Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Mume gaidi sehemu ya kumi na saba (17)

 


Tina aliporudi ndani alimkuta Tusa anacheka.

TINA: Kinachokuchekesha ni nini sasa?

TUSA: Nilikwambia Tina, mshika mawili moja humponyoka dada.

TINA: Sasa ndio ucheke? Yani na wewe hujui madili kabisa sijui ukoje Tusa. Umenikera sana leo.

TUSA: Ndio ujipange sasa kumchagua mmoja. Kusuka au kunyoa?

TINA: Kwenda zako huko, huna lolote wewe. Yako yamekushinda, utaweza yangu wewe?? Huna ulijualo hapo ulipo.

Tina akakaa chini kwa hasira, mara akasikia anaitwa ila hakutoka kule nje, ikabidi Deborah aende ndani na kumshika Tina mkono na kutoka nae pale nje.


Tina alikuwa ameinamisha macho chini tu pale nje kwa aibu.

DEBORAH: Haya sasa, nataka utamke kwa mdomo wako mwenyewe. Wako ni Yuda au Tulo?

TINA: Sijui.

DEBORAH: Khee! Huna hata aibu, eti sijui. Inamaana hujui unampenda nani? Au hujui kama unampenda au la! Wewe ni waajabu sana. Hapa ni kusema tu wako ni yupi, na kama huwataki wote sema niwatimue hapa.

Tina akajifikiria sana, akafikiria mambo mengi na mtihani aliopewa hapo. Ikabidi achague moja kuliko kukosa vyote, alitaka amchague Tulo kwaajili ya pesa alizo nazo ila kauli ya Tusa ilimrudia sana kichwani mwake kuwa aangalie mapenzi ya kweli na si pesa, hivyo basi akaamua kumchagua Yuda.

Deborah akamuomba Tulo aondoke, Tulo aliumia sana moyo wake na kuamua kuondoka na Mwita, hakuamini kama Tina angemfanyia vile baada ya mambo yote aliyomuahidi.


Adamu na ndugu zake hawakuacha kumjadili Patrick, Deborah akawaomba sana na kuwasihi kuwa waache kumjadili Patrick.

DEBORAH: Naomba muache kumjadili Patrick, wakati familia yenu imelaaniwa.

REHEMA: Unamaana gani Deborah?

DEBORAH: Patrick nimempigia simu na amesema kesho anarudi, kesho nitaweka kikao na kuwaelezea jambo fulani najua wote mtastaajabu na kushangaa.

Hawakumuelewa Deborah, na wote wakawa wakijiuliza maswali kuwa ni jambo gani ambalo Deborah alihitaji kumwambia.


Mwita na Tulo walienda baa ili kujiliwaza kwa yale majanga yaliyomkuta Tulo siku hiyo.

Mwita alikaa karibu na Tulo ili kumchunguza zaidi kazi afanyazo ila Tulo hakulitambua hilo.

Mwita alianza kugundua mambo mengi sana kuhusu Tulo.


Patrick aliweka mtego wa kumnasa Mashaka, alimtegeshea mtego mdogo wa mtoto wa kike kwani Mashaka alipenda sana wanawake. Patrick akaona kuwa hiyo ndio itakuwa njia pekee ya kumpata Mashaka.

Patrick alitaka amshughulikie Mashaka na Maiko kwa mikono yake mwenyewe, bila ya kujua kuwa Maiko nae anampango huo huo na Mashaka.

Mashaka aliingia hotelini na binti yule bila kujua kuwa chumba alichoingia yupo Patrick.



Mashaka aliingia hotelini na binti yule bila kujua kuwa chumba alichoingia yupo Patrick.

Mashaka hakuwa na habari wala nini, akashangaa akikabwa kwa nyuma na kuanza kufurukuta, alipogeuka mbele ana kutana macho kwa macho na Patrick, kwanza kabisa Mashaka hakuamini kama ni kweli yupo mikononi mwa Patrick au anaota.

Akataka kupambana na Patrick, ila akapewa ngumi moja ya kishindo na kutulia.

PATRICK: Na utulie hivyo hivyo, tunatoka hapa hotelini kuna mahali tunaenda. Ukileta papara tu, leo nitakumaliza.

Ikabidi Mashaka awe mpole kwani hakutaka kupoteza nguvu zake kupambana na Patrick ilihali anajua wazi kuwa atashindwa.

Patrick alitoka na Mashaka kimya kimya na kuingia nae kwenye gari ya Mashaka ambapo Dereva alikuwa ni Mashaka mwenyewe, alipeleka gari kulingana na alivyoelekezwa na Patrick.


Adamu akaitwa na mama yake ili wazungumzie swala la Deborah analotaka kuwaambia.

REHEMA: Eti, unafikiri Deborah ana jambo gani la kutuambia?

ADAMU: Kwakweli sijui mama, yani sijui chochote.

REHEMA: Au huyo Patrick ni mwanao?

ADAMU: Mama, Deborah kwangu hakuondoka na mtoto wala mimba. Kwakweli hata mi mwenyewe sijui huyo mtoto amezaa na nani.

REHEMA: Kama alikuficha je kumbe alikuwa na mimba yako?

ADAMU: Mama, kwajinsi ilivyokuwa Deborah angekua na mimba ningejua tu hata kama ingekuwa ya mwanaume mwingine. Deborah kwangu hakuondoka na mimba wala mtoto na nilipojaribu kumdadisi kuhusu baba wa mtoto wake alikuwa mkali sana, mi nahisi alibakwa baada ya kutoka kwangu ndomana yupo hivyo.

REHEMA: Sasa, anachosema kuwa amegundua kuhusu familia yetu ni kitu gani?

ADAMU: Mama, hata usijipe presha. Deborah ukimzoea ndo maneno yake hayo hayo. Mi sidhani kama anachaajabu kutueleza ila nia yake kubwa ni tuache kumzungumzia huyo jangili wake.

REHEMA: Na sasa je una mpango gani na huyo Patrick?

ADAMU: Ni kumfungulia kesi tu hata kama hatuna ushahidi, ila kiukweli mama yangu simpendi yule kijana balaa, namchukia sana kwani amenitesea sana mwanangu ila nashindwa kujielewa kwanini hadi sasa nashindwa kumchukulia hatua.

Adamu akawa anatafakari kitu cha kumfanya Patrick.


Patrick alienda porini na Mashaka, kulekule alipoenda na Tulo hadi akatokewa na mzimu wa mzee Ayubu. Sasa aliamua kwenda na Mashaka.

Alikwenda nae kimzobe mzobe kwani haikuwa rahisi kwa Mashaka kuingia porini.

Mashaka akaamua kutumia nguvu zake ili kuweza kupambana na Patrick ili pengine aweze kutoka mikononi mwake, na mpambano ukawa mkali sana.

Patrick alimdhibiti Mashaka kwa kumfunga kwenye mti, mwili wote wa Mashaka ulijazwa kamba alizofungwa na Patrick, kisha Patrick akamtazama na kuanza kumuongelesha.

PATRICK: Huwa sipendi kusumbuliwa, ungetulia hata yasingefikia yote haya.

Mashaka alimuangalia tu Patrick na kukosa cha kumjibu.

PATRICK: Haya bila papara wala vurugu, nahitaji unijibu haya maswali kwa ufasaha. Kwanini umesema kuwa mimi ndiye niliyemuua mzee Ayubu?

MASHAKA: Si kwamba nilikutaja wewe, Maiko ndiye aliyekutaja. Mimi nilisema kuwa Maiko ndiye aliyeua.

PATRICK: Na kwanini ulisema kuwa Maiko ndiye aliyeua? Ulitaka nini?

MASHAKA: Sikutaka chochote.

PATRICK: Na kwanini ulitoa oda ya kumuua mzee Ayubu ilihali unajua kuwa Maiko ni mwanae?

MASHAKA: Mimi sikujua kama Maiko ni mwanae, kwanza tambua kwamba nilichokuwa najua mimi ni kuwa Maiko ni mwanangu, jambo ambalo lilikuwa sivyo. Ayubu aliwahi kuwa bwana wa dada yangu Rehema, na baada ya kuachana kumbe akahamisha makombora kwa dada yangu mwingine ila nadhani hakujua hilo kama Neema na Rehema ni ndugu.

PATRICK: Kwahiyo umemuua kwasababu hiyo tu?

MASHAKA: Hapana, ila Ayubu alinichukulia mwanamke wangu ambaye alikuwa mama wa mwanangu niliyemdhania ndiye Maiko. Niliapa kwa Ayubu kuwa nitamlipizia kisasi, oda ya kumuua ilikuja kwa hitaji la biashara na hitaji binafsi la kulipa kisasi.

PATRICK: Hadi sasa umeua watu wangapi?

MASHAKA: Kwakweli sijui.

PATRICK: Huwezi kujua ndio, idadi yao ni kubwa sana. Hivi ni nani atakayekuelewa hayo uyasemayo Mashaka? Hivi wewe ni mtu kweli katika watu? Kumlipiza mtu kisasi ndio kumuua?

Mashaka aliendelea kumtazama Patrick huku akimsihi amfungue kwenye ule mti.

PATRICK: Kwa leo adhabu yako ni hiyo, utalala hapohapo mi naondoka. Nataka ufe taratibu ili ujue uchungu wa kifo.

Halafu Patrick akaanza kuondoka, jambo pekee ambalo Patrick hakulijua ni kuwa muda wote alikuwa anafatiliwa na Maiko kwa tahadhari kubwa sana.


Kesho yake Pamela na Fausta nao wakajadili na kusemezana.

FAUSTA: Unaonaje tukimwambia Tusa ukweli kuhusu kifo cha babu yake?

PAMELA: Unamaana tumwambie kuwa Patrick ndio kaua?

FAUSTA: Hapana, ila tumueleze kuwa babu yake alishakufa ili nae apate kujua.

PAMELA: Nadhani itakuwa ni jambo la busara maana Tusa hajui chochote kile.

Wakaamua kumuita Tusa ili kumwambia ukweli.


Baada ya mikasa kutulia ya wale vijana wawili yani Tulo na Yuda. Tina alijihisi kuwa ametua mzigo uliokuwa umemuelemea ingawa alikuwa na mawazo kiasi.

TUSA: Hujakosea Tina, uamuzi uliochagua ni sahihi na ipo siku utanishukuru kwa ushauri wangu.

TINA: Sawa ila nimepiga teke fuko la hela.

TUSA: Usimdharau Yuda, anakupenda sana. Naimani ataendelea kukujali na kukutunza. Hujapoteza kitu ila umechagua jambo jema.

TINA: Vipi na wewe hatma yako?

TUSA: Ushauri wako mbovu ndio ulioniponza, hilo fuko la hela unalosema ndio linalonitesa kwasasa.

TINA: Kwani Patrick anafanya kazi gani?

Mara Tusa akaitwa na mama yake.


Walimueleza Tusa kila kitu kuhusu kuuwawa kwa babu yake kasoro hawakumwambia aliyemuua.

Tusa akalia na kuomboleza sana kwani alimpenda sana babu yake hata ile safari ya kipindi kile yeye na Sele kwenda Morogoro alitaka waende kwa babu yake huyo.

Tusa aliona huo ni mkasa mwingine katika maisha yake, na kilichomuumiza zaidi ni kule kuambiwa kuwa aliuwawa kikatili.


Tulo alikuwa na machungu bado ya kukataliwa na Tina.

TULO: Unajua bado siamini kama kweli Tina kanikataa kwaajili ya kale kavulana!

MWITA: Inabidi ukubaliane na hali halisi kwamaana hakuna cha kufanya.

TULO: Cha kufanya kipo, lazima nimkomeshe yule kijana.

MWITA: Utamfanyaje sasa?

TULO: Wewe tulia tu, mimi ndio Tulo na atajuta kuzaliwa mwanaume na kunifahamu mimi.

Mwita alizidi kuingiwa na wasiwasi juu ya mwenendo wa Tulo na hakutaka kuachana nae, aliongozana nae kila mahali kupata taarifa tu.


Marium na Anna nao wakajiandaa na kwenda kwa Deborah kwani alishawaambia kuwa anawahitaji dada zake ili atakapoyasema aliyonayo moyoni wote wawepo.

ANNA: Deborah nae anatutisha!

MARIUM: Yani kama anataka kufa vile loh!

ANNA: Ile familia nayo iliyomzunguka pale ni balaa.

MARIUM: Ile familia ni nuksi wewe, ina majanga hakuna mfano.


Rehema aliamua kuwaida Pamela na Fausta na kuwaeleza kuwa wao ni ndugu zake kabisa kwani Neema ambaye ndiye aliyekuwa mama yao alikuwa ni ndugu wa damu na yeye kwani walikuwa ni watoto wa baba mkubwa na mdogo na baba zao hao walikuwa mapacha.

Wote wakabaki wakistaajabu.

FAUSTA: Inamaana tumeoana ndugu kabisa wa damu?

REHEMA: Huo ndio ukweli.

Wakati wanazungumza hayo, mara akatokea Tusa na kuwafata tena kwa maswali kuhusu kifo cha babu yake.

TUSA: Niambieni ukweli nani kamuua babu?

PAMELA: Hatujui mwanangu.

REHEMA: Hebu mwambieni ukweli mtoto.

PAMELA: Ukweli upi mama?

REHEMA: Kama aliyemuua babu yake ni Patrick.

TUSA: Patrick yupi?

REHEMA: Patrick mumeo.

Tusa hakuamini kabisa, mara Patrick nae akawa amerudi na kuingia ndani.

Tusa alivyomuona alinyanyuka na kukimbilia jikoni, kisha akachukua kisu na kumfata nacho Patrick kwa hasira.


Tusa alivyomuona alinyanyuka na kukimbilia jikoni, kisha akachukua kisu na kumfata nacho Patrick kwa hasira.

Tusa alikuwa amejawa sana na hasira dhidi ya Patrick, alikishika kile kisu kisawasawa na moja kwa moja alitaka akilengeshe kwenye kifua cha Patrick ila kabla hajafanya hivyo Patrick alimdaka mkono Tusa na kumpokonya kile kisu.

Tusa akaanza kumzenga zenga Patrick kwa maneno mengi makali, aliongea huku akilia na machozi kumtoka.

TUSA: Niue na mimi Patrick, naomba uniue kama ulivyoua hao tengine.

PATRICK: Kwani wewe mwanamke vipi? Una mashetani au?

Kisha Patrick akamsukumia Tusa pembeni na yeye akaelekea chumbani kwake, Tusa akaona kuwa ana kazi ya ziada kwa Tusa.


Maiko alienda moja kwa moja pale ambako Mashaka alipofungwa, Mashaka alishakata tamaa kwani hakuona msaada wowote ukizingatia ni porini.

Maiko alimwangalia na kumwambia.

MAIKO: Nimekuja kukusaidia kwa lengo na nia yangu moja kubwa sana.

Mashaka hakujali nia ya Maiko kwa muda huo ni nini ila alichojari ni kupatiwa huo msaada.


Yuda nae akajitahidi kumtafakari Tina ambaye alimshangaa tabia yake kwa muda mfupi kiasi kile.

SELE: Usiumize kichwa ndugu yangu, kuwa na Tina kunahitaji uvumilivu tu hata usiwe na wasiwasi.

YUDA: Uvimilivu si tatizo, tatizo ni kuwa hana msimamo bhana. Atakuwaje na mimi halafu anamkubali mwanaume mwingije.

SELE: Usijari, Tina yupo katika mabadiliko ya maisha yake na atakuwa kwenye mstari uliyonyooka tu hata usiwe na wasiwasi ndugu yangu.

Yuda alimpenda sana Tina na ndiomana alijitoa sana dhidi ya Tina.


Adamu alipoingia pale sebleni kwa Deborah akashangaa kubambana na kilio cha binti yake, na alipouliza akagundua ukweli kuwa binti yake analia kifo ch babu yake ambaye yeye ni baba yake.

Wote walikereka kwa kutambua uwepo wa muuaji ndani ya nyumba ila wote waliogopa sana hata kumgusa, ni Tusa pekee ndiye aliyejaribu kumsogelea mwilini Patrick.

Deborah naye alipofika akakutana na lile zogo, alipoambiwa.

DEBORAH: Mnanishangaza sana nyie binadamu msio na fadhila, sasa kumnywesha hiyo sumu ya unafki Tusa mnataka afanye nini? Nadhani mnataka amchukie zaidi ya vile anavyomchukia, ila sumu mnayoipandikiza mtainywa wenyewe.

ADAMU: Sasa hukupenda aujue ukweli?

DEBORAH: Ukweli mnaushahidi? Bora mie niliyeficha ukweli kwa muda mrefu nikingoja ushahidi ila Mungu si Athumani hatimaye ushahidi nimepata.

REHEMA: Tatizo Deborah hutaki kukubali kuwa unafuga maradhi ndani.

Ndugu wa Deborah wakawasili, nao ni Marium na Anna walikuja kwaajili ya kikao ambacho Deborah amewaitia.


Tina aliyekuwa chumbani akiendelea kujitafakarisha mwenyewe, aliamua kwenda sebleni aliposikia kuna kikao. Na alipoona majonzi ya Tusa akaamua kumbembeleza kwani wao walishaliaga na yakaisha.

TUSA: Kinachoniumiza ni kusikia kuwa Patrick amehusika.

TINA: Usiamini sana Tusa, hakuna mwenye ushahidi hata hivyo Patrick hawezi kufanya unyama ule.

Tina alizidi kumbembeleza Tusa na kumliwaza.


Deborah akamuita mwanae Patrick ili waweze kuzungumza.

PATRICK: Kwani kikao kinahusu nini? Kuachana mimi na Tusa? Kama kinahusu hivyo, mimi nasema hapana. Simwachi Tusa.

TUSA: (Kwa ukali), unaning'ang'ania mimi ndugu yako?

PATRICK: Nani umesikia anahaja na undugu na wewe na ukoo wako huo? Mi nakung'ang'ania kwa pesa yangu uliyopoteza toka nakufatilia, na kama kuna wa kumlaumu kwa hili basi mlaumu Maiko aliyekuwa akinishauri nitoe pesa nyingi sana kwako. Nadhani aliwajua ukoo wake kama mnapenda pesa.

PAMELA: Halafu sisi sio kwamba tunapenda pesa kama unavyofikiria.

PATRICK: Uliona wapi mzazi mwenye mapenzi mema na mwanae akamuozesha kwa posa ya milioni kumi na tano? Si uchizi huo, ukoo wenu umelaanika nyie.

DEBORAH: Mwanangu acha kabisa hayo marumbano, leo nataka kusema kitu ambacho nimekiweka moyoni kwa muda mrefu sana.

PATRICK: Nadhani itakuwa kuhusu baba yangu ila sidhani kama hawa wengine wanahusika.

ADAMU: Ni kweli hatuhusiki, hapa tuongelee mambo ya msingi. Kwanza kabisa kwanini mwanao kaua baba yetu na pia kwanini anaendelea kumtesa mtoto wetu.

DEBORAH: Hili jambo wote linawahusu na ndiomana nimewaita wote ili nipate kuwajuza na mjue kila kitu kilichotokea. Najua Adamu unapotezea sababu hutaki maovu yako ya nyuma yawe wazi, ila kosa dogo ulilotenda kipindi hicho cha nyuma leo ndio lililozua balaa, tafrani na mtafaruku katika maisha yenu.

MARIUM: Bora tu uelezee ulichotuitia Deborah, hayo unayoyaongea hayana msaada wowote kwenye hiyo familia iliyo laanika.

Adamu akachukia sana kwa hiyo kauli juu ya familia yake kuwa imelaanika.

ADAMU: Chunga kauli yako mwanamke.

MARIUM: Kauli yangu!! Kwani uongo? Familia gani kaka na dada wanazaa pamoja, halafu baba anabaka mwanae kama sio laana ni kitu gani?

Adamu alizidi kuchukia na kutamani kutoka kwenye kile kikao.


Mwita aliomba na ruhusa kazini kwaajili ya kuendelea kuchunguza mambo ambayo yanaonyesha kumpa utata mkubwa sana. Alihisi kuwa kuna kazi ambazo si halali zinazotendwa na Tulo pamoja na baba yake bwana Maiko.

Mwita aliendelea kuwa karibu na Tulo haswa kuhusu kisasi alichotaka kulipiza kwa Yuda. Mwita alitaka kujua kuwa Tulo atafanya kitu cha aina gani, akaandaa mtego wa kumkutanisha Tulo na Yuda bila ya Tulo kujua kama ni mtego tu.


Wakiwa tayari kuanza kikao baada ya marumbano ya hapa na pale kuhusu familia ya Adamu, gafla walisikia kelele nyingi nje kama vile mtu anakabwa. Kelele zile ziliwashtua na kuwafanya watoke nje kuangalia kuna nini.

Walipotoka nje walikuta damu nyingi sana imetapakaa pale nje ila hawakuona mtu yeyote.

Wote wakashangaa kuwa ni kitu gani.

http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Wote wakashangaa kuwa ni kitu gani.

Marium ndio alikuwa wa kwanza kuuliza,

MARIUM: Mambo gani haya jamani?

DEBORAH: Hata sielewi ni kitu gani.

Adamu akainama na kuangalia ile damu,

ADAMU: Ila hii damu inaonyesha kuwa ni ya mtu.

PAMELA: Mtu gani sasa?

ADAMU: Sijui.

Patrick alikuwa kimya kabisa huku akitafakari mambo mbali mbali katika akili yake bila ya kupata jibu.

Alijiuliza vitu vingi bila ya majibu.

"Inamaana kuna mtu kauwawa hapa kwetu? Kama yupo je yuko wapi? Au ni mauzauza ya mzee Ayubu?"

Akakosa jibu, akawaacha wote pale nje na kurudi ndani.

Nao wakamshangaa Patrick kuonekana kamavile hajashtushwa na lile tukio, tena kamavile amelipuuzia na kuona halina maana au ni kitu cha kawaida.

REHEMA: Itakuwa anaelewa kilichotokea, wengine tunaumiza vichwa hapa wakati mwenzetu kashaelewa kilichotokea.

Tusa na Tina nao wakaamua kurudi ndani na kuwaacha wazazi wao pale nje kwani waliogopa kukutwa na makubwa pale nje.

DEBORAH: Sasa aliyeelewa ni nani?

REHEMA: Mwanao Patrick atakuwa anajua kila kitu.

DEBORAH: Naona unamchukia sana Patrick, ila ukweli utakapokuwa wazi najua utaona haya.

ADAMU: (kwa ukari), Sio maneno ya kumwambia mama yangu hayo.

DEBORAH: Wee mwanaume wewe tafadhari sana, mfokee mkeo sio mimi. Tena ukome kunikaripia, kumbuka hapa ni nyumbani kwangu, nina uhuru wa kufanya na kusema chochote ninachojisikia.

ADAMU: Siku hizi una kiburi sana wewe mwanamke.

DEBORAH: Ndio nina kiburi na jeuri pia.

FAUSTA: Jamani, msianzishe zogo lingine hapa. Kama vipi tukaendelee tu na kikao chetu.

PAMELA: Sasa nyinyi hizi damu mnaona tu ni kitu cha kawaida?

FAUSTA: Si kitu cha kawaida Pamela ila haina jinsi na hakuna la kufanya.

DEBORAH: Damu huwa ni kiashirio cha vitu vingi sana, pia najua inatukumbusha mambo mengi ya nyuma ama tuliyofanya au tuliyofanyiwa.

MARIUM: Sawa, basi turudini ndani.

Bi.Rehema akamvutia Adamu kwa pembeni wakati wengine wanarudi ndani.


Bi.Rehema akamuuliza tena Adamu kuhusu Deborah.

REHEMA: Kwani wewe na huyu mwanamke mna tatizo gani? Mliachana kwa mateke na ngumi nini?

ADAMU: Hapana mama, huyo mwanamke ni kisirani tu huwa hata sijui ana matatizo gani.

REHEMA: Au bado mnapendana?

ADAMU: Aaah mama!! Maswali gani hayo? Si unamuona mwanamke mwenyewe alivyo jeuri jamani.

REHEMA: Ndio kawaida ya wanawake wakipata mali, ila wewe vumilia mwanangu ili tuondoke hapa kwa usalama.

ADAMU: Sawa mama, hakuna tatizo.

Adamu akakubaliana na mama yake kutulia.


Tulo na Yuda wakakutana kama ambavyo Mwita amepanga mtego wa kuwakutanisha.

TULO: Niambie kidume, wewe si ndio unajifanya kidume.

YUDA: Sio najifanya, mimi ni mwanaume niliyekamilika.

TULO: Kumbe umekamilika eeh!!

YUDA: Ndio nii mwaname niliyekamilika na kujiamini sana.

TULO: Napenda sana wanaume wa aina yako.

Yuda hakutaka kuendelea kuwepo eneo lile na kuamua kuondoka hata kumshangaa aliyemuita pale bila kumuon.

Wakati Yuda anaondoka, akili ya Tulo ilishapanga kitu kingine juu ya Yuda.


Deborah na wengine wakataka kuanza kuzungumza yaliyowafanya waweke kikao humo ndani.

DEBORAH: Mbona hawarudi Adamu na mama yake?

Mara na wao wakarudi mule ndani na kukaa kwaajili ya mazungumzo.

PAMELA: Jamani mimi nina wazo, kabla ya kuanza kikao hapa wangetoka hao wanaume na kwenda kuangalia angalia nyumba nzima ili tujiamini kuwa tuko salama.

Patrick na Adamu wakajifanya kama vile hawajasikia kitu chochote kinachozungumzwa na Pamela kwani walikuwa kimya kabisa.

Pamela hakuna na imani na ile damu ukizingatia imeachwa pale nje, akapata wazo la kwenda kuifukia ile damu.


Kitu ambacho Maiko alikifanya hakuna aliyekijua kwa wakati huo ila Maiko mwenyewe alikuwa kama vile mtu aliyechanganyikiwa na hakujielewa kabisa kwa mambo aliyoyafanya.

Alidhani moyo utasawazika na kitu alichofanya, cha zaidi zaidi aliendelea kujiuliza kuwa kwanini amefanya alivyofanya.

Maiko alikuwa ndani ya gari, karibu kabisa na nyumbani kwa Deborah akatamani ajitokeze ili aongee anachotaka kusema ila alishindwa kwa kuona kuwa watamchukuliaje na kumuonaje.


Yuda akiwa anaondoka, akaamua kupita njia za mkato ili kurudi kwao.

Wakati anatembea sasa, mbele yake akazuiwa tena alizuiwa kwa kukabwa kwa nyuma.

Yuda akakukuruka sana, alipogeuka alikutana tena na Tulo, ila Tulo alikuwa tayari kwa mpambano safari hii.

Kwahiyo Tulo na Yuda wakaanza kupambana, kurushiana mateke, kupigana ngumi na kupimana mabavu. Kila mmoja alijifanya gangwe mbele ya mwingine.

Matukio yote haya yalikuwa yakishuhudiwa na Mwita aliyetumia mbinu za kijeshi kuwafatilia bila ya wao kujua.

Mpambano kati ya Yuda na Tulo ulikuwa mkali sana, Tulo akatoa bastola na kumnyooshea Yuda kwa lengo la kummaliza kabisa.

Mwita akashangaa kumuona Tulo na bastola, akajiuliza kwa raia wa kawaida kama Tulo atawezaje kumiliki bastola? Ana kibali gani cha kumiliki silaha kama ile?

Wakati Mwita akitafakari hayo, mlio mkari wa risasi ukasikika masikioni mwake "Paaaaaa"

Mwita akapatwa na mshtuko, huku moyo wake nao ukilia paaaa kwani ni yeye aliyeamua kuwakutanisha Yuda na Tulo siku hiyo ili ajue kile ambacho Tulo amepanga kumfanyia Yuda.


Sele aliyekuwa yupo ndani kwao, akapatwa hofu juu ya Yuda. Akahisi kuwa kuna kitu kibaya kimempata ndugu yake huyo.

Akaamua kumfatilia kwa njia aliyoondokea ili labda akutane nae njiani kwani hofu ilimjaa sana juu ya Yuda, ukizingatia hakuelewa kuwa Yuda aliitwa na nani kwani tangu alivyopigiwa simu na kuondoka hakurudi tena na wala hakuaga vizuri aendako.


Pamela alikuwa na uhitaji sana wa kutoka ili akaifukie ile damu kwani hakuona kuwa ni kitu kizuri wao kukaa na mazungumzo ndani wakati wanajua kuwa kuna damu imetapakaa nje ya nyumba ile.

Deborah hakutaka kujali sana kuhusu ile damu ila yeye alitaka kuendelea na maongezi yake aliyowaitia toka mwanzo.

DEBORAH: Nitapenda historia hii niieleze kwa makini ila sitahitaji swali lolote hadi pale nitakapohitimisha.

PATRICK: Kwani ni historia ya maisha yako au ni historia ya nini?

DEBORAH: Ni historia ya maisha yangu ila najua wengi itawagusa, na wengi wataelewa kile ambacho nitakieleza. Na huu ndio ukweli mtupu wa maisha yangu.

Pamela akaingilia kati wakati Deborah akiendelea kuzungumza.

PAMELA: Samahani kwa kukukatisha Deborah, ila nina ombi kidogo.

DEBORAH: Ombi gani? Hutaki niwataje majina yenu halisi kwenye stori hii.

PAMELA: Hapana sio hivyo, ombi langu ni jingine. Ila hata hivyo, unamaana unataka kuelezea yale yaliyopita zamani?

DEBORAH: Ndio, kwani kuna ubaya?

PAMELA: (Huku akisitasita), aaah hapana hakuna ubaya ila sidhani kama watoto wetu itawahusu.

DEBORAH: Itawahusu ndio, napenda wajifunze kuwa duniani kuna watu wa tofauti na umdhaniaye siye kumbe ndiye. Labda kama una lingine Pamela.

Pamela aliona Deborah anataka kumuumbua tu, jinsi yeye na Adamu walivyomsaliti ila hakuna jinsi ilimradi Deborah kaamua kuongea akaamua wamuache tu aongee.

PAMELA: Ila nilikuwa naomba nikafukie ile damu pale nje maana si kitu kizuri kuzungumza ndani wakati nje kukiwa na damu isiyoeleweka ni ya nini.

Deborah akamruhusu Pamela aende.

Pamela akatoka nje na muda huo huo akarudi ndani na kuwaambia kuwa ile damu haipo.

DEBORAH: Unamaana gani?

PAMELA: Ile damu haipo, sijaikuta pale ilipokuwa.

Deborah akaamua kwenda kuangalia mwenyewe.



Deborah akaamua kwenda kuangalia mwenyewe.

Alipofika nje hakuona chochote na kurudi ndani.

DEBORAH: Ni kweli hakuna chochote, ile damu imepotea kweli.

Wote wakabaki kumtazama tu.

FAUSTA: Sasa hiyo damu inamaana gani? Kuja na kupotea?

DEBORAH: Kiukweli inakuwa ngumu kuelewa.

MARIUM: Mi nadhani tutoke nje na kutazama nyumba kwanza.

Wote wakakubaliana kutoka nje, wakati wananyanyuka, Patrick wala hakujishughulisha nae, aliendelea kukaa pale pale walipokaa.

Tusa nae akamvuta Tina na kumzuia kutoka nje ili waweze kujadili mambo yao.


Tina alikaa karibu na Tusa pale alipomwita.

TUSA: Unajua kwanini nimekuzuia?

TINA: Niambie kwanini, mi sijui.

TUSA: Nimeona wanajisumbua tu hakuna lolote, nadhani kuna mtu anawafanyia mchezo bila ya wao kujua.

TINA: Mmmh!! Kweli Tusa?

TUSA: Huo ndio ukweli wenyewe ila hao watu huwa hawashauriki, waache wajisumbue wakisharidhika na yao watarudi ndani.

Mara wakamuona Patrick akiinuka pale kwenye kochi na kuelekea chumbani kwake.

TINA: Na mbona Patrick yuko vile?

TUSA: Atakuwa ana mipango yake mibovu tu pale alipo, roho inaniuma sana tangu nisikie kuwa kamuua babu ila sina la kufanya kwamaana Patrick ana nguvu sana. Lakini nitalipa kisasi tu.

TINA: Mi nadhani kuwa yote tumuachie Mungu.

Wakamuona Patrick akirudi tena pale sebleni, wakaamua kunyamaza kwasasa.


Wakiwa pale nje na kujadili.

REHEMA: Ila mimi nawashangaa sana, tuatoka nje ila muhusika tunamuacha ndani.

DEBORAH: Tafadharini sana, mwacheni Patrick wangu. Maswala ya kumsemasema siyapendi.

PAMELA: Mmh!!

Wakajaribu kuzunguka zunguka ila hawakuona chochote na kuamua kurudi ndani.

DEBORAH: Nadhani tukaendelee na kikao chetu.

FAUSTA: Haya mambo yanachanganya sana hadi tunakuwa kama machizi kwa kufatilia kitu tusichokijua wala kukitambua.

Wakarudi tena ndani, kama walivyotoka ndivyo walivyorudi.


Mwita aliumia sana moyoni na kuinuka pale alipokuwa kisha akaanza kukimbilia eneo ambalo Yuda na Tulo walikuwa wakipambaniana.

Kufika pale akagundua kuwa ile risasi ambayo Tulo aliipiga ilikuwa ni risasi hewa kwani alipiga hewani na si mwilini kwa Yuda.

Mwita akaanza kumsihi Tulo asifanye chochote kwani bado alikuwa ameshikilia bastola mkononi.

Mwita alipoona Tulo ni mgumu kuachia bastola, akaamua kutumia mbinu zake za kijeshi kuipata na kusahau kuwa Tulo ni jasusi.


Sele alipofika eneo la tukio alishangaa sana kuona nduguye amenyooshewa bastola.

Wakati Mwita akiwa anapokonyana ile bastola na Tulo, Sele nae akatumia muda huo kukimbia na nduguye Yuda na kuamua kukimbilia nyumbani kwa mama yao mdogo Deborah.


Deborah akaanza kuzungumza tena pale sebleni.

DEBORAH: Jamani yaliyopita yamepita, hebu tuzungumze mengine yanayotuhusu sasa.

REHEMA: Ila nyumba yako ina maajabu sana Deborah.

DEBORAH: Ila maajabu yake hayawezi kufikia maajabu ya ukoo wenu.

ADAMU: Hivi Deborah huwezi ongea bila kutaja ukoo wetu?

DEBORAH: Lazima niutaje, ukoo wenu umeniharibia sana maisha. Umeniharibia mwanangu Patrick, mtoto niliyemkuza huku nikimtegemea kuwa ni faraja yangu na atakuwa nami katika shida na raha. Ila ukoo wenu umemuharibu Patrick na bado mnataka kumuandama kwa maneno mengi na chuki.

Wote wakawa wametulia wakimsikiliza Deborah anavyobwabwaja ya moyoni mwake.

ADAMU: Sema mama sema, leo ni siku yako ya kutoa ya moyoni.

Deborah hakuacha kuwaambia jinsi gani wanamkera pale wanapomuongelea Patrick kwa mabaya tu wakati Patrick anawahusu.

Mara Yuda na Sele wanaingia kwa Deborah huku wakihema juu juu.


Ikabidi waulizwe ni kitu gani kinachowafanya waheme vile, Yuda akaelezea kwa ufupi ilivyokuwa.

Mara gafla wakamuona Patrick akiinuka na kutaka kutoka, Deborah nae akainuka na kumzuia.

DEBORAH: Mwanangu, hiki kikao kinakuhusu wewe. Tafadhari usiondoke mwanangu, si wameshasema kuwa wamemuacha na Mwita? Basi hakuna kitakachoharibika maana Mwita ni mwanajeshi.

PATRICK: Ila mama umezidi kuzungusha mambo, baada utueleze yanayohusika wewe kitu kidogo unakatisha mada. Kama nitarudi kukaa basi utueleze yanayohusika kwa makini.

DEBORAH: Usijari mwanangu, hiki kikao kina umuhimu sana kwako na maisha yako kwa ujumla. Napenda ujue ukweli wote uliojificha katika maisha yangu na katika maisha yako, kuna siri kubwa sana kati yangu na yako unatakiwa kuijua Patrick. Sitaki uende popote bila ya kuijua siri hii mwanangu.

PATRICK: Sawa mama, nimekuelewa.

Wakarudi wote pale sebleni, na wengine wakiendelea kumpa pole Yuda kwa kilichotokea.

MARIUM: Mkiambiwa msikilize maneno ya watu wazima mnayapotezea.

Haya sasa, yakishawapata ya kuwapata ndo mnakupuka mliyoonywa kabla.

Marium alikuwa kama vile anawakumbusha wanae kwa kauli zake ya kuwa waachane na Tina na Tusa kwani watawaletea mabalaa.


Kikao kiliendelea sasa na Deborah kuanza kueleza yaliyojiri, kumbe huku nje Maiko alikuwa amekuja na mfuko tena mfuko uliokuwa unavuja damu, ilionyesha kuwa kuna kitu alikibeba ndani ya mfuko huo.

Maiko na mfuko wake alisogea hadi kwenye mlango wa nyumba ya Deborah, uleule mlango wa kuingia sebleni.

Maiko ndio alisimama hapo na mfuko wake.


Maiko ndio alisimama hapo na mfuko wake.

Akatamani kugonga ule mlango ila akasita, akatamani kuingia bila ya hodi napo akasita.

Aliposikilizia kwa makini alimsikia Deborah akianza kuelezea historia ya maisha yake.

Ikabidi akae chini akiwangoja wamalize kuzungumza yale maongezi yao ili na yeye apeleke vyake.


Mwita alimshikilia Tulo na sasa alitumia kazi yake ya usalama wa taifa, hakutaka tena kuleta mambo ya urafiki.

MWITA: Tulo, unamiliki silaha kwa misingi ipi?

TULO: Maswali gani ya kuniuliza hayo bhana?

Mwita akaona hapa itakuwa longolongo, akaamua kujitoa kupambana na Tulo ili kumpeleka kituoni na maswali yale akayajibie kituoni kama wengine wafanyavyo.


Deborah alianza kwa umakini kabisa kuwaelezea na alipenda wote wapate kuelewa na kutambua ilivyokuwa toka mwanzo. Alitaka kueleza kila kitu kilivyokuwa hadi kilivyo sasa kwani yeye alijiona kama kiungo kikubwa cha katikati kwenye yale marumbano ya familia.


"Katika familia yetu ya watoto watatu yani mimi, dada yatu Marium na mdogo wetu Anna.

Wazazi walifariki na kutuacha tukiwa bado wadogo, shangazi yetu ndiye aliyechukua jukumu la kutulea sisi.

Tulikaa kwa shangazi huku tukimtegemea kwa kila kitu, kipindi hicho alikuwa akiishi hapa hapa Mwanza.

Nilipokuwa binti, alikuwa baba mdogo, ambaye ni mdogo wake na baba yetu mzazi, akamuomba shangazi anichukue mimi ili ampunguzie mzigo kidogo wa kulea, na alinichagua mimi kwavile nilikuwa mchangamfu sana na niliweza kumudu maisha mbalimbali.

Bamdogo alikuwa akiishi Arusha, hapo ndipo nikapata safari ya kutoka nje ya Mwanza na kwenda Arusha.


Kwa mara ya kwanza niliingia Arusha na kuona ni mji wa tofauti kidogo na Mwanza ambako nilikuzoea.

Bamdogo hakuwa mtu wa shida kwa kifupi alikuwa na pesa za kutosha hata nikamshangaa kwanini amechagua kunilea mimi tu wakati uwezo wa kutulea wote na ndugu zangu alikuwa nao.

Kwakweli niliyafurahia maisha ya Arusha haswaa pale nyumbani kwa bamdogo.


Kulikuwa na kijana aliyekuwa na urafiki na bamdogo, kijana huyo alikuwa anakuja mara kwa mara nyumbani kwa bamdogo, na huyu kijana ndio Maiko.

Alionyesha kuvutiwa sana na mimi kwani kila alipokuwa akija kwa bamdogo alikuwa anabeba zawadi mbalimbali na kuniletea, ila mimi sikuvutiwa nae wala sikumpenda. Nikamuona kama sehemu ya familia tu.

Kuna kipindi bamdogo alinituma nimpelekee mzigo wake Dar es salaam, alinikatia tiketi nami nikasafiri na kwenda huko.

Nilikaa Dar es salaam kwa muda wa wiki moja, nilifikia nyumbani kwa rafiki wa bamdogo yani kule nilikopeleka mzigo.


Nikiwa Dar es salaam, siku moja kabla ya safari yangu ya kurudi Arusha, nilimuomba mtoto mmoja wa ile familia niliyofikia anipeleke baharini ili nami nikashangae maji ya bahari kidogo kabla sijarudi Arusha.

Tukiwa baharini, akatokea kijana aliyejitambulisha kwetu kwa jina la Jumanne, kijana huyu alionyesha kuvutiwa sana na mimi kwani alimuomba nafasi ya kuzungumza na mimi yule mtu niliyekuwa nae kule baharini. Na yule dada akatupisha kidogo tuzungumze.

Jumanne akaanza kwa kunipa sifa kedekede na kunitongoza nikafurahia kwavile hata mimi nilivutiwa nae ila sikumuonyesha moja kwa moja kuwa namkubali, tukaongea ya hapa na pale ila nikakumbuka kuwa kesho yake natakiwa nisafiri na kurudi Arusha, nilipomwambia yule kaka alisikitika sana ila akaniomba nimuelekeze ninapoishi huko Arusha, sikukataa kumuelekeza kwavile nilivutiwa nae, nikamuelekeza kila kitu ila sikuwa na imani kama anaweza kufika Arusha kwaajili yangu tu.

Kesho yake kama ilivyopangwa, nikasafiri na kurudi Arusha.

INAENDELEA

Post a Comment

0 Comments