Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Uchawi wa mama mkwe sehemu ya nane (08)

 


“Mama?”

“Ndiyo anahusika na…?”

“Anahusika na nini wakati tukio linatokea alikuwa hapa nyumbani?”

“Hapana. Ametajwa na yule mchawi aliyenasa ambaye tunamshikilia kituoni.”

“Mchawi?”

“Kwani mzee huna habari kwamba hapo kwa jirani yako kuna mchawi leo usiku amenaswa?”

“Najua na mke wangu nimemuagiza amsindikize shoga yake.”

“Yupo kwenye gari na shoga yake. Alijaribu kukataa tusije naye lakini nimemlazimisha na tunaye kwenye gari pamoja na majirani zako.”

“Ahaa, mke wangu shuka basi tujadili kabla mama hajachukuliwa,” akasema.

“Mzee huo siyo utaratibu, lakini muite na mzungumze,” alielekeza yule askari.

Nilishuka na kumfuata mume wangu. Tuliingia ndani na kumkuta mama mkwe akiwa ametoa macho kama vile amekabwa.

“Ehee huko polisi mambo yalikuwa vipi?” aliniuliza mume wangu kwa kunong’ona ili askari aliyekuwa nje ya nyumba yetu asiweze kutusikia.

“Yule mchawi kamtaja. Kasema walikuwa na mama mkwe lakini yeye ndiye aliyeingia ndani na mama akabaki nje,” nami nilimnong’oneza.

“Hakuna njia, inabidi tumsindikize.”

Tulitoka nje tukiwa na mama, kama ilivyo ada, watu wakajaa tele nje ya nyumba yetu wakitaka kujua kwa nini polisi wamefika tena kwa king’ora.Watu walizungumza mengi, wengine wakisema mama mkwe ndiye aliyesababisha yule mchawi anase, wengine wakawa wanasema naye aliingia ndani lakini kwa kuwa ni ‘mzima’ kishirikina, alichomoka na kumuacha yule mchawi kijana akiwa ameng’ang’ana sakafuni.

Lakini wapo waliopatia na kusema kwamba mama mkwe wangu alimsindikiza yule mchawi kuwamaliza wale majirani huku wengine wakimtoa kabisa na kuona kuwa yeye alikwenda kuwaonesha nyumba tu ili mchawi amalize kazi kwa wale jirani.

Mazungumzo hayo watu walikuwa wakiyasema kwa sauti na sisi wote tulikuwa tukiyasikia waziwazi na kumuongezea hofu mama mkwe wangu ambaye alikuwa hajui hasa atakachofanywa polisi.

Nilimuangalia nikamuona anatetemeka kama vile alikuwa anaumwa malaria kali kwani hata kanga ilikuwa inamshinda kuifunga ikawa inaanguka, uzuri ni kwamba ndani alikuwa na gauni refu.

Ilibidi kila wakati nimfuate na kumfunga vizuri kanga yake iliyokuwa ikianguka wakati tunakwenda kupanda gari la polisi.


Kabla sijapanda gari nilimuuliza mume wangu kama mtoto wetu Ajigale alikuwa ndani au la kwa sababu alitakiwa aende shule, akasema alimkodishia teksi na tayari ameshafika shuleni kwa sababu aliwasiliana na mwalimu wake wa darasa akamjuza.

Mama mkwe aliingizwa kwenye gari nami nikamfuata lakini mume wangu alikuwa akitufuata kwa nyuma akiwa kwenye gari lake.Kama tulivyokuja nyumbani, safari ya kurejea polisi ilikuwa fupi tulifika na kukuta watu kibao wakiwa wanangoja ili wajue kitakachoendelea.


BOFYA HAPA KUDOWNLOAD APP YA MFANIKIO


ITAENDELEA   


Post a Comment

0 Comments