Nje ya kituo cha polisi walikuwepo watu wengi mno kuliko wale tuliowaacha, habari zilishazagaa kwamba kuna mchawi amenasa kwenye nyumba moja na amepelekwa polisi.
Gazeti la Uwazi nalo likawa limetoa habari kuhusiana na mkasa huo ukurasa wa mbele. Lilikuwa limeandika kwa wino uliokolezwa ;Mchawi anaswa laivu'.
Bila shaka toleo lile lilikuwa maalum kutokana na habari yenyewe jinsi ilivyosisimua, nadhani bodi ya uhariri ikaona itoe habari ile ikisindikizwa na picha kibao zilizoenea ukurasa wote wa kwanza.
Naamini gazeti hilo lilichangia kufanya watu kujaa pale kituo cha polisi.
Mara baada ya gari la polisi kuingia kituoni, watu walilisogelea ili kumuona mchawi, hawakujua kuwa alikwisha ingizwa selo.
"Yupo wapi, yupo wapi," zilikuwa ni kelele za watu waliotaka kushuhudia.
Baadhi ya watu walidhani mchawi aliyenasa ni mama mkwe, lakini wengine wakawa wanabisha na kusema kwamba aliyenaswa ni mwanaume.
Gazeti ndilo lililokuwa likiaminiwa kwa hiyo niliona baadhi ya watu wakikusanyana kwenye makundi na kusoma mstari kwa mstari habari iliyoandikwa na Makongoro Oging' na Chande Abdallah kwenye kurasa za gazetini.
Tuliingia ndani ya chumba cha mahojiano na mama mkwe alianza kuhojiwa.
Baada ya kuulizwa jina lake na umri akaambiwa aanze kusimulia mkasa wa usiku uliosababisha yule mchawi anase kwenye nyumba ya watu.
"Ni kweli huyu mchawi alikuja nyumbani na wenzake na akataka afanye dawa kwenye nyumba ya huyu jirani, (akinyoosha kidole kuelekea kwa mwenye nyumba."
Polisi aliandika na baada ya kuona yupo kimya anasita kuendelea akamhoji:
"Ehee, ikawaje bibi?"
"Baadaye tulipofika kwenye nyumba, nilimuambia aingie yeye kwa sababu ndiye aliyekuwa na dawa za kutia ndani ya nyumba ile."
"Kwani dawa zile zilikuwa za nini?"
"Dawa za kudhuru."
"Kudhuru nini au nani?"
"Dawa za kudhuru watu."
"Kwa nini mlitaka mdhuru watu ambao hawajawakosea?"
"Ilikuwa ni amri ya mkuu wa wachawi."
"Mkuu wa wachawi? Ni nani huyo?"
"Anaitwa mzee Ngwamba."
"Mzee Ngwamba anaishi wapi?"
"Anaishi Kijiji cha Mabatani."
"Kwa hiyo wewe hujui sababu ya mzee Ngwamba kuamuru watu waliokuwa katika nyumba jirani kuwekewa dawa ya kuwadhuru?"
"Najua."
"Tueleze basi."
"Ni kwamba huyu bwana (alinyoosha mkono kumuelekeza askari aliyekuwa akihoji kwa baba mwenye nyumba ya jirani), alikuja pale nyumbani na mkewe, akawakuta mwanangu na mkwe wangu, akasema kuna wachawi wanakuja pale nyumbani kila siku."
"Ehee, baada ya kusema hivyo?"
"Huyu baba akasema baba yake anajua dawa ya kinga au zindiko la nyumba, hivyo alimuahidi kwamba leo angewapeleka."
"Kwa hiyo mzee Ngwamba alijuaje hayo?"
"Ni mimi nilimuambia."
"Na aliposikia hilo akasemaje?"
"Ndipo akaamuru kuwa wakawekewe dawa ili wamalizwe wasiweze kuwapeleka hawa kwa baba yake."
"Wewe mbona hujanasa, uliingia ndani ukatoka salama?"
"Hapana, mimi sikuingia, niliishia nje aliingia yule kijana tu, kazi yangu ilikuwa kuonesha nyumba ya hawa jirani."
"Baada ya hapo ikawaje?"
"Alipoingia ndani tu, akaniambia kuwa hawezi kunyanyua mguu kwenda mbele wala kurudi nyuma, kuona hivyo nilirudi nyumbani kumuambia mzee Ngwamba."
"Mzee Ngwamba baada ya kupata taarifa hizo alifanya nini?"
"Alitoa dawa akasema tukammwagie yule aliyenasa, tulikwenda lakini hakunasuka."
"Ehee, ikawaje?"
"Zilifanywa kila mbinu kwa kutumia dawa mbalimbali ili kumnasua lakini zote ziligonga mwamba ndipo wakaamua kuwa aachwe tu maana ilishindikana kumtoa."
"Asubuhi mambo yakawaje?"
"Nilimsikia mama mkwe wangu huyo hapo akimuamsha mwanangu na kumfahamisha kuwa kuna mchawi kanaswa, kachungulia dirishani na nikawa nasikia kelele nyingi za watu nikajua mambo yameharibika."
Maelezo mengi ya mama mkwe yalikuwa yakishabihiana na ya yule mchawi aliyenaswa. Lakini polisi walitaka kujua zaidi kuhusu lengo lake la kualika wachawi kuja nyumbani kwa mtoto wake.
"Sikuwa na lengo lingine isipokuwa nilitaka afundishwe uchawi ili nikifa aweze kurithi mikoba yangu," alisema mama mkwe hali iliyomfanya mwanaye, yaani jirani yangu kutokwa na jasho japokuwa kulikuwa hakuna joto pale ndani ya kituo cha polisi.
"Mama ina maana ulikuwa unataka unifundishe uchawi mama!" alidakia jirani yangu.
"Usiingilie mahojiano mzee. Elewa kwamba hapa ni polisi au niwatoe nje ya kituo?"
"Hapana. Nimeshangaa kumsikia mama anasema hayo aliyoyasema wakati mimi sijui chochote kuhusu hilo. Kama hivyo ndivyo mbona hakuniambia lolote baada ya tukio na kabla?"
"Mzee tuliza mori," alisisitiza polisi.
"Au niwatimue wote?"
Nilitamani nimnyamazishe yule jirani yangu kwa kuona kuwa tukitimuliwa, hatutajua mengi zaidi kuhusu kundi lile la wachawi.
"Sasa kwa nini mwanao hujamjulisha kuhusu ujuzi wa uchawi uliotaka arithi?"
"Ndiyo maana walikuwa wakija nyumbani wachawi wenzangu ili kumchukuwa na kujaribu kumpumbaza akili ili baadaye nikimuambia asipinge."
"Kwa hiyo ulijua kuwa ukimuambia angengataa?"
"Najua kabisa kuwa kama ningemuambia akiwa na akili zake timamu angekataa. Mara nyingi tuna uzoefu ni watu wachache sana ambao wakiambiwa watapewa uchawi wanakubali. Hawa wasomi huwa hawakubali na zaidi huwa wakali. Hawataki kabisa kusikia habari hiyo."
"Sisi polisi tuliambiwa mlitaka kuwaua jirani zenu hawa (huku akiwageukia wale jirani zetu) na ndiyo maana mkaenda kuingia ndani ya nyumba yao japokuwa wewe hukuingia. Hamkuona kuwa hilo lilikuwa kosa kubwa la kuua na kuingia nyumba ya watu?"
"Ni kweli mwenzangu aliingia ndani ya nyumba na akanasa kama mlivyomuona, mimi nilikaa nje, sikuingia, ilikuwa bahati yangu.""Kwani mnapofanya uchawi, mnapata faida gani?
Swali hilo mama mkwe hakujibu, alimuangalia yule polisi kisha akainamisha kichwa chini.
"Sasa itabidi tuwapeleke mahakamani, mama unasemaje?"
"Unataka nifungwe? Utapata faida gani? Acha kuwa na roho hiyo mwanangu!"
"Achana na faida, kwani wewe ulipokuwa ukifanya mambo haya ya ulozi ulikuwa unapata faida gani?"
Yule polisi aliyekuwa akimhoji mama mkwe aliandika mambo fulani kwenye jadala ambalo alikuwa analitumia kunakili mahojiano.
Alimuangalia mama mkwe kisha mwanaye na akanyanyua mkono wa simu ya mezani. Nilikuwa karibu naye nikaona anabonyeza namba moja, mbili nne kisha akaiweka sehemu ya kusikilizia sikioni.
"Mwambie Koplo Beti aje ofisini kwangu." Jibu la upande wa pili sikulisikia lakini yeye akajibu.
"Ndiyo, aje amchukue huyu bibi, mwambie achukue ufunguo wa mahabusu."
Nilijua kuwa huyo Koplo Beti alikuwa anakuja kwa ajili ya kazi moja; kumchukua mama mkwe na kwenda kumtupa mahabusu.Mama ni mama, nilimuona mume wangu akitetemeka baada ya yeye kujua kuwa mama yake anakuja kuchukuliwa na kwenda kufungiwa mahabusu.
Moyoni nilikuwa na furaha sana kuona sheria inaanza kufuata mkondo wake. Nilikuwa nawaza kama wangefanikiwa kumfanya mume wangu mchawi na kumrithisha mikoba ya kichawi mambo yangekuwaje.
Niliamini kuwa lile litakuwa fundisho kwake na wote ambao watasikia habari ile kupitia vyombo vya habari.
Wakati nawaza hayo, yule Koplo Beti akawa amefika.
Wakati nawaza hayo, yule Koplo Beti akawa ameshafika.
"Jambo afande?" akasalimia huku akipiga guu chini na kutoa saluti kwa mkuu wake wa kazi.
"Mchukue huyu bibi, kamfungie lokapu mpaka nitakapotoa maelekezo mengine."
"Haya bibi inuka, songa mbele," aliamuru yule askari wa kike.
Mama mkwe kwanza alionekana dhahiri kwamba alikuwa akishindwa kuinuka bila shaka kutokana na wasiwasi wa kwenda kufungiwa selo.
Mama mkwe na yule mchawi aliyenasa kwenye nyumba ya jirani wakawa wameshafungiwa lokapu.
Mume wangu alijitahidi kuomba kwa kamanda wa polisi ili mama yake asiwekwe ndani na badala yake amuwekee dhamana alishindwa.
"Unajua mzee, hatumuweki ndani huyu bibi ili kumkomoa, tunamuweka tukiwa na maana yetu," alisema yule kamanda wa
polisi."Nakuomba sana kamanda, kwa nini asiende kulala nyumbani na kesho nikamleta?" alizidi kuomba mume wangu.
"Sisi jeshi la polisi hatufanyi kazi kwa kubabaisha. Ni kwamba, kutokana na tukio analohusishwa nalo kuna taarifa za kintelejensia watu wenye hasira kali wanamsubiri ili wampige. Wanaweza kuchoma moto nyumba yako na ukapata hasara mara mbili.
Kuuawa kwa mama yako na kupoteza mali kwa kuchomwa nyumba na vitu vyako. Hatuwezi kujua. Wanaweza kujichukulia sheria mkononi usiku mkiwa mmelala."
"Sasa ina maana nimuache hapa polisi siyo?"
"Ndiyo maana yake. Elewa tukimuachia na balaa likazuka huko kwako, wakubwa wetu watatuona hatukutumia ujuzi wetu wa miaka mingi katika kazi hii, naomba sana usituponze na usijiponze pia."
"Ukimpa dhamana sitampeleka nyumbani, nitamhamishia kwa mtu mwingine, naomba sana."
"Mzee unasema tu, huko nje umechungulia? Kuna watu kibao wanasubiri kuwaona hawa. Wapo wenye magari na waendesha bodaboda. Watakufuatilia kwa nyuma kwa hiyo usitake kuhamishia tatizo hili katika nyumba ya mtu mwingine," alisema yule kamanda huku akifunika jalada la kesi hiyo, akainuka na kuliweka kabatini.
Tuliangaliana na mume wangu baada ya jibu la kamanda, akilini mwangu nilijisemea kwamba anachosema kiongozi huyo ni kweli kabisa, kwani nje ya kituo cha polisi kulikuwa na umati wa watu waliokuwa wakiimba; "Tunataka watolewe, wachawi hao, tuwaue."
Nilitishika sana kusikia maneno hayo ambayo yaliashiria kuwa watu walikuwa na hasira kubwa kwa mama mkwe na yule kijana mchawi aliyenasa ndani ya nyumba ya jirani.
Yule kamanda aliondoka ofisini kwake baada ya kulifungia jadala la maelezo ya mama mkwe na yule mchawi mwenzake na alituacha tukiwa mle ndani.
"Baba Ajigale unasikia huko nje, tutafakari sana kuhusu huyu mama, wanaweza kumuua hawa," nilimshauri mume wangu."Ni kweli mke wangu, nadhani tukubaliane na haya wanayosema polisi, tusing'ang'anie kumtoa."
Hakukuwa na njia nyingine isipokuwa kumsubiri kamanda ili tumuage na tuondoke. Wakati nawaza hili na lile yule kamanda aliingia akiwa na karatasi ambayo nilikuwa sijajua ilikuwa ya nini.
"Mzee, na nyinyi mlioingiliwa ndani na wachawi, mnaweza kwenda na RB ya kesi yenu hii hapa," alisema huku akimpa jirani yetu ile karatasi.
"Tafadhali tueleze utaratibu wa kesho," mume wangu alitaka ufafanuzi.
"Kesho tunatarajia kulipeleka jalada ofisi ya mkurugenzi wa mashitaka na kama litarudi tutaona watafunguliwa mashitaka gani. Cha muhimu ni kwamba jioni mleteeni chakula bi mkubwa," alishauri yule askari kamanda wa polisi.
Tuliondoka wote wanne, yaani mimi na mume wangu na jirani na mkewe hadi nyumbani. Tulijisikia aibu kutokana na kitendo cha mkwe wetu kwenda kwa jirani na kutaka kuwaangamiza.
* * *
Kulipopambazuka tulijiandaa kumpelekea bibi chai. Nilichemsha chai na maandazi na kuweka kapuni. Tulipofika polisi tulikuta mkusanyiko mkubwa wa askari, walipotuona wote waligeuza shingo zao kutuangalia.
"Mmekuja, jamani njooni ofisini kwangu," alisema yule kamanda wa jana.
Tulipokwenda akatuambia kuwa asubuhi alipokwenda kuwaangalia watuhumiwa waliokuwa lokapu, alikuta mama mkwe amefariki dunia.
Tulipigwa na butwaa na kuuliza maiti yake ipo wapi, kamanda alituambia kuwa tayari wameipeleka mochwari kuhifadhiwa.Binafsi sikuhuzunika sana nilijua kuwa hiyo yote ni mipango ya Mungu na niliamini kuwa ameniepushia na mambo mazito ambayo nilihisi yangeweza kutokea mbele ya safari.
Wakati nikitafakari hayo, mawazo yangu akamanda wa polisi.
“Daktari amempima amesema alikuwa na presha,” alisema.
Sikulia hata kidogo kutokana na matendo aliyokuwa anatufanyia.
INAENDELA
0 Comments