“Kwanza nataka tukubaliane kitu kimoja”
“Kitu gani?”
“Utakikubali?”
“Nitakikubali, niambie ni kitu gani?”
“Nikupeleke kwetu ujinini tukaithibitishe ndoa yetu kabla ya kurudi Tanga”
“Sasa tutakwendaje huko Ujinini wakati tutakapotoka tu ninakamatwa na polisi?”
“Mimi ndiye ninayejua, wewe kubali tu ninachokwambia”
“Mimi nimeshakubali”
Mlango uliendelea kugongwa.
“Hawa wako ndani wanatusikia lakini wanaleta jeuri” Tukaisikia sauti ya polisi mmoja akiwambia wenzake nje ya mlango.
“Basi acha tuvunje mlango” Tukasikia sauti nyingine ikisema.
“Zena mlango unavunjwa!” nikamwambia Zena kwa hofu.
Zena akanyanyuka na kuniambia.
“Na wewe nyanyuka ushike hayo mabegi yako”
Nikayachukua yale mabegi mawili, moja nililipachika begani kwangu na moja nililishika mkononi.
Zena naye akalipachika begani begi lake.
Sasa mlango ulikuwa unavunjwa!
“Njoo usimame sambamba na mimi”
Nikajisogeza kwake na kuwa naye bega kwa bega.
Zena akachora msitari kwenye sakafu kutoka kulia kwenda kushoto. Ulianza kwenye usawa wake ukafika hadi kwenye usawa wangu.
Baada ya hapo alinishika mkono akaniambia.
“Fumba macho yako”
Nikafumba macho.
Sasa mlango ulikuwa umeshavunjwa na kufunguka.
Nikaona polisi wakiingia kwa vishindo.
“Piga hatua haraka uvuke huo mstari niliouchora hapo chini” Zena akaniambia.
Nikainua mguu wangu wa kulia kwa haraka na kupiga hatua kuuvuka mstari huo kabla ya wale polisi kutufikia.
“Sasa fumbua macho yako” nikasikia sauti tulivu ya Zena ikiniambia.
Nikafumbua macho yangu. Kama ni mshangao, mshangao nilioupata hapo haukuwa na mfano!
Hatukuwa tena kwenye kile chumba cha hoteli. Tulikuwa ufukweni mwa bahari! Sikuweza kujua mara moja tulikuwa kwenye ufukwe wa bahari gani.
Ulikuwa ufukwe wenye mchanga mweupe na mbele yetu kulikuwa na msitu ulioshiba. Nyuma yetu ndio kulikuwa na bahari.
Jua lilikuwa limekuchwa likitoa mionzi ya rangi ya kimanjano iliyokuwa ikimemeta baharini nyuma yetu.
Sikuweza kutambua mara moja tulikuwa katika ufukwe wa nchi gani uliokuwa ukipendeza kiasi kile. Ufukwe huo ulikuwa kimya na hakukuwa na chombo chochote kilichokuwa kikionekana baharini.
“Tuko wapi hapa?” nikamuuliza Zena.
“Ufukweni mwa bahari”
“Bahari ya wapi?”
“Bahari ya kwetu ujinini”
“Mbona tumefika mara moja”
“Kawaida. Lakini nilikukimbiza wewe usikamatwe na wale polisi”
“Itakuwa bado wako mle chumbani?”
“Wapo wanashangaa shangaa lakini wameambilia matupu”
Mabegi tuliyokuwa tumechukua tulikuwa nayo vile vile. Begi langu moja lilikuwa begani na jingine lilikuwa mkononi. Na begi alilokuwa amelishika Zena alikuwa bado analo.
Nilitupa macho yangu kwenye ule msitu uliokuwa mbele yetu kisha nikamuuliza Zena.
“Tunaelekea upande gani?”
“Huko unakoona msitu”
“Huko ndiko kuna mji wenu?” nikamuuliza.
“Mji uko huko. Twende”
Kusema kweli wakati wote nilikuwa nimejikaza kiume lakini nilianza kupata hofu tangu Zena aliponiambia kuwa pale tulikuwa katika ufukwe wa ujinini.
Pengine ningemuuliza ujinini ipo upande gani katika ramani ya dunia. Katika kusoma kwangu Jeografia kuanzia shule ya Msingi hadi Sekondari sikuwahi kuiona ramani ya ujinini katika upande wowote wa dunia.
Lakini niliona swali hilo halikuwa na umuhimu wa kuliuliza wakati ule. Kama kulikuwa na umuhimu ulikuwa ni kumuuliza tulifika pale kwa usafiri wa aina gani? Kama usafiri wenyewe ulikuwa haueleweki hata hiyo ramani ya ujinini inaweza isieleweke.
“Tuanze kusonga, bado tuna kipande cha mwendo wa miguu” Zena aliendelea kuniambia huku akitangulia kwenda mbele kuelekea katika ule msitu uliokuwa unatisha.
Wakati nikimfuata nyuma nilimuuliza.
“Lakini Zena sitapatwa na madhara yoyote huku?”
“Madhara kama yapi?”
“Mimi najua kuwa majini wengine wanadhuru watu?”
“Ni kweli wapo majini wanaodhuru watu”
Kukiri kwake kwamba kuna majini wanaodhuru watu kukaniongezea ile hofu yangu.
“Sasa itakuwaje, si nitakatwa vipande vipande?”
Nilipomwambia hivyo Zena akacheka.
“Huwezi kukatwa vipande vipande, si uko na mimi. Mimi ndiye mwenyeji wako ambaye nitakulinda wewe”
“Utaweza kunilinda Zena?”’
“Bila shaka yoyote. Hakuna jini yoyote atakayeniuliza chochote kuhusu wewe. Kwanza ukoo wetu unaheshimiwa sana na mimi najulikana kwamba ni jeuri”
Tuliingia katika ule msitu. Tulikuta njia nyembemba tukaifuata. Macho yangu yalikuwa yakiangalia kwenye ile miti.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hivi hao majini nitawaona kwa macho yangu?” nikamuuliza Zena baada ya kimya kifupi.
“Utawaona. Ngoja tutokeze kwenye mji”
“Wakoje?”
“Wako kama watu tu. Kama utaona tofauti ni ndogo sana. Sisi tunakuwa na maumbo ya kiasili na ya kujigeuza kama binaadamu. Sasa ukimuona jini katika umbo lake la asili ndio atakutishia kidogo lakini baadaye utawazoea”
“Kwani tutarudi lini huko Tanga?”
“Labda kesho. Nataka nikuoneshe kwa wazazi wangu ili wajue mtoto wao anaishi na nani”
Baada ya muda kidogo tuliona tumetokea katika majabali marefu. Yalikuwa mengi na mengine yalikwenda juu yakaonekana kama minara.
“Ni kitu gani?” nikamuuliza Zena.
“Ndio tumetokea kwenye mji wenyewe”
“Mji ndio huu?”
“Ndio huo unaouona”
“Mnakaa kwenye majabali?”
“Hizo ndio nyumba zetu za ghorofa”
“Una maana kwamba mle ndani ya ile minara kuna watu?”
“Si watu ni majini ndio wanaoishi humo”
Nikawa naikodolea macho ile minara. Ilikuwa na matundu kama madirisha ya kuingiza hewa.
Hata hivyo ilionesha kama ilikuwa ni kazi ya kale ya kisanaa. Niligundua kuwa yale majabali na ile minara ilikuwa imechongwa na kuwezeha kuwa nyumba za majini.
Karibu minara yote ilikuwa na rangi nyeupe kama iloiyopakwa chokaa.
Baada ya mwendo mfupi tulitokea katika eneo la wazi ambalo lilionekana kama uwanja mpana. Tulikuta viumbe wengi kama watu wakiwa katika harakati mbali kwenye uwanja huo.
Nilimuuliza Zena pale palikuwa ni wapi na wale tuliokuwa tukiwaona walikuwa kina nani.
“Hapa ni kwenye gulio. Wale ni majini, wengine wanauza bidhaa zao na wengine wananunua” Zena akaniambia.
“Sasa ni bidhaa gani zinazouzwa pale?”
“Bidhaa mbali mbali. Bidhaa za vyakula na bidhaa nyinginezo”
“Hizo bidhaa wanazipata wapi?”
“Zinapatikana humu humu. Bidhaa nyingine zinatoka Bara Arabu, India na hata China”
“Hizo bidhaa zinafikaje huku?”
“Kuna majini wanaokwenda kununua na kuzileta huku”
“Mnatumia pesa gani?”
“Kwa huku kwetu pesa si muhimu. Mara nyingi biashara inayofanyika ni ya mali kwa mali. Unatoa kibaba cha mchele, mwenzako anakupa kibaba cha ngano. Lakini wako majini wanaouza na kununua vitu kwa pesa. Pesa zinazotumika ni rupia, real ya uarabuni na pesa za Kichina”
“Pesa za Kitanzania hazitumiki”
“Hazitumiki”
“Kwanini?”
“Majini hawaendi kununua vitu kule”
Tulikiuwa tumeshalipita lile eneo lakini mimi bado nilikuwa nikishangaa shangaa.
Tulikuwa tukipishana na watu mbalimbali ambao Zena aliniambia kuwa walikuwa ni majini.
Kulikuwa na wengine waliokuwa wakinitazama kwa macho makali lakini Zena aliniambia nisiwajali.
“Labda wananishangaa kuona nimekuja katika mji wenu?” nikamwambia.
“Wanakushangaa kwani hawawajui binaadamu? Wewe si binaadamu wa kwanza kufika huku”
“Na hao binaadamu wengine wanafikaje huku?”
“Wanaletwa na majini wao kufundishwa uganga au kutembea tu. Tena wanakaa muda mrefu hadi wanajua lugha yetu”
“Na mimi naweza kuwaona hao binaadamu wenzangu?”
“Huku kila mmoja ana lake. Siwezi kujua wako wapi na hao waliowaleta sihusiani nao”
Tukafika katika jabali moja lililokuwa na mnara mrefu. Zainush akaniambia kuwa pale ndio kwao.
Wakati tunataka kuingia kwenye mlango wa jabali hilo wakaja majini watatu kutupokea. Walikuwa wanawake watupu tena wasichana wadogo. Lugha ya Zena ikabadilika, akawa anaongea kikwao.
Walitupokea yale mabegi wakatangulia nayo ndani na sisi tukafuata nyuma. Zena akaniambia kuwa wale walikuwa wadogo zake.
“Sisi tuko thelathini, wanawake tuko kumi na saba, waliobaki ni wanaume”
“Mko wengi sana. Nyote ni baba mmoja na mama mmoja?”
“Baba mmoja na mama mmoja”
“Wewe ni wa ngapi kuzaliwa?”
“Ni wa saba lakini kwa wanawake mimi ni wa pili”
“Hao ndugu zako wengine wako humu?”
“Wale wakubwa wana masikani zao zingine. Walioko hapa ni wale wadogo tu”
Tukafika mahali ambapo tulikuta pazia zito la rangi nyeupe.
Zena alilipenua pazia hilo tukapita na kutokea kwenye chumba kipana kilichokuwa kama sebule. Kilikuwa kimetandikwa mazulia yenye mistari rangi tatu tofauti, rangi nyeupe, rangi nyekundu na rangi ya bahari.
Kulikuwa na mito ya pamba ya kukalia ambayo ilikuwa imewekwa chini kuzunguka sebule nzima.
Wale wadogo zake Zena walielekea kwingine. Zena akaniambia.
“Tukae hapa”
Akatangulia yeye kukaa kwenye mto mmojawapo na mimi nikakaa kwenye mto mwingine.
“Hapa ndio nyumbani kwetu” akaniambia.
Nilikuwa nikikizungushia macho kile chumba kuangalia nakshi zilizokuwa zimetiwa mle ndani. Kwa mbali nikasikia harufu kama ya marashi na udi wa Unguja.
“Kwa hiyo wazazi wako wako hapa?” nikamuuliza Zena.
“Wako hapa. Mama yangu atakuja sasa hivi, yuko ndani”
Haikutimu hata dakika moja mwanamke mmoja wa kiarabu akachomoza na kusogea karibu yetu. Alikuwa mtu mzima sana. Mwili wake wote ulikuwa umezibwa na shuka nyeupe. Sikuweza kuona hata miguu yake.
Kilichokuwa kikionekana ni uso wake. Ingawa alikuwa mwanamke lakini alikuwa na ishara za kutoka sharafa. Alikuwa na macho ya kijivu yaliokuwa na mboni zilizounda mstari mwembamba.
Akatuambia. “Assalaam alaykum”
Tukamuitikia. “Waalayka ssalaam”
Baada ya hapo mwanamke huyo alibadili lugha akawa anaongea kijini na Zena. Sikuelewa walikuwa wakizungumza nini.
Yule mama hakukaa. Alibaki amesimama vile vile. Wakati anazungumza na Zena mara kwa mara alikuwa akinitazama mimi.
Mwishowe Zena akaniambia kwa Kiswahili.
“Umemuona mama yangu”
“Ndiye huyu?” nikamuuliza huku nikiogopa kumtazama kutokana na macho yake.
“Ndiye yeye lakini hajui Kiswahili vizuri. Hutaweza kuzungumza naye”
Yule mama akacheka.
“Ninajua. Kwanini yeye ajue mimi nisijue” akaniambia kwa Kiswahili chenye lafidhi ya kiarabu kisha akaniuliza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unaitwaje mwanangu?”
“Naitwa Amour”
“Mmekubaliana nini na Zena?”
Kidogo nilisita kujibu. Zena akanitazama na kuniambia.
“Mwambie”
“Aliniambia tuje huku” nikamjibu.
“Kufanya nini?”
Nikamtazama tena Zena.
“Amour unaulizwa, mbona unanitazama mimi”
“Nisaidie kujibu, wewe ndiye uliyenileta huku”
Mama akabadili lugha na kuanza kuongea na Zena kwa ukali.
Walijibizana kwa muda kidogo kisha Zena akaniambia.
“Si tumekubaliana tuje huku tuoane?”
Kabla sijajibu yule mama akamuuliza Zena kwa Kiswahili.
“Muoane kwa idhini ya nani?”
Zena akanyamaza kimya.
“Mwenye idhini ni baba yako, umeshamwambia?” mwanamke huyo akamuuliza Zena.
“Si ndiyo tumekuja hivi?”
“Sasa mwambie baba yako, akikukubali uoane na huyo kijana ndio mtaweza kuoana”
“Wewe pia si unaweza kutoa idhini”
“Nitoe idhini mimi ni mwanume?”
Yule mama alipouliza swali hilo na kukosa jibu aligeuka na kuondoka. Nikamuona Zena akishusha pumzi ndefu.
“Kwanini mama yangu anapokuuliza maswali unasita kujibu?’ akaniuliza.
“Sijui nijibu nini”
“Kwani mimi na wewe si tumekwishaoana kule Somalia?”
“Mimi nilioana na Shamsa. Baadaye ndio ukatokea wewe”
“Ulioana na mimi si Shamsa, si nilikwambia?”
Nikanyamaza kimya.
“Huyu mama nilitarajia atakuwa upande wangu, naye ameshaanza kuleta taabu” Zena akajisemea peke yake kisha akainuka na kuniambia.
“Twende”
“Twende wapi?’ nikamuuliza huku nikiinuka.
“Nifuate”
Tukatoka katika lile jabali ambalo ukiingia ndani yake ni kama uliyeingia kwenye nyumba, tukaelekea katika jabali jingine dogo lililokuwa kando ya lile.
Tulipoingia katika jabali hilo Zena aliniambia kuwa pale ilikuwa ni sahemu yake ya kupumzika.
“Tukae hapa” akaniambia. Palikuwa na sebule ndogo iliyokuwa na mito iliyowekwa chini.
Tukakaa.
“Amour usiwe muoga. Kama utaulizwa umenipenda, sema ndio usisitesite. Ukisitasita watajua nimekulazimisha”
Wakati Zena akiniambia hivyo akaingia jini mmoja aliyekuwa kifua wazi. Alikuwa amejifunga shuka nyeupe kiunoni. Ndevu zake nyeupe zilikuwa zikikaribia kufika kweye tumbo lake kubwa. Kifua chake kilikuwa kimejaa manyoya meupe na marefu.
Alimsalimia Zena kisha akamwambia ana ujumbe kutoka kwa baba yake Mzee Jabalkeys.
“Anasemaje?” Zena akamuuliza.
“Amenituma nikwambie kwamba huyo kijana uliyekuja naye umrudishe huko huko ulikomtoa”
Moyo wangu ulishituka na kuanza kwenda mbio.
“Nitamrudishaje wakati tumekuja kuoana na ametaka kuwajua wazazi wangu!” Zena akasema.
“Unajua baba yako amekasirishwa na kitendo chako cha kutaka kuoana na binaadamu. Amesema yeye hawezi kutoa idhini uoane na binaadamu na hataki kabisa kusikia kitu kama hicho”
“Lakini wenyewe si tumeshakubaliana”
“Lakini Zena wewe ni jinni, utaolewaje na binaadamu halafu mtaishi vipi?”
“Majini wanaoa binaadamu na wengine wanaolewa na binaadamu labda useme baba hajui tu”
“Hata kama ni hivyo lakini huko ni kukiuka kawaida yetu. Hilo jambo halifai”
“Kama yeye baba amesema hivyo basi mimi nitajiozesha mwenyewe, si lazima nipate idhini yake”
“Sasa huo ni ukosefu wa adabu kwa baba yako”
“Potelea mbali!”
“Sasa nikamwambie hivyo?”
“Nenda”
Yule jinni aliyeonekana kukasirika akatoka na kumuacha Zena akigomba peke yake.
“Najuta kuja huku! Wazee gani hawa wasiolewa mambo. Wamekuwa washamba kiasi hiki!”
Ghafla nikamuona mzee mwingine aliyekuwa amefuatana na yule mzee aliyeondoka pamoja na mzee mwingine.
“Wewe mtoto mwenye laana ulimjibu nini huyu Subyani?” Yule mzee akamuuliza Zena kwa sauti ya ukali.
“Lakini baba ungenisikiliza mimi mwenyewe badala ya kusikiliza watumishi wako. Hao wanaongeza maneno”
“Mimi sihitaji kukusikiliza kwa sababu najua wewe umekuwa jeuri na asi. Ninachokwambia ni kwamba mrudishe huyu kijana ulikomtoa na kwamba sitaki kusikia tena kwamba unataka kuoana na binaadamu!”
Zena akafura kama chatu.
“Mimi lazima nitaoana naye, iwe itakavyokuwa. Kama hamtaki nitajiozesha mwenyewe!”
Zena akainuka pale alipokuwa ameketi akatoka kwa hasira huku yule mzee niliyemdhania kuwa ndiye Jabalkeys akimtazama.
“Huyu mtoto amekuwa shetani kabisa, si jini tena” akasema kisha akanisogelea mimi.
“Mwanangu amekutoa wapi yule shetani?” akaniuliza.
“Amenitoa kwetu”
“Wapi”
“Tanga”
“Mlikubaliana mje muoane huku?”
“Yeye ndiye aliyekuwa analazimisha. Amenitia kwenye matatizo mengi. Naomba msaada wako”
“Hata kama nitawambia hawa watumishi wangu wakurudishe, bado ataendelea kukufuata na atakusumbua lakini suala lake nitalipeleka kwa Sultani wetu. Wewe subiri hapa hapa”
Majini hao wakaondoka. Nikabaki peke yangu. Sikujua Zena alikuwa amekwenda wapi na angerudi saa ngapi. Na pia sikujua ningeendelea kukaa pale hadi muda gani. Kusema kweli ile hali ya Zena kuanza kutibuana na wazazi wake ilianza kunitia hofu.
Baada ya kama nusu saa hivi yule jini aliyekuja kwanza akarudi peke yake akiwa ameshika bahasha.
“Begi lako ni lipi na lipi?” akaniuliza.
Nikamuonesha yale mabegi mawili niliyokwenda nayo. Yule jini akayabeba yote mawili kisha akaniambia.
“Twende”
Nikatoka naye katika lile jabali tukashika njia ambayo mimi na Zena tulikwenda nayo. Tukashuka chini baharini. Ikumbukwe kwamba muda ule ulikuwa ni usiku lakini ulikuwa usiku wa mbalamwezi.
INAENDELEA

0 Comments