Ilikuwa ni kipindi cha mvua za masika, na siku hiyo mvua ilikuwa inanyesha. Kijana Patrick alikuwa ndani na mama yake bi. Deborah, hoja ya Patrick ilikuwa ni moja tu kuhusu baba yake mzazi.
PATRICK: Mama, hivi kwanini hutaki kuniambia ukweli kuhusu baba yangu.
DEBORAH: Mwanangu ni historia ndefu sana, tafadhari usinikumbushe.
PATRICK: Mama, mimi ni kijana mkubwa sasa. Niambie ukweli, baba yangu ni nani? Hayo machungu yako, machungu gani? Ninachotaka mimi ni kumjua baba yangu tu.
DEBORAH: Hii ndio tabu yenu watoto wa kiume.
Mara Patric akainuka na kuelekea nje.
DEBORAH: Jamani mwanangu, unaenda wapi na mvua hii?
PATRICK: Kutembea.
DEBORAH: Kutembea na mvua utalowa mwanangu, halafu humu ndani hakuna hata mwamvuli.
PATRICK: Unanijali eeh!!
DEBORAH: Ndio nakujali mwanangu.
PATRICK: Kama kweli unanijali, ungenitajia baba yangu ni nani.
DEBORAH: Siwezi mwanangu siwezi.
PATRICK: Ndio hapo unaponikera mama, haya bhana badae.
DEBORAH: Jamani Patrick.
Patrick hakujali chochote, alitoka nje na kuondoka.
Deborah alikuwa na siri nzito juu ya mtoto wake Patrick, hakutaka kuusema ukweli kwa kipindi hicho, alijua wazi ukweli huo utamsononesha sana Patrick.
Deborah akiwa amesimama mlangoni na kumuangalia mwanae akitokomea kwenye mvua, mara akamuona dada yake aliyeitwa Marium akiwa anakuja na mwamvuli.
MARIUM: Vipi? Mbona umesimama mlangoni halafu namuona Patrick akitokomea mvuani.
DEBORAH: Dada we acha tu, karibu ndani kwanza.
Akamkaribisha dada yake ndani na kuzungumza nae hili na lile. Akamueleza na nia ya Patrick hadi kuondoka vile kwa hasira.
MARIUM: Debo, hunabudi kumueleza Patrick ukweli. Watoto wa kiume na baba zao mdogo wangu.
DEBORAH: Mmmh!!
MARIUM: Mbona unaguna sasa? Si umwambie tu Patrick kama baba yake ni Jumanne, na aende akamtafute huko Dar.
DEBORAH: Dada, hujui chochote kuhusu mimi na Patrick.
MARIUM: Inamaana hata Jumanne si baba yake? Ulizaa na mwanaume mwingine Deborah, sasa nimeelewa sababu kubwa ya Jumanne kukuacha wewe.
DEBORAH: Dada, usilolijua ni sawa na usiku wa giza.
MARIUM: Sawa, endelea kukaa na siri yako moyoni, nadhani utaitoa kaburini siku utapokufa.
DEBORAH: Jamani dada!!
MARIUM: Ndio hivyo Deborah.
Wakaongea mambo mengine ila Deborah akaendelea kubaki na siri yake moyoni.
Badae, mwanae Patrick alirudi akiwa amelewa sana kwahiyo akapitiliza kulala.
Kesho yake asubuhi, Patrick alikuta mama yake akiwa amemuandalia supu, baada ya kunywa alirudi na kukaa tena na mama yake kumuuliza vizuri.
PATRICK: Mama ni kweli unanijali sana, tena unanipenda sana ila ingekuwa vyema kama ningemjua na baba yangu.
DEBORAH: Patrick mwanangu, ni historia ndefu sana kuhusu baba yako.
PATRICK: Jana nilienda kwa mamdogo Anna, nae ameniambia kuwa inawezekana baba yangu akawa Jumanne. Je huyo Jumanne ni nani? Na je ni kweli ndiye baba yangu?
DEBORAH: Hapana Patrick, Jumanne si baba yako mwanangu.
PATRICK: Jamani mama, sasa baba yangu ni nani? Je ni yule tuliyekuwa tunaishi nae Arusha bwana Maiko?
DEBORAH: Hata Maiko si baba yako.
PATRICK: Sasa baba yangu mimi ni nani? Nahitaji kujua mama, nahitaji kutambua. Hata kama ulibakwa hadi kunipata mimi, niambie tu mama.
DEBORAH: Unapofikia ni pabaya huko Patrick, mi sijawahi kubakwa.
PATRICK: Sasa mbona baba yangu humjui?
DEBORAH: Ipo siku nitakwambia ukweli wote, ila sio sasa.
PATRICK: Mama, ni kweli umenisomesha. Umenilea vyema ila kumbuka kwamba kumjua baba yangu ni haki yangu, haijalishi alikutenda mambo gani mama ila nina haki ya kumjua.
DEBORAH: Sawa mwanangu, nitakueleza tu. Ipo siku utaujua ukweli wote Patrick.
Patrick alijiona hana umuhimu wa kuendelea kuishi nyumbani tu bila ya kufanya kazi maalum. Ikabidi atafute kazi na kuamua kupanga safari ya kwenda kwani alipata kazi kwenye mkoa wa Morogoro.
Patrick akasafiri bila ya kumuaga mama yake, kwa madai yake kuwa amempa adhabu mama yake ya kutomtajia baba yake.
Wakiwa njiani, basi lao likapata ajali kwani liligongwa na lori na kupinduka. Watu waliumia sana, haikuwezekana kuendelea na safari tena.
Majeruhi wakabebwa na kupelekwa hospitali, baada ya matibabu Patrick akaamua kurudi kwa mama yake. Kwakweli Deborah alimuhurumia sana mwanae.
PATRICK: Naomba unisamehe mama, najua yote hii ni laana ya kuondoka bila ya kukuaga mama yangu.
DEBORAH: Usijari mwanangu, cha muhimu hapa ni uzima wako tu mwanangu.
Patrick aliendelea kujiuguza mpaka pale alipopona kabisa. Ila ile kazi ya Morogoro haikuwepo tena kwani muda mrefu uliku umepita.
Patrick akaamua kutafuta kazi tena, na safari hii akapata kazi mkoani Arusha. Akahitajika kwenda huko, akaamua kumuaga mama yake.
DEBORAH: Ila mwanangu, huko Arusha mi sikuamini kabisa.
PATRICK: Kwanini mama?
DEBORAH: Sababu ya Maiko.
PATRICK: Mama usijali, kwanza hata sipakumbuki anapoishi huyo bwana. Siwezi kwenda mama.
DEBORAH: Najua ulimzoea Maiko kama baba yako, ila Maiko ni mtu asiyefaa kabisa mwanangu.
PATRICK: Mama, tumeondoka Arusha tangia nikiwa na miaka sita. Siwezi kumjua tena huyo Maiko, wala yeye hawezi kunikumbuka mama.
DEBORAH: Nakuhurumia mwanangu, ukimuona mkimbie kabisa. Atakufundisha tabia mbaya. Ila nakuombea kheri mwanangu.
PATRICK: Sawa mama usijali, huko Arusha nitafanya kilichonipeleka tu. Na pia nitakuwa nakuja huku Mwanza kukuona mama yangu.
DEBORAH: Sawa mwanangu, ila kuwa makini sana na Maiko, ni mtu hatari sana huyo.
PATRICK: Sawa mama, ingawa nae sijui alikufanya nini?
DEBORAH: Hiyo ni siri yangu mwanangu, ila jitenge nae.
PATRICK: Sawa mama nimekuelewa.
DEBORAH: Nakupa baraka zangu zote mwanangu.
PATRICK: Asante mama, najua nitakaporudi utakuwa tayari kunitajia baba yangu.
DEBORAH: Mmh na wewe, kila mara baba baba kama wimbo wa Taifa!
PATRICK: Ni wajibu wangu kumjua mama.
DEBORAH: Sawa mwanangu, ipo siku nitakwambia ukweli.
Deborah na mwanae wakaongea mengi kwani kesho yake asubuhi ndio ilikuwa siku ya safari, siku ya Patrick kuiacha Mwanza na kwenda Arusha kikazi.
Alfajiri na mapema, Patrick akasindikizwa na mama yake hadi kituo cha mabasi na kumuacha Patrick akiwa ndani ya basi akielekea Arusha.
Safari ilikuwa ni ndefu sana, hadi muda ambao Patrick alifika Arusha alijihisi akiwa na uchovu mwingi. Wazo pekee alilopata kichwani kwa muda huo ni kutafuta nyumba ya wageni ambayo atapumzikia siku hiyo.
Akiwa pale stendi, mara kuna mtu akamshika bega, Patrick alipogeuka akapatwa na kitu cha ajabu sana.
Akiwa pale stendi, mara kuna mtu nyuma yake akamshika bega. Patrick alipogeuka akapatwa na kitu cha ajabu sana, kwani alishtukia akishindikwa ngumi usoni kitu kilichofanya aone kizunguzungu na kabla hajajitetea alijikuta akisokomezwa ndani ya gari, akiwa anafurukuta wakampulizia kitu cha ungaunga usoni na kujikuta akilala bila ya kubisha zaidi.
Patrick alipozinduka alijikuta kwenye kiti akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi.
Patrick akakumbuka tukio la mwisho baada ya kupigwa ngumi ni kuwa alipakiwa kwenye gari na kupuliziwa unga usoni. Akiwa anayatafakari hayo, mara akaingia mtu mule ndani na kuita huku akicheka.
"Patrick, Patrick"
PATRICK: Kwanini mnanitenda hivi jamani?
Yule mtu wa nyuma akazunguka mbele na kumuangalia usoni Patrick huku akisema.
"Mimi ni Maiko"
PATRICK: Maiko baba yangu.
MAIKO: (Akacheka sana), Patrick mimi si baba yako. Na vile vile mimi sina mtoto yeyote hapa duniani. Kama Deborah alikwambia kuwa mi ni baba yako basi amekudanganya.
PATRICK: Sasa mbona umenifunga hivi?
MAIKO: Kama utaongea na mimi kwa ustaarabu basi nitakufungua. Najua wewe Patrick ni mtoto mtukutu sana.
PATRICK: Ila mimi Sina tatizo na wewe na tutaongea vizuri tu.
Basi Maiko akaita vijana wake ambao walimfungua kamba Patrick na kwenda nae sebleni. Na hapo ndipo Maiko akaanza kumwambia Patrick kusudio lake.
MAIKO: Nahitaji kufanya kazi pamoja na wewe.
PATRICK: Lakini mimi nimekuja huku Arusha kwenye kazi nyingine, sio kazi yako baba.
MAIKO: Patrick, umesomeshwa kwa pesa yangu. Ni halali yako kuniita baba, na lazima unipe fadhila kwa kufanya kazi yangu.
PATRICK: Ila mimi nimesomeshwa na mama.
MAIKO: Hahahaha, mama yako ni mshenzi sana. Aliniibia pesa yule, kwahiyo ni pesa yangu ndio iliyokusomesha Patrick. Deborah alidhani amenikimbia milele kwa kuishi Mwanza, hakujua kama nina mtandao mkubwa. Kwa kipindi chote hiki nilikuwa namuangalia tu.
PATRICK: Hata kama alikuibia ni yeye, na hata hivyo mimi nitakapofanya kazi zangu nitakulipa. Tafadhari niachie niende nilipoitwa.
MAIKO: Hujui kama hapa ndipo ulipoitwa? Hukushangaa kupata kazi kwenye kampuni ambayo hujaomba? Au ulidhani ni mchezo wa bahati nasibu!! Patrick umesoma, ila umeshindwa kutafakari. Unafikiri kuna unarihisi wa kupata kazi namna hiyo? Tumia akili Patrick, jua kuchanganua mambo.
Patrick hakujua kama Arusha aliitwa na Maiko, akakumbuka matukio ya nyuma kuwa ameitwa kuanza kazi Arusha. Patrick akajiona mpumbavu sana kwa kutokufikiria mapema kuwa anapata vipi kazi kwenye kampuni asiyoomba.
PATRICK: Sasa hapa nitafanya kazi gani?
MAIKO: Kazi zipo nyingi tena zinalipa kupita maelezo, utakapofanya kwa kujitoa unaweza kuwa tajiri kunipita mimi. Patrick, tangia ukiwa mdogo nimekuona kuwa wewe ni kijana jasiri najua hii kazi utaiweza na utafika mbali Patrick.
PATRICK: Kazi gani sasa?
MAIKO: Kazi yenyewe unatakiwa ule kiapo kwanza kabla ya kuifanya.
PATRICK: Mmmh!! Kazi ya kula kiapo kwanza!! Dah!! Sasa kama wewe si baba yangu, baba yangu mimi ni nani?
MAIKO: Hilo swali muulize mama yako Deborah, maana kwangu alikuja akiwa na mtoto mchanga ambaye ndio wewe, alikuwa akikunyonyesha huku akilia muda wote. Kuna mengi nitakwambia ila ufanye kazi yangu kwanza.
Patrick hakuwa na la kusema wala la kuongezea, akawa anajiwazia tu kuhusu hiyo kazi ambayo atapewa na Maiko. Na pia alimuwaza huyo baba yake aliyemfanya mama yake alie muda wote wakati yeye akiwa mtoto mdogo.
Deborah akiwa amelala akamuota mwanae Patrick, akajikuta akishtuka na kusema kwa nguvu "Patrick"
Mara akamsikia mtu akigonga mlango wake, alipoinuka na kwenda kufungua alikuwa ni mdogo wake Anna. Akamkaribisha ndani,
ANNA: Dada mbona nimesikia ukiita Patrick kwa nguvu?
DEBORAH: Kuna ndoto mbaya imenijia kumuhusu Patrick.
ANNA: Kwani Patrick mwenyewe yuko wapi?
DEBORAH: Ameenda Arusha kikazi.
ANNA: Mmh!! Hata kuaga jamani! Hivi huyu mtoto wako baba yake ni nani?
DEBORAH: Jamani, kwani haiwezekani kuwa na mtoto bila ya baba?
ANNA: Acha maneno yako hayo, kila mtoto ana baba yake tatizo ni kuwa wengine wanawatambua baba zao na wengine hawawatambui.
DEBORAH: Sasa wewe unataka nini?
ANNA: Nataka kumtambua baba yake Patrick.
DEBORAH: Hakuna anayeweza kumtambua baba yake na Patrick hata mimi mwenyewe.
ANNA: Khaaaa, inamaana ulibakwa dada!!
DEBORAH: Ndio kitu pekee unachowaza, sijawahi kubakwa. Siri ya mwanangu Patrick ninayo mwenyewe moyoni mwangu.
ANNA: Au Joseph ndio baba yake na Patrick?
DEBORAH: Hayakuhusu.
Joseph alikuwa ni mwanaume aliyempenda sana Deborah na amekuwa akimfatilia mara kwa mara jambo ambalo linamfanya Anna ahisi kuwa huenda Joseph ndio baba mzazi wa Patrick.
Deborah hakutaka kabisa kuulizwa chochote kuhusu Patrick, kwani ni siri kubwa sana aliyoiweka moyoni mwake miaka na miaka, hakutaka mtu yeyote kuijua siri hiyo. Akawa anajisemea tu,
"Ila muda ukifika nitamwambia ukweli Patrick, nadhani atanielewa kwanini nimekaa na siri hii miaka yote"
Siku zote tangu Patrick akiwa mtoto mdogo, Deborah hakutaka kabisa kuulizwa kuhusu baba yake na Patrick.
Patrick akaitwa na Maiko ili aweze kula kiapo cha hiyo kazi.
PATRICK: Nitakulaje kiapo cha kazi nisiyoijua?
MAIKO: Ni lazima ule kiapo kwanza, kazi utaijua hapo baadae.
PATRICK: Hapana siwezi, kama kazi ya kuua watu je? Siwezi.
MAIKO: Inamaana mimi ni muuaji? Kama ningekuwa hivyo ningemuua mama yako na wewe mwenyewe kipindi kile.
PATRICK: Kwanini usinitajie hiyo kazi kwanza?
MAIKO: Lazima ule kiapo kwanza.
PATRICK: kwakweli siwezi kula kiapo kwa kazi ambayo siijui.
MAIKO: Unakataa kula kiapo Patrick!!
PATRICK: Siwezi kabisa kula kiapo kwa kazi nisiyoijua.
Maiko akabadilika gafla kitendo ambacho kilimtetemesha Patrick.
Maiko akabadilika gafla kitendo ambacho kilimtetemesha Patrick.
MAIKO: (akaongea kwa ukali), Sema tena Patrick.
Patrick akawa anajiuma uma tu kwani hakujua kitakachompata, akakumbuka maneno ya mama yake kuwa Maiko ni mtu hatari sana.
PATRICK: Nakuomba basi hata nimuulize mama aniruhusu kwanza.
MAIKO: Wewe ni mtoto wa kiume Patrick, mama kitu gani?? Wajibu wako kwa mama yako kwa sasa ni kumpelekea pesa tu.
PATRICK: Hata kumuomba ushauri pia.
MAIKO: Akupe ushauri gani mwanamke?? Nishakwambia mpelekee pesa tu uone atakavyochekelea hadi jino la mwisho tena atakupenda zaidi.
PATRICK: Ila mama ananipenda siku zote hata nilipokuwa nyumbani bila kazi.
MAIKO: Acha kujidanganya Patrick, nitakueleza mambo ambayo yataufumbua ubongo wako na kukuelewesha kwanini mwanamke akawa mama.
PATRICK: Mambo gani hayo?
MAIKO: Utajua vingi baada ya kukubali kula kiapo na kuanza kazi, jambo ni moja tu sitakuruhusu kutoka kwangu bila ya kula kiapo.
Patrick hakuwa na la kufanya, alishindwa namna ya kumkwepa Maiko. Na ubaya wa kazi ya Maiko ukiianza huwezi kuiacha, akawaza vitu vingi sana Patrick, akawaza pale mama yake atakapojua ukweli kuwa yuko na Maiko. Akajisemea kuwa atafanya kuwa kama siri ili mama yake asigundue.
Hatimaye Patrick akaamua kula kiapo, kitendo ambacho kilimfurahisha sana Maiko.
MAIKO: Sasa Patrick utajiri unanukia katika maisha yako.
Patrick alifurahi machoni ila moyoni alihudhunika kwa kumsaliti mama yake.
Deborah alikuwa na mawazo sana, mawazo ya kukosa mawasiliano kutoka kwa mtoto wake Patrick.
Alikuwa amekaa na dada yake Marium akimlalamikia.
DEBORAH: Tangia Patrick aondoke ni mwaka sasa umepita, hakuna cha simu wala nini sijui mwanangu amepatwa na kitu gani!
MARIUM: Usiwaze sana dada, muombee tu kwa mwenyezi Mungu.
Wakasikia muungurumo wa gari ukiishia kwao, ila hawakufikiria kama gari hiyo inakuja kwao.
Mara mtu akaanza kugonga mlango, kwenda kufungua ni Patrick, kwakweli Deborah alifurahi sana, alimkumbatia mwanae kwa furaha na kumshangaa jinsi alivyobadilika.
Patrick alimbebea zawadi nyingi sana mama yake na akaongea nae mambo mengi ila hakumwambia ukweli kama anafanya kazi kwa Maiko, hilo jambo alimficha kabisa hakutaka mama yake ajue.
PATRICK: Mama, nitakaa hapa wiki mbili.
DEBORAH: Kweli mwanangu?
PATRICK: Ndio mama, yani nilikukumbuka sana mama yangu.
DEBORAH: Na mbona hata simu ulikuwa hupigi?
PATRICK: Mama swala la kuwapigia majirani kukuulizia nilichoka, ndiomana nimeamua kukununulia simu yako.
MARIUM: Inaelekea kazi uliyopata inalipa sana Patrick, yani ndani ya mwaka ndio umebadilika hivyo!!
PATRICK: Aaah! Mambo madogo tu haya mamkubwa.
DEBORAH: Ila ni kazi gani hiyo mwanangu?
PATRICK: Nipo mgodini mama.
MARIUM: Hongera sana Patrick.
Walikuwa wakiongea mambo mengi ya hapa na pale, ilikuwa ni siku ya furaha sana kwa Deborah.
Tusa alikuwa ni binti mrembo na wa kupendeza machoni mwa watu. Mwanaume yeyote rijali lazima akimuona Tusa ajihisi tamaa ya kuwa naye.
Sura yake ya mviringo, mashavu yenye vibonyeo, meno meupe na yaliyokwenye mpangilio mzuri na mwanya. Ukimuona Tusa amecheka utatamani muda wote uyatazame meno yake yalivyo. Kwakweli alipendeza sana, hakuwa mrefu wala mfupi, umbo lake la wastani na rangi yake ya machungwa vilimfanya avutie zaidi. Tusa alizoea sana kudeka labda kwa vile alikuwa ndio mtoto wa kwanza wa bwana Adam na mkewe Pamela, na pia alikuwa ndio mtoto pekee wa kike kwenye familia yao ya watoto watatu.
Tusa alipenda sana kutumia mitandao ya kijamii hasa hasa facebook, tangu amalize kidato cha sita hadi alipoenda chuo muda wake mwingi aliutumia kwenye facebook, akiweka picha nyingi na kuandika jumbe mbali mbali kila leo, alikuwa na mpenzi wake aliyeitwa Sele ambaye aliichukia sana ile tabia ya Tusa kuwa facebook muda wote.
SELE: Kwakweli Tusa hiyo tabia yako siipendi, hakuna muda tunaoongea vizuri muda wote wewe na simu tu.
TUSA: Jamani nachat na rafiki zangu.
SELE: Huo mtandao siupendi Tusa, au unanidharau kwavile sijasoma kama wewe.
Tusa alikuwa hapendi kusemwa kuhusiana na swala la facebook, mara nyingi alikuwa anaenda kulalamika kwa dada yake aliyeitwa Tina ambaye alikuwa ni mtoto wa mama yake mkubwa.
TUSA: Ila Sele anakera sana dada.
TINA: Tatizo lako Tusa hutaki kuachana na huyo Sele, mwanaume gani huyo hata aendani na wewe.
TUSA: Sasa unataka niwe na nani? Hata hivyo Sele nampenda.
TINA: Nitakutafutia pedeshee mdogo wangu, kwa jinsi ulivyo na mvuto ni wakati wa kutengeneza pesa sio kukalia uzuri wako kwa mtu kama Sele.
TUSA: Simtaki yeyote zaidi ya Sele tu.
Siku zote Tusa alikuwa anajazwa ujinga na Tina.
Patrick aliamua kutembelea ndugu, jamaa na marafiki wa pale Mwanza ambao wote walimshangaa Patrick jinsi alivyobadilika.
Akiwa kwa rafiki yake John wanaongea.
PATRICK: John, yani wewe na simu tu muda wote.
JOHN: Nyie wenzetu mshatoka kimaisha, wenzenu tunajiliwaza tu humu.
PATRICK: Acha vituko John, unajiliwaza vipi na simu?
JOHN: Nipo facebook, kuna binti flani hivi anaitwa Tusa namfukuzia kinoma.
PATRICK: Hahaha, kweli John wewe ni domo zege, yani mademu wote mtaani huwaoni hadi uwafukuzie wa huko facebook?
JOHN: Hujui tu Patrick kuna mademu wana mvuto humu balaa.
PATRICK: Aah!! Huwa naisikia tu hiyo facebook, basi na mi niungie niwe nawaona hao mademu.
JOHN: Poa, ngoja nikufungulie sasa hivi kwa namba yako ya simu. Na wewe ulivyo kicheche nadhani utataka kuwalamba wote wewe.
Wakaanza kucheka, huku John akimuunganisha Patrick na facebook.
PATRICK: Ila mi sio kicheche bhana, nitajiunga ili kuwaangalia tu ila sina hata haja nao.
Patrick alirudi nyumbani kwao huku jina la Tusa likitembea kwenye fikra zake.
Patrick alirudi nyumbani huku jina la Tusa likitembea kwenye fikra zake.
Alipokuwa nyumbani kwao, akajaribu kuingia facebook ili amuone huyo Tusa. Alipoandika jina, wakaja Tusa wengi wengi, akashindwa kutambua Tusa aliyetajwa na John ni yupi, akaingia kwa John napo akakuta John ana marafiki watatu wenye jina hilo la Tusa. Akakuta,
=> Tusa Adam
=> Tusa the cute baby
=> Tusa the daughter of P&A.
Na akaona kuwa wote watatu wanaufanano. Nia kubwa ya Patrick ni kumjua huyo Tusa aliyetajwa na John. Ikabidi apange kesho yake kwenda tena kwa John ili akapate maelezo ya kutosha kumuhusu huyo Tusa, alitaka kujua ni kwanini John amepagawa na binti huyo.
Patrick alimfata John kama alivyopanga, alipofika wakapiga story za hapa na pale.
PATRICK: Jana nilikusikia ukimtaja binti mmoja hivi wa kwenye facebook, je ndio demu wako?
JOHN: Unamsema Tusa? Hapana si demu wangu ila narusha ndoano ni mgumu kweli.
PATRICK: Hebu nione picha yake.
John akaifungua picha ya Tusa na kumpa Patrick aiangalie, nia kubwa ya Patrick ni kuona Tusa anatumia jina lipi mbele zaidi ya Tusa. Akaona imeandikwa Tusa the cute baby. Akalishika hilo jina vilivyo.
PATRICK: Ni mkali kweli John.
JOHN: Umeona alivyo kifaa, yani siachi hadi anikubali.
PATRICK: Nipe namba zake za simu nikusaidie kumwaga swaga.
JOHN: Ninazo basi!! Amenigomea kunipa. Hata kama ningekuwa nazo nisingekupa sela.
Wakawa wanacheka ila Patrick akawa ameshamjua huyo Tusa anayemuhitaji.
Akarudi kwao na kumsikia mama yake akizungumza na Anna.
DEBORAH: Namshukuru Mungu kwakweli tangu Patrick arudi sijamsikia kabisa habari ya baba.
ANNA: Labda ameshamjua.
DEBORAH: Hakuna anayemjua.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mara Patrick akaingia ndani na kuwafanya wote washtuke, akawasalimia na kuingia chumbani. Jina la Tusa liliendelea kucheza kwenye akili yake, alienda moja kwa moja na kuingia facebook, akatafuta jina na kumuona kwakweli akavutiwa nae sana, picha nyingi za Tusa ziliendelea kumvuta Patrick, akaamua kumuomba urafiki. Ila hakukubaliwa ombi lake kwa siku hiyo, aliendelea kuangalia tu picha za Tusa. Akakumbuka kuwa muda wake wa kukaa Mwanza umeisha, inambidi apange safari ya kurudi tena Arusha.
Wazo lingine likamjia kuwa amtumie ujumbe Tusa ili ajaribu kama atamjibu.
Tusa akiwa na Tina kama kawaida yao.
TUSA: Sipendi watu wanaoomba urafiki bila ya picha.
TINA: Mwingine tena amekutumia?
TUSA: Ndio anaitwa Patrick, tena inaonyesha ni mgeni kwenye huu mtandao maana limenitumia na meseji eti unaitwa nani.
TINA: Hahaha, Mkubalie tu umfundishe mji Tusa, inakuwaga mijinga hiyo, inamaana hajaona jina lako hapo juu!
TUSA: Labda ni account fake.
TINA: Kama fake si utamblock tu, wee mkubalie kwanza, litakuwa jinga hilo.
Tusa akaamua kukubali ombi la urafiki toka kwa Patrick.
TUSA: Nishalikubalia.
TINA: Hiyo ndio mimbulula Tusa, unaweza ukalidanganya chochote humo.
Waliongea mengi bila kujua furaha ya Patrick ya kukubaliwa urafiki na Tusa, akajisemea kuwa atahakikisha anampata huyo Tusa hata awe mgumu wa kiasi gani.
Patrick alianza kutumiana ujumbe na Tusa na kufanya nae mazungumzo ya mara kwa mara kwenye mtandao ila kila akijaribu kumuomba namba ya simu Tusa alionyesha kuwa mgumu kutoa namba yake.
Siku ikafika ya Patrick kurudi Arusha, akaamua kumuaga mama yake na kumauachia pesa kiasi za kumsaidia hapo nyumbani. Halafu akamkataza mama yake kufanya kazi aliyokuwa anaifanya, kazi ya usafi kiwandani.
DEBORAH: Kwanini mwanangu umenikataza kwenda kwenye kazi?
PATRICK: Ile kazi haikufai mama yangu, naomba upumzike kwa sasa. Nitakuwa nakutumia pesa kila mwezi, na ukiwa na shida yoyote niambie.
DEBORAH: Ila mwanangu, ile kazi nimeifanya miaka na miaka.
PATRICK: Naelewa mama, ila haikufai tena. Nitakutumia pesa nyingine ya biashara ila sitaki uende tena kwenye ile kazi mama.
DEBORAH: Sawa mwanangu.
PATRICK: Ila kitu kimoja nakuomba mama yangu.
DEBORAH: Kitu gani tena Patrick.
PATRICK: Nikirudi tena niandalie maelezo ya kutosha kuhusu baba yangu na Maiko.
DEBORAH: Mmh mwanangu!!
PATRICK: Ndio hivyo mama, nataka kujua ukweli.
Akili ya Patrick iliwaza vitu vingi sana, maneno ya Maiko kuwa mama yake alimuibia pesa yalimjia mara kwa mara. Nyumba aliyoishi na mama yake ilikuwa ni nzuri ukilinganisha na kazi, na akajiuliza sana kama mama yake aliiba pesa na kwanini akafanya kazi ya usafi, na pia kwanini Maiko hakumtafuta Deborah siku zote hadi alipomnasa yeye Arusha. Kwakweli Patrick aligubikwa na maswali mengi ambayo alijua wazi majibu ya maswali hayo anayo mama yake bi. Deborah na bwana Maiko, alihitaji kufanya uchunguzi kwa siri na kuwauliza taratibu labda aweze kupata majibu ya maswali yake.
Safari ya Patrick ikakamilika na kumuaga mama yake na kuondoka zake kurudi Arusha.
Alipokuwa Arusha hakuacha kuendelea kuwasiliana na Tusa kwenye facebook.
Siku moja Maiko alimkuta Patrick akiwa na mawazo sana, alipomuuliza Patrick akamueleza kuhusu Tusa.
MAIKO: Sasa tatizo ni nini?
PATRICK: Hataki kunipa namba zake za simu.
MAIKO: Tatizo dogo sana hilo, nitakufundisha njia rahisi ya kupata namba zake na atakupa mwenyewe bila hata ya kumlazimisha.
PATRICK: Njia gani hiyo?
Patrick alihitaji sana kujua njia ambayo Maiko angempa ili aweze kumpata Tusa.
PATRICK: Niambie hiyo njia basi.
MAIKO: Patrick, Patrick. Unajua mtu mwenye pesa yu tofauti kabisa na mtu asiye na pesa?
PATRICK: Niambie basi.
MAIKO: Hakuna mwanamke anayeweza kukubabaisha ukiwa na pesa, Patrick wewe ni level nyingine sasa na unauwezo wa kumpata mwanamke yeyote umtakaye. Kwahiyo swala la huyo Tusa ni dogo sana, halafu umesema ni binti mrembo eeh!!
PATRICK: Ndio ni mrembo, tena ni mrembo sana.
MAIKO: Oooh!! Kama ndio hivyo nitakusaidia kumpata pale utaposhindwa niambie maana huyo anaweza kuwa msaada tosha kwenye kazi yetu.
PATRICK: Atatusaidiaje sasa?
MAIKO: Usijali, ukishampata nitakwambia. Ngoja nikupe njia za kumpata huyo mrembo wako.
Maiko akamfundisha Patrick njia kadhaa za kupata namba za Tusa na hatimaye kumpata kabisa na kumuweka katika himaya yake.
Patrick akaanza kutumia njia hizo kwa kasi ya ajabu.
Tusa akiwa amekaa nyumbani kwao, huku simu yake ikiwa kiganjani akifanya mawasiliano na Patrick kwa njia ya facebook.
PATRICK: Nikufanyie kitu gani Tusa ili unipatie namba yako?
TUSA: Sijui.
PATRICK: Naomba nifanye deal na wewe.
TUSA: Deal gani?
PATRICK: Nitakutumia namba za vocha uingize kwenye simu yako, halafu ukizipata unitumie namba zako ili nimalizie nusu ya vocha hiyo kwa kukurushia.
TUSA: Hebu tuma nione.
PATRICK: Unatumia mtandao gani?
TUSA: Natumia tigo.
PATRICK: Basi ingiza, 4262 6698 2898 195.
TUSA: Poa.
Tusa akaichukua hiyo namba ya vocha na kuingiza kwenye simu yake, mara gafla akapiga ukelele wa kicheko uliomshtua mama yake.
PAMELA: Jamani, laiti kama huyo mwanzilishi wa facebook angejua shida ninayopata huku nyumbani angeufunga kabisa huo mtandao, maana mwanangu unakaribia kuwehuka, unaongea mwenyewe na kucheka mwenyewe nikiuliza nini najibiwa facebook loh!!
TUSA: Sio hivyo mama.
PAMELA: Ila ni nini?
TUSA: Kuna rafiki mpya nimempata humu facebook ameniomba namba zangu nimegoma kumpa, amenitumia namba ya vocha. Nikajua utani mama kumbe ni kweli, maana nimeingiza imesoma elfu tano.
PAMELA: Jamani mwanangu hebu nirushie buku na mimi maana simu yangu haina hata hela.
TUSA: Mama nawe tamaa tu, tena ameniambia kuwa nikimtumia namba atanimalizia nusu ya vocha kwa kurusha kwahiyo atanitumia elfu tano nyingine.
PAMELA: Kheee mwanangu hebu mtumie na mie unirushie elfu mbili.
TUSA: Kheee mama!! Unapenda vya bure wewe, mi sitaki kutoa namba yangu.
PAMELA: Kama wewe hutaki mtumie yangu basi.
TUSA: Hahahaha, utapigwa na baba wewe. Namtumia yangu bhana.
PAMELA: Mtumie tu, kwani namba kitu gani Tusa? Unaogopa nini? Mtu mwenyewe hakujui mwanangu.
TUSA: Namuogopa Sele mama.
PAMELA: Hebu usiniletee hicho kichefuchefu chako cha huyo mlanda mbao, sitaki hata kumsikia.
Pamela alikuwa ni mmoja kati ya watu waliopinga mapenzi ya Tusa na Sele, kwavile Tusa na mama yake walikuwa kama marafiki kwahiyo mambo mengi ya Tusa, Pamela aliyajua.
Alimpinga sana Tusa kuwa na Sele kwasababu moja tu, nayo ni kuwa Sele hakusoma kama Tusa.
Tina nae alifikia kwenye mazungumzo hayo,
TINA: Nimesikia yote Tusa, na mimi nirushie jero basi.
TUSA: Mmh!! Wewe Tina na huyu mamako mdogo mnaweza kumteketeza mtu kwaajili ya pesa nyie.
TINA: Acha maneno mengi Tusa, mtumie hiyo namba na mimi unipunguzie vocha.
Tusa akamtumia Patrick namba yake ya simu na Patrick akafanya kama alivyomuahidi ili kuzidi kumvuta Tusa na fikra zake.
Patrick akampigia simu Tusa na kuzungumza nae mawili matatu na hiyo ikawa furaha yake.
Mawasiliano ya Tusa na Patrick yakawa ya mara kwa mara.
INAENDELEA

0 Comments