Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Beyond Love (Zaidi Ya Mapenzi) Sehemu Ya Kumi Na Nne (14)



“Kwa hiyo alivyokuja pale alikuja na mwanamke mwingine anayeitwa Juliana. Hata hivyo Mariam alivyomfuata alimtambulisha kwamba ana mpenzi mwingine, mbaya zaidi Juliana alimtukana Mariam hiyo ndiyo sababu iliyosababisha matatizo  yote haya!”

“Poleni sana, kwani Papaa Bill alikuwa hajui kwamba Mariam alikuwepo chuoni?”

“Alikuwa hajui!”

“Mbona sielewi kivipi?”

“Walipotezana muda mrefu sana na hata hivyo Papaa Bill alivyokuja Mariam hakujua kama ndiye mpenzi wake wa zamani!”

“Kwanini asijue?”

“Papaa Bill siyo jina lake halisi!”

“Kumbe anaitwa nani?”

“Tom!”

“Ok nimeanza kuelewa, tupeni nafasi kidogo tufanye kazi yetu!”

Pamela na wenzake wakatoka nje na kuwaachia wauguzi waendelee na kazi ya kumpatia matibabu Mariam. Jopo la madaktari watatu walikuwa bize kuhakikisha hali ya Mariam inakuwa nzuri.  Kazi ya kupandisha mapigo yake ya  moyo ilianza mara moja na matumaini yakaanza kuonekana.

Baadaye Muuguzi aliyekuwa akizungumza na akina Pamela  alitoka nje uso wake ukionyesha alikuwa na jambo la kuzungumza nao. Macho yake yalionyesha wasiwasi mwingi jambo ambalo liliwazidishia hofu Pamela na wanafunzi wengine waliokuwepo.

“Muuguzi nini kinaendelea huko ndani?” Pamela alikuwa wa kwanza kuuliza.

“Punguzeni hofu, Mariam anaendelea vizuri!”

“Ameamka?”

“Bado lakini hali si mbaya!”

“Ahsante Mungu!”

“Mnaweza  kwenda na kurejea kesho asubuhi!”

“Ahsante sana na Mungu akubariki!”

“Nanyi pia!”

****

Majina ya Tom na Mariam yalikuwa gumzo  chuo kizima, kila kona walikuwa wakizungumziwa wao,  hakuna hata mmoja aliyeelewa siri iliyokuwepo kati yao. Wengi walimwonea huruma sana Mariam lakini kuna ambao walimwona kama mtumwa wa mapenzi anayemng’ang’ania Tom kwa sababu ya fedha alizokuwa nazo.

Kilichokuwa nyuma ya pazia hakuna aliyekifahamu kwani ilikuwa ni siri kubwa iliyojificha katikati ya moyo wa Mariam ambaye alimweleza siri hiyo rafiki yake pekee Pamela.

“Hivi anaendeleaje Mariam?”

“Hajambo!”

“Ametoka?”

“Bado ila ameshapata fahamu!”

“Mh!”

“Mbona unaguna?”

“Sababu iliyompeleka hospitali!”

“Sasa hiyo ni ya kuuliza?’

“Ndiyo kila mtu anajua alianguka lakini sababu ya kuanguka kwake ndiyo inayonitatiza!”

“Si mapenzi?” Mwingine akadakia.

“Ishu sio mapenzi bali ni nani anayempenda!”

“Jamani huyu naye si Papaa Bill!”

“Sasa haoni kama hawaendani naye?”

“Msiingilie mambo ya watu hivi mnajua nguvu ya mapenzi ninyi?” Pamela aliuliza kwa ukali.

“Rafiki yako naye amezidi kujipendekeza kwa watu wenye fedha zao,  halafu anajifanya mgumu utafikiri binti mlokole, hajawahi kusimama na mwanaume hata siku moja lakini hii inashangaza mpaka akazimia?”

“Ndiyo maana nasema hamfahamu kitu kinachoendelea hivyo kaeni kimya!”

“Sasa kama  unajua si utuambie?”

“Ya ngoswe muachie ngoswe mwenyewe mmekuja kusoma au kujua ya watu?”

“Mh! Na wewe una majibu...shauri yako wewe mwendekeze tu huyo shoga yako!”

“Fyuuuu bakini  na umbea wenu!” Pamela akasema huku akisonya na kuondoka zake.


***

Siku tatu baadaye Muuguzi aliyekuwa akipita raundi  ya asubuhi alishangazwa na hali ya Mariam ambaye alikuwa ameanza kufumbua macho na kupepesa huku na kule. Mara moja muuguzi akasogea  katika kitanda cha Mariam kisha akaketi.

“Pole!”

“Ahsante!”

“Unajisikiaje sasa?”

“Sijambo, kwani hapa ni wapi?”

“Hospitali!”

“Hospitali?”

“Ndiyo!”

“Nililetwa hapa kufanya nini?”

“Uliletwa hapa ukiwa hujitambui umepoteza fahamu!”

“Mungu wangu!” Akili ya Mariam ikafanya kazi kwa haraka. Akavuta kumbukumbu tataribu.


Nataka kwenda kwa Tom...

Napanda kwenye gari lake...

Namkumbusha mimi ni nani...

Ananiambia ana mchumba...

Baadaye anamwita...

Ni mwanamke mrembo sana...

Anaonekana ana dharau...

Anavuta midomo yake...

Ananiambia mimi ni mwanamke mbaya...

Mimi mbaya?...

Nakimbilia chini ya daraja, nalia...

Pamela

“No! Haiwezekani Tom kwanini unanitesa kiasi hiki Tom? Mimi ni mwanamke mbaya kiasi hicho? Nimelala hospitali kwa miaka mitano kwa sababu ya kukuokoa uhai wa baba yako lakini haukujali yote hayo unaniletea mwanamke anitusi. Tom! Kwanini mimi?” Pale pale Mariam alianza kulia baada ya kukumbuka picha nzima ya tukio lote lilivyokuwa.

“Pole sana binti haya ndiyo maisha!”

“Lakini inaniuma sana!”

“Najua lakini usijali, Mungu atakupa mwanaume mwingine!”

“Dada, si kama Tom wangu niliyempenda na kujitoa kwake!”

“Jitahidi tu!”

“Siwezi,  siwezi nimekaa miaka yote hiyo nikimsubiri yeye, sikujua alipoelekea  sasa amerudi namhitaji!”

“Mariam!”

“Bee!”

“Wewe hivi sasa ni mgonjwa unahitaji kutulia na kufikiria afya yako kwanza!”

“Najua, lakini inaniuma sana!”

“Pole sana!”

“Ahsante!” Muda huo huo Pamela akaingia akiwa na maua mkononi mwake.

“Mariam umezinduka?” Pamela aliuliza kwa mshangao.

“Ndiyo namshukuru Mungu!”

“Pole, unaendeleaje sasa?”

“Nasikia vizuri!”

“Utapona usijali!”

Walizungumza mambo mengi  na Mariam kuhusu tukio zima lilivyokuwa na jinsi wanafunzi wanavyomchukulia. Pamela alitumia muda mwingi sana kumshauri na kumfanya ajisikie kawaida. Ilikuwa  kazi ngumu  lakini  aliimudu ipasavyo.

Wiki moja baadaye ikiwa  ni baada ya Mariam kupata Ushauri Nasaha kwa  madaktari hali yake ilirejea vizuri na alikuwa tayari  kuishi bila Tom. Akarejea chuoni na kuendelea na masomo kama kawaida.

***

Mapenzi ya Tom na Juliana yalipamba moto huku mipango ya ndoa ikiwa katika hatua za mwisho kabisa. Tayari ndoa yao ilishaandikishwa Kanisani na ilitarajiwa kufungwa wiki moja baadaye. Tom akapata safari ya ghafla kikazi ya kwenda Arusha. Alishindwa ni jinsi gani angemweleza Juliana akamwelewa juu ya safari hiyo lakini ilikuwa ni lazima amweleze.

Alichokifanya ni kuwahi nyumbani kisha akaoga pamoja na mpenzi wake baadaye wakaungana pamoja mezani kwa chakula cha usiku. Tom aliona hiyo ndiyo ilikuwa nafasi pekee ya kumweleza mchumba wake juu ya safari iliyokuwa mbele yake. Hata hivyo alisita.

“Darling inaonekana kuna  kitu kinakutatiza leo!”

“Ahaaa, hapana usijali mpenzi nipo sawa tu!”

“Nakujua vizuri sana mpenzi wangu si kawaida yako kuwa hivyo!”

“Ni kweli mpenzi lakini nafikiria ni namna gani utakavypokea ujumbe ninaotaka kukueleza!”

“Ni ujumbe gani, hata kama ni mbaya nieleze tu!”

“Nimepata safari ya ghafla ya kwenda Arusha kesho mchana!”

“Kuna nini tena?”

“Akina Jamali wameniita, kuna tatizo kidogo kule kwenye ofisi yangu ya kule sina budi kwenda ili nikalitatue, hata hivyo kesho kutwa tu nitakuwa hapa!”

“Mh! Darling nitabaki na nani?  Kumbuka zimebaki siku chache tu kabla ya ndoa yetu!”

“Sasa?”

“Siyo vizuri kusafiri!”

“Hizo ni imani tu, ondoa shaka mpenzi wangu wewe umeshakuwa wangu tayari!”

“Sawa, lakini usizidishe kesho kutwa!”

“Usijali”

Siku  iliyofuata Tom alijiandaa kwa safari ya kwenda Arusha na baadaye akiwa safarini kuelekea Uwanja wa Ndege akapigiwa simu na kufahamishwa kwamba tatizo lilishatatuliwa,  kwa maana hiyo hakuhitajika tena kwenda huko. Tom alifurahi lakini aliamua kumshtukiza mkewe.

Akaondoka na kwenda  kwa marafiki zake Msasani,  alikaa huko mpaka saa tano za usiku ndipo aliporejea nyumbani. Baada ya mlinzi kumfungulia aliegesha gari mahali pazuri kisha akafungua mlango mkubwa na kwenda moja kwa moja chumbani kwake. Macho yake hayakutaka kumeza yalichokiona mbele yake.

Juliana alikuwa na mwanaume kitandani, tena rafiki mkubwa wa Tom aliyeitwa Joseph. Tom aliyatoa macho bila kuamini alichokiona, akafikiria siku ya ndoa yake, akafikiria  jinsi alivyoalika wageni wengi, akawaza juu ya gharama alizozitumia kuandaa sherehe hiyo,  akachanganyikiwa.

“Juliana...Joseph,  mnanifanyia hivi?” Tom alisema maneno hayo akitetemeka. Ghafla akaanguka chini kama mzigo, puuu!

Picha ya Mariam ikamjia kichwani  mwake. Akapoteza fahamu.



Kilikuwa chumba kizuri kuliko kawaida, dari lilikuwa limepigwa rangi nyeupe, chini kukiwa na zulia la manyoya laini lenye rangi nyeupe, ukuta ulikuwa umepigwa rangi nyeupe, mashuka nayo yalikuwa meupe kabisa huku feni iliyokuwa juu ikisambaza hewa nzuri chumbani mle ikiwa nyeupe!

Kila kitu kilikuwa cheupe! Macho yake yalikuwa yakizunguka kila kona ndani ya chumba hicho bila kujua alikuwa mahali gani, baadaye akataka kuamka, lakini akashindwa! Alishindwa kwasababu alihisi maumivu katika mkono wake wa kuume, ni hapo alipogundua kwamba mkono wake ulikuwa umetobolewa na dawa iliyokuwa ikitokea kwenye drip ilikuwa ikiingia katika mishipa yake ya damu!

Huyu ni Tom au Papaa Bill kama alivyojulikana na wengi, hapo akili yake ikafanya kazi ipasavyo. Akagundua kwamba alikuwa hospitalini! Anaumwa nini? Ni swali ambalo alijiuliza bila kupata jibu sahihi. Baadaye alipogeuza uso wake akamuona Muuguzi akiwa amesimama mbele yake. Akatabasamu.

“Pole sana kaka!”

“Ahsante sana!”

“Unajisikiaje sasa?”

“Vizuri, kuna nini?”

“Unaumwa!”

“Na nini?”

“Huwezi kukumbuka, ulipoteza fahamu!”

“Hapa ni hospitali gani?”

“Ocean Road!”

“Umesema Ocean Road?”

“Ndiyo!”

“Nani alinileta?”

“Juliana!”

“Nani?”

“Juliana!”

“Umesema Juliana?”

“Ndiyo!”

Hapo picha nzima ikamjia, akakumbuka tukio zima la fumanizi kati ya Juliana na Joseph, moyo wake ulisononeka sana. Machozi yakaanza kutiririka machoni mwake kama maji yatiririkavyo katika kijito kilichopo mlimani. Moyo wake ulipata majeraha makubwa sana, hakuwa tayari kupata maumivu makali kiasi kile, akamchukia sana Juliana.

“Kwani vipi kaka?”

“Dada dunia hii...dunia dada!”

“Imefanya nini? Kwanza ni nini kilitokea?”

“Dada nimeamini unaweza kuwa na fedha nyingi sana lakini ukakosa mapenzi ya dhati kutoka kwa mtu mwenye penzi la dhati!”

“Unamaanisha nini kaka yangu?”

“Dada ninavyokuambia wiki ijayo nilitakiwa kufunga ndoa na mpenzi wangu wa moyo Juliana, lakini alichonifanyia siwezi kusahau katika maisha yangu yote!”

“Amefanya nini?”

“Si ulisema Juliana ndiye aliyenileta hapa?”

“Ndiyo!”

“Basi huyo mwanamke ndiye ambaye nilikuwa natarajia kufunga naye ndoa wiki ijayo, lakini nimemfumania na mwanaume mwingine, mbaya zaidi ni rafiki yangu wa karibu ambaye ninamsaidia vitu vingi ikiwemo pesa!”

“Pole sana Mungu atakusaidia!”

“Nashukuru sana dada yangu! Hivi, nilizimia kwa muda mrefu sana?”

“Siyo sana, uliletwa jana usiku na sasa ni saa saba na nusu mchana!”

“Yaani nimepoteza fahamu kwa masaa yote hayo?”

“Ndiyo, lakini usijali hali yako sasa inaendelea vizuri na utapata nafuu, usijali!”

“Nashukuru sana!”

INAENDELEA

Post a Comment

0 Comments