Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake hakimu aliahirisha kesi kwa wiki moja.
Nilikuwa nikienda kazini kama kawaida ila pikipiki yangu ndiyo ilikuwa imezuiwa na polisi. Wakati mwingine nilikuwa nikijipa moyo kuwa nitashinda kesi na wakati mwingine nilikata tamaa. Niliona jela ilikuwa inaningoja kwa vile sikuwa na pesa za kulipa faini wala kulipia gharama za shirika la umeme.
Siku ya kesi ikawadia. Upande wa mashitaka ukaeleza kuwa ulikuwa umemaliza mashahidi wake. Na mimi nikatakiwa nipeleke mashahidi kama nilikuwa nao.
Nikasema kwamba sikuwa na shahidi. Kesi ikaahirishwa tena ili kuupa nafasi upande wa mashitaka kuandaa maelezo ya mwisho ya kuishawishi mahakama inione kuwa nina hatia. Na pia kunipa nafasi mimi ya kuandaa utetezi wangu baada ya kusema kuwa sikuwa na shaahidi.
Kuahirishwa kwa kesi hiyo kulifanywa kwa wiki mbili. Wiki mbili zikapita kwa haraka, tukakutana tena mahakamani.
Upande wa mashitaka ukatoa maelezo yake ya mwisho ya kuionesha mahakama kuwa nilikuwa na hatia.
Mwendesha Mashitaka alisema “ Ushahidi uliotolewa hapa umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa kosa aliloshitakiwa mshitakiwa limetendeka na aliyehusika ni mshitakiwa aliyeko kizimbani”
Akaendelea.
“Ushahidi wa raia mwema muuza machungwa katika eneo la Mabanda ya Papa umethibitisha wazi kuwa mshitakiwa hakusimama mahali ambapo alitakiwa asimame ili kupisha magari na pikipiki zinazotoka upande wake wa kulia na hivyo kusababisha gari lililokuwa linapita, kufunga breki ghafla na kusababisha ajali”
“Ushahidi wa polisi wa usalama wa barabarani umethibitisha kuwa baada ya ajali kutokea mshitakiwa alikimbia na alikuja kukamatwa baada ya wiki mbili”
Mwendesha Mashitaka akaendelea kueleza.
“Kukamatwa kwake kuliwezeshwa na msamaria mwema aliyekuwa akiuza machungwa katika eneo hilo ambaye aliwatajia polisi namba ya pikipiki hiyo pamoja na muhusika mwenyewe”
Baada ya hapo Mwendesha Mashitaka alitaja vifungu vya sheria za usalama barabarani ambavyo alidai nilivikiuka na kuieleza mahakama kuwa nilistahili kupewa adhabu kali ikiwemo kulipia gharama za za shirika la umeme.
Mwendesha Mashitaka huyo alikwenda mbali zaidi akataja adhabu ya kifungo nilichostahili kwa kosa langu ni kwenda jela miaka mitano au kulipa faini siyopungua shilingi milioni kumi pamoja na kulipa ghrama za uharibu niliousababisha.
Hakujua ni jinsi gani alikuwa amenishitua na hakujua ni jinsi gani nilikuwa nikimlaani kwa kutaka kuniharibia maisha yangu. Hapo hapo niliona uso wangu ukifadhaika kama vile tayari nilikuwa nimeshahukumiwa.
Baada ya maelezo marefu ya Mwendesha Mashitaka, hakimu alinitaka nijitetee. Nikaanza kujitetea.
“Mheshimiwa hakimu licha ya maelezo marefu ya Mwendesha Mashitaka ya kutaka nifungwe na kulipa faini, bado ninaisisitizia mahkama yako kuwa si mimi niliyetenda kosa. Mimi nimefananishwa tu kwa bahati mbaya. Mimi sijavunja sheria yoyote ya barabarani”
Nikaendelea kueleza.
“Nilishangaa sana nilipoona nakamatwa na kuambiwa nimesababisha ajali. Jambo hilo si kweli. Mashahidi wote waliokuja kutoa ushahidi dhidi yangu ni waongo wakubwa, wamerubiniwa na polisi ili nipatikane na hatia. Kwa hiyo naiomba mahakama yako inione sina hatia na iniachie huru”
Hakimu aliandika maelezo yangu kisha akapanga tarehe ya kutoa hukumu.
Wakati niko uraiani nikisubiri hukumu yangu, nilikonda kwa mawazo. Ningekuwa ni mtu mwenye uwezo wa kulipa faini na kulipia gharama zilizotakiwa, nisingejali. Lakini nillikuwa masikini niliyekuwa nikitegemea mshahara wa kila mwezi ambao mimi mwenyewe pia haukunitosha.
Nilijiambia kama nitafungwa miaka mitano maisha yangu yatakuwa yameharibika. Nitakapotoka hapo nitakuwa sina kazi, sina bazi. Nitakuwa ninaanza maisha upya nikiwa sina uhakika wa kupata kazi mahali pengine.
Pia sikuwa na uhakika kuwa nitaweza kukaa gerezani kwa miaka mitano. Itakuwa ni kifo. Si ajabu nikarudishwa nikiwa maiti.
Katika kipindi hicho nikuwa naswali na kuomba Mungu. Nilimkumbuka Mungu sana.
Lakini sikuacha kumfikiria yule msichana wa kijini aliyenisababishia lile balaa. Nilikuwa nikijiambia kama si yeye balaa lile lisingenitokea.
Niliwahi kueleza kwamba nilikwenda kwa mganga kuroga ile kesi. Katika kipindi hicho cha kusubiri hukumu nilikwenda tena kwa waganga wasiopungua watatu.
Niliambiwa kulikuwa na mganga mmoja wa kimakonde aliyekuwa akiishi Kijiji cha Kigombe wilaya ya Muheza ambaye alikuwa hodari wa kuzima kesi, nikaenda na kaka yangu.
Baadaye tena nilikwenda kwa mganga mwingine aliyekuwa wilaya ya Mkinga. Alikuwa sharifu aliyekuwa akitumia uganga wa vitabu. Akanifanyia visomo vya kuzima kesi.
Mganga wa tatu alikuwa Pangani. Yeye alikwenda kunifanyia kafara baharini akanitabiria kwamba nitapata misukosuko mingi lakini nitakuja kuwa tajiri.
Siku moja kabla ya hukumu niliota ndoto ya kutisha. Ndoto ile ilikuwa kama inanitabiria kifungo. Niliota mzee mmoja aliyevaa nguo nyeupe akiniambia kuwa uganga niliofanya ulikuwa wa bure.
Kwa pembeni yangu nilimuona yule msichana wa kijini amesimama akinicheka. Alikuwa amebeba mkoba uliokuwa umeja kinyesi ambacho alikuwa akikichota na kunirushia, mpaka mwili wangu wote ukatapakaa kinyesi.
Hapo hapo nikaona nimesimamishwa kwenye kizimba. Hakimu akaniambia amenitia hatiani na kunihukumu kifungo cha miaka saba jela bila faini na kunitaka nililipe shirika la umeme shilingi milioni kumi na tano.
Nikamuona mama yangu ambaye alikuwa hapo mahakamani akiangua kilio.
Nilipozinduka usingizini niliona jasho limenitoka mwili mzima na moyo ulikuwa ukinienda mbio.
Niliwasha taa kisha nikalaani. Saa yangu ilionesha ilkuwa saa kumi alfajiri. Sikulala tena. Mawazo yangu yote yalikuwa kwenye kufungwa. Nilijua kuwa ile ndoto ilkuwa imenibashiria kifungo ambacho ningepambana nacho siku ile.
Asubuhi kulipokucha nilipanga vitu vyangu vizuri kwa kujua kuwa ninakwenda kufungwa. Nilipomaliza nilikwenda kuoga, nikarudi kuvaa.
Nilihakikisha kila kitu nimekiweka sawa ndipo nilipotoka. Nilikwenda nyumbani kwa mama yangu barabara ya tisa ambako nilimkuta kaka yangu akinisubiri.
Baada ya kusalimiana nao, nililetewa chai nikanywa. Kwa sababu ya fadhaa niliyokuwa nayo nilikunywa kikombe kimoja tu na silesi tatu za mkate.
Kaka yangu akaitazama saa yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Inakaribia kuwa saa mbili sasa” akasema.
Na mimi nikatazama saa yangu.
“Twendeni. Muda umekaribia sana” nikawambia.
“Ngoja nikuombee Mungu” Mama akaniambia.
Nilitaka kuwaeleza kuhusu ile ndoto niliyoota lakini nikoana hakukuwa na haja. Kaka yangu angeona niliota kwa sababu ya uoga wa kufungwa, wakati yeye siku zote alikuwa akiniambia niache uoga kwa vile alikuwa akiamini kuwa ningeshinda ile kesi.
Mama yangu akaniombea dua iliyonipa faraja sana. Baada ya dua yake ndefu akatuambia.
“Sasa twendeni”
Tukatoka. Tulipanda teksi iliyotupeleka mahakamani. Tuliingia ndani ya mahakama tukakaa kusubiri hakimu aingie.
Muda ulipowadia hakimu aliingia. Sauti ya koooort ikasikika. Watu wote tukasimama kutoa heshima ya mahakama kisha tukaketi pamoja na hakimu.
Jalada la kesi yangu ndilo lililoitishwa kwanza. Lilipotajwa jina langu nikasimama na kupanda kizimbani.
Hakimu akaniambia kwamba siku ile ndio angesoma hukumu ya kesi yangu. Nikamwambia “Sawa”
Nilikuwa nimeshajitolea kwa lolote litakalotokea, kufungwa au kuachiwa huru.
Hakimu alianza kutaja kesi iliyokuwa inanikabili. Akaeleza kwamba nilikana mashitaka niliyoshitakiwa na hivyo hukumu yake ilitegemea sana ushahidi uliotolewa mahakamani.
Hakimu aliendelea kuuchambua ushidi huo uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashitaka kuanzia shahidi wa kwanza hadi wa mwisho.
Mwisho wa maelezo yake hakimu alisema, ameridhika kwamba ushahidi huo ulikuwa wa kweli na haukuwa na shaka yotote licha ya mimi mshitakiwa kuupinga.
Hakimu alipofika hapo nilishituka nikajiambia ubashiri wa ndoto niliyoota sasa ulikuwa unatimia.
Miguu ilianza kunitetemeka lakini nilijikaza kiume. Nikajiambia wanaofungwa pia ni binaadamu kama mimi.
“Kwa sababu hiyo nimekutia hatiani mshitakiwa katika makosa yote uliyoshitakiwa” hakimu akasema kisha akanitazama.
“Mshitakiwa uliopo mbele yangu ninakuhukumu kifungo cha miaka mitatu au ulipe faini ya shilingi milioni sita. Na pia ninakuamuru ulilipe shirika la umeme shilingi milioni kumi na tano kutokana na hasara uliyolisababishia shirika hilo”
Moyo wangu ulishituka na miguu yangu ikazidi kutetemeka.
“Utatumikia kifungo au utalipa faini pamoja na kulifidia shirika la umeme?’ Hakimu akaniuliza.
Sikuwa hata na la kujibu, ndipo nilipomuona msichana mmoja miongoni mwa watu waliokuwa wakisikiliza hukumu yangu akinyanyuka.
“Mheshimiwa nitamlipia faini mshitakiwa pamoja na gharama aliyotakiwa kulipa” akasema.
Nikamtazama vizuri msichana huyo.
Unadhani alikuwa nani?
Alikuwa Zena. Yule msichana ambaye nilimgundua kuwa ni jini!
“Utamlipia wewe faini ya shilingi milioni sita na shilingi milioni kumi na tano za kulilipa shirika la umeme?’ Hakimu akamuuliza.
“Ndiyo mheshimiwa”
“Unazo hapo?”
“Ndiyo mheshimiwa”
“Haya nenda kalipe”
Msichana huyo aliyekuwa ameweka begani mkoba wa rangi ya samli, alitoka kwenye mabenchi ya kukalia mahakamani akaongozwa na polisi kulekea sehemu ya kulipia pesa.
Wakati akitembea watu wote walikuwa wamegeuza uso wakimtazama. Pengine ni mimi peke yangu niliyejua kuwa hakuwa binaadamu, bali alikuwa jini aliyekuwa akijigeuza binaadamu.
Mama yangu na kaka yangu ambao walikuwepo hapo mahakamani wakiwa wameketi katika safu za mbele pia walikuwa wamepigwa na butwaa wakimtazama yule msichaana bila kumuelewa.
Polisi mwingine alinishusha mimi kizimbani na kunipeleka pale mahali ambapo Zena alitakiwa kunilipia faini na gharama za shirika la umeme.
Kitendo kile cha Zena kilikuwa kimenishitua na kunishangaza sana. Kwanza sikuwa nikijua kwamba alikuwepo pale mahakamani na kama alikuwepo sikujua alijuaje kuwa nilikuwa na kesi na kwamba siku ile ningetakiwa kulipa pesa hizo.
Nikasimamishwa karibu naye. Alikuwa amevaa baibui la kiiran lililonakishiwa mistari ya rangi ya samli. Alikuwa amejitia manukato yaliyokuwa yakisikika. Wakati ameuweka moba wake juu ya meza na kufungua zipu nilimuona kama adui ambaye ghafla amegeuka na kuwa mkombozi wangu.
Siku za nyuma nilikuwa nikijiambia nitakapomuona popote nitamkimbia. Lakini siku ile sikuweza kumkimbia kwani yeye sasa alikuwa kama kimbilio langu.
Baada ya kufungua mkoba wake alitia mkono ndani ya mkoba huo na kutoa mabunda ya noti nyekundu na kuyaweka juu ya meza. Nilihesabu jumla ya mabunda ishirini na moja ambayo aliyatoa.
“Hizo hapo shilingi milioni ishirini na moja. Milioni sita za faini na shilingi milioni kumi na tano za shirika la umeme” akasema.
Pesa hizo zilihesabiwa na kuthibitishwa kuwa zilikuwa ni kiasi kilichotakiwa.
Pamoja na pesa hizo kulipwa, utaratibu wa kuachiwa kwangu ulichukua karibu saa nzima. Wakati natoka katika jengo la mahakama sasa nikiwa huru nilikuwa nimefuatana na Zena. Mama yangu na kaka yangu walikuwa nyuma. Bado walikuwa hawajui yule msichana alikuwa nani.
Tulipotoka nje ya mahakama Zena akaniambia.
“Ningependa nikutane na wewe leo saa kumi na moja jioni katika bustani ya Uhuru Park”
Wakati ule nilijihisi kuwa mdogo kama piritoni, nikamwambia.
“Sawa”
“Timiza ahadi”
“Nitatimiza’
“Sawa. Mimi nakwenda zangu”
Zena akaondoka na kuniacha. Mama na kaka yangu wakafika nilipokuwa nimesimama.
“Yule msichana ni nani?” kaka akaniuliza.
Zena alikuwa ameshakata kona na kutupotea.
“Yule si ndiye msichana aniliyewambia”
“Yupi?”
“Si ndiye yule jini mwenyewe aliyenipeleka kule Mikanjuni siku ile”
Mama na kaka walishituka.
“Kumbe ndiye yule!” Kaka akasema kwa mshangao.
“Sasa mbona amekulipia pesa?’ Mama akaniuliza.
“Sijui mwenyewe”
“Alikuwa anakueleza nini?” aliuliza kaka.
“Ameniambia nikutane naye Bustani ya Uhuru Park leo saa kumi na moja jioni”
Nilipowambia hivyo mama yangu aliguna.
“Mkutane kwa ajili gani?” akaniuliza.
Nikabetua mabega yangu.
“Sijui. Ameniambia hivyo tu”
“Na wewe umemjibu nini?” Kaka akaniuliza.
“Nimemwambia nitakwenda kukutana naye”
“Usiende peke yako, tutakwenda sote. Mimi pia nataka kumuona” Kaka akasema.
“Ni vizuri mwende nyote, asiende peke yake” Mama alisisitiza.
“Sawa. Tutakwenda pamoja” nikawambia.
Baada ya hapo tukaondoka. Tulikwenda kupanda teksi tukarudi nyumbani kwa mama.
Hatua ile ya kuachiwa huru na mahakama ilinifariji sana kwani tayari nilikuwa ninakwenda kufungwa. Yule mwanamke wa kijini ambaye ndiye aliyenitia katika tatizo lililonikabili aliibuka kama mkombozi wangu bila mimi kutarajia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilipata wasiwasi aliponiambia nikutane naye katika bustani ya uhuru. Nikawa najiuliza alikuwa anataka nini tena wakati ile kesi ilikuwa imeshakwisha. Na kama ni uhusiano wetu ulikuwa haupo tena.
Kusema kweli sikupenda tena kuwa karibu na yule msichana. Kitendo cha kumkubalia kukutana naye kilitokana na hofu tu. Nilishindwa kumkatalia. Angeweza kunizushia tatizo jingine.
Nilikaa kwa mama hadi saa kumi na moja jioni. Kaka aliondoka tangu saa tisa akarudi dakika chache kabla ya saa kumi na moja.
“Naona muda umewadia” akaniambia nakuongeza.
“Twenzetu”
“Sawa. Twende”
Tukamuaga mama na kuondoka. Tulipanda tena teksi ikatupeleka Bustani ya Uhuru ambayo ilikuwa karibu na baharini. Kutoka barabara ya tisa hadi mahali hapo ulikuwa mwendo wa karibu kilometa mbili.
Bustani ya Uhuru ilikuwa katika eneo la mijini kabisa. Enzi hizo tulizoea kukuita uzunguni.
Ilikuwa bustani nzuri ya kupendeza yenye eneo la mita kumi hivi za mraba. Mbali ya kuzungushiwa ukuta mfupi ilikuwa na mti ya vivuli na viti vilivyotengezwa kwa saruji.
Mida kama ile ya jioni watu mbalimbali hupenda kufika katika bustani hiyo kupunga upepo au kupumzika.
Tulipofika, tayari watu walikuwa wakionekana wamejilisi katika kila kona. Tulipata kiti kilichokuwa kitupu chini ya mti mmoja tukakaa.
Niliangaza macho yangu kila upande kuona kama yule mwanamke ameshafika lakini sikumuona. Walikuwepo watu wengine tu.
“Naona bado hajafika” Nikamwambia kaka ambaye alitazama saa yake.
“Saa kumi na moja bado” akaniambia.
“Bado dakika ngapi?’
“Bado dakika mbili”
“Basi atafika sasa hivi”
Tukasubiri.
Saa kumi na moja ikafika. Hatukuona mtu. Dakika zikaendelea kwenda. Kila wakati kaka yangu alikuwa akitazama saa yake. Haukupita muda mrefu akaniambia.
“Sasa ni saa kumi na moja na nusu”
Na mimi nikatazama saa yangu. Ni kweli ilikuwa saa kumi na moja na nusu.
Nikaangaza macho yangu kila upande.
“Mbona hatokei?” nikajiuliza lakini kwa sauti iliyosikika.
“Labda ameghairi”
“Yeye alinisisitiza kwamba nisivunje ahadi”
“Basi tuendelee kusubiri, anaweza kutokea”
Tukaendelea kusubiri hadi saa kumi na mbili jioni.
“Sidhani kama atakuja tena” Kaka akaniambia.
“Basi twenzetu”
“Twenzetu”
Tukanyanyuka.
“Ametupotezea muda wetu bure” Kaka akasema.
“Nashukuru pia hivyo ambavyo hakutokea’
Kaka akacheka.
“Kwanini useme hivyo?’
“Yule mwanamke mimi nilishapanga nisikutane naye tena!”
“Lakini ndiye aliyekuokoa”
“Kwani yale matatizo si ameniletea yeye!”
Tulikuwa tumeshatokea barabarani.
“Naona turudi kwa miguu tu” nikamwambia kaka.
Tukarudi kwa miguu.
Tulipofika nyumbani kwa mama, mama akatuuliza.
“Mlikutana naye?”
“Hakuja” nikamjibu.
“Tumekaa mpaka tumechoka” Kaka akaongeza.
“Kwanini asije na alikwambia mkutane hapo saa kumi na moja”
“Labda amebadili mawazo” nikamwambia.
“Ndiyo vizuri”
“Mimi pia nimemwambia kaka ni vizuri kama hakuja, simuhitaji. Namuona kama nduli”
“Ni nduli kweli. Angekuharibia maisha yako” Mama akaniambia.
“Lakini haikuwa vibaya kumsikiliza kujua alitaka kukwambia nini” Kaka akaniambia.
“Basi yameshapita”
Baada ya hapo mimi na kaka tulimuaga mama na kuondoka. Kaka alikwenda kwake na mimi nikarudi nyumbani kwangu Msambweni.
Nilipofika nilioga. Nilipomaliza kuoga nilikaa sebuleni na kujiwazia.
Mpaka muda ule nilikuwa siamini kama niliachiwa na mahakama na nilikuwa huru.
Niliona hivyo kwa sababu kuachiwa kwangu kulikuwa kwa miujiza sana. Kila aliyekuwa akisikiliza ile hukumu alijua kuwa nafungwa kwani nisingeweza kupata zile pesa zilizotakiwa.
Lakini yule mwanamke alishajua kuwa ningetakiwa kulipa pesa zile na pia alijua kuwa nisingekuwa nazo, hivyo akaja nazo na kusubiri hukumu.
Kwa upande mwingine nilikuwa sijajua nia ya yule msichana. Sikujua alikuwa akitaka nini kwangu kwani hatukuwahi kuwa na makubaliano yoyote tuliyokubalina.
Wakati niko katika lindi la mawazo sebuleni kwangu simu yangu ya mezani iliyokuwa pembeni mwa sebule ikaita. Ilinishitua sana. Simu hiyo ilikuwa haipigwi mara kwa mara. Wakati ule hakukuwa na waswahili wengi waliokuwa wakimiliki simu hivyo mawasiliano ya simu yalikuwa madogo sana.
Nikanyoosha mkono wamgu na kukinyakua chombo cha simu cha kusemea.
“Hallow!” nikasema nikiwa simjui aliyenipigia.
“Hallow!” Sauti nyembamba ya mwanamke ikajibu kutoka kwenye simu.
“Amour hapa, nani mwenzangu?”
“Unazungumza na Zena”
Moyo wangu ukashituka.
“Nani…Zena?”
“Ndiyo Zena”
Nilishajua kuwa huenda alikuwa yule msichana wa kijini lakini nilitaka kuthibitisha.
“Zena nani?”
“Ohoo umenisahau leo. Nilikwambia tukutane saa kumi na moja jioni katika bustani ya Uhuru”
“Ndiyo nilifika na nilikusubiri lakini wewe hukutokea”
“Ninajua kwamba ulifika na ulinisubiri lakini mimi sikutokea”
“Kwanini?”
“Umeniudhi”
“Nimekuudhi?”
“Ndiyo”
“Nimekuudhi kwa vipi?”
“Ulikuwa pamoja na nani?”
Nikasita kidogo kabla ya kumjibu.
“Nilikuwa na kaka yangu”
“Kaka yako mimi namjua?”
“Hapana, hunjui”
“Sasa ulikuja na kaka yako kwa ajili ya nini?”
“Alikuwa amenisindikiza tu”
“Lakini tulikubaliana tukutane mimi na wewe. Kwanini ulimleta kaka yako?” Hapa Zena alisema kwa ukali kidogo.
Nikanyamaza.
“Sasa uliyevunja ahadi ni mimi au wewe?” Zena akaniuliza.
Sikumjibu kitu.
“Sema ni wewe. Mimi nilipoona umekuja na mwenzako kinyume na makubaliano yetu sikujitokeza”
“Basi nisamehe”
“Nimeshakusamehe ila kuna kitu nataka kukwambia”
“Fika tena kesho saa nne asubuhi pale Uhuru Park”
“Utakuja?”
“Ndiyo nitakuja”
“Sawa, basi nitafika”
“Kwaheri”
Simu ikakatwa.
Niliuweka mkono wa simu nikawa najiuliza, msichana huyo aliipata wapi namba yangu ya simu. Sikukumbuka kama niliwahi kumtajia namba yangu ya simu. Kitendo kile cha kunipigia kilikuwa kimenishitua na kunishangaza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Sasa nikawa nimetambua sababu ya Zena kutofika mahali ambapo tuliahidiana kukutana. Kumbe ilikuwa ni kwa sababu nilikwenda na kaka wakati yeye hakupenda awepo mtu mwingine.
Nikawa nimeshapata wasiwasi, nikavaa nguo na kutoka. Nilikwenda kwa mama yangu nikamueleza.
Mama akaniambia niende nikamueleze kaka yangu aliyekuwa akiishi eneo la Chuda, nikaenda. Ilikuwa karibu saa tatu usiku.
Kaka aliponiona akashituka.
“Vipi ndugu yangu?” akaniuliza.
“Yule mwanamke amenipigia simu” nikamwambia.
“Kumbe ulimpa namba yako?” akaniuliza.
“Hapana, sikumpa”
“Aliipata wapi?”
Nikabetua mabega yangu.
Sijui. Hata mimi mwenyewe nimeshangaa”
“Amekwambia nini?”
“Ameniambia hakutokea kwa sababu nilikwenda pale nikiwa na wewe”
“Yaani alitaka uwe peke yako?”
“Ndiyo hivyo”
“Kumbe alituona tuko wawili!”
“Bila shaka”
“Sasa amekwambiaje?”
“Ameniambia tukutane tena kesho saa nne”
“Kwani anataka nini?”
“Sijajua”
“Sasa wewe umeamuaje?”
“Nataka ushauru wako”
“Mimi nakushauri nenda”
“Basi nitakwenda”
“Kwa sababu hujui anataka kukwambia nini. Pengine anataka kukwambia kitu cha maana kwako”
“Ni kweli”
“Huwezi jua, anaweza kukupa utajiri”
“Unasema kweli kaka?”
“Wewe nenda kamsikilize, usiogope”
“Sawa. Nitakwenda”
Baada ya kuzungumza na kaka kwa dakika kadhaa nikamuaga.
“Basi kaka mimi narudi nyumbani”
“Acha nikusindikize”
Kaka akanisikindikiza hadi eneo la stendi ya mabasi, tukaachana.
Siku iliyofuata nikajiandaa kwenda kukutana na yule msichana. Nilipotoka nyumbani nilikwenda nyumbani kwa mama. Nikamjulisha kwamba ndio ninakwenda kukutana na yule msichana wa kijini.
“Jana nilipokwambia uende ukakutane na kaka yako ulikwenda?” Mama akaniuliza.
“Nilikwenda nikamjulisha akaniambia niende nikakutane naye”
“Na wewe mwenyewe umeridhika?”
“Sina la kufanya mama, inabidi niende nikamsikilize”
“Basi omba Mungu. Mungu atakusaidia”
“Sawa mama”
Saa tatu na nusu nikaondoka nyumbani kwa mama. Kwa sababu ya kihoro nilichokuwa nacho hata chai sikuwahi kunywa. Kusema kweli sikujisikia kunywa chai.
Nilipofika katika bustani ya Uhuru ilikuwa saa nne kasoro dakika tano. Nikakaa mahali pale pale nilipokaa na kaka jana yake.
SASA ENDELEA
Nikaanza kutupia macho watu waliokuwa wakipita barabarani hasa wasichana nikitazamia ningemuona Zena akiwa mmojawao.
Dakika zikandelea kupita. Zena sikumuona. Mara kwa mara nilikuwa nikitazama saa yangu. Hakukuwa na siku ambayo saa ilinishughulisha kama siku ile. Kila baada ya muda mfupi nilikuwa nilitazama saa.
Mpaka inafika saa nne kasoro dakika moja niliinua uso wangu nikawa ninaangalia barabarani upande ambao nilitarajia kuwa Zena angetokea. Niliangalia kwa shauku yenye hofu kwa kujua kuwa muda wowote ningemuona Zena.
Kutoka saa nne kasoro dakika moja nilianza kuhesabu sekunde kwani dakika hazikuwepo tena.
Nilianza kuhisi baridi ya hofu ikininyemelea mwilini. Sikujua yule msichana atakapotokea atanieleza nini. Ile picha ya kumuona siku ile akiwa na miguu ya kwato na mwili wenye manyoya kama wa shetani ilianza kunijia akilini mwangu. Picha hiyo ndiyo iliyonitisha na kunikumbusha mkasa mzima ulionitokea siku ile.
Ghafla niliona teksi ikisimama kando ya barabara jirani na bustani ya uhuru. Ilikuwa teksi ya rangi nyeupe na sikujua ni kwanini niliikodolea macho.
Mara nikamuona msichana mrembo akishuka. Alikuwa amevaa dera la mikono mirefu lenye ushungi uliofinika kichwa chake na kuteremka hadi usawa wa kiuno chake.
Alikuwa amevaa miwani ya jua iliyoficha uso wake lakini midomo yake iliyokolezwa rangi ya waridi ilitokeza na kuonekana waziwazi.
Mara tu aliposhuka kwenye teksi alianza kutembea kuelekea katika lango la bustani ya uhuru kwa hatua za taratibu.
Zilinichukua sekunde kama tano hivi kumtambua. Alikuwa ni Zena!
Ile akili yangu iliponiambia kuwa ni Zena, moyo wangu ulipiga kwa nguvu mara moja kisha ukatulia. Nikaona waziwazi pumzi zangu zimebadilika. Nilikuwa ninahema kwa nguvu. Nikawa nashindana na mapafu yangu kuyazuia ili nisionekane kuwa ninapumua hivyo.
Zena alishaingia kwenye eneo la bustani, akawa anatembea kuelekea mahali nilipokuwa kwa mwendo ule ule wa taratibu. Alionekana wazi kuwa mtu mwenye ahadi adhimu.
Wakati anazidi kunikaribia, upande mmoja wa akili yangu ulishindwa kuamini kuwa yule msichana alikuwa ni jini. Alikuwa mzuri sana.
“Asalaam alay kum” akanisalimia aliponikaribia kabla ya kuketi kando yangu.
Hapo hapo niliskia harufu ya manukato aliyokuwa amejitia na hewa ya mahali hapo ikawa ni ya mawaridi.
“Wa alayka salaam” nikamuitikia huku nikijaribu kutabasamu ili kuficha fadhaa niliyokuwa nayo usoni.
Alipoona ninatabasamu na yeye akatabasamu.
“Ninaitwa Zena” akaniambia ingawa sikuwa nimemuuliza jina.
Akaongeza. “Habari ya tangu jana?”
“Nzuri. Sijui yako wewe”
“Mimi mzima. Tukikutana kama hivi hatuna budi kumshukuru Mungu”
“Ni kweli”
Msichana akajiweka sawa na kuutoa mkoba wake uliokuwa umezibwa na ushungi wake aliokuwa amejitanda. Akaufungua na kukitoa kile kitabu changu nilichomuazima siku ile.
“Nimekurudishia kitabu chako ulichokuwa umeniazima” akaniambia huku akinipa kitabu hicho.
Wakati nakipokea akaniambia.
“Samahani kwa kukucheleweshea kitabu chako”
“Bila samahani. Nilikuwa nimeshakisahau kutokana na misuko suko”
“Pole”
“Asante”
Msichana akageukia upande wangu. Ilikuwa vyema kuwa alivaa miwani, vinginevyo angenipa wakati mgumu kutazamana naye.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni kwaninini siku ile uliondoka nyumbani bila kuniambia, ukaacha pikipiki yako na viatu vyako?” akaniuliza.
“Siku ile nilitishika sana. Nilikuona katika umbo tofauti kabisa!” nikamwambia.
Zena akacheka. Alipofanya hivyo haiba ya uso wake ilibadilika na kuwa ya kupendeza zaidi.
“Uliniona katika umbo gani?” akaniuliza.
“Mwili wako ulikuwa na manyoya marefu na miguu yako ilikuwa na kwato kama ya punda. Kwa kweli nilipatwa na uoga mkubwa”
“Ndiyo maana siku ile uliponiona kule Mabanda ya Papa ukaongeza mwendo mpaka ikatokea ile ajali?”
“Kumbe unajua. Ni kweli niliongeza mwendo baada ya kukuona wewe”
Msichana akacheka tena.
“Hukupaswa kunikimbia. Iile umbo uliloniona nalo nyumbani siku ile ndilo umbo langu kwa maana mimi si binaadamu bali ni jini”
“Nilishafahamu kuwa wewe si binaadamu. Binaadamu hawezi kuwa na umbo kama lile”
“Nimefurahi kama umenielewa, kwa hiyo usiniogope tena”
“Kukuogopa ni lazima kwa sababu sijakuzoea”
“Taratibu tu utanizoea. Mimi nimekuwa na wewe kwa miaka mingi bila wewe mwenyewe kujua”
“Umekuwa na mimi kwa miaka mingi?”
“Ndiyo. Naweza kusema tangu ukiwa kijana mdogo”
“Ulikuwa uko wapi?”
“Nilikuwa na wewe”
“Sijawahi kukuona”
JAMANI MMEYASIKIA MANENO HAYO?! MWANAMKE WA KIJINI KAMHUSUDU BINAADAMU! MAKUBWA!!!! KWELI DUNIANI KUNA MAMBO! SIJUI MAZUNGUMZO YAO YATAENDELEAJE?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA

0 Comments