Familia nzima ilifika Dar es salaam, ndugu wa Deborah hawakuacha kuambatana nae ili kujua vyote na mipango yote itakapoelekea kwani bado familia nzima iligubikwa na wasiwasi na mashaka ukizingatia mambo yaliyopita mbele yao ni makubwa sana.
Patrick hakutaka kwenda Dar es salaam ila alikubali kwenda kwa heshima ya mama yake aliyempenda kuliko kitu chochote.
Pamela aliwakaribisha vizuri ambapo Deborah alikuwa anangoja wale waliotokomea Arusha warudi pale na wapate kuondoka na Yuda kurudi nae Mwanza ili kama mipango mingine ifanywe badae.
Wakina bi.Rehema nao wakawasili na kupokelewa vizuri sana ingawa walichoka mno kutokana na hali halisi ilivyokuwa.
Wakaeleza mambo yaliyowapata. Adamu akaelezea ilivyokuwa na mambo waliyokumbana nayo.
"Kwakweli sikufikiria kama tungepona, hii itakuwa fundisho kwetu katika maisha yetu yote. Maana tusingeng'ang'ania kurudi kule yote haya yasingetupa."
Bi.Rehema aliongea kwa uchungu mno,
"Sikutegemea kabisa kama mtoto wangu wa kumzaa mwenyewe anaweza kufanana na jini kiasi kile. Sasa nakubaliana na wewe Deborah kuwa mwanangu Maiko alikuwa ni mume gaidi. Nashindwa kuamini na kuelewa hadi sasa kwa mambo yaliyotukuta"
DEBORAH: Msijari sana, katika maisha kila kitu hutokea kwasababu maalum kwahiyo yote yaliyotokea yalikuwa na maana yake na mafunzo yake ili tusirudie tena kosa lililotendeka.
Deborah alionekana sasa kuwa mtu makini sana katika kushauri kwani aliweza kuwaweka wote kwenye mstari.
Yuda hakuwa na hamu kabisa na ukoo wa Maiko ila bado aliendelea kumpenda Tina. Sele nae alikuwa anaendelea kusikilizia tu hatma ya Tusa na Patrick.
Zilipita siku mbili bila kuwepo kwa dalili yoyote ya Fausta wala Pamela kutaka kusema ukweli, ilionyesha bado hawakuwa wazi kueleza mambo ambayo yamepita nyuma katika maisha yao.
Ikabidi Deborah aamue kufanya kikao cha lazima kwani yeye na familia yake walihitaji kurudi kwao Mwanza.
DEBORAH: Jamani, ukweli humuweka mtu huru. Patrick ni kijana mkubwa sasa anatakiwa kujua ukweli kuhusu wazazi wake, nani mama yake na nani baba yake. Naona kimya kimezidi, tafadhari Fausta na Pamela fungukeni maana mimi nina hakika kuwa Patrick ni mtoto wa mmoja wenu.
PATRICK: Ila mama, mimi sihitaji kuwajua tena hao wazazi wangu. Wewe tu unanitosha.
DEBORAH: Kuna ulazima wa kuwajua Patrick, angalia hapo Tusa ni mke wako na muda huo huo ni dada yako. Ni bora ukweli ujulikane ujue hatma yako na Tusa sio kazi ya kufanya kukutenganisha na Tusa kisiri bila kujua ukweli.
Deborah aliongea hayo kwani alimuona Pamela akifanya kazi ya kumkwepesha Tusa kwa Patrick.
REHEMA: Ni kweli usemayo Deborah, mengi yamepita sasa ni wakati wa kuweka mambo yote wazi.
Pamela akainama chini kisha akapiga magoti na kumfata Patrick kwa kilio,
"Nisamehe baba, mimi ndio mama yako mzazi"
Patrick alishtuka na kushangaa kwani hakuhisi kabisa kama mama yake atakuwa Pamela, Tusa nae machozi yakawa yanamtoka.
Kila mmoja alimtazama Pamela kwa makini.
Kila mmoja alimtazama Pamela kwa umakini.
Pamela alikuwa anamwaga machozi na kugundua kuwa alichofanya nyuma ndio kimemuumbua sasa.
Patrick aliendelea kuangalia kwa mshangao.
PATRICK: Inamaana Tusa ni dada yangu?
PAMELA: (Huku akiendelea kulia) ndio ni dada yako.
PATRICK: Acha unafki wa kulia kizembe, wakati unanitupa je ulilia au mbwembwe tu.
Pamela hakuwa hata na la kujitetea na kuishia kulia tu.
Ikabidi wakina Deborah waingilie kati na kuanza kujaribu kumtuliza Patrick aliyeonyesha kuwa amepandwa na jazba.
PATRICK: Kwakweli huyu mama nitamchukia maisha yangu yote, mama aliyenilea ndiye mama yangu.
DEBORAH: Hata Pamela pia ni mama yako mwanangu.
PATRICK: Siwezi kumkubali mama alinitupa kweli, je nisingeokotwa leo hii angemuomba msamaha nani?
DEBORAH: Yote ni mapito jamani, ni mapito ya maisha ila na wewe Pamela ilikuwaje hadi ukadiriki kumtupa mtoto wako mwenyewe?
Pamela akawa analia na kujaribu kujieleza.
"Si kwamba nilitaka kumtupa mtoto wangu, hapana kabisa ni maisha tu na mimba yenyewe iliingia bahati mbaya.
Kipindi naonaoka Dar es salaam na kukimbilia Morogoro nilikuwa ni mjamzito kipindi hiko na ubaya zaidi Deborah alishanigundua kuwa nina ujauzito, nilipomueleza muhusika akanishauri niitoe ili tuendelee kufaidi maisha mengine.
Kwa hapa Dar nilijaribu mara mbili kunywa dawa za kutoa mimba ila ilishindikana, mimba haikutoka zaidi ya damu kutoka kidogo na kukata.
Ndipo nilipoamua kwenda Morogoro kwa Fausta ambaye ni dada yangu, nilipomweleza akanishauri kuwa ni bora kuitoa ila kuepukana na matatizo yasiyo ya lazima.
Fausta akaenda kuniletea dawa toka kwa daktari wake, dawa ambazo hata yeye amewahi kutumia.
Basi na mimi nikatumia zile dawa ila ikawa ola kama mwanzo ile mimba haikutoka wala nini na ikaendelea kukua, dada akanishauri niitoe kwa njia ya kujifungua mwanzoni nilikataa kabisa na mimba nayo ikaendelea kukua. Sijui ni kwa nini ilishindikana kutoa kwa njia ya kunywa dawa.
Ile mimba ilipoendelea kukua ikawa inanisumbua sana nikashindwa kufanya kitu chochote, dada akaniambia kwavile tumejaribu kuitoa mara kwa mara ndiomana imeanza kunisumbua.
Hadi pale Adamu alipofika Morogoro, akanikuta niko hoi kabisa sitamaniki kutokana na ile mimba sikuweza kufanya kitu chochote.
Adamu akatoa ushauri kuwa nikafanyie hata operesheni kuweza kukitoa kiumbe hicho na tukashauriana kama huyo mtoto tumlee au la ila Fausta akasema yule mtoto atakuwa tahira kwani atakuwa ameshaathirika na yale madawa ya kutolea mimba, na mimi sikuwa tayari kulea tahira tukashauriana kuwa tukimtoa tumtupe kwani hatokuwa mwanadamu wa kawaida.
Tukaenda hospitali moja kule Morogoro na kumuomba daktari anifungulishe naye akanipima na kukuta mimba imekaa vibaya hapo uoga na wasiwasi mwingi vikanishika.
Adamu akaamua kusafiri na kurudi Dar na kutuambia kuwa tujitahidi kukamilisha mambo kabla hayajaharibika.
Ni hapo kesho yake mimi na Fausta tukakubaliana turudi Dar kushughulikia hili swala kwani dada alikuwa anajuana na madaktari wengi, tulipofika kwa daktari tukamueleza kila kitu naye akasema ni kweli kuna uwezekano mkubwa sana wa mtoto atakayezaliwa kuwa ameathirika na madawa niliyokunywa kabla, lazima atakuwa na kasoro na kutofautiana na binadamu wa kawaida na hatoweza kuchukua muda mrefu wa kuishi.
Nilimuomba anitoe tu hivyo hivyo ili nipate kupumua.
Nikiwa mimi na dada pale hospitali, niliingizwa chumba cha kufanyia operesheni na huko nilikuwa nusu kaputi hata mtoto gani aliyezaliwa sikubahatika kumuona alivyokuwa.
Nilipozinduka jambo la kwanza niliulizia kuwa mtoto mwenyewe yuko wapi, daktari akaniambia kuwa dada yangu amemchukua nikachukia sana kwani nilihitaji kwanza kumuona mwanangu.
Daktari aliniambia mtoto niliyejifungua alikuwa wa kiume ila afya yake imedhoofika sana kutokana na madawa niliyokunywa kuitoa mimba ile.
Roho iliniuma sana kumuhusu huyu mtoto na sikujua kwanini dada amechukua maamuzi ya gafla ya kwenda kumtupa mwenyewe bila kuningoja mwenye mtoto nishtuke na nitoe maamuzi yangu.
Sikutamani hata kulala tena, nilikuwa namngoja tu dada arudi ili anipeleke alipokwenda kumtupa mwanangu laiti kama kungekuwa na simu kama sasa basi ningempigia na kumsihi asimtupe mwanangu.
Nilimngoja na hatimaye akarudi, niligombana nae sana kwa maamuzi yake ya haraka kwenda kumtupa mtoto, nikamwambia kuwa namtaka mwanangu akasema atakuwa ameshakufa nikamwambia hata kama namtaka hivyo hivyo nikamzike mwenyewe kuliko kumtupa.
Kuteseka nayo ile mimba na aibu yake ndio vilivyonifanya niwaze kuitoa na kujaribu kufanya hivyo ila alipotolewa mtoto uchungu ulinishika sana juu ya huyo mtoto, nilikuwa tayari kwa lolote juu ya mtoto huyo ila ndio hivyo alikuwa ameshatupwa.
Ilikuwa usiku hata sikutaka kusubiri pakuche kwani nilihofia kukuta mwanangu ameliwa na mbwa.
Nilimlazimisha dada anipeleke tukamchukue mwanangu, ingawa nilikuwa na maumivu ya operesheni ambako sikutakiwa kulia wala kuhangaika sana ili kuepusha nyuzi kukatika.
Niliondoka na dada pale hospitali hadi eneo alilotupa mtoto, tulitafuta sana ila hatukumuona na mawazo machafu yakanijua kuwa mwanangu atakuwa ameliwa na mbwa tu.
Nililia sana na kujikuta nikiampa lawama zote dada yangu Fausta, nililia hadi mshono ukafumuka.
Maumivu makali ya kidonda na ubaridi wa hapo sikuweza kusogea kwani nilikuwa hoi kabisa kabisa, dada akatafuta gari na kuniwahisha tena hospitali.
Nikashonwa tena, ila kila nikishtuka na kuwaza kuhusu mwanangu kuliwa na mbwa machozi yalinitiririka sikuwa na wazo kabisa kama mtoto yule ameokotwa na mtu.
Nilipopona kiasi eneo lile ndio lilikuwa mahali pa kupumzikia, nilikuwa nikimkumbuka mwanangu basi naenda kulekule ambako dada alimtupa mtoto wangu. Nalia sana na kurudi nyumbani.
Ndipo nilipoamua na dada yangu turudi pale Dar tulipokuwa tukiishi mwanzo na badae yeye kwenda Morogoro na kuniacha mimi pale, niliamua kurudi ili nikaongee na Deborah nilitaka kwenda kumueleza ukweli na kumuomba msamaha kwani niliona kama ile ni laana tu.
Kufika pale mtaani nikakutana na habari nyingi sana kuhusu mtoto wa Deborah, roho iliniuma sana kwani Jasmini nilimchukulia kama mwanangu wa kumzaa.
Ndipo nikapata habari kuwa Deborah aliacha skendo na asingeweza kurudi tena, hapo tumaini la kuonana na Deborah likaisha.
Nikaonyeshwa msichana aliyekatwa miguu na Deborah ambaye alikuwa ni mtoto wa mama mwenye nyumba yake, kwanza nilishindwa kuelewa kwanini Deborah kachukua uamuzi ule.
Yule binti alikaa hospitali mwezi mzima na aliporudi alikuwa anatembelea baskeli za walemavu kwani miguu yote miwili hakuwa nayo tena.
Na habari nyingine ni kuwa nilikuja kusikia kuwa yule binti alipata ajari na kufa.
Adamu aliporudi kwake alikutana na maskendo hayo na alitakiwa asaidie upelelezi ambapo walifika hadi Mwanza kumsaka Deborah ila hawakumpata na hakuna aliyejua alipo.
Ikabidi mahusiano yangu na Adamu yaanze upya na ni hapo tulipoamua kuhama mtaa na alipoamua kubadili jina toka Jumanne hadi Adamu ili kusahau yaliyopita na kufanya kuwa yamepita, ingawa tulipokwenda kwa mzee Ayubu akatuambia kuwa sisi ni ndugu haitakiwi tuwe mume na mke tukampuuzia na kumwambia kuwa sisi tumeshapendana hatuwezi kuachana.
Akatusihi sana ila hatukumsikiliza na sasa ndio tunaelewa laana tuliyojijengea sisi wenyewe.
Siku Deborah anaelezea historia kuhusu maisha yake na Patrick iliniuma sana kujua kuwa Patrick ni mwanangu tena kamuoa Tusa mwanangu. (Pamela akainama na kulia tena).
Roho inaniuma sana hata sijui kwanini imekuwa hivi, najua Patrick huwezi kunisamehe, najua Tusa mwanangu nimekusababishia kidonda kikubwa ambacho hakitakuja kufutika kamwe maishani mwako ila ndio hivyo Patrick ni kaka yako tena wa damu moja"
Pamela alikuwa analia sana, bi.Rehema akamsogelea kumbembeleza.
Adamu alihisi kuchanganyikiwa kabisa kuwa Tusa ameolewa na kaka yake kwani hakufikiria kabisa kama Patrick mwanae, alihisi Patrick ni mtoto wa Fausta na Maiko, kwakweli alijihisi kulaanika kabisa.
Tusa alikuwa akilia tu na yeye, huku wakibembelezana na Tina ambaye naye alibakwa na baba yake mzazi.
TUSA: Huu ukoo kweli una laana tena umelaanika toka kwenye kilele chake.
Patrick alikaa kimya kabisa akitafakari bila hata kuelewa kuwa kwanini imekuwa vile ambavyo imekuwa, hakuna aliyetarajia kuwa vile.
Marium naye aliwawaza tu watoto wake wawili Yuda na Sele ambao nao wanahitaji kuingia kwenye ukoo huo, alitamani warudi utotoni ili akawafungie ndani.
Anna alikuwa anamuwaza mwanae Mwita ambaye ni mmoja wa watu kwenye ukoo huo ambaye naye tayari alikwisha mbaka dadaye Tusa.
Ukoo ulijaa laana na ulinuka laana ambayo kiini chake hakikujulikana kwa wakati, hadi pale Mwita alipotoa barua ambayo iliachwa na Maiko kuhusu Mashaka. Barua ambayo bi.Rehema aliichukua na kuiangalia.
MWITA: Nadhani maelezo ya humu yanaweza kutupatia hata taswira ya nini kilitokea hadi kupelekea kuwa hivi, haya ni makosa yaliyofanyika tangu awali na hayakupatiwa ufumbuzi mapema ndomana ukoo umeweza kutoa magaidi ya kutosha.
Mwita aliongea hivyo kwani hata yeye mwenyewe hakuwa na tofauti sana na magaidi yaliyotangulia na ndiomana aliweza kumbaka hata dada yake bila ya kujua.
Tusa alimwangalia sana Mwita kwa kujiongelesha kuwa ukoo wao umejawa na magaidi ya kutosha.
Akajisemea moyoni,
"Ingekuwa amri yangu haya magaidi ya ukoo huu yote ningeyafyekelea mbali kasoro Patrick"
Tusa alijikuta akijawa na imani sana juu ya Patrick ingawa alishamfanyia mambo mengi mabaya.
Kila mmoja alikuwa akiwaza yake kwa muda huo kwani hakuna aliyeongea akaeleweka kwa mwingine moja kwa moja, mara gafla bi.Rehema akaanza kulia.
Gafla bi.Rehema akaanza kulia.
Wote wakamtazama kwa mshangao na kumuuliza kwanini analia,
REHEMA: Hii barua ya Mashaka imeniumiza sana na kunikumbusha vitu vingi vilivyopita.
ADAMU: Vitu gani mama?
REHEMA: Yani Tusa anaposema kuwa ukoo huu umelaaniwa hata hajakosea, tatizo limekuwa ndani ya chimbuko la ukoo wenyewe.
FAUSTA: Tueleze tupate kujua maana tushachanganyikiwa tayari.
REHEMA: Nitawaeleza kile ninachokifahamu na maelezo mengine mtayapata kwenye hii barua ya Mashaka.
Wote wakatulia ili kumsikiliza bi.Rehema maana hali ya ukoo huo tayari ishakuwa tete na inatakiwa wairekebishe kabla ya vizazi vyao vitakavyokuja mbele.
Bi.Rehema akaanza kuelezea,
"Baba yangu kwao walizaliwa mapacha yani yeye na bamdogo ambaye ni baba yake na Neema ambaye ndio mama wa Fausta na Pamela.
Baba alimuoa mama yangu na bamdogo alimuoa mama yake na Neema, kuzaliwa kwangu na Neema hakukutofautiana sana yani tulifatana sana kuzaliwa na wakatuweka kama mapacha ndomana mimi nikaitwa Rehema na yeye Neema.
Familia zetu tulipendana sana na tulikuwa tukitembeleana kila mara, haikuwa kitu cha ajabu mimi kulala kwa bamdogo au Neema kulala kwetu.
Siku zikapita taratibu na mapendo kati yetu yakaendelea kukua hadi alipokuja huyu mwanamke kwenye maisha yetu, mwanamke ambaye mimi namfananisha na shetani kwani alisambaratisha familia yetu yote na upendo wote kati yetu ukafa sababu ya huyu mwanamke.
Na hapa nikapata kujua mengi, si kila anayekuja kwenye familia ni mtu mwema wengine ni waharibifu na haitakiwi kumuamini kila mtu katika maisha wengine hawaaminiki na hawatakiwi kuaminiwa.
Kwa kipindi hiko nilikuwa mtoto wa pekee kwa baba yangu na mama alikuwa na ujauzito ambao nilitarajia kupata mdogo wangu.
Siku moja nilimsikia baba akizozana na mama, inaonyesha kuwa baba alikuwa akimwambia mama kuwa amepata mwanamke mwingine na anataka kumuoa. Mama akapinga swala la baba kuoa mke mwingine kwani mama yangu hakutaka uke wenza ila baba akaoa kwa lazima huyo mwanamke ambaye mimi namfananisha na shetani.
Mama hakukubali kumkaribisha huyo mwanamke kwenye nyumba yake, ni hapo kwa mara ya kwanza nilishuhudia baba akimpiga sana mama na alimpiga kweli bila ya kujali ujauzito aliokuwa nao. Roho iliniuma sana ila kwa utoto ule sikuwa na la kufanya.
Kesho yake mama aliamka vidonda mwili mzima, yule mwanamke alimwangalia mama na kumcheka huku akimkejeli.
Mama hakuweza kuvumilia, baba aliporudi akamdai taraka ili arudi kwao kwani hawezi kuishi na mtu ambaye hawaelewani ila baba alikataa kumpa mama taraka.
Kwa hali isiyotegemewa, siku hiyo nilimuona yule mwanamke akiingia chumbani kwa mama wakati mama amelala na baada ya muda akatoka, mimi nikakimbia kuona kuna nini maana yule mwanamke hakupatana na mama, ni hapo nilipokuta mama akiwa chini kabisa hajitambui, nikajaribu kumuamsha lakini hakuamka nikapiga yowe na watu wakafika badae nikaambiwa kuwa mama yangu amefariki nililia sana yule mwanamke akaniambia nisijari yeye atanilea ila bado nililia kwani upendo wa mama hakuna wa kufananisha nacho.
Baada ya msiba nilimueleza baba kuwa kabla ya kifo cha mama yule mwanamke aliingia mule ndani, nikamwambia kuwa nahisi amemuua mama ila baba alinikataza na kuniambia kuwa sitakiwi kuhisi watu vibaya.
Maisha yakaendelea na huyu mama mpya aliyejaa vitimbwi vya kila siku.
Akapata ujauzito, ni hapo ambapo baba akaanza kunichukia mimi na nikaamua kukimbilia kwa bibi, naye bibi akaniambia kuwa nisijari ni hali ya muda mfupi tu.
Nikiwa kwa bibi tukapata taarifa kuwa mama yake na Neema amefariki tena kifo cha gafla kabisa kwakweli nilisononeshwa sana kwani na yeye nilimuona kama mama yangu.
Kwahiyo Neema hakuwa na mama na mimi sikuwa na mama zaidi ya yule mwanamke wa baba.
Siku moja nikiwa kwa bibi na Neema, Neema akaniambia kuwa amekutana na yule mwanamke na amempa pole ya kufiwa na kumwambia kuwa asijari atamlea.
Tukafikiri kuwa labda yule mwanamke ana moyo wa upendo ila haikuwa vile tulivyodhani.
Laiti baba angejua kama yule mwanamke anafata mali basi hata asingelazimisha kumuoa.
Yule mwanamke ilikuwa kama una mali basi utampata.
Akajifungua mtoto wa kiume ambaye baba alimuita Mashaka, kwakweli baba alimpenda sana Mashaka kuliko mimi kwavile Mashaka alikuwa mtoto wa kiume na siku zote baba alitaka mtoto wa kiume atakayeongoza familia na kurithi mali zake.
Mashaka alipofikisha miaka miwili tabia ya mama yake ilibadilika zaidi, mara nyingi hakuonekana nyumbani wala wapi.
Kuna kipindi akapotea kwa miezi miwili, baba akamtafuta sana kuja kugundua kumbe anaishi kwa bamdogo huko anapika na kupakua.
Kwakweli sijui huyu mwanamke aliwapa nini baba zangu hawa.
Kikawekwa kikao cha familia na yule mwanamke alikiri kuwa ana ujauzito aliopewa na bamdogo.
Ikabidi bamdogo na baba waamue moja kuwa nani abaki na yule mwanamke, wote waligoma kwani baba alitaka kurudi na yule mwanamke nyumbani kwakuwa ni mke wake na wana mtoto mdogo na bamdogo nae akataka aende na yule mwanamke kwake kwakuwa ana ujauzito wake, wote wawili walimng'ang'ania ndipo wazee walipomtaka yule mwanamke achague na hawakuweza kumpa adhabu sababu ya ule ujauzito.
Yule mwanamke akachagua kwenda kwa bamdogo.
Yule mwanamke misingi yake ilikuwa ni kwa mwanaume mwenye mali na kwavile bamdogo alikuwa na mali nyingi kushinda baba ndio akachagua huko.
Ilimuuma sana baba yangu tena sana ukizingatia yule mwanamke amemtafuta mwenyewe.
Ndipo baba alipotamka kauli kuwa yeye na bamdogo wasijuane tena na undugu wao ufe, na bamdogo nae akaafiki, sijui huyu mwanamke alikuwa na mimi hadi kuweza kuua undugu wa mapacha wale.
Wazee walijitahidi sana kusuruhisha lakini ilishindikana, vikao vingi vikawekwa kwaajili ya baba na bamdogo ila bado hawakupatana.
Undugu ulikufa kabisa, si mimi wala Neema tulioruhusiwa kuonana.
Roho iliniuma sana kutenganishwa na Neema ila sikuwa na la kufanya kwani yalikuwa ni maswala ya familia.
Mara moja moja nilionana na Neema kwa bibi na alikuwa akinieleza jinsi vile mwanamke yule alivyomchoyo, Neema alikonda sana utafikiri baba yake hakuwa mtu mwenye mali nyingi.
Baada ya bibi kufariki ukawa ni mwisho wa mimi na Neema kuonana hadi ambapo nimekutana na watoto wake wawili Fausta na Pamela ambao wameingia kwenye majanga na watoto wangu.
Kwenye kukua kwangu nilikuwa na mdogo wangu Mashaka ambaye badae tabia yake ilibadilika sana.
Kwani mimi nilipoanzisha mahusiano na mzee Ayubu hadi kupata ujauzito, nyumbani walikataa nisiolewe nae kwakuwa tumetofautiana kabila.
Kwetu hawakutaka mtu aolewe na kabila tofauti, hivyo basi nilipojifungua wale mapacha na kukua kua kidogo tukaamua kugawana watoto. Wazee hawakutaka kabisa mimi nionane tena na mzee Ayubu na akafukuzwa pale kwenye kijiji chetu ndipo alipoondoka na mwanangu Jumanne na mimi kubakiwa na Juma, sikupata kumuona tena mzee Ayubu hadi pale kwenye mazishi yake.
Nilibahatika kuolewa kule kijijini na kupata mtoto wa kike, ila Mashaka aliniulia mwanangu na kufanya niachike nilipoolewa na hapo wakagundua kuwa akili ya Mashaka si nzuri, akakamatwa na kupelekwa Mirembe.
Mara ya mwisho kurudi nyumbani akadai amepona, nilimpokea kwakuwa ni mdogo wangu ila akaja kutoroka na mwanangu Juma ambaye ndio huyo nimemjua ukubwani akiwa gaidi wa kutupwa huku akitumia jina Maiko.
Kwakweli mdogo wangu Mashaka ameniumiza sana tena sana"
Bi.Rehema alimaliza huku akijifuta machozi, Deborah akauliza.
DEBORAH: Inamaana huyo mwanamke aliwapa dawa mama zenu za kuwaua au aliwapa dawa baba zenu za kumpenda?
FAUSTA: Labda aliwapa limbwata, ndiomana familia hii haieleweki. Ilitakiwa pale mwanzoni kumtokomeza huyu shetani ambaye alijivaa kwa mwanamke huyo ila kwa kipindi hiko hayakuonekana madhara makubwa kama haya.
REHEMA: Barua aliyoandika Mashaka ndiyo iliyoniliza sana, Mashaka hakuwa mtu mzuri kabisa.
Ikabidi Patrick aichukue ile barua na kuanza kuisoma,
"Mimi Mashaka, natumaini kama mmeipata barua hii na kuisoma basi sipo tena duniani ila maandishi yangu tu ndio yaliyobaki.
Najua kwa yeyote atakayesoma barua hii hatokuwa na maswali zaidi kwangu kwani hata kama akiwa nayo hayo maswali sitaweza kumjibu kwavile sipo tena duniani ila nadhani mtanielewa kwa kile nilichoandika na mtaelewa kwanini nipo kama nilivyokuwa.
Katika kukua kwangu sikufurahia kabisa maisha ya kukua bila mama tena huku nikiambiwa kuwa mama yupo kwenye familia nyingine ya bamdogo.
Kuna wakati nilikuwa nakutana na mama kinyemela akiniambia vitu vingi kuwa bado anampenda baba sema bamdogo kambana, nilitamani nikue upesi ili niweze kupapambana na bamdogo. Kwani nilidhani kuwa bamdogo ndio mtu mbaya kwa kumuiba mama toka kwa baba. Lakini bamdogo hakuwahi kulihisi hilo na hakuwahi kunifukuza nyumbani kwake ila nilimchukia sana.
Katika kukua kwangu niliwaza jambo moja tu kupapambana na bamdogo ambaye sikuwahi hata kuishi naye.
Mama hakuruhusiwa kufika nyumbani ndiomana nilikuwa naonana nae kinyemela.
Ila nilipokua nilianza kwenda mwenyewe kwa bamdogo kumsalimia mama ambaye alikuwa na mtoto wa kike, bamdogo hakuwa mtu mbaya ila mama alisisitiza kuwa bamdogo ni mtu mbaya na anamtesa sana, anatamani kurudi kwa baba ila anashindwa kwasababu ya kubanwa nae. Nilimuahidi mama kuwa nitamsaidia kwahiyo asijari kitu. Upande wa baba sikuwa na shaka nao kwani najua kuwa baba alimpenda mama na bado aliendelea kumpenda ingawa kwa kipindi hiko alikuwa ameweka mke mwingine nyumbani kwaajili ya kujiliwaza tu.
Kwa mara ya kwanza nikaamua kufanya kitu cha ajabu pale kwa bamdogo ili kumfurahisha mama.
Ila ilikuwa kinyume kwani kitu nilichofanya ndio kilichofanya niwe kama nilivyokuwa.
kitu nilichofanya ndio kilichofanya niwe kama nilivyokuwa.
Ila niliomba ushauri kwanza, kipindi hiko nilikuwa na mpenzi wa kuitwa Maria.
Nadhani Maria hakuwa mshauri mzuri kwangu kwani yeye alitakiwa kunikataza kitu hiki cha hatari ila yeye aliniruhusu na kunielekeza njia ya kufanya.
Siku hiyo nilikuwa na Maria nikamweleza kila kitu kuhusu familia yangu na kumwambia kuwa nataka kummaliza bamdogo yani kumuua kwani nilijua kwa kufanya hivyo kutampa nafasi mama ya kurudi tena kwa baba, Maria akaniambia kuwa kama nimeamua hivyo basi ni sawa na nikamuuliza nifanyeje akaniambia nitumie sumu, nimuwekee yule baba kwenye chakula anachopenda sana.
Sikuwa mtaalamu sana na maswala ya simu ila Maria alizijua sumu porini.
Sikutaka kumshirikisha mama kwa hili kwani angeniona mtoto wake ni muuaji. Wala sikutaka kumshirikisha mdogo wangu mzuri wa kike aliyezaliwa na mama kwa kupitia bamdogo, mdogo wangu mzuri Chaurembo aliyekuwa mrembo kweli kama jina lake.
Nilipokuwa tayari kwa zoezi hilo, Maria akanipeleka porini na kunichumia majani hayo ya sumu.
Akaenda kuyaponda kisha kuyachanganya na maji na kuyachuja halafu akaweka kwenye kichupa na kunikabidhi, aliniambia kuwa ile ni sumu inayoua mara moja na kweli kwa hilo hakuongopa kabisa.
Siku hiyo nikaenda kwa bamdogo kwa lengo moja la kummaliza tu.
Nilipofika nikakuta mama ameandaa chakula mezani, nikamwambia mama kuwa nina njaa ila mama akaniambia nisile kile chakula ni cha baba. Ningoje ataniandalia changu, kwakweli niliposikia hivyo nilifurahi sana, nikavizia mama ametoka nje nami nikafunua kichupa changu cha dawa na kutia kwenye bakuli la mboga ambayo ilikuwa ni nyama ya kuku iliyoungwa vizuri sana.
Baada ya kutia ile dawa, mama akaniita nje akaniambia nimuendee kwa fundi nguo kumchukulia nguo yake halafu nikirudi nitakuta chakula changu kiukweli nilichukia kwani nilitaka kumshuhudia yule baba akila kile chakula nikamuuliza kuwa kwanini asingewatuma wakina Neema na Chaurembo? Mama akaniambia kuwa nao wametoka kidogo, wamepeleka maziwa kwa wateja wao ikabidi nisibishe sana. Niliamua kwenda aliponituma mama huku nikiamini kuwa nitakaporudi lazima nitapata habari ya msiba tu.
Nilipotoka kwa fundi na nguo ya mama kwenye mfuko, nilimkuta Neema akiwa nje amekaa huku akisononeka nikajua lazima mambo yameharibika tayari nikamuuliza mbona yupo nje akaniambia kuwa njaa inamuuma, nikamshangaa wakati chakula kipo ndani nikajiuliza labda anangoja baba yake ale kwanza.
Nikamuuliza kwanini asile, alinijibu
"Mama kaniambia nisile hadi niende kuchukua mahindi kule bondeni wakati baba amekataa kula kile chakula alichoandaliwa nae amesema ameshiba, baada ya kuniachia mimi na Chaurembo tule kile chakula eti yeye ndio kaamua kula na Chaurembo sijui kwavile mimi sio mwanae wa......"
Kabla hajamalizia ile sentensi nilihisi kama moyo wangu umeripuka, niliangusha ule mfuko pale pale na kukimbilia ndani.
Nilimkuta mama akiwa chini huku akitapatapa, mdogo wangu Chaurembo ndio hakutamanika kabisa pale chini. Nilimuita Neema kwa nguvu na kumwambia alete maziwa ili tujaribu kuwanusuru ila ilisemekana kuwa maziwa yote yaliuzwa na yaliyobaki mama aliyaficha, hali ilikuwa mbaya sana ila Neema alienda kuomba maziwa kwa majirani huku tukijaribu kutafuta uwezekano wa kuwawahisha hospitali. Kwakweli ilikuwa kazi ngumu kwani hata maziwa aliyoleta Neema nayo hayakusaidia na kufika nao hospitali walikuwa tayari marehemu.
Hili lilikuwa ni pigo kubwa sana kwangu hata pale msiba ulipoisha bado nilikuwa na pigo kubwa sana.
Nilijikuta nikimchukia Maria kupita maelezo kamavile yeye ndiye aliyeshauri kuwa niue.
Ila sikuachana nae kwavile bado nilikuwa nampenda.
Ila moyoni nilikuwa namuwazia mawazo mabaya sana Maria bila ya yeye kujua laiti kama angejua basi angejiepusha na mimi mapema sana.
Nilikuwa mtu wa mawazo tu na kumuona kwangu bamdogo nikaona kama akinizidishia maumivu tu ya kuendelea kumkumbuka mama yangu.
Nikafanya mpango wa kummaliza bamdogo ila bado ilishindikana.
Kipindi hicho nyumbani kulikuwa na mgogoro wa dada yangu Rehema na mwanaume ambaye amezaa nae, wakati tukirumbana hadi kufikia kugawana wala watoto na yule mwanaume kufukuzwa pale kijijini kumbe Maria nae alikuwa amejifungua mtoto wangu ila alikaa kimya bila hata ya kuniambia.
Bado nilikuwa na uchungu juu ya bamdogo na kipindi hicho baba na bamdogo walianza kupatana patana tena, na mimi nikaitumia nafasi hiyo kummaliza bamdogo.
Nikaweka mtego shambani kwa bamdogo kwa bahati mbaya baba na bamdogo walienda pamoja kwenye lile shamba na ule mtego ukamvaa baba yangu na kummaliza papo hapo.
Ukoo mzima ukamchukia bamdogo na kumwambia kuwa ndio chanzo, bamdogo akafukuzwa pale kijijini na akaondoka na binti yake Neema kwenda kuanza maisha mengine kabisa.
Roho iliniuma kwa kusababisha kifo cha baba na mama na mdogo wangu ila yote ni katika harakati za kummaliza bamdogo.
Nikawa kama vile mtu aliyechanganyikiwa, nikapotea nyumbani na kuzamia Mombasa, nilikaa huko kwa miaka mitano huku nikipanga namna ya kummaliza bamdogo.
http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Niliporudi bado sikuwa na amani ya moyo, nilimkuta dada ameolewa ila akiwa mjamzito tena na katoto kake ka kwanza kakiwa kamekua kua vya kutosha.
Nikapata wazo la kumtembelea Maria, nikamkuta nae akiwa na mtoto halafu ni mjamzito.
Nilichukia sana, nilipomuuliza alidai kuwa yule mtoto ni wangu ila hakuniambia kwavile nilipotea ila ule ujauzito kuna mwanaume amempata, kuja kufatilia nikagundua kuwa huyo mwanaume ndio yule aliyezaa na dada yangu mtoto wa kwanza, roho ikaniuma sana kuona yule mwanaume kaona haitoshi kuniharibia dada yangu na sasa amehamia kwa mchumba wangu.
Nikaapa kuwa lazima nije kulipa kisasi.
Ila labla ya kuanza mapinduzi ya kisasi niliamua kwanza kuondoka na wale watoto wa kiume ili nikawafunze kazi huko Mombasa.
Dada nikamdanganya kuwa natoka na mwanae mara moja, kisha nikaenda nae hadi kijiji cha kina Maria na kumchukua mwanangu huku nikidai kuwa naenda kutembea nae tu.
Kwakweli watoto hawa wawili niliweza kuwatofautisha kwa majina tu ukizingatia sijaishi nao.
Niliondoka na watoto wale hadi Mombasa, nikakaa huko kwa siku chache kisha nikawakabidhi kwa rafiki yangu na mimi kurudi tena kijijini, lengo lilikuwa ni kumshawishi dada yangu ili niende nae Mombasa ila ile kurudi tu kijijini dada yangu akaanza kunishambulia kwa maneno na kunidai mtoto wake ila alikuwa ameshajifungua na ana mtoto mchanga, nikaachana nae pale na kuelekea kwa Maria kwani nilijua kuwa na yeye lazima atakuwa amejifungua, moyoni nikajisemea kuwa lazima nikammalize huyo mwanaume.
Nilipofika kwa Maria naye alianza kunidai mtoto wake na yule mwanaume sikumuona, nikaona Maria ananiletea longolongo tu hivyo hata sikumchelewesha, nilichukua kisu na kumchoma nacho tumboni yani sikuwa na huruma kabisa kisha nikaondoka.
Kurudi tena kwa dada naye akawa anadai mtoto wake namwambia yuko Mombasa hataki kunielewa anamtaka mwanae halafu akaniitia polisi.
Nilikuwa kama mtu niliyechanganyikiwa, nilijikuta nikimnyanyua yule mtoto mchanga wa dada na kumuinua juu kisha kumbamiza chini kama mzigo, na alilia mlio mmoja tu kisha ikawa kimya.
Wale mapolisi wakaona wanikamate kinguvu ili kuepusha majanga mengine.
Nikapelekwa jela ila mambo ambayo nilikuwa nafanya humo ikaonekana kama vile sina akili nzuri, hivyo wakanipeleka jela ya vichaa na kwakweli nilikuwa kichaa kwa kipindi hiko kwani nilifanya mambo ya ajabu hadi ya kujishtukia.
Nilikaa jela kwa miaka mitano kasoro, badae nikaanza kutafuta namna ya kutoroka pale gerezani.
Nilipopata nafasi sikuangalia nyuma nilitoroka moja kwa moja na kukimbilia kwa bamdogo kule ambako alikuwa amehamia tangia kifo cha baba, ni mimi tu niliyepajua kwa bamdogo kwakuwa ndugu zake na ukoo mzima walimtenga nami nikaona kuwa kule nitakuwa salama zaidi.
Nilimkuta Neema akiwa na mabinti wawili kwa kuwakadilia miaka huyu mkubwa alikuwa na miaka nane na mdogo miaka minne.
Pale kwa bamdogo hapakuwa na tatizo kwani Neema alinihudumia vizuri sana tatizo lilikuwa kwa huyu binti yake mkubwa huyu wa kuitwa Fausta alikuwa na nyodo sana halafu alikuwa ananidharau sana mara nikiwekewa chakula aseme kuwa mimi nakula sana, nikimtuma kitu anakataa kwakweli huyu binti alikuwa ananikera sana na kama ingekuwa amri yangu basi ningekimaliza muda mrefu sana.
Roho iliniuma kwa kusodolewa na binti mdogo kama Fausta ila nikawa navumilia tu, kitu kibaya ni kuwa Neema hakuweza kumgombeza mtoto wake huyo ingawa alikuwa anaona mambo ya ajabu aliyokuwa ananifanyia, ukimwambia anajibu ni utoto tu huo msamehe bure dah huyu mtoto nilimchukia sana.
Nilikaa kwa bamdogo miaka miwili kasoro hadi pale Fausta ambaye anatetewa na mama yake kuwa ni utoto alipokwenda kunishtaki polisi kuwa mimi ni muharifu, nilishangaa mapolisi kuja na kunikamata.
Nilichukia sana na kuapa kuwa laziama nimmalize yule mtoto nikitoka jela.
Safari hii nilikaa tena jela kwa miaka mitatu hadi pale nilipopata nafasi ya kutoroka ila niliwapa mapolisi wawili sumu na nilipotoka jela safari yangu ilikuwa ni kwa bamdogo kwa lengo la kummaliza Fausta.
Kufika pale nilimkuta mama yao ndani, nilipomuuliza alikataa kunitajia Fausta alipo hata nilipojaribu kumtishia bado hakutaja, nikaona ananiwekea usiku tu nikachukua kisu na kumchoma nacho habari yake ikaisha.
Wakati natoka nikakutana na bamdogo mlangoni.
Bila kuchelewesha muda nilimchoma na kisu ili kupoteza ushahidi kisha nikaingia chumbani na kusomba pesa zote milizozikuta na kuondoka nazo, zikaniwezesha kusafiri na kwenda tena Mombasa.
Kufika kule niliwakuta watoto wamekua kweli ila bado waliwataka mama zao nikawaambia kuwa mama zao wamekufa ila hawakutaka kukubali, Maiko alipoona nimebadilika akatulia ila Juma alijifanya mbishi na kuendelea kunisumbua sana, sikutaka kero hivyobasi nikamfyekelea mbali huku nikijua nimemfyeka mtoto wa dada yangu kumbe nimemfyeka mwanangu na kumuacha mtoto wa dada yangu dah Maiko ni mshenzi sana.
Nikawa nafanya biashara za magendo na watu wa kule ila kila leo biashara za magendo zinatanuka hadi kufikia kuuza viungo vya watu, nikasafiri nchi nyingi kupeleka viungo hivyo na nikawa na pesa nyingi pia ni hapo nilipoamua kulipa kisasi kwa yeyote niliyejisikia kummaliza, hata oda ya kummaliza mzee Ayubu niliitoa mimi kwani alitembea na mpenzi wangu.
Katika kisasi changu nimesumbuliwa na kiumbe mmoja tu huyu wa kuitwa Fausta. Mungu akupe maisha marefu ila ukweli ni kwamba nakuchukia sana na ningekumaliza siku nyingi sana wewe.
Najua mpo mtakaoumizwa na hii barua ila ndio hivyo yalishatokea ya kutokea.
Na katika watu walioniharibia mpango wangu wa kuwa bilionea kwasasa ni huyu wa kuitwa Patrick, nakuchukia sana wewe kijana. Umeharibu maisha yangu sana.
Ila samahanini kwa yote niliyowakosea, ni mimi MASHAKA"
Kila mmoja alijikuta akipumua kwa nguvu baada ya ile barua.
Kila mmoja alikuwa kimya kabisa, Deborah akauvunja ukimya ule.
DEBORAH: Jamani kila mmoja nadhani amesikia maelezo ya hiyo barua.
REHEMA: Yani nimeumizwa sana kuona mdogo wangu alifanya vitendo vya makusudi kiasi hiko. Ameharibu ukoo mzima.
DEBORAH: Ni kweli ila kinachotakiwa ni kuvunja hiyo laana kwenye ukoo wenu.
REHEMA: Kitu kingine ni ndoa ya Pamela na Adamu, nyie wawili mlikosea sana kuoana ndugu sasa watoto wenu mtawaweka wapi?
Amina alikuwa ameinama na kutoa machozi ukizingatia kifo cha mtoto wake Tulo halafu na barua iliyosomwa ilimuumiza sana, naye akaamua kusema.
AMINA: Jamani huyo Maria ndio mama yangu mzazi ambaye nilipewa habari kuwa aliuliwa kikatili kumbe aliyemuua ni huyu jamaa!!
Amina alisikitika sana na wakaamua kumbembeleza.
DEBORAH: Mmh!! Na huyo mzee Ayubu nae ilikuwaje kuzaa na huyu na huyu na huyu?
REHEMA: Ngoja nimtetee kwa hilo, kwanza kabisa alizaa na mimi ila kwetu wakamkataa na tukagawana watoto, pili akazaa na Neema nadhani bamdogo pia alimkataa kwakuwa bado anasheria za kule, tatu akaenda kuzaa na huyo Maria ambaye aliuliwa na Mashaka kwakweli hakuwa na la kufanya hapo jamani. Ila ninachomlaumu ni kuwa alipoona kijiji hakimtaki angehama kabisa na asingethubutu kuzaa na mwanamke mwingine yeyote wa karibu ila nadhani kifo cha Maria ndio kilichomkimbiza Morogoro, pole sana mzee Ayubu.
Ikabidi wajadili hatma ya Tusa na Patrick, safari hii Patrick bila kinyongo akaamua kuachana na Tusa kwa amani tu ili kuepusha mabalaa mengine katika ukoo.
PATRICK: Kwa hiyari yangu na kwa amani kabisa naamua kuachana na Tusa ila Deborah ataendelea kuwa mama yangu siku zote za maisha yangu.
Kauli ile ilimfurahisha sana Deborah kwani aliona swala la Patrick kuachana na Tusa ni swala zuri sana na pia ilikuwa furaha kwa Sele aliyempenda Tusa kupitiliza hata Tusa nae alifurahi ila kilichomuuma ni kuwa kwanini Patrick atokee kuwa kaka yake.
Adamu na Pamela waliumia kitu kimoja kikubwa nacho ni kukataliwa na Patrick.
Marium bado alikuwa na swali kwa mwanae kuwa kwanini hawezi kuachana na Tusa.
MARIUM: Hivi mwanangu Sele huyu mwanamke alikupa nini hadi hutaki kumuacha?
SELE: Mama, mimi na Tusa tulikula kiapo cha milele najua Tusa hawezi kuishi na mwanaume yeyote ila mimi. Nampenda sana naye ananipenda sana.
PATRICK: Ni kweli kabisa asemavyo Sele, Tusa hawezi kuishi na mwanaume yeyote yule. Kwa jinsi ambavyo nimeishi na Tusa na mambo mengi niliyomfanyia ni wazi kuwa Tusa hawezi kuishi na mwanaume yeyote zaidi ya huyo Sele.
DEBORAH: Kama ndio hivyo tuwaache waoane tu maana wanapendana, ingekuwa mwanaume mwingine angemuacha Tusa kitambo kwa mapito aliyopitia ila kwakuwa Sele ana mapenzi ya dhati basi na amuoe Tusa.
PATRICK: Sele anapaswa kuigwa kwenye jamii, na nitasimamia harusi yao yote.
Tusa alimshangaa sana Patrick kwani hakuwazia kuwa ipo siku Patrick atakuwa ni mwanaume wa kutamka maneno mazuri kiasi kile.
Mwita nae aliungana na ndugu zake na kuamua kuvunja laana zote ambazo zimeikumba hiyo familia.
Harusi ikapangwa kisha Sele na Tusa wakafunga ndoa.
Kila mmoja aliwatakia maisha marefu Sele na Tusa, kisha Deborah akamwambia Sele.
DEBORAH: Natumaini utakuwa mume mwema, nawatakia maisha marefu na usithubutu kuwa kama MUME GAIDI, pesa tafuta kwa njia halali na Mungu atakuwezesha.
Waliyafurahia yale mahusia na kupiga makofi.
Baada ya hapo kikafanyika kikao cha mwisho cha familia na hapo ndipo Yuda nae akatangaza kumuoa Tina na hukuna aliyepinga.
Deborah aliamua kuwaaga na ndugu zake kuwa wanataka kurudi kwao Mwanza ila kabla ya kuondoka Patrick aliweka sherehe ya kuagana na familia ya kina Tusa.
Katika sherehe hiyo alimsimamisha Deborah na kuongea maneno haya,
"Huyu mwanamke mnayemuona mbele yenu, ndiye mama yangu, chakula changu, furaha yangu, amani yangu na kila kitu katika maisha yangu. Nampenda sana huyu mama, sitamtupa wala kumtenga hadi naingia kaburini"
Kisha akamuangalia kwa karibu Deborah na kumwambia,
"Nakupenda sana mama"http://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akamkumbatia kwa furaha na kesho yake wakasafiri kurudi Mwanza wakiwa na furaha iliyopitiliza.
Pamela aliumia sana na kujiona kuwa na mkosi mkubwa sana maishani mwake. Kitendo cha kumtupa mtoto kilimuumiza sana.
Walipokuwa Mwanza, siku hiyo Patrick alilala usiku na kutokewa na mzimu wa mzee Ayubu kisha ukampungia mkono kama ishara ya kumuaga tena huku akitabasamu.
MWISHO

0 Comments