Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Mwanamke jini sehemu ya kumi na moja (11)



 “Twende”

Nikatoka naye mle chumbani.
Tulishuka ngazi, akatumia mlango wa nyuma wa hoteli kunitoa. Nilikuta gari limewekwa sambamba na mlango. Nikafunguliwa mlango wa nyuma wa gari, nikajipakia bilakuambiwa.
Mzee naye aliingia katika siti ya nyuma. Kulikuwa na mtu aliyekuwa kwenye siti ya dereva ambaye sikuweza kumuona vizuri. Sikujua alikuwa nani.
Kama ningemchunguza ningeweza kumjua lakini akili yangu haikuona umuhimu wa kutaka kumjua wala kujua nilikuwa napelekwa wapi.
Gari likapigwa moto na kuondoka. Safari ikaanza. Mji ulikuwa kimya na hakukuwa na watu wowote walioonekana barabarani zaidi ya walinzi wa maduka waliokuwa wakisinzia.
Baada ya mwendo wa karibu kilometa tano nilihisi kuwa tulikuwa tumeuacha mji kwani sikuona tena majumba ya ghorofa isipokuwa nyumba ndogo ndogo.
Tulikuwa tumeingia katika maeneo ya ambayo kwa lugha ya kwetu tungeyaita ‘uswahilini’
Mwanga wa gari tulilokuwemo ulimulika mapaka yaliyokuwa yakirandaranda kutafuta vyakula vilivyotupwa kwenye mapipa ya takataka. Ingawa ilikuwa usiku maji taka yalikuwa yakitiririka kutoka kwenye majumba ya watu na kuunda vidimbwi vya maji taka kandokando ya barabara.
Wakati wote nilikuwa nashindana na akili yangu. Nilikuwa naona kichwa kizito kama niliyelemewa na usingizi, wakati huo huo sikutaka usingizi unichukue.
Kila muda nilikuwa najigutuka na kukaza macho yangu ili nisilale. Lakini mwisho wake nilizidiwa nguvu, usingizi wa moja kwa moja ukanichukua ghafla.
Hata sikuweza kujua tena lile gari lilielekea wapi.
Lakini nilipokuja kuzinduka nilijiona mimi na yule mzee tumekaa kando ya shimo lililokuwa mbele yetu. Shimo hilo lilichimbwa usawa wa kaburi kando ya mti mkubwa. Mahali tulipokuwa palikuwa ni porini.
Kulikuwa na taa ya chemli iliyokuwa inawaka pembeni mwa kaburi hilo na kufanya sehemu ile tuliyokuwa iwe na mwanga kwani eneo lote lilikuwa na kiza totoro.
Yule mzee wa kisomali aliingia kwenye lile kaburi akasimama na kuniambia.
“Ingia”
Na mimi nikaingia.
“Kaa hapo chini”
Akanionesha mahali pa kukaa, nikakaa. Nikaona analishika sikio langu la upande wa kulia na kusema maneno kwa lugha ya kisomali kama mtu aliyekuwa anasoma dua kisha akaniinamia na kukigandamiza kichwa chake kwenye komo langu.
Alinishika na kunigandamiza kwa nguvu sana mpaka nikasikia maumivu ya kichwa. Nilitaka kupiga kelele nilipomuona amerushwa na kuanguka chini. Alikuwa kama aliyerushwa na umeme.
Akainuka taratibu na kutoka kwenye lile kaburi. Kilichofuatia baada ya hapo sikukifahamu, nilishitukia tu nikiamka kitandani pale hoteli nilipokodiwa chumba na Abdi.
Nikahisi kwamba labda nilikuwa katika ndoto. Moyo ulikuwa ukinienda mbio. Nikainuka na kwenda kuutazama
mlango wa mle chumbani. Niliukuta umefungwa kwa ndani. Kitu ambacho kiliashiria kuwa hakukuwa na mtu aliyeingia humo chumbani.
Lakini ni ndoto gani ile? Nikajiuliza. Kila kitu nilikiona waziwazi kama vile kinatokea kweli.
Kama ilikuwa ndoto ilikuwa ya ajabu sana, nikajiambia.
Wakati ule nilipoamka kulikuwa kumekucha. Nikaingia maliwatoni. Nilipotoka nikavaa nguo. Nilivaa suti ile ile niliyonunuliwa na Abdi.
Nikashuka chini na kuingia mkahawani. Nilipatiwa kifungua kinywa. Wakati nakunywa chai nikamuona Abdi akiingia.
“Amour salaam alaykum” akanisalimia kwa bashasha huku akinipa mkono.
“Alayka salaam. Habari ya tangu jana?”
“Nzuri bwana, umeamkaje?”
“Nashukuru, nimeamka salama. Sijui wewe”
Na yeye akaagiza kifungua kinywa.
“Kuna sehemu nataka twende” akaniambia.
“Wapi?”
“Mogadishu ni kubwa sana. Kuna sehemu nyingi nataka kukuonesha”
“Sawa”
Tulipomaliza kunywa chai tukatoka.
“Jana nilikufuata usiku nikakuta umelala” Abdi aliniambia wakati tunatoka.
“Nililala mapema kwa sababu ya uchovu”
“Niliwambia wale wasichana wasikuamshe. Nilijua ulikuwa na uchovu mwingi”
Tulitoka nje ya hoteli tukajipakia kwenye gari. Lilikuwa ni gari la aina nyingine sio lile la jana yake.
Baada ya kujipakia tukaondoka.
“Nataka uuone mji wetu vizuri” Abdi alikuwa akinizungumzisha huku gari likiwa katika mwendo wa taratibu au wa kinyonga . Nilikuwa sijui tunakwenda wapi.
“Mji wenu ni mzuri sana. Una majumba makubwa na umejengeka sana” nikamwambia.
“Bado. Kuna maeneo mengi hujayaona”
“Inavyoonekana mmepiga hatua kubwa ya maendeleo”
“Sana”
Baada ya mwendo wa karibu nusu saa tuliingia katika maeneo ya mashamba. Nilikuwa nikijiuliza alikuwa akinipeleka shambani kwake au alitaka kunionesha kitu gani?
Tulitokea katika mtaa mmoja uliokuwa umezagaa uchafu. Tulipishana na mbuzi, kondoo na kuku wa kienyeji. Abdi alikuwa akikata kona ovyo kukwepa mashimo na vidimbwi vya maji machafu.
“Tuache gari hapa” Abdi akaniambia huku akifunga breki pembeni mwa njia. Bila shaka alishindwa kuendesha kutokana na barabara yenyewe kujaa mazagazaga.
Tulishuka tukatembea kwa miguu. Tulizipita nyumba mbili za ghorofa. Zilikuwa nyumba zilizoonekana zimeshapitwa na muda wake wa kuishi watu kwani zilichakaa sana. Huenda zilijengwa miaka mia moja iliyopita. Enzi za utawala wa kikoloni.
Tuliingia mtaa mwingine uliokuwa na tifutifu jingi. Tukapita msikiti. Tulikwenda mbele kidogo, Abdi akasimama mbele ya mlango wa nyumba moja iliyokuwa imepakwa rangi nyeupe.
Mlango wake ulikuwa umechorwa picha ya nyota na mwezi.
Abdi alibisha mlango huo. Baada ya muda kidogo mlango ukafunguliwa.
Mzee mmoja akachungulia nje. Alimtazama Abdi kisha akanitazama mimi.
“Karibuni” akatuambia na kurudi ndani.
Abdi akaingia na kuniambia.
“”Karibu”
Na mimi nikaingia. Tulitokea katika ukumbi mpana kama darasa. Harufu tuliyokutana nayo humo ndani ni ya udi na marashi.
Katikati ya ule ukumbi palitandikwa jamvi. Katika lile jamvi niliona sinia iliyotiwa vitu mbalimbali kama vile ndizi mbivu, vipande vya miwa, mkate wa mchele, tende na vitu vingine ikiwemo chupa kubwa lenye asali.
Katika kila pembe ya lile jamvi kuliwekwa nazi moja. Jumla zilikuwa nazi nne.
Yule mzee wa kisomali alikuwa amesimama nyuma ya mlango.
Alimwambia Abdi maneno kwa lugha ya kisomali. Abdi akaniambia mimi.
“Twende tukakae pale”
Alinionesha lile jamvi.
Tukaenda kukaa. Yule mzee wa kisomali alitoka uani. Baadaye akarudi tena akiwa ameshika kitabu kikubwa cha kiarabu na yeye akakaa kwenye lile jamvi.
Sasa niliweza kumuangalia vizuri. Nikajiuliza mbona amefanana na yule msomali niliyemuota akinichukua kule chumbani? Alikuwa mrefu vile vile na pua yake pia ilikuwa ndefu.
Nikashangaa sana.

Mzee huyo wa kisomali akamtazama Abdi kisha akamuuliza maneno na kwa kisomali.
Abdi akanitazama kisha akamwambia.
“Amour”
Nikahisi labda alimuuliza jina langu.
Mzee wa kisomali akanitazama kisha akafungua kitabu chake. Karasa zilikuwa zimegandana akakigusisha kidole chake kwenye ulimi kukitia mate kisha akaufungua ule ukurasa.
Akaanza kusoma maneno ya kiarabu. Sikuwezaa kujua alikuwa anasoma nini lakini nilisikia akitaja jina la Zena Binti Jabal Keysi. Wakati mwingine akitaja jina langu.
Mara kwa mara nilikuwa nikimtazama Abdi kuona kama mwenzangu alikuwa anaelewa chochote. Abdi alikuwa amenyamaza kimya. Alikuwa ametulia kama aliyekuwa anaaguliwa.
Ghafla tukaona nazi iliyokuwa katika pembe moja ya lile jamvi inapasuka yenyewe. Mzee alikuwa akiendelea kusoma tu. Naizi ya pili ikapasuka. Ilipopasuka nazi ya tatu ukuta wa uliokuwa mbele yetu ulifanya ufa akatokea mtu.
Alikuwa mwanamke aliyevaa vizuri. Gauni alilovaa lilikuwa limedariziwa vimemeta vya dhahabu. Alikuwa amevaa mkufu wa dhahabu na bangili za dhahabu. Masikioni alikuwa amevaa vipuli vya dhahabu.
Kichwani kwake nywele zake zilibanwa kwa taji la dhahabu lililomfanya aonekane kama malikia wa visiwa vya Sheba.
Alipotokea sote tulishituka tukamtazama. Ilinichukua sekunde mbili au tatu kutambua kuwa alikuwa Zena!
Zena alikuwa amependeza kuliko siku zote nilizowahi kumuona. Alikuwa aking’ara kama mwezi mpevu! Sikuweza kujua ni kitu gani kilichomleta pale na kwanini alitokea katika hali tofauti na anavyotokea siku zote.
Siku zote nilizokutana naye alinitokea katika hali ya kawaida, si hali kama ile ya kuibuka kutoka kwenye ufa wa ukuta. Ilikuwa hali ambayo si tu ilinitisha mimi, ilimtisha hata Abdi aliyekuwa ameketi karibu yangu. Nilimuona akimtazama kwa shauku iliyochanganyika na hofu.
Mzee wa Kisomali alimtazama kisha alimwambia maneno kwa lugha ya kiarabu.
Zena hakusema chochote. Akiwa miguu pekupeku alikuja taratibu hadi ilipokuwa ile sinia iliyokuwa na vitu akaipindua kwa miguu. Sinia ilipinduka, na vitu vyote vilimwagika chini.
Alipomaliza kuipindua ile sinia alimfuata yule mzee wa kisomali akampiga kibao cha shavu. Mzee alianguka chini. Hakuinuka tena. Sasa akamfuata Abdi. Abdi alipoona anafuatwa aliinuka haraka akatoka mbio. Na mimi nikainuka na kutoka mbio kumfuata Abdi.
Tulitoka kwenye mlango. Abdi kama ambaye alibadili mawazo alirudi kwenye mlango huo na kuchungulia. Na mimi nikarudi kuchungulia.
Zena hatukumuona tena. Tulimuona yule mzee akijiinua na kukaa. Abdi akarudi. Mimi sikurudi.
Nilibaki kwenye mlango nikichungulia.
Nikawasikia Abdi na yule mzee wakizungumza kwa lugha ya kisomali. Mzee alikuwa akifoka na akimuashiria Abdi aondoke.
Abdi akatoka na kuniambia.
“Twenzetu”
Wakati tunatembea kurudi tulikoliacha gari Abdi hakunieleza chochote na mimi sikumuuliza chochote.
Nilibaki kujiuliza mwenyewe ni kitu gani kilichokuwa kimetendeka pale hadi Zena akatokea na kumwaga vile vitu na kisha kumpiga kibao yule mzee? Sikupata jibu.
Nilihisi kuwa jibu alikuwa analo Abdi lakini hakuonesha dalili yoyote ya kutaka kunieleza chochote. Na mimi nikashindwa kumuuliza.
Niliona uso wake ulikuwa umefadhaika na alikosa raha. Hakuwa hata akinitazama.
Tulirudi kwenye gari lake tukajipakia na
kuondoka.
Wakati Abdi akiendesha gari kurudi mjini aliniambia.
“Nina hoteli mbili. Ile unayokaa wewe na nyingine mpya. Nataka uwe mneneja wa ile hoteli yangu mpya”
“Nitawezaje kuwa meneja wa hoteli yako wakati nataka kuondoka?” nikamuuliza.
“Huwezi kuondoka bila paspoti. Subiri nikutengezee paspoti”
“Utanitengezea lini?” nikamuuliza.
“Usiwe na haraka Amour. Ninakuhakikishi
a kuwa nitakutengezea isipokuwa katika kipindi hiki cha kusubiri paspoti yako iwe tayari nataka uwe meneja wa hoteli yangu. Nitakupa nyumba na gari na kama utahitaji mke wa kisomali nitakutafutia msichana mrembo”
Abdi alianza kunitia tamaa ya maisha na kunipa ushawishi wa kubaki Somalia.
Hata hivyo moyo wangu ulikuwa mzito kukubaliana naye. Nilikuwa simuelewi japokuwa mipango aliyonieleza ilikuwa ya maana kwa upande wangu.
“Unataka kurudi Tanga, kuna nini? Kama utakaa hapa kwa muda mfupi tu Amour unaweza kupata maendeleo makubwa na ukarudi kwenu ukiwa tajiri” Abdi aliendelea kunishawishi.
Muda wote nilikuwa nimebaki kimya nikiyatafakari maneno yake. Alipoona nipo kimya na yeye akanyamaza. Sikuweza kujua ni kwanini aliileta ile mada ya hoteli wakati kulikuwa na tukio jingine la kuibuka kwa Zena ambalo ndilo alilopaswa kunieleza.
Kwanza kile kisomo alichokuwa anasoma yule mzee hadi nazi zikapasuka na Zena akatokea, nilijiuliza, kilikuwa kiosomo cha nini. Hapo pia sikupata jibu.
Dakika chache baadaye Abdi alilisimamisha gari mbele ya nyumba moja iliyokuwa katika mtaa mtulivu.
Aliniambia tushuke, tukashuka.
“Nifuate” akaniambia.
Tuliingia katika geti la ile nyumba tukakuta mafundi wakipaka rangi kwenye kuta. Alizungumza nao kwa kiomali kisha tukaingia ndani ya ile nyumba.
Ilikuwa nyumba nzuri na ya kupendeza. Abdi alitazama sehemu zilizokuwa zimeshapigwa rangi, akaniambia.
“Hii ni nyumba yangu. Ninaifanyia ukarabati kwa ajili yako. Wewe utakuja kuishi hapa”
“Wewe mwenyewe unaishi wapi?”
“Nitakupeleka ukapaone nyumbani kwangu”
“Ni lini hii nyumba itakuwa tayari?”
“Leo watamaliza kupiga rangi. Labda keshokutwa unaweza kuhamia. Kesho nitakuwekea fanicha mpya”
Alifungua milango ya vyumba na kunionesha ndani.
“Patakufaa sana hapa” akaniambia.
Sikumjibu kitu. Nilikuwa bado ninajadiliana na moyo wangu kuhusu suala la kubaki pale Somalia.
“Amour unafikiria nini. Unataka kuiacha bahati kama hii?” Abdi aliniambia kisha akacheka peke yake.
“Twenzetu” akaniambia.
Tukatoka tena. Tulijipakia kwenye gari tukaondoka.
Breki ya kwanza ilikuwa mbele ya hoteli moja iliyokuwa katika mtaa mwingine. Ilikuwa hoteli ndogo ya ghorofa moja, Ilikuwa imeandikwa kwa herufi kubwa. AL ASAD.
“Hii ndio hoteli ambayo nitakuachia wewe, itakuwa kama mali yako kwani tutakuwa tunagawana faida kila mwezi na kila mwaka kama utapenda kuendelea kubaki Somalia” Abdi aliniambia tukiwa bado tupo kwenye gari.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipoona nilikuwa nikiiangalia angalia ile hoteli, aliniambia.
“Tushuke uione vizuri”
Tukashuka.
Tuliingia ndani ya ile hoteli. Kwa kweli ilikuwa imechangamka.
“Sasa nani anaiendesha kwa hivi sasa?” nikamuuliza.
“Yuko mtu lakini nitamuondoa”
“Sasa ni kwanini umuondoe?”
“Lengo langu ni kukunufaisha wewe rafiki yangu au nimefanya kosa?’
“Hapana. Ni vizuri”
Abdi alinitembeza hoteli nzima kisha tukaingia katika ofisi ya meneja.
Meneja mwenyewe alikuwa mtu mzima. Kichwa chake kilishaanza kutoka mvi.

Walizungumza kwa kisomali huku meneja huyo akinikodolea macho.

Walizungumza kwa karibu robo saa kisha tukatoka.

“Yule ndiye meneja aliyeko sasa” Abdi aliniambia wakati tunatoka nje ya hoteli hiyo.

“Utamuhamishia mahali pengine au unammuondoa kabisa?’ nikamuuliza.

“Nitamfikiria”

“Umeshamwambia?”

“Nilitaka kwanza nikubaliane na wewe”

“Mimi nimeshakubali”

“Una uzoevu wa kuendesha hoteli?”

“Kwa kweli sina uzoefu huo”

“Utajifundisha hapa hapa. Ninaamini hutaweza kushindwa”

“Nitajaribu”

“Kazi yako itakuwa kuongoza na kukagua. Kuna kijana ambaye amesomea uendeshaji wa hoteli yuko pale atakusaidia”

“Nafikiri nitaweza. Usiwe na wasiwasi”

Baada ya hapo hatukuzungumza tena. Mwenzngu alikuwa amenyamaza, sikujua alikuwa akiwaza nini. Mimi nilikuwa na mawazo ya kubaki Somalia kuendesha shughuli ya hoteli.

Kikubwa kilichonipa tamaa ni kuwa kazi ya umeneja wa hoteli ni ya heshima na aliniambia kuwa angenipa ile nyumba pamoja na gari. Isitoshe tungegawana mapato ya hoteli..

Nilijiambia kama ningeweza kuchuma pesa pale Somalia na kurudi kwetu nikiwa na utajiri kama alivyoniahidi Abdi, sikuona haja ya kung’ang’ania kurudi Tanga ambako sikuwa na hakika kama nisingefukuzwa kazi kutokana na kutoonekana kazini kwa kipindi kirefu bila taarifa yoyote.

Abdi akanipeleka nyumbani kwake. Ilikuwa nyumba nzuri ya ghorofa moja iliyokuwa ndani ya geti. Mlinzi wake alitufungulia geti. Gari la abdi likaingia.

Kulikuwa na banda la magari lakini Abdi alilisimamisha gari hilo mbele ya mlango wa nyumba yake ya kifahari.

Tukashuka. Abdi alikwenda kufungua mlango akaniambia.

“Karibu kaka”

Tukaingia ndani. Alikuwa na sebule ya kupendeza iliyokuwa imepambwa vizuri kwa fanicha za thamani. Wakati tunaingia kulikuwa na msichana mmoja aliyekuwa akifanya usafi kwa kutumia kufaa maalum cha kuondoa vumbi.

“Karibu ukae” Abdi aliniambia huku naye akikaa. Akaongeza.

“Jisikie uko nyumbani. Hapa ndio kwetu bwana”

Nikawa natupa macho huku na huko kuiangalia sebule.

“Asante. Nimefurahi kupafahamu nyumbani kwako”

“Utakunywa kahawa?” Abdi akaniuliza.

“Hapana”

“Tangu uje Somalia sijakuonesha nyumbani kwangu. Hii nyumba ni yangu na mimi ninaishi hapa” Abdi aliendelea kuniambia kisha akaongeza.

“Unaweza kuona nyumba iko kimya kwa sababu watoto hawapo”

“Wako wapi?”

“Shemmeji yako amekwenda kwao Kismayuu. Mama yake ni mgonjwa. Atarudi pindi mama yake akipata nafuu”

Yule msichana aliyekuwa akifanya usafi alikuwa ameshaondoka.

“Nilipomuona huyu msichana nilidhani ndiye shemeji?”

“Hapana. Yule ni mfanyakazi wangu. Kwa sasa ninaishi na wafanyakazi wangu tu”

Hatukukaa sana hapo. Abdi akainuka na kuniambia.

“Sasa acha nikurudishe kule hoteli. Nataka niende shambani kwangu. Niliambiwa baadhi ya ng’ombe wangu ni wagonjwa”

Tukatoka na kujipakia tena kwenye gari, tukaondoka.

Abdi alinirudisha hotelini akaniacha na kuondoka. Niliingia chumbani nikaketi. Mawazo ya Zena yakaanza kunijia. Sikutaka kuendelea kumuwaza mwanamke huyo wa kijini lakini mawazo yake yalinijia kwa nguvu na sikuweza kuyazuia.

Kikubwa kilichosababisha nimuwaze ni kule kujitokeza nyumbani kwa yule mzee wa kisomali na kumpiga kibao yule mzee. Mpaka muda ule tukio lile lilikuwa kama kitendawili nilichoshindwa kukitegua.

Lakini jambo moja ambalo halikuwa na shaka akilini mwangu ni kwamba Abdi na yule mzee wa kisomali walikuwa wanajua ni kwanini Zena alitokea pale.

Kama walikuwa hawajui ni lazima Abdi angeonesha mshangao wake na angenieleza kitu. Lakini hakutaka kunieleza chochote kama vile ilikuwa ni siri.

Kadhalika sikuweza kujua yule mzee alikuwa ni nani, ana uhusiano gani na Abdi na kwanini nilimuota usiku akiniingiza ndani ya kaburi?

Pia nilijiuliza kile walichokuwa wanasoma pale ni kitu gani na kwanini kuliwekwa vitu mbalimbali kama vya uganga? Kwa kweli licha ya kujiuliza mara kadhaa sikupata jibu la kuridhisha.

Kwa vile sikuweza kuelewa kitu niliona nisiumize kichwa kwa kujiuliza maswali ambayo hayakuwa na majibu. Nikayaacha mawazo yale.

Siku ile sikumuona tena Abdi hadi siku ya pili yake ambapo alikuja hoteli asubuhi kunijulia hali.

“Nyumba yako itawekewa fanicha mpya leo. Kesho utaanza kuishi kule na kesho kutwa utakwenda kuanza kazi kule hotelini. Yule meneja ataondoka leo” Abdi akaniambia.

“Sawa”

“Amour unajua kuendesha?”

“Kuendesha nini?”

“Nina maana kuendesha gari”

“Ninajua lakini sikuja na leseni yangu”

“Si tatizo. Tutakwenda studio utapiga picha kadhaa za  paspoti, baadhi yake tutazitumia kukutengezea leseni ya hapa Somalia”

“Nitaipata lini hiyo leseni?’

“Kesho tu utaweza kuipata”

“Bila mimi mwenyewe kwenda kujaribiwa?”

“Hiyo kazi niachie mimi. Hata paspoti utapata bila kwenda wewe mwenyewe”

“Lakini hiyo paspoti itakuwa ya nchi gani?”

“Wewe ulitaka ya nchi gani?”

“Ya Tanzania”

“Utaipata bila shaka yoyote. Hapa kuna mabingwa wa kugushi. Nipe wiki moja tu. Utawekewa na mihuri ya tarehe uliyoingilia hapa Somalia”

Aliponiambia hivyo nilitabasamu.

“Inaonekana wewe hushindwi na kitu hapa Somalia” nikamwambia.
CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Serikali yenyewe nimeiweka mikononi mwangu. Kuna maafisa wa polisi ambao wanakuja kuchukua mishahara kwangu kila mwezi kwa ajili ya kulinda miradi yangu. Wewe umeona mwenyewe juzi meno ya tembo tulivyoyaingiza na kuyapakia kwenye meli. Usifikiri kuwa polisi hawajui, wanajua. Baadhi ya mawaziri pia ni marafiki zangu. Likitokea tatizo niwapigia simu”

INAENDELEA

Post a Comment

0 Comments