuni ya kutoa mizigo Bandarini aliumia sana, kwa sehemu ishu hiyo ilimfanya akubaliane na ushauri wa baba yake wa kutafuta kibarua chochote cha kufanya.
“Ila Dullah kwa jinsi ninavyokuona sijui kama utaweza kufanya kazi ngumu, kwa kuwa umeamua basi vizuri jiandae ili kesho twende pamoja,” fundi Yassin alimwambia Dullah aliyekuwa akivaa miwani sababu ya kusumbuliwa na macho kwa mbali.
“Fundi Yassin, haina haja ya kusubiri kesho, hivi unavyoniona nipo full, labda niende nikachukue nguo za kufanyia kazi, nimechoka kukaa nyumbani,” Dullah alimwambia fundi Yassin aliyeishia kucheka.
“Haya bwana, nenda kachukue nguo hizo ili nami nijiandae kisha tuanze safari, ukija nitakwambia tunakokwenda,” fundi Yassin alimwambia Dullah .
Baada ya kuambiwa hivyo, kijana huyo wa Kisukuma alikwenda kwao akachukuwa shati kuukuu, suruali ya zamani na raba ambazo hakuwa akizivaa kwa sababu zilianza kuchoka akaziweka kwenye begi.
Wakati Dullah ambaye nimeshakwambia ni handsome boy haswa akijiandaa, nyumbani kwa fundi Yassin mkewe alimwuliza alikuwa akizungumza na nani.
Fundi Yassin alimsimulia kila kitu mkewe, ambaye hakuamini kama kweli Dullah aliyekuwa akimfahamu kwa usmati wake angeweza kufanya kazi ya ujenzi aliyokuwa akiifanya mumewe.
“Yaani baba Tatu, Dullah huyu sharobaro mvaa miwani ataweza kweli kubeba zege, matofali, kuchota maji au kubeba mbao?” mkewe Yassin alimwuliza mumewe.
“Nami nimemuuliza hivyo kaniambia ataweza, wewe ngoja niende naye halafu tukirudi ndiyo nitakueleza kitakachojiri huko,” fundi Yassin alimwambia mkewe, wakacheka.
Wakati fundi Yassin akizungumza na mkewe, nyumbani kwa akina Dullah , baba yake alipomuona kijana wake kabeba begi muda ule wa alfajiri alihisi huenda alikuwa akitoroka kufuatia kumwambia aanze kujitegemea.
“Dullah mbona na begi alfajiri yote hii, unakwenda wapi?” mzee huyo alimwuliza kijana wake.
Baada mama Dullah kuchangamshwa damu asubuhi ile alimshukuru mumewe, akiwa anachekacheka aliamka na kwenda kuandaa maji ya kuoga, wakaoga pamoja kisha alimwandali kifungua kinywa.
Baba Dullah alipomaliza kunywa chai aliondoka kuelekea kwenye pilika za kutafuta riziki, akiwa njiani akawa anamtafakari Dullah aliyemweleza anakwenda kumsaidia kazi fundi Yassim.
“Kama ataweza nitasema kweli amekuwa lakini kwa jinsi ninavyomjua atakapotoka huko ataniambia hatakwenda tena,” mzee huyo aliwaza.
Dullah akiwa na begi lake alipofika nyumbani kwa fundi Yassin, alimkuta akiwa anamsubiri. Hawakupoteza muda, fundi huyo aliamuga mkewe kisha alichukuwa zana zake za kazi na kuanza safari ya kwenda site.
Kwa kuwa bado ilikuwa ni alfajiri walipofika kituo cha daladala lilifika DCM la Mwenge wakapanda, kwa bahati walikaa siti moja.
Wakiwa wanaendelea na safari fundi Yassin ambaye mpaka muda huo alikuwa aamini kama kweli Dullah aliyekuwa akimfahamu vizuri kwa kupenda mambo ya usharobaro aliamua kwenda kufanya kazi za ujenzi.
“Dullah hivi ni kweli umeamua kwa dhati kufanya kazi ngumu ninazofanya?” fundi Yassin alimwuliza .
“Fundi bwana! Sasa kama wewe unaweza mimi nitashindwaje? Mimi mtoto wa kiume bro!” Dullah alimwambia fundi Yassin aliyeishia kucheka.
Katika daladala walilopanda, kiti cha kushoto alikaa kaka mmoja upande wa dirishani na kufuatia demu mmoja mkali ambaye alfajiri hiyo alikuwa akiangalia mambo ya dunia katika simu yake ya kisasa ‘Smartphone.’
Wakati msichana huyo akiwa bize na simu yake, Dullah alikuwa akimtupia macho kwa chati na kumsifia moyoni kwamba kweli Mungu alijua kumuumba na kuishia kusema kama alikuwa ana boyfriend wake basi alikuwa akila vinono.
Hata hivyo, Dullah ambaye alikuwa akiwapenda watoto wazuri alipanga kama demu huyo atashukia Mwenge amuombe namba yake, alipanga kujaribu tu zali la mentali.
DCM walilopanda lilipofika Mwananyamala Hospitali, Yule dada mkali aliinuka moyo wa Dullah ulipiga pa kwani alijua mahesabu yake ya kuomba namba yalifeli, akajisemea moyoni; kudadeki.’
Wakati Dullah akiwa katika wakati huo mgumu, alimuona Yule kaka aliyekaa upande dirishani na yule msichana mkali akasogea dirishani, moyo wa Dullah ukajaa furaha.
“Vipi Dullah naona upo mbali, unawaza kazi za huko site nini?” fundi Yassin alimshtua Dullah ambaye mawazo yake yalikuwa kwa Yule demu.
“Hapana fundi, mambo mengi tu kichwani si unajua hali ilivyo ngumu siku hizi!” Dullah alimwambia fundi Yassin.
Kwa kuwa muda huo wa hakukuwa na jamu, kufumba na kufumbua walijikuta wamefika Makumbusho abiria wakaanza kuteremka kutoka garini, kwenye siti ya akina Dullah alianza yeye, upande wa kushoto Yule demu,
Kufuatia zana za kazi alizokuwa nazo, fundi Yassin ilibidi watu wote washuke ili asiwabughudhi, Dullah na Yule msichana wakiwa chini, kijana huyo handsome boy aliamua kumsalimia na kumsifia kwa jinsi alivyojaaliwa uzuri na alivyopendeza.
Kama ambavyo nimekuwa nisema mara kwa mara kwamba kama kuna mtu hapa duniani akisifiwa huwa hafurahi ujue ana matatizo, Yule dada alimshukuru Dullah na kuachia tabasamu pana.
“Huyu kaka nilikuwa sijamwangalia vizuri, kumbe ni handsome boy namna hii, yaani alivyotabasamu dimponsi zake zimempendeza,” yule dada akajisemea moyoni.
Kama vile Dullah alikuwa akijua alichokuwa akikiwaza yule mrembo, akajisemea moyoni kwamba ‘kama unampata mtoto mzuri kama huyu… mbona dunia utaiona tamu!’
Kwa kuwa Dullah ambaye kichwa chake kushika vitu kilikuwa kama kompyupa, fasta alimuomba yule dada amtajie namba yake ya simu, kwa kuwa Dullah hakuwa na simu yule dada akamwuliza kama angeweza kuikariri.
“Hiyo mbona kazi ndogo sana, kichwa changu kwa kukariri ndiyo chenyewe,” Dullaha akamwambi.
Haya, sifuri, Sita ,tano,nane, arobaini na mbili, arobaini…..” mtoto mzuri akataja. Dullah aliikariri nyema namba hiyo, alipomuuliza jina akamwambia akimpigia au kumtumia ujumbe atamtajia.
Wakati Dullah anamaliza kuzungumza na yule binti mkali, fundi Yassin aliwasikia akaishia kutabasamu na kujisemea moyoni kwamba; “Hawa vijana wa siku hizi wana mambo mengi, kwa muda mfupi tayari amezoeana na mrembo!”
Yule msichana akiwa kama alikuwa akisubiri kuambiwa jambo na Dullah, fundi Yassin akamwita Dullah na kumwambia auchukue ule mfuko uliokuwa na chepe na vifaa vingine vya kujengea.
Kuhofia kupata aibu ya kuonekana na yule mrembo kama alikuwa fundi washi licha ya kuonekana kijana wa kisasa, Dullah alijifanya hakumsikia na kumuaga yule mrembo.
“Poa, tutawasiliana si unajua mida ya kazi hii!” yule msichana ambaye hakuelewa chochote baina ya Dullah na fundi Yassin alimwambia Dullah ambaye naye alimjibu poa.
“Ila wewe dogo unatisha kama moto wa gesi, mara hii umempata mrembo, kweli sikuwezi,” fundi Yassin alimwambia Dullah.
“Kawaida tu bro, sisi vijana unapomuona mtoto mzuri kama yule siyo vyema kumuacha bila kumsalimia na kumsifia, si hata wewe umemuona alivyoumbika?” Dullah alimwambia fundi Yassin na kutabasamu.
Fundi Yassin ambaye licha ya kwamba umri wake ulikwenda lakini naye alikuwa mzoefu wa mambo ya mjini, akaishia kucheka na kusema haya bwana!
Maongezi hayo yalijiri wakati fundi Yassin na Dullah wakisubiri basi la kwenda Tegeta Kibaoni, haukupita muda mrefu lilifika wakapanda ambapo fundi aliuweka mfuko wa zana zake za kazi nyuma ya kiti cha dereva, kama ilivyokuwa awali pia waliketi siti moja.
Wakati safari ikiendelea mtaalam Dullah ambaye kichwa chake kilikuwa kama kompyuta akaanza kuzitaja zile namba za yule mrembo kimoyomoyo, sifuri, Sita ,tano,nane, arobaini na mbili, arobaini ishirini na….hahaha” akaishia kutabasamu kwani alikuwa ana uhakika hakukosea.
“Mwenzangu vipi mbona unatabasamu?” fundi Yassin alimwuliza Dullah.
“Kanifurahisha huyo kondakta kwa staili yake ya Kata K, yaani ukivuta kidogo hiyo suruali atabaki na boksa tu!” Dullah alimchomekea fundi Yassin wakati si kweli alifurahishwa na jambo hilo.
“Huo si ndiyo uvaaji wenu vijana wa karne hii, huwa nashindwa kuelewa, hivi kijana huwezi kuvaa vizuri ukaonekana wa kileo mpaka uoneshe nguo yako ya ndani?” fundi Yassin alimwuliza Dullah.
Dullah aliishia kucheka na kumwambia hayo ni mambo ya vijana japo yeye hakuwa na tabia hiyo, ambapo fundi Yassin alikubaliana na kusema hata yeye (Dullah) alikuwa na ugonjwa wake.
“Mh fundi, ugonjwa gani?” Dullah alimwuliza fundi Yassin huku akicheka.
Baada ya Dullah kubaini watu walimshangaa alivyoangua kicheko akamwambia fundi Yassin kwamba wayaache mazungumzo yale kwanza hadi watakapofika site.
“Haya tubadili mada, lakini dogo leo nimekuvulia kofia kwa jinsi ulivyomzoea yule mrembo,” fundi Yassin alimwambia Dullah .
“Fundi bwana, mbona mambo ya kawaida tu kwa sisi vijana!” Dullah alimwambia fundi wake, wakacheka.
Basi walilopanda lilipofika kituo cha Africana Mbezi waliteremka kama abiria sita wakapanda wengine wakiwemo wasichana wawili wazuri naliovaa kwa mpangilio.
Mmoja wa wasichana hao alikaa siti iliyokuwa mbele ya akina Dullah na mwingine ambaye alikuwa mweupe, mwenye shepu ya kimisi alikaa siti ya kushoto iliyokaribiana na Dullah .
“Dogo umeyaona mambo yako?” fundi Yassin alimtania Dullah .
“He bwana siyo mchezo, yaani nimeamiani mida hii ya asubuhi kwenye madaladala kunakuwa na watoto wakali aisee!” Dullah alimwambia fundi Yassin kwa sauti ya chini, wakacheka.
Wakati akitoa kauli hiyo kumbe yule msichana aliyekuwa amekaa siti ya kushoto alimsikia Dullah , akaachia tabasamu lililoona na kijana huyo mwenye dimponsi.
Dullah alimbinya pajani fundi Yassin na kumweleza yule msichana aliwasikia, ambapo fundi huyo akacheka na kumsifia kwamba kweli alikuwa ma masikio shapu!
Basi lilipofika njia panda ya kwenda Bahari Beach, wale wasichana walishuka kitendoa mbacho hakikumpendeza Dullah akaishia kusikitika moyoni.
“Da! Watoto wazuri kumbe wanashukia hapa,” Dullah aliwaza lakini hakuweza kuwazuia na kubaki kusonya ndani kwa ndani.
Kama vile fundi Yassin alijua Dullah hakupenda wale watoto wazuri washuke, akamtania kwamba licha ya kujifanya mjanja hakuweza hata kuwapa hi wale warembo.
“Yaani bro wewe acha tu kama umejua nilivyoumia warembo kushuka pale, kama wangeshukia Tegeta ndiyo ungejua mimi ndiyo Abdallah Mzamba kijana wa Kisukuma,” Dullah alimwambia fundi Yassin wakacheka.
Kutokana na kunogewa na stori, walishtukia basi limesimama Tegeta waliteremka ambapo fundi Yassin alichukuwa mfuko uliokuwa na zana za kazi na kumfahamisha Dullah kwamba walitakiwa kupanda mabasi yanayokwenda Kisauke.
“Kisauke ndiyo wapi?” Dullah ambaye ndiyo mara yake ya kwanza kusikia jina hilo alimwuliza fundi Yassin.
Fundi Yassin alipoulizwa hivyo aliishia kucheka na kumfahamisha Dullah kwamba ni mbele ya Madale ambako wenye nazo wengi wameporomosha mahekalu ya nguvu.
INAENDELEA

0 Comments