ILIPOISHIA
Vile tulivyokuwa tumekaa pamoja ndani ya gari niliyakumbuka maneno ya Shamsa kuhusiana na Abdi, nikaona kama niliyekuwa nimekaa na nyoka mwenye sumu kali.
Tukaendelea na safari.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilikuwa nikimfahamu vizuri Yusufu mdogo wake Abdi ingawa hakuwa karibu sana na mimi. Muda mwingi alikuwa akishughulika na mambo yake mwenyewe.
Niligundua pia kuwa Abdi hakuwa akisikizana sana na mdogo wake jambo ambalo lilifanya mara kwa mara wakwaruzane.
Lakini ndugu ni ndugu. Licha ya kuwepo kwa hali hiyo, Abdi alipopata habari kuwa mdogo wake alikuwa hafahamiki alipo ameanza kupata wasiwasi na kumuhangaikia.
Tulifika kituo cha polisi ambapo Abdi alikuwa akifahamika vizuri. Aliwaeleza polisi tatizo lake.
Polisi hao wakamfahamisha kuwa hawakuwa na taarifa yoyote ya mdogo wake.
“Amepotea tangu lini?” Polisi mmoja akamuuliza.
“Si kwamba amepotea bali hajulikani yuko wapi”
“Tangu lini?”
“Tangu jana alipoondoka nyumbani kwake hajarudi hadi sasa na hajulikani yuko wapi”
“Ana mke na watoto”
“Ndio ana mke na watoto”
“Hakuwahi kumwambia mke wake anakwenda wapi?”
“Huyo mke wake ndiye aliyenifahamisha mimi kuwa Yufusu hajarudi nyumbani tangu jana”
SASA ENDELEA
“Mmemtafuta kwa ndugu na jamaa?”
“Yusufu si mwendawazimu. Hawezi kwenda kwa ndugu na jamaa na kubaki huko huko bila mke wake kuwa na habari”
“Sasa nakushauri uende ukamtazame mahospitalini huenda amepata ajali bila ya nyinyi kujua”
“Basi ngoja twende tukamtazame huko” Abdi akawambia polisi.
Tukatoka tena na kujipakia kwenye gari.
Tulizunguka katika mahospitali mbalimbali kuanzia yale ya serikali na ya binafsi lakini Yusufu hatukumkuta.
Wakati tunarudi, Abdi akiwa amekasirika aliniambia.
“Huyu ni mtu mzima si mtoto. Asisumbue akili zetu. Ngoja nikurudishe hotelini kwako na mimi niende zangu, atajua mwenyewe na mke wake”
Abdi akanirudisha hotelini na kuniacha, akaenda zake.
Ilipofika saa tisa mchana Abdi akanipigia simu.
“Nisubiri ninakuja twende polisi”
“Kuna nini tena?” nikamuuliza.
“Polisi wameniita. Wameniambia kuna mtu wanataka nikamtambue kama ndiye huyo mdogo wangu ninayemtafuta”
“Yuko wapi?”
“Hawakuniambia. Wameniambia niende nitajua huko huko”
“Sawa. Nakusubiri”
Baada ya muda mfupi Abdi akafika, tukaondoka na gari.
Tulipofika kituo cha polisi tukaambiwa kuwa kuna mtu ameonekana karibu na sehemu inayotupwa taka taka za jiji.
Polisi hao hawakutufafanulia vizuri isipokuwa walituambi tufuatane nao kuelekea sehemu hiyo ili tukamuone huyo mtu.
Polisi waliondoka na gari lao na sisi tukaondoka na gari letu na kuwafuata.
Tulipofika katika hilo eneo tuliloambiwa tulikuta polisi wengine pamoja na watu kadhaa wamezunguka mahali palipokuwa na shimo.
Na sisi tukaenda mahali hapo. Tulijipenyeza katika kundi la watu tukasogea katika kingo za shimo hilo na kutazama ndani.
Kusema kweli mimi na Abdi tulishituka tulipoona mtu tuliyeambiwa tukamtambue ni maiti ya Yusufu iliyokuwa imelazwa ndani ya shimo hilo.
Abdi akanitazama kwa macho yaliyokuwa yametaharuki.
“Yusufu ameuawa!” akaniambia.
“Sasa ameuawa na nani?” nikamuuliza.
“Sisi sote ndio tumefika hapa na kuikuta hii maiti. Polisi ndio watatueleza.
“Ndiye yeye mliyekuwa mnamtafuta?” Polisi mmoja akatuuliza.
“Ndiye yeye. Ni kitu gani kimemtokea?” Abdi akauliza.
Abdi akaelezwa kwamba polisi waliarifiwa kwamba kulionekana mwili wa mtu aliyeuawa katika eneo hilo akiwa ndani ya shimo, ndipo polisi walipofika na kuukuta mwili huo ambao ulionekana ulikuwa umelala ndani ya shimo hilo kutoka jana yake.
“Itakuwa ndugu yangu ameuawa?” Abdi akawauliza polisi.
“Hatujafahamu lakini marehemu amekutwa na alama ya kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani mwake”
“Hicho kitu alichopigwa nacho ndicho kilichomuua”
“Tunafikiri ndio hivyo lakini polisi tutakuwa na uchunguzi wetu”
“Uchunguzi huo ni lazima ubainishe nani amemuua mdogo wangu na kwa sababu gani?”
“Hiyo ndiyo kazi yetu, tunao wataalamu wetu wa uchunguzi”
Abdi akaitazama tena maiti ya mdogo wake kisha akatikisa kichwa kusikitika.
“Sijui amewakosea nini hao watu”
Sikumjibu kitu kwa vile na mimi nilikuwa nimefadhaika. Yule mtu jana yake tu nilimuona akiwa mzima na mwenye afya njema.
Mwili wa Yusufu ulitolewa kwenye lile shimo baada ya polisi kumaliza kuupiga picha na kuchukua vipimo vyao.
Mwili huo ulipakiwa katika gari la polisi na kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
Mimi na Abdi tulitakiwa kurudi tena kituo cha polisi ambapo Abdi alitakiwa kuandikisha maelezo yake. Baada ya kuandikisha maelezo yake tulifuatana na polisi hadi nyumbani kwa Yusufu.
Mke wa Yusufu alipoona polisi alishituka na kuuliza.
“Kuna nini?”
Abdi akamueleza kwa utulivu kilichokuwa kimetokea.
Mwanamke huyo hakuamini alichoelezwa akataka kwenda kuiona maiti ya mume wake.
“Utapelekwa ukaione maiti ya mume wako lakini tulikuwa tunahitaji maelezo yako” Polisi mmoja akamwambia mwanamke huyo.
“Maelezo gani?”
“Tuambie marehemu aliondoka lini hapa nyumbani?”
“Aliondoka jana”
“Majira ya saa ngapi?”
“Aliondoka mchana baada ya kula chakula, ndio hatukumuona tena”
“Kwa kawaida anapoondoka nyumbani huwa anakwenda wapi”
“Huwa haniambii”
“Na jana alipoondoka hakukwambia anakokwenda?”
“Hakuniambia”
“Sasa ngoja upelekwe hospitali ukauone mwili wa marehemu halafu tutakuhitaji kituo cha polisi uandikishe maelezo yako” Polisi aliyekuwa akizungumza na mke wa Yusufu alimwambia.
Baada ya hapo sisi na polisi hao tukaenda hospitalini ambako mke wa Yusufu aliuona mwili wa mume wake na kuangua kilio. Alimpa Abdi kazi ya ziada ya kumnyamazisha.
Mwanamke huyo aliponyamaza tulikwenda kituo cha polisi ambako mke wa Yusufu alitoa maelezo yake ambayo yaliandikishwa. Kisha tukarudi nyumbani kwa Yusufu.
Abdi akaniambia atashughulikia mpango wa mazishi ya ndugu yake ambayo alitaka yafanyike jioni ya siku ile ile. Kwa
hiyo alituma watu kutoa taarifa ya kifo hicho kwa ndugu na jamaa mbali mbali.
Mpaka inafika saa nane mchana mwili wa marehemu ulishachukuliwa na wanafamilia kutoka hospitali na kuletwa nyumbani kwake ambako uliandaliwa haraka haraka kwa ajili ya mazishi.
Saa kumi na moja jioni Yusufu akazikwa. Abdi akatangaza kuwa hakukuwa na matanga. Aliwambia watu kuwa matanga ni mila za kizamani ambazo zimepitwa na wakati na hazimo katika dini.
Siku ile nilirudi hotelini saa nne usiku kwani muda wote nilikuwa bega kwa bega na Abdi katika shughuli zote za mazishi.
Baada ya kupita wiki moja mke wangu akaniambia tena.
“Unajua kuwa Abdi anaweza kupata
kichaa!”
“Kwanini” nikamuuliza.
“Tamaa yake ya kupata utajiri imepita kiasi. Kila anapokaa anawaza utajiri tu, sasa mbaya zaidi anafanya mambo mabaya yasiyostahili”
“Anafanya mambo gani?”
“Nataka nikupe siri nyingine, unaju Abdi ndiye aliyemuua Yusufu!”
Nikashituka.
“Unasema kweli?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Abdi ndiye aliyemuua ndugu yake, alikwenda naye kule akampiga chuma kisha akajifanya anamtafuta”
Nikatikisa kichwa changu kusikitika.
“Sasa kwanini amuue ndugu yake?”
“Si ile tamaa yake ya utajiri! Aliambiwa na yule mganga wake kwamba kabla ya kukushika wewe na kukutoboa utosi kwa msumari, kwanza amuue Yusufu”
“Amuue kwa kisa gani?”
“Kwa sababu yule mganga alimwambia yule jini akitoka kwako anaweza kuingia kwa Yusufu kwa sababu wao ni ndugu tumbo moja”
“Ndio akaamua amuue?”
“Ndio akamuua”
“Yule ni chizi kweli!”
“Sasa jihadhari, nadhani wakati wowote anaweza kushughulika na wewe”
“Yaani aniue mimi”
“Sasa akishakutoboa utosi kwa msumari unadhani utapona, si utakufa!”
“Haniwezi. Nitapambana naye. Yule mtu dhaifu sana, hana afya hata kidogo. Nikimpiga ngumi moja sidhani kama ataamka”
Wakati ninazungumza na Shamsa, ghafla Abdi akaingia.
Akatusalimia kisha akaniambia.
“Nimekufuata twende shamba”
“Kuna nini?” nikamuuliza.
“Matembezi tu”
Nilitaka kumkatalia lakini nilishindwa. Nikamwambia.
“Sawa”
Nikamuga Shamsa na kutoka na Abdi.
Huko nje akaniambia tutatumia gari lake. Tukajipakia kwenye gari lake na kuondoka.
Shamba la Abdi lilikuwa umbali wa kilometa kumi na mbili nje ya jiji la Mogadishu. Lilikuwa shamba kubwa la mitufaa na mimea mingine mchanganyiko ikiwemo minazi na mikorosho.
Katikati ya shamba hilo alikuwa amejenga nyumba yake kubwa ambayo alikuwa akiitumia akiwa shambani hapo.
Lakini baada ya muda kidogo niligundua kuwa tulikuwa hatuelekei shambani kwa Abdi kwani nilikuwa nakufahamu.
Abdi alikuwa ameacha njia ya kuelekea shambani kwake akakata kushoto na kuingia katika njia iliyoelekea katika msitu.
Kwa vile alikuwa akinizungumzisha, nilighafilika kumuuliza alikuwa anaelekea wapi. Ghalfla akakata tena kushoto. Tukawa tumeingia kwenye msitu.
Alilisimamisha gari chini ya mti akafungua mlango na kushuka bila kuniambia tulifuata nini mahali pale.
Aliposhuka nilimuona akielekea kwenye vichaka. Na mimi nikashuka na kumfuata. Alikuwa ameshatokomea kwenye kichaka kimojawapo, nilipoona watu watatu wakitokea kwenye kichaka hicho na kunifuata.
Walikuwa mapandikizi ya watu wenye sura za kijahili. Nilipoona wamenizunguka nikasimama.
“Amekwenda wapi huyu jamaa?” nikawauliza.
Hakukuwa na yeyote aliyenijibu zaidi ya kunitazama kiubabe. Kitendo hicho kikanishitua sana.
Mmoja wa watu hao ambao alikuwa amekata sharubu zake kama herufi ya M alinisogelea akanishika ukosi.
Kabla sijajua nini kingetokea, alinitandika ngumi moja ya shavu. Mwenzake mmoja aliishika mikono yangu miwili kwa nyuma.
Wakawa wananikokota kuelekea kule alikoelekea Abdi.
“Mbona mnanipiga?” nikawauliza.
“Ulitaka tukubusu sio?” Mwenye sharubu akaniuliza kwa dharau.
Waliniingiza kwenye kile kichaka. Nilipoona siwaelewi nikapiga kelele kumuita Abdi.
Abdi sikumuona. Tukatokea upande wa pili wa kile kichaka. Palikuwa na mti wa mwembe. Chini ya ule mti palikuwa na shimo. Urefu wa shimo hilo ulikuwa kama mita sita hivi na upana wake ulikuwa kama wa kisima cha maji.
Kulikuwa na watu wawili waliokuwa ndani ya shimo hilo wakiwa wameshika kamba. Walikuwa wamesimama kama waliokuwa wakisubiri kitu.
Juu ya lile shimo palipita tawi la ule mwembe. Juu ya tawi hilo palikuwa na mtu mwingine aliyekuwa amekaa.
Mimi nilikuwa nimekazana kumuita Abdi ambaye nilikuwa simuoni. Wale jamaa walinikokota hadi karibu na lile shimo kisha ghafla wakanisukuma nikaangukia ndani ya shimo hilo.
Wale jamaa wawili waliokuwa ndani ya shimo hilo walinidaka wakaniangusha chini. Mmoja alinishika mikono yangu ili nisiinuke, mwingine aliishika miguu yangu na kunifunga ile kamba.
Baada ya kunifunga miguu yangu, ncha moja ya ile kamba walimrushia yule mtu aliyekuwa juu ya tawi, akaidaka. Aliivuta na kuikunja. Ilikuwa kamba ndefu.
Baada ya kuikunja kamba yote, aliwarushia wale watu waliokuwa juu ya shimo. Watu hao waliidaka na kuanza kuivuta.
Ile kamba ilipita juu ya lile tawi la mti kisha ikaenda kwa wale watu, hivyo walipoivuta ilipitia juu ya lile tawi. Waliivuta hadi mwisho. Sasa miguu yangu ambayo ilifungwa kwa kamba hiyo ikaanza kuinuliwa. Iliinuliwa hadi ikawa juu.
Kamba iliendelea kuvutwa. Mwisho nikawa nimenin’ginizwa kichwa chini kama mkungu wa ndizi. Kamba iliendelea kuvutwa hadi mwili wangu wote ukawa unanin’ginia kichwa chini miguu juu.
Ghafla nikamuona Abdi akiingia kwenye lile shimo akiwa ameshika kikombe cheupe na nyundo.
“Abdi ndio nini hivi” nikamuuliza.
Abdi hakunijibu chochote. Aliimpa mtu mmoja ile nyundo akatoa msumari kutoka mfukoni mwake na kumpa.
“Sasa mtoboe utosi wake. Mimi nitakinga damu yake kwenye kikombe” alimwambia yule mtu aliyempa ile nyundo na msumari.
Jamaa akaupachika msumari kwenye utosi wangu. Nikajua ni yale aliyoniambia Shamsa. Nikaanza kupiga kelele.
“Abdi mbona unataka kuniua…nimekuko
sea nini…?”
Wakati napiga kelele Abdi alikuwa akimuihimiza yule mtu aupige nyundo ule msumari ili atoboe utosi wangu.
“Mpige nyundo haraka Garbela…toboa utosi huo…?”
“Abdi acha ukatili huo…usiniue Abdi…!” niliendelea kumpigia kelele Abdi ambaye hakuonesha kunijali hata chembe.
Nilikuwa nikiwatazama kiupande upande kwani nilikuwa nimening’inizwa kichwa chini kama mnofu wa nyama buchani.
Nikamuona yule mtu aliyetajwa kwa jina la Garbela akiinua nyundo ili aupige ule msumari ambao tayari alikuwa ameukita kwenye utosi wangu na kunisababishia maumivu makali. Ghafla nikaona kitu kama kiza kikivamia katika lile eneo. Lakini hakikuwa kiza, kilikuwa kivuli kilichotokea kwa juu na kushuka chini kwa kasi ya ajabu.
Naam kilikuwa kivuli cha nondo! Joka kubwa ambalo lilianguka kutoka juu ya ule mti. Lilikuwa ni lile lile lililoibuka katika ile boti siku ile niliyotaka kutoswa baharini.
Joka hilo liliugonga utosi wa Abdi kwa meno yake yaliyokuwa nje Nikamuona Abdi anaanguka chini kwa taratibu kama mlevi huku utosi wake ukitokwa na damu.
Yule mtu aliyekuwa anataka kunitoboa utosi aliduwaa ghafla. Alipozinduka alitupa nyundo na msumari pembeni, akawa anawania kupanda juu ya lile shimo ili akimbie. Lakini hakuwahi. Wakati ule anaparamia lile shimo, joka hilo liligeuza kichwa na kumgonga utosini.
Nikamuona anarudi chini taratibu kama mtu aliyepoteza nguvu zote. Akaanguka.
Wale watu waliokuwa wameshikilia kamba niliyokuwa nimening’inizwa nayo waliiachia na kukimbia. Walipoiachia kamba ilijivuta nikaanguka chini kama gunia.
Lile joka lilitoka kwenye lile shimo na sikujua lilitokomea wapi.
Nikajifungua ile kamba kisha nikamsogelea Abdi na kumuinua. Hakuweza kuinuka. Alikuwa amepoteza nguvu zote na alionekana alikuwa taabani.
Pengine lile joka lilipomgonga lilimtia sumu. Nikajua Abdi asingeweza kupona tena.
Huku nikiwa nimekishikilia kichwa chake nilimtazama kwa huzuni hasa vile nilivyoona kuwa anakufa.
“Abdi ulikuwa unataka kuniua ndugu yanngu…nilikukosea nini?” nikamuuliza.
“Nisamehe sana. Wewe ni ndugu yanngu wa damu. Baba yako mkubwa alikuja huku Somalia kutoka Tanzania na kunizaa mimi na Yusufu. Lakini nilifanya makosa. Nakiri kuwa nilifanya makosa…”
Alinyamaza baada ya kuishiwa na pumzi. Alipumua kwa sekunde kadhaa kisha akaendelea.
“Nilitaka kukuua kwa sababu niliambiwa na mganga kuwa una jini wa utajiri ambaye mimi nilikuwa namtaka na hicho ndicho kilichonifanya nikulete huku Somalia….”
Abdi alinyamaza tena akapumua kwa sekunde kadhaa kisha akaendelea.
“Kwa kudhani nikimpata huyo jini ningetajirika, nilimuua mke wangu na juzi juzi tu nilimuua mdogo wangu na leo nilitaka kukuua wewe kwa sababu mganga aliniambia nikutoboe utosi kisha nijipake da,mu yako…”
Abdi hakuweza kuendelea kusema baada ya pumzi kumuishia. Alipumua tena kwa sekunde kadhaa kabla ya kuweza tena kufungua mdomo wake.
“Anayeniua mimi ni jini wako. Alikuja kukuokoa baada ya kuona utakufa…”
Wakati Abdi anazungumza, mimi nilikuwa nikitikisa kichwa wakati wote
kumsikitikia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kweli ninaamini sasa kuwa usiilalie mlango wazi bahati ya mwenzako. Nisamehe ndugu yangu kwa upumbavu wangu”
Abdi alitia mkono kwenye mfuko wa suruali yake akatoa funguo mbili zilizofungwa pamoja akanipa.
“Ufunguo mmoja ni wa nyumba yangu iliyoko shamba. Ukiingia ndani katika chumba cha mkono wa kulia kuna mlango wa kuteremka chini ambako pia kuna chumba. Ukiingia katika chumba hicho utakuta sefu ya chuma. Utaifungua kwa huo ufunguo wa pili ambao ni mrefu…”
Kuna nini humo ndani?” nikamuuliza baada ya kuona amenyamaza.
“Nimeweka sanduku lililojaa dhahabu pamoja na dola za kimarekani. Kuna dola milioni moja. Utachukua wewe hilo sanduku. Pia utachukua magari yangu, nyumba zangu na hoteli zangu. Utakuwa mrithi wangu….”
Abdi hakumaliza maneno yake, sauti yake ilififia akakata roho mikononi mwangu. Bila shaka ile sumu ya lile joka ilikuwa imeshamuathiri moyo wake.
Nikakiweka kichwa chake chini huku nikijiambia.
“Ameyataka mwenyewe”
Nilimpekua mifukoni nikachukua pochi yake pamoja na funguo ya gari na funguo ya nyumbani kwake. Nikasimama na kutoka kwenye lile shimo. Niliona jamaa wawili miongoni mwa wale watu waliokuwa pamoja na Abdi wakikimbia. Kumbe walikuw a wakituchungulia ndani ya lile shimo.
Nilitembea kwa hatua za ukakamavu kuelekea pale lilipokuwa gari la Abdi. Nikafungua mlango wa dereva na kuliwasha. Nikarudi mjini.
Nilikuwa nimepata majonzi kweli kweli kutokana na kifo kile cha Abdi. Nilihuzunika kama vile si yeye aliyekuwa anataka kuniua.
Nilijiambia kama maisha ya Abdi yamekwisha na maisha yangu pale Somalia pia yamekwisha. Kama nitaendelea kuishi pale Somalia, mwenyeji wangu atakuwa nani? Nikajiuliza bila kupata jibu.
Nilifika nyumbani kwangu nikamueleza Shamsa mkasa mzima uliotokea. Shamsa akashangaa sana.
“Amenirithisha kila kitu. Nataka kwenda nyumbani kwake nikapekua. Kama kutakuwa na kitu muhimu nikichukue”
Shamsa alikuwa akiendelea kuhuzunika.
“Masikini Abdi. Amejidhulumu mwenyewe nafsi yake…”
“Muda wake umeshafika” nikamwambia Shamsa.
“Lakini naona huyo jini bado anakuandama”
“Bila shaka, lakini ajabu ni kwamba hajanitokea wala kunisumbua kama zamani”
“Kama si yeye ungekufa wewe leo”
“Ni kweli ningekufa. Sasa mimi naenda kwa Abdi”
“Twende sote” shamsa akanimbia.
“Twende”
Shamsa akavaa baibui lake tukatoka. Tulijipakia kwenye gari ya Abdi tukaondoka.
Tulifika nyumba kwa Abdi nikafungua mlango. Nyumba ilikuwa kimya. Abdi hakuwa na mke wala mtoto na alikuwa ameshafukuza wafanyakazi wake wote.
Tuliipekua nyumba nzima. Katika kabati la Abdi lililokuwa chumbani mwake tulikuta shilingi za kisomali milioni kumi. Shamsa akaniambia tuzichukue. Tukazichukua. Tukafunga milango na kurudi nyumbani kwetu.
Nilimshusha Shamsa pamoja na zile shilingi milioni kumi. Nilimwambia kuwa nilitaka kwenda shambani kwa Abdi kuchukua hilo sanduku la dhahabu ambalo pia lilikuwa na dola za Kimarekani.
Nikaanza safari ya kuelekea shambani kwa marehemu Abdi. Nilipofika. Nilikuta gari la Ismail, rafiki yake Abdi likiwa limeegeshwa mbele ya nyumba ya Abdi.
Niliposhuka kwenye gari nilikwenda kuujaribu mlango wa nyumba hiyo,. nikakuta ulikuwa umefungwa. Nikaizunguka ile nyumba kumtafuta aliyekuja na gari lile.
Sikuona mtu. Nikapatwa na wasiwasi. Ghafla nikasikia hatua za mtu anayenyata nyuma yangu. Nikageuka haraka nitazame nyuma lakini sikuwahi, nilihisi kitu kizito kama nyundo kikipiga kichwani kwangu. Hapo hapo nilidondoka na kuzirai.
Nilipozinduka nilijikuta nilikuwa nimelala mahali pale pale nilipoanguka. Kabla ya fahamu kunijia sawasawa nilijiuliza nilikuwa wapi na kwanini nilikuwa nimelala chini.
Kichwa kilikuwa kizito kama kilichokuwa kimebebeshwa mzigo na mwili ulikuwa umechoka utadhani nililala kwenye sakafu kwa masaa kadhaa.
Nilipojaribu kukumbuka nini kimenitokea, kichwa kiliniuma na nilihisi kizunguzungu.
Lakini taratibu kumbukumbu zilianza kunijia. Kumbukumbu ya kwanza kunijia ilikuwa ni ile ya kutaka kuuliwa na Abdi.
Nikakumbuka nilivyokuwa kwenye shimo huku Abdi akimuihimiza mtu aliyekuwa amempa nyundo apigilie msumari kwenye utosi wangu.
Kumbukumbu hiyo ilinijia kama sinema ya kutisha akilini mwangu. Ingawa ni tukio ambalo lilishapita lilinitia hofu kama vile ndio kwanza linatokea.
Kumbukumbu ya pili kunijia ilikuwa ni ya kufika katika shamba la Abdi, kusimamisha gari na kukuta gari la Esmail. Nikakumbuka jinsi nilivyozunguka nyuma ya nyumba ya Abdi kumtafuta mwenye gari lile lakini ghafla nikasikia hatua za mtu nyuma yangu.
Niliposikia hatua hizo nikataka kugeuka ili nitazame nyuma lakini sikuwahi kuona kitu, nilishitukia nikipigwa na kitu kizito kama nyundo kichogoni kwangu, macho yangu yakafunga kiza na sikuelewa tena kilichotokea.
Nikapeleka mkono wangu kichogoni na kupapasa pale mahali nilipopigwa, nikaona palikuwa na jeraha na dami ilitoka na kuganda.
Sasa nikainuka huku nikijiuliza ni nani aliyekuwa amenipiga. Nilitazama kila upande, sikuona mtu. Kila wakati nilikuwa najipapasa pale kwenye kijaraha na kutazama ile damu mkononi mwangu.
Swali la nani aliyenipiga lilikuwa halina jibu kwani sikuona mtu yoyote. Eneo lote lilikuwa kimya. Nilirudi kwenye mlango wa ile nyumba, nikauona uko wazi. Wakati nilipokuja na gari langu mlango huo ulikuwa umefungwa.
Sasa nikaanza kupatwa na wasiwasi.
Ni nani aliyeufungua huo mlango wakati funguo nilikuwa nayo mimi?
Wakati najiuliza hivyo nilijipekua mifukoni. Zile funguo sikuziona. Nikaingia haraka mle ndani. Niliingia katika kile chumba alichonielekeza Abdi. Milango yote niliikuta wazi. Nikashuka katika kile chumba cha chini kwa chini ambacho Abdi aliniambia kulikuwa na sefu ya chuma na ndani ya sefu hiyo kulikuwa na sanduku lenye dhahabu pamoja na dola za Kimarekani alizokuwa amezificha.
Sefu niliikuta lakini ilikuwa wazi. Nilipochungulia ndani ya sefu hiyo sikukuta chochote. Sefu ilikuwa tupu kama mkono uliorambwa!
Nikatoka nje ya ile nyumba. Sasa fahamu zikanijia vizuri. Nilikumbuka wakati ule natoka katika lile shimo nililoingizwa na kina Abdi, niliona watu wawili wakikimbia. Bila shaka walisikia wakati Abdi alipokuwa ananiagiza nije nichukue lile sanduku lililokuwa na dola pamoja na dhahabu.
Kwa kutaka wanufaike wao, walikimbilia wao kuja hapa lakini wakashindwa ama kuingia katika ile nyumba au walishindwa kulifungua ile sefu kwa sababu hawakuwa na funguo. Ndipo wakaamua kunisubiri na mmoja wao ndiye aliyenipiga chuma hadi nikazirai.
Ndio sababu nilikuta lile gari la Esmail lakini baada ya kuzirai na kurejewa na fahamu, gari hilo sikuliona. Walikuwa wameshalichukua lile sanduku na kuondoka.
Esmail rafiki yake Abdi nilikuwa nikimfahamu vizuri. Bila shaka na yeye alikuwemo katika ule mpango wa kutaka kuniua.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikajimbia sitawaachia wachukue dhahabu ile pamoja na dola za Kimarekani ambazo Abdi alikwishanipa
“Hawa watu kweli ni majambazi!” nikajiambia kimoyomoyo na kuongeza.
“Huu walionifanyia ni ujambazi kamili. Lakini nitapambana nao!”
Nilirudi kwenye gari langu nikaliwasha na kuondoka.
Kwanza nilikwenda kwenye zahanati moja nikaoshwa lile jeraha kisha nikafungwa dawa. Nilipotoka katika zahanati hiyo nilikwenda katika duka la nguo nikanunua pama na kulivaa kuficha lile jaraha.
Nikaendesha gari kuelekea nyumbani kwangu huku nikiwaza jinsi majambazi hao wa Abdi walivyonizunguka. Nilishukuru kwamba nilikuwa na afya njema, vinginevyo kile chuma walichonipiga kichogoni kingenimaliza kabisa.
“Fedha haina udugu wala urafiki” niliwaza kimoyo moyo.
Abdi alitaka kuniua kwa sababu ya fedha. Alijua nikishakufa atampata jini ambaye atampa fedha ili atajirike, ainunue Mogadishu yote iwe mali yake.
Wenzake nao walinipiga chuma bila kujali ningedhurika kiasi gani kwa sababu ya fedha. Abdi alivunja udugu na wenzake walivunja urafiki kwa sababu ya kitu fedha.
Nikaendelea kujiambia, sasa mimi ni nani niiachie, nitawatafuta na kuwasulubu. Watajua mimi nani.
Nilirudi nyumbani.
nikamueleza Shamsa masahibu yaliyonipata. Nilimuonesha lile jaraha ambalo nilikuwa na hakika kwamba nilipigwa chuma.
SASA ENDELEA
Shamsa aliposikia ile habari alisikitika sana.
“Pole sana. Walitaka kukuua” akaniambia.
“Lakini sikufa na nimeshawajua, sitawaachia”
“Utawatafuta?” Shamsa akaniuliza.
“Sitawaachia wachukue ile dhahabu pamoja na dola zangu. Abdi alikwishanipa mimi”
“Watakuumiza!”
“Hawathubutu. Kama ni kwa ngumi hakuna yeyote anayeweza kusimama na mimi. Nina hakika nitawagaragaza vibaya sana”
“Una uhakika na unachokisema?”
“Mirungi imeshawamaliza, hawanitishi!”.
“Sasa sikiliza nikuambie”
“Unataka uniambie nini?”
“Mimi napajua anapokaa Esmail. Sasa nataka ukimfuata twende sote”
“Hakuna tatizo, tutakwenda lakini ujue kama litazuka suala la ngumi tutazichapa”
“Kama tumekubaliana hivyo, sawa”
Shamsa akaingia chumbani. Alipotoka alikuwa amebadili nguo. Alivaa baibui na ndani yake alivaa jinzi.
“Twende” akaniambia.
Tukatoka. Wakati tunataka kujipakia kwenye gari Shamsa aliniambia.
“Nitaendesha mimi”
Nikampisha kwenye sukani. Shamsa aliliwasha gari tukaondoka. Tulikwenda katika eneo moja lililokuwa kando kidogo ya jiji hilo. Tuliingia katika mtaa mmoja uliokuwa mtulivu.
“Mtaa huu ndio anaoishi Esmail” Shamsa akaniambia na kuongeza.
“Nyumba yake ni ile pale yaliposimama magari”
Niliyaona magari hayo. Yalikuwa yameegeshwa nje ya nyumba ya saba mbele yetu.
Shamsa alikuwa amepunguza mwendo. Kitu ambacho kilinipa moyo ni kuwa moja ya gari hilo ndilo lile nililoliona limeegeshwa kule shamba.
SEkunde chache tu baadaye tukawa tumeifikia nyumba hiyo. Shamsa akaliegesha gari nyuma ya gari la Esmail. Wakati analizima moto gari hilo tuliona mtu akitoka katika nyumba hiyo. Alikuwa amebeba begi lililokuwa limejaa na alionekana dhahiri kuwa alikuwa na wasiwasi na alikuwa akikimbizia kitu.
Alishuka haraka haraka kwenye baraza ya nyumba akajipakia kwenye lile gari lililokuwa mbele ya gari la Esmail na kuondoka kwa kasi.
Tulishuka haraka kwenye gari tukaenda kwenye mlango wa nyumba ya Esmail. Mimi nilitaka kubisha mlango lakini Shamsa aliusukuma. Mlango ukafunguka. Shamsa akaingia na mimi nikamfuata.
Kisaikolojia tu nilikgundua kuwa Shamsa alikuwa amebadillika. Macho yake yalionesha dhahiri kuwa alikuwa amepanga shari.
Kusema kweli sikujua nini kingetokea humo ndani.
Kusema kweli sikujua nini kingetokea humo ndani.
Tulipofika sebuleni tulikuta maiti ya mtu iliyokuwa ikivyja damu kichwani.
Shamsa akanitazama na kuniambia.
“Unaona! Wanamalizana wenyewe kwa wenyewe. Yule aliyetoka na begi amemuua mwenzake ili apate yeye pesa na dhanhabu”
“Na ameshakimbia. Sijui tutampataje?’
“Tutampata. Napajua anapoishi Esmail”
“Basi twende tumfuate kabla hajatokomea na zile pesa”
Tukatoka.
Tulijipakia kwenye gari. Aliyekuwa akiendesha alikuwa Shamsa.
Tulikwenda hadi nyumbani kwa Esmail. Shamsa akaniambia nijifiche nyuma ya mlango. Yeye ndiye aliyebisha mlango.
Dakika chache baadaye mlango ukafunguliwa. Shamsa akaingia.
“Amour njoo” akanimbia.
Na mimi nikaingia. Niliona Shamsa alikuwa amemtolea bastola Esmail.
“Tunataka zile pesa pamoja na dhanhabu a Abdi” Shamsa alimwambia Esmail akiwa amemuelekezea bastola.
Esmail alikuwa ameinua mikono juu akirudi kinyume nyume.
“Sina pesa wala dhahabu za Abdi” akasema huku macho yake yakionesha wasiwasi.
“Eti nini? Si tumekuona ukikimbia na begi la pesa na dhahabu baada ya kumuua mwenzako. Toa lile begi mpumbavu wewe kabla sijakisambarati
sha kichwa chako kwa risasi!”
“Subirini, nitawapa”
“Hakuna cha kusubiri. Toa lile begi haraka”
Esmail alifungua mlango wa chumba kimojawapo.
“Unataka kwenda wapi?” Shamsa akamuuliza.
“Lile begi liko humu”
“Huwezi kuingia peke yako. Ngoja tuingie sote”
Shamsa akaingia pamoja na Esmail ndani ya kile chumba na mimi nikawafuata.
Kilikuwa chumba kilichotumika kama astoo. Esmail alilitoa begi alilokuwa amelificha nyuma ya kabati bovu.
Wakati anampa begi hilo Shamsa alipambana na risasi ya kichwa. Esmail akaanguka chini. Shamsa akalichukua lile begi.
Alilifungua na kulitazama ndani kasha akaniambia.
“Twende zetu”
Tukatoka na kujipakia kwenye gari.
Tulirudi nyumbani. Shamsa akanimabia tusilale nyumbani tutakamatwa. Tulikusanya nguo zetu pamoja na vitu vyetu muhimu rukavitia kwenye begi kasha tukatoka tena.
Tulijipakia kwenye gari. Shamsa akaniambia tunakwenda katika mji ulioko mpakani mwa Kenya ili tuondoke nchini humo.
Tulipofika katika mji huo tulikodi chumba katika hoteli moja. Lengo letu lilikuwa ni kusubiri wakati wa usiku tuvuke mpaka kwa njia za panya ili tuingie Kenya. Tulipanga lile gari tulilokuwa nalo tulitelekeze pale pale hoteli. Tusiwengeweza kuingia nalo Kenya kwani tungeweza kukamatwa kirahisi.
Tukiwa katika chumba cha hoteli tulishangawa tulipoona tangazo kwenye televisheni lililohusu kuuawa kwa Abdi na Esmail. Msemaji wa polisi alieleza kuwa polisi wanashuku kwamba watu hao waliuawa na mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja la Amour ambaye alikuwa mfanyakazi wa Abdi.
Huku picha yangu ikioneshwa katika tangao hilo msemaji huyo wa polisi aliendelea kueleza kuwa polisi wananitafuta kuhusiana na mauaji hayo na kwamba nilikimbia mara tu baada ya kufanya unyama huo.
Aidha taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya kufanya uuaji huo nilipora mamilioni ya pesa na watu hao kukimbia.
Msemaji wa polisi akaelea kuwa yeyote atakayetoa taarifa ya kukamatwa kwangu atazawadiwa mamilioni ya pesa za Somalia.
Kutokana na mshituko na mshangao nilioupata nikatazamana na Shamsa.
“Kumbe polisi wananitafuta!” nikamwambia Shamsa.
“Usijali, sisi tutaondoka usiku huu kwenda Kenya”
“Unadhani hawatanikamata?”
“Watakupata wapi. Nani anajua kama uko hapa?”
“Basi tuharakishe tuondoke”
“Hapa itabidi tuondoke saa nne usiku. Tutakaa tu humu chumbani”
Ilipofika saa tatu nikaona gari la polisi likisimama mbele ya hoteli. Nilikuwa niikichungulia kwenye dirisha nikaliona. Niliona polisi sita waliokuwa na bunduki wakishuka kutoka kwenye gari hilo.
Shamsa njoo uone!” nikamwambia Shamsa.
“Kitu gani?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Polisi wamekuja. Nadhani wamepata taarifa kuwa niko hapa”
“Wamejuaje” Shamsa akaniuliza huku akisogea kwenye dirisha na kuchungulia.
“Watu wameiona picha yangu iliyotolewa kwenye lile tangazo. Inawezekana wamepigiwa simu na wafanyakazi wa hii hoteli baada ya kuiona ile picha”
“Usijali”
“Kwanini unaniambia nisijali wakati nitakamatwa wakati wowote?”
“Amour hutakamatwa. Kaa kwenye kitanda nikwambie”
Nikakaa kwenye kitanda na Shamsa naye akakaa na kunitazama.
“Unajua kwamba uko na Zena?” Shamsa akaniambia kwa kuniuliza.
“Huyo Zena yuko wapi?” nikamuuliza.
“Ni mimi”
“Wewe ni Zena! Shamsa unafanya mzaha!”
“Si mzaha. Mimi ni Zena kweli. Wewe ulioana na Zena si Shamsa. Sikiliza nikueleze…”
Shamsa akanipa hadithi ya ajabu iliyonishangaza. Aliniambia kwamba alipoona Abdi alikuwa anataka kuniozesha Shamsa akajigeuza yeye Shamsa na Shamsa halisi alimfanya kuwa taahira na alimsafirisha katika mji mwingine.
Aliniambia kwamba siku zote nilikuwa nikiishi naye nikimdhani kuwa ni Shamsa kumbe siye.
Hadithi ile ilinishitua sana. Nikamwambia Shamsa.
“Nitaaminije kuwa wewe ni Zena na si Shamsa?”
“Subiri” Shamsa akaniambia na kuufinika uso wake kwa kanga.
“Sasa nifunue hii kanga” Sauti yake ikaniambia.
Nikaifunua ile kanga. Nilipomtazama. Nikaona alikuwa ameshabadilika na kuwa Zena. Wakati mimi nimepatwa na mshangao, yeye alikuwa anatabasamu.
“Kumbe ni kweli!” nikajisemea.
“Je utaendelea kuniogopa tena wakati umeshanizoea?” Zena akaniuliza huku akiendelea kutabasamu.
Unadhani ningemjibu nini wakati polisi wameshafika pale hoteli?”
“Sitakuogopa tena”
“Nimefurahi kusikia kauli yako hiyo”
Mara tukasikia mlango unagongwa kwa kishindo. Nikajua walikuwa ni wale polisi. Walikuwa wameshaelekezwa chumba tulichokuwemo.
“Sasa Zena tutafanyaje?” nikamuuliza Zena.
INAENDELEA...

0 Comments