“Ninakuamini. Mambo yako ni makubwa!”
Nilipomsifu Abdi alicheka akanipa mkono. Alionekana kuwa ni mpenda sifa.
Tuliondoka hapo Hoteli tukaenda studio kupiga picha za papo kwa papo. Alichukua picha zangu kadhaa za usawa wa paspoti.
Wakati ananirudisha hotelini, nilimwambia kuwa nilikuwa ninahitaji saa.
“Saa tu, twende dukani tukanunue” akaniambia.
Abdi akageuza gari. Tulikwenda katika duka moja la kuuza saa akaniambia nichague saa niliyokuwa nahitaji. Nikachagua saa moja. Abdi akailipia.
“Unahitaji nini tena?” akaniuliza.
“Nilikuwa nahitaji saa tu”
“Basi twenzetu”
Tukaondoka. Alisimama tena kwenye duka moja akashuka na kuniambia nimsubiri. Baada ya muda kidogo alirudi akiwa ameshika gomba lililokuwa limefungwa vichnga vya mirungi.
Akaliweka kwenye siti kisha akawasha gari tukaondoka. Alinirudisha hoteli akaniacha hapo na kuondoka.
Sikumuona tena hadi siku ya pili yake. Alikuja hotelini saa nne akaniambia nichukue vitu vyangu.
“Kule nyumba iko tayari”
“Sawa. Ngoja nitie nguo zangu kwenye begi, sina vitu vingi hapa”
Nilitia vitu vyangu kwenye begi nikalishika begin a kumwambia Abdi.
“Twenzetu”
Tukatoka. Tukiwa nje ya hoteli tulijipakia kwenye gari tukaondoka.
Tulikwenda katika ile nyumba ambayo Abdi alikuwa ameitayarisha kwa ajili yangu.
Tulipoingia ndani nilikuta ilikuwa imebadilika. Kulikuwa kumewekwa fanicha mpya. Nilikagua sebule, vyumba, hadi jiko. Kote kulikuwa kunaridhisha sana.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu ndio nilianza kuishi katika nyumba yenye hadhi kama ile. Kama ingekuwa Tanga ningeonekana mtu wa kuheshimika sana. Lakini historia inaonsha mara nyingi mtu hupata utukufu mbali na kwao. Ndiyo ilivyokuwa kwangu mimi.
“Umeangalia kila kitu, labda kuna kitu kilichopungua” Abdi akaniuliza baada kuipitia nyumba nzima.
“Naona kila kitu kipo”
“Mimi nafikiri bado kitu kimoja tu?” Abdi akaniambia.
“Kitu gani?” nikamuuliza.
“Nyumba inahitaji kupambwa”
“Ipambwe kivipi?”
Abdi akacheka kidogo.
“Hivi hujaelewa kama nyumba hupambwa kwa kuwa na mke mzuri”
“Na mimi nikacheka.
“Ni kweli, sasa huyo mke yuko wapi?”
“Ndiyo nataka tukae chini tulizungumzie suala hilo”
“Sawa”
“Sema mwenyewe unataka mke wa kibarawa, wa kigunya au wa kisomali?”
“Wote uliowataja wanafaa”
“Nikutafutie mke wa kisomali aliyechanganya na ubarawa, mweupe kama karatasi”
Abdi aliponiambia hivyo tukacheka.
“Abdi bwana! Mweupe kama karatasi?”
“Huyo akiwa chumbani uhitaji kuwasha taa, nuru yake inatosha kabisa kuangaza chumba!”
“Atapatikana kweli?”
“Mbele ya fedha hakuna kisichopatikana”
“Sawa. Mimi namsubiri”
“Nipe muda kidogo nikuchagulie mke anayefaa. Najua kuwa wewe unahitaji mke mweupe”
“Umenijuaje”
Abdi akacheka kisha hakunijibu chochote, akagonga mkono wangu na kuelekea kwenye mlango. Alikuwa kama aliyetaka kutoka kisha akageuka na kunitazama.
“Suala lako ninalishughulikia, usijali. Nilikuahidi kukupatia gari, ungependa gari hii ninayotumia au nikupatie gari jingine”
“Wewe ndio utajua”
“Basi ngoja nikupatie leseni hapo kesho, nitakupa gari zuri”
“Sawa”
Nilipomjibu hivyo Abdi aligeka akafungua mlango na kutoka bila kuniambia chochote. Nilimchungulia kwenye dirisha nikaona akipanda gari lake na kuondoka.
Alikuwa kama aliyekwishamaliza kazi.
Niliingia katika chumba changu nikafungua kabati na kulikagua ndani. Lilikuwa tupu na safi. Nikaanza kupanga nguo zangu chache..
Nilipomaliza nilitoka nikaenda kukaa sebuleni kujipumzisha Siku ile nilishinda pale nyumbani. Saa saba mchana Abdi alikuja akanipa shilingi laki moja za kisomali kwa ajili ya matumizi yangu.
Akaniambia kwamba leseni yangu inashugulikiwa. Alinichukua kule hotelini kwake tukala chakula pamoja kisha akanirudisha nyumbani.
Saa mbili usiku alikuja tena tukaenda kula.
Siku ile nililala peke yangu katika ile nyumba. Asubuhi kulipokucha Abdi alinifuata kwa ajili ya kunipeleka kule hoteli kuanza kazi.
Tulipofika alinitambulisha kwa wafanyakazi kama meneja mpya. kuanzia siku ile. Abdi pamoja na mtu ambaye aliwekwa awe msaidizi wangu walinitembeza katika hoteli nzima kabla ya kunikabdidhi ofisi pamoja na nyaraka zote zinanazihusu shughuli za hoteli.
Kutoka siku ile nikaanza kazi ya umeneja katika hoteli ya AL ASAD. Siku iliyofuata Abdi alinipatia leseni ya kuendesha na akanikabidhi moja ya magari yake.
Baada ya kuendesha kazi kwa mwezi mmoja Abdi akaniambia kuwa alikuwa ameshanitafutia mchumba.
“Ni nani?” nikamuuliza.
“Shamsa. Naona Shamsa anakufaa, au unasemaje?”
Shamsa alikuwa ni yule msichana wa kisomali aliyekuwa akifanya kazi katika ile hoteli ya Abdi niliyofikizia.
“Shamsa anafaa sana” nikamwambia.
“Yule baba yake ni msomali lakini mama yake ni mbarawa”
“Umeshazungumza naye?”
“Nimeshazungumza naye”
“Amekubali?”
“Kwanini akatae amri ya bosi wake. Kiufupi ni kuwa amekubali. Hivi leo ndio nataka kuwakutanisha mzungumze wenyewe”
“Utatukutanisha wapi?”
“Popote utakapotaka wewe”
“Anaweza kuja nyumbani ninakoishi?”
“Kwa mila za wasomali hawezi kuja nyumbani kwako ila wewe mfuate kazini kwake, gari si unayo?”
“Ndiyo gari ninato”
“Sasa wewe mfuate kazini, utakaa naye mtazungumza”
“Sasa nimwambieje?”
Nilipouliza swali hilo Abdi akacheka.
“Usicheke Abdi. Mimi sijui mila zenu huku!”
“Muulize umepata ujumbe wangu kutoka kwa Bwana Abdi. Sasa akikupa jibu ndio, mtaendeleza mazungumzo yenu”
“Sawa. Nitakwenda baadaye kidogo”
“Na mimi nitamjulisha kuwa utakwenda kuongea naye”
“Sawa”
Nilisubiri hadi nilipopunguza kazi zangu nikatoka kwa gari niliyokuwa nimepewa na abdi. Muda huo ilikuwa ikaribia kuwa saa tano.
Nilipofika nilitafuta meza nikakaa. Shamsa alishaniona akanifuata na kuketi na mimi.
“Asalaam alaykum” akanisalimia huku akinitolea tabasamu la aibu..
“Wa alayka salaam. Hujambo Shamsa?”
“Sijambo, sijui wewe”
“Mimi nashukuru sana”
Nikayakumbuka maneno ya Abdi.
“Je umepata ujumbe wangu?” nikamuuliza.
“Nimeupata”
Alponiambia hivyo nilitabasamu.
“Ndiyo nimefuata jibu”
Shamsa akanitazama kwa makini mpaka nikaona aibu. Labda alikuwa akinihakiki kama ni mume ninayeweza kumfaa.
“Mbona tulishakubaliana” akaniambia baada ya kimya cha sekunde chache..
“Mimi sielewi. Mlikubaliana nini?”
“Kwani wewe si ulikuwa unataka mchumba?”
“Ndiyo”
“Nimekubali kuwa mchumba wako”
Aliponiambia hivyo niliushika mkono wake aliokuwa ameuweka juu ya meza. Niliushika kirafiki tu kisha nikamtazama. Nilimuona alikuwa amevutiwa na kitendo changu.
“Shamsa una umri gani?” nikamuuliza.
“Miaka ishirini na mitano. Na wewe una umri gani?”
“Miaka ishirini na tisa. Ikifika mwakani mwezi wa nne nitatimiza miaka thelathini”
“Ni mwenyeji wa wapi?”
“Abdi amekwambia mimi ni mwenyeji wa wapi?”
“Sikumuuliza hivyo”
“Unaonaje kama utamuuliza yeye?”
“Kwanini nimuulize yeye wakati mwenyewe upo?”
Nikanyamaza kidogo kabla ya kumwammbia.
“Mimi natokea Tanzania”
“Wewe ni mzigua”
“Ndiyo mimi ni mzigua”
“Hata babu yangu mzaa mama alitokea huko huko zigua”
“Kwa hiyo wewe ni mzigua?”
Shamsa akacheka kidogo.
“Hapana. Babu yangu mzaa mama ndiyo alikuwa mzigua lakini mimi mwenyewe ni msomali, upande mwingine ni mbarawa”
“Mmezaliwa wangapi katika familia yenu?”
“Tulizaliwa wawili tu, mimi na dada yangu ambaye alishafariki zamani. Kwa hiyo nimebaki mimi peke yangu”
“Wazazi wako wapo?”
“Pia walishafariki. Kwa sasa hivi mtu pekee ambaye niko karibu naye ni Abdi”
“Oh Pole sana”
“Asante. Abdi ameniambia kama nitafunga ndoa na wewe, yeye ndiye atakayenisimamia kwa sababu sina ndugu”
“Nimekuelewa. Pole sana”
“Asante. Abdi ameniambia wewe ni ndugu yake, ni kweli?”
“Ni kweli”
Hapo nilisema uongo kumuunga mkono mwenyeji wangu. Abdi hakuwa ndugu yangu. Kwa vile alishamwambia
msichana huyo kuwa mimi ni ndugu yake, nikaona nikubali. Pengine Abdi alimwambia hivyo ili msichana huyo aweze kunikubali kirahisi.
“Kwa hiyo umeamua kuja kuishi hapa Somalia?” Shamsa akaniuliza.
“Ni ushauri wa Abdi, amenitaka nibaki huku”
“Ameniambia amekupa ile hoteli yake ya Al Asad?”
“Amenipa kwa maana ya kuiongoza”
“Lakini wewe si ndiye meneja wake?”
“Ndiyo”
“Sasa turudi katika mazungumzo yetu, unatarajia utanioa lini?”
“Hilo ni suala ambalo nitalipanga na Abdi. Kwa upande wangu ningependa tuoane haraka iwezekanavyo”
“Sawa”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Usiku wa siku ile Abdi alikuja nyumbani kwangu akaniuliza.
“Mmezungumzaje na Shamsa?”
“Tumekubaliana”
“Umemuonaje yule binti, si anakufaa?”
“Anafaa”
“Sasa ungependa umuoe lini?”
“Mimi nakusikiliza wewe”
“Wazazi wake walishafariki na hana ndugu. Nimemwambia kuwa ndoa yake nitaisimamia mimi”
“Sasa panga siku”
“Nisingependa ichukue muda mrefu, unaonaje kama tutasubiri kwa wiki mbili hivi?”
“Si mbaya”
“Si najua kuna matayarisho ingawa nisingependa iwe ndoa ya sherehe kubwa”
“Sawa”
Siku iliyofuata Abdi alimzuia Shamsa kuja kazini kwa ajili ya maandalizi ya ndoa yetu. Abdi ndiye aliyeshughulikia kila kitu. Kutoka siku ile nilikutana na Shamsa mara mbili tu.
Baada ya hapo sikukutana naye tena hadi siku ya ndoa yetu. Ndoa ilifanyika usiku. Niliozeshwa mke msikitini saa mbili usiku. Baada ya ndoa, mimi, Abdi na wasindikizaji wetu tulikwenda nyumbani kwa shamsa. Nikampa mke wangu mkono.
Usiku huo huo nikamchukua mke wangu nyumbani kwangu. Hakukuwa na sherehe kubwa. Abdi aliniambia sherehe kubwa itazusha umbeya.
Baada ya kuoana na Shamsa ndipo nilipoanza kusahau kwetu. Msichana alinionesha mapenzi ya kisomali ambayo nilikuwa siyajui. Aliniheshimu, alionesha upendo wa dhati na alijivunia kuolewa na mimi.
Siku zikapita. Biashara ya hoteli ilikuwa inakwenda vizuri. Abdi aliniruhusu kuchukua kiasi chochote cha pesa ninachotaka kila mwezi ila niweke katika hesabu.
Aliniambia kuwa kila mwaka tutakuwa tunagawana mapato.
Kwa vile nilishadhamiria kuendelea kuishi Somalia nilikubaliana naye.
Sikuona kitu cha kunirudisha nyumbani. Nilikuwa na nyumba nzuri ya kuishi. Nilikuwa na gari zuri la kutembelea
nilikuwa na kazi nzuri iliyokuwa ikinipatia kipato cha kutosha, isitoshe nilikuwa na mke mzuri wa kunituliza. Sikuona sababu yoyote ya kutaka kurudi Tanzania.
Siku moja baada ya chakula cha usiku, Shamsa aliniambia.
“Unajua huyu ndugu yako Abdi ana siri kubwa sana”
“Siri ya nini?”
“Unajua alitaka kukuozesha wewe mke lakini yeye hana mke?”
“Hivi hana mke, siku zote ananiambia mke wake yuko kwao. Kumbe ananidanganya”
“Hana mke”
“Aliachana naye au hajaoa”
“Ni afadhali angeachana naye”
“Kumbe…!”
“Kulikuwa na tetesi kuwa alimuua!”
“Ha! Unaniambia ukweli? Kwanini amuue mke wake? Alimkosea nini?”
“Ni afadhali angemkosea lakini hakumkosea kitu chochote”
“Alimuua bure bure tu?”
“Alimuua kutokana na imani zake za kishirikina”
Nikanyamaza kimya na kumtazama Shamsa ili aendelee kunieleza.
“Huyu ni mtu tajiri lakini anataka utajiri zaidi…”
“Una maana kwamba alimuua mke wake ili apate utajiri kwa njia za kishirikina?”
“Ina fanana na hivyo lakini yeye aliambiwa na mganga wake kuwa katika familia yao kuna jini la utajiri. Mganga alimwambia hivyo baada ya kuona ile pete anayovaa, alimwambia ile ni pete ya jini ambaye ukiwa naye unakuwa tajiri wa kupindukia”
Hapo ndipo nilipoanza kuzinduka.
Shamsa akaendelea kunieleza kuwa alivyoelezwa na Abdi mwenyewe kuwa asili yake ni mzigua. Baba yake alitoka Tanga, Tanzania. Alikuwa mvuvi wa samaki. Siku moja boti aliyokuwa anavulia samaki na wenzake ilipata hitilafu wakiwa baharini.
Walikokotwa na maji hadi katika pwani ya Somalia. Wenzake wane walifariki dunia lakini yeye alipona. Baada ya kuokolewa na wavuvi wa Somalia alihifadhiwa kwenye nyumba ya mvuvi mmojawapo na akalowea huko huko Somalia.
Shughuli zake zikawa ni zile zile za uvuvi. Akaoa mke wa kisomali akamzaa Abdi na mdogo wake ambaye anaitwa Yusufu.
Abdi hakupata elimu yoyote lakini ni mjanja, ana akili ya kuzaliwa. Tangu akiwa mtoto alionekana kuwa na kipaji.
Alipokuwa mkubwa alijiingiza katika biashra za magendo ya pembe za ndovu zilizompa utajiri mpaka akaweza kununua hoteli anazomiliki pamoja na kuanzisha miradi mengine.
Baba yake Abdi alikufa wakati Abdi akiwa mkubwa. Huyo baba yake ndiye aliyekuwa na ile pete aliyokuwa anavaa Abdi. Abdi aliichukua siku baba yake alipokufa akaivaa yeye bila kujua maana yake.
Kwa vile Abdi ni mpenda ushirikina alikuwa mganga wake mzee mmoja mrefu ambaye alimwambia kuwa ile pete ni ya jini mwanamke ambaye alikuwa mke wa babu yake aliyekufa zamani huko Tanga.
Abdi akaambiwa kwamba kama atampata jini huyo na atamuoa na yeye atakuwa tajiri. Hapo ndipo Abdi alipopata kichaa. Akaanza kufanya makafara ya kumvuta huyo jini lakini ilishindikana.
Akaambiwa na mganga, kwa vile yeye ameshaoa mke, huyo jini hawezi kumpata kwani jini huyo haendi kwa mtu mwenye mke wake. Asubiri kama mke wake atakufa ndio huyo jini anaweza kumpata.
Abdi akaona hakuwa na sababu ya kumtaliki mke wake akamtilia sumu kwenye chakula ili afe. Baada ya kumuua mke wake akarudi tena kwa yule mganga. Akafanyiwa makafara lakini huyo jini hakutokea.
Safari hii akaambiwa kwamba huyo jini tayari ana mtu mwingine na mtu huyo ni ndugu yake aliyeko Tanga, yaani mwana wa baba yake mdogo.
Akaambiwa ndugu yake huyo anaitwa Umari au Amiri au Amour na nyota yake ni Nge.
Shamsa aliendelea kunieleza kuwa mganga alimwambia Abdi kuwa dalili ya kumtambua huyo ndugu yake ni kuwa anapokabiliwa na hatari jini wake anajigeuza joka kubwa na kuwashambulia watu wanaotaka kumdhuru huyo ndugu yake.
Siku moja wakati Abdi yuko kwenye boti yake akifuatilia pembe zake za ndovu kutoka Tanzania, alielezwa na nahodha wa boti iliyotoka Tanzania kuhusu mkasa uliowafika ambapo baada ya kumkamata mtu waliyemdhania kuwa ni mpelelezi likatokea joka ambalo liliwaua wenzake.
Abdi aliposikia mkasa huo akayakumbuka yale maneno ya mganga wake kwamba huyo ndugu yake mwenye huyo jini, jini wake hujigeuza joka.
Shamsa alinieleza wazi kuwa mimi ni ndugu yake Abdi na jini anayemtaka Abdi ni Zena.
Siku ile nilipokutana na Abdi kwenye ile boti, Abdi aliniambia.
“Wewe unaitwa Umar au Amiri au Amour”
Nikamwambia ninaitwa Amour.
Akajua ndio mimi mwenye huyo jini aliyekuwa anamtaka. Maelezo ya Shamsa yalinifanya nigundue sababu ya Abdi kunichukua kwa nguvu huko Somalia.
Mganga wake pia nilishamfahamu, alikuwa ni yule mzee mrefu wa kisomali.
Kumbe ndiyo maana yule mzee alinifuata usiku akanichukua pale hoteli kimiujiza na kunipeleka katika shimo. Kumbe alikuwa ananifanyia uganga wa kumpata Zena!
Halafu siku ile Abdi alinipeleka kwa yule mganga ambaye alifanya makafara yake mpaka Zena akatokea na kumpiga kofi, mimi na Abdi tukakimbia. Kumbe zile zilikuwa jitihada za kumpata Zena!
Shamsa alinieleza kuwa mganga alishindwa kumchomeka Zena kwa Abdi na hivyo walibuni mpango mwingine.
Mpango huo ulikuwa ni wa kuniua mimi kikatili. Abdi aliambiwa anikamate na kunining’iniza kichwa chini kisha atoboe utosi wangu kwa msumari. Damu itakapotoka aikinge kwenye kikombe cheupe kisha ajipake yeye kwenye utosi wake ili aweze kumpata Zena.
“Shamsa umeijuaje habari yote hii?” nikamuuliza Shamsa baada ya kunieleza mkasa huo.
“Hii ni habari ya siri, usimwambie Abdi na wala usiniulize nimeijuaje isipokuwa mtahadhari Abdi. Abdi ni ndugu yako lakini ni mshenzi. Au utakataa kwamba huna baba yako mdogo aliyepotea baharini miaka ya nyuma.?”
“Yupo. Niliambiwa kuwa alipotea baharini lakini mimi nilikuwa mdogo au sijazaliwa”
“Basi ndiyo hivyo”
“Siku zote nilikuwa ninajiuliza kwanini Abdi amenileta hapa Somalia kwa nguvu, kwanini ananiita ndugu yake na kwanini alilitambua jina langu mara tu baada ya kuniona. Kumbe kuna vitu vilivyojificha nyuma ya pazia
“Pia nilikuwa nikijiuliza kwanini alinipeleka kwa yule mganga na kwanini Zena alitokea na kumpiga kibao…”
“Amekubali apate gharama za kukuweka wewe hapa Somalia, lengo lake ni hilo”
“Nashukuru kwa kunifahamisha. Sasa unanishauri nifanye nini?”
“Endelea kumuangalia tu, jifanye kama hujui lolote”
“Si anataka kuniua?”
“Huo mpango wao bado, siku watakayotaka kufanya hivyo nitakwambia”
“Mh! Kwa kweli umenitia hofu!”
“Una maana kwamba huniamini mimi mke wako?” Shamsa akaniuliza.
“Ninakuamini” nikamjibu.
“Kama unaniamini endelea kuniskiliza mimi na fuata vile ambavyo nitakwambia”
“Sawa. Lakini ninataka kujua wewe umejuaje habari zote hizo?”
“Mimi niko karibu sana na Abdi”
“Na kuhusu upande wa baba yangu mdogo aliyekuja huku Somalia umejuaje habari zake?”
“Hakuna kisichofahamika Amour. Au ulikuwa hutaki miye mke wako nijue habari zako?”
“Hapana. Ukijua habari zangu ni vizuri kwa sababu mimi ni mume wako”
“Sasa tulia. Endelea na kazi yako kama kawaida, zungumza na kaka yako Abdi bila uoga, siku ya watakayopanga kufanya ushenzi wao nitakwambia siku moja kabla na nitakupa mbinu ya kufanya”
“Nakushukuru sana mke wangu kwa kunizindua. Umejibu maswali yangu mengi niliyokuwa nikijiuliza bila kupata majibu. Ninaamini kuwa wewe ni mke wangu wa kweli”
“Na mimi nakushukuru sana mume wangu kwa kunisikiza na kuniamini. Wewe utakuwa mume wangu wa kudumu”
“Asante sana”
Shamsa alitabasamu kisha akanipiga busu kwenye shavu langu.
“Hebu niambie ilikuwaje siku ile kwenye ile boti wakati wale jamaa walipotaka kukutosa?” akaniuliza.
Nikamueleza Shamsa ilivyokuwa.
“Lilipotokea hilo joka na kuwazamisha hao waliotaka kukutosa, wewe ulifikiri nini?” akaniuliza.
“Leo ndio nimepata jibu kutoka kwako. Hilo swali nilikuwa nikijiuliza sana. Nilikuwa sijui ni kwanini lile joka linetokea na lilitoka wapi. Kumbe ni jini linalonifuata mimi”
“Kumbe wewe siku zote tunaishi lakini kulikuwa na kitu unanificha!”
“Kitu gani?”
“Kwamba una jini wa kike mwenye utajiri”
“Kwa kweli niliogopa kukutia hofu. Huyu jini mimi simtaki na amekuwa akinifanyia vituko vingi sana mpaka nimekimbia huko kwetu…”
Sikutaka kumueleza mengi kwamba jini huyo hataki nioe mke wa binaadamu, anataka nimuoe yeye.
Nilidhani Shamsa angeniuliza ni vituko gani alivyokuwa akinifanyia huyo jini lakini hakuniuliza.
“Sasa mwenzako anamtaka huyo jini kwa udi na uvumba” akaniambia.
“Kwa kweli kama alifikia kumuua mke wake kwa sababu ya jini ambaye hamjui, ni mtu hatari na mshirikina sana”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ile mirungi anayokula inaharibu akili yake lakini mwenyewe hajui. Inamfanya awaze utajiri wakati wote. Na kila apatavyo hatosheki”
“Mtu namna ile mwisho wake ni kufa tu. Wahenga wanasema tamaa mbele mauti nyuma binaadamu katikati”
Shamsa akacheka.
“Amour umenichekesha!” akaniambia huku akiendelea kucheka.
“Kweli kabisa. Mtu namna ile mwisho wake ni kufa tu”
“Akifa wewe na Yusufu mtarithi mali zake”
“Ni mpaka aandike hivyo”
“Hata asipoandika ni lazima mtamrithi”
“Yusufu hatakubali”
“Labda kwa hapo. Lakini kama atamwambia kuwa wewe ni ndugu yao, unaweza kupata sehemu ya mali yake”
“Siwazii sana huko, mimi nawazia maisha yangu yatakavyokwenda. Naona sitakaa sana hapa Somalia”
“Hutakaa sana utakwenda wapi?”
“Nitarudi kwetu”
“Na mimi utaniacha na nani wakati nimeshakuwa mke wako?”
“Nitakuomba twende tukaishi Tanzania, si utakubali?”
Shamsa akabetua mabega yake.
“Nitakubali, nitafanyaje sasa wakati umeshanioa!”
Jibu lake lilinifurahisha nikamvuta kwangu na kumkumbatia. Shamsa alijilegeza nikamtuliza kifuani kwangu. Nilikuwa nikiusikia moyo wake ulivyokuwa ukipiga taratibu, pu! pu! pu!
Kwa vile aliendelea kutulia kifuani kwangu na mimi niliendelea kumkumbatia.
***********
Asubuhi ya siku iliyofuata nilikwenda kazini kwangu huku nikijua kuhusu mambo kadhaa ambayo nilikuwa siyajui.
Moja ya mambo hayo ni kuhusu Abdi kunileta pale Somalia kinguvu na kunipa shughuli ya kufanya.
Sasa nilijua lengo la Abdi lilikuwa ni kumtaka jini aliyekuwa akinisumbua ili apate utajiri.
Kama ni hilo tu nisingeshituka wala nisingejali. Abdi amekwenda mbali zaidi kutaka kuniua. Jambo hilo halikuwa la
kupuuza. lakini nilimtegemea sana Shamsa aliyenidokolea siri hiyo.
Kutokana na mpango wake huo niliamini kwamba Abdi alikuwa mpumbavu sana. Ushirikina wake ulikuwa ni wa hatari na si wa kupuuzwa na mtu yeyote mwenye akili timamu.
Nilipofika kazini kwangu niliendelea kufanya kazi huku nikiwa nimetingwa na mawazo ya mchanganyiko. Mara kwa mara Shamsa alikuwa akinipigia simu kuniuliza jinsi nilivyokuwa ninaendelea na kazi.
“Naendelea vizuri” nilimjibu.
“Abdi hajafika hapo?”
“Hajafika bado”
“Tafadhali usimuulize chochote”
“Sitamuuliza kitu”
“Na wewe pia kuwa na amani. Usiwaze sana”
“Nisiwaze nini?”
“Yale niliyokueleza jana usiku”
“Yale hayapo tena kichwani mwangu, naendelea na kazi yangu”
“Sawa”
Nilipomaliza tu kuzungumza na Shamsa nilimuona Abdi akiingia ofisini kwangu. Uso wake ulikuwa umetaharuki.
Kabla hata ya kunipa salamu aliniambia.
“Watu wengine sijui wana tabia gani?”
Jinsi nilivyouona uso wake umetaharuki na yale maneno aliyosema, vilinishitua nikamuuliza.
“Kuna nani?”
“Si huyu mpuuzi!”
“Nani?”
“Yusufu ameondoka nyumbani kwake tangu jana. Hajamuaga mke wake anakwenda wapi. Mke wake sasa ananisumbua mimi!”
“Una maana kwamba tangu jana hajafika nyumbani kwake?”
“Hajafika na hajulikani yuko wapi”“Kwani walikuwa na ugomvi?”
“Hawakuwa na ugomvi wowote. Yule mdogo wangu tu hana akili. Ndio maana sielewani naye”
“Sasa atakuwa amekwenda wapi?”
“Nitajuaje?”
“Mh…!”
Pakapita kimya kifupi Abdi akionesha kuchukizwa akaniambia.
“Nimekufuata twende kituo cha polisi kumuulizia”
“Unadhani atakuwa amekamatwa?” nikamuuliza.
“Si lazima awe amekamatwa, anaweza kuwa amepata ajali na ripoti yake kufikishwa polisi”
“Haya twende”
Tukatoka mimi na Abdi. Tulijipakia katika gari lake na kuelekea kituo cha polisi.
Vile tulivyokuwa tumekaa pamoja ndani ya gari niliyakumbuka maneno ya Shamsa kuhusiana na Abdi, nikaona kama niliyekuwa nimekaa na nyoka mwenye sumu kali.
Tukaendelea na safari.
Nilikuwa nikimfahamu vizuri Yusufu mdogo wake Abdi ingawa hakuwa karibu sana na mimi. Muda mwingi alikuwa akishughulika na mambo yake mwenyewe.
Niligundua pia kuwa Abdi hakuwa akisikizana sana na mdogo wake jambo ambalo lilifanya mara kwa mara wakwaruzane.
Lakini ndugu ni ndugu. Licha ya kuwepo kwa hali hiyo, Abdi alipopata habari kuwa mdogo wake alikuwa hafahamiki alipo ameanza kupata wasiwasi na kumuhangaikia.
Tulifika kituo cha polisi ambapo Abdi alikuwa akifahamika vizuri. Aliwaeleza polisi tatizo lake.
Polisi hao wakamfahamisha kuwa hawakuwa na taarifa yoyote ya mdogo wake.
“Amepotea tangu lini?” Polisi mmoja akamuuliza.
“Si kwamba amepotea bali hajulikani yuko wapi”
“Tangu lini?”
“Tangu jana alipoondoka nyumbani kwake hajarudi hadi sasa na hajulikani yuko wapi”
“Ana mke na watoto”
“Ndio ana mke na watoto”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hakuwahi kumwambia mke wake anakwenda wapi?”
“Huyo mke wake ndiye aliyenifahamisha mimi kuwa Yufusu hajarudi nyumbani tangu jana”
ITAENDELEA

0 Comments