Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Mwanamke jini sehemu ya nne (04)

 


ILIPOISHIA

Zena akacheka. Alipofanya hivyo haiba ya uso wake ilibadilika na kuwa ya kupendeza zaidi.
“Uliniona katika umbo gani?” akaniuliza.
“Mwili wako ulikuwa na manyoya marefu na miguu yako ilikuwa na kwato kama ya punda. Kwa kweli nilipatwa na uoga mkubwa”
“Ndiyo maana siku ile uliponiona kule Mabanda ya Papa ukaongeza mwendo mpaka ikatokea ile ajali?”
“Kumbe unajua. Ni kweli niliongeza mwendo baada ya kukuona wewe”
Msichana akacheka tena.
“Hukupaswa kunikimbia. Iile umbo uliloniona nalo nyumbani siku ile ndilo umbo langu kwa maana mimi si binaadamu bali ni jini”
“Nilishafahamu kuwa wewe si binaadamu. Binaadamu hawezi kuwa na umbo kama lile”
“Nimefurahi kama umenielewa, kwa hiyo usiniogope tena”
“Kukuogopa ni lazima kwa sababu sijakuzoea”
“Taratibu tu utanizoea. Mimi nimekuwa na wewe kwa miaka mingi bila wewe mwenyewe kujua”
“Umekuwa na mimi kwa miaka mingi?”
“Ndiyo. Naweza kusema tangu ukiwa kijana mdogo”
“Ulikuwa uko wapi?”
“Nilikuwa na wewe”
“Sijawahi kukuona”
SASA ENDELEA
“Ni kweli. Sikutaka unione wala kujitambullisha kwako kwa sababu muda wa wewe kunitambua mimi ulikuwa haujafika”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikaguna. Lakini niliguna moyoni mwangu.
“Siku ile niliyokuazima kitabu ndio siku ambayo nilipanga kujitokeza rasmi kwako”
Nikabaki kimya nikimsikiliza. Maneno yake yalikuwa yameshitua akili yangu.
“Samahani kwa matatizo yote yaliyokutokea ambayo kwa namna moja au nyingine niliyasababisha mimi. Haikuwa kusudio langu kukusumbua bali nililazimika kufanya vile ili uweze kunitambua” Zena aliendelea kuniambia.
“Umeniambia kwamba wewe ni jini, ni jini wa aina gani na unaishi wapi?” nikamuuliza ili niweze kumuelewa vizuri.
“Mimi ni jini wa ukoo wa Ummi Subian, yaani nimechanganya kabila mbili, upande mmoja ni ruhani na upande mwingine ni subian. Yaani ninatumia bara na pwani lakini zaidi mila zangu ni za kipwani”
Nilidhani alikuwa amemaliza. Akaendelea.
“Umeniuliza ninaishi wapi. Kwetu ni Sham na kwa hapa Afrika Mashariki maskani zangu zipo katika eneo lote hili la pwani ya Afrika Mashariki kuanzia Somalia, Kenya na Tanzania.
“Niliwahi kukwambia jina langu ninaitwa Zena. Baba yangu anaitwa Jabalkeys na mama yangu ni Ummi Mariam. Huko ujinini mimi natambulika kama Zainush binti Jabalkeys”
Alipofika hapo Zena alinitazama akaniuliza.
“Umenielewa vizuri?”
“Nimekuelewa” nikamjibu.
“Kuna kitu kimoja nataka nikwambie” akaniambia.
“Niambie”
“Nimekuchunuka na ninataka uwe mume wangu. Ninakuahidi kuwa nitakupa utajiri”
Nikashituka.
“Kama wewe ni jini, nitawezaje kuwa mume wako?” nikamuuliza.
“Majini huoana na binaadamu. Kama huamini nenda kwa bibi yako aliyemzaa baba yako, muulize baada ya kuachika yeye mume wake alioa mke gani?”
“Una maana gani, una maana kwamba babu yangu alioa jini?” nikamuuliza kwa mshangao.
“Nataka uende ukamuulize yeye, akueleze”
“Sawa. Nitakwenda kumuuliza”
“Tutakutana lini tena?”
“Niambie wewe”
“Unadhani ni lini utakuwa na jibu?”
“Labda keshokutwa”
“Basi nitakutafuta”:
“Sawa”
Zena akafungua mkoba wake. Nilikuwa namtazama pembeni mwa macho yangu.
Nikaona akitoa kitita cha noti nyekundu. Nilizikisia zilikuwa zaidi shilingi milioni moja. Akanipa bila kuzihesabu.
“Chukua hizo zitakusaidia” akaniambia.
“Asante sana” nikamwambia.
Zena akafunga mkoba wake na kunitazama huku akitabasamu.
“Una kitu chochote unataka kuniambia?” akaniuliza.
“Hapana, sina kitu cha kukwambia”
“Basi tuagane uende zako na mimi niende zangu”
“Mimi nashukuru tu kukutana na wewe”
Huku tabasamu likiendelea kutawala usoni kwake akaniambia.
“Asante”
Akanyanyuka.
“Kwaheri” akaniaga na kuondoka.
Nikiwa bado nimekaa nilimtazama wakati akienda zake. Alivuka viti kadhaa kabla ya kutokea kwenye njia iliyokuwa ndani ya bustani. Kulikuwa na vijana wawili waliokuwa wamekaa katika kiti kimoja nyuma yetu. Walikuwa na baskeli waliyokuwa wameiegesha mbele ya kiti walichokuwa wamekaa.
Walipomuona yule msichana Zena anaondoka waliinuka wakapakiana kwenye baskeli na kumfuata.
Wakati wanampita, yule kijana aliyekuwa amepakiwa nyuma aliuvuta mkoba wa Zena akauchomoa na kuuchukua. Zena alipogutuka vijana hao walimpita na baskeli na kukimbia.
Zena akabaki amesimama akiwatazama vijana hao kwa hasira. Mkoba wake ulikuwa umekwenda!
Nikanyanyuka kwenye kiti na kumfuata haraka. Wale vijana walikuwa wameshafika barabarani wakaelekea upande wa Chumbageni kwa mwendo wa kasi.
“Wamepora mkoba wako?” nikamuuliza.
“Basi waache tu, huwezi kuwafanya kitu” Zena alisema. Sauti yake ilikuwa tulivu lakini ilionesha ghadhabu.
“Wale vijana walikuwa wamekaa muda mrefu nyuma yetu, kumbe walikuwa na lao wanalongojea”
“Hakuna tatizo”
Nilikuwa nafuatana naye kuelekea kwenye lango la kutokea kwenye bustani hiyo.
“Dah!....”
“Usijali, waache tu. Mimi nakwenda zangu”
Ile teksi iliyomleta Zena ikatokea tena na kusimama mahali pale pale pa mwanzo.
Zena akaifuata na kujipakia. Teksi ikaondoka. Niliisindikiza kwa macho hadi ilipokata kona.
“Majini pia wanapanda teksi!” nikajisemea moyoni mwangu kisha nikaanza kutembea kwa miguu kurudi nyumbani.

Kile kitendo cha wale vijana kilikuwa kimefadhaisha akili yangu.
Sikurudi nyumbani moja kwa moja, nilikwenda nyumbani kwa kaka. Aliponiona tu akaniuliza.
“Ulifika huko Uhuru Park?”
“Nimefika na nimekutana naye”
“Enhe amekueleza nini?”
“Kwanza amenirudishia hiki kitabu changu nilichokuwa nimemuazima siku ile kisha akaniomba msamaha kwa usumbufu wowote ambao niliupata kutokana na yeye”
“Enhe…?”
“Baada ya hapo akanithibitishia
mwenyewe kwamba yeye ni jinni. Akaniambia kwamba nisimuogope kwani hatakuwa na madhara na mimi. Lakini la msingi aliloniambia ni kuwa anataka niwe mume wake…”
“Mume wake kivipi?”
“Nafikiri anataka tuoane”
“Eh…utamuweza kweli mke wa kijini? Kumbe ana makubwa!”
“Nimemuuliza kwani majini wanaoana na binaadamu? Akaniambia niende nikamuulize bibi mzaa baba, eti baba yangu baada ya kumuacha yeye alioa mke gani?”
“Alikuwa na maana gani?”
“Ameniambia nikamuulize tu halafu nije nimpe jibu”
“Kumbe anamjua pia bibi yetu?”
“Ameniambia amekuwa na mimi tangu nikiwa mdogo lakini hakuwa amejitokeza, kwa hiyo familia yetu atakuwa anaijua”
“Itakubidi hayo maneno ukamueleze mama”
“Nitakwenda kumueleza”
“Twende kwake sasa hivi”
Tukatoka na kaka kwenda nyumbani kwa mama. Tulienda kwa miguu. Njiani tulikuwa tukiendelea kuzungumza.
CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ameniambia kama nitaoana naye atanipa utajiri”
“Hilo si tatizo, tatizo ni kuwa na mke jini” Kaka akaniambia.
Nikajua suala hilo lilikuwa limemshitua na yeye.
Tulipofika nyumbani kwa mama, nikamueleza mazungumzo yote tuliyozungumza na Zena. Mama naye akashituka.
“Hebu nenda ukamuulize bibi yako kuhusu huyo babu yako usikie atakueleza nini lakini nakushauri usikubali kuoana na huyo mwanamke hata kama atakupa utajiri” Mama akaniambia.
“Mimi sijakubali, bado niko kwenye utafiti”
“Wewe ni binaadamu huwezi kuishi na mwanamke ambaye ni jini” Mama aliendelea kunisisitizia.
“Nitazingatia ushauri wako na nitakwenda kwa bibi hapo kesho” nikamwambia.
Bibi mwenyewe alikuwa akiishi Mwambani, mwendo wa kama kilometa kumi kutoka Tanga mjini. Kitongoji hicho kipo upande wa Kaskazini mwa jiji la Tanga katika barabara inayoelekea wilaya ya Pangani.
Siku ya pili yake nikaenda huko Mwambani kwa kutumia pikipiki yangu. Nilipofika nilimkuta bibi yuko barazani mwa nyumba yake akisuka ukili wake. Ingawa alikuwa kikongwe sana lakini bado alikuwa akijiweza kiasi kwamba alikuwa anaweza kusuka ukili wake.
Nilikuwa nimemnunulia kilo tano za sukari, nikampa.
Baada ya kuulizana hali nilimwambia licha ya kwenda kumsalimia pia nilikuwa na shida yangu.
“Shida gani?” akaniuliza.
“Nilikuwa nataka kujua eti baada ya wewe kuachana na marehemu mume wako yaani babu yangu, babu alioa mke mwingine?”
“Ndio alioa”
“Enhe niambie alimuoa nani?”
“Inasemekana alioa mke wa kijini, alikuwa akiitwa Zena na huyo Zena ndiye aliyefanya babu yako aniache mimi. Lakini mimi sikuwahi kumuona”
Nikashituka niliposikia maneno yale.
“Alimpata wapi huyo mke wa kijini?” nikamuuliza.
“Alimchunuka tu akamwambia aniache mimi amuoe yeye. Babu yako akakubali kuniacha kwa ajili ya kupata utajiri”
“Na ni kweli alipata utajiri?”
“Alipata utajiri mkubwa sana lakini siku chache kabla ya kufa kwake utajiri wote ulipotoea na huyo mke wake alitoweka pia”
“Wakati huo alikuwa umeshamzaa baba?”
“Baba yako alikuwa ameshazaliwa pamoja na kaka yake Abdul yaani baba yako mkubwa ambaye alifariki nchi za nje”
“Sasa baada ya babu kuoa mke wa kijini, nani aliwalea kina baba?”
“Aliniachia nao mimi, nikawalea hadi wakawa wakubwa”
Nikanyamaza kimya nikijiuliza kama Zena anayemsema bibi ndiye yule anayetaka nioane naye.
“Kwanini umeniuliza hivyo?” Bibi aliniuliza na kunizindua.
“Nimekuuliza tu bibi, kuna mzee mmoja alikuwa akifahamiana na marehemu babu, alinieleza kuhusu kisa hicho ndio nikaona nije nikuulize” nikamdanganya bibi. Sikutaka kumueleza ukweli kwamba kuna mwanamke wa kijini alinituma nimuulize.
“Ulikuwa huamini?”
“Nilikuwa siamini lakini baada ya wewe kunithibitishia sasa ninaamini”
“Wakati babu yako anakufa, watu walishangaa kuona mali yote aliyokuwa nayo imepotea. Na yule mke wake naye hakuonekana tena. Alitoweka wiki moja kabla ya kifo cha babu yako”
“Na huyo babu na mke wake walikuwa wakiishi maisha ya aina gani?”
“Waliishi maisha ya kawaida tu lakini mke wake alikuwa hajitokezi katika shughuli za watu”
“Babu alipokuacha uliona uchungu sana bibi?”
“Kwa kweli niliumia sana kwa sababu sikuwa nimemtenda kosa lolote na bado nilikuwa nampenda babu yako”
“Pole sana bibi”
“Oh! Wanipa pole leo wakati mambo yameshapita zamani!”
“Lakini bibi uliona babu alifanya jambo la busara kuoa mwanamke wa kijini?”
“Alilazimishwa na yule jini na aliahidiwa kupata utajiri. Kuna mganga mmoja aliniambia kama babu yako asingeniacha yule jini angeniua”
“Eh kumbe ni viumbe hatari kiasi hicho!”
“Ndivyo nilivyoambiwa, sijui kama ningeuliwa kweli”
Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa. Bibi alikuwa akiendelea kusuka ukili wake na mimi nilikuwa nikiumiza kichwa kwa kuwaza. Hatimaye nikauondoa ule ukimya.
“Kwa mfano mimi nikipata mke wa kijini, unanishaurije nioane naye?” nikamuuliza.
Bibi akacheka.
“Bibi mbona unanicheka?”
“Unanichekesha. Huyo mke wa kijini utampata wapi?”
“Kwani babu alimpata wapi?”
“Yule ni mpaka akuchunuke mwenyewe”
“Sawa. Je akinichunuka na kuniambia anataka tuoane, nikubaliane naye?”
“Hayo ni mawazo yako sasa, mimi nikushauri nini?”
“Unaweza kunishauri kwamba nioane naye au la”
“Hilo sio jambo la kushauriwa, ni uamuzi wako na huyo jini kama utampata. Kwani na wewe unataka kupata utajiri?”
“Hakuna asiyetaka utajiri bibi”
“Angalia sana, utajiri mwingine una matatizo. Ni bora uishi masikini hivyo hivyo”
Baada ya kimya kingine kifupi nikamuaga bibi. Wakati nataka kuondoka nikampa shilingi elfu ishirini. Bibi akanishukuru.
“Haya bibi nakwenda” nikamuaga bibi na kupanda pikipiki yangu.
“Uende salama, nisalimie wenzako”
“Nitakusalimia”

Nikawasha pikipiki yangu na kuondoka. Wakati narudi mjini mawazo yalikuwa yamesonga katika kichwa changu kuhusu yale maneno aliyonieleza bibi.
Sikuwa nikijua kama babu yangu alimuacha mke wake na kuoa mke wa kijini. Kwa vile babu mwenyewe alikufa zamani habari zake zilikuwa zimeshahaulika.
Lakini nilijiuliza Zena alijuaje habari ile? Nikawa na shaka sana kwamba huyo Zena aliyetajwa na bibi ndiye Zena yule yule.
Nikakumbuka kwamba aliniambia alikuwa na mimi kwa miaka mingi isipokuwa hakuwa amejitokeza kwangu hivyo nilikuwa sijui kama nina jini aliyenichunuka.
Pamoja na kufahamu ukweli wote huo bado nilikuwa na mtihani mgumu mbele yangu, mtihani wa kukubali kuoana na Zena kama alivyoniambia au kumkataa.
Mpaka muda ule naondoka kwa bibi sikuwa na uamuzi wowote. Nilitegemea kupata ushauri kwa kaka yangu na kwa mama yangu.
Nilikwenda moja kwa moja nyumbani kwa kaka. Nikamwambia.
“Ninatoka Mwambani kwa bibi”
“Umezungumza naye?” akaniuliza kwa shauku.
“Nimezungumza naye na anawasalimia”
“Amekuelezaje kuhusu madai ya babu kuoa mke wa kijini?”
“Amesema ni kweli, babu alioa mke wa kijini baada ya kumuacha yeye”
Kaka akashituka.
“Kumbe babu alioa mke wa kijini!”
“Tena alikuwa anaitwa Zena, jina lile lile la huyu anayenifuata mimi”
Kaka alikuwa amepigwa na butwaa.
Nikamueleza kwa kirefu maelezo ya bibi ambayo yalimshangaza sana.
“Isije kuwa jini huyo ndiye huyu huyu amejitokeza tena”
“Hata mimi nimekuwa nikijiuliza swali hilo hilo”
“Huyo bibi alikwambia aliwahi kumuona?’
“Ameniambia hakuwahi kumuona”
“Mimi nadhani jini mwenyewe ndiye huyo huyo, amejitokeza kwako”
“Inawezekana lakini nitakuja kumuuliza tupate uhakika”
“Sasa umeamua nini?”
“Bado ninakabiliwa na maswali mengi. Ninahitaji ushauri wenu ili niweze kuamua”
“Nenda nyumbani umueleze mama, usikilize atakwambia nini”
“Kwa upande wako unanishauri nini?”
“Hili ni suala la kujadiliana sote kwa pamoja lakini kwanza nenda kamueleze mama tusikie kauli yake”
“Sawa. Nitakwenda kumueleza mama”
CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kuzungumza kirefu na kaka nikaondoka nyumbani kwake na kwenda nyumbani kwa mama.
Wakati nafika nyumbani, mama alikuwa amelala. Mjukuu wake alikwenda kumuamsha chumbani. Alipoamka akaja sebuleni.
“Shikamoo” nikamwamkia.
“Marahaba. Habari za huko?” Mama akaniuliza.
“Huko ni kwema. Natoka Mwambani kwa bibi?”
“Ndio ulikwenda kumuuliza kuhusu babu yako?”
“Nimemuuliza ameniambia kwamba babu yetu alimuacha yeye akaoa mke wa kijini”
“Unaniambia ukweli mwanangu?” Mama akaniuliza kwa mshituko.
“Ameniambia bibi mwenyewe”
“Kumbe babu yako alioa mke wa kijini?”
“Alioa, na bibi anasema waliishi pamoja hadi babu alipofikiwa na umauti, yaani wiki moja kabla ya babu kufariki jini huyo alitoweka”
“Kama ni hivyo inaelekea babu yenu alikuwa mtu hatari sana!”
“Bibi ameniambia babu alipomuoa jini huyo alipata utajiri mkubwa, yaani yule jini alimpa utajiri lakini alipokufa utajiri wake ukapotea”
“Hata kama alipata utajiri, si jambo la kukubaliana nalo kirahisi”
“Sasa kitu ambacho kimenitisha ni kuwa huyo jini alikuwa anaitwa Zena kama jini huyu anayenifuata mimi!”
“Isije kuwa ndiye jini huyo huyo. Kwanini alikuwambia uende ukamuulize bibi yako”
“Inawezekana ndiye jini huyo huyo”
“Sasa sikiliza mwanangu, huyo jini epukana naye mara moja!”
“Kwanini mama?”
“Atakuharibia maisha yako, kama ni kuoa oa binaadamu mwenzako si jini”
“Kwa hiyo unanishauri hivyo?”
“Inawezekana ni ushauri au ni amri yangu na naomba unisikilize”
“Sawa, nitakusikiliza. Nilitaka tu nijue una maoni gani”
“Atakapokufuata tena mwambie mimi siwezi kukuoa wewe, nitaoa binaadamu mwenzangu. Kwani majini madume hakuna mpaka akufuate wewe!”
“Ndio nashangaa!”
“Huyo mke wa kijini kweli utamuonesha kwa wa watu, uwambie mke wangu huyu!”
“Hiwezekani”
“Kwanza watu watakushangaa na hawatakuja kwako. Mimi pia sitakuja”
Mama alikuwa amekasirika, sikutaka tena kumjibu kitu. Nikanyamaza kimya.
“Upuuzi mtupu! Amekutia katika misuko suko chungu nzima halafu uje uishi naye kama mke wako, kwanza hao watoto mtakaozaa watakuwa ni watoto wa aina gani...epukama na huyo shetani asikuletee mikosi. Kama ndiye huyo aliyeolewa na babu yako atokomee huko huko alikokuwa. Mimi simtaki!” Mama aliendelea kuniambia kwa hasira.
“Sawa mama nimekusikia”
Nilipoondoka kwa mama nikarudi nyumbani kwangu. Kusema kweli nilikuwa na mawazo mengi sana. Maneno ya mama yalikuwa yameingia akilini mwangu na wakati huo huo nilikuwa nafikiria endapo nitamueleza yule jini kwamba siwezi kuoana naye atanifanya nini.
Wakati naendelea kutafakari nikasikia mlango wangu wa mbele unabishwa. Nikanyanyuka na kwenda kuufungua.
Nilimuona mzee mmoja aliyekuwa amevaa koti jeusi na kanzu ya darizi pamoja na baraghashia. Nikamuamkia.
“Shikamoo mzee?”
“Marahaba, waonaje hali yako?”
“Nzuri, karibu”
“Asante. Nadhani hunifahamu?” akaniuliza.
“Ndiyo sikufahamu mzee wangu”
“Ninaishi mtaa wa pili. Kuna mwanangu mmoja ndiye aliyenielekeza hapa kwako”
“Una tatizo gani?” nikamuuliza kistaarabu.
“Unakumbuka jana majira ya saa nne asubuhi mpaka tano ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa maeneo ya mjini”
“Bila shaka ulikuwa umekaa katika Bustani ya Uhuru na msichana mmoja?”
“Ndio nilikuwa nimekaa hapo”
“Nimeambiwa kwamba wakati yule msichana uliyekuwa naye anaondoka, kuna vijana wawili waliokuwa na baiskeli walimpora yule msichana mkoba wake na kukimbia nao, ni kweli?’
“Ni kweli’
“Yule mzee alinyamaza kimya akitafakari kwa sekunde zisizopungua tano kisha akaniuliza.
“Huyo msichana ni nani wako?”
“Tunafahamiana tu, tulikuwa tumekaa tunazungumza”
“Sasa nataka kukueleza kitu kimoja. Mmoja wa wale vijana waliompora huyo msichana ni mwanangu. Jana usiku aliporudi nyumbani hatukulala”
“Kwanini?”
“Yule kijana alipoingia chumbani mwake tulisikia anapiga kelele. Mimi nikaenda kumuuliza ana matatizo gani, akaniambia kwamba kila anapopitiwa na usingizi anamuona mwanamke anampiga bakora. Nikamuuliza ni mwanamke gani huyo, ndio akanieleza kwamba kuna mwanamke walimpora mkoba wake na ndiye huyo anayemuona anampiga bakora.
“Hiyo hali iliendelea hadi asubuhi, kila akifumba macho tu anamuona, anamtandika. Bakora zimeota mgongoni mwake. Huyo mwanamke haonekani, anamuona yeye tu pale anapolala.
“Hii asubuhi tukaenda kwa huyo mwenzake, kumbe na yeye hali ni hiyo hiyo. Amepigwa bakora usiku kucha. Bakora zimeota kwenye mgongo wake. Kwa kweli nimewagombesha sana wale vijana kwa kututia aibu sisi wazazi wao kwa kujihusisha na vitendo vya kihalifu wakiwa bado wadogo, kuibia watu, kupiga watu na kuvuta bangi. Imebidi niwaulize ni mwanamke gani huyo waliyempora mkoba wake ndipo mwanangu aliponielekeza kwako. Kumbe alikuwa anakufahamu.
“Sasa mwanangu nimekuja, nakuomba unioneshe yule mwanamke nimlipe ule mkoba wake na nimuombe radhi ili wale vijana waondokewe na ile hali”
Yale maneno aliyonieleza yule mzee yalinishangaza na kunishitua. Wakati yule mzee ananieleza mimi nilikuwa natokwa na jasho.
“Kwani mpaka hii asubuhi wanaendelea kuchapwa bakora?’ nikamuuliza.
“Labda wakae bila kusinzia au kulala. Wanapolala kidogo tu tayari wanapiga kelele wanasema wanachapwa. Ni mpaka hii asubuhi hawajalala tangu jana wako macho tu. Wameshadhoofika. Kama hii hali itaendelea watakufa”
“Mzee wangu nikwambie ukweli, yule mwanamke tulikutana pale pale. Sijui anapoishi na sidhani kama nitamuona tena”

Mzee akashituka na kujishika kichwa.
“Mimi nilidhani unajuana na huyo mwanamke. Basi wale vijana hawatakuwa na maisha tena” Mzee akasema kisha akaniuliza.
“Unasema kweli, hujuani naye kabisa?’
“Sijuani naye mzee wangu, siwezi kukudanganya. Tulikutana pale pale, kila mmoja alikuja kivyake na aliondoka kivyake’
Mzee aliduwaa kwa sekunde zisizopungua kumi, alipozinduka aliniuliza.
“Hivi mwanangu utanisaidiaje na balaa hili?”
“Mzee wangu sina namna yoyote ya kukusaidia”
“Tuseme yule mwanamke alikwenda kwa mganga kuwaroga wale vijana?”
“Kwa waswahili hilo jambo linawezekana lakini siwezi kujua”
“Sasa nifanyeje?”
Sikumjibu yule mzee. Alionesha wazi alikuwa amechanganykiwa. Alipoona nipo kimya, aligeuka bila kuniaga na kushuka kwenye baraza ya nyumba yangu. Nikamsikia akisema peke yake.
“Kama hawatakoma, hawatakoma tena!”
Alipofika chini ya baraza ndipo alipokumbuka kuniaga.
“Haya kwaheri mwanangu” akaniambia.
Nilimuangalia yule mzee hadi alipokata kona mtaa wa pili, lakini mawazo yangu yalikuwa kwa Zena. Kitendo kile cha kuwatandika wale vijana bakora kilionesha kuwa mwanamke yule wa kijini alikuwa wa hatari.
Nilikumbuka wakati wale vijana wamempora mkoba wake alionekana mtulivu ingawa alionesha kuwa na hasira. Aliniambia “Waache tu” kumbe alikuwa na lake alilokuwa amelipanga.
Japokuwa niliwahurumia hao vijana lakini sikujua ningempata wapi huyo Zena ili nimwambie awasamehe hao vijana. Na hata kama ningekutana naye na kumwambia hivyo sikudhani kama angenisikia.
Nilirudi ndani na kuendelea kujiwazia. Nilihisi kwamba hata mimi maisha yangu yangeweza kuwa katika hatari kama nitakataa kumuoa Zena na kwa kweli hata hapo nitakapokutana naye nitashindwa kumueleza ukweli kwamba sikubaliani na matakwa yake ya kumuoa.
Kwa vyovyote vile yule mwanamke anaweza kunidhuru!
Nilipowaza hivyo nilitoka tena. Nikafunga mlango wangu na kuondoka na pikipiki yangu, nikaenda nyumbani kwa mama.
Kitendo cha kurudi tena kwa mama kilimshitua, akaniuliza.
“Kulikoni?”
“Nimerudi tena” nikamwambia.
“Ndio mana nimekuuliza kulikoni?”
Nikamueleza mama kile kisa cha yule jini kuwatandika bakora wale vijana waliomuibia mkoba wake.
“Baba wa mmoja wa wale vijana ameniambia hao vijana hivi sasa wako taabani wanamtafuta yule msichana wamuombe msamaha” nikamwambia.
Mama naye alishituka.
“Yaani wanapolala ndio wanamuona huyo msichana anawatandika bakora?”
“Ndio mama, na inakuwa usiku kucha na mchana kutwa. Miili ya wale vijana imeota makora migongoni”
“Huyo jini ni mbaya sana”
“Sasa nimefikiri hata mimi anaweza kuja kuniletea madhara kama nitakataa kumuoa”
“Ni kweli, sasa nikupeleke kwa mganga”
“Wapi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kule Mnyanjani, ni hodari sana kwa majini”
“Ndio maana nimekuja ili tushauriane kwenda kwa huyo mganga, vinginevyo naweza kupata balaa”
“Sasa nikupeleke lini?”
“Leo, twende leo”
“Saa ngapi?’
“Maliza kazi zako nitakufuata saa tisa twende”
“Sawa. Basi njoo hapo saa tisa twende”
Tulipokubaliana na mama nikaondoka. Wakati nafika nyumbani kwangu nikakutana na yule mzee akiondoka.
“Nimegonga mlango, nimeona kimya. Nilikuwa naenda zangu” akaniambia.
“Nilitoka kidogo”
“Nimekuja kukujulisha kuwa yule mwanangu ameshafariki dunia”
Nikashituka.
“Eh ameshafariki!”
“Amefariki kama nusu saa hivi iliyopita akiwa kwa mganga. Tulikuwa tumempeleka kwa mganga baada ya mateso kumzidia”
“Poleni sana jamani. Yule mwenzake naye anaendeleaje?’
“Sijapata habari zake. Nimekuja kukwambia hivyo, kwaheri mwanangu”
Mzee huyo akaondoka. Nilipata hofu sana. Sikuweza hata kuingia ndani. Niliona kama vile nitakutana na jini huyo, nikageuza pikipiki na kurudi kwa mama.
Nilipofika nilimuhadithia lile tukio la kufa kwa mmoja wa wale vijana.
“Nimekuja nikusubri hapa hapa, sikuingia hata nyumbani kwangu” nikamwambia.
Chakula cha mchana nilikula pale pale kwa mama. Baada ya kula ndipo tulipoondoka. Nilimpakia mama kwenye pikipiki tukaelekea huko Mnyanjani.
Wakati huo eneo hilo la Mnyanjani lilikuwa kama kitongoji cha mji huo. Likiwa karibu na ufukwe wa Bahari ya Hindi, lilikuwa moja ya maeneo ya kiasili ya mji wa Tanga yenye historia iliyosheheni utamaduni wa jiji hilo.
Eneo hilo hivi sasa limebadilika na kuwa na nyumba za kisasa na kuwa sehemu ya jiji hilo.
Ili ufike Mnyanjani unapita vitongoji kadhaa pamoja na viunga vya minazi. Ni mwendo wa karibu kilometa kumi.
Mama alinionesha nyumba ya mganga huyo iliyokuwa imejengwa kwa miti na udongo na kuezekwa makuti ya minazi.
Tukasimama na kubisha mlango.
“Karibuni” tukasikia sauti ya kiume ikitukaribisha.
Tukaingia ndani. Ukumbi ulikuwa giza. Kulikuwa na mwanga hafifu uliotokea kwenye mlango wa nje na wa uani.
Mganga mwenyewe alikuwa amekaa kwenye jamvi lililokuwa limetandikwa pale ukumbini. Alikuwa akikatakata mizizi ya dawa.
“Karibuni” akatuambia tena huku akitutazama.
“Tumeshakaribia” mama akamwambia na kisha kumuuliza hali.
Mimi nikamuamkia. “Shikamoo”
“Marahaba. Karibuni mkake kwenye jamvi”
Tukakaa kwenye jamvi.
“Tumekuja tuna shida” Mama akaanza kumwambia mzee huyo aliyekuwa amevaa kikoi cha rangi nyeupe.
“Shida gani?”

Mama akamueleza mkasa mzima. Yule mganga naye alishangaa akasema.
“Huyo atakuwa Ummi Subian au Kamari wa Subian”
“Tunataka aondoke kwa mwanangu, asimfuate fuate tena”
“Ngoja nimtazame nijue ni jini gani”
Mganga akachukua kitabu akakifungua kisha akatazama saa yake.
“Ni saa nane sasa” alisema peke yake kisha akatazama kwenye kitabu.
“Aliyetawala muda huu ni Zuhra Kadhi Lhawaiju” Mganga aliendelea kujisemea kisha akatutazama.
“Huyu mwanamke wa kijini ni ruhani aliyechanganya na usubian”
“Yeye mwenyewe pia aliniambia hivyo hivyo” nikamkubalia mganga huyo.
“Hawa majini ni ving’ang’anizi sana na ni wabishi, akitaka jambo lake ni mpaka alitimize”
“Lakini ataweza kumuacha huyu mwanangu?” Mama akamuuliza kwa wasiwasi.
“Ni kazi kubwa. Huyu jini ni wa kurithi, zamani aliwahi kuwa na babu yake huyu kijana”
“Ni kweli, bibi yangu alinieleza leo” nikamwambia mganga huyo.
“Alikuelezaje?”
“Aliniambia kuwa babu yangu alikuwa na mke wa kijini, anaitwa Zena”
Mganga akamtazama mama.
“Unasikia. Sasa kumtoa jini wa aina hii inataka kazi kubwa, si kazi ndogo”
“Sasa tufanyeje?” Mama akamuuliza.
“Nitahitaji mbuzi watatu, wa rangi nyeupe, rangi nyeusi na rangi mchanganyiko” Mganga alituambia kisha akatuuliza.
“Mtaweza kuwapata?”
“Watapatikana” nikajibu mimi.
“Mbali na hao mbuzi watatu, mnipatie maji ya bahari lita tatu, mchanga wa pwani unaofikia kilo moja na kipande cha mti kilichotoka katika eneo lililopiganwa vita”
“Hicho kipande cha mti tutakipata wapi?” nikamuuliza.
“Najua hiki kitawapa tabu, nitawapatia mimi”
“Huo mchanga wa pwani na maji ya bahari pia ungetusaidia wewe, tunaona hapa ni karibu na bahari”
“Gharama yake itakuwa shilingi elfu kumi na tano”
“Sawa.Tutatoa”
“Hao mbuzi watatu pia mnaweza kuwapata hapa hapa kama mtataka”
“Watakuwa kiasi gani?”
“Kila mbuzi mmoja ni shilingi elfu arobaini”
“Kwa hiyo kwa mbuzi watatu itakuwa shilingi laki moja na ishirini elfu”
“Ingiza na hizi elfu kumi na tano za vifaa”
“Zitakuwa laki moja na hamsini na tano elfu”
“Na kazi yangu shilingi laki moja”
“Jumla laki mbili na hamsini na tano elfu”
“Hizo pesa zikipatikana, njooni niwafanyie kazi yenu”
“Pesa zipo lakini zipo nyumbani, labda utupe muda nikazichukue” nikamwambia mganga huyo.
“Hizo pesa nikizipata leo, kwanza nitashughulikia kupata hivyo vitu, Kesho saa mbili asubuhi ndio nitakushughulikia wewe mwenyewe”
“Sawa. Sasa acha turudi. Baadaye nitakuja na hizo pesa.
Baada ya kukubaliana na mganga huyo tuliondoka. Nilimpakia mama kwenye pikipiki nikamrudisha nyumbani kwake kisha mimi nikaenda nyumbani kwangu kuchukua hizo pesa. Zilikuwa ni pesa zile zile alizonipa Zena.
Nilitia mfukoni shilingi laki tatu nikaondoka tena na pikipiki kwenda Mnyanjani. Nilipofika nilimpa yule mganga shilingi laki mbili na hamsini na tano elfu.
“Sasa nenda, uje kesho saa mbili asubuhi, utakuta kila kitu kipo tayari” Mganga akaniambia.
“Sasa nilikuwa na ombi moja” nikamwambia.
“Ndio”
“Nina wasiwasi huyo jini anaweza kunifuata hii leo kutokana na hivi ambavyo nataka kumshughulikia, sasa itakuwaje?
“Nitakupa hirizi, kuwa nayo mfukoni hadi hapo kesho”
“Nikiwa na hiyo hirizi hatanifuata?’
“Abadani. Hawezi kukufuata”
“Basi nipatie hiyo hirizi’
Hirizi yenyewe ilikuwa imeshatayarishwa tayari. Mganga akanipatia. Nikaichukua na kuitia mfukoni.
Nikatoka na kupanda pikipiki yangu. Sasa kidogo moyo wangu ulikuwa na matumaini. Ile hofu niliyokuwa nayo ya kukutana na Zena ilikuwa imenitoka.
Wakati nakaribia kulitoka eneo la Mnyanjani, niliona mtu amesiamama pembeni mwa barabara chini ya mti wa mwembe. Nilipoukaribia mwembe huo nilishituka nilipoona mtu mwenyewe alikuwa Zena. Alikuwa amesimama kama aliyekuwa akisubiri mtu.
Nikaongeza mwendo ili kumkwepa na nikajifanya sikumuona. Wakati pikipiki imeshika kasi nikahisi kama kulikuwa na kitu nyuma yangu. Nikageuza uso wangu kutazama nyuma. Nilishituka tena. Alikuwa ni Zena aliyekuwa amekaa kwenye siti ya nyuma ya pikipiki yangu!
Sikuweza kujua alipakiaje kwenye pikipiki yangu wakati alikuwa amesimama kwenye mti ambao nilikwishaupita, tena nikienda kwa kasi. Kutokana na mshituko nilioupata mikono yangu ilitetereka nikajikuta ninaanguka na pikipiki. Mimi na Zena tukawa chini!
Nikainuka haraka. Lakini Zena alikuwa mwepesi zaidi. Nilimkuta tayari ameshasimama.

“Inua pikipiki yako” akaniambia.
Nikiwa nimetahayari nikaushika usukani wa pikipiki na kuiinua.
“Isimamishe” akaniambia tena.
Nikaiwekea standa.
“Unatoka wapi?”
“Mimi?’
“Jamani kwani nazungumza na nani?”
“Natoka kule…”
“Wapi?”
“Mnyanjani”
“Kufanya nini?”
Nikatunga uongo.
“Kumsalimia mjomba wangu”
Zena akanitazama kwa karibu nusu dakika bila kuniambia chochote. Bila shaka aligundua kuwa nilikuwa namdanganya. Wakati Zena akinitazama jasho jembamba lilikuwa linanitoka. Nilikuwa nikilihsi likitiririka kwenye uti wa mgongo wangu.
Nilikuwa najiuliza yule mganga alinipa hirizi akaniambia nikiwa nayo mfukoni Zena hatanifuata, mbona niko naye hapa?
CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Humo mfukoni umetia nini?” Sauti ya Zena ikanishitua.
Alikuwa akiutazama mfuko wa suruali yangu ambao nilitia ile hirizi.
“Wapi?” nikamuuliza tena nikijifanya sikumuelewa.
“Nimekuuliza humo mfukoni mwako umetia nini?” Zena akaniuliza tena sasa kwa sauti ya ukali kidogo.
“Sijatia kitu, ni pesa zangu tu” nikamjibu.
“Hebu tia mkono wako mfukoni” akaniambia.
Nikatia mkono kwenye mfuko mwingine.
“Sio huo, tia kwenye mfuko huu”
Zena alinionesha mfuko huo kwa kidole chake.
Nikatia mkono kwenye mfuko huo.
“Hebu toa hicho kitu ulichokigusa”
Bila kupenda niliitoa ile hirizi.
“Hebu nioneshe”
Nikamuonesha, hata haikumshtua.
Akaishika na kuiweka kwenye kiganja chake kisha akanitazama.
“Nini hii?’ akaniuliza kwa dharau.
Sikumjibu. Nilikuwa nimefadhaika sana.
“Wewe unajidanganya sana, sikujua kama unaweza kuwa mpumbavu kiasi hicho. Shika hirizi yako” akaniambia.
Nikaichukua ile hirizi.
“Itupe kule!” akaniambia akinionesha kitu kilichokuwa kando yetu.
Nikaitupa. Ningefanyaje? Sikuwa na la kufanya. Hirizi yenyewe haikumtisha hata kidogo. Bora kuitupa tu.
“Nipakie twende zetu” akaniambia akiwa ameridhika kwa kile kitendo cha kuitupa ile hirizi.
Sikutaka hata kumuuliza twende wapi, nikawasha pikipiki iliyokuwa imezimika kisha nikaipanda. Zena akakaa nyuma yangu. Nikatia gea na kuondoka.
Nilikuwa naendesha pikipiki huku natetemeka mpaka Zena akaniuliza.
“Unatetemeka nini?”
“Sitetemeki” nikamjibu huku nikijua kuwa nilikuwa natetemeka.
Akanyamaza kimya. Hakunisemesha kitu mpaka tulipoingia mjini.
“Nishushe hapa” akaniambia mara tu tulipoipita hospitali ya Makorora.
Nikashukuru kusikia kauli hiyo. Nilikuwa nikihisi kama nimepakia chatu nyuma yangu. Nikaisimamisha pikipiki haraka na kushusha mguu wangu.
Zena akashuka.
“Niache hapa hapa. Wewe nenda zako” akaniambia.
Ingawa sauti yake ilikuwa tulivu lakini uso wake ulikuwa umekasirika. Nikamuona anavuka barabara na kuelekea upande wa hospitali ya Makorora.
Nikatia gea na kuiondoa pikipiki yangu taratibu. Sikutazama nyuma tena. Nilipofika kwenye mzunguko wa barabara ya Pangani nilikata kulia nikaelekea nyumbani kwa mama. Sikutaka kwenda nyumbani kwangu ingawa palikuwa karibu na hapo.
Nilipofika nyumbani kwa mama nikamueleza tukio zima lililokuwa limenitokea. Mama akashituka.
“Sasa huyo shetani amekwenda wapi?” akaniuliza.
“Sijui amekwenda wapi. Nimemuacha karibu na hospitali ya Makorora”
“Ina maana alikufutilia kule kwa mganga”
“Nafikiri. Amejua kuwa nimepewa hirizi na akaona iko mfukoni mwangu”
“Sasa itakuwaje?”
“Hata sijui. Hapa mwili wote unanitetemeka”
“Sasa ungerudi umueleze yule mganga”
“Unanishuri nirudi tena kwa yule mganga?”
“Ndio. Umueleze habari yote. Yeye ndio atajua la kufanya”
“Sasa twende sote. Yule jini asije akanifuata tena”
“Ngoja twende”
Dakika chache baadaye mimi na mama yangu tukawa kwenye pikipiki tukielekea Mnyanjani kwa yule mganga. Tulipofika pale mahali nilipoanguka na pikipiki nilimuonesha mama.
“Mahali tulipoanguka ni hapa” nikamwambia.
“Na huyo jini mwenyewe ulimuona amesimama wapi?”
“Alikuwa amesimama kwenye mti ule pale”
Nikamuonesha mti wa mwembe nilipomuona Zena amesimama.
“Inaonekana alikuwa akikufuatilia wewe” Mama akaniambia.
Tulipofika nyumbani kwa mganga tulikuta vilio vimetawala ndani ya nyumba huku nyumba yenyewe imeja watu hadi nje.
“Kuna nini?” nikamuuliza mama kabla ya kushuka kwenye pikipiki.
“Ngoja tuulize” Mama akaniambia.
Tulishuka kwenye pikipiki. Mtu mmoja alipotuona tulikuwa wageni akatufuata.
“Karibuni” akatuambia.
“Tumeshakaribia” Mama akamjibu.
“Habari za hapa?” nikamuuliza.
“Hapa si kwema, tumepata msiba” yule mtu akatuambia.
“Msiba wa nani?”
“Msiba wa huyu bwana aliyekuwa anaishi katika nyumba hii”
Nikatazamana na mama yangu kisha nikaendelea kumuuliza yule mtu.
“Sisi tunachojua ni kuwa mwenye nyumba hii ni yule mganga wa kienyeji”
“Niye huyo huyo aliyefariki”
Nikatazamana tena na mama yangu, sasa kwa mshituko.
“Dakika chache tu zilizopita si nilikuwa naye hapa?” nikauliza.
“Kufariki kwake kulikuwa kwa miujiza sana. Niliambiwa alikuwa akizungumza na mteja wake mmoja aliyefika na pikipiki, nafikiri ulikuwa wewe”
“Nadhani nilikuwa mimi kwani si muda mrefu sana nilipoondoka hapa”
“Basi mara tu ulipoondoka, yule mganga aliingia chumbani mwake. Mke wake alikuwa jikoni akasikia sauti ya mume wake akipiga kelele kuwa anakabwa na mwanamke. Mpaka mke wake anaingia chumbani alimkuta ameshakufa”
“Nikaguna na kumtazama mama.
“Mama umelisikia hilo tukio?”
“Nimelisikia” Mama akajibu kwa sauti iliyonywea kisha akaniambia.
“Basi twende zetu”
“Nilikuwa nimempa pesa kwa ajili ya kunifanyia kazi yangu ambayo tulipatana aifanye kesho lakini nitamsamehe” nikasema.
“Ulimpa kiasi gani?’ yule mtu akaniuliza.
“Kama laki mbili hivi. Lakini nitasamehe”
“Kama umeamua kuzisamehe ni jambo zuri”
“Poleni sana kwa msiba huo” nikamwambia na kupanda kwenye pikipiki yangu.
“Haya kwaheri baba” Mama akumuaga yule mtu kabla ya kukaa nyuma yangu. Tukaondoka.

“Mama umeona mambo hayo!” nikamwambia mama wakati ninaendesha pikipiki kurudi mjini.
“Nimeona. Kwa kweli ni kifo cha kushangaza sana”
“Mimi nadhani ni yule jini amekuja kumuua yule mganga”
“Itakuwa ndiye yeye, kwa sababu alisema kuna mwanamke anamkaba. Sasa alikuwa mwanamke yupi kama sio yule jini?”
“Sasa haya yamekuwa mapambano!”
“Tutatafuta mganga mwingine”
“Sasa usalama wangu utakuwa wapi? Nimeshashuhudia watu wawili waliouawa leo. Yule kijana aliyekuwa anatandikwa na huyu mganga. Bado kuna na yule kijana mwingine. Naona pia atakuwa ameshakufa”
“Tukifika tutakwenda kulizungumza vizuri hili suala pamona na kaka yako”
“Sasa nimeshaona huyu mwanamke ni wa hatari”
Nilimpeleka mama nyumbani kwake kisha nikaenda Chuda kumchukua kaka.
Nilimueleza kwa kifupi hayo matukio.
“Mama ameniambia nije nikuchkue twende tukayazungumze haya mambo”
Ule muhutasari wa habari niliomueleza kaka tayari ulikuwa.
Nikampakia kwenye pikipiki yangu tukaondoka.
Tulipofika nyumbani kwa mama tukalizungumza lile suala ambalo kaka lilimshitua sana.
“Kumbe yule jini ni hatari sana. Tulivyomuona pale mahakamani siku ile alionekana ni msichana mpole sana” Kaka akasema kwa mshangao.
“Lile umbile ulilomuona nalo ni la kujipachika, si umbile lake halisi. Katika umbile lake halisi anatisha” nikamwambia kaka.
“Kwa kweli inabidi muepukane haraka, sasa tutafanyaje wakati mtaalamu muliyemtegemea ndio ameuawa kwanza?”
“Itakuja kuwa yeye!” Mama akamalizia akimaanisha mimi.
“Sasa tufanyeje jamani, jua linakuchwa hili!” nikawahimiza wenzangu.
“Hapa la kufanya ni kumuona mganga mwingine haraka iwezekanavyo” Kaka akashauri.
“Bila kupata mganga mwingine, mimi leo sitalala, nina hofu” nikawambia.
“Usijali, tutkwenda kwa mganga wa Amboni. Yeye pia namfahamu. Ni hodari” Mama akasema.
“Sasa twende sasa hivi kwa sababu jua linakuchwa”
“Ingekuwa kaka yako anapafahamu angekupeleka lakini itabidi nikupeleke mimi”
“Mpeleke tu halafu mtakuja kunijulisha” Kaka akamwambia mama.
Dakika chache baadaye tulikuwa tumetoka nje, nilimpakia mama kwenye pikipiki. Kaka yangu naye akaondoka kurudi kwake kwa miguu.
Amboni ni kitongoji cha mji wa Tanga kinachokuwa kwa haraka. Kipo katika barabara ya Horohoro inayokwenda Mombasa nchini Kenya. Kutoka Tanga hadi Amboni ulikuwa mwendo upatao kilometa nane hivi.
Kitongoji hicho kimepata umaarufu kutokana na mapango yaliyoko katika eneo hilo, maarufu kama Mapango ya Amboni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati tunafika Amboni jua lilikuwa limeshakuchwa. Matumaini yangu yalikuwa madogo sana kupata huduma katika muda ule. Hofu yangu kubwa ilikuwa ni kwa usiku. Kama Zena alikusudia kunifanyia jambo baya lolote, nilijua kuwa alikuwa akisubiri usiku nikiwa niko nyumbani peke yangu.
Hapo Amboni palikuwa na eneo linaitwa Mafuriko. Eneo hilo liliwahi kupata mafuriko makubwa katika miaka ya nyumba na kusababisha kupewa jina hilo.
Mganga tuliyemuendea alikuwa akiishi katika eneo hilo. Kwa vile mama aliwahi kufika kwa mganga huyo katika siku za nyuma hatukusumbuka kuuliza. Tulikwenda moja kwa moja kwenye nyumba yake.
Tulikuta mzee aliyeketi barazani mwa nyumba hiyo akivuta Mtemba. Alikuwa amekaa kwenye kiti cha uvivu kando ya mlango wa nyumba yake.
Kumbe alikuwa ndiye mganga mwenyewe tuliyemuendea.
Tulisaliana naye. Mama akamwambia kuwa tulikuwa tumemfuata yeye.
“Karibuni ndani” akatuambia.
Nikapata matumaini kidogo.
Mganga huyo alikuwa na chumba chake maalum cha uganga. Tulipoingia katika chumba hicho alitukaribisha kwenye majamvi, yeye mwenyewe aliketi kwenye kigoda kidogo kilichokuwa kwenye pembe moja ya ukuta.
“Habari za huko mtokako?” akatuuliza.
“Habari si nzuri. Tuna matatizo” Mama akamwambia.
“Matatizo gani?”
“Ni matatizo ambayo si ya kawaida. Huyu niliyenaye hapa ni mwanangu. Yeye ndiye anayehusika na hayo matatizo….”
Mama akamueleza matatizo yaliyokuwa yametupeleka. Mganga akatuambia.
“Subirini kidogo niwaite wenyewe muwaeleze”
Akamuita mke wake. Mwanamke huyo alipokuja alimwambia amletee moto. Baada ya muda kidogo mwanamke huyo alileta makaa ya moto kwenye chetezo ambacho alikiweka mbele ya mganga huyo.

INAENDELEA

Post a Comment

0 Comments