Niliichekelea sana fursa
hiyo. Kwanza ingenipa fursa ya kupumua hewa safi ya nje. Hewa asilia ya
oksijeni itokayo katika mimea na kusambazwa na upepo badala ya hii tuliyokuwa
tukiitumia ambayo sikujua ilitokea wapi. Lakini pia kufikia Zanzibar ilikuwa
ndoto yangu ya muda mrefu. Toka nchi hizi zilipoungana na sifa za Karume za
mapenzi kwa nchi yake zikiimbwa katika vyombo vya habari azma yangu ya
kukanyaga ardhi ya nchi
hiyo ilikuwa ikiongezeka siku baada ya siku.
Toka wakati ule ningali
belubelu bado, mkakati wangu wa kufanya biashara ya chumvi kati ya Zanzibar na
Bagamoyo ulipokwama, niliishia kujifariji kwa kusoma na kusikiliza tu, kila
kilichozungumza juu ya nchi hiyo. Nilijifunza kuwa ilikuwa moja ya nchi zenye
historia pekee duniani. Kwa mfano, wataalamu wa historia wanaamini kuwa miji
katika visiwa hivyo ni vya kale kuliko nchi nyingi za dunia. Inaaminika kuwa
waanzilishi wa taifa hilo makabila ya Wahadimu na Watumbatu walianza kuishi
katika visiwa hivyo, wakitokea katika pwani za Afrika Mashariki miaka 1000
iliyopita. Watu hao waliishi katika vijiji vidogovidogo vya ukoo, bila uongozi
wa pamoja jambo lililofanya wakose uwezo wa kutetea haki yao ya umiliki pale
walipoanza kuingia katika visiwa hivyo.
Wafanyabiashara toka
nchi za Kiarabu hasa Iran na Iraq na Wahindi wanaelezewa kufanya biashara na
nchi hiyo miaka nenda rudi. Katika karne ya 11 na 12 baadhi ya wafanyabiashara
hao walianza kuifanya Zanzibar makazi yao ya kudumu wengi wao ikiwa pamoja na
kuanza kuoana na wenyeji. Matokeo ya ndoa ni kuibuka kwa watawala kama Mwinyi
Mkuu au Jumbe miongoni mwa wahadimu au mashaha miongoni mwa Watumbatu. Viongozi
hao hawakuwa na nguvu nyingi. Lakini angalau walisaidia kulinda uhalisia katika
makabila yao.
Yule naodha machachari
wa Kireno, Vasco da Gama, alifika Zanzibar ,waka 1499 na kufungua njia ya
wageni wa kutoka Ulaya nchini humo. Mwaka 1505 nchi hiyo ilifanywa koloni la
Ureno pale walipoamua kuiteka kabisa.
Mwaka 1698 Zanzibar
ikafanywa sehemu ya mali
za Oman, hatua
iliyofuatiwa na Sayyid Said bin Sultan al
Busaid ambaye akiwa na
umri wa miaka 15, mwaka wa 1806 kuhamishiwa makao yake ya kifalme mjini humo.
Baadaye utawala wa pamoja wa Zanzibar na Oman uligawanyika mwaka 1861 baada ya
kifo chake, wanawe ambao walikuwa wakigombea madaraka walipofikia uamuzi wa
Sayyid Majid bin Said alipochukua madaraka ya na Zanzibar na ndugu yake Sayyid
Thuwaini kuwa Sultan wa Oman.
Baada ya hapo historia
ya Zanzibar ina mlolongo mrefu wa kugombea au kupokonyana madaraka baina ya
Waarabu na Waarabu, Wajerumani kwa Waingereza na hatimaye Waarabu kwa
Waingereza. Ni pilikapilika za aina hiyo zilizofanya Zanzibar iingie katika
historia kama nchi iliyovunja rekodi kwa kupigana vita fupi kuliko zote
duniani. Vita hiyo ilipiganwa kwa dakika 45 tu. Ilikuwa baina ya majeshi ya
Uingereza na yale ya Sultan Sayyid Khalid bin Bargash ambaye, alipokonya
madaraka na kujitangaza Sultan wa nchi hiyo wakati Waingereza waliamini mtawala
halali angekuwa Hamoud bin Mohamed. Waingereza walimwamuru Bargash kuachia
madaraka; akakataa. Wakampa muda wa kuondoka huku manowari zao zikiwa baharini
tayari kupiga mizinga iwapo angeendelea kukaidi. Muda waliompa ulipokwisha
manowari hizo zililipua mizinga ambayo ililiharibu jengo la Beit al Hokum.
Majeshi ya bargash yalijaribu kujibu kwa bunduki zao lakini hazikufua dafu.
Dakika 45 baadaye Bargash alikimbilia katika ubalozi wa Ujerumani, vita
ikasimamishwa na Maoud bin Mohamed akatawazwa kuitawala Zanzibar.
Utawala wa Mwingereza
nao ulikoma katika kisiwa hicho mwaka 1963 pale nchi hiyo ilipotoa uhuru na
uchaguzi ulipofanyika muungano wa ZNP na ZPPP uliposhinda kwa hila dhidi ya ASP
ya wazalendo akina Abeid Aman Karume na kufanya Waarabu waendelee kuwa
madarakani. Utawala
huo haukudumu. Mwaka
mmoja baadaye, Januari 12, 1964 wazalendo walipindua serikali hiyo na uongozi
kuwekwa chini ya Karume.
Hayakuwa mapinduzi
rahisi kama mtu unayeweza kufikiria Waarabu wengi wanadaiwa kuuawa, maelfu
wengine wakitupwa gerezani. Aidha, Karume alitumia mapinduzi hayo kurejesha
hadhi ya mtu mweusi kwa kutoa amri mwanamume kuoa mwanamke yeyote wa Kiarabu au
Kihindi anayempenda. Amri chungu ambayo ilipigiwa kelele na baadhi ya nchi
duniani, lakini kwa nchi iliyobobea kwa ukandamizaji, ambayo wakati fulani
iliaminika kuwa robo tatu ya raia wake walikuwa watumwa wa Waarabu hatua ipi
zaidi ingeweza kurejesha usawa na umoja haraka zaidi ya zile ndoa za lazima?
Misuguano ya ndani na
vitisho toka nje kwa taifa hilo dogo ilikoma pale nchi hiyo ilipoungana na
Tanganyika na kuzaliwa taifa jipya la Tanzania april 12, 1964 ikiwa miezi
mitatu tu baada ya mapinduzi.
Hiyo ndiyo Zanzibar ya
kale, ambayo kudra za Mungu
ziliniwezesha kuwa
safarini kuiendea.
Mfungwa hachagui njia,
mfungwa hachagui siku ya safari. Yeye ni mtu wa kukurupushwa tu, kama mifugo.
Ndivyo ilivyokuwa kwetu. Fununu za safari zilianza ghafla kwa minong’oni baina
ya wafungwa. “Skochi jamani…. Skochi ya Zanzibar…’ zilivuma taarifa hizo katika
selo. Nadhani ‘skochi’ ni lugha moja ya zile lugha za kijelajela iliyokuwa na
maana ya ‘escort’ kwa kiingereza kwani mfungwa haendi popote bila askari jela
wa kuwasindikiza.
Sikujua Kama ningekuwa
mmoja wa wateule hao hadi siku ya safari, jina langu lilipoitwa na kuamriwa
kupanda karandinga. Tulikuwa kama wafungwa mia hivi na askari kumi wa
kutulinda. Safari yetu ilianza asubuhi ya jumatatu
moja, tukaifuata
barabara ya Dar es Salaam. Tulipofika Moshi tulisimama kwa nusu saa, mkuu wa safari
aliposhuka kupata kifungua kinywa.
Nilitamani kuuona mji wa
Moshi kwa mara nyingine, lakini niliishia kuuchungulia tu kupitia katika nyavu
za waya za karandinga letu, hali ya hewa ilikuwa ileile, tamu inayosisimua.
Mlima Kilimanjaro uliendelea kuinamia mji, kama unaolinda kwa maovu, kwa
utukufu wake. Kitu kilichonivutia zaidi kwa mji wa Moshi ni usafi. Barabara
zilikuwa zikimeremeta, majengo yaking’ara kwa rangi. Ilikuwa nadra sana kuona
uchafu ukizagaazagaa mitaani kama ilivyo miji mingi niliyopata kuitembelea.
Safari ilipoanza tena
nilikuwa tayari nimepata upenyo mzuri wa kuchungulia nje. Barabara safi, ya
lami ilikuwa ikiteleza chini ya matairi ya gari letu kwa uhakika kabisa.
Tulikuwa tukielekea Mashariki hadi tulipofika Himo ambapo kuna njia panda ya
kuelekea Taveta nchini Kenya na ile ya Dar es Salaam ambayo kwa kiais fulani
ilielekea Kusini. Tulipita Kifaru, tukaingia Mwanga. Toka hapo niliweza kuliona
kwa mbali bwawa la nyumba ya Mungu. Tukateleza hadi Same, Hedaru, Mkomazi,
Mombo na baadaye Korogwe ambapo tulipumzishwa katika gereza moja dogo ambalo
sikubahatika kufahamu jina lake. Hapo tulipewa chakula na kutakiwa kumaliza
haja zetu za kimaumbile, kubwa na ndogo kabla ya kuanza safari.
Tulifika Segerea na
kuiacha barabara inayokwenda Tanga hadi Mombasa tukashuka na kuvuka mto Wami
hadi Msata. Hapo viongozi wetu wa safari walisimama kwa muda kujadiliana, ama
wafuate barabara ile ndogo isiyo na lami ambayo inachepuka hadi Kiwangwa,
Kilola na hatimaye Bagamoyo au ile iliyozoeleka, lakini ya mzunguko, ambayo
ingetufikisha Chalinze,
Mlandizi na Kibaha kabla ya kuingia Dar es Salaam. Kumbe safari yetu ya Unguja
ilikuwa ianze Bagamoyo. Nadhani kwa usalama wao au wetu waliamua kupita njia
ndefu ya Dar es Salaam.
Nilishangazwa na wingi
wa watu na majengo niliyoyaona hasa kutokea Mlandizi, mara tu baada ya kuvuka
mto Ruvu. Nilipopita kwa mara ya kwanza eneo hili lilikuwa pori la kutisha
ambalo lilimilikiwa na nguruwe mwitu na ndege wa porini. Sasa lilijaa binadamu
na majengo tele. Wakati huo ilikuwa usiku wa saa tatu hivi, lakini taa za umeme
toka maeneo mbalimbali, wingi wa magari barabarani na watu tuliwapitia kando ya
barabara uliashiria wingi wa watu na pilikapilika nyingine za kibindamu.
Pilikapilika hizo ziliongezeka
maradufu mara tulipoingia Mbezi na hatimaye Kimara. Gari letu lilikwenda kwa
mwendo wa kinyonga kutokana na msongamano wa magari. Kandokando mwa barabara,
kulia na kushoto, nilishangazwa na wingi wa baa za pombe na wateja waliofurika
kelele za muziki wa kileo, ambao baadaye niliambiwa kuwa unaitwa Bongo flavour
ziliweza kusikika ndani ya gari hiyo kwa uwazi kabisa. Katika baa moja
mwanamuziki mmoja alikuwa akicheza kwa nguvu zake zote;
Kuku kapanda baiskeli,
Bata kavaa raizoni…
Wimbo huo ulitufikia
vizuri kabisa katika gari. Wengi wetu ambao tulizowea nyimbo za akina Marijani
Shabani, Wema Abdallah au Mbaraka Mwishehe tuliishia kucheka kwa mapinduzi haya
ya kisanaa. Hatukujua kama tunakwenda mbele au tunarudi nyuma katika fani hiyo
ya muziki.
Zaidi ya nyimbo kitu
kingine kilichotufikia ndani ya
gari hilo ni harufu ya
nyama choma. Yale mapande ya nyama,
mishikaki na kuku
waliokuwa wakiokwa katika mabaa hayo yalisambaza harufu tamu ambayo ilitutia
uroho wa nyama, mboga iliyopatikana kwa nadra sana gerezani.
Tulifika Dar es Salaam
yapata saa nne na robo usiku. Ule muujiza nilioutegemea ulijidhihirisha. Dar es
Salaam haukuwa mji tena bali jiji. Majumba mengi yaliyopanda juu, watu wakiwa
tele mitaani muda wote. Biashara ya baa ilishamiri karibu kila mahala. Nchi hii
haina biashara nyingine?
Tulitoka Ubungo na
kuelekezwa Mwenge. Gari likageuzwa na kuelekea Kaskazini tulikotokea tukifuata
barabara ya Bagamoyo. Kwangu barabara hiyo ilikuwa muujiza mwingine. Tofauti
kabisa na ile tuliyoitumia na akina Leakey miaka kadha wa kadha iliyopita hii
ilikuwa barabara pana ya lami. Na ilifurika magari muda wote. Lile pori la
wakati ule halikuwepo tena. Badala yake mji ulikuwa umemeza kila kitu kiasi cha
kufanya kambi ya jeshi la Lugalo, ambayo zamani ilionekana kujengwa porini sasa
iwe katikati ya mji wa kiraia, ambao ulisambaa hadi Pwani yake uwe hadi ufukwe
wa Kunduchi. Vile vilivyojulikana kama vijiji vya Tegeta, na Bunju sasa ilikuwa
sehemu ya jiji la Dar es Salaam ambalo lilibakiza kilometa mbili tu kuungana na
mji wa Bagamoyo, Bagamoyo ambako tulifikishwa katika gereza la Kigongoni
kusubiri safari ya Zanzibar.
Ulipata kusikia kuwa
binadamu ana mkia? Kama ulipata, je ulipata kuona mkia huo? Ni watu wachache
sana duniani waliopata kuuona; mimi nikiwa mmoja wao. Bahati au balaa hiyo
nilikutana nayo katika gereza hilo ambalo ni maalum kwa kilimo.
Awali sikuyaamini macho
yangu pale nilipowaona watu wa ajabu. Miili yao ilikuwa inatisha, ngozi
ikiogofya. Fikiria ngozi ya mtu yeyote, uliyopata kuiona maishani mwako,
fikiria
hata mgonjwa wa UKIMWI
aliye taabani sana; bado kamwe hutaweza kumfananisha na miili ya baadhi ya
wafungwa tuliokutana nao katika gereza hilo. Walinyauka, walisinyaa na kuifanya
miili yao ifikie kiwango hicho cha kutisha. Lakini zaidi ya ngozi ya miili hiyo
hali ya kukonda ilitisha zaidi. Baadhi yao, waliokuwa taabani zaidi walionekana
kama mifupa iliyounganishwa na aina fulani ya ngozi! Ni pale walipovua mashati
ndipo nilipoweza kuona mkia wa binadamu!
Mimi pia nilikuwa
mfungwa. Lakini hali ya baadhi ya wafungwa hawa ilinifanya nitokwe na machozi!
Nilipouliza nini kinatokea wenyeji walininjibu kwa urahisi tu; Luba.
Luba ndio nini?
Ugonjwa. Unatokana na
wadudu ambao hushambulia mpunga. Unajua kilimo cha mpunga kilivyo? Inabidi
kuingia katika maji au tope. Kwa mfungwa kulazimishwa kuingia katika maji ya
tope linalofika hadi shingoni ni jambo la kawaida. Humo ndimo hukutana na
wadudu hawa ambao hushambulia mpunga na hivyo wao pia kushambuliwa.
Msemaji alikuwa mfungwa
mzoefu. Ilikuwa vigumu kuamini kweli ni mfungwa kwa jinsi alivyokuwa msafi,
kiribatumbo kimejitokeza wazi chini ya kifua chake.
“Ni wajinga,” aliongeza.
“Wanaingia kichwakichwa katika miji ya watu. Wangeuliza maradhi hayo
yasingewapata.”
“Kwa vipi?” Nilimuuliza.
Alikohoa, kabla hajajibu
akisema, “Iko namna. Kuna dawa. Wenzao kabla ya kuzama katika tope lile
tunajipaka tumbaku. Wadudu hawatusogelei wala kutudhuru.”
“Kwa nini hamkuwaambia
hayo mapema?” nilimsaili. “Si nimekwambia wanaingiamiji ya watu kichwakichwa?”
lilikuwa jibu lake.
Kwa mara ya kwanza
nilijisikia kumpiga mtu makonde.
Mtu mwenyewe hakuwa
mwingine zaidi ya mzee huyu anayezungumzia maisha ya binadamu wenzake kana
kwamba anajadili suala la paka. Ili kuepuka kufanya hivyo nilimwacha akiendelea
kubwabwaja na kujiunga na wenzangu tuliokuwa nao katika ‘skochi’.
Nilishukuru pale siku
mbili baadaye tulipochukuliwa na magari kuelekea pwani ya Bagamoyo, ambako
majahazi mawili yalitupeleka Unguja yalitia nanga yakitusubiri.
Kutoka pwani hiyo hadi
Zanzibar ilikuwa safari ya kilometa zipatazo 25 tu, lakini kwa wenzangu wengi
ilikuwa safari ndefu, ngumu iliyojaa mashaka. Mawimbi na upepo vilifanya wengi
wapatwe na ule ugonjwa uitwao ‘homa ya bahari.’ Baadhi walitapika, baadhi
wakiwa taabani kana kwamba wanakaribia kukata roho. Askari wawili
waliotusindikiza pia walikuwa wakitapika huku wenzao wakiwacheka.
Wakati tunakaribia kutua
pwani tulipata burudani tosha toka kwa pomboo, wale viumbe wa baharini ambao
mimi huwaita samaki lakini wataalamu uwachukulia kuwa ni wanyama wa majini kwa
kuwa wananyonyesha watoto wao kinyume na samaki wengi, kawaida. Viumbe hawa
ambao wengi huwaita ‘Dolphins’ walilizingira jahazi letu, mara kwa mara
wakichupa angani na kutuchungulia kwa namna ya kusisimua.
Pomboo, ambao nyama yake
ni tamu sana ni viumbe wanaofugika na kufundishwa. Nchi kadhaa tayari
wamewafundisha michezo mbalimbali kama kushindana, kuruka kwa pamoja kudaka
mpira na mambo mengine tele ambayo huvuta watalii. Baadhi ya nchi
zilizoendedelea tayari wanawafundisha kubaini mabomu ya kutegwa baharini na
hivyo kuepusha madhara.
Kwangu walikuwa burudani
tosha na walitusindikiza hadi tulipotia nanga ufukwe wa Zanzibar, mji mkuu wa
nchi hii ambayo inadaiwa iko chini kidogo ya usawa wa bahari. Baadhi ya
wataalamu wanadai kuwa iko siku nchi hiyo itamezwa na maji na kutoweka katika uso
wa dunia. Lakini hiyo ni hadithi nyingine. Yetu ni kwamba mara tulipofika
magari ya wafungwa yalikuwa yakitusubiri tayari kutupeleka katika gereza la
kiinua mguu ambako tungepumzika kidogo kabla ya kusafirishwa tena hadi Pemba
yaliko mashamba mengi zaidi ya karafuu.
Tulilundikwa katika
makarandinga, ambapo hayakutofautiana sana na yale ya bara. Yakatiwa moto na
kuondoka. Kwa kiu yangu ya kuufahamu mji wa Zanzibar nilifanya kila jitihada
kuhakikisha nachungulia nje na kujionea chochote ambacho ningeweza kukiona. Kwa
mbali, niliweza kuiona hoteli maarufu ya bwawani ambayo ilijengwa na serikali
ya Karume. Wakati tukipita mitaani, eneo la Kichenzani nilishangaa kuona mitaa
yote ikiwa imemezwa na majumba marefu sana, takribani mita mia tano kila
nyumba. Nyumba hizi ambazo zilikwenda juu kwa gorofa tatu au nne tu
zilielekezwa kuwa ilikuwa kazi nyingine ya Karume kwa wananchi wake alipotoa
amri akisema, ‘Wazungu wanashindana kujenga nyumba ndefu kwenda juu kwa ajili
ya uhaba wa ardhi yao, sisI tutajenga nyumba ndefu kwa upana.’ Matokeo ya kauli
hiyo ndiyo nyumba hIzo ambazo zilikuwa mkombozi kwa wananchi ambao wengi wao
walikuwa masikini sana baada ya kukandamizwa na wageni miaka nenda rudi.
Katika eneo la darajani
nilishangazwa na wingi wa waendesha baiskeli. Katika maneno fulani ilibidi
waongozwe na askari wa barabarani kama ilivyo kwa magari. Eneo hilo lina soko
kuu, wenyewe wakiliita ‘markiti’ bila shaka jina
hilo lilitokana na neno
‘market’ la Kiingereza. Kilichonivutia zaidi hapo ni mavazi, kanzu nyeupe ndala
miguuni na baragashia kichwani vilitawala mavazi ya mwanaume. Kwa wanawake
mabaibui yaliyofunika sura gubigubi yalitamalaki na kunikumbusha miji ya Tanga.
Utamaduni mwingine niliobahatika kuuona hapa katika muda mfupi ni kitendo cha
wanaume wengi zaidi kuwa na makapu kununua mahitaji ya nyumbani. Ilikuwa nadra
sana kuwaona wanawake wakifanya manunuzi hayo.
Tuliiacha darajani na
kuambaa pembeni mwa mji mkongwe. Macho yangu yalivutiwa na nyumba za kale,
ambazo baadhi zilijengwa zaidi ya miaka mia mbili iliyopita lakini bado
zinatumiwa na binadamu hadi leo. Ajabu ni kwamba nyumba hizo zilijengwa kwa
udongo, mawe na miti migumu kama mikoko ambayo mingi ingali imara hadi
leo. Kitu kinachovuta
macho zaidi ni katika mji huu mkongwe ni mitaa yake. Nyumba hizo zilijengwa
katika hali ya kubanana sana kiasi kwamba mitaa yake haiwezi kuruhusu gari
kupita na hata baiskeli na pikipiki zililazimika kupita kwa uangalifu sana.
Sura hii ya aina yake ya mji huu mkongwe ni moja ya sababu zilizopelekea
shirika la elimu la Umoja wa Mataifa liutangaze kama moja ya maeneo ya
kihistoria ambayo yanahitaji kuhifadhiwa.
Katika mwambao huo wa
bahari nilifurahi sana kuliona jengo maarufu Beit el Ajaib lililojengwa na
Sultani Bargash mwaka 1883. Jengo ambalo lina simulizi tele za kila aina. Kwa
mfano inaaminika kuwa chini ya kila nguzo ya jengo hilo alizikwa hai mtumwa
mmoja. Juu yake likiwa na mnara wenye saa kubwa pia linadaiwa kuwa la kwanza
nchini na pengine Afrika nzima kutumia umeme na lifti.
Kando yake
nililitembelea pia jengo jingine lililokuwa
likitumiwa kama ngome
kuu ya Waarabu. Jengo hilo lenye ukumbi mkubwa na kuta pana lilipanda juu
ambako kuna majengo na matunda maalum ya kutumia wakati wa vita. Hata hivyo
sisi tulikuta tayari jengo hilo lina maduka, kumbi za wazi za burudani na
biashara mbalimbali za sana.
Zanzinbar haina wanyama
wengi kama bara. Inaaminika kuwa nchi hiyo haina tembo hata mmoja. Jambo ambalo
linawashangaza sana wataalamu wa masuala ya wanyama pori kwani mwaka 1295,
msafiri mmoja aliyeitwa Marco Polo aliitembelea Zanzibar kutoa taarifa ya
kuwepo kwa mamia ya tembo na wanyama wengine.
Kama tusingekuwa
wafungwa tungeshiriki katika ngoma ya ‘mwaka kongwa’ iliyokuwa ikipigwa wakati
tukipita eneo la Makunduchi. Tuliishia kuchungulia dirishani tu na kuona
wanaume wanavyotoana jasho kwa ndizi na migomba katika ngoma hiyo maarufu ya
kila mwaka.
Zanzibar hiyo! Kwa
machache niliyobahatika kuyaona, machache niliyopata kuyasikia na kuyasoma
sikushangaa pale macho yagu katika tundu nililokuwa nikitumia kuchungulia nje
yalipoweza kuona idadi kubwa ya watalii wa Kizungu wakipita hapa na pale katika
mitaa, vichochoro na fukwe ya Zanzibar. Nilipata pia kusoma mahala kuwa
takribani wageni wapatao 100,000 hutembelea visiwa vya Zanzibar kila mwaka kwa
ajili ya shughuli za kitalii.
Gereza la Kiinua Mguu
halikuwa tofauti na magereza mengine niliyopata kuyatembelea. Hadithi ilikuwa
ileile, chakula kibovu, mlundikano katika selo, chawa na kunguni wakitawala,
maradhi ya kila aina na vifo. Tulilala hapo siku tatu kabla ya kupakiwa katika
moja ya zile meli zao ziendazo kasi, ambayo ilitufikisha pemba, katika mji wa
Wete. Huko
tulielekezwa katika
mashamba ya karafuu kuanza kazi.
Nilikuwa nikiifahamu
karufuu kwa ladha tu, baada ya kuila sana katika pilau kule Pangani. Aidha,
niliifahamu kwa harufu yake tamu puani toka katika marashi ya akina mama wa
mjini wanaojiandaa kutoka. Sikupata kufahamu kuwa zao hilo lilikuwa na maajabu
zaidi. Kwa mfano, sikujua kama karafuu ilikuwa tiba pia ambayo mafuta yake
yalitumiwa kumchua mtu aliyeteguka viungo pamoja na tiba ya meno kwa mwenye
maumivu. Nilishangaa zaidi kusikia kuwa karafuu, kwa baadhi ya watu, waliitumia
kama sigara wakichanganya na vitu vingine walivyofahamu wao.
Kwa mujibu wa kumbukumbu
za kihistoria Sultan Sayyid Said aliyeitawala Zanzibar katika karne ya kumi na
nane, alipofika kwa mara ya kwanza nchini humo alishangaa kuona mikarafuu
miwili mitatu iliyoota hapa na pale kwa bahari tu ikiwa imestawi vizuri. Wakati
huo karafuu likiwa zao hadimu kwa kupatikana katika maeneo machache ya Asia,
Sultan huyo alipata wazo. Aliamini kuwa zao hilo lingeweza kuupa nguvu za
kiuchumi na umaarufu utawala wake. Hivyo, alilima shamba lake binafsi kama
mfano, akapanda miche arobaini na tano. Kisha, akatoa amri kila mtu kulima
mikarafuu. Amri ambayo alihakikisha inatekelezwa kwa nguvu zake zote. Hadi
anafariki Sultani huyo aliacha tayari biashara ya pembe za ndovu na watumwa
ikitishiwa kiuchumi na ile ya karafuu.
Mkarafuu unapendeza kwa
macho kama ilivyo harufu yake. Ni mti ambao unakuwa katika rangi yake halisi ya
kijani kwa mwaka mzima. Mti huu huenda juu kwa mita kumi hadi ishirini. Maua
yake ndiyo karafuu yenyewe. Yako katika sura na maumbile mbalimbali. Maua hayo
hupitia rangi mbalimbali kama kahawia, kisha kijani na hatimaye wekundu ambao
ndio
huwa dalili ya kukomaa
na hivyo huvunwa.
Tulifundishwa yote hayo
tukiwa katika uvunaji kazi ambayo ilituweka kisiwani humo kwa miezi mitatu.
Pengine kwa ajili ya
ugumu wa usafiri toka kisiwani humo, pamoja na ugeni wetu, hatukushindwa sana
kama ilivyokuwa bara na Unguja. Tuliruhusiwa kuchanganyika na wenyeji na,
hivyo, kujipatia marafiki wengi wa Kipemba. Hata hivyo, tatizo lilikuwa
kuelewana. Ilituchukua muda mrefu kukielewa Kiswahili chao ambacho ama
kilichanganyika na kiarabu ama kiliathiriwa na makabila ya asili.
Pemba ilikuwa nyuma
kimaendeleo ukiilinganisha na Unguja. Pamoja na kuwa mzalishaji mkuu wa zao
hilo la karafuu na mazao mengine, bado wananchi wake wengi zaidi waligubikwa na
umasikini. Nyumba zao nyingi zilisikitisha kwa kukosa hata milango, mavazi yao
yalikatisha tamaa. Watoto na watu wazima kutembea pekupeku bila viatu ilikuwa
jambo la kawaida sana.
Karume amejitahidi. Kila
alichokifanya Unguja alikifanya pemba pia. Yale majumba yake marefu yalijengwa
pia Wete na mkoani. Wanachi waliishi bila malipo. Hoteli kubwa kama ile ya
bwawani pia ilijengwa katika kisiwa hiki kwa kiwango kilekile. Bado wananchi
engi walikuwa taabani na
nyuso zao zilionyesha kitu kama kutoridhika au kukata tamaa. Pemba kunani
jamani? Nilijiuliza. Kwa kweli, pamoja na uhuru tuliokuwa nao miezi mitatu
tulioishi huko niliona kama miaka mitatu ya kuishi katika gereza jingine la
aina yake.
YA ISHIRINI NA TATU
Tumaini Lilirorejea
asaibu ya maisha
yanaweza kukupangia jambo ambalo hata hukupata kulifikiria. Mfano mzuri ukiwa
wangu mwenyewe. Maishani mwangu
sikukusudia kuwa mhalifu
wala sikupata kutarajia kamwe kujikuta nikiishi gerezani kama mfungwa. Lakini
ufungwa nao una yake. Ufungwa wangu ulianza kugeuka kuwa utalii.
Mawazo hayo niliyapata
tuliporejea toka Zanzibar na kupumzishwa wiki mbili kabla ya baadhi yetu
kupangiwa safari nyingine. Mara hii safari yetu ilikuwa ya kueleka Kusini,
mkoani Mtwara, ambako tuliombwa kusaidia kazi ya kuchimba mtaro wa kupitisha
gesi katika eneo fulanifulani ambayo waajiriwa wa kawaida waligoma kwenda
kutokana na ugumu wa mazingira. Sisi, watumwa wasio na wenyewe tulipewa amri
tu, ‘Skoch’ ya Mtwara kesho.
Sikupata kufikiria
kwenda Mtwara hata mara moja katika ndoto zangu za kimaisha. Mtwara kufanya
nini? Wana Mtwara wenyewe walikuwa wanaikimbia. Msamiati wa ‘Wamachinga,’ wale
wafanyabiashara vijana, ambao huzunguka na bidhaa zao kila mtaa na kila
uchochoro wa jiji la Dar es Salaam, ulizaliwa kutokana na vijana wa Mtwara,
pale walipoanza kumiminika mjini baada ya kukata tamaa
vijijini. Walikuja kwa
mamia, kutwa wakisaga lami na vumbi la Dar, usiku wakilala kwa dhiki katika
vichochoro vya Kariakoo, biashara zao maelfu zikilindwa kama roho zao. Taratibu
walianza kuwatishia wamiliki wa maduka, wengi wao wakiwa Wahindi, pale wateja
wao walipopunguza kuingia madukani na kuishia kwao. Waliwatishia pia maafisa wa
kodi kwani kodi toka kwa wenye maduka zilipungua na kumdai Mmachinga ambaye
hujui anaishi wapi, duka lake anatembea nalo, haikuwa kazi rahisi.
Wakati huo ‘Wamachinga’
walichukuliwa kama Wamakua na Wamakonde pekee. Hata jina lao lilitokana na kile
kijiji cha Mchinga kilicho Pwani ya Bahari ya Hindi, maili chache toka Lindi.
Lakini mafanikio yao tayari yamewavuta Wasambaa na biashara zao za matunda toka
Tanga, Wagogo na kahawa zao toka Dodoma, Waha na baiskeli zao toka Kigoma na
wengineo. Wote wanafanya kazi za kimachinga na wameafiki jina hilo la
Wamachinga pamoja na serikali kuwatafutia majina mbalimbali ya kutia matumaini
kama ‘Wajasiriamali, ‘ au ‘Wafanyabiashara wasio rasmi.’
Moja ya sababu
zilizofanya nisiote ndoto ya kwenda Mtwara ni zile sifa za ugumu wa safari za
kwenda huko. Usafiri wa meli haukuwa na uhakika. Ilisikika habari ya meli moja
tu, tena ya mizigo, ambayo ungeisubiri kwa mwezi au miezi kabla ya safari. Meli
ambayo ilidaiwa kufurika kupita kiasi na hivyo kuhatarisha maisha ya wasafiri
mara kwa mara. Enzi hizo kufikiria safari ya barabara ilikuwa wazimu zaidi.
Njia ilikuwa ndefu kuliko ilivyostahili kutokana na ubovu. Yalikuwepo maeneo
yasiyopitika, magari ya madereva vichwa ngumu yakizama au kukwama kwa zaidi ya
wiki katika tope kabla ya kufikia kivuko cha mto Rufiji na matawi yake.
Pengine kama si
kizingiti cha barabara hiyo Mtwara ya leo ingeweza kuwa mfano wa aina yake wa
utajiri wa Tanzania, kwani neema ya uchumi ilikuwa imeishukia Mtwara mwaka 1948
Waingereza walipouteua mkoa huu na kongwa Dodoma, maalumu kwa ajili ya kilimo
cha karanga. Ekari milioni 325 au kilomita za mraba 13,200 zilitarajiwa kulimwa
katika kipindi cha miaka sita na hivyo kuilisha Tanganyika Ulaya nzima karanga
na mazao yote yatokanayo na karanga.
Mradi huo ulitengewa
dola za Marekani milioni 25. Askari wastaafu laki moja na wakazi wengine tele
waliojitokeza kufanya kazi hiyo. Hata hivyo, baada ya jitihada za muda mrefu na
kupotea kwa dola milioni 49 zaidi ya zilizotarajiwa kazi ilishindikana. Sababu?
Ukosefu wa barabara. Reli iliyokuwepo, ambayo ilitarajiwa kutumiwa kwa
usafirishaji wa vifaa na mazao ilichukuliwa na mafuriko ya mto Kinyensungwe.
Usafirishaji wa vifaa kama matrekta na mbolea kupitia mto Ruvu nao ulikutana na
vizingiti tele; tembo, vifaru na viboko walitishia maisha ya wafanyakazi na
hivyo wengi kukimbia. Maradhi ya malaria na matumbo kwa ajili ya maji yasioaminika
nako kulichangia.
Jambo jingine ambalo
lilisababisha mradi huu kushindikana ni mibuyu. Vifaa vidogovidogo vilivyoweza
kufika huko havikuwa na uwezo wa kuing’oa mibuyu mikubwa iliyotanda katika
baadhi ya maeneo ya shamba. Si hivyo, baadhi ya mibuyu hiyo ilikuwa na maajabu yake.
Baadhi ya mibuyu ilishindikana kutokana na wingi wa nyuki waliokuwa wameweka
makazi yao humo, ambao waliwatawanya wakulima hao hadi wakashindwa kufanya kazi
yao. Mibuyu mingine ilitumiwa na wenyeji kama matambiko, wasingekubali kamwe
ing’olewe. Mbuyu mmoja
ulitumiwa kama gereza kwa ajili ya wahalifu. Huu pia usingeng’olewa.
Hayo na mengine tele
yalisababisha tani 2000 tu za karanga zipatikane baada ya miaka tele ya
majaribio kabla ya bunge la Uingereza halijatamka rasmi kuuachilia mbali mradi
huo mwaka 1951. Kupotea kwa tumaini hilo kuliambatana na kusahauliwa kwa
Mtwara, na hivyo kuibuka kwa ukimbizi wa vijana wenye nguvu, kwenda mijini
kutafuta maisha kwa ‘Umachinga’.
Hivyo, kugunduliwa kwa
gesi, kulikofanywa na kampuni ya Artumas Co. katika mkoa huo ilikuwa neema ya
pekee kwa Mtwara na wakazi wake. Lilikuwa tumaini lilirorejea kwa Wamachinga.
* * *
Kwa mujibu wa taarifa
zisizo rasmi, ambazo kama wafungwa tulizipata toka hapa na pale wakati
tukifanya kazi yetu ya kuchimba
mitaro ni kwamba gesi
hiyo iliyogunduliwa ingeweza kutumiwa na mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kupikia,
kuendeshea viwanda na mahitaji yote ya umeme kwa zaidi a miaka 800.
Taarifa hizo ziliongeza
kuwa uamuzi wa serikali ulikuwa kuhakikisha wakazi wa Mtwara, ambao kwa mwaka
2002 walikuwa 1,128,523 wote wanapatiwa fursa ya kuitumia nishati hiyo kwanza
kabla haijaruhusiwa kwenda kuwahudumia watu wengine.
Gesi hiyo iligunduliwa
Mnazibay, ambako tulipelekwa kufanya kazi. Zilikuwepo pia fununu za nishati
hiyo kugunduliwa katika sehemu mbalimbali za mikoa hiyo ya kusini.
Kazi ya kuchimba mitaro
hiyo haikuwa rahisi. Kulikuwa na ule wa kupitisha bomba la kuileta gesi hadi
Dar es Salaam ambako tuliambiwa kuwa viwanda kadhaa kikiwemo kile maarufu cha
Simenti, Wazo, tayari vilikuwa kutumia nishati hiyo badala ya umeme wa TANESO
uliozolekea. Umeme ambao ulitegemea zaidi maji ya mvua hivyo, licha ya gharama
kuwa kubwa miaka yenye mvua haba ulikuwa matatizo kibao kiasi cha kuanzisha
msamiati wa aibu ‘mgao wa umeme.’
Tulifanya kazi yetu
kikamilifu, siku tulizopangiwa tulirejeshwa Ukonga, siku zangu za kukaa
kifungoni zikifikia ukingoni.
Siku moja bado tukiwa
huko Mtwara, nilitembelewa na wazo la ajabu. Kuoa! Sijui wazo hilo lilipenyaje
katika kichwa changu kilichofura kwa matatizo na migogoro isiyo na kifani.
Mfungwa, asiye na mbele wala nyuma, nawezaje kufikiria kuoa?
Mimi wazo hilo
lilinitembelea. Chanzo chake hakikuwa zaidi ya Lulu, msichana wa Kimakua ambaye
alitembelea gereza tulilokuwemo akiwa amefuatana na maafisa wenzake wa ustawi
wa jamii. Walituweka kikao kwa maelezo kuwa wamekuja kuzungumza nasi kuhusu ya
maisha ya uraiani kwani wengi wetu vifungo vyetu vilikuwa vikifikia ukingoni.
Walizungumza mengi.
Lakini naapa kuwa hakuna aliyekuwa akiwasikiliza. Lulu, akimeremeta kwa ngozi
yake laini ya maji ya kunde, sauti yake ya upole na tabasamu lililosindikiza
kauli zake alivutia zaidi ya nasaha zao. Wafungwa wengi walionekana hivyo na
walinong’onezana hivyo. Hali ambayo ilidhihirisha zaidi pale tulipopewa wasaa
wa kuuliza maswali. Mfungwa wa kwanza alielekeza swali lake moja kwa moja kwa
Lulu “Samahani dada Lulu, umeolewa?”
Kila mtu alicheka, ikiwa
pamoja na Lulu mwenyewe. “Sijaolewa. Unataka kunioa?” alimjibu na kumtupia
swali pia.
“Huyu akuoe? Atakulisha
nini?” alidakia mfungwa mwingine na kuongeza. “Kwanza ni mzee. Kisha hajui
kusoma wala kuandika. Kama kuna mume hapa ni huyu mdogo wetu,” alisema
akielekeza kidole chake kwangu. “Ni msomi, anazungumza Kiingereza kama
Kiswahili. Hata humu ndani amekuja kama ajali tu,” aliongeza.
Sikutarajia kauli kama
hiyo. Nilishikwa na aibu kuona kila mtu akinitazama. Lulu Kalenje, kama
alivyojitambulisha, alitabasamu kabla hajatamka taratibu, “Naona nimeshapata
mchumba. Kwani kaka unaitwa nani?” aliniuliza.
“Petro Kionambali.”
Nilimjibu
“Unatoka upande upi wa
nchi hii?” aliongeza swali jingine.
“Natokea Kigoma.” “Wewe
Muha?” “Haswaa.”
Lulu akacheka tena kabla
hajasema. “Sioni kama uchumba wetu utadumu. Watu wa Kigoma hamtuwezi kabisa
Wamakua. Tuna tofauti kubwa ya kiutamaduni.”
Nilimwelewa haraka.
Nilikuwa nimejifunza mawili matatu juu ya mkoa wa Mtwara na makabila yake
kadhaa.
Wageni hao walipoona
maswali ya kijelajela yakiongezeka badala ya yale waliyoyakusudia waliaga na
kuondoka. Wenzangu walitawanyika. Mie nilibakia palepale kwa muda nikitafakari.
Wazo la kupenda na kuoa kwa ujumla lilitokea kusikojulika. Lilijikita kwa muda
katikati ya ubongo wangu.
Nilitamani kuoa!
Nilitamani kumwoa Lulu!
Nikamfikiria Lulu, mtoto
wa Kimakua. Sikupata kuishi Mtwara. Lakini katika maongezi na tafiti zangu
vitabuni nilikuwa nafahamu mengi juu ya mila na tamaduni za Wamakuwa na jirani
zao Wayao.
Mtwara, ambayo iko
kusini mwa Tanganyika, ikiwa imetengana na nchi ya Msumbuji kwa mto Ruvuma
inayo makabila mengi. Makubwa kati yake yakiwa Wamakonde na Wamakua ambao
waliingia kutokea Msumbiji. Wayao wanaaminika kutokea Malawi. Hizo zikiwa zile
enzi za kuhama kabla ya ujio wa watu weupe ambao walifuatiwa na uamuzi wa uroho
na uchoyo uliopelekea kuwekeana mipaka baada ya kupora hiki na kile.
Wamakua na Wayao
wanapofikia umri wa miaka kumi hadi kumi na mbili lazima wapitie unyago. Jukumu
hilo, huendeshwa na wazee wa kike waliobobea katika masuala ya familia.
Wahusika hulazimishwa
kutunza siri yoyote watakayo fundishwa au kuonyeshwa katika mafunzo hayo.
Miongoni mwa mafunzo hayo ni jinsi ya kujitunza. Wavivu na jeuri hupewa maneno
ya kuwatisha ili waachane na tabia hizo na masuala mengine ambayo somo ataona
lazima kuyasisitiza.
Mafunzo hayo hufuatiwa
na sherehe za mkesha, ngoma aina mbalimbali kama chimakuani, mtotamto, mselemba
na nyinginezo hutumbuiza. Sherehe ambazo huambatana na vinywaji hasa pombe ya
mtama ambayo huandaliwa maalum kwa shughuli hiyo.
Yote hayo niliyachukulia
kama kawaida. Ambacho nilikiona kizito ni ule utamaduni wao wa kumfanya mtoto
mali ya mama zaidi ya alivyo kwa baba. Kwa maana nyingine mtoto
anamsikiliza zaidi
mjomba. Ujombani ndio kwao zaidi na ndiko anakokulia.
Kwa falsafa yao mama
ndiye hasa anayemjua baba wa mtoto na mama ndiye anayekaa na mtoto tumboni kwa
miezi tisa na kumnyonyesha kwa miaka miwili. Baada ya hapo ni yeye anayemlisha
na kumvisha hadi anapofikia umri wa kuweza kujitegemea. Hali hiyo husababisha
Mmakua au Myao anapooa anahama kwao na kwenda ukweni ambako atapewa shamba na
kuonyeshwa mahala pa kujenga ‘mdule’ nyumba zao, ambazo hujengwa kwa fito na
udongo paa likiwa la nyasi. Huo huwa
mwanzo wa maisha mapya
ya kijana huyo ambaye hata majina ya watoto wake hutolewa na wajomba.
Kwa jinsi nilivyomfahamu
baba yangu, mzee Karimanzira Kionambali, sikuiona namna yoyote ambayo angeweza
kukubali niingie katika utamaduni wa aina hiyo.
Jingine lililonitisha ni
ule utamaduni wao wa kula ‘dagaa changa’ yaani panya. Makabila mengi ya kusini
panya ni mlo halali wanaouthamini sana. Unaweza kutengenezewa kitoweo murua,
ambacho kitavutia sana, ukala na kushiba bila kujua kuwa unakula panya. Sikuwa
tayari kubahatisha hilo pia!
Kwa kheri Lulu!
nilivunja uchumba kimoyomoyo. Uchumba ambao hata ulikuwa haujaanza rasmi,
mchumba mwenyewe akiwa hata hazifahamu hisia zangu.
* * *
Sitaweza kuisahau tarehe
ya kufunguliwa kwangu. Ni tarehe ambayo nimeishi nayo akilini kwa takribani
miaka ishirini nikiisubiri kwa hamu. Lakini pale ilipofika na jina langu
kutajwa nikiitwa ofisini nilijikuta nikitetemeka kidogo. Wakati wafungwa
wenzangu wakinipongeza kwa kutoka
kwangu salama, mimi
nilitokwa na machozi. Waliyachukulia kuwa machozi ya furaha. Laiti wangejua!
Nilikabidhiwa vitu
vyangu. Suruali mbili, mashati mawili, viatu na kabrasha langu la vitabu.
Nililipokea kabrasha hilo harakaharaka na kulikagua. Kitu nilichokuwa na shauku
ya kukiona kilikuwepo! Kitabu changu cha benki. Nikakifunua. Akiba yangu
ilikuwa kama nilivyoiacha, shilingi 3,500. Nikakitia mfukoni. Nikakabidhiwa
tiketi ya treni, daraja la tatu, ambayo ingenifikisha hadi stesheni ya Kigoma.
Toka hapo ningejitegemea kufika Kasulu na hatimaye kijijini kwetu.
Nilikuwa mgeni sana Dar
es Salaam. Toka nilivyofika kwa muda ule mfupi na akina Leakey sikupata kurudi
tena. Sikuwa na wenyeji wala rafiki ambaye angeweza kunipokea. Hivyo, pale
lango la gereza lilipofunguliwa nami nikaruhusiwa kutoka sikujua toka hapo
ningeelekea upande gani wa dunia.
Kweli Mungu si Athumani.
Wakati bado nashangaa hapo nje gari la mkuu wa gereza lilitokea. Aliponiona
akaniita. “Hongera,” alisema “Nategemea hutajiingiza tena katika jambo lolote
la kinyume cha sheria ambalo linawea kukurejesha hapa.” Baada ya maneno hayo
aliutia mkono wake mfukoni na kuuchomoa ukiwa na noti tatu za elfu kumikumi.
Shilingi 30,000! Sikuyaamini macho yangu.
“Mbona nyingi sana
mzee?” nilimuuliza
“Nyingi?” alijibu
akicheka. “Hazikutoshi, lakini zitakusadia.” Akalitia gari lake moto na
kuondoka zake hata kabla sijamshukuru kikamilifu.
Kwa maelekezo ya wapita
njia nilifika kituo cha mabasi ya mjini wenyewe waliyaita ‘daladala’. Nikauliza
basi la kuelekea stesheni ya treni, nikapanda, kondakta, kijana mdogo mweye
lugha ya kihuni alikuwa mtu wa kwanza aliyenipa mshangao
wangu wa kwanza. Ni pale
aliponiomba nauli nami kumpa moja ya zile noti nilizopewa na mkuu wa jela.
Nilihesabu kwa makini chenji alizonipa. Alikata shilingi mia mbili.
“Nauli mia mbili?”
nilifoka.
“Kumbe ngapi?” alinijibu
kwa swali vilevile. Alinitazama kwa makini. Nywele zangu zilizoanza kuingia mvi
ziliashiriwa ovyoovyo. Suruali yangu iliyopauka ilikuwa pana kiunoni, fupi
miguuni ikinifanya nionekane kama moja ya vile vikatuni vinavyochorwa magazetini,
sura yangu pia, nadhani ilionyesha ugeni na mshangao kwa kila nilichokiona,
wingi wa watu wa magari, wingi na ukubwa wa majengo na kadhalika.
“Au umetoka pale
mjomba?” Yule kondakta alihoji. “Pale wapi?” nilimuuliza
Pale mtakuja, ukumbi wa
wanaume,” alijibu akielekeza mkono maeneo ya gereza.
“Unauliza jibu?” abiria
mmoja alidakia.
Sikuwajibu. Hofu
niliyokuwanayo juu ya maisha ya uraiani ilianza kunirejea. Shilingi mia mbili
kabla sijaingia gerezani ilitosha kumsomesha mtoto wa mwaka mzima. Wakati
huohuo kodi ya chumba kwa mpangaji ilikuwa senti ishirini, shati senti kumi.
Nauli halali ya basi kama hilo isingezidi senti tano.
Kumetokea nini?
Nilijiuliza. Tulipita Tabata, tukaingia barabara ya Mandela na kuifuata hadi
Buguruni ambako tulichukua barabara ya Pugu kueleka mjini. Barabara hiyo ikiwa
barabara pekee inayoelekea uwanja wa ndege wa Julius Nyerere magari yalikuwa
tele barabarani yakishindana kwa kasi. Aidha, barabara hiyo ilikuwa katikati ya
viwanda mbalimbali vilivyotapakaa hadi Chang’ombe na Vinginguti, hali iliyozidi
kuipa purukushani za aina yake. Mwendo wa kasi
wa magari hayo na
majonjo ya dereva wetu utadhani hana roho vilinitia roho mkononi hadi
tulipofika kituo cha stesheni ambapo nilishuka.
Mshangao wa pili
ulinisubiri nilipofika stesheni. Nilikuta pamefurika watu, wengi wao wakiwa na
mizigo tayari kwa safari. Lakini nilipofika dirisha la tiketi kwa nia ya
kuithibitisha tiketi yangu niliulizwa swali ambalo sikutarajia.
“Unataka kuondoka lini?”
“Leo.”
“Haiwezekani. Nafasi
zimejaa. Labda ufanye booking ya siku nyingine.”
“Haya, nipe tiketi ya
kesho.” “Kesho hakuna treni.” Sikuelewa. “Kwa nini?”
“Treni ni mara tatu kwa
wiki,” alinifafanulia. “Na ratiba yangu hapa inaonyesha kuwa daraja la tatu
limejaa hadi baada ya wiki tano hivi.”
Sikuamini kama nilikuwa
nimemsikia vizuri. Treni inasafiri kwenda bara mara tatu kwa wiki! Treni
hiyohiyo ambayo wasafiri ni wengi kiasi cha kuifanya ijae hadi kwa wiki tano
zijazo! Treni hiyohiyo ambayo ilikuwa ikisafiri kila siku na abiria wakichagua
kiti cha kukaa!
“Kwani kumetokea nini?”
nilimuuliza karani huyo.
Alinitazama kwa macho ya
mshangao kana kwamba nina pembe ya faru usoni. Nadhani aliishuku hata akili
yangu. Kwani badala ya kunijibu alifunga dirisha lake.
Kijana mmoja aliyekuwa
pembeni akifuatilia majibizano yetu alinivuta kando na kuniuliza “Unataka
tiketi ya kuondoka leo? Toa kitu kidogo tu utasafiri.”
“Tiketi ninayo.”
Nilijibu nikimwonyesha.
“Sasa tatizo lako nini?
Treni ikifika panda. Hakuna
atakayekushusha. Mradi
uwe tayari kwenda wima.” “Wima! Toka Dar es Salaam hadi kigoma!”
Niliamua kuufuata
ushauri wa kijana huyo. Bado zilikuwepo saa sita kabla ya treni kufika, masaa
mawili kabla ya muda wa kuondoka. Nikaamua kuutumia muda huo kutafuta benki
ambayo nilikuwa nimefungua akaunti yangu.
Ilikuwa kazi nyingine
ngumu. Mji ukiwa umepanuka sana, majengo mengi yakishindana kwenda angani, huku
watu wakiwa tele na pilikapilika kibao ilinichukua muda kabla ya kumpata mtu
aliyenielekeza hadi kuifikia benki hiyo.
Afisa niliyeelekezwa
kwake alinipokea kwa heshima zote katika chumba chake kidogo chenye hewa safi
iliyokuwa ikitoka katika kiyoyozi. Hewa ambayo iliniburudisha sana kutokana na
jasho tele lililokuwa likinitoka. Akapokea kitabu changu na kukitazama kwa
mshangao kidogo. Nadhani kwa umri wake hakupata kuona aina hiyo ya kitabu,
kwani vilishabadilishwa mara nyingi. Hata hivyo, alipoichezea kompyuta yake kwa
muda mrefu aliliona jina langu.
“Petro Kionambali sio?”
akauliza. “Ndiyo,” nilimjibu kwa matumaini. “Mbona huna pesa?” aliniuliza tena
Sikumwelewa, “Kwa vipi?
Mara ya mwisho nilikuwa na elfu tatu.”
“Ni kweli kabisa,”
alijibu. “Miaka ipatayo ishirini na mbili akiba yako ilikuwa elfu tatu. Halafu
ukapotea. Gharama za kutunza akaunti yako na kushuka kwa thamani ya pesa
kumefanya uwe huna pesa kabisa. Kwa kweli, benki inakudai.”
Ulikuwa mshangao wangu
wa tatu katika siku yangu ya kwanza uraiani. Nilihisi naishiwa nguvu, miguu na
mikono
ikitetemeka. Pamoja na
kiyoyozi jasho jembamba lilianza kunitoka. Kwa sauti dhaifu niliuliza,
“Unasema? Sijakuelewa… Nilitarajia fedha zangu ziwe zimeongezeka sana. Unajua
wakati ule fedha zile zingenitosha kununua magari hata mawili na kujenga
nyumba?”
“Ni kweli kabisa,”
alinijibu. “Tatizo lilikuwa lako wewe. Benki ikaendelea kukata gharama zake,
fedha zikaendelea kushuka thamani. Kibenki elfu tatu ni elfu tatu tu.
Ungekuwepo ukazitumia zingezalisha faida. Kwa bahati mbaya ulipotea. Kwani
ulikuwa wapi mzee?”
Sikumjibu. Nilijikongoja
kuinuka. Nikapepesuka. Nikajikongoja tena kutoka nje ya ofisi hiyo, macho
yakiwa hayaoni vizuri, miguu ikiwa haina nguvu.
.
YA ISHIRINI NA NNE
Dar jiji la Raha na
Karaha
ar es Salaam niliiona
chungu. Watu, majengo, magari na kila nilichokiona mbele yangu kilinitisha na
kuniogofya. Ndiyo, mji ulikuwa
mzuri, uking’ara kwa
usafi. Barabara zilimeremeta kwa usafi, magari yakipendeza ubora na thamani.
Watu pia walipendeza mitaani.
Wengi wao walivaa mavazi
ya bei, waliharakisha kwenda hapa na pale huku nyuso zao zikiwa na dalili za
matumaini kinyume cha ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Yote hayo niliyaona na
yalinivutia, lakini bado Dar es Salaam niliiona chungu. Ilikuwa baada ya lile
pigo la mwisho pale benki. Pigo ambalo liliniacha taabani, nusu hai nusu maiti.
Sikujua nilitoka vipi
pale benki hadi stesheni ya reli. Sijui ilikuwaje hata nikafika huko bila
kugongwa na moja ya magari tele yaliyotapakaa barabarani kama siafu. Mradi
nilijikuta mbele ya stesheni, macho yangu yakikodolea macho saa kubwa ya kwenye
mnara. Ilionyesha kuwa bado kulikuwa na saa kama tano kabla ya treni kufika!
Saa tano, ambazo niliziona kama miaka mitano! Sikuwa na jinsi. Ilibidi
niendelee
kusubiri. Kila dakika
moja ya kuendelea kusubiri ilinitesa kama msumari wa moto moyoni.
Mara kwa mara, nilitoa
zile senti zangu nilizopewa na mkuu wa gereza na kuzihesabu. Nilikuwa
nimezipunguza kwa nauli ya daladala. Mia moja nyingine nililazimika kuzitumia
kwa huduma ya choo! Nilikuwa na kiu lakini kila bomba nililofungua halikutoa
maji. Baadhi ya ‘wamachinga’ walikuwa wakiuza maji ya chupa. Chupa ndogo mia
tatu, kubwa mia saba hadi elfu moja. Maji ya kununua? Maji ambayo utoto wangu
wote nimeyachezea katika mito, katika maziwa na hata baharini! Niliamua
kujikaza kisabuni.
Nilikuwa na njaa
vilevile. Lakini sikuthubutu hata kuuliza bei ya chakula. Nilijua ingebomoa
zaidi visenti vyangu ambavyo sasa ilikuwa akiba yangu pekee maishani mwangu.
Akiba ambayo ilikuwa lazima inifikishe nyumbani kwetu. Nikaamua kuivumilia njaa
vilevile, nikifumbia macho watu wanaokula na kuizibia pumzi harufu tamu ya
maakuli.
Saa zilikuwa haziendi.
Nikaamua kupitisha muda kwa kutembeatembea mitaani. Nilifuata barabara ya
Samora. Macho hayana mipaka, yangu yalipenya vioo vya maduka mbalimbali na
kushuhudia vitu vilivyofurika madukani. Vifaa vya elekrtroniki, kama
televisheni, deki, dvd, projekta na vinginevyo vilikuwa tele katika sura na bei
mbalimbali. Nguo, viatu, pochi za kinamama na vinginevyo vilikuwa tele. Duka
moja lilibandika bei kwenye bidhaa zake, viatu 120,000/= suti 550,000/= pochi
85,000/=! Sikuelewa. Sikuelewa zaidi pale nilipoona maduka hayo yakiwa yamejaa
watu wakinunua vitu hivyo kwa fujo kana kwamba wana viwanda vya kuchapa noti.
Macho yangu yalivutwa pia na watu, hasa wasichana.
Mavazi yao yalinitisha.
Baadhi walivaa nguo fupi sana,
mapaja wazi, sehemu
kubwa ya tumbo nje huku wakitembea hadharani bila wasiwasi wowote. Baadhi
ilikuwa vigumu kujua kama walikuwa wasichana au wavulana kwa suruali zao za
jeans. Fulana na kofia kwenye vichwa. Kitu kingine kilichonishangaza ni kuona wasichana
wengi walivyofanana. Karibu wote walikuwa weupe! Karibu wote walikuwa na nywele
za kizungu! Wengi midomo yao iling’ara kwa rangi nyekundu kama ndege! Wengi
walinukia manukato makali ambayo siku za nyuma ungeamini kuwa umepishana na
jini! Sikuelewa hali hii hadi nilipofikia duka moja lililokuwa likiuza aina
mbalimbali za nywele kama nilizoona kwenye vichwa vya akina dada na kila aina
ya vipodozi! Kumbe!
Wavulana wengi nao
walinikatisha tamaa. Walivaa jeans zao ambazo zilichakaa au kuchakazwa makusudi,
sweta au fulana zenye picha za wacheza sinema wa Marekani kama Rambo na
eb 3, 2021
Thread starter
Add bookmark
#175
schwarznegger, huku
wakiwa wamefunika vichwa vyao kwa kofia au vitambaa vyenye nembo za bendere ya
Marekani. Baadhi yao walisuka nywele zao, baadhi walivaa hereni! Ilikuwa vigumu
kujua kuwa vijana hao walikuwa Watanzania au Wamarekani weusi hadi pale utakapowasikia
wakizungumza Kiswahili. Lakini Kiswahili hicho nacho kilikuwa na manjonjo yake.
Kwa kweli, kilistahili kuitwa Kiswaengilish kwa jinsi kilivyochanganywa maneno
ya Kiingereza na hata ya mitaani ambayo watu kama Shaaban Robert wangefufuka,
wangeweza kuangua kilio.
Wakati huo nilikuwa
tayari nimeloa chapachapa kwa jasho. Joto la hapa, mara nyingi linatisha.
Nilitamani kununua leso kama nilivoona wengine wakifanya lakini sikuthubutu.
Shilingi mia tatu za kulipia kitambaa hicho niliziona kama milioni. Nikawa
nikitumia kiganja au kiwiko cha mkono walao
kupunguza jasho la usoni
ili niweze kuona niendako.
Wingi wa watu lilikuwa
tatizo jingine. Mara kwa mara, niligongwa na mtu au kupigwa kikumbo
kilichofanya nikaribie kula mweleka. Nilipogeuka kumtazama mtu niliyegongana
naye alikwishakwenda zake bila hata kugeuka nyuma. Hiyo ilinifanya nikumbuke
kile nilichosoma nikiwa gerezani juu ya kasi ya ongezeko la watu jijini hapa.
Kwamba mwaka 1925 mji huu ukiitwa Mzizima ulikuwa na watu 30,000 tu. Leo
unatisha.
Nilifika katikati ya mji
wa Dar es Salaam. Pale nilipopita miaka mingi iliyopita na kusimama mbele ya
sanamu ya yule Mjerumani machachari Bismarck akiwa na bunduki mkononi
kaielekeza baharini. Sanamu hiyo haikuwepo tena badala yake ilijengwa sanamu ya
askari mweusi kama mkaa, ikiwa na silaha vilevile kuashiria tulivyopigana na
kufa kwa vita ambavyo havikuwa vyetu. Niliitazama kwa muda kabla ya kuendelea
na safari yangu, taratibu hadi nilipoifikia bustani ya Ikulu. Miti mingi ya
asili ilikuwemo kama nilivyoiona mara ya mwisho. Hata hivyo, nilihisi kuwepo
kwa aina fulani ya upungufu. Nini kilichopungua? Nilijiuliza. Nikajibiwa na
ukimya mkubwa wa eneo hilo. Ni ukimya huo ulionipa jibu. Zile kelele za wanyama
na ndege mbalimbali, hasa tausi, hazikuwepo tena. Tausi wale, ambao mara ya
mwisho walinivutia sana kwa jinsi walivyoipamba bustani hiyo kwa maringo na ulimbwende,
mara kwa mara wakitoa sauti zao nzuri na kuifumua mikia yao iliyoficha kila
aina ya rangi hawakuwepo tena. Walienda wapi? Nilijiuliza bila matarajio ya
jibu lolote.
Nikashuka kilima cha
Ikulu na kufika Pwani ya Magogoni. Kigamboni ilikuwa upande wa pili wa bahari
kama nilivyoiacha. Lakini, sasa, badala ya kuvuka kwa mitumbwi ya makasia
kulikuwa na chombo maalum ambacho kilipakia
watu, magari, mazao na
hata mifugo yao na kuwavusha upande huu au ule. Nilitamani kuvuka katika
kupoteza muda. Lakini nilipoambiwa kuwa ningelazimia kulipia, niliachana na
mpango huo.
Nikalisogelea soko la
mnada wa samaki. Biashara ilikuwa ikiendelea kama kawaida. Kando kidogo, akina
mama walioitwa ‘mama ntilie’ walikuwa kazini wakitoa huduma ya chakula kwa
haraka na kwa bei nafuu. Wakati huo tayari natetemeka kwa njaa, chango
likinguruma kudai chochote, nilishindwa kujizuia zaidi. Nikaingia katika banda
la mmoja wao na kuomba wali kwa samaki. Nilikula wali mtamu sana wa nazi ambao
sikupata kuula kwa takribani miaka ishirini. Hata kabla sijakitafuna kichwa cha
samaki wangu mmoja kunguru tele waliozagaa huko na huko jiji zima alitua ghafla
na kukipokonya. Huyoo, akapaa hadi juu ya paa na kuanza kukila huku kunguru
wenzake wakimshangilia. Watu wawili watatu walicheka. Mama ntilie wangu
akaniongeza mboga, nikaendelea kula nikimlaani kunguru yule.
Nikakumbuka kusoma
mahala, ama gazetini ama kitabuni, juu ya tatizo la ndege hao waliozagaa mjini
Dar es Salaam, kwamba wameondokea kuwa kero ya kitaifa; wanaiba kila
kinachoibika ikiwa pamoja na nyaya za umeme au vifaa vingine vya kiufundi.
Kwamba ndege hao waliletwa nchini, kupitia Zanzibar mnamo miaka ya 1900 na
wakoloni wa Kiingereza kwa kusudi la kuwafanya wasaidie usafi kutokana na tabia
yao ya kula mabaki ya chakula, mizoga na takataka nyinginezo. Lakini hadi
kufikia mwaka 1930 walijifanya ndege wa mjini ambao ni nadra sana kuonekana
vijijini.
Nikauliza saa. Nilikuwa
nimetumia saa moja na robo tu toka nilipoondoka stesheni. Bado nilikuwa na muda
wa
kutosha. Nikaamua
kutembea tena, safari hii nikielekea Kariakoo. Kinyume na safari yangu ya
mwisho mjini hapo sikuona pori wala jani. Kisutu ambayo zama zile nusu yake
ilikuwa pori, fisi wakirandaranda kutafuta chochote, sasa ilikuwa sehemu ya mji
iliyotapakaa watu na majengo hadi upeo wa macho. Kilabu cha askari wa zamani
kilikuwa pale. Lakini sasa kilijengwa jengo bora zaidi la ghorofa likiwa na
wapangaji tele wenye shughuli zao. Ukumbi ulikuwa pale lakini haukuwa na
pilikapilika zile za zamani. Ama wanachama wengi walikuwa wamekufa kwa umri
mkubwa ama wamekata tamaa.
Kariakoo nayo ilikuwa
muujiza mwingine. Pengine soko jipya lililojengwa juu ya lililokuwa handaki la
kivita enzi za Mjerumani lilikuwa limevuta watu toka kila pembe ya mji na nchi
ama Mungu alikuwa amedondoshea neema eneo hilo. Si haki kabisa kusema watu
walikuwa wengi, bali walifurika! Mitaa ya Kongo na Msimbazi ilikuwa haipitiki.
Kila mmoja akiwa na pilikapilika zake. Nje na ndani ya soko ndiyo ilikuwa
kabisa. Kupumua peke yake ilikuwa shida, achilia mbali kutembea.
“Dingi vipi… mbona
unashangaashangaa? Ambaa tupite,” kijana mmoja alinifokea baada ya kunipiga
kikumbo.
Nikageuka kumtazama.
“Unashangaa nini?
Kashangae feri, ambako shilingi inazama meli inaelea. Siyo hapa.”
Aliongeza.
Sikumwelewa kabisa.
Nikajikokota kuondoka.
Ilikuwa kazi kubwa
kujichoropoa toka katika umati huo na kuifuata barabara ya Uhuru hadi stesheni
ambako niliamua kukatisha moja kwa moja na kuisubiri treni.
Nilijiunga na wasafiri
wenzangu, wengi wao wakiwa na
mizigo na familia zao.
Mmoja kati yao, aliyekuwa na mizigo mingi zaidi alikuwa msichana wa Kizungu.
Mwembamba, mwenye pua ndefu na sura ya utulivu. Alikuwa peke yake akilinda
mizigo yake kwa makini. Hali hiyo ilinifanya mie pia nizikumbuke pesa zangu. Nikatia
mkono wangu mfukoni kwa nia ya kuzipapasa.
Mfuko ulikuwa mtupu!
Nilishtuka kama niliyeguswa na waya wa umeme. Nikainuka na kukagua kila mfuko
wangu. Hamkuwa na kitu. “Nimeibiwa!” nilisema kwa sauti huku nikitetemeka.
Msafiri mmoja aliyekuwa akisubiri usafiri kama mimi aliniuliza taratibu,
“Umeibiwa nini mzee?”
“Pesa,”” nilimjibu.
“Nyingi?”
“Hapana za kutosha
lakini. Zilikuwa pesa zangu pekee.”
“Pole sana. Alisema.
Umeibiwa hapa?” “Hapana. Bila shaka ni Kariakoo.”
Alinishangaa, “Ulienda
Kariakoo? Kule hakufai kabisa.” Nikamkumbuka yule kijana aliyenipiga kumbo na
kisha kuniita ‘Dingi’. Nilihisi hatukugongana naye kwa bahati mbaya.
Alikusudia. Ni yeye aliyeniibia au kuandaa mazingira ya kuibiwa kwangu. Sasa
sina hata shilingi moja. Sina kitu chochote ninachoweza kuuza nipate walao
nauli ya kunitoa
Kigoma mjini na
kunifikisha Kasulu!
Badala ya kulia
niliangua kicheko. Kwa jinsi nilivyovaa, nilivyochakaa kwa jasho na vumbi,
nadhani watu waliokuwa wakinitazama walishuku iwapo nilikuwa na akili timamu au
la. Sikujali. Niliendelea kucheka, peke yangu. Kilikuwa kicheko cha uchungu,
ambacho baadaye kiligeuka kuwa kilio. Nilijificha katika uchochoro mmoja na
kuruhusu machozi kunitririka.
Muda wa treni kufika
ulikaribia. Kila mmoja alikaa tayari kwa vita ya kuwahi kuingia ndani. Lakini
pale mmoja wa makarani wa TRC alipouendea ubao wa matangazo na kuandika kitu
kwa chaki kila mtu alipigwa na butwaa. Mimi nilichanganyikiwa zaidi, mara baada
ya kuusoma ujumbe ule. Yule mwanamke wa kizungu, ambaye bila shaka hakujua
Kiswahili vizuri alinisogelea na kuniuliza kwa Kiswahili chake
kibovu, “Hiyo maana yake
gani?”
Nikamfahamisha kwa
Kiingereza. “Wanasema leo hakuna treni, hadi kesho.”
Yeye pia alipigwa na
butwaa. Akanikazia macho ya mshangao kabla hajauliza tena, “Kwa sababu gani?”
“Sijui. Hawakuandika
sababu.” “Na hiyo kesho, ni saa ngapi?” “Hilo pia hawakueleza,” nilimjibu.
Mama wa watu alitazama
lundo la mizigo aliyokuwa nayo, akatazama kundi la watu waliokuwa pale, ambalo
hakuweza kupambanua nani alikuwa msafiri kweli nani kibaka; akazidi
kuchanganyikiwa.
Minong’ono mingi ilikua
ikiendelea. Habari zilikuwa zimevuja. Treni ya mizigo ilikuwa imeanguka huko
Kilosa na kufunga njia. Jitihada za kuinua na kisha kurekebisha uharibifu
uliotokea zisingekamilika hadi kesho yake. Hivyo, hakukuwa na namna ya kuondoka
hadi jioni ya kesho, kama tutakuwa na bahati.
Nilimfahamisha hayo yule
mama wa Kizungu. Kiasi alielewa. Akanishukuru. Nikamwona akihangaika kutafuta
namna ya kuondoka na vitu vyake vingi. Masanduku, maboksi na vikorokoro tele
ambavyo hata sikuweza kubuni vina nini ndani. Nikajitolea kumsaidia. Tulibeba
mizigo hiyo kwa taabu hadi chini ya mnara wa saa ambapo alizungumza na dreva
mmoja wa teksi,
wakakubaliana. Tukapakia vitu hivyo katika gari hilo.
“Wewe je? Utalala wapi?”
Aliniuliza wakati akijiandaa kuingia ndani ya gari hilo.
“Nitafanya maarifa.”
Nilimjibu
Alinitazama kwa muda
kabla hajaifungua pochi yake ndogo na kutoa noti ya shilingi elfu kumi ambayo
alinikabidhi. Katika hali ya kawaida nisingeweza kupokea fedha hizo, lakini kwa
hali niliyokuwa nayo na shida ingekuwa dhambi kubwa kuzikataa. Nilimshukuru mara
mbilimbili, kimoyomoyo nikimshukuru mara elfu na mbili. Ilikuwa kama nimepata
milioni kumi!
Nikarudi stesheni.
“Maarifa” niliyokusudia kufanya yalikuwa ni kuupitisha usiku hapo stesheni,
ikiwezekana nilale juu ya viti vyao vya mbao, kuisubiri kesho. Sikuwa na bahati
hiyo. Mara tu nilipopata kiti na kujipumzisha alikuja askari mmoja wa shirika
hilo na kututangazia kuondoka hapo mara moja, utadhani tulipenda kuwa hapo.
Tulipositasita walianza kutuswaga kama mifugo. Hatukuwa na namna zaidi ya kuinuka
na kuondoka.
Niende wapi?
Nilijiuliza. Wakati huo usiku ulishaingia, yapata saa mbili hivi. Tukio la
mchana kule Kariakoo lilikuwa limenitia hofu kubwa ya kuibiwa tena. Kutembea
usiku kucha pia kuliniogopesha. Hatari elfu moja na moja zingeweza kunitokea;
ningeweza kupigwa na majambazi kwa kufikiriwa kuwa nina pesa; ningeweza
kukamatwa na polisi na kurudishwa jela kwa kosa la uzuluraji. Ningeweza hata
kuuawa na walinzi wa mabenki na majumba mengine kwa kisingizio cha kujaribu
kuiba; na kadhalika na kadhalika.
Wakati nikijiuliza hayo
nilikuwa nikirandaranda mitaani kwa hofu ya kukaa mahala pamoja kwa muda mrefu
na kushukiwa.
Nilishangazwa na utulivu wa mji, tofauti kabisa na mchana. Watu wengi walijaa
katika vituo vya mabasi wakipigania kurudi makwao, pembeni mwa mji. Katikati ya
mji watu wengi niliowaona walikuwa Wahindi. Walipita katika magari yao au
kuketi katika sehemu zinazotengenezwa vinywaji na kuku choma wakitumia. Nasikia
wao, kwa ajili ya rangi zao na imani ya watu wengi kuwa wana fedha nyingi zaidi
ni waoga wa kuishi uswahilini. Wako tayari kuishi mtu na mkewe na mama na na
baba na watoto sita katika kijumba chenye chumba na sebule badala ya kwenda
kando ya mji ambako wangechanganyika na Waswahili.
Niliacha barabara ya uhuru,
nikaifuata ya Bibi Titi. Nikaifikia bustani ya Mnazi mmoja. Nikashangaa kuona
kundi la watu, wakubwa kwa wadogo wakiwa humo ndani. Baadhi walikuwa wakipika
kwa kuni.
Nikawasogelea kwa
matumaini ya kupata hifadhi ya kupumzika hadi kesho. Haikuwa. Kumbe hawa
walikuwa ombaomba, jamii mpya iiliyokuwa imeibuka na kujengeka nchini. Wakati
wazazi walikuwa na tatizo moja au jingine, ama katika viungo ama katika mfumo
wa kufikiria, watoto walitumiwa zaidi katika kuomba wapita njia, hasa wenye
magari. Watoto hawa hawakuwa na mipango wala matumaini ya kwenda shule. Hivyo,
walikuwa wakiandaliwa kuwa ombaomba wazoefu au majambazi sugu wenye hasira na
maisha. Zaidi ya kuwakamata mara kwa mara na kuwarejesha vijijini, ambako
walikaa siku mbili tatu na kurudi zao mijini, hakuna jitihada kubwa ya dhati
iliyofanyika kuondoa tatizo hili linalozidi kuchanua.
Jamii hiyo haikuonyesha
dalili za kunitaka katika kundi lao. Hata salamu zangu hazikujibiwa. Badala
yake walinong’ona wenyewe kwa wenyewe kabla ya kuanza kutafuta silaha zao,
fimbo, mawe na hata upanga. Sikusubiri
kufukuzwa. Nikajiondoa
harakaharaka na kuendea kituo cha mabasi kilichokuwa na watu tele.
Naweza kupata wapi
sehemu ya kulala? Nilimuuliza mtu mmoja aliyekuwa akisubiri basi.
Alinitazama kwa macho ya
dharau, bila shaka akinichukulia kama kibaka aliyekuwa akitafuta namna ya
kujichanganya ili baadaye apore chochote kinachoporeka.
Mtu wa pili alinijibu
kwa kunielekeza kwa mkono. Nikainua uso wangu. Jengo kubwa lililopaa angani kwa
takribani gorofa nane lilikuwa likimeremeta mbele yangu kwa nuru ya rangi
mbalimbali toka katika vioo. Maandishi yenye maremborembo yalikuwa yakicheza kwa
kuwaka na kuzimika, kila herufi kwa wakati wake na kusomeka, Peacock hotel.
Nikamtazama jamaa yule
na kumcheka kimoyomoyo, jambo ambalo hakunielewa. “Kama haikufai,” alisema.
“Ziko nyingine tele. Zipo za shilingi 500,000 kwa siku. Ziko za 100,000/= na
hata zile za 20,000/=. Ni mfuko wako tu. Unaweza kulala Sheraton, unaweza
kulAla Kilimanjaro hotel au ukitaka Holiday Inn. Kama unataka hoteli za
ufukweni nenda zAko Kipepeo Kigamboni, nenda Kunduchi au Bahari. Ziko tele…”
Nikabaini kuwa nanidhihaki.
Nikasogea na kumnong’oneza karibu kabisa na sikio lake, “Natafuta hoteli za
chumba cha shlingi elfu moja au mbili, sio zaidi.”
Akacheka. Kisha akasema,
“Hizo pia nyingi tu. Utazipata Manzese kwa mfuga mbwa, Buguruni kwa Bibi
Tarabushi au hata Mwananyamala kwa Mama Zakaria. Ukiwa na bahati hata Mapipa
utapata.”
“Ni wapi huko?”
nilimuuliza. “Panda basi, nitakuonyesha.”
Nilimfuata ndani ya
basi. Tukaketi kiti kimoja. Alishajua
kuwa nilikuwa mgeni wa
mji. Hivyo, alinipa hadithi moja baada ya nyingine juu ya mji na vitongoji
vyake.
“Unajua kwa nini
panaitwa Mapipa?” alitaja. “Zamani palikuwa na vibanda vilivyojengwa kwa
mapande ya mapipa juu na chini. Mapipa hayo ni yale yaliyotupwa wakati wa
ujenzi wa barabara ya Morogoro. Yalikuwa na soko kubwa pale Mapipa.
“Lakini wakati ule
Magomeni haikuwa kama hii ya leo. Mitaa yote ilikuwa na lami. Umeme uliwaka
kila mtaa. Mifereji ya maji machafu ilikuwa imejengwa na inahudumiwa vizuri.
Leo hii kila kitu kimekufa. Maji machafu yanamwagika hadi barabarani. Taa
zimekufa, lami imekufa. Hata mabomba hayatoi maji.”
“Nini kilitokea?”
nilimuuliza. “Sijui,” alijibu
Pamoja na maelezo yake
nilikuwa nikishangazwa pia na ukubwa wa mji wa Dar es Salaam. Toka katikati ya
mji hadi tunafika Magomeni isipokuwa jangwani ambako wakati wa masika hufurika
maji, sikuona pori. Mji ulikuwa umeungana, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa.
Wakazi walikuwa hawalali. Karibu kila mtaa niliona baa mbili au tatu, zikiwa
zimechanganyika na makazi ya watu, makelele ya muziki yalishindana kwa sauti.
“Hivi hakuna biashara
nyingine Dar es Salaam?” nilimuuliza mwenyeji wangu huyo.
“Kwa nini?”
“Naona baa kila mahala.”
Pombe ndiyo bidhaa
inayotoka kuliko nyingine,” alinijibu. “Maduka mengi ya vitabu yamefungwa. Watu
hawanunui isipokuwa kile kilicholazimishwa na Wizara ya Elimu. Maduka ya madawa
pia yameanza kukosa wateja. Watu hawana uwezo
wa kununua dawa dukani
wala hospitalini. Mtu anaweza kufa hata miguuni mwa daktari, kama hana pesa za
dawa hakuna matibabu.”
“Kwa nini?” Nilimuuliza
kipumbavu. “Sijui,” alinipa jibu lilelile nililostahili.
Karibu kila kituo cha
basi tuliwaona wasichana wadogowadogo waliovalia mavazi yao ya kutisha, wenyewe
wakiyaita ya kisasa; wakiwa wamesimama. Hawakupanda basi lolote wala kuonyesha
kuwa na haraka yoyote, usiku mwingi kama huo. Niliwatazama kwa mshangao.
Mwenyeji wangu aliusoma
mshangao wangu, “Changudoa!” akasema.
“Nini?”
“Wale pale! Wanajiuza.
Tunawaita Changudoa,” alifafanua.
“Si nasikia kuna maradhi
hatari yanayoitwa UKIMWI?” “Naam,” alinijibu. Tena omba kusikia usiombe kuuona
kwa macho. Lakini kwa
wale, UKIMWI ni ajali kazini!” Sikuelewa. Nikanyamaza.
Tulifika Manzese.
Tukashuka kituo cha karibu na daraja pekee la angani, lililoikata barabara ya
Morogoro toka kulia hadi kushoto kupunguza ajali za barabarani ambazo
niliambiwa ziliua waenda kwa miguu kwa wingi kuliko UKIMWI au malaria.
Nilielekezwa kuelekea
kushoto. Kona moja, uchochoro; kona ya pili; uchochoro. Mara tukamezwa na kiza
kizito. Bila msaada wa nuru hafifu toka katika vyumba vya wakazi wa eneo hilo
nadhani hata mwenyeji wangu angeweza kupotea. Nilimfuata katika vichochoro
hivyo, vilivyobana na kugubikwa na uchafu mwingi. Mara kwa mara tulikanyaga
dimbwi la tope.
Mara mbili tatu
tulikurupusha wanyama wadogowadogo ambao mimi nilidhani ni paka lakini mwenyeji
wangu akaniambia, panya!
“Mbona wanene vile?” nikauliza.
Wanakula na kushiba.
Manzese hii mjomba,” alijibu. Tulizidi kuingia ndani. Mwenyeji wangu alitembea
haraka akipenya hapa na kutokea pale. Nilianza kuogopa. Kwanza, nilihisi kuwa
hajui tunakokwenda. Pili, nilianza kumshuku kuwa huenda alikusudia
kunitendea ubaya.
Nikatamani kugeuka nirudi nilikotoka. Hata hivyo, hofu ya kupotea na kupatwa na
mabaya zaidi ilinizuia. Badala yake nikamuuliza taratibu, “Mbona hatufiki?”
Aligeuka na kunitazama.
Aliisoma hofu katika macho yangu. Akacheka. “Hofu ya nini?” aliuliza baadaye.
“Hapo ulipo hata laki huna, achilia mbali milioni. Nataka kukusaidia upate
mahala pa kulala, kwani unaonekana kuwa unahitaji msaada. Nikikuacha utapigwa
na vibaka na kuvuliwa hata nguo ulizovaa.”
Nikamwamini.
Hatimaye tukaifikia
nyumba ya wageni aliyoikusudia. Nje ya nyumba hiyo kwenye uchochoro mmoja
kulikuwa na watu wanaokunywa pombe, wake kwa waume. Mwenyeji wangu alionekana
mwenyeji hapa. Alimwita mmoja wa watumishi wa nyumba hiyo kwa jina, “Rehema!
Mpe chumba mjomba wangu. Mchagulie chumba safi. Sawa?”
Rehema, msichana mkubwa
mnene, aliyeonekana kalewa aliniashiria kumfuata. Nyumba haikuwa na umeme.
Mishumaa miwili, mmoja uliowekwa mlango wa mbele na mwingine mlango wa nyuma
ndiyo iliyotuongoza. Niligeuka
ili kumshukuru mwenyeji
wangu. Hakuwepo. Alikwishapenya uchochoro mwingine na kuondoka zake. Nikamfuata
Rehema. “Unataka chumba che bei gani?” Aliniuliza. “Vipo vya
elfu mbili na elfu na
mia tano.” “Nipe cha elfu na mia tano.”
Kilikuwa chumba cha
uwani, kidogo sana. Dirisha lilikuwa moja, dogo vilevile. Kitanda chao
kilitosha mtu mmoja tu, si zaidi.
“Kinakufaa?”
“Kinafaa sana.”
Nilimjibu.
“Ngoja nilete mshumaa.
Umeme umekatwa huu mwezi wa tatu. Na kishoka leo kachelewa kuja.”
“Kishoka ndiyo nani?”
nikaomba kuelewa.
“Jamaa yetu ambaye huja
usiku kuturudishia umeme. Asubuhi sana huja tena kuukata kabla TANESCO
hawajapita mitaa hii,” alifafanua.
“Kwani mnadaiwa pesa
nyingi?” nilihoji.
“Nyingi sana. Kama
milioni tatu na laki sita hivi. Maji yenyewe mwaka wa nne hayajatoka. Lakini
bili yao imefika laki tisa na nusu.”
Nikashangaa. Kwa hesabu
za haraka haraka nyumba hiyo, yenye vyumba sita pekee na baa ya uchochoroni
haikuwa na uwezekano wa kupata walao laki mbili kwa mwezi. Gharama hiyo ya
umeme na maji ilitokea wapi? “Mtalipa?” nilimuuliza.
“Nani alipe? Unalipa
deni linalolipika. Lisilolipika unaachana nalo,” alinisomesha.
Rehema alipoondoka
nilipanda kitandani kwangu kulala. Ndio kwanza nikabaini kuwa godoro lilikuwa
kuukuu, pengine halikupata kubadilishwa toka nyumba hiyo ilipojengwa. Mbavu
zangu zilikwenda moja kwa moja kukutana na chaga
za mbao. Si hilo tu,
dakika mbili tu za kupumzika juu ya kitanda hicho, nilikaribishwa na mbu na
kunguni. Wakati mbu wakiuma baada ya kelele zao za vitisho masikioni, kunguni
wao walinitesa kwa kufyonza damu yangu kimyakimya na kunisababishia maumivu
mengine. Nilifanikiwa kuwaua kunguni wawili watatu. Lakini harufu yao kali na
damu nyingi toka kwa wateja wao ilinitia kichefuchefu
Adha ya tatu ilikua
ikinisubiri. Joto. Chumba kilichemka kwa joto kama tanuru. Nikainuka na
kufungua lile dirisha pekee. Tendo hilo lilileta karaha badala ya faraja.
Harufu nzito, ya kutisha iliyoingia chumbani humo toka dirishani ilinifanya
niamke na kumwita Rehema. “Harufu hii ya nini?” nilimuuliza. “Hilo dirisha huwa
alifunguliwi!” alinionya akilifunga
mara moja. “Kuna mfereji
wa maji machafu hapo. Haujazibuliwa leo mwaka wa sita. Kwa hiyo, maji
yametuwama uchafu umeoza na kufanya harufu ya kutisha.”
“Kwa nini hauzibuliwi?”
“Sijui”
Nikazidi kushangaa.
Mambo gani haya ninayoyashuhudia, siku moja tu baada ya kutoka jela. Kama
maisha ya uraiani ndiyo haya, malazi ndiyo haya, iko wapi tofauti ya kuishi
uraiani na gerezani?
Tofauti kati ya maeneo
ya Manzese na katika ya mji pia ilinishangaza sana. Wakati kule kulionekana
kama Peponi huku hakukutofautiana sana na Jehanamu. Kama ungetokea moto,
uteketeze nyumba moja ni dhahiri kuwa mamia ya nyumba yangeungua na maelfu ya
watu kupoteza maisha. Nikaelewa kwa nini yanapozuka maradhi kama kipindupindu
na hata UKIMWI hayaondoki kabla ya kuteketeza mamia ya watu katika maeneo kama
haya. Huu ndio uhuru tulioupigania na kuupata? Nilijiuliza. Huu ndio Ujamaa
niliousikia mara
kwa mara toka gerezani?
Au ndio Azimio la Arusha lililopigiwa sana kelele?
Wakati nikiwaza hayo
jambo la ajabu likatokea. Umeme uliwaka. Kishoka alikuwa amefika nadhani. Feni
chafu lililokuwa darini likapata uhai. Ama liliwafukuza mbu ama waliogopa
kelele zake, kwani niliona mbu wakipungua ghafla. Kunguni nao walijificha.
Nikapanda kitandani na kujilaza. Usingizi ukanichukua.
Niliamka kesho yake saa
tatu. Nilikuwa mgeni peke yangu katika nyumba hiyo. Rehema alikuwa akipita
chumba hadi chumba kukusanya shuka kwa ajili ya kuzifua. Alinionyesha bafu
ambalo lilikuwa na maji ya ndoo, kipande cha sabuni ya mchi kikiwa pembeni.
Nilioga na kujisikia nikiburudika kidogo, hali ambayo ilinifanya nisikie njaa
ikianza kulitekenya tena tumbo langu. Niliishtakia kwa Rehema ambaye
alinielekeza uchochoro wenye ‘mama ntilie’ pekee eneo hilo. Nilimpata. Nikanywa
chai ya shilingi hamsini, chapati mbili za mia na maharage ya mia. Chakula na
bei vilinifuraisha sana.
Nikaanza kazi ya
kutafuta njia ya kurudi barabarani. Nilielekezwa mara nne na kupotea mara mbili
kabla ya kumwuliza bwana mmoja mtanashati ambaye aliniambia nimfuate.
“Ni afadhali kupotea New
York, kuliko katika vichochoro vya Manzese. Humu unahitaji akili za ziada kujua
njia ya kwenda na kutoka kwako,” alisema kiongozi wangu huyo mpya wa msafara.
“Kwa nini inakuwa hivi?”
Nilimuuliza. “Umeshafika mwanza?” Alinijibu kwa swali jingine. “Zamani sana.”
“Fika sasa hivi uone,”
alisema “Kule watu wanajenga hata juu ya mawe. Ile mandhari nzuri ya asili
imepotea kabisa
kwa ajili ya watu
kutafuta makazi ya kuishi. Tatizo unaloliona hapa
Jane aliweza kumfuatilia
sokwe toka anazaliwa, anakua, anabalehe hadi naye anapata mtoto, alinukuu
mwenendo na tabia zao, chakula chao, tiba zao na hulka zao mmoja baada ya mwingine.
Alimfahamu kila sokwe na kila familia ya sokwe vilivyo, kiasi cha kujua nani
kiongozi wao, nani anapinduliwa uongozi na nani kapindua. Utafiti makini wa
aina yake duniani ambao tayari umempatia shahada ya udaktari.
“Unajua hujaniambia jina
lako?” Alinizindua. “Naitwa Petro Mtukwao Kionambali,” nilimjibu.
Jane alifahamu Kiswahili
kidogo sana. Kati ya machache aliyoyafahamu jina la ‘Mtukwao’ au ‘Kionambali’
lilimpa maana fulani, lakini hakuweza kuifafanua mara moja. Aliyataja majina
hayo mara mbili tatu, akikosea, kabla hajakata tamaa na kuniuliza maana yake,
“Petro bila shaka ni Peter kwa Kiingereza. Ni jina lenye asili ya Kigiriki
likiwa na maana ya mwamba au jabali. Hii Kionambali au Mtukwao ina maana gani?”
Jane alinitazama , “Ni
la Kiebrania,” nilimjibu. “Lina maana ya Mungu ni mwenye fadhila sio?”
nilimuuliza kabla ya kumjibu.
Jane alionyesha
mshangao. Nadhani hakutegemea kuwa pamoja na hali niliyokuwa nayo ningeweza
kufahamu mambo mengi kama ilivyokuwa. “Ni kweli kabisa,” alijibu baada ya
tabasamu fupi, “Kiona mbali?” alisisitiza.
Wazazi wangu hawakupata
kuniambia maana hasa ya majina yangu. Nadhani yalitolewa na babu kwa sababu
zake.
Hata hivyo nilimweleza
Jane hili na lile juu ya maana ya majina hayo.
Sidhani kama aliridhika.
Mara nilimwona akibadilika ghafla kama mtu aliyekumbuka jambo “Kionambali…. Mtu
kwao… nadhani nilipata kuyasikia majina hayo kabla ya leo,” alisema.
Nikacheka. “Unacheka
nini?”
“Nina hakika hujawahi
kulisikia mahala popote. Ni jina dogo sana katika nchi hii. Sijawahi kuandika
kitabu wala kucheza mpira hata nijulikane.”
“Hapana, nimelisikia
likitajwa. Si mara moja si mara mbili,” alisisitiza.
Sikuamini. Nikijua kuwa
alitokea kwao Uingereza, akakaa Kenya kwa muda kabla ya kuja nchini sikuona
vipi angeweza kukutana na jina langu. Hasa ikizingatiwa kuwa muda mwingi
nilikuwa gerezani.
“Unakwenda wapi?”
alinihoji. “Kigoma.”
“Nyumbani kwenu?”
“Ndiyo.”
“Kwa hiyo, safari yetu
moja.” “Bila shaka.”
Alisita kwa muda kabla
hajauliza swali jingine, “Kwa hiyo, unakwenda likizo?”
“Ndiyo na hapana,”
nilimjibu. “Una maana gani?”
“Nina maana kuwa ndiyo
nakwenda nyumbani; hapana siendi likizo.”
Jibu langu lilimshangaza
Jane, “Kwani unatokea wapi?”
Sikuona sababu ya
kumficha, “Jela.”
Kiasi nilimwona
akishtuka. Lakini, akiwa mwanamke mwenye roho ya chuma, anayeweza kuishi na
kuvumilia hasira za ghafla za wanyama hatari kama sokwe, alijirekebisha mara
moja. Badala yake aliniuliza kwa upole, “Nini kilitokea?”
Alikuwa binadamu wa
kwanza uraiani aliyetaka kujua masaibu yangu toka nilivyofungwa hadi
kufunguliwa. Akawa binadamu wa kwanza niliyepata kumsimulia, kwa tuo, yote
yaliyonitokea hadi nikatupwa gerezani kwa miaka mingi. Sijui kwa nini niliamua
kuwa wazi kwake. Nadhani ni kwa kuwa sikuwa na shaka kuwa ni mtu mwenye huruma
sana. Kama anaweza kuishi na sokwe…
Nilipofika sehemu ambayo
nilimtaja Dakta Leakey kama mwajiri wangu pekee ambaye niliishi naye kwa muda
mrefu nilimuona Jane akishtuka. Mara akanikatiza kwa kuuliza, “Leakey yupi?”
“Leakey unaemjua wewe.
Na mke wake Mary… wagunduzi wa fuvu la kale zaidi nchini,” nilimjibu.
Jane aliinuka na
kunikodolea macho ya mshangao. “Sasa nimefahamu wapi nilisikia jina lako kwa
mara ya kwanza,” alisema baadaye.
“Wapi?”
“Kwa akina Leakey.
Walikuwa hawaachi kukutaja. Walishangazwa sana na kutoweka kwako ghafla, bila
kuaga, mtu ambaye walidai kuwa walimtegemea sana katika shughuli zao.”
Ikawa zamu yangu
kushangaa, “Unawafahamu?” “Vizuri sana,” Jane alinijibu. “Walipata kuniajiri
pia.
Kutokana na mapenzi
yangu kwa wanyama na mazingira
Leakey alinishawishi
kwenda kwenu Kigoma kufanya utafiti
wa wanyama wale, binamu
zetu.”
Sikuwa na la kusema,
nikauliza, “Hawajambo?” “Nani?”
“Akina Leakey.”
Jane akacheka, “Wazima
sana. Kwa nini ulifanya vile?” “Kufanya nini?”
“Kufungwa.Kukubalikufungwabilakuwaarifu.
Wangeweza kukusaidia.”
Ilikuwa wazi kuwa Jane
hajui maana ya kufungwa, hasa katika nchi zetu za dunia ya tatu. Mnyama
anayefugwa ana uhuru mara mia zaidi ya mfungwa.
Wakati nikizungumza na
Jane nilimwona msichana mmoja, msafiri kama sisi, akinitazama sana. Nilimtupia
macho. Nikamwona akiyakwepa macho yangu kwa namna ya haya kiasi. Kitu fulani
kilinifanya nipate hisia kuwa namfahamu. Wazo ambalo nililipuuza mara moja. Jana
tu nimetoka jela, nitamjulia wapi msichana huyu?
Kitu kimoja kilinivutia
kumtazama msichana huyu alikuwa ana tofauti kubwa na wasichana wengine wengi
niliowaona jijini hapo. Alikuwa Mwafrika halisi. Nywele zake zilikuwa fupi,
ambazo hazikupata kuathiriwa na madawa. Ngozi yake laini maji ya kunde, pia
haikuwa na dalili zozote za kuathiriwa na madawa hayo. Hata mavazi yake
yalikuwa ya heshima. Gauni jekundu lililomkaa vizuri lilimfunika hadi miguuni.
Lakini kuna kitu cha
ziada ambacho kilinivutia zaidi kwa msichana huyu. Halikuwa umbile lake wala
mavazi yake. Kilikuwa kitu fulani. Kwa bahati mbaya sikuweza kubaini mara moja
ni kipi hasa kilichonivutia zaidi kwake. Ningeweza
kukisomakituhichokatikamachoyake,lakinitayari
aliyakwepa macho yangu na kutazama upande mwingine.
Honi ya treni iliyokuwa
ikiingia stesheni iliniokoa kujibu swali la Jane pamoja na kuendelea kusumbua
fikra zangu juu ya msichana yule. pilikapilka za kuingia katika mabehewa
zikaanza. Mimi nikiwa sina mzigo wowote nilifanya kazi ya kumsaidia kupakia
vitu vyake katika chumba cha daraja la pili alicholipia. Mimi, nikiwa sina
namba ya kiti, nilipata debe moja la msafiri mwenzangu na kulikalia. Roho yangu
ilipumua pale dakika ishirini baadaye treni ilipoanza safari ya kuelekea bara.
Jing... jang… jing…
jang… tuliuacha mji na kuingia Buguruni. Jing… jang… jing… jang … vingunguti.
Jing… jang… jing… jang… Karokota. Taratibu tukauacha mkoa wa Dar es Salaam na
kuingia Pwani. Tulizipita stesheni za Soga, Ruvu na Magindu kabla hatujaiacha
Pwani na kuingia Morogoro katika stesheni za Kidugalilo, Ngerengere, Mikesa na
hatimaye Morogoro mjini.
Wakati huo usiku
ulikwishaingia. Sikuweza kuziona vizuri stesheni za Mkata, Kimamba na ile ya
Kilosa. Toka hapo tuliingia stesheni ya mpaka wa Morogoro na Dodoma, Kidete
kabla ya kufika Godegode, Gulwe na Kikombo. Tulifika Dodoma alfajiri ya siku ya
pili.
Jane alikuwa
akinitafuta. Alinikuta nikiwa nimeegemea mlango nikijaribu kupata chochote
ambacho ningeweza kupata juu ya mji wa Dodoma, makao makuu ya serikali baada ya
kuhamishwa toka Dar es Salaam. Zaidi ya majengo kadhaa, barabara pana zaidi na
watu wa kutosha zaidi bado Dar es Salaam niliyoiacha jana ilifanya Dodoma
ionekane kama mzaha kuiita makao makuu.
“Unajisikiaje?” Jane
aliniuliza
“Safi kama chuma cha
pua,” nilimjibu
Akacheka. “Twende
tukapate kifungua kinywa,” aliniambia.
“Wapi?”
“Mgahawa wa humu ndani.”
Nikamfuata. Tulipita
mabehewa kadhaa kabla ya kufikia behewa la chakula. Tukaketi. Aliagiza chapati
mbili, supu ya kuku na chai kwa kila mmoja wetu. Kwangu ulikuwa mlo ambao
sitapata kuusahau kwa muda mrefu. Toka nilipopata chai na maharage ya ‘mama
ntilie’ kula Manzese tumbo langu lilikuwa halijaonja chakula zaidi ya karanga
za mia moja nilizonunua humo ndani.
Tulikula taratibu. Kila
mara Jane akinidodosa juu ya mipango niliyokuwa nayo baada ya kutoka gerezani.
Hakunielewa pale nilipomwambia kuwa nilikuwa na mpango mmoja tu katika akili
yangu, ambao haukuwa ziadi ya kufika nyumbani, kumwona babu na wazazi wangu,
kama wako hai.” “Bila shaka ulitoka kwenu mikono mitupu… unataka
kurudi mikono mitupu?”
alinihoji. “Sina jinsi.”
“Kwa nini?”
Asingeweza kuelewa.
Asingeelewa hata kidogo hata kama ningemwelewesha vipi. Kwamba lazima nikaombe
radhi kwa kupoteza hirizi! Kwamba nina hakika mikosi na balaa nyingi ninazopata
zilitokana na kuipoteza baraka ile, hivyo lazima nioshwe kwa kutemewa mate
usoni. Mzungu, mwenye utamaduni tofauti na wangu angeelewaje? Sikujisumbua
kumwelewesha.
Jane akaamua kuifichua
siri iliyokuwa moyoni mwake. Alinitaka twende wote Gombe nimsaidie kazi. Kwamba
alikuwa na mipango ya kufungua kituo kingine cha sokwe kusini mwa ziwa
Tanganyika, katika milima ya Mihale, kilometa zipatazo
120 toka mjini Kigoma.
Kwa mujibu wa Jane milima hiyo ilikuwa na sokwe waliokadiriwa kuwa 700 katika
makundi kama kumi na mitano. “Siwezi kufanikisha peke yangu. Lazima niwe na mtu
mwaminifu, mwadilifu na pia tunayeelewana lugha vizuri,” alisema
“Halafu,” aliongeza.
“Mume wangu ana mpango wa kutengeneza filamu kubwa, itakayojumuisha vivutio
mbalimbali vya Tanzania. Kwa historia yako na uzoefu wako hakuna mtu ambaye
atamfaa zaidi yako.”
Hili la pili lilinivutia
zaidi. Ningependa sana kuwa sehemu ya historia ya mtu atakayefanikisha kazi
hiyo. Lakini nilikwishajiwekea nadhiri ya kutojihusisha na jambo lolote kabla
ya kufika kwetu. Ama niwaone wazazi wangu, ama niyaone makaburi yao.
Nilimweleza hivyo Jane.
Bado hakunielewa. Lakini hilo lilikuwa tatizo lake, halikuwa langu.
Safari ya mchana
ilivutia zaidi. Tulisimama dirishani mimi na Jane tukiangalia nje, kituo baada
ya kituo. Nkungu, Nala, Bahi, Kintinku, Saranda, hatimaye tukaingia Manyoni.
Watu na mazingira maeneo yote haya havikunifurahisaha sana. Ardhi ilijaa vumbi,
mtu mmoja hapa na pale. Hali iliyonifanya hisia za nusu jangwa zinijie akilini.
Hali kadhalika hali za wakazi wengi iliashiria umasikini mkubwa. Mavazi ambayo
wengi wao walivaa, baadhi wakitembea bila hata kandambili. Ilikuwa dalili tosha
ya umasikini. Hata wale waliokuwa na bidhaa, bidhaa zao ziliashiria kuganga
njaa tu. Mtu mzima
akiwa na vichane vitatu
vya ndizi, mwingine akiwa na chupa moja ya asali, yule sinia la karanga! Kwa
gari moshi ambalo hupita hapo mara mbili tatu kwa wiki sikuona kama biashara
hizo zilikuwa na namna yoyote ya kuwaondoa katika vibanda vya tembe tulivyokuwa
tukiviona toka tunaingia Dodoma hadi tunaiacha.
Stesheni ya Manyoni
ilishamiri kwa biashara ya kuku, walio hai kwa waliokaangwa.
Takribani kila mtu
alikuwa na sinia yenye mapaja ya vidari vya kuku wanaotamanisha kuwala. Bila
shibe ya mlo alionipa Jane ningejikongoja kununua paja moja. Ingawa baadhi ya
watu hudai kuwa hawa si kuku wa kawaida kwa ajili ya wingi wao. Wanadai baadhi
ya tunaowadhania kuku waliokaangwa ni kunguru na ndege wengine wa porini
waliozagaa katika maeneo hayo. Kwa kweli, ulikuwa mzaha wa watani wa Wanyaturu
na Wanyiramba.
Toka Manyoni tuliingia
Itigi, kaskazini hadi Malingwe. Jua likaanza kuzama. Jane alirudi chumbani kwake
kujisomea kitabu mimi nikaendelea kuranda ndani ya mabehewa hayo mengi.
Tukafika Nyama, tukaingia Igagula. Saa mbili za usiku tulifika Tabora. Hapo
tulichukua muda mrefu kutokana na pilikapilika nyingi za kubadili mabehewa,
kukagua vichwa vya treni na pengine kufanya ukarabati.
Nilitamani kuutumia muda
huo kuchepuka kidogo nikautupie macho, walao kidogo mji wa Tabora, ambao uko
kidogo nje ya stesheni hiyo. Hata hivyo kwa kuchelea kuachwa sikuthubutu.
Niliishia kuchungulia tu nje ya stesheni ambako niliiona ile miembe iliyozeeka
lakini bado ilikuwa ikipamba na kuzaa embe tamu za dodo na bolibo.
Niliona pia kundi kubwa
la mbuzi wasio na mlinzi wakirandaranda kando ya barabara hiyo. Mbuzi wa
Tabora?
Nilijiuliza
nilipokumbuka simulizi ya mji wa Tabora kuwepo na mbuzi wengi wasio na mmiliki
ambao hutembea ovyo mitaani bila kubugudhiwa, mbuzi ambao inaaminika kuwa kwa
namna moja au nyingine wanahusiana na ama ushirikina ama laana fulani. Mwenyewe
alifariki zamani na kufanya wawe hawana mwenyewe, lakini kila mtu ambaye
huthubutu kuwala hudhurika na hata kupoteza maisha. Jambo ambalo lilisababisha
hata wezi wa mjini hapo wawaogope.
Honiyakuashiriasafariikapigwa.Nikarudiau
kuparamia behewa lolote lililokuwa karibu. Dakika tano baadaye safari ikaanza.
Ilikuwa awamu ya mwisho ya safari hiyo ndefu ya kilometa 2600 toka Dar es
Salaam hadi Kigoma. Hamu niliyokuwa nayo ya kufika nyumbani ikaanza kuingia
nyongo. Hofu ikaanza kuchukua nafasi. Hofu ya kutojua lipi nitalikuta huko
nyumbani. Habari za kufurahisha au kuhuzunisha, heri au shari. Hali kadhalika,
aibu ya kurudi mikono mitupu kama nilivyoondoka, baada ya miaka nenda rudi ya
kuhangaika pia ilinitesa sana. Sio siri, nilitamani garimoshi hilo lipate
ajali, mtu mmoja tu apoteze maisha;
Petro
Haikuwa. Treni
iliendelea kukata mbuga. Ikiwa safari ya usiku sikuweza kuona mabadiliko ya
ardhi toka ile ya nusu ukame. Ya Dodoma hadi Tabora hadi ile yenye rutuba
nyingi ya kutokea Tabora hadi Kigoma. Kelele za wasafiri kila tulipofika
stesheni ndizo ziliniashiria tuko wapi; Usoke, Kaliua, Suinge, Malagalasi,
Uvinza, Simbo, Luiche na hatimaye Kigoma
Ulikuwa mkesha wa aina
yake. Pilikapilika za kuingia katika mabehewa kila stesheni zilikuwa kubwa na
za fujo kubwa. Mizigo ilirushwa ndani ikifuatiwa na wababe; wake kwa waume.
Ilikuwa rahisi kwa mgeni kufikiria kuwa watu
wa Kigoma wana asili ya
vurugu. Lakini kamwe mwenyeji asingeweza kufikiria hivyo. Watu hawa hawakuwa na
njia nyingine yoyote ile ya usafiri. Maeneo mengi hayakuwa na barabara
iliyowaunganisha na upande mwingine wa dunia zaidi ya treni. Hivyo, kuachwa na usafiri
huo kulimaanisha kuharibikiwa kwa mipango yako ya safari pengine kwa wiki nzima
au zaidi. Hivyo, kutumia nguvu na ubabe lilikuwa jambo la lazima.
Tulifika Kigoma saa moja
na nusu za asubuhi, lakini kwa sababu za kijiografia ndio kwanza jua lilikuwa
likichomoza. Miale yake ilipenya milima ya Bangwe na kutuangazia pale stesheni,
kando kabisa mwa Pwani ziwa Tanganyika. Ziwa ambalo liliupokea mwanga huo,
likaujumuisha na maji yake yasiyo na rangi na kufanya limeremete kwa
mchanganyiko wa nuru ya rangi ya dhahabu toka angani na buluu toka katika lindi
la maji na kutoa sura ya kusisimua sana.
Nilishuka na kusimama
kwa muda hapo nje nikitazama huku na kule kana kwamba siamini kuwa nimerejea
nyumbani. Macho yangu yalivutwa na jengo imara la stesheni hiyo, lililojengwa
na Mjerumani toka enzi zile. Zaidi ya ukarabati wa rangi na pengine bati jengo
lile lilikuwa imara kama walivyoliacha. Wala halikuwa na dalili zozote za
kupoteza uimara wake katika siku za usoni.
Nikahamisha macho kwenye
jengo na kuyatupa ziwani. Kwa mbali, niliweza kuona mitumbwi na mashua za
wavuvi wakirejea Pwani baada ya shughuli zao za usiku kucha, lakini
kilichovutia zaidi macho yangu ni meli kubwa, yenye rangi nyeupe iliyotia nanga
katika bandari hiyo. Jina lake liliweza kusomeka hapo niliposimama, MV LIEMBA.
Hii ni mali yenye
historia ya pekee duniani. Kwanza,
inaaminika kuwa ni meli
ya kale kuliko zote duniani ambayo bado inafanya kazi. Pili, imezitumikia enzi
zote muhimu za historia ya Tanganyika ikiwa imeletwa na kuunganishwa na
Wajerumani miaka ya 1914 na kupewa jina la Graf Von Goetzen. Mjerumani
alipozidiwa katika vita ya pili aliizamisha katika lindi la ziwa Tanganyika wa
nia ya kumkomoa Mwingereza aliyechukua madaraka. Lakini wao walifanya kila
jitihada kuiibua majini na kuitengeneza. Ikaanza kazi kwa jina jipya la SS
Liemba. Tanganyika ilipopata uhuru wake Liemba ilikarabatiwa tena na mitambo
yake badala ya kutumia mvuke ikawa ikitumia dizeli, hivyo ikaitwa MV Liemba.
Meli hiyo hadi sasa ni tegemeo kuu la usafiri katika mwambao wa ziwa Tanganyika
hadi bandari za Mpulungu Zambia, Bunjumbura, Burundi na Kelemie Kongo.
Upande wa pili wa ziwa
hilo macho yangu yalivutwa na baadhi ya milima ya nchi hizo. Burundi kwa upande
wa kaskazini na Kongo ilionekana mbele yangu, magharibi ya nchi yetu. Hali ya
hewa ikiwa safi, anga likiwa angavu niliweza kuiona milima ya nchi hizo kwa
uwazi kabisa.
Sijui ningesimama hapo
kwa muda gani kama nisingeshikwa bega na nilipogeuka nikakutana na uso mpole wa
yule msichana aliyenivutia pale stesheni ya Dar es Salaam. Sura yake ilikuwa
iliyojaa haya. Hata hivyo, alijitahidi na kuniuliza kwa sauti yake ya upole,
“Samahani kaka. Hivi unaitwa Petro Kionambali?”
“Naam,” nilimjibu.
“Ulipata kuishi katika
maeneo ya Bonde la Ufa?” aliongeza swali jingine ambalo pia nililikubali.
Nikamwona akibadilika sura. Kwanza alitabasamu. Kisha tabasamu lake likamezwa na
uso uliojaa huzuni, machozi yakimlengalenga machoni.
“Vipi kwani?”
nilimwuliza kwa mshangao. “Petro… Hunikumbuki?”
Sikuweza kuelewa
anachozungumza. “Nakumbuka kukuona juzi pale stesheni, Dar es Salaam, kwa mara
ya pili nakuona leo hapa Kigoma,” nilimjibu
Pamoja na machozi yake
nilimwona akitabasamu kisha alisema, “Petro wewe ulipata kuokoa maisha yangu
kwa kuhatarisha yako. Ulinichukua hadi Singida ambako ulinipeleka misheni
ambako walinilea kiimani na kielimu. Sasa hivi nina kazi nzuri hapa Kigoma.”
Akili zangu zilikimbia
na kunirejesha nyuma zaidi ya miaka ishirini iliyopita. Nikamwona yule msichana
wa Kimasai aliyekuja katika kambi yangu huku akitetemeka. ‘...Nisaidie
...Naogopa’ Nilikumbuka
jina lake, “Nashifa sio?”
Nilimwona akichangamka.
“Unalikumbuka hata jina langu? Hata hivyo nilibatizwa na kupewa jina jipya la
Maria. Lakini sijaliacha jina langu la asili. Nimefurahi sana kukuona Petro.
Siku zote nilikufikiria usiku na mchana. Nilikuwa na hakika kuwa ingetokea siku
nikakutia machoni. Imetokea…” alisita kuzungumza na kuangua kilio.
eb 4, 2021
Thread starter
Add bookmark
#193
Sikujua kilichotokea
nilijikuta nimemkumbatia kwa namna ya kumfariji huku yeye pia akinikumbatia na
kukilaza kichwa chake juu ya kifua changu akiendelea kulia huku akinong’ona
maneno fulani ambayo sikuyasikia vizuri. Nilisikia machache tu, “Uliokoa maisha
yangu… kwa gharama ya kuharibu yako… sikupata kujisamehe kwa kitendo kile…”
Nilicheka kidogo kabla
ya kumnong’oneza vilevile, “Maisha yangu ni hadithi nyingine. Masaibu yako
hayahusiani hata kidogo na yale yaliyotokea. Yangu nayajua mimi na Mungu
wangu.”
Tulikuwa bado
tumekumbatiana. Kama si macho ya wapita njia kututazama kwa mshangao sijui
tungekaa katika hali hiyo kwa muda gani. Macho yao yalifanya nijikumbuke na
kujitazama. Nilitoa picha ya kuchekesha sana kwa mavazi yangu ambayo hayakuwa
zaidi ya midabwada, kumkumbatia msichana huyu mtanashati ambaye sasa alivaa
vitenge vilivyomkaa kana kwamba alizaliwa navyo. Nikajikwanyua toka mikononi
mwake na kumtaka radhi.
“Samahani ya nini? Huju
nilivyofarijika Petro.” Alisema. “Lakini tayari njia zetu zimetofautiana sana.
Mimi ni ndege wa jela asiyestahili kukukumbatia hadharani. Tazama
nilivyo,” nilisema
nikijitenga naye zaidi ili anione vizuri zaidi.
Kwa mshangao wangu
alicheka kabla ya kusema, “Najua yaliyokusibu. Nilikuwa nikifuatilia kwa karibu
maongezi yako na yule mama wa Kiingereza. Anaitwa nani vile, Jane siyo?”
Nilikubali kwa kichwa.
“Hivyo huna haja ya
kuniambia chochote zaidi. Najua umerudi kwenu. Najua umerudi mikono mitupu.
Usijali. Nitakusaidia kadri ya uwezo wangu. Uliniokoa kwenye mvua mimi pia
nitakuokoa kwenye jua.”
Alitia mkono wake kwenye
pochi lake la mkononi na kutoa kadi ambayo alinikabidhi. Ilikuwa na majina yake
na namba za simu. Kilichonivutia zaidi ni cheo chake. Afisa uhamiaji wa mkoa!
Niliduwaa.
“Matunda ya wema wako
hayo.” Alinifafanulia. “Wamisheni wale walinipa elimu bora hadi chuo kikuu.
Mara kadhaa nimepelekwa
nje kuongeza ujuzi. Huu ni mkoa wangu wa tatu toka nilipopanda cheo.”
Nilizidi kuduwaa. Safari
hii aliniondoa mshangao kwa kunishangaza zaidi. Alitia tena mkono wake mfukoni
na
kunipa kitita cha fedha.
Kwa hesabu za haraka haraka zilipata kuwa shilingi laki moja.
“Za nini?” nilimuuliza.
“Zitakusaidia kidogo.
Najua una matatizo mengi. Fika
nyumbani, wasalimu
wazazi halafu njoo mjini tushauriane.”
Nilitamani kulia. Kwa
nini siku zote maisha yangu yamekuwa ya kukutana na binadamu wenye roho mbaya
kama shetani na wale wenye roho nzuri mfano wa malaika? Nilijiuliza huku nikiwa
nimemkodolea macho. Unajua wewe ni malaika. Unajua utafika mbinguni? Nilitamani
kumwabia hivyo. Nilishindwa. Badala yake nilijikongoja kumwuliza,
“Umeshaolewa?”
Alinipa jibu jingine
ambalo liliniacha taabani zaidi, “Nilikuwa nikikusubiri wewe.” Nilipomtazama,
aliyaepuka macho yangu na kutazama chini. Mara nikaelewa kilichonivutia zaidi
juu yake. Haya! Pamoja na elimu yake, pamoja na cheo chake, bado alikuwa msichana
wa kiafrika halisi, mwenye uso wa soni tofauti kabisa na wasichana wengi wa
kileo.
“Sina budi kuondoka,”
aliseme. “Tafadhali tuwasiliane.
Sawa Petro Kionambali?”
“Bila shaka.” Nilimjibu
Akaifuata gari ambayo
muda wote ilisimama nje ya stesheni ikimsubiri. Akaingia upande wa pili wa
dereva na kupunga mkono wakati gari ikitiwa moto na kuondoka.
Mara alipotoweka machoni
mwangu, nilihisi upweke wa pekee ambao sikupata kuujua huko nyuma.
Nilizihesabu tena fedha
alizonipa. Nilikuwa na laki moja na hamsini. Sikuhitaji kufikiria sana.
Niliendea duka la karibu la nguo na kununua shati mbili, suruali mbili na shuka
la kujifunika.
Nilikuwa na mfuko wa
nguo mpya mkononi ndiyo kwanza nilijiona nilivyochakaa. Nilikuwa nanuka!.
Niliweza hata kuisikia harufu chafu ya mwili wangu mimi mwenyewe. Jasho la joto
la Dar es Salaam na vumbi la Dodoma, purukushani za Tabora na malazi mabaya ndani
ya behewa lililotoa mchanganyiko wa kutisha. Nikaamua kuiacha bandari na
kuufuata ufukwe nikielekea Mtanga hadi nilipopata sehemu faragha ambayo nilivua
nguo zangu na kujitupa ziwani. Sikuwa na sabuni wala mswaki. Nilitumia mchanga
na vidole kujisugua. Nikapiga mbizi mara mbili tatu. Kweli, aliyeogelea hafi
maji, kwani nilijikuta nikielea juu ya maji kana kwamba maisha yangu yote
nilikuwa ziwani humo.
Nilipotoka majini
nilijihisi mtu mpya. Hisia fulani ziliniambia kuwa kwa kuoga katika ziwa hili
lenye historia ya pekee nilikuwa nikisafisha mikosi na mikasa yote
iliyoniandama na kuanza maisha mapya.
Pengine haikuwa uongo.
Ziwa Tanganyika lilikuwa mwujiza mwingine wa dunia. Kwanza lilikuwa refu kuliko
maziwa yote duniani. Pia, kina chake kwenda chini kilivunja rekodi ya maziwa
yote ya ulimwengu.
Likiwa limeenda chini
kwa takribani meta 2400 toka kilele cha milima ya Mahele iliyopo kilometa 150
toka Kigoma mjini au meta 1500 toka ardhi ya kawaida ya mkoani humo mwisho wa
kina hicho uliwiana na usawa wa bahari kwa miji ya Dar es Salaam na Zanzibar.
Inaaminika kuwa kuwepo kwa ziwa hilo ni matokeo ya mabadiliko makubwa
yaliyopata kuitokea dunia, kama matetemeko ya ardhi au volkano ambayo pia
yanaaminika kuibua vitu kama Bonde la Ufa. Walikotokea samaki ainaaina na
viumbe wengine hai waliomo tele ziwani humo ni fumbo jingine ambalo mwanadamu
hajapata kulipatia ufumbuzi.
Sikuhitaji gari kutoka
kigoma hadi Mwanga. Mwendo wa dakika ishirini kwa mguu uliniwezesha kufika
katikati ya mji huo. Mwanga ilichangamka. Vijana waliokuwa wakifanya kazi za
kushevu walikuwa tele katika ofisi zao zinazovutia kwa vioo na viyoyozi. Niliingia
katika kimojawapo cha vibanda hivyo na kukinga kichwa changu.
“Nywele na ndevu,”
nilisema.
“Utahitaji tukuwekee na
super black, kaka?” niliulizwa na kijana huyo
“Kwa nini?”
“Mvi zinakuanza. Unaona
hapa?” alielekeza.
Nikajitazama katika
kioo. Kweli, kulikuwa na mvi mbili tatu katikati ya kichwa changu. Nazeeka!
niliwaza kwa mshtuko kidogo. Kuzeeka kabla ya kufanya jambo lolote ambalo
familia, jamii na nchi yangu itaweza kujivunia haikuwa dhamira yangu hata
kidogo.
“Hapana, shevu tu,”
nilimwambia. Sikuona haja ya
kuficha shahada ya umri
wangu.
“Ndevu unashevu kwa
mashine au magic?” “Ndiyo nini hiyo mejiki?”
Akanionyesha dawa
fulani. “Hii inafanya kidevu kiwe kama cha mtoto mdogo,” Alifafanua.
“Na bei yake?” “Iko juu
kidogo.”
“Kama ni hivyo tumia
mashine.”
Muda mfupi baadaye
nilikuwa mtu mwingine kabisa, mtu anayependeza kwa usafi hasa kwa kijana huyo
kunipaka mafuta ambayo yalilainisha ngozi yangu. Nilijitazama kwenye vioo
vyake, mbele na nyuma, kwa muda kabla ya kumlipa na kuondoka.
Niliuliza magari ya
kwenda Kasulu. Niliambiwa kuwa nimekwishachelewa, kwamba lilikuwepo basi moja
tu la Mwarabu ambalo huondoka saa kumi na mbili za asubuhi kila siku.
Pia, nilidokezwa kuwepo
kwa malori ya mizigo ambayo huondoka asubuhi hadi saa tatu. Nilipoitazama saa
yangu iliitimu saa nne na nusu za asubuhi. Nikaamua kutafuta hoteli ya bei
nafuu ili nijipumzishe hadi hiyo kesho.
Kabla ya kuchukua chumba
niliamua kuuvinjari kidogo mji wa Mwanga. Kama miji mingine nchini Mwanga
ilipanuka sana. Maeneo kama Vumilia na Majengo ambayo zamani yaliogopwa na
kudharaulika sasa viwanja vyake vilioneka lulu. Majengo yalikuwa yakiota kama
uyoga. Kwa bahati mbaya sana, kama yalivyokuwa maeneo mengi mapya, maeneo haya
pia yalikosa huduma muhimu. Hayakuwa na mifereji ya maji machafu, hayakuwa na
mfumo wa maji safi, umeme wa barabarani ilikuwa ndoto na hata barabara zilijaa
na kujitunza zenyewe. Hali iliyopelekea mafuriko na uchafu kuivuruga dhamira
nzima ya wamiliki.
Nilienda Mwanga
Katubuka. Nikaingia Sokono. Macho yangu yalikuwa yakiwatafuta samaki
niliowazoea na wale ambao nimekuwa nikisikia sifa zao toka utotoni; nonzi, wale
samaki wakubwa wanaofanana na ndege, kuhe, samaki mtamu ambaye ana hadhi;
singa, samaki mnono aliyejaa mafuta mwili mzima, nika, samaki mwenye nguzu za
umeme ambaye kumshika lazima utumie mdomo wake wa chini vinginevyo utarushwa na
kumwachia; kuvungwe, anayeitwa nguruwe wa majini kwa umbile na masharubu yake.
Ningependa pia kuwaona
kungura, ndubu, kambale na wengineo. Sikuwa na bahati hiyo. Samaki niliowaona
sokoni humo siku hiyo ni migebuka ambayo ilikuwa imekufa kwa
wingi. Ndubu? Siku hizi
hapatikani sana. Kibonde? Alikuwepo mmoja tu leo, amegombewa kama mpira wa
kona. Nikakata tamaa. Nikaenda soko la dagaa ambamo kulikuwa na dagaa wabichi
wenyewe wakiwaita “mteke” na samaki wadogo wadogo walioitwa “Masembe.”
Nilipochoshwa na ziara
hiyo nilitafuta hoteli na kuagiza chakula. Ningekula nini zaidi ya ugali wa
muhogo kwa migebuka iliyokaangwa kwa mafuta ya mawese? Ulikuwa mlo mtamu
uliofanya nijisikie shibe isiyo na kifani.
Baadaye nilipanda basi
kwenda Ujiji. Sikujisikia kuondoka Kigoma bila kuuona mji huo wa kihistoria.
Mji ambao ulikuwa na uzito mmoja na ile ya Bagamoyo, Zanzibar na Kilwa. Lakini
mara niliposhuka kilima cha kutoka Mnarani na Mawemi matumaini yangu ya kuiona
Ujiji inayosisimua ilizimika. Macho yangu yalipokelewa na mji wa kale, kama
ulivyokuwa enzi za kina Tip Tippu na Livingstone.
Mji uliomezwa na nyumba
nyingi ambazo ziliezekwa kwa nyasi au bati kuukuu. Baadhi ya nyumba zilikuwa
kuukuu zikiashiria jambo lilelile ambalo nimekuwa nikiliona huku na huko toka
nilipotoka kifungoni; Umasikini.
Hali ya mitaa mingi pia
ilitia huzuni. Kwa mtu aliyetoka katika miji inayokua, hata Mwanga tu, Ujiji
ingeweza kumtoa machozi. Mitaa mingi ilimezwa na majani. Baadhi ya mitaa
majirani walianza kulima mahindi na maharage. Kuna nini? Nilijiuliza. Yako wapi
magari yachangamshe mitaa? Wako wapi watu waitie uhai? Nini kimetokea hapa?
Nikafikia uamuzi. Bila
shaka biashara ya utumwa ilikuwa na laana. Vinginevyo mji huu ambao Dakta
Livingstone alitia kambi miaka ya 1871 wakati akifanya utafiti katika nchi za
Kongo na Malawi. Mji ambao Novemba 10, mwaka huohuo
Henry Stanley, baada ya
kutumwa kumtafuta alikutana naye ufukweni na kusEma “Dr livingstone…! I
presume…” mwaka mmoja kabla ya kifo chake. Ukiwa njia na kituo kuu cha
wafanyabiashara wa Arabuni, Ulaya na Amerika katika kujipatia bidhaa za meno ya
tembo na ile biashara haramu ya watumwa. Mji ambao huwezi kuandika historia ya
Afrika bila ya kuutaja! Hadi leo uko hivi! Kama si laana ni nini?
Nilishuka kwenye basi,
nikaifuata barabara ya Livingstone ambayo ilinifikisha Pwani ya Ujiji, pale
Livingstone alipokutana na Stanley kwa mara ya kwanza. Palijengwa nguzo ya
kumbukumbu yenye maelezo ya hafla yao ile. Nikatupa macho yangu ziwani na
kuziona boti za jahazi ya wavuvi waliokuwa katika pilikapilika za safari, ama
kuondoka ama ndio kwanza wanafika toka maeneo hayo mbalimbali ya ndani na nje
ya nchi.
Nikarejea Mwanga na
kuanza kutafuta hoteli ya kulala. Ujiji haikuwa na nyumba ya aina hiyo. “Nenda
Mwanga… nenda Kigoma mjini. Hapa utalala nje bure,” niliambiwa na msamaria
mwema, mtu mzima aliyevaa kanzu na baragashia. Mkewe alivalia baibui
lililomfunika gubigubi isipokuwa sehemu ndogo ya macho na miguu. Wazee hao
walinikumbusha Bagamoyo na Pangani.
Wakati azana ya
kuwakumbusha waumini kuwasili zinaanza kutoka misikiti mbalimbali mimi nilikuwa
nikipanda basi kurudi Mwanga.
Hirizi Iliyopotea Na
Maajabu Yake
SURA YA ISHIRINI NA SITA
engine kwa ajili ya
safari ndefu ya wima toka Dar es Salaam, pengine kwa ajili ya chumba murua
chenye hewa safi nilicholala nilijikuta
nimechelewa kuamka.
Hivyo, basi la Mwarabu liliniacha. Nilioga harakaharaka, nikanywa chai kwa
dagaa wa mteke, kisha huyoo, nikawahi malori ya mizigo. Nilipata moja
lililokuwa likipakia mabati na vifaa vingine vya ujenzi. Kwa namna ya muujiza
nilipata kiti cha mbele, tukiwa abiria wawili tu na dereva. Muda mfupi baadaye
gari liliondoka.
Nikiwa nimekaa dirishani
nilipata fursa nzuri ya kutazama nje, macho yangu yalivutwa na ardhi nyekundu,
mimea ya asili, mashamba ya wenyeji na zaidi ya yote watu. Toka Mwanga hadi
Gungu na baadaye Mwandiga yalikuwa maeneo ya watu, nyumba ambazo
hazikutofautiana sana na zile za Mwanga na Ujiji. Hii hapa ikiwa imejengwa kwa
saruji bati na samani nyingine zikiwa zimeipamba; ile ikiwa nyumba ya tope,
ilijengwa kwa matete na mianzi na kuezekwa kwa nyasi.
Toka Mwandinga mambo
yalibadilika zaidi. Nyumba duni zilianza kutamalaki huku zile za afadhali
zikizidi kupungua. Watu pia walibadilika. Wengi walivalia mavazi
duni, baadhi yakiwa
yamechanikachanika. Ilikua rahisi sana kumshuku mtu kuwa ni mwendawazimu
kutokana na hali hiyo. Lakini pale unapoona idadi kubwa zaidi iko katika hali
hiyo, hasa watoto ambao wengi wao walitembea nusu watupu, miguu iliyojaa vumbi
jekundu ikiwa pekupeku, unajikuta ukiondokana na wazo lako na kupata jibu mara
moja, rahisi; umasikini.
Nyuso za watu wengi
zilionyesha dalili ya kukata tamaa. Walicheka ndio, lakini kicheko hicho
kilionekana mdomoni tu, moyoni ungeweza kusoma kitu kingine kabisa.
Walizungumza pale ulipozungumza nao, lakini sauti zao ziliashiria kuifadhi
jambo fulani ambalo hawakuwa na uwezo wa kulifafanua. Sura hizi za msiba,
majengo mengi ya maombolezo na ardhi nzuri ambayo haikuwa ikichekelea kwa pamba
na kahawa kama nilivyoizowea utotoni ni jambo ambalo lilinitia hofu badala ya
shahuku ya kufika nyumbani. Nilihisi huzuni ikinigubika katika fikra zangu
katika safari hiyo nzima.
Ndiyo, nchi yetu ni
masikini. Lakini umasikini huu unazidiana kati ya mkoa na mkoa. Pengine iko
mikoa iliyo taabanizaidi ya Kigoma, hilo halikunisumbua. Kilichonisumbua ni kwa
nini Kigoma iwe katika kundi hilo? Kigoma haikuwa na sababu yoyote ya kuwa kama
ilivyo. Ni mkoa uliojaaliwa kila ambacho binadamu anahitaji. Ardhi ilikuwa na rutuba
tele, mali asili zikiwa zimefurika katika misitu na ardhini. Mito, mabwawa na
baba lao; ziwa Tanganyika vikiwa vimejaa samaki tele ambao ladha yake ina uwezo
wa kumshangaza mtu yeyote duniani zaidi ya hiyo Kigoma ni lango muhimu kwa nchi
za Kongo, Burundi na hata Zambia. Ukweli huo pekee wa kijiografia ni rasilimali
tosha. Historia ya Kigoma, hasa Ujiji pia ni rasimali nyingine muhimu ambayo
kuitumia vyema
kungeweza kuubadili mkoa
kiuchumi.
Kitu gani kimetokea hata
mkoa uwe ukirudi nyuma badala ya kwenda mbele? Kitu gani kimesahauliwa? Nani
alaumiwe? Nilijiuliza hili na lile. Yako mengi ambayo hayakuhitaji utafiti wa
kina kuyaona. Moja la haraka likiwa usafiri. Ilikuwa rahisi zaidi kutoka Kigoma
kwenda Burundi au Kongo kuliko kwenda Tabora au Mwanza, achilia mbali Dar es
Salaam. Wakati huu wa Kilimanajaro au Arusha anaweza kutoka Dar es Salaam hadi
kwao na akarudi jioni au kesho yake ilimchukua mtu wa Kigoma wiki mbili au
zaidi kufanya safari hiyo, hali ambayo muuza nyanya au samaki ataishia kuiona
bidhaa yake ikioza mbele ya macho yake.
Barabara ilikuwa tatizo
la kwanza lisilohitaji mjadala barabara pia lilikuwa tatizo la pili. Kigoma
ulikuwa mmoja kati ya mikoa iliyo kimya sana. Pamoja na kukisiwa kuwa na eneo
la kilometa za mraba 37,037 mkoa wa Kigoma ulikuwa hauna kiwanda hata kimoja.
Hata wale samaki, aina ya migebuka ambao katika misimu fulani huliwa kwa
mamilioni huishia kuharibika bure na kutupwa badala ya kusindikwa; achilia mbali
dagaa wanono wenye sifa zote.
Hata mafuta ya mawese,
yatokanayo na michikichi ambalo ni zao linalostawi sana mkoani humu hayajapata
kujengewa kiwanda cha kuyasindika ili yauzwe kimataifa. Nani atafikiria kufanya
mradi kama huo mahala ambapo hakuna hata barabara?
Barabara pekee ambayo
haikuaminika sana ya kutoka Kigoma kwenda nje ya mkoa na hiyo tuliyokuwa
tukiitumia. Sehemu ndogo sana zilikuwa na lami. Sehemu kubwa ikiwa changarawe
na tope ambalo lilifanya safari iwe shughuli kubwa badala ya starehe. Lakini
hilo halikuwa tatizo kubwa.
Tatizo hasa lilikuwa
mzunguko wa njia hiyo ulioifanya kuwa ndefu kupita kiasi. Ili kwenda Dar es
Salaam au Tabora miji iliyoko mashariki ya mkoa ulilazimika kwenda kaskazini,
upite Kasulu, Kibondo hadi Biharamulo kabla hujageuka kuelekea kusini ili ufike
Kahama na Nzega kabla ya kuingia Tabora. Toka Tabora unapanda kaskazini tena na
kuridi Nzega kabla ya kwenda Igunga, Iramba, Singida hadi Manyoni. Toka hapo
utafika Dodoma na kutelezea Gairo, Morogoro, Chalinze na baadaye Dar es Salaam!
Pema hapo?
Ndiyo, Kigoma kuna
uwanja mdogo wa ndege. Ndege ndogondogo vilevile huja na kuondoka mara mbili au
tatu kwa wiki. Licha ya ukweli kuwa hazitoshi, bado nauli kubwa ya ndege
imefanya ziwe na wenyewe badala ya kila mtu. Si kila mtu mwenye laki mbili au
tatu kwa safari ya saa nne kwenda na kurudi.
“Vipi unashukia wapi?”
dereva alinizindua. “Naona uko mbali sana kimawazo,” aliongeza.
Nikapekecha macho yangu
kwa kidole change cha shahada kabla ya kumuuliza, “Kwani hapa ni wapi?”
“Tumeshapita Simbo. Hapa
ni Kitawe. Baada ya hapa tunaingia Mayange. Toka hapo ni moja kwa moja hadi
Kasulu, mwisho wa safari yetu.”
Sikujua nimjibu nini.
Kwa kweli, sikujua hata mahala pa kushuka. Niliondoka nikiwa mdogo sana.
Kumbukumbu nilizokuwa nazo zilionyesha kuwa hatukuwa mbali sana na mji wa
Kasulu. Lakini udogo, mabadiliko makubwa ya mazingira na hasa kutoweka kwa
misitu mingi ambayo ningeweza kuikumbuka kulifanya nisijue wapi pa kuanzia
upelelezi wangu wa kutafuta chochote nitakachoweza kupata juu ya wazazi wangu.
Nadhani dereva alizisoma
hisia zangu. Kwani alirahisisha kazi yangu pale alipouliza, “Yaelekea wewe ni
mgeni sana huku?”
“Nadhani, maana
niliondoka nikiwa mdogo sana. Hata sifahamu nianzie wapi kuwatafuta wazee
wangu,” niliropoka bila kutegemea.
Kwa wakazi wa mkoa ambao
hauna ajira za kutosha, ambao mkoloni aliutumia kama shamba la kuchukulia
manamba wakakate mkonge huko Tanga na Kilimanjaro maelezo yangu hayakumshangaza
dereva huyo hata kidogo. Alihitaji maelezo mafupi tu; niliondoka lini. Tulikuwa
tukiishi wapi, ukoo wangu ni upi na mengineyo. Nilipomweleza juu ya hofu yangu
juu ya vijiji vya Ujamaa alinielewa mara moja. Akanishauri nishuke katika
kijiji kinachofuata, kinachoitwa Mayange, ambacho ni kikubwa na kilikusanya
familia mbalimbali toka maeneo mengi.
“Walisema kingekuwa
kijiji cha mfano kwa maendeleo,” alisema akicheka kwa kebehi. “Hebu katazame
hayo maendeleo halafu utatuambia.”
na ushauri wake.
Tulipofika Mayenge nililipa nauli yangu, nikateremka na kuanza kazi ya kutafuta
‘kwetu’.
Kama nilivyotegemea
kijiji cha Mayange kilikuwa kinyume kabisa na matarajio ya awali kama
ilivyokuwa kwa vijiji vingine vyote tulivyovipita njiani, Mayange ilitoa
taswira ileile, umasikini unaonuka. Karibu watoto wote walichakaa miili na
mavazi, wakifanya kazi ndogondogo kama kubeba mizigo ya wasafiri kwa mikokoteni
yao ya miti au kuomba tu kwa wapita njia. Baadhi walivaa sare za shule. Lakini
sare nyingi kati ya hizo hazikufanana kabisa na malengo ya wizara
kwa kuchoka na kuchakaa.
Watu wazima nao walikuwa
na yao. Wengi wao walikuwa taabani, suruali zikiwa zimejaa viraka, shati zikiwa
zimepasukapasuka, miguu iliyokuwa peku ikiwa imebadilika rangi kutokana na
vumbi jekundu lililowapiga pindi wakihangaikia mkono kwenda kinywani.
Waliahidiwa huduma
muhimu kama barabara; hazikupata kujengwa au kukarabatiwa. Waliahidiwa maji ya
bomba; hawakupata kuyaona. Waliahidiwa umeme; ilikuwa ndoto za mchana.
Waliahidiwa huduma ya matibabu; sasa ilibidi kuyalipia kwa fedha ambazo huna.
Kwa ujumla, ahadi zote zilizotumiwa ili kuwaondoa katika makazi ya baba na babu
zao ziligeuka hewa. Jambo hilo lilifanya nyuso za kila mtu unayekutana naye
zitangaze dalili zote za kukata tamaa.
Kazi ya kuitafuta
familia moja, kati ya familia zaidi ya mia saba zilizohamishiwa hapo toka
maeneo tofauti haikuwa ndogo. Nilitumia zaidi ya saa mbili kabla ya kumpata
mzee mmoja ambaye alimfahamu babu, “Familia ya Kionambali, sio? Wala
usihangaike. Wako humuhumu. Mtoto wake Karimanzira huwa namwona mara kwa mara.”
Nikapata matumaini. “Ni
babu? Kionambali mwenyewe?” niliuliza.
“Huyo sina habari zake.
Sijui kama bado yuko hai au tayari ametangulia,” mzee alinijibu. Laiti angejua
kauli yake ilivyonishtua.
Nikiwa na matumaini
mapya nilianza awamu ya pili ya kuwatafuta wazazi wangu. Zikiwa safari za mguu,
katika kijiji kikubwa kisicho walao na jina la mtaa ilinichukua saa moja na
nusu kabla ya kuonyeshwa kwa mbali nyumba iliyoaminika kuwa ya baba.
Ilikuwa nyumba
iliyofanana na nyingine nyingi kijijini hapo; tofali za tope ambazo zilichakaa
kabla ya kupata lipu, achilia mbali rangi. Juu nusu iliezekwa bati kuu kuu nusu
nyasi. Sakafu ilikuwa ardhi ileile waliyoikuta palepale.
Nje ya nyumba hiyo alikuwepo
bibi mmoja mchovu kama wengine wote kijijini hapo, akisuka ukili. Nilisogelea
na kumwamkia. Kisha niliuliza kama hapo palikuwa nyumbani pa mzee Karimanzira.
Swali langu lilimfanya bi mkubwa huyo ainuke na kunitazama kwa makini. Mara
nikamwona akianza kutetemeka. Machozi yakianza kumtoka.
“Wewe ni Mtukwao!...
Mwanangu! Umerudi…” alisema akinijia na kunikumbatia kwa nguzu zake zote.
Alikuwa mama! Mama yangu
kipenzi! Fuko nililokuwa nalo mkononi lilidondoka pwaa, mikono yangu pia
ikamkumbatia kwa nguvu. Masikioni nilisikia sauti nzito ya kiume ikilia! Kilio
cha kwikwi. Ilinichukua muda kubaini kuwa ilikuwa ni mimi niliyekuwa nikilia.
Mara mzee mmoja akatoka
nje ya nyumba hiyo. Alikuwa mchovu vilevile. Umbile lake refu lilipinda kwa mbele,
ndevu zenye mchanganyiko na mvi zilimeza kidevu na kichwa chake kizima.
Akitetemeka miguu na mikono yeye pia alinijia na kunikumbatia, machozi
yakimlengalenga.
Baba! Amezeeka kabla
hajapata kuwa kijana!
Dakika mbili tatu
baadaye nyumbani palifurika. Watu waliotoka huko na huko walijazana kushangilia
ujio wangu. Kila mtu alisema lake, ingawa mada ilikuwa ileile; Mwana mpotevu
karejea!
Niliingizwa ndani,
nikapewa kiti cha kifalme; kigoda cha baba. Fumba fumbua togwa tamu ikaletwa.
Nikapewa kata kubwa iliyojaa. Kabla haijaisha nililetewa mihogo mitamu,
huko nje nikiwaona
vijana wakikimbizana na jogoo.
Baba na mama
hawakubanduka ubavuni mwangu. Walikuwa na mengi ya kuniuliza mengi ya
kunisimulia. Kwa bahati mbaya, hali haikuruhusu. Watu walikuwa tele,
wakinishangaa kana kwamba nimetoka mwezini. Kelele pia zilishamiri. Watoto
ambao hata sikuwafahamu walijipenyeza na kukaa miguuni mwangu, wakijitahidi
sana kunikumbatia, walao miguu.
Kwa kweli sikutarajia
mapokezi makubwa kama haya. Nikiwa mtu aliyepotea kwa zaidi ya miaka
thelathini, mtu aliyerudi akiwa mikono mitupu kama nilivyokuwa, nilitarajia
kupokelewa kwa kejeli au dharau. Si vicheko na kushangiliwa kwa takribani
kijiji kizima kama ilivyokuwa. Hata hivyo, nilijihisi kama mtu aliyeutua mzigo
mzito uliomlemea. Nilijihisi kama ambaye nilifutiwa madhambi yangu yote hata
kabla ya kuomba radhi.
Kitu kimoja tu kilikuwa
kikinisumbua. Mtu niliyetamani kumwona pengine kabla ya wengine wote hakuwa
katika kundi la watu waliojitokeza kunilaki. Mtu huyohuyo nilihitaji sana
kumwomba radhi kwa kumwamgusha katika matarajio aliyokuwa nayo juu yangu na
kumpotezea hirizi yake muhimu. Nilimtegemea awe katika mjumuiko huo, aniite
kando ambako tungeketi peke yetu na kuteta kama mtu na baba yake. Sikumwona.
Wala sikuthubutu kuuliza harakaharaka kwa kuchelea kupewa jibu ambalo lingeweza
kunitia ugonjwa wa moyo; Babu yake! Mbona alikufa zamani?
Kuku alikwishachinjwa na
kupikwa. Ugali mweusi wa nyangwe uliletwa mbele yangu kwa kitoweo cha kuku
huyo. Bila kuambiwa wageni walianza kupungua ili kuniachia faragha ya kufaidi
chakula changu. Nilishindwa kujizuia. Kabla
ya kumega tonge la
kwanza nilimuuliza baba, “Babu yuko wapi?” nilisubiri jibu lake kwa hofu kubwa,
moyo ukinidunda. Lakini nilipomwona baba akitabasamu kabla hajanijibu hofu
ilitoweka moyoni mwangu.
“Babu yako kwani
humjui?” baba alisema. “Aligoma katakata kuhama. Jeshi la polisi, jeshi la
mgambo na hata sungusungu walishindwa kabisa kumtoa. Hivi sasa yuko peke yake
ndani ya msitu mkubwa wa yaliyokuwa makazi yake. Kila wiki huwa nakwenda
kumjulia hali.”
Nikapumua. “Bibi?”
niliuliza.
“Yeye hatuko naye tena.
Alitutoka miaka mitatu iliyopita. Alipatwa na ugonjwa wa malale uliokataa kila
aina ya dawa.”
Ladha ya kuku ikaniishia
palepale.
***
“Nilijua utarudi salama…
nilikuwa nikikusubiri… nisingeweza kufa kabla hujarudi, mjukuu wangu,” ilikuwa
kauli ya kwanza ya babu mara aliponitia machoni na kunipapasa kichwani.
Sikuweza kuyastahimili
machozi yaliyomiminika toka machoni mwangu. Babu alinikumbatia, huku mkono wake
ukiendelea kunipapasa kichwani kwa namna ya kunibembeleza. Kitendo hicho
kilizidisha uchungu moyoni mwangu na kunifanya nizidi kulia. Kwa mara ya kwanza,
hakunishutumu kwa kitendo hicho. Niliinua uso na kumtazama kwa wizi. Yeye pia
alilowa macho kwa machozi.
Babu analia, chuma cha
pua!
Kwangu, alikuwa zaidi ya
babu. Alikuwa kila kitu; baba, babu, rafiki, mwalimu na zaidi ya hayo. Hayo
nilibaini na kuyahakikisha muda huo ambao mzee hataweza kustahimili
kabisa kuficha udhaifu
wake kwangu! Nitamsimuliaje malaika huyu kuwa jitihada zake zote za kupita
mabonde, milima na misitu yenye hatari zote za dunia, hadi kunifikisha nchi ya
Wahaya ili nipate elimu zilikuwa kazi bure? Nitaanzaje kumwambia kuwa ile
hirizi yake, urithi pekee alioniachia ilipotea kwa uzembe? Niliteseka vibaya
sana akilini nilipowaza hayo.
Nilikuwa nimemlazimisha
baba alfajiri tu ya siku iliyofuata aniongoze kuja kumwona babu. Yeye
akisisitiza kuwa ningepumzika walao siku mbili kabla ya kufanya safari hiyo.
Jambo ambalo sikuafikiana nalo.
Kwa kutokuwa na uhakika
wa kuwapata wazazi wangu, wakiwa hai nilifika nyumbani mikono mitupu. Hivyo,
nilipopata fursa ya faragha ya kumkabidhi baba shilingi 50,000 kati ya zile
laki moja nilizobakiwa nazo nilionekana shujaa mkubwa. Baba alianza mipango ya
‘kumaliza bati’ mama aliongea juu ya kulimisha shamba. Ilikuwa kama nimetoa
milioni hamsini. Tulimkuta babu akifunga mbuzi wake nje ya nyumba.
Alivaa nguo zake zile
alizozipenda, kaptula na shati nyeupe. Ziling’ara kama nilivyoziacha! Miguuni
alitilia buti zake ambazo nazo ziling’ara kwa kiwi, ingawa zilianza kuchoka.
Alikuwa peke yake katikati ya pori, isipokuwa kwa mifugo mingi ya mbuzi, kuku
na bata. Watu wa pwani wangeweza kuapa kuwa ni jini jeupe linalokaa peke yake
msituni. Babu alikuwa ametusikia toka mbali. Hivyo, alimfunga mbuzi yule
harakaharaka na kusimama akitukodolea macho. Alipotuona alitukimbilia na
kunidaka juujuu. Angeweza kunibeba… angeweza kunitia mweleka…. Babu alikuwa na
nguvu zake. Ilikuwa kama ni binadamu pekee aliyebishana na uzee. Binadamu
ambaye hakukubali kusalimu amri kwa kifo.
Pamoja na baba tulikuwa
na vijana wengine wawili ambao nilielekezwa kuwa ni ndugu zangu. Vijana hao
walipewa amri ya kumkamata beberu mkubwa kuliko wote na kumchinja. Akachunwa.
Moto ukawashwa. Muda mfupi baadaye, tulikuwa tukimla mbuzi yule, wa kuchoma. Babu,
akiwa na meno yake yote alitafuna mguu mzima wakati wengine tukishika shika
hapa na pale.
Baadaye babu aliwataka
baba na wale wenzetu wengine kuondoka kwa maelezo kuwa alikuwa na mengi ya
kuzungumza na mjuu wake faragha. Usiri wangu na babu halikuwa jambo geni kwa
baba, toka utoto wangu. Hivyo, hakutia ubishi, walichukua nyama ya kula
nyumbani wakaondoka zao kwa ahadi ya kunifuata kesho.
Nikapata wasaa wa
kuchomoa zile elfu hamsini nilizobakiza na kumkabidhi babu. “Zawadi pekee
niliyoweza kukuletea ni hii,” nilisema kwa masikitiko.
Babu hakuzipokea. Badala
yake alicheka kabla ya kusema, “Sidhani kama nazihitaji. Za nini? Kaa nazo,
zitakufaa wewe zaidi. Naamini bado unasafari nyingine ndefu, yenye mafanikio
makubwa zaidi. Halafu, bado tuna mengi ya kuzungumza, mimi na wewe.”
“Bila shaka. Niliitikia.
“Miaka mingapi vile toka
tumetengana?” Babu aliniuliza. “Mingi sana. Ni aibu kuitaja.” Nilimjibu.
“Aibu ya nini? Mwanaume
anayeonea aibu masaibu yake hafai. Kwa nini ufanye jambo ambalo utalijutia
maishani mwako?”
Nilijua darasa la babu
limeanza. Sikuwa tayari kwa darasa lolote wala somo lolote kabla ya kumtaka
radhi. Hivyo nikajikongoja na kumwambia, “Babu ningeomba nianze kwa kukutaka
radhi.”
“Radhi ya nini?”
“Hirizi.” “Ilifanyaje?” “Ilipotea!”
Nilitarajia babu
abadilike, akasirike. Lakini kwa mshangao nilimwona akiachia tabasamu jembamba.
“Nisubiri kidogo,” alisema akiinuka na kuingia ndani, aliporejea alikuwa na
hirizi mkononi.
“Hirizi hii siyo?”
Niliitazama kwa makini.
Nisingeweza kuisahau. Ilikuwa
ileile!
Sikuyaamini macho yangu.
Nikamkodolea babu macho
ya mshangao.
“Hii ndiyo
inayokusumbua?” babu aliongeza baada ya kicheko kingine. “Usiwe na wasiwasi.
Ilipotea ikatafuta njia, ikarudi nyumbani kukusubiri.”
Bado sikuweza kuelewa.
Hirizi hiyo ilipotea porini katika purukushani za kuikimbiza isianguke mikononi
mwa padri. Yule kimbelembele, Byabato, alinihakikishia kuwa aliiokota tena na
kumrudishia padri Backhove ambaye aliichoma, ikakataa kuungua. Kwamba baadaye
ilitupwa baharini. “Ilifikaje kwako?” nikamuuliza.
“Ni hadithi ndefu. Ili
kuifanya fupi pengine nikuambie tu kuwa ililetwa.”
“Na nani?” nilizidi
kumbana babu. “Na mizimu ya babu zetu.”
Bado nilikuwa
sijamwelewa. Nikamwambia hivyo. “Mizimu ina njia nyingi ya kuwalinda wahanga
wake,”
alifafanua. “Chochote
kilichokutokea hadi hirizi hii kutengana nawe wahanga walikuwa wakiona. Ama kwa
kujigeuza ndege,
ama kwa kuwatuma ndege,
hirizi hii ililetwa hadi katika mikono yangu.”
Babu alipoona kuwa bado
sijaridhika na ufafanuzi huo aliamua kuwa wazi zaidi. Alisema kuwa jioni moja
alikuwa akiwinda katika mwambao wa mto Malagalasi. Mara akaona kundi kubwa la
ndege aina ya hondohondo wakitua hatua chache toka alipokuwa. “Walikuwa wengi.
Kama elfu moja hivi. Waliponiona waliruka kunikimbia. Lakini mwenzao mmoja
hakuweza kuruka. Alikuwa akipigapiga mabawa kwa nia ya kupaa lakini hakuweza.
Nikamsogelea kuona kapatwa na nini. Nikabaini kuwa shingo yake ilikabwa na
kamba nyeusi ambayo ilinasa kwenye kichaka cha mti. Nilipomshika ili kumkwamua
ile kamba nilishangaa kuona kuwa ilikuwa hirizi ile niliyokupa. Nikaitoa na
kumwacha ndege ambaye alipaa kuwaendea wenzake waliokuwa wakihangaika angani
kumsubiri.”
Ilikuwa habari ya ajabu
kwangu. Hirizi yangu, iliyopotea zaidi ya miaka thelathini iliyopita imerejea
mikononi mwangu. Niliipokea, nikaipapasa. Ilikuwa ileile, kwa rangi na uzito.
Kwamba imerudi mikononi mwangu halikuwa jambo la ajabu sana, ni namna
iliyoifanya irudi ambayo kichwa changu hakikuweza kupokea.
Falsafa nyingi zilipita
kichwani mwangu. Kama kweli ilitupwa ziwani bila shaka ingeweza kuoza. Kama
hilo halikutokea ni wazi kuwa ilimezwa na samaki ambaye huenda alivuliwa na
kuliwa. Kama ilikuwa hivyo hirizi itakuwa ilitupwa kama sehemu ya uchafu wa
matumbo ya samaki wanayotayarishwa kwa ajili ya minofu kusafirishwa Ulaya na
“mapanki” kuvamiwa na akina baba na mama ntilie. Inawezekana kuwa katika
jitihada za kujitafutia chochote ndege yule alijikuta ameivaa hirizi ile na
kuisafirisha bila
kujua? Kama ni kweli kwa
nini ailete hadi miguuni mwa babu? Katika pitiapitia yangu vitabuni nilikuwa
nimesoma mahala tabia za ndege. Moja ya tabia zao za ajabu ni ile ya kuhama au
kusafiri safari za mbali kila ifikapo msimu fulani. Mara nyingi ndege hao wanaweza
kusafiri safari za mbali toka Marekani au Ulaya hadi Afrika. Inaaminika kuwa
wengi uhama katika vipindi vya hali fulani ya hewa na kurudi hali
inapotengemaa. Inaaminika pia huko ambako huenda ndiko ambako ndege huzaliana
na kurejea likiwa kundi kubwa zaidi. Inawezekana kabisa kuwa hondohondo
aliyebeba hirizi yangu alikuwa katika msafara huo. Anaweza kuwa alikuwa akitoka
zake Ulaya au nchi za
Kiarabu na kuelekea Afrika Kusini!
Babau alikuwa kama
anayeyasoma mawazo yangu. Alikohoa kidogo kabla ya kusema, “Naona na wewe
tayari umeambukizwa yale maradhi yenu.”
“Maradhi gani?
“Maradhi ya kisomi.
Naona unavyoona shida kuamini kuwa mizimu ya babu wa babu zako imekurejeshea
hirizi hii! shauri lako. La msingi ni kwamba hirizi yako imerejea na tangu leo
utaivaa tena. safari hii milango yote uliyoshindwa kuifunguwa itafunguka,” alisema
akinivisha hirizi hiyo na kisha kunitemea mate kichwani na kifuani.
“Kuna jambo la pili.”
Alisema akiinuka tena na kurudi ndani. Aliporejea alikuwa na bahasha tatu
mkononi. Alinikadhi. Ilikuwa barua. Juu ziliandikwa jina lake na anuani ya kiji
chake. Ilielekea barua hizo zilitoka nje ya nchi, kwani stempu zote zilikuwa na
picha ya malkia au wafalme wazungu, muhuri ukiosomeka waziwazi
“Stockholm-sweden”. Tarehe kwenye mihuri hiyo zilionyesha kuwa zilitumwa zaidi
ya miaka kumi na mitano iliyopita!
“Barua!” Niliropoka.
“Ndiyo,” babu alijibu
“Mbona hazijafunguliwa? Ni za zamani sana,” nilisaili.
Babu naye akaonyesha
mshangao wake kwangu, “Mjukuu wangu, zinalekea kuwa ni barua muhimu sana.
Unadhani ningeweza kumpelekea mtu yeyote asome siri zangu na kuanza
kunitangaza? Nilikuwa nakusubiri, nilijua ungerudi salama.”
“Ni wewe peke yako
utakayekuwa wa kwanza kuelewa chochote kilichoandikwa humo.”
“Zilifikaje hapa?”
Niliuliza nikianza kufungua moja
niliyoiona ya zamani
zaidi.
“Zililetwa. DC alileta
kwa mkono wakemwenyewe.
Alinishawishi kufungua
lakini nilikataa katakata.”
Baada ya maelezo hayo
babu alikunjua kiti chake cha uvivu, kilichotengenezwa kwa ngozi ya nyati na
kujilaza kimya kwa namna ya kunipa wasaa wa kusoma barua hizo kwa tuo. Barua ya
kwanza ilikua ndefu kidogo. Ilianza kwa salamu za siku nyingi, ikaendelea kwa
taarifa ya kuipongeza kazi yake alipokuwa nchini humo, “Tumetengeneza filamu
mbili za ile michezo uliyoshiriki kuicheza. Filamu hizo zimependwa sana Ulaya
nzima zinanunuliwa kama peremende. Taarifa tuliyoichapisha hapa chini ni malipo
yako ya mrabaha hadi sasa. Tunaomba ufanye kila uwezalo kuwasiliana nasi ili
upokee malipo yako,”
ilieleza barua hiyo.
Sehemu ya pili ya barua
hiyo ilikuwa na mahesabu ya idadi ya mikanda iliyouzwa na televisheni
zilizonunua hakimiliki na hakishiriki. Kwa hesabu za harakaharaka asilimia ya
babu ilionyesha kama dola 227,000. Sikuyaamini macho yangu. Nikainua macho
kumtazama. Alikuwa amesinzia, tabasamu likiwa mdomoni.
Nikafungua barua ya
pili. Hii iliandikwa mwaka mmoja baadaye. Ilisisitiza, umuhimu wa babu kwenda
haraka au kumtuma mrithi wake yeyote anayeaminika. Iliongeza kuwa iwapo kuna
tatizo lolote la vitambulisho mwakilishi huyo alichotakiwa ni kwenda na ile
hirizi ambayo ilikuwa haibanduki shingoni mwake. “Benki yetu tayari imearifiwa
juu ya hilo. Usiwe na wasiwasi,” iliongeza barua hiyo.
Barua ya tatu
iliambatanishwa na hundi. Hesabu zilizoandikwa juu ya hundi hiyo
zilinitatanisha dola 812,000! Barua ilisisitiza fedha hizo kuchukuliwa.
Ikiongeza kuwa benki yao tayari imefungua matawi nchini katika miji ya Dar es
Salaam na Mwanza, haikuwepo haja ya kusafiri hadi Ulaya tena.
Mara nikaanza kupata
njozi za mchana. Nilijiona nikiandika kitabu, ambacho kiliyahusu maisha yangu
mwenyewe. Niliyaumba na kuyaumbua matukio, mikasa na visa vyote vilivyonikumba
toka katika safari zangu kuu mbili safari ya kimaisha iliyonifikisha kila pembe
ya nchi na ile ya kimaumbile ambayo ilinitoa utotoni na kuniingiza ukubwani.
Nilihisi hata jina la kitabu likinijia akilini; Kiguu na Njia.
Zikanijia njozi
nyingine. Katika njozi hizi nilijiona nikiwalekeza watu wa masuala ya filamu
wapi pa kuelekeza kamera zao, katika filamu niliyokua nikiitengeneza.
Niliwataka ihusishe maeneo yote muhimu ya nchi yetu, mbuga za wanyama, maziwa
na mito yote ambayo haikupata kutangazwa vizuri. Kwa njozi niliona mikanda ya
filamu hiyo ikigombewa na kuwafanya watazamaji waone hazina kubwa
iliyosahauliwa ambayo walijaliwa na Muumba.
Nikaona jinsi
nilivyokuwa nikiishi na mke wangu Nashifa kwa furaha. Watoto wetu wawili wenye
afya njema
wakicheka na kufurahi…
Halafu nikamkumbuka
mwenye fedha zake, ambazo zingeniwezesha kufanikisha ndoto hiyo. Nikageuka.
“Babu!” niliita tena
nikimtazama.
Alikuwa bado amelala
vilevile kwenye kiti chake cha uvivu. Tabasamu lake lilikuwa bado limesahauliwa
palepale usoni kama mtu aliyekuwa katika dimbwi la starehe. Niliinuka na
kumshika bega. Nikamtikisa taratibu, baadaye kwa nguvu kidogo, “Babu… babu…
babu…!
Kimya! Kimya!
Nikashtuka. Alikuwa kama
hapumui! Nikamshika kifua kusikiliza mapigo ya moyo. Hayakuwepo. Hata mwili
wake tayari ulikuwa umepoa. Ndio kwanza nikabaini kuwa babu hatukuwa naye tena
duniani! Tabasamu lake lililobakia palepale kama ishara ya ushindi kwa jambo
zito lililokuwa likimsumbua kwa muda mrefu.
Nilitetemeka mwili
mzima. Nguvu zikaniishia, furaha, faraja na matumaini makubwa niliyoyapata mara
baada ya kuisoma barua yake, ikatumbukia nyongo.
MWISHO

0 Comments