ILIPOISHIA
Nilishindwa kuamini macho yangu! Lilikuwa dude kubwa kama joka lililokuwa na mikono yenye vidole vyenye kucha ndefu. Urefu wake ulikuwa kama guzo la umeme. Lilipokuwa ndani ya ile boti lilikuwa limejikunja. Mwili wake ulikuwa na magamba makubwa kama ya samaki.
Kwa kutumia kucha zake lilimvamia mtu mmoja na kuruka naye juu kisha likajitosa baharini likiwa na mtu huyo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sote tulikuwa tumetaharuki na hatukujua ni jambo gani lilitaka kutokea. Wakati wale watu wanajiinua pale chini, joka hilo likaibuka tena likiwa halina mtu. Likavamia mtu mwingine na kuruka naye kisha likajitosa baharini.
Watu hao wakawa wanapigana vikumbo ndani ya boti kutafuta pa kujificha. Kutahamaki joka hilo likatokea tena, likamnyakua mtu mwingine na kuzama naye chini ya bahari. Watu wote wakamalizwa nikabaki mimi na Mapama
Mapama alikuwa akihangaika akijua kwamba joka hilo litaibuka tena na kumchukua yeye.lakini dakika zikapita hatukuliona. Kwa sababu ya hofu na kujiona amebaki peke yake mtu huyo alikuja kunifungua zile kamba.
“Njoo huku” akiniambia akitangulia kuingia katika kile kijichumba kilichokuwa ndani ya ile boti.
Nikainuka na kumfuata. Mikono yangu ilikuwa imekufa ganzi kutoka na kufungwa kamba kwa muda mrefu. Nikawa ninainyooshanyoosha.
Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kioo cha kutazamia mbele. Pia kulikuwa na sukani na mitambo ya boti.
“Samahani bwana, naona tumebaki sisi wawili tu. Sijui lile lilikuwa joka gani na limetokea wapi?” Mapama akaniambia kwa hofu.
SASA ENDELEA
“Nadhani limekuja kuwaua kutokana na ule unyama wenu wa kututosa baharini bila hatia”
“Sio mimi, ni wale jamaa. Mimi sikuweza kuwazuia”
Nikaona yule mtu alikuwa akijitetea kwa kusema uongo wakati yeye ndiye aliyeamrisha tutoswe.
Sikutaka kumsuta kwa sababu hata mimi nilikuwa nimepata hofu na sikuwa nikijua hatima yangu.
“Lakini sidhani kama litakuja tena” nikamwambia kumpa moyo. Hata hivyo nilijisemea tu bila kuwa na uhakika.
Mapama alikuwa akiendesha lile boti huku akiwa matu matu. Kila mara alikuwa akitupa macho pande zote za boti. Nilijua alikuwa akihofia lile joka ambalo hata mimi liliniweka katika hali ya wasiwasi.
“Tuombe Mungu. Tukinusurika tutatajirika” Mapama akaniambia.
“Kwani tunaelekea wapi?” nikamuuliza.
“Tunakwenda Somalia”
“Kumbe mlikuwa mnakwenda Somalia?”
“Mnunuzi wa hizi pembe yuko Somalia, ndio tulikuwa tunampelekea”
“Ni mali ya nani?”
“Mwenyewe yuko Dar. Mimi ndiye msimamizi wake na mmiliki wa hii boti. Mara kwa mara ananituma kupeleka pembe zake Somalia”
“Huwa mnazihifadhi kwenye kile kisiwa?”
“Pale ndio tunazificha tunapozikusanya kutoka kwa majangili”
“Mnapokwenda pale mnachinja mbuzi kwa ajili ya nini?’
“Kile kisiwa kinakaa majini. Hivyo tunapofika tunawapa kafara ili wasitudhuru. Na wewe ulifuata nini pale?”
“Pale nilifika jana kwa kogelea. Mimi nilikuwa ninatoka Pemba kwenda Dar. Boti yetu ilizama.”
“Ndiyo nilisikia. Kwa hiyo ulilala pale pale?’
“Ndiyo nililala juu ya mti. Sasa nilipowaona leo asubuhi nikawafuata kuwaomba msaada lakini inaelekea hamkunielewa”
“Unajua hii kazi ni ya siri na ya hatari, wale wenzangu walipokuona walidhani wewe ni mpelelezi ulikwenda pale kufanya uchunguzi”
Jamaa yule alikuwa akiwasingizia wenzake kila kitu wakati yeye ndiye aliyekuwa akinituhumu.
“Sasa ukifika Somalia unarudi lini huku Tanzania”
“Tukifika tu tunapakua huu mzigo na kuupakia kwenye boti nyingine halafu tunarudi”
“Hiyo boti tutaikuta wapi?”
“Tukiingia Somalia tu tunaikuta inatusubiri”
“Halafu hizi pembe zinapelekwa wapi?’
“Zinasafirishwa kwa meli na kupelekwa nchi za kiarabu. Waarabu wanatengezea mipini ya majambia”
Sikuwa nikijua kuwa pembe za ndovu hutengezwa mipini ya majambia. Hata hivyo niliyaacha yale mazungumzo ya pembe. Dukuduku langu lilikuwa ni kurudi nyumbani.
“Tutafika leo huko Somalia?” nikamuuliza.
“Hapa tuko katika bahari ya Mombasa nchini Kenya. Mpaka ikifika saa kumi na moja alfajiri tutaingia Somalia”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Eh! Kumbe safari bado ni ndefu?”
“lakini tumeshafika nusu ya safari yetu”
“Kama ni kurudi itakuwa kesho”
“Kesho si mbali. Sasa hivi jua litakuchwa, usiku utaingia”
Mapama aliposema hivyo alitoa kicheko cha kujilazimisha akaondoka kwenye sukani baada ya kuitegesha muelekeo aliokuwa anautaka. Akafungua kabati lililokuwa humo ndani na kutoa sufuri iliyokuwa imefunikwa.
Aliiweka kwenye kimeza kisha akafunua ule mfiniko. Ndani ya sufuria hiyo mlikuwa na pilau na vipande vya nyama. Sijui ilikuwa nyama ya nini.
Akapakua ile pilau kwenye sahani na kuniambia.
“Tule”
Kusema kweli nilikuwa na njaa lakini zile nyama ziliniogopesha kwa sababu zilikuwa nyingi na sikujua zilikuwa nyama za mnyama gani kwani zilikuwa na mafuta mengi.
“Hizi ni nyama za nini?” nikamuuliza.
“Nyama ya nyati, ni tamu sana. Hebu onja”
Aliokota kipande cha nyama bila kuosha mkono akanipa.
Alinishangza sana. Mikono yake ilikuwa imeshika kila kitu. Imeshika magwanda ya polisi waliowatosa baharini. Imeshika mapembe ya ndovu. Imeshika sukani ya boti. Imeshika bangi…loh! Hawa watu wachafu kweli!
Alipoona nimesita nikimtazama akagutuka na kuinuka.
“Ngoja nioshe mkono” akaniambia.
Aliosha mkono kwa kutumia maji yaliyokuwa yamewekwa kwenye dumu.
“Na wewe njoo uoshe mikono yako” akaniambia.
Wakati wote nilikuwa nikisema na moyo wangu kuhusu kile chakula. Nilikuwa nikijiuliza nile kile chakula au nisile. Ukweli ni kwamba nilikuwa na njaa na njaa haina ustaarabu. Ikikushika unaweza kula hata kisocholika. Japokuwa kwanza nilisita sita lakini hatimaye niliinuka kwenda kuosha mikono.
Baada ya kuosha mikono tukarudi pale tulipokuwa.
“Kula” Mapama akaniambia.
Tukaanza kula. Pilau ilikuwa ikinuka moshi wa kuni. Nikahisi kwamba waliipika wao wenyewe kwa kutumia kuni walizoziokota fukweni mwa bahari..
Kwa sababu ya njaa niliyokuwa nayo nilikula sana mpaka nikahisi kwammba ningevimbiwa. Pilau ilikuwa nyingi hatukuimaliza.
Nilimuacha Mapama akiendelea kula.
“Ukiwa katika hali ya baridi unatakiwa ule sana” Mapama aliniambia.
Tonge zake zilikuwa kubwa na nilihisi alikuwa akimeza bila kutafuna.
Alipotosheka na yeye aliiacha. Akairudisha sinia kwenye kabati.
Baada ya kuosha mikono Mapama alinipa maji ya kunywa nikayanywa. Na yeye akanywa.
“Sasa baridi hatutaisikia. Tunaweza kuendelea na safari” Mapama akaniambia.
Tukakaa na kuendelea kuzungumza. Mara moja moja alikuwa akitazama mitambo. Nilikuwa nimejifunza kwamba boti haikuwa ikiendeshwa kama gari.
Haihitaji kushikiliwa sukani wakati wa kuendesha. Unaweza kuweka muelekeo wako na ukaiacha iende yenyewe.
Ndivyo Mapama alivyokuwa akifanya. Hatimaye Mapama alianza kusinzia. Alikuwa akisinzia huku akishituka.
“Nikuache uangalie, mimi najinyoosha kidogo” akaniambia.
Nikajua kuwa pilau aliyokuwa ameila kwa wingi ilikuwa imemlewesha.
“Wewe lala, baadaye nitakuamsha” nikamwambia.
Mapama akajitupa chini. Baada ya muda kidogo nilimsikia akikoroma.
Huku boti ilikuwa ikiendelea na safari. Masaa yalipita. Saa yangu ilikuwa imesimama kutokana na kuingia maji ya chumvi, sikuweza kujua ilikuwa saa ngapi.
Mawazo yangu yalikuwa ni kurudi kwetu salama. Nilijiambia Zena alikuwa amenifikishia mkasa wa kutatanisha sana ambao sikutegemea kama ungenitokea.
Niliamini kuwa siku zangu za kufa bado zilikuwa mbali, vinginevyo ningelikwishakufa.
Kama nisingekufa kwenye ile ajali ya meli, ningekufa wakati Zena ananikokota baharini. Na kama nisingekufa baharini, ningekufa kwenye kile kisiwa chenye majoka na baridi.
Lakini bado, japo nilinusurika kote, wale washenzi wenye ile boti wangeniua kama walivyowaua wale polisi waliowatosa. Na kama hawakuniua ningeuliwa na lile joka lililowaua watu wote na kumbakisha Mapama na mimi. Mpaka muda ule nilishindwa kujua joka lile lilitoka wapi na pia nilishindwa kujua jinsi nilivyonusurika
.
Kusema kweli niliona kunusurika kwangu kulikuwa kwa ajabu sana.
Wakati nikiwa kwenye mchanganyiko huo wa mawazo huku macho yangu yakitazama mbele tunakoelekea, niliona kitu kama kimulimuli kikielekea upande wetu. Nikashituka na kuangaza macho vizuri.
“Nini kile?” nikawa najiuliza kimoyo moyo.
Baadaye kidogo niligundua kuwa ilikuwa boti iliyokuwa na kimuli muli na ilikuwa na maandishi yaliyosomeka POLISI KENYA.
“Mama yangu we!”
Kwa haraka nikamuamsha Mapama.
“Hebu amka uone!”
“Nini?” Mapama aliniuliza akiwa bado amefumba macho.
“Polisi. Kuna boti ya polisi inatuufuata. Amka!” nikamwambia.
“Polisi?”
“Tunafuatwa na boti ya polisi!”
Mapama akainuka.
“Iko wapi?” akaniuliza.
“Inakuja, imewasha kimulimuli. Simama uione”
Mapama akainuka na kuitazama ile boti kwenye kioo. Nilidhani angeanza kubabaika kama nilivyokuwa nikibabaika mimi. Badala yake nilimuona akiizima boti na kujipekua mifukoni. Alitoa burungutu la pesa za Kenya akalishika mkononi.
“Usiogope” akaniambia na kuongeza.
“Watakwenda zao sasa hivi”
Ile boti ya polisi ikatufikia. Ikawa ubavu kwa ubavu na boti yetu. Mapama akalirusha lile burungutu la noti kwenye ile noti. Polisi mmoja akalidaka. Hapo hapo nilimsikia akisema.
“Safari njema”
Mapama akaiwasha boti. Tukaendelea na safari. Ile boti nayo ikaelekea upande mwingine.
“Wale wanataka pesa tu” Mapama akaniambia na kuongeza.
“Kila tunapokuja huku tajiri wetu anatupa pesa maalum kwa ajili ya kuwapa polisi wa Kenya wanaofanya doria baharini. Wao wenyewe wanajua, wakiiona hii boti wanafuata pesa tu. Hawakagui kitu”
“Mimi nilikuwa na wasiwasi sana. Nilijua tutaishia polisi”
“Hapana. Hizi ni kazi zetu za kila siku, lazima tujuane na polisi. Huwezi kuvuka kwenda Somalia bila kukupamba nao”
“Kile kimulimuli kilinitisha kweli”
“Ile ni mikwara tu ya kutaka pesa. Hebu iangalie kama utakiona tena kimulimuli”
Nikatazama upande ule ilikoelekea ile boti. Sikuona kimulimuli wala sikuiona boti yenyewe.
“Boti yenyewe haionekani tena”
“Ni kwa sababu wamekizima kimulimuli”
“Huko Somali itakuwaje sijui?”
“Hakuna tatizo. Huyo tunaempelekea huu mzigo ni mtu mzito sana. Serikali pia inamjua”
Baada ya hapo tukabaki kimya.
Hatimaye aflfajiri ilianza kuchomoza. Sikuona dalili yoyote ya kufika Somalia. Usingizi ukaanza kuniuma.
“Uliniambia tutaingia Somalia wakati wa alfajiri” nikamwambia Mapama.
“Bado kidogo, usiwe na wasiwasi”
“Nasikia usingizi” nikamwambia.
“Lala kidogo”
Nikajilaza pale chini. Usingizi ukanichukua hapo hapo.
Mpaka nakuja kuzinduka lilikuwa jua la utosi. Mapama ndiye aliyeniamsha. Boti ilikuwa imesimama na kulikuwa na boti nyingine kubwa iliyokuwa imesimama kando ya ile boti tuliyokuwamo. Ilikuwa boti kubwa na nzuri.
“Tumeshafika?” nikamuuliza Mapama.
Sikujua kabisa kuwa Mapama angenigeuka na kunisaliti kwa magaidi..
Bila shaka, zile boti ndio zilikuwa zimekutana. Ile boti ya pili ilikuwa ndiyo ile ambayo Mapama aliniambia tutakutana nayo tutakapoingia Somallia ili ifaulishe ule mzigo wa pembe za ndovu.
Wakati ule namuuliza Mapama kama tumeshafika, niliona mtu mmoja akitoka katika boti ile ya pili na kuingia katika boti ya Mapama. Alikuwa kijana. Ingawa alikuwa mwembamba alionekana kunawiri na alivaa mavazi yalliyompendeza japo shati alilovaa lilionekana kubwa kutokana na wembamba wake.
Alikuwa Msomali mweusi mwenye nywele za singa. Mkono mmoja alikuwa ameshika kichanga cha mirungi aliyokuwa akitafuna na mkono mwingine alishika sigara iliyokuwa ikifuka moshi.
Katika kiganja cha mkono wake wa kushoto alivaa pete kubwa iliyokuwa inang’ara.
Niliukadiria umri wake kutozidi miaka thelathini na mitano. Alikuwa amenizidi kiumri kidogo.
Kijana huyo alisalimiana na Mapama aliyekutana naye nje ya kile kijichumba nilichokuwemo. Nilimshangaa Mapama kwa jinsi alivyokuwa ametaharuki kiasi kwamba alipuuza hata kunijibu nilipomuuliza kama tumeshafika. Alikuwa amebadilika kabisa. Niliona kama hakuwa mwenzangu tena.
Aliposalimiana na yule msomali alimuonesha ule mzigo wa Pembe. Msomali huyo aliutazama kisha akamuuliza.
“Wenzako wako wapi?”
“Nilikuja nao lakini tulipata matatizo makubwa”
“Matatizo gain?”
“Nitakueleza. Wambie jamaa wafaulishe huu mzigo”
Msomali huyo alitumia lugha ya kisomali kuwambia wasomali wenzake waliokuwa katika ile boti ya pili waingie katika boti ya Mapama na kufaulisha ule mzigo. Wasomali hao walioonekana kama wapagazi wakaingia na kuanza kazi.
Mapama na yule msomali niliyemdhania kuwa ndiye tajiri wa ule mzigo wakaingia katika ile boti nyingine. Sikujua walikwenda kuzungumza nini. Baada ya muda Mapama alirudi peke yake na kuniambia.
“Yule jamaa anataka kukuona?”
“Jamaa gani?” nikamuuliza.
“Yule msomali niliyekuwa nazungumza naye”
“Kwani mimi nahusikaje?”
“Sasa utakwenda au utaleta ubishi?” Mapama akaniuliza kwa ukali.
Kabla sijamjibu, Msomali mwenyewe akatokeza kwenye ile boti na kuninyooshea mkono kama ishara ya kuniita, nikaenda. Niliingia katika ile boti akanishika mkono na kuniingiza katika chumba kilichokuwa katika boti yake.
Chumba hicho kilikuwa kikubwa kuliko cha boti ya Mapama na kilikuwa kizuri kilichozungukwa na kuta za vioo. Ndani kilikuwa na sehemu ya kulala na makochi ya kukalia.
“Karibu, kaa hapo” Msomali akaniambia akinionesha moja ya makochi yaliyokuwa katika kile chumba.
Nikakaa.
“Asalaam alaykum” Msomali akaniambia huku akiketi upande wa pili wa chumba hicho.
“Waalaika Salaam” nikamjibu kwa sauti iliyonywea huku nikimtazama usoni kwake.
“Nimeelezwa na Nahodha kuhusu wewe na mkasa uliowatokea mlipokuwa mnakuja. Ameniambia kulitokea joka kama nondo na kuwaangamiza wenzake, ni kweli?”
“Ni kweli”
“Kwani walitaka kukufanya nini?”
“Walitaka kuniua”
“Wapumbavu wale, mtu unaomba msaada wanataka kukuua. Sasa hilo joka lilitoka wapi?”
Nikabetua mabega yangu.
“Sijui”
“Bila shaka hilo ndilo lililokuokoa usiuawe, ungekuwa umeshatoswa na kuliwa na papa”
Hapo sikumjibu kitu.
“Wewe unaitwa Umar?” Msomali akaniuliza.
“Hapana”
“Unaitwa Amiri?”
“Hapana”
“Basi utakuwa unaitwa Amour”
Nikamkubalia.
“Ndio naitwa Amour, umejuaje?”
Msomali huyo akacheka. Badala ya kunijibu akaniambia.
“Nataka twende Somali mara moja”
Nikashituka na kumuuliza.
“Kwani hapa tuko wapi?’
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapa ni Somalia, nina maana nataka twende Mugadishu”
“Kufanya nini?”
“Nitakuwa na kazi na wewe”
“Mimi nataka kurudi. Nilishamwambia Nahodha akishafaulisha mzigo wake turudi”
“Sasa amri ni yangu mimi si ya Nahodha. Mimi nataka twende Mugadishu”
“Mimi sitakwenda huko”
Msomali huyo hakunisikiliza akainuka na kutoka katika kile chumba. Na mimi nikainuka na kumfuata.
Alipoona nimetoka alihamaki akaniuliza.
“Unataka kuleta ubishi?”
“Hapana”
“Nani amekuamrisha utoke?”
“Nilikwambia sitakwenda Mugadishu, nahitaji kurudi”
Msomali huyo hakusema kitu tena, alitia mkono ndani ya shati lake akatoa bastola na kunielekezea.
“Sasa chagua moja, nikutoe roho au baki kwenye hii boti!” akaniambia kwa hasira.
Nikanywea hapo hapo.
“Nenda kakae”
Ikabidi nirudi kwenye kile chumba. Nilijua kama nitaendelea kubishana naye anaweza kuniramba risasi. Wasomali hawa hawana huruma, kuna wengine hawana utu kabisa.
Nikakaa kinyonge kwenye kohi huku macho yangu yakimtazama yule Msomali kwa macho ya kulaani. Nikamuona mapama akiingia kwenye ile boti.
Akasimama na yule Msomali na kuzungumza naye kwa kirefu. Sikuweza kusikia walichokuwa wanazungumza. Mara moja moja Mapama alikuwa akinitazama. Nilikuwa nikimuonesha ishara ya kumuita ili nimuulize mbona ananigeuka.
Lakini Mapama licha ya kuona kuwa nilikuwa ninaashiria kumuita hakunijali hata chembe.
Pembe za ndovu zilikuwa zikiendelea kingizwa kwenye boti hiyo. Kazi ilipokwisha, Msomali aliingia katika kile chumba akafungua dawati mojawapo na kutoa mfuko ambao alitoka nao.
Ule mfuko ulikuwa na pesa. Sikujua zilikuwa pesa za wapi isipokuwa niliona Msomali akitoa vitita vya noti na kumhesabia Mapama. Mapama naye alizitia pesa hizo kwenye mfuko wa ngozi aliokuwa ameushika kisha nikaona wanaagana kwa furaha.
Hapo ndipo nilipotoa sauti nikamuita.
“Nahodha!”
Nilimuita zaidi ya mara tatu lakini hakunipatiliza akatoka kwenye ile boti na kuingia kwenye boti yake. Yule Msomali akaingia kwenye kile chumba. Bastola yake ilikuwa bado mkononi ingawa aliishika kwenye mtutu.
Boti ya Mapama ikawashwa moto. Nikajua kuwa Mapama alikuwa ameshaniuza kwa wasomali hao. Kwa lugha nyingine ilikuwa sawa na kusema kuwa Nilikuwa nimetekwa nyara na kupelekwa mahali bila hiyari yangu.
Boti ya Mapama ikaondoka, ilikata kona ndefu na kugeuka ilikotoka. Nikaachwa mikononi mwa wasomali.
Nilikuwa nimetaharuki na akili yangu iliniruka. Boti ya wasomali ikawashwa, nayo ikaondoka kuelekea Somalia.
Sikujua Mapama alikuwa amezungumza nini na yule msomali na pia sikujua walikuwa wananipeleka Somalia kwa ajili gani.
Pia nilikuwa nimeshangazwa na jinsi msomali huyo alivyolitambua jina langu ambalo sikuwahi kumtajia hata Mapama.
Kijana huyo wa kiosamali alikuja kukaa kando yangu na kuendelea kutafuna mirungi yake. Bastola yake aliipachika kiunoni. Bila shaka alifanya hivyo mbele yangu ili kunionya nisimletee ukaidi.
Lakini ukiacha muda ule aliponichomolea bastola hiyo ambapo alionesha kukasirika, uso wake ulikuwa wa kirafiki wakati wote.
“Mimi naitwa Abdi” akaniambia wakati akiendelea kutafuna mirungi kisha akaniuliza.
“Unakula mirungi?”
Nikatikisa kichwa. Mdomo ulikuwa mzito kumjibu.
“Najua wewe ni mzaliwa wa Tanga lakini sijui unaishi sehemu gani?” akaniuliza.
Swali lake hilo nalo lilinishangaza. Alijuaje kuwa mimi ni mzaliwa wa Tanga?
“Ninaishi sehemu inayoitwa Msambweni” nikamjibu.
“Wazazi wakao wako wapi?”
“Baba yangu alikwishakufa, mama yangu ndio yupo”
Msomali huyo alinikubalia kwa kichwa.
“Unafanya shughuli gani?”
“Nimeajiriwa katika shirika moja linaloitwa CTC”
“Najisikia ni mwenye furaha sana kukutana na mtu kama wewe”
“Umelitambuaje jina langu pamoja na mahali nilipozaliwa?” nikamuuliza.
Badala ya kunijibu aliangua kicheko.
“Nilikuwa nakisia tu kumbe nilipatia”
“Haiwezekani ukisie halafu iwe sawa”
“Amour sina jibu jingine la kukupa kwa sasa”
“Uliwahi kufika Tanga?”
Abdi akatikisa kichwa.
“Sijawahi”
“Kwanini unalazimisha twende Somalia?”
“Ni kwa sababu za kiudugu na kiurafiki tu. Utakuwa huko kwa muda tu halafu utarudi kwenu na kama utapenda kuendelea kuishi huko huko nitakupatia nyumba, kazi na gari”
“Kwa vyovyote vile itabidi nirudi, mama yangu na ndugu zangu hawajui niko wapi”
“Basi utarudi”
Boti iliendelea kusonga mbele. Baada ya mwendo wa kilometa tano hivi tukakutana na meli iliyokuwa imetia nanga. Boti ilikwenda kusimama ubavuni mwa meli.
Abdi aliniacha akatoka kwenye kile chumba. Kuna ngazi iliyoshushwa kutoka kwenye meli. Abdi alipanda ngazi hiyo akaingia ndani ya meli. Baada ya muda kidogo alishuka akiwa na maafisa wawili wa meli hiyo ambao niliwatambua kutokana na mavazi yao.
Waliyakagua yale meno ya tembo kisha nikaona krini ya meli inashushwa kutoka kwenye meli. Yale meno ya tembo yalikuwa yamepangwa kwenye turubai. Turubai hilo lilikuwa na vipete vinne vilivyowekwa kwenye pembe nne za turubai hilo. Kamba ikapitishwa kwenye vipete hivyo kisha ikapachikwa kwenye mkono wa krini.
Turubai likavutwa juu pamoja na pembe zake. Zilivutwa juu kuupita usawa wa meli kisha zikaingizwa ndani ya meli.
Abdi pamoja na wale maafisa wawili wa meli walirudi melini. Walipoteza muda wa karibu saa nzima kabla ya Abdi kurudi akiwa peke yake.
Aliingia kwenye kile chumba akiwa na mfuko uliotuna ambao aliuweka kwapani. Akafungua dawati mojawapo na kuuweka.
“Hizi ni pesa” akaniambia bila kumuuliza.
Sikumjibu kitu. Akarudi kuketi pale alipokuwa.
“Zile pembe zinakwenda Oman kwa waarabu” akaniambia lakini mimi bado nilikuwa kimya. Kitendo kile cha kunipaleka Mogadishu kwa lazima kilikuwa kimenifadhaisha sana.
Sikuwa nimeamini zile sababu zake kwamba alinipeleka kwa sababu za kiudugu na kiurafiki. Sikuwa na udugu naye wala urafiki naye na hatukuwa tukijuana zaidi ya kukutana siku ile.
Nilihisi kuna kitu ambacho alizungumza na Mapama ndio wakapanga niende Mogadishu. Sasa sikujua kama walikuwa wanakwenda kuniua au kunifanya nini.
Wakati niko katika lindi la mawazo nilianza kuona mataa kwa mbali. Ilikuwa ni bandari ya Mogadishu. Tulifika katika gati moja boti ikasimama.
Abdi akasimama alifungua dawati akauchukua ule mfuko wake wa pesa akaniambia.
“Tushuke”
Tulishukia kwenye gati. Tulikuta gari ndogo ya kifahari ya rangi nyekundu ikitusubiri.
Abdi alifungua mlango wa nyuma wa gari hilo akaniambia nijipakie. Nikajipakia.
Yeye alifungua mlango wa mbele kando ya dereva akajipakia. Gari ikaondoka.
“Tunakwenda wapi?” Mtu aliyekuwa akiendesha alimuuliza Abdi tulipoingia kwenye mitaa.
“Nipeleke hotelini kwangu nikamuweke mgeni wangu halafu utaniachia gari”
Hapo ndipo nilipoliona na kulijua jiji la Mugadishu. Ilikuwa ni kabla ya serikali ya Somalia ya Rais Siad Barre kupinduliwa na kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoendelea hadi leo hii na kuzua vikundi vya kigaidi.
Jiji lilikuwa zuri na la kisasa. Nililifananisha sana na jiji la Nairobi ambalo niliwahi kufika.
Baada ya kupita katika barabara kadhaa, gari hilo lilisimama mbele ya hoteli moja iliyokuwa na ghorofa tano.
“Zima gari unipe funguo” Abdi alimwambia dereva wa gari hilo ambaye alilizima gari na kuchomoa funguo akampa Abdi.
“Utatumia ile gari nyingine” Abdi alisema huku akifungua mlango wa gari na kushuka.
“Amour shuka twende nikakupatie chumba”
Abdi aliniambia huku akivuta hatua kuelekea kwenye mlango wa hoteli hiyo.
Nikafungua mlango wa gari hilo na kushuka, nikamfuata Abdi Msomali.
“Hii ni hoteli yangu” akaniambia na kuongeza.
“Inaitwa Handeni Hotel”
Alipotaja jina ‘handeni’ nilishituka kidogo kwa sababu Handeni ni moja ya walaya za mkoa wetu wa Tanga.
“Inaitwa Handeni au sikukusikia vizuri?” nikamuuliza.
“Inaitwa Handeni, pia ndio jina la eneo hili tuliopo”
“Handeni ni moja ya wilaya za mkoa ninaotoka mimi”
“Ninajua. Niliwahi kusikia kuwa Wasomali wanaoishi katika eneo hili wana asili ya kizigua. Ninajua kwamba Wazigua wako Handeni au nimekosa?”
“Ni kweli. Hata mimi ni mzigua”
“Basi hapa utakutana na ndugu zako”
“Lakini ndugu zangu hao ni Wasomali?”
“Ndio ni Wasomali kama mimi lakini babu zao walitokea Handeni miaka mingi iliyopita”
“Nimekuelewa”
SASA ENDELEA
“Kama usingefika hapa ungeijuaje historia?”
“Kwa kweli nisingeijua”
Tulikuwa tumeshaingia ndani ya jingo hilo la hoteli. Tulikwenda mapokezi ambapo niligundua msomali huyo alikuwa akiheshimiwa sana na wafanyakazi wa hapo.
“Nipatieni chumba kimoja” alimwambia mmoja wa wahudumu wa mapokezi huku akiegemea kaunta hiyo.
Mhudumu huyo ambaye alikuwa msichana wa kisomali aliyekuwa amevaa sare ya koti jeusi na sketi alichukua kitabu cha wageni na kukifungua.
“Niandike jina gain bosi?” akamuuliza Abdi kwa nidhamu huku akishika kalamu.
“Niandike mimi mwenyewe” akamwambia.
“Nitumie jina gani?”
“Una maana hujui ninaitwa nani?”
“Samahani bosi, ninalijua jina lako”
Msichana aliandika kwenye kitabu hicho kisha akainua uso wake na kumtazama Abdi.
“Niandike chumba cha daraja gani?”
Abdi akanitazama. Bila shaka alikuwa akinipima kama ninastahili chumba cha daraja gani.
“Mpatie chumba cha daraja la kwanza”
Mhudumu aliandika kisha akanitazama mimi.
“Ungependa ukae ghorofa ya ngapi?”
“Ghorofa ya kwanza au ya pili”
“Nitakupatia ghorofa ya kwanza”
Msichana alijaza kwenye kitabu kisha akamtazama Abdi.
“Mgeni atakaa kwa siku ngapi”
Abdi akanitazama tena kisha akamjibu.
“Hapo paache tu…”
Msichana akageuka na kuchukua funguo.
“Nimekupatia chumba namba 85 ghorofa ya pili” akaniambia.
Sikumjibu kitu kwa sababu hicho chumba sikukitaka mimi.
“Mpeleke” Abdi akamwambia.
“Twende nikakuoneshe chumba chako” Msichana akaniambia.
Alitoka nyuma ya kaunta akaelekea kwenye ngazi.
“Mfuate akakuoneshe chumba utakachokaa” Abdi akaniambia.
Nilimfuata yule msichna. Wakati anapanda ngazi nilikuwa nyuma yake. Niliuona mwili wake. Ulikuwa wa kuvutia. Alikuwa na umbo lililofinyangwa kisomali hasa..
Nilifuatana naye hadi ghorofa ya kwanza. Akanionesha chumba namba 84. Akakifungua na kuingia ndani pamoja na mimi.
Baada ya kukiona chumba hicho msichana alitoka na kuniacha. Kwa vile sikuwa nimepata maelezo yoyote kutoka kwa Abdi na mimi nikatoka. Nilifunga mlango nikashuka ngazi.
Nilimkuta Abdi akinisubiri mapokezi.
“Umekiona chumba?” akaniuliza.
“Nimekiona”
Akamgeukia mhudumu wa mapokezi.
“Mtakuwa mnamuhudumia kwa kila kitu muda wote atakaokuwa hapa. Mtampatia chai ya asubuhi, chakula cha mchana na cha jioni, vinywaji na kila kitu atakachohitaji ikiwa ni pamoja na kufua nguo zake na kuzipiga pasi. Bili itakuwa juu yangu” akamwambia.
“Sawa bosi, tumekuelewa”
Abdi akanitazama.
“Twenzetu” akaniambia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sikujua aliniambia twenzetu wapi lakini kwa vile nilishakuwa kama mateka wake sikumuuliza kitu nikamfuata.
Tulitoka nje ya hoteli tukajipakia kwenye gari lake na kuondoka.
Tukiwa ndani ya gari nilitarajia angeweza kuniambia tunakwenda wapi lakini hakuniambia kitu. Nilimuona alikuwa katika lindi la mawazo. Sikujua alichokuwa akiwaza.
Baadaya kukata mitaa miwili mitatu alilisimamisha gari mbele ya jingo moja
la ghorofa lililokuwa na maduka makubwa. Akaniambia tushuke.
Tukashuka na kuingia katika duka mojawapo. Wakati tunaingia aliniambia.
“Hili pia ni duka langu”
“Ahaa…kumbe pia una maduka?” nikamuuliza.
Licha ya kwamba nilikuwa na fadhaa kwa kutojua hatima yangu, nilijaribu kujichangamsha na kuzungumza naye kwa vile alionesha kama ananijali.
“Sina maduka, nina duka moja tu” akaniambia.
Tulipoingia ndani ya duka hilo nililiona lilikuwa duka kubwa la nguo za wanaume. Kulikuwa na suti, mashati, fulana, suruali na aina kadha wa kadha ya nguo za kiume.
“Angalia nguo unazopenda, upate nguo za kubadili” akaniambia.
Ilikuwa kweli nilihitaji kubadili nguo. Licha ya kuwa sikuwa na nguo za kubadili, zile nilizovaa zilikuwa zimechafuka na zilikuwa zinanitia aibu.
Nikachagua nguo. Nilichukua shati moja
na suruali moja pamoja na viatu na soksi.
“Ongeza” Abdi akaniambia.
Nikaongeza shati moja.
Abdi akanichagulia mashati mengine matatu.
“Ongeza suruali tatu” akaniambia.
Nikachagua suruali zingine tatu, nikawa na suruali nne.
Abdi akaniita upande uliokuwa na suti.
Nilipokwenda alinaiambia.
“Mimi napenda sana kuvaa suti na wewe chagua suti moja ya kuvaa”
Nikatabasamu. Ilikuwa ni mara ya kwanza kukunjua uso wangu tangu ile boti tuliyokuwa tukisafiria kutoka Pemba ilipozama.
Abdi alipoona natabasamu akacheka.
“Chagua suti moja au nikuchagulie mimi?” akaniuliza.
Kabla sijamjibu alishachomoa suti moja ya rangi ya kijivu.
“Chukua hii” akaniambia.
Nikaichukua ile suti.
“Nenda kajaribu hizo nguo kwenye kile chumba pale” akaniambia huku akinionesha mlango wa chumba hicho.
Nikaingia kwenye hicho chumba. Unapoingia katika chumba hicho unajiona mwenyewe kwani kilikuwa na vioo vitupu. Nilizijaribu nguo zote na kuona zilikuwa sawa.
Nilipotoka katika chumba hicho nilimwambia Abdi.
“Bado viatu na soksi”
“Kachague jozi mbili za viatu na soksi” akaniambia.
Nikaenda kuchukua jozi mbili za viatu na jozi mbili za soksi.
Abdi alinifuata na kuninong’oneza.
“Chukua na chupi kumi”
Aliponiambia hivyo sote tukacheka.
Baada ya kufanya manunuzi hayo ambayo Abdi aliyalipia kwa dola za Kimarekani tuliondoka kwa gari. Tulirudi kule hoteli ambako Abdi aliniacha.
“Nitakupitia baadaye” aliniambia wakati nikishuka kwenye gari. Alinyamaza kidogo kisha akaongeza.
“Najua utahitaji kujiweka vizuri kidogo na pia kupata chakula kizuri”
“Ndio. Nahitaji vyote hivyo”
“Kwa upande wa chakula nimeshaagiza utakula unachopenda”
“Sawa”
“Mimi naondoka kidogo, nitakupitia baadaye”
Abdi akatia gea gari lake na kuondoka.
Niliingia hotelini nikiwa na begi langu lililokuwa na nguo. Mhudumu mmoja alioniona aliniekea lile begi akapanda ngazi na kwenda kunisubiri kwenye mlango wa chumba changu.
Nilipofika nilifungua mlango nikamwambia.
“Karibu ndani”
Alikuwa msichana mweupe wa kisomali mwenye mwili wa kutamanisha.
Msichana alitabasamu akaliingiza lile begi chumbani kwangu kisha akaniaga
na kutoka.
Sikujua kama wasomali walikuwa wanazungumza Kiswahili. Pale hotelini niligundua baadhi ya wasomali walikuwa wanajua kuzungumza Kiswahili tena Kiswahili cha kipwani kilichonyooka.
Nilipobaki mle chumbani nilivua nguo nikaenda kuoga. Niliotoka bafuni nilivaa ile suti mpya aliyoninunulia Abdi. Nikajitazama kwenye kioo na kuona nilipendeza. Angalau ilinisahaulisha madhila niliyokuwa nayo moyoni.
Baada ya kuvaa nilishuka chini nikaingia katika eneo la mkahawa. Yule mhudumu aliyeniokea begi alinifuata.
Akanisemea kwa kisomali.
“Sijui hiyo lugha labda mnifundishe” nikamwambia.
“Unajua Kiswahili peke yake?” akaniuliza.
“Na kizigua”
“Unatoka Handeni Tanzania?”
“Umejuaje”
“Kule ndio kuna wazigua”
“Nasikia na nyinyi pia mna asili ya huko”
“Babu zetu wametoka huko lakini mimi unaniona mweupe mama yangu ni mbarawa”
“Mmejifundisha Kiswahili?”
“Mimi nilizaliwa Garisa nchini Kenya, kule watu wanazungumza Kiswahili. Wenzangu wengine wametoka Mombasa”
“Nashukuru kwa mazungumzo, ninahitaji chakula”
“Upatiwe menyu?”
“Kwani wewe si ndiye unayehusika”
“Mimi pia nahusika lakini kuna mhudumu maalum wa hapa. Ngoja nimuite”
Shamsa akamuita msichana mmoja na kumwambia.
“Mgeni wa bosi. Bosi ameagiza apatiwe kila atakachohitaji. Bili itakuwa juu yake”
“Sawa” Msichana alimkubalia kisha akaniuliza.
“Nikupatie menyu?”
“Ndio nipatie”
Menyu alikuwa anayo mkononi, akaniwekea juu ya meza.
Nikaishika na kutazama orodha ya vyakula. Nikachagua wali kwa samaki na juisi.
Wasichana wote wawili waliondoka na kuniacha.
Baada ya muda kidogo nililetewa chakula nilichoagiza. Wakati nakula nilianza kujiwazia mustakbali wangu kule Somalia. Nilijiuliza Abdi alikuwa na madhumuni gani kunichukua mimi Somalia, kuniweka hoteli na kunihudumia kama rafiki yake wakati tulikuwa hatujuani.
Pia nilijiuliza ningekaa Somalia hadi lini. Ingawa niliingia kienyeji lakini wakati ule Somalia ilikuwa na serikali. Nilitakiwa kuwa na paspoti. Nilijiambia kama ningekamatwa nitakuwa na kosa la kuingia nchi ya watu bila paspoti.
Nilishindwa kumuuliza Abdi kuwa ningekaa hapo Somali kwa siku ngapi, hasa nikikumbuka muda ule alionitolea bastola kwa kumhoji niende Somalia kufanya nini.
Niliogopa kuwa ningeweza kumkasirisha na hivyo akanipiga risasi na kwenda kuutupa mwili wangu jalalani. Mtu mwenyewe licha ya kuwa mchangafu, mkarimu na anayependa kutabasamu, alionekana kuwa katili na asiyejali kitu.
Mtu wa aina yake kuua ni kazi ndogo tu!
Nilipomaliza kula niliondoka nikarudi ghorofani. Niliingia chumbani nikaenda kusimama kando ya dirisha na kutazama mandhari ya nje.
Niliendelea kusimama hapo nikiangalia magari na watu waliokuwa wakipita barabarani huku akili yangu ikitafuta jibu la kwanini niko pale Somalia lakini sikupata jibu.
Nilipitisha kama nusu saa nikiwa hapo, nikaingia chumbani na kuvua koti kisha nikajilaza kitandani.
Nilikuwa nina uchovu na nilikuwa na usingizi. Kwa vile moyo wangu kidogo ulikuwa umetulia nikaona naweza kulala.
Na nililala. Nilipokuja kuzinduka niliona giza. Ilikuwa ni usiku. Kwa vile sikuwa na saa sikuweza kujua ilikuwa ni usiku wa saa ngapi.
Nikainuka kitandani na kuwasha taa. Pale mchagoni mwa kitanda palikuwa na simu. Nikainua mkono wa simu na kuzungumza na opereta.
“Abdi ameshafika?” nikamuuliza.
“Wewe nani?”
“Mimi ni mgeni wake, niko ghorofa ya kwanza”
“Alifika, akakupigia simu lakini haikupokelewa akajua umelala”
“Sasa yuko wapi?”
“Ameshaondoka, ametuambia tukuambie kuwa mtakutana asubuhi”
“Ni saa ngapi sasa?”
“Saa mbili inakwenda kwenye na nusu”
“Nitashuka sasa hivi kuja kupata chakula”
“Sawa, chakula kipo”
Nikauweka mkono wa simu mahali pake na kuvua nguo. Nilikwenda kuoga tena.
Nilipomaliza nilirudia kuvaa suti yangu kisha nikashuka chini. Niliingia katika ukumbi wa mkahawa wa hoteli hiyo.
Mhudumu aliponiona tu akanifuata na kunipa menyu.
“Nahtaji chai tu” nikamwambia.
“Chai na nini?”
“kama kuna sambusa nipatie tatu”
Mhudumu aliondoka. Baada ya muda kidogo alirudi akiwa na chano kilichokuwa na kisahani kilichokuwa na sambusa tatu, birika ndogo ya maziwa, kipakiti cha majani ya chai, jagi la sukari na kikombe kitupu kikiwa na kisahani chake.
Aliniwekea juu ya meza. Nikachukua birika na kumimina maziwa kwenye kikombe nikatia kijiko kimoja na nusu cha sukari na kukoroga.
Baada ya sukari kukolea, nilitumbukiza kile kipakiti cha majani ya chai ambacho kiliyafanya maziwa kuwa na rangi ya chai.
Nilitumia nusu saa nzima kunywa chai huku nikijiwazia. Mpaka muda ule sikuwa nimeitambua dhamira ya Abdi.
Nikajiambia baada ya siku tatu nitamwambia kuwa nahitaji kuondoka kurudi kwetu kwani sikuwa na sababu yoyote ya kuendelea kukaa Somalia huku ndugu zangu na mama yangu wakiwa hawajui niliko.
Baada ya kumaliza kunywa chai nilikwenda kujipumzisha kwenye eneo la wazi la hoteli ambapo palikuwa na upepo mwanana kutoka Bahari ya Hindi.
Pale nilipoteza dakika kadhaa kabla ya kuamua kurudi chumbani kwangu.
Mawazo ya Zena yalinijia usiku ule. Nikajiambia msichana wa kijini aliamua kunisaliti kwenye kile kisiwa baada ya kukataa kuoana naye.
Kitendo cha kutoonana tena na Zena kilinipa picha kwamba Zena aliamua kuachana na mimi.
Nikajiambia kama kweli alikuwa ameamua hivyo lilikuwa jambo la kushukuru sana kwani msichana yule alikuwa ananisababishia matatizo makubwa.
Baada ya kuwaza sana nilipitiwa na usingizi. Sikujua nililala kwa muda gani lakini nilihisi kama nilishituka katikati ya usiku au nilikuwa katika ndoto. Nikaona kama mlango wa chumba nilichokuwa nimelala unafunguliwa taratibu.
Kitendo hicho kilitokea nikiwa na kumbukumbu kamili kichwani mwangu kwamba mlango wa chumba hicho niliufunga kwa ndani na kuhakikisha kuwa ulikuwa umefungika.
Mlango ulipokuwa wazi nilimuona mtu akiingia. Alikuwa mzee mwembamba na mrefu. Wembamba wake ulichanganyika na kukonda. Alikuwa na nywele ndefu, nyeupe tupu.
Alikuwa amejifunga shuka nyeupe kiunoni na mabegani alijitanda shuka nyingine nyeupe kuziba kifua na tumbo lake. Hata hivyo upande mmoja wa kifua chake ulikuwa ukionekana. Mbavu zake zilikuwa zimetokeza na kuhisabika.
Akaingia mle chumbani kwa kunyata. Wakati akiingia nilikuwa nikijiuliza nilikuwa ninaota au nilichokuwa nakiona kilikuwa ni kweli.
Muda huo niligundua kuwa sikuwa sawa. Nilikuwa kama niliyepatwa na jinamizi. Mwili wangu haukuwa na uwezo wa kufanya chochote hata kupiga kelele.
Kadhalika akili yangu ilikuwa imepoteza uwezo wake na nilikuwa kama taahira au zezeta. Sikuweza kujua ni kwanini nilijihisi kuwa vile.
Yule mzee wa kisomali alikuja hadi karibu na kitanda nilichokuwa nimelala.
Nilimuona vizuri. Alikuwa na pua ndefu na macho makali na madogo. Akasimama na kuniita.
“Amour!”
Nikanyamaza kimya. Nikamuona anasema maneno fulani kwa lugha ya kisomali kisha akanyoosha mkono wake na kupapasa kitanda nilichokuwa nimelalaa akashika mkono wangu na kuubana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliubana kwa nguvu nikaona kama nilishikwa kwa koleo.
“Inuka” akaniambia.
Kwa sababu nilikuwa kama taahira nisiyejielewa nikainuka kweli.
“Shuka kwenye kitanda” akaendelea kuniambia.
Nikashuka kwenye kitanda. Nilikuwa nimevaa chupi tu. Akaichukua ile shuka aliyoitanda mabegani mwake akanifunga nayo kiunoni kisha akanishika tena mkono na kuniambia.

0 Comments