Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Mume gaidi sehemu ya kumi na nane (18)



Nilipokuwa Arusha, sura ya Jumanne haikuweza kutoka machoni mwangu. Ingawa nilimuona kwa siku moja tu ila moyo wangu ulimpenda sana ila sikufikiria kama Jumanne na yeye amenipenda kiasi kile nilichompenda mimi.

Ilikuwa hata akipita mtu mwingine mwenye jina hilo na kuitwa nilikuwa nashtuka mimi, hii yote ni jinsi gani Jumanne aliingia vizuri kwenye akili na mawazo yangu.

Siku zilipita bila barua wala mawasiliano yoyote kutoka kwa Jumanne na kipindi hicho ilikuwa simu ni kitu cha nadra sana labda zile za mezani ambayo pia namba yake nilimpa ila sikuwahi kuitwa kuwa kuna mtu ananipigia.

Nilijua Jumanne ameshanisahau kama kawaida ya wanaume ilivyo, anakukumbuka akikuona machoni tu, ukiwa mbali naye kumbukumbu juu yako anapoteza.

Ikabidi nianze kujilazimisha taratibu ili niweze kumsahau Jumanne.


Nikiwa nimetulia ndani, wazo la Jumanne likanijia tena kichwani, nikajikuta nikipiga kichwa changu kwa ulimbukeni wa kufikiri huku nikijilaumu kuwa kwanini namfikiria huyo Jumanne muda wote.

Alikuja mtoto wa bamdogo na kunishtua na huyu ndiye aliyekatisha mawazo yangu, akaniambia nje kuna mgeni wangu ananiningoja. Nikachukia sana kwani nilihisi kuwa huenda akawa Maiko kwani na yeye siku zingine alikuwa anafanya hivyo ili apate wasaa wa kuzungumza na mimi, nilitamani nisiende ila nikaamua kwenda ili nijue huyo Maiko kaja na mpya gani maana kama kumkataa nilishamkataa sana hadi kuchoka sasa.

Nilipofika nje nilimuona mtu kasimama chini ya mti halafu amegeuzia mgongo getini kwetu, nikajiuliza mgeni mwenyewe ndio yule au ni nani, nikarudi tena ndani kumuuliza mdogo wangu, akanielekeza alivyovaa ndipo nikajua kuwa mgeni mwenyewe atakuwa ni yule.

Nikatoka na kumfata pale chini ya mti, nikamgusa bega ili nimuulize kuwa ameniitia nini, kugeuka ni Jumanne.

Kwanza kabisa sikuamini macho yangu, nilijihisi kama vile naota. Nilijikuta nikimkumbatia kwa furaha, na kitu cha kwanza alichosema,

"Umeamini kuwa kweli nakupenda Deborah?"

Nikaitikia kwa kichwa tu kwani sikuamini kama Jumanne alifunga safari ya kutoka Dar kuja Arusha kwaajili yangu.

Tukaongea mengi sana pale chini ya mti, hadi alipoondoka na kuniahidi kuja tena kesho.


Penzi langu na Jumanne lilikua siku hadi siku, Jumanne alikaa Arusha kwa muda wa mwezi mmoja, akaniambia kuwa anapenda niwe mke wake ili niweze kurudi nae Dar kuishi wote kama mke na mume, nilifurahia sana na ndoto yangu kubwa ikawa kuwa mke wa Jumanne siku zote za maisha yangu.

Nilimuamini sana Jumanne kwani si kitu rahisi mtu kufunga safari ndefu vile kwaajili ya mwanamke tu wakati wanawake wapo wengi.


Usumbufu wa Maiko ulinikera sana, sikutaka hata kumuona mbele ya macho yangu, kumbe Maiko alimwambia bamdogo kuwa anataka kunioa na kuishi na mimi.

Bamdogo akaanza kunilazimisha kuwa niolewe na Maiko ila mimi nikakataa katakata, nikamwambia bamdogo kuwa nina mchumba na yupo tayari kunioa, bamdogo hakutaka hata kunisikia kuhusu huyo mchumba. Bamdogo akaniambia kuwa,

"ukiolewa na mtu mwingine tofauti na Maiko, ujue huna radhi na mimi"

Nilimuomba sana bamdogo anikubalie kuolewa na mtu nimtakae ila bamdogo alikataa kabisa, sikujua cha kufanya ili niweze kuolewa na kuishi na Jumanne.


Jumanne alikuwa na nia ya kunioa kweli kwani alitafuta watu wa karibu kule Arusha ili wazungumze na bamdogo nae apate kibali cha kuja kujitambulisha ila bamdogo hakutaka hata kumuoa Jumanne.


Hakukuwa na la kufanya kwani bamdogo alizidi kung'ang'ania kuwa mimi niolewe na Maiko, wakati Jumanne amerudi Dar nikakubaliana nae kuwa nitatoroka kwa bamdogo na kwenda Dar kuishi nae halafu tutaenda kujitambulisha kwa shangazi Mwanza.


Bamdogo aliendelea kunilazimisha kuolewa na Maiko ndipo nilipoamua kufanya nilichodhamiria, nikapanda gari na kutoroka kwenda Dar kwa Jumanne.

Tukiwa njiani, akapanda mdada aliyekaa jirani na mimi, alijitambulisha kwangu kwa jina la Pamela.

Tukajikuta tukipiga stori nyingi sana na kuzoeana gafla hadi tunafika Dar es salaam.

Kwa bahati nzuri, alipokuja Jumanne kunipokea sababu nilimpa taarifa tukajikuta na yule mdada tukienda nae mtaa mmoja.


Niliishi na Jumanne kama mke na mume, baada ya muda tukapanga safari na kwenda Mwanza kwa shangazi, nilipomuelezea shangazi hakupinga bali alitupa baraka zote na taratibu za posa zikafanyika hapo nyumbani kwa shangazi.

Mimi na Jumanne tulirudi Dar na kuishi kwa amani sasa kwani tulishatambulika kwa ndugu zetu.


Nikapata ujauzito, mtu pekee na rafiki wa karibu alikuwa ni Pamela. Alionekana kunisaidia kwa mambo mengi sana kipindi changu chote cha ujauzito hadi kujifungua.

Nilipojifungua, mume wangu alifurahi sana na nilijifungua mtoto mzuri wa kike aliyeitwa Jasmine.

Bibi yake na Jumanne alifurahi sana kumuona Jasmine na akasema amekuwa hai muda wote akingoja kumuona mjukuu atakayefanana nae, na Jasmine alifanana kweli na bibi huyo.

Jumanne alimpenda sana mtoto wetu.

Siku chache baada ya kujifungua niliona tabia ya Jumanne imebadilika, nilihisi huenda ana mwanamke mwingine nje.


Siku chache baada ya kujifungua, niliona tabia ya Jumanne imebadilika. Nilihisi huenda ana mwanamke mwingine nje.

Nikajaribu kumshirikisha swala hili rafiki yangu Pamela ili anisaidie kwa mawazo, akaniambia kuwa ni kawaida ya wanaume kuwa kama alivyo Jumanne kwa wengi huwa wanachukizwa na harufu za watoto wakiwa bado wachanga.

Nikashindwa kuelewa kuwa inakuwaje Jumanne achukizwe na harufu ya mtoto wetu? Sikuona harufu mbaya kwa mtoto kusema hadi yeye achukizwe na kubadilika kitabia.

Ilikuwa tofauti na nilivyozoea, Jumanne alikuwa anarudi usiku sana na mara nyingine analala huko huko bila taarifa yoyote ile.


Kukikucha, Pamela anakuja nyumbani kwangu tunaongea mengi na kufanya vingi pamoja. Jioni anaondoka, hata kama siku hiyo Jumanne kawahi kurudi ila anapoondoka Pamela nae alikuwa anaondoka na kutokomea huko huko.

Kwakweli sikumfikiria vibaya Pamela, nilimuamini sana kwani alikuwa mtu wa karibu yangu akinisaidia mambo mbali mbali, nilimuelezea yote yaliyonisibu, naye alikuwa mstari wa mbele kunifariji na kunibembeleza.


Mtoto wangu aliendelea kukua na kuzidi kupendwa na watu wengi, kwani alikuwa ni mtoto mzuri na anayependa kucheka muda wote. Kila mtu alimpenda Jasmine.

Mara nyingi Pamela alifika nyumbani kwangu ili tu amuone Jasmine wangu, ila bado tabia ya Jumanne ilizidi kunishangaza, nilishindwa hata kuelewa ni shetani gani aliyemkumba na kuchukua upendo wote aliokuwa akinipenda.


Baada ya miezi kadhaa nilimuona Pamela akibadilika, na kwavile hata mimi nilishawahi kuwa mjamzito nikaweza kugundua mapema kuwa naye ni mjamzito ila nilipomuuliza alipinga kuwa hana ujauzito.

Siku zikapita na hali yake ikazidi kubadilika, sasa ilionyesha wazi kuwa ni mjamzito, nikamuuliza tena ila hakunijibu chochote aliniaga na kuondoka na hakurudi kwangu tena, nikaja kusikia habari kwa majirani kuwa Pamela amesafiri yuko Morogoro na anaishi huko kwa sasa.

Nikashangaa sana kuwa kwanini ameondoka bila hata ya kuniaga, nikahisi labda hakutaka nijue kama anasafiri au basi alisahau kuaga.


Maisha yaliendelea hivyo hivyo nikiwa na mwanangu Jasmine, baada ya miezi mitatu Jumanne akaniaga kuwa anasafiri anaenda Morogoro kikazi, nikamuomba twende wote na mtoto wetu ila aligoma.

Lakini nilishukuru kwa kuagwa maana mara nyingine huondoka bila ya kutoa taarifa yoyote ile.


Hakukuwa na mawasiliano kati yangu mimi na Jumanne, kwani sikuwa na simu ya kuweza kuwasiliana nae chochote. Nilingoja barua zake au apige simu kwa jirani ila haikuwa hivyo, Jumanne alikuwa kimya kabisa kama vile hajaacha mtu nyumbani.


Mwanangu Jasmine, alipenda sana kubebwa na pia aliwahi kuongea na kutembea.

Ikitokea jirani amwambie Jasmine njoo nikubebe mgongoni, mwanangu hakusita bali alienda na kubebwa hadi pale mtaani wakamtunga jina na kumuita "cha mgongo" kwavile alikuwa anapenda sana kubebwa mgongoni.

Wengi walimpenda Jasmine kwa utundu wake na uzuri wake.


Siku moja nikiwa ndani napika, mwanangu Jasmine akiwa na umri wa mwaka mmoja na nusu alitembea toka pale jikoni hadi nje, nikajua mwanangu yupo kucheza na wenzie pale upenuni kwani pale kulikuwa na watoto wengine na wote walipenda kucheza na mwanangu Jasmine. Kwavile mwanangu alikuwa mtundu, alipotoka nje niliona afadhari ili nipike haraka haraka nikamchukue na kumpa maziwa.http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

Na kweli nilipika haraka haraka, nilipotoka nje kwenda kumchukua mwanangu sikumuona, ikabidi niwaulize watu wa pale kuwa mwanangu kaenda wapi, mtoto mmoja wa miaka saba akanijibu kuwa Jasmine amechukuliwa na Vero mtoto wa mama mwenye nyumba kasema anaenda nae dukani.

Nikajikuta roho ikiniuma gafla na kujiuliza kwanini hakuja kuchukua ruhusa kwangu mwenye mtoto.

Nikamfata mama Vero na kumwambia kuwa tabia ya mwanae Vero kumchukua mwanangu Jasmine bila taarifa yoyote sijaipenda. Mama yake akasema kuwa akirudi atamsema Vero.


Muda ulipita bila ya Vero kurudi na mwanangu, hofu ikanitanda na uoga kunishika kuwa Vero atakuwa wapi na mwanangu maana kama ni dukani wangekuwa wamesharudi.

Ikabidi niende maduka ya karibu kuwatizama ila sikuona dalili yoyote ya uwepo wa Vero, nikamfata tena mama Vero kumwambia kuwa Vero hajarudi na mwanangu hadi muda huo.

Mama yake nae akashangaa kuwa Vero atakuwa amepitia wapi hadi hajarudi kumrudisha mtoto ila akanipa matumaini kuwa Vero atarudi tu huku akifoka kuwa akirudi atamsema sana kwa kuchukua mtoto bila taarifa na kutokomea nae.


Kufika jioni ndio tunamuona Vero akirudi tena peke yake bila ya mwanangu Jasmine. Kwakweli nilipatwa na mshtuko sana, ikabidi tumuulize Vero amemuacha wapi mtoto akawa anakataa kuwa hajaondoka na mtoto wakati watu wengi walimuona akiondoka nae, tulimuuliza sana ila akagoma kusema kwakweli sikuweza kuvumilia.

Nilienda moja kwa moja kituo cha polisi na kuwaeleza kila kitu kuhusu upotevu wa mwanangu, nilihisi kuchanganyikiwa kabisa.

Polisi walifika pale tunapoishi na kumkamata Vero ili akaonyeshe mahali alipompeleka Jasmine.

Mwanzoni alikuwa anagoma ila polisi wakampiga sana na mwisho wa siku akakubali kutupeleka.


Jamani hili swala ulisikie kwa mwenzio tu, usiombe likutokee maishani mwako.

Vero alitupeleka katikati ya migomba, mwili wa mtoto mdogo ulikuwa umelala chini hauna ngozi. Mwanangu Jasmine alichunwa ngozi, ooh mwanangu mimi sijui aliliaje jamani sijui alihangaika vipi mtoto mdogo kama yule tena malaika wa Mungu, sijui alilia kilio gani mwanangu Jasmine.

Kumchunguza vizuri alikuwa amekatwa sehemu za siri, ni ukatili gani huu jamani kwa mtoto mdogo kama Jasmine. Sijui mwanangu aliwakosea nini hadi wakamfanya vile walivyomfanya.

Uchungu nilioupata hauelezeki, ni uchungu wa milele. Kila nikikumbuka mwili wa mwanangu Jasmine machozi hunitoka, najihisi kulia muda wote sijui mwanangu aliwakosea nini. (Deborah aliinama na kulia kwa muda, Patrick akasogea na kumbembeleza mama yake. Kisha akaendelea kusimulia mkasa mzima)


Sikuwa na ndugu Dar es salaam, Jumanne nae hakuwepo. Rafiki wa karibu niliyemtegemea hakuwepo, nani wa kunifariji Deborah nani wa kunifuta machozi muda huo. Nilikuwa na maumivu makubwa sana.

Mwili wa mwanangu ulipelekwa hospitali kwa uchunguzi kisha tukarudishiwa kwenda kuzika, majirani walinisaidia sana ila sikuona umuhimu wao, nilichotaka ni mwanangu Jasmine tu.

Walinisaidia na kufanikisha maziko ya mwanangu Jasmine, kilichoendelea hapo ni maumivu, uchungu na kilio nilitamani ardhi ipasuke na kunimeza kabisa ili nisiwepo katika uso wa nchi.

Vero alishikiliwa na polisi kwa uchunguzi ambapo alisema kuwa kuna vijana walimpa pesa na kutaka kupelekewa mtoto ila hao vijana hawakujulikana ni wakina nani.


Ulipita mwezi mzima bila Jumanne kurudi na mimi niliendelea na maumivu yangu.

Vero nae aliachiwa na polisi kwa kigezo kuwa wamempima na kumuona kuwa hana akili nzuri yani akili yake inakuja na kupotea. Roho iliniuma sana kumuona aliyehusika na kifo cha mwanangu akidundika mtaani.

Siku aliyorudi Jumanne jambo la kwanza ilikuwa ni kumuulizia Jasmine kuwa yuko wapi.

Nilitokwa na machozi tu bila ya kuwa na maelezo ya kuhusu Jasmine. Majirani walimuita Jumanne na kumueleza ilivyokuwa.

Jumanne aliporudi ndani nilijua atakuja kunifariji na kuomboleza wote, ila alikuja kwa maneno makali sana tena kwa kufoka.

"wewe mwanamke ni mpumbavu sana, huna akili kabisa wewe. Umemuachia mwanangu mpaka kauwawa? Hujui kulea kabisa wewe. Na kwa kiburi chako ukamzika mwanangu bila ruhusa yangu! Sijapata kuona mwanamke mpumbavu kama wewe. Kwakweli najilaumu na kujuta sana kwa uamuzi wangu wa kuishi na mwanamke mpumbavu kama wewe. Itabidi nianze kujifikiria upya kuoa mwingine"

Muda wote nilikuwa nalia tu mule chumbani.

Jumanne hakutaka hata kunisogelea, akaniambia kuwa anaondoka tena na hatarajii kurudi wala nini, alichoniomba ni kufungasha vyangu na kuondoka ili atakaporudi asinikute.


Roho iliniuma sana pale Jumanne alipoondoka kweli, nikaamua kufanya kitu cha kijasiri, kulipa kisasi japo kidogo tu.

Nikatoka nje na kumuita Vero kwa upendo kabisa huku nikimchekea kuwa kuna kitu nataka anisaidie ndani na bahati nzuri pale nje hapakuwa na mtu yeyote zaidi yake.

Alipokuja sikumlazia damu, nilimponda kichwani na kitu kizito akaanguka chini na kupoteza fahamu, kisha nikachukua upanga na kukata miguu yake kwani ile ndio iliyomtembeza kumpeleka mwanangu kuuwawa, sikujali kusema hana akili nzuri wala nini.

Baada ya hapo nikajiandaa kutoka sasa kwaajili ya kutoroka.


Baada ya hapo nikajiandaa kutoka sasa kwaajili ya kutoroka.

Nilichukua mkoba wangu uliokuwa na baadhi ya nguo na vitenge kisha nikaubeba, nikachungulia nje bado niliona kupo kimya, nikatumia mwanya huo kutoka na kuondoka.

Nakumbuka njiani nilikutana na mama Vero akiwa anarudi nyumbani, alinishangaa kwa zile harakati nilizokuwa nazo, akaniuliza "vipi unasafiri?"

Nilimjibu hapana naenda kumpelekea nguo rafiki yangu mmoja hivi, akauliza tena kuwa mbona naenda usiku, nikamjibu kwavile mchana huwa yupo kazini.

Nikaenda hadi kituoni na kupanda daladala ila kiukweli sikujua pa kuelekea ila nilitaka kujificha kwani nilijua kwamba wakijua tu kuwa nimemkata mtu miguu lazima nitafunguliwa kesi bila kujali maumivu yangu na mimi juu ya mwanangu.

Sikuwa na pesa ya kuweza kufika Mwanza, kwakweli sikujua cha kufanya.


Kufika njiani na lile daladala nikashuka, yani nilikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa, sina pa kuelekea, sina ndugu Dar es salaam na hakuna wa kunisaidia.

Nikawa natembea bila ya kuelewa ninakoelekea, nikaona bonde, nikadhani itakuwa vyema nikienda kupumzika pale bondeni.

Kulikuwa na mti wa mwembe pale karibu na bonde, nilienda na kukaa chini ya ule mti kama vile najikinga jua wakati ulikuwa ni usiku.

Wakati nimekaa pale chini ya mti nikiwa na mawazo yangu ya pa kwenda, mara gafla nikasikia sauti ya mtoto akilia, nilidhani ni mawenge yangu juu ya Jasmine ila kadri nilivyokaa ndivyo sauti ya kitoto ilivyozidi.


Nikainuka na kuangaza huku na kule kuwa labda kuna mtu anapita na mtoto, ila eneo lile halikuwa na njia wala nini.

Ikabidi niangalie ni wapi sauti inatokea, wakati natafuta tafuta nikaona kitoto kidogo sana kimetupwa, kilikuwa kidogo kweli kimeviringishwa kwenye khanga.

Roro ya uchungu ikanishika, nikamuinua yule mtoto, nikachukua baadhi ya vitenge vyangu kumkinga na baridi. Alikuwa mdogo sana, nadhani alitoka kuzaliwa na mama yake kuamua kumtupa labda sababu ya ugumu wa maisha.

Nikakaa nae chini, alikuwa bado analia nikajua kuwa ana njaa pia.

Nikachukua ziwa langu ambalo bado lilikuwa linaendelea kutoa maziwa kwani Jasmine alikufa wakati bado sijamuachisha kunyonya. Nilipokamua chuchu yangu na kuona inatoa maziwa, nikamnyonyesha mtoto yule.

Alinyonya na kutulia, nikanyanyuka pale chini na kuendelea na safari, na sasa nilikuwa naenda kituo cha mabasi ya mikoani ili nikaombe japo msaada wa safari.


Nilikuwa naomba msaada kwa mtu yeyote aliyembele yangu huku nikimwambia kuwa nimetelekezwa na mume na kuachiwa mtoto mchanga yule niliyembeba.

Wengi walinionea huruma na kunipa pole za mdomo tu, ndipo nikakutana na huyu mzee mmoja hivi aliyejitambulisha kwangu kwa jina moja la Patrick.

Nikamuelezea tatizo langu, akanihurumia sana, akaniambia nisijari atanisaidia nifike niendako kwakuwa nilimwambia nataka kurudi kwetu Mwanza kutokana na kutelekezwa huko na mume.

Mzee huyo aliniambia kuwa kesho yake mapema yeye na familia yake wanasafiri wanaenda Sindida kwa usafiri binafsi kwahiyo nitasafiri nao kisha atanisafirisha kwenda Mwanza.

Akanipakia kwenye gari yake na kwenda nae kwake maeneo ya kimara.

Usiku kucha sikulala maana mtoto alikuwa ananisumbua sana, muda mwingi nilikuwa nambembeleza kwa kuhofia kuwakera walioko mule ndani ya ile nyumba.


Alfajiri na mapema safari ikaanza, na tulifika Singida usiku kutokana na ubovu wa barabara kipindi hiko.

Yule mzee alinitafutia nyumba ya kulala wageni na nikalala humo na mwanangu kwani yule mtoto alishakuwa mwanangu kwasasa, sikutaka kumpoteza kabisa, sikutaka atoke mikononi mwangu na kama kufa basi nilikuwa tayari afie mikononi mwangu ila namshukuru Mungu, yule mtoto alikuwa ni mkakamavu licha ya misukosuko ila bado alihimili vishindo vya dunia.


Asubuhi na mapema, yule mzee alikuja kunifata na kwenda kunipakia magari yaendayo Mwanza, kisha akanipa pesa kiasi ya kunisaidia nilimshukuru sana kwani si rahisi mtu kukusaidia hivyo wakati hakufahamu.

Safari ya kwenda Mwanza ikaanza, mawazo yangu ni vile ambavyo shangazi atanipokea, sikujua atanichukulia kwa njia gani ila nilienda tu.


Tuliingia Mwanza kwenye mida ya saa moja usiku napo ni kutokana na barabara mbona na kuharibika haribika kwa gari nililopanda na mvua iliyonyesha siku hiyo.

Nilienda moja kwa moja hadi nyumbani kwa shangazi, nikiwa mlangoni kabla sijaingia ndani nilimsikia shangazi akizungumza.

"watoto wa kuokota sio watoto kabisa, mtoto akishatupwa na wazazi wake ujue ana laana hafai kabisa. Kwakweli mimi mtu yeyote akileta mtoto wa kuokota humu ndani, nitaenda kumtupa jamani. Sitaki kabisa watoto wa kuokota"

Kwanza kabisa nilishtuka na kujiuliza shangazi amejuaje, ila sikuelewa mazungumzo yao yalihusu nini hadi shangazi kusema vile ila nikajipa moyo na kusema kuwa lazima niendelee na ileile stori ya kutelekezwa ili shangazi amuhurumie mwanangu.


Nikaingia ndani, wote wakashangaa kuniona kwani hakuna aliyetarajia kuniona kwa wakati ule.

Shangazi akauliza kwa hamaki,

"mbona gafla jamani!! Kwema huko kweli?"

Nilikuwa nalia tu, nikamwambia shangazi kuwa Jumanne kanifukuza na kunitelekeza na mtoto yule, nilijua shangazi atanielewa ila shangazi hakunielewa na hakutaka kunielewa kabisa.

"Kwa mila za kwetu, kijana anapochoka kuishi na binti inabidi aje yeye mwenyewe kukukabidhi kwetu. Kingine nimekuozesha bila mtoto halafu wewe unanirudia na mtoto kwa misingi ipi?? Haiwezekani kabisa na siwezi kukupokea, bora hata ungekuwa peke yako ila na mtoto hapana. Itabidi tu urudi kwa mumeo, leo utalala hapa ila kesho sitaki kukuona. Rudi tu kwa mumeo."

Nililia sana, nilimkumbuka baba na mama. Kweli mzazi ni mzazi, sidhani kama wazazi wangu wangekataa kunipokea kiasi kile.

Sikuwa na raha kabisa, niliwaza tu niende wapi na yule mtoto.

Wazo likanijia kuwa niende Arusha kwa bamdogo, nikamuombe msamaha labda atanipokea.


Kesho yake, nikaondoka nyumbani kwa shangazi walijua narudi Dar ila nilienda Arusha kwa bamdogo.

Mwili wangu ulikuwa unanuka sana, sikuwahi kuoga tena toka nitoke Dar kwa kuhofia kumuacha mtoto chini na kupatwa matatizo.


Kufika Arusha nyumbani kwa bamdogo, huko ndio ilikuwa balaa zaidi. Bamdogo hakutaka hata kuniona, akanifukuza kama mbwa huku akisema nitakula jeuri yangu. Bamdogo aliongea mengi sana kuwa alinikataza kuolewa na Jumanne ila kiburi changu kimeniponza.

Nilikaa nje ya nyumba ya bamdogo, chini ya ule mti ambao Jumanne alisimama kwa mara ya kwanza aliponifata Arusha kwa bamdogo.

Nilikumbuka mengi sana na kulia sana, nilijiuliza maswali mengi kuwa upendo ule wa Jumanne alionipenda Mwanzo uko wapi, maana aliniacha kabisa, hakunitaka tena wala kunitamani. Nililia sana wala sikufikiria kama Jumanne aliyenipenda kiasi kile angenitenda vile.

Mara akaja mtu na kunishika bega, kumuangalia alikuwa ni Maiko.

Akanishika mkono, akanipakiza kwenye gari yake na kunipeleka nyumbani kwake.


Kufika kwake, akaniambia nisijari. Atanilea, atanitunza mimi na mwanangu nisiwe na shaka yoyote.

Nilifurahi sana kupata msaada ila sikujua kitu kimoja, kumbe Maiko alikuwa na mpango wake kabambe juu ya yule mtoto.



Kumbe Maiko alikuwa na mipango yake iliyojificha juu ya mtoto.

Sikujua mipango yake mwanzoni, mi niliendelea kulea na kumuhudumia mwanangu.

Kuna kipindi Maiko alikuwa anasafiri safiri ila kitu kilichonishangaza nyumbani kwa Maiko kwani kuna chumba kimoja ambacho huwa anaingia na kutoka yeye mwenyewe.

Hakuna aliyeruhusiwa kuingia kwenye kile chumba zaidi ya yeye mwenyewe. Nilihisi labda hutunza baadhi ya mali zake humo ndomana hapendi watu waingie ingie.

Sikujua kazi rasmi ya Maiko, ila badae nikagundua kuwa anafanya kazi za magendo.

Maiko alikuwa akimtamani sana yule mtoto na kunitamkia wazi wazi kuwa anamtamani, sikujua anamtamani kwa lipi ila aliniambia.

"mtoto huyu asingekuwa shupavu ungesikia mengine hapa, ila nadhani atanifaa sana kwenye biashara zangu huyu"

Kumuelewa moja kwa moja ilikuwa ngumu kuwa alikuwa na mipango gani hadi kusema kuwa ningesikia mengine.


Mwanzoni nilipoamua kumuhoji kuwa anafanya kazi gani, aliniuliza.

"kwani hapa huli, hunywi, huvai?"

Nilibakia kumuangalia tu kwani alikuwa ni mtu wa ajabu kupita maelezo.

Huku nikijisemea kuwa naishi na mtu nisiyejua kazi yake, kumbe alikuwa anangoja mtoto akue kidogo ili mimi na mwanangu tuingie humo kwenye kazi yake hiyo haramu.


Mtoto alipofikisha mwaka mmoja, ndipo aliponiambia kuwa mimi nahitajika kusafiri ili kufata mzigo wa biashara, sikujua ni mzigo gani na sikuweza kukataa kwani niliishi kwake na kula kwake.

Nikamuomba niwe nasafiri na mtoto, mwanzoni alikataa ila badae akakubali.

Sikupenda kufanya safari ya mbali na kumuacha mwanangu nyuma, mwanangu niliyeamua kumpa jina la Patrick kutokana na mzee Patrick kunisaidia na kunifadhili. Nilipenda Patrick nae akiwa mkubwa awe na moyo wa kusaidia watu kama huyo mzee.


Nilianza kusafiri rasmi kwaajili ya biashara hiyo, kumbe biashara yenyewe ilikuwa ni ya madawa ya kulevya ambapo nilitakiwa kumeza, kisha nikirudi nayatoa kwa njia ya haja.

Nilikataa kazi hiyo ila Maiko akanitisha na kuniambia kuwa siwezi kukataa wakati washanifikisha eneo la tukio na sina pa kwenda kwani popote nitakapoenda atakuwa ananifatilia.

Nikakubali na kufanya hiyo kazi ya kubeba madawa tumboni mwangu.

Nikawa mtumwa wa Maiko tayari ukizingatia sina pa kwenda na mwanangu.


Kuna kipindi alikuwa anapenda kutembea sana na mtoto hadi nikapatwa na wasiwasi, kumbe alikuwa akifanya nae ile ile biashara, alimuweka madawa ya kulevya sehemu za siri kisha kuzunguka nae na kuyasambaza kwa wenzie.

Alikuwa anambebesha mzigo mkubwa sana, usipojua unaweza ukahisi kuwa labda mtoto amevishwa nepi ila haikuwa hivyo.

Maiko ni mwanaume katili sana, alikuwa anajua mtoto hana simile na kukojoa alichokuwa akikifanya ni kumfunga solotepu pale pa kutolea haja ndogo kisha kumbebesha madawa yake hayo.

Nilipomuhoji akanieleza ukweli, niliumia sana na kujaribu kumkataza ila hakutaka kunisikiliza.

Hii siri ya kumbebesha mtoto madawa ni mimi tu niliyekuwa naijua, moyo wangu uliumia sana kwa yale mateso ambayo Maiko alimpa mwanangu, yani mzigo wake ukitua tu basi mwanangu atakoma katika usambazaji.


Mtoto huyu sikumzaa ila aliniuma hakuna maelezo, nikamwambia na kumuomba Maiko aache kumtesa mwanangu ila napo alikataa.

Ikabidi nimuombe kuwa yale madawa anayombebesha mwanangu basi niwe nayabeba mimi mwenyewe na kuyasambaza, akaniambia kuwa mimi wanaweza wakanigundua, ikabidi tutafute njia mbadala.

Kwavile mwanangu alikuwa akimbebesha sehemu za siri basi nilimuomba mimi niyabebe kwenye matiti yangu, tukajaribu kufanya hivyo na kufanikiwa kuyasambaza kwani hakuna aliyejua kama kwenye matiti zangu zaidi ya sidiria kuna kingine nilikuwa nabeba.

Ila Maiko hakupenda mimi kumzuia mtoto kubeba yale madawa pia, ila nilimuomba tungoje akue.

Akasema wakati tukingoja akue itabidi mimi nibebe mzigo mkubwa zaidi tumboni wakati wa kusafirisha kwani mtoto nae angehusika ila kwavile nilimkatalia itabidi nibebe mimi mwenyewe.


Mzigo wa madawa niliokuwa naubeba ulikuwa mkubwa sana, haikuwezekana tena kutoa kwa njia ya haja bali walikuwa wakinifanyia operesheni ndogo kuyatoa.

Tumbo langu liliharibika sana kwa ile biashara, nilitamani kutoroka ila je nikitoroka nitaenda wapi? Sikuwa na pa kwenda ndio kitu pekee kilichonikalisha nyumbani kwa Maiko kwani nilijua kuwa shangazi hawezi kunikubali na mtoto hata iweje.

Niliendelea kupata mateso tu pale nyumbani kwa Maiko huku nikiyavumilia kwa kungoja mwanangu akue kidogo hata nitakapoamua kufanya nae maisha ya kuzurula mitaani iwe rahisi.


Ukiacha biashara ya madawa, Maiko alikuwa akifanya biashara nyingine ambayo kwa kipindi hiko sikuijua.

Mimi niliendelea tu kuwa kontena la madawa ya kulevya hata mwili nao ukawa umeshazoea ile hali.


Nilifanya ile biashara kwa muda mrefu sana.

Kuna kipindi Maiko alitoka kidogo na kusahau funguo wa kile chumba chake, nikaenda kufungua na kuangalia.

Nilichokiona kiliniumiza sana, viungo vya binadamu wakubwa kwa watoto, ngozi, sehemu za siri huku vichwa baadhi vya watu alikuwa ameviweka kwenye friji, niliogopa sana nilijiuliza huyu Maiko ni mtu wa aina gani.

Uchungu ulinishika pale nilipoona ngozi za watoto wadogo, moja kwa moja nilimuhusisha Maiko na kifo cha mwanangu, machozi yalinitoka sana ila bado sikupata tafsiri ya Maiko kuwa ni binadamu wa aina gani, kukaa na viungo vya watu ndani tena bila uoga wa aina yoyote ile.

Nilipotoka mule ndani akili yangu ilivurugika sana ila nikasema kuwa sitakubali hadi pale nitakapoondoka kwenye ile nyumba, nilitamani kulipa kisasi kwa Maiko ila sikujua nitaanzia wapi.


Maiko aliporudi alihisi kuwa kuna kitu nimegundua, nikakataa na kumwambia sijui chochote.

Akanipiga sana ili nimwambie ukweli, nimweleze kile nilichogundua kuhusu yeye ila bado nilikataa kwani nilijua kusema kwangu ukweli ndio kujiandalia kuuwawa na Maiko.

Baada ya kile kipigo nikaamua kubeba mwanangu na kutoroka ila Maiko alinitafuta hadi kunipata kisha mi na mwanangu akaturudisha nyumbani kwake.

Akanipiga tena sana zaidi ya pale mwanzo huku akinipa onyo kuwa nisithubutu kutoroka kwani nitakapofanya hivyo tena ataniua.


Mimi na mwanangu tukawa watumwa wa Maiko, alitutesa sana na kutuonea. Kosa dogo nilikuwa napewa kipigo cha haja huku akisema kuwa ananilipizia kwa kumkataa mwanzoni wakati ananitongoza.

Nakumbuka siku nyingine niliyojaribu kutoroka, Maiko aliponikamata akanifunga mikono na miguu kisa akachukua kisu na kukiweka kwenye moto, kikishika moto vya kutosha akawa ananibandika nacho mwilini, maumivu niliyokuwa nayapata kwakweli hayasimuliki.

Nilijuta kuzaliwa, nilijuta kumfahamu Maiko haswa nikikumbuka kifo cha mwanangu na yeye ndiye msababishaji kwani alikuwa anauza viungo vya binadamu.

Alimchukua Patrick mwanangu na kumfunga kwenye mti, kichwa chini miguu juu.

Mtoto alilia sana na mimi niliumia sana ila Maiko hakuwa mwanaume mwenye huruma hata kidogo, yeye ni ukatili tu na ukatili na yeye.


Baada ya adhabu hiyo, akanihakikishia wazi kuwa nikijaribu tena kutoroka basi kifo kinaniita tena akasema kuwa ataniua taratibu kwa kunichinja, ikabidi niwe mpole nifanye vile anavyotaka yeye.

Nilikuwa kama mke kwenye nyumba yenye mume gaidi, alinilazimisha kufanya kile anachotaka yeye hapakuwa na ladha ya mapenzi bali ni mateso tupu.

Kila alipotaka mapenzi ilikuwa ni lazima anipige kwanza, mwili wangu ulikuwa kama ngoma huku tumbo likiwa kontena la madawa ila nikajisemea kuwa yote mapito, niliamini ipo siku Mungu atasikia kilio changu na kunitoa kwenye mikono ya Maiko.


Nilifanya kila anachotaka kufanya, mengine hayaelezeki. Kwakweli Maiko alinitesa sana.

Ndipo safari hii niliondoka na huyo wa kuitwa Mashaka ili nikabebe mzigo mwingine, kufika huko nae akanibaki na kunifanya vibaya vibaya kisha kuniwekea ule mzigo nirudi nao Tanzania.

Nikiwa na mwanangu pembeni huku tumeongozana na mlinzi ambaye Maiko alitupa ili tusiweze kutoroka. Nilisema sasa inatosha.

Niliamua kufanya kitu kingine cha khatari katika maisha yangu.


Niliamua kufanya kitu kingine cha khatari katika maisha yangu.

Nacho ni kumuwinda yule kijana ambaye hakuacha hata tupumue na mwanangu, alitufata kila sehemu kitu ambacho kilinikera sana kwani yeye ndio alikuwa ni kikwazo kwangu katika kutoroka nyumbani kwa Maiko.

Madawa ambayo niliyabeba safari hii yalikuwa ni mengi sana kupita kawaida, na mara nyingi Maiko huwa na wateja wake wa kutosha kwani yeye alikuwa ni msambazaji mzuri sana wa hayo madawa hapa nchini.

Yule kijana kama kawaida alitufata huku na kule na nikajua wazi nikitoroka tu lazima itakuwa ishu kubwa na kama nikingoja hadi nirudi nyumbani kwa Maiko basi sitaweza kutoroka wakati nilishachoka na mateso ya Maiko, mi mwenyewe nilionekana kama vile mjamzito kwa yale madawa yalivyonielemea.

Baada ya kushuka uwanja wa ndege, alikuja kijana mwingine wa Maiko na gari kutupokea.

Kwakweli hawa vijana walinichefua sana, kwani sikuweza fanya chochote sababu yao.


Tukiwa kwenye gari dogo tunaelekea kwa Maiko, nilimuomba kwa hali yote yule kijana asimamishe gari niweze kujisaidia haja ndogo ambayo ilinishika vilivyo, mwanzoni alikataa katakata na kusema kuwa nitajisaidia nikifika kwa Maiko. Hadi nikaanza kutoa machozi kwa kuwaomba na badae akakubali, tukamuacha dereva kwenye gari na mwanangu halafu mimi na yule kijana tukashuka.

Nilifika mahali na kuona jiwe kubwa kiasi chini, nikachuchumaa hapo kujisaidia wazo la gafla likanijia kuwa nimponde yule kijana na lile jiwe, hata sikujifikiria mara mbili kwakweli. Nikafanya tukio la haraka sana, nikanyanyua jiwe na kumponda nalo yule kaka kichwani ambaye alikuwa anangoja nijisaidie, na hata yeye hakutarajia kwahiyo hakujiandaa kwa chochote kile, alianguka chini kama mzigo.

Nikamfata na kumpapasa mifukoni, kisha nikachukua pesa kidogo aliyokuwa nayo na bastola yake.


Nikawa kama jambazi wa kike sasa, nikarudi kwenye gari alipo mwanangu na dereva ambaye ni kibaraka wa Maiko.

Huyu naye alinikera sana kwani mara zote nilizotoroka yeye ndiye aliyehusika kunikamata na kunirudisha mikononi mwa Maiko, nikajikuta nikimchukia sana na huyu.

Nilipofika nilipanda kwenye gari, akageuka na kuniangalia kisha akauliza yule mwingine yuko wapi, hapa sikuchelewesha hata wakati, nikamnyooshea ile bastora kwa haraka sana na kumfyatua nayo, sikutaka hata aseme kitu.

Kisha mimi na mwanangu aliyekuwa na miaka mitano kipindi hiko tukasaidiana kumtoa kwenye gari yule dereva kisha nikapanda mimi na kuanza kuendesha kwani nilijifunza kuendesha gari nikiwa nyumbani kwa mjomba.


Safari ilikuwa moja kwa moja kwa daktari aliyependa kutumiwa na Maiko katika kunifanyia operesheni ndogo ya kutoa madawa tumboni.

Nilipofika nilimwambia kuwa nimetumwa na Maiko, hakusita akaniingiza ndani na kunifanyia operesheni hiyo.

Baada ya hapo alichukua simu yake ya mezani ili kumpigia Maiko kuwa ameshamaliza kazi, ila kabla hajapiga, nilishangaa gafla mwanangu huyu mdogo akitoa bastora na kumfyatua nayo, nilimwangalia mwanangu kwa mshtuko sana na kumuuliza kwanini amefanya hivyo akanijibu.

"Tukimuacha huyu atasema halafu tutapewa adhabu kama ya kipindi kile"

Kumbe mwanangu alijiwa na kumbukumbu ya adhabu tuliyopewa kabla.

Madawa yalikuwa mengi sana, tukayaweka kwenye begi na kuondoka hapo nyumbani kwa daktari huku na yeye akiwa chini.

Najua hata Maiko hajui kama yule daktari aliuwawa na mie.


Safari iliyofata ni kwa mteja maarufu wa Maiko, nilimpelekea mzigo na kumwambia kuwa natakiwa kuondoka na pesa kabisa mahali hapo, hakuwa na pesa za kutosha kununua mzigo wote kwahiyo alinikabidhi pesa taslimu nusu na nyingine akaniandikia hundi (cheque).

Nikakubaliana nae kuwa asimueleze Maiko ili liwe dili kati yangu na yake na ukizingatia nilimpunguzia bei alifurahi sana na nikamuahidi kumpelekea mzigo mwingine.


Baada ya kutoka hapo na pesa ile ya kutosha, tulirudi uwanja wa ndege, nikakata ndege ya safari siku hiyo. Nilikuwa tayari kupanda ya kwenda kokote ili nikatulize akili kwanza.

Tulipata ndege ya kwenda Dodoma.

Mimi na mwanangu tulisafiri hadi Dodoma na baada ya siku kadhaa tukaenda kuishi Tabora yote hiyo ni kukimbia kupatikana na Maiko.


Silaha zile nilitupa na kuanza maisha mapya na mwanangu, nikaamua kumrudia Mungu wangu kabisa kwani sikutaka kukumbuka ya kale tena ila ya kale hayakuacha kutembea akilini mwangu.

Ile pesa ya madawa ili nisaidia sana mimi na mwanangu.

Nikamtumia pesa dada yangu Marium na kumuomba anijengee nyumba huku Mwanza ila nyumba iliyo mbali kidogo na maeneo ya watu. Na wakati nahamia kweli ilikuwa mbali na watu wengine ila wote hawa wamesogea hivi karibuni.


Kwa kipindi hicho nashukuru vipindi vya dini vilimsaidia sana mwanangu kutulia na kusahau yaliyopita.

Muda mwingi nilikuwa namfundisha na kumueleza ya hapa na pale, anapojaribu kuniuliza kuhusu tulipotoka nilikuwa namgelesha na kumletea habari zingine kama hadithi za sungura na fisi.


Baada ya miaka mitano ndani ya Tabora huku nikifanya biashara ndogo ndogo ili tu kuwa makini kwa kujishughulisha niliamua kurudi Mwanza kwenye nyumba niliyomuomba dada yangu anijengee, sikutaka kufanya biashara yoyote kubwa.

Biashara yangu ilikuwa ni ndogo tu, dada yangu Marium alijaribu sana kunidadisi kuwa pesa nimetoa wapi ila sikumwambia nilimgelesha tu kwani sikutaka mtu yeyote ajue maisha yangu ya nyuma na sikutaka kukumbuka maisha ya nyuma.

Nilimuomba shemeji ambaye alikuwa ni mume wa Marium anitafutie kazi, naye akanitafutia kazi ya usafi niliyokuwa nafanya.


Kuna kipindi Patrick alienda kumtembelea bibi yake yaani shangazi yangu mimi, huko waliongea mengi sana.

Patrick alivyorudi akaja na maswali na hoja zake kibao, akauliza.

"mama, eti kuna watoto wengine huwa wanaokotwa?"

Nikamuuliza anamaana gani, akaniambia yani hutupwa na wazazi wao na wengine huwaokota kuwalea. Nikajaribu kumuelimisha mwanangu ila nikasita kumwambia ukweli kuhusu yeye, na alisema.

"Bibi kaniambia kuwa watoto wanaookotwa huwa na laana. Bora mimi nina mama na wala sijaokotwa namshukuru Mungu sana. Ingawa sina baba ila mama ninae."

Halafu akaendelea kusema huku mimi nikiumizwa na ukweli halisi.

"Asante mama kwa kutokunitupa, maana kama ningeokotwa mimi mmh ningejiua yani nisiwe na wazazi kweli? Nakupenda sana mama."

Alisogea na kunikumbatia, niliumia sana moyoni nikajisemea kuwa nitaitunza siri hii siku zote za maisha yangu.


Nilimlea Patrick na kumsomesha, sikutaka tena kuolewa, sikutamani kuishi na mwanaume yeyote yule duniani kwani Patrick alikamilisha furaha yangu hadi pale alipokua mkubwa na kuanza kuulizia kuhusu baba yake mzazi.


(muda wote ambao Deborah alikuwa akielezea, Patrick, Fausta na Pamela walionekana kuwa katika majonzi makubwa sana.)

Ila nikaja kugundua kitu na kitu hiki ndio kimefanya niwaeleze kuhusu maisha yangu.

Kitu chenyewe ni cha kushangaza na kusikitisha.



Kuna kitu ambacho nimekigundua na kitu hicho ndio kilichofanya niwaeleze kila kitu kuhusu maisha yangu.


Patrick amenisumbua kwa kipindi kirefu sana kutaka kumjua baba yake akadiriki kuniambia kuwa hata kama nilibakwa nimueleze ukweli ajue kwani yeye ni kijana mkubwa sasa.

Hakujua ni ugumu gani naupata katika kumueleza ukweli.


Nakumbuka swala la Patrick kutaka kumjua baba yake lilianza baada ya kifo cha shemeji yangu yani mume wa Marium aliyeuwawa gafla kabisa na tukamzika kiwiliwili bila kichwa, nilishangaa sana siku ambayo Maiko amefika hapa kisha dadangu akamvamia, kumbe Maiko ndiye aliyemuua shemeji. Bado sijajua huyu Maiko alikuwa na maana gani kufanya kama alivyofanya.


Ingawa Patrick nilimsomesha kwa shida ila sikumnyima uhuru, nilimruhusu kufanya chochote kinachopendeza machoni mwa watu na kumpendeza Mungu.

Mwanangu alitamani sana kuanza kazi, alishachoka kukaa nyumbani na mimi ukizingatia nilikuwa simjibu swali la alipo baba yake.

Ningemjibu vipi wakati hata mama yake simjui? Ningemwambia vipi vitu vya kuumiza kiasi hiki?

Nilimvumilia sana licha ya maneno makali aliyoongea kwangu kuhusu baba yake, kweli kuna umuhimu kwa mtoto kuwajua wazazi wake, je ningemueleza kuwa hata mimi si mama yake mzazi angejisikiaje? Kwakweli nimevumilia sana, Patrick alikuwa ni msumbufu sana katika kumjua baba yake.


Patrick alipopata kazi Arusha kwanza kabisa nilimkatalia asiende kwa kuhofia kuwa angekutana na Maiko kwani Maiko ni mtu mbaya sana na niliogopa kuwa atamfundisha tabia mbaya mwanangu ila Patrick aling'ang'ania sana kuwa lazima aende kwani kazi ndio hitaji lake kwasasa.

Nilitamani mwanangu apate kazi sehemu nyingine tu ila si Arusha.

Kitu kikubwa nilichomsisitizia Patrick ni kuwa asioe bila kuja kunitambulisha huyo mwanamke kwanza, nilihofia vitu vikubwa viwili yani kukutana na familia ya Jumanne na pia kukutana na familia ya Maiko.

Sikutaka kabisa Patrick kujihusisha na familia hizi mbili kwamaana kwa upande wangu sikuhisi kama angejenga familia njema na hizi familia mbili. Ingawa si vizuri kumchagulia mtoto mchumba ila kwa Patrick kutokana na historia za nyuma nilipenda kama ataamua kuoa basi huyo mwanamke atokee Mwanza au atoke kwenye familia tutakayotambulishana kwanza.


Patrick akiwa Arusha, mwanzoni alikuwa akiwasiliana sana na mimi tena sana hadi mara nyingine niliweza kugundua kuwa kuna kitu anatamani kuniambia ila anashindwa ila mawasiliano hayakukatika mpaka siku aliyorudi tena Mwanza na gari yake mwenyewe kunisalimia.

Aliporudi tena Arusha mambo yalibadirika sana, mawasiliano yangu na Patrick yalikuwa hafifu mno.

Haikuwa kama ilivyokuwa mwanzo, kuna kitu nilikihisi kama mama. Patrick hakuwa mwanangu wa kumzaa ila kuna kitu kikubwa sana ambacho kimeniunganisha na Patrick, siku zote sikuacha kumpenda Patrick kama mwanangu naye hakuacha kunipenda kama mama yake.

Hali ile ya mawasiliano hafifu kati yetu iliniumiza sana, mara ukimpigia hapatikani mara sijui nini nilijikuta nikiwa na mawazo tu juu ya mwanangu kipindi hicho.

INAENDELEA

Post a Comment

0 Comments