“Niletee mavumba yangu na shuka yangu” Mganga akaendelea kumuagiza.
Mwanamke huyo alikwenda pembeni mwa chumba hicho ambako kulikuwa na meza iliyokuwa na vitabu pamoja na vichupa na vikopo kopo. Alichukua kikopo kimoja, akatungua na shuka moja ya rangi nyeupe iliyokuwa imetundikwa kwenye ukuta.
Alikwenda navyo kwa mganga akakiweka kile kikopo mbele yake kisha akamfinika ile shuka pale alipokuwa amekaa.
“Na wewe ukae hapa hapa, usiondoke” Mganga akamwambia mwanamke huyo.
Mwanamke huyo akakaa karibu yetu.
Mganga alikisogeza kile chetezo cha moto karibu yake kisha akakifungua kile kikopo kilichokuwa na mavumba akachota kidogo na kuyatia kwenye ule moto kisha akajifinika shuka vizuri ili ule moshi uliokuwa unafuka uingie ndani ya ile shuka.
Baada ya sekunde chache yule mganga akaanza kusema maneno niliyodhani kuwa yalikuwa ya lugha ya Kijerumani.
Nilisikia maneno kama “Dachi…pontia…n
a mengine ambayo sikuweza kuyakariri.
Wakati huo uso wake alikuwa ameufunika ndani ya shuka. Ghafla akafunua shuka na kuutoa uso wake. Alikisogeza kile chetezo pembeni kisha akatutazama.
“Dachi…jerumani nimekuja hapa” akasema lakini hatukuelewa maana ya maneno yale.
Mke wa mganga akatueleza.
“Anasema yeye ni jini wa Kijerumani anaitwa Dachi, amekuja kuwasikiliza”
“Sawa, tumemuelewa” Mama akamjibu.
“Asalaam aleykum” mganga akaendelea kwa kutupa salamu.
“Wa alaykumu salaam” tukamuitikia.
“Nini shida yenu?”
“Mwanangu anasumbuliwa na jini mwanamke” Mama akamwambia.
“Mwanao yuko wapi?”
“Huyu kijana niliyenaye hapa”
“Oh mwano amepata mchumba wa kijini, anaitwa Zainush”
Mgnga huyo alipotuambia hivyo mimi na mama tukatazamana. Tulitazamana kwa mshangao kwa jinsi alivyoweza kujua lile jina la Zena ambalo hatukuwa tumelitaja.
“Mwanangu hataki mchumba wa kijini, tunataka aondoke asimfuate tena mwanangu” Mama akamwambia.
“Yule jini ni mkorofi, ameshaua watu watatu” Mganga huyo aliendelea kutuambia.
Tukatazamana tena na mama. Mama hakulieleza suala hilo la watu waliouawa, yaani yule mganga wa Mnyanjani na wale vijana wawili walioiba mkoba wa Zena.
Tukawa tunajiuliza amelijuaje tukio hilo la kuuawa kwa yule mganga na wale vijana.
Kama ambaye aliyagundua mawazo yetu, mganga huyo akacheka.
“Huyo jini anakufuata wewe kila wakati, ameshapata wasiwasi. Anajua unataka kumfukuza” akatuambia.
Alinyamaza kimya kisha akaendelea.
“Lakini mimi haniwezi, naweza kumpiga makofi mara moja”
“Sasa utatusaidiaje?” nikamuuliza mganga huyo.
“Mimi naweza kumuita halafu nitamfunga kamba, hataweza kukufuata tena”
“Utamuita lini?” nikamuuliza tena.
“Nitamuita kesho”
“Sasa leo akija kunidhuru usiku?”
“Nitamzuia” Mganga akaniambia kisha akaitenga shuka na kunyanyuka.
“Nisubirini hapa hapa” akatuambia na kutoka.
Tulisubiri kwa karibu nusu saa. Mke wake alituambia kuwa mganga huyo alikuwa amekwenda kuchuma dawa makaburini.
Aliporudi alikuwa ameshika rundo la majani, akampa mke wake.
“Yaroweke kwenye maji” alimwambia.
Mke wake aliyekuwa ameketi na sisi aliinuka na kuyachukuaa yale majani.
“Changanya na huu mvuje” Mganga aliendelea kumwambia mke wake huku akielekea kwenye meza iliyokuwa na chupa na makopokopo. Alichukua kopo mojawapo akachota kiasi cha mvuje uliokuwa umesagwa na kumpa mke wake.
Baada ya hapo mganga alirudi kwenye kigoda chake.
“Nimekutayarishia dawa ambayo utakwenda kuoga na nyingine utajifukiza” akaniambia.
“Sawa. Kwa hiyo nitakwenda kuoga nyumbani?”
“Hapana. Utaoga hapa hapa na utajifukiza hapa hapa”
“Sawa”
Baada ya kama dakika tano hivi mke wa mganga alirudi akiwa amebeba ndoo ya maji ambayo aliitia yale majan.
“Tayari” akasema.
“Sasa nenda kamuwekee chooni” Mgnaga akamwambia.
Mwanamke huyo akaibeba tena ndoo hiyo na kutoka nayo.
Mganga akanitazama.
“Mfuate, utakwenda kuyaoga yale maji yote” akaniambia.
Nikanyanyuka na kumfuata yule mwanamke. Tulitoka uani mwa ile nyumba. Mwanamke huyo aliingia kwenye choo akaiweka ile ndoo kisha akatoka.
“Haya nenda sasa’ akaniambia.
Nikaingia kwenye kile choo. Nilivua nguo nikazitundika kwenye mlango wa choo. Niliona kata iliyokuwa imetiwa kwenye ndoo nyingine niliyoikuta mle chooni, nikaichukua na kujimwagia yale maji. Yalikuwa yakinuka harufu mbaya sana isiyovumilika.
Lakini kwa vile nilikuwa na shida nilivumilia hivyo hivyo. Nilipomaliza nilijifuta futa maji kwa mikono kisha nikavaa nguo zangu na kutoka na ile ndoo ambayo niliiacha pale uani.
Nilienda kule chumbani kwa mganga huku maji yakiwa yametosa shati langu.
“Umeshaoga?” Mganga akaniuliza.
“Nimeoga” nikamjibu.
“Umemaliza maji yote?”
“Nimeyamaliza yote”
“Sasa bado dawa ya kujifukiza” Mganga aliniambia kisha akawageukia mke wake na mama yangu.
“Hebu mpisheni ajifukize dawa” akawambia.
Mama yangu na yule mwanamke wakatoka.
Mganga akanipa shuka.
“Vaa shuka. Vua nguo zako kisha chutama ujifukize dawa”
Nikajifunga ile shuka kiunoni kisha nikavua suruali yangu pamoja na shati. Mganga alinisogezea kile chetezo cha moto. Akakitia aina fulani ya dawa ya unga. Chetezo kikawa kinatoa moshi.
Nilikuwa nimeshachutama. Ile shuka ndio nilijifunika kukinga ule moshi uingie mwilini mwangu. Harufu yake ilifanana na yale maji niliyooga.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati ule moshi ukinipata mwilini. niliisikia sauti ya mganga akisema maneno kwa lugha ambayo sikuweza kuijua huku akilitaja jina la Zainush.
Moshi ulipokwisha, mganga aliniambia nininuke na nivae nguo zangu. Nikainuka na kuvaa nguo.
“Sasa kazi yako imekwisha kwa leo, rudi nyumbani ila kesho asubuhi uje tena” Mganga akaniambia.
“Hii kazi yaa leo ni shilingi ngapi?” nikamuuliza mganga huyo.
“Kwa leo utanipa shilingi elfu ishirini”
“Nikatoa shilingi elfu ishirini na kumpa mganga huyo.
“Sasa mnaweza kwenda zenu”
“Yule jini hataweza kunifuata tena leo?” nikamuuliza.
Mganga akatikisa kichwa.
“Hawezi kukufuata. Hiyo harufu unayonuka hataweza hata kukusogelea”
“Nashukuru sana’
“Ila kumbuka kitu kimoja. Ukifika nyumbani usioge tena. Lala hivyo hivyo”
“Sawa”
Baada ya kumalizana na mganga huyo nilitoka ukumbini. Mama yangu alikuwa amekaa na mke wa mganga, nikamwambia.
“Twenzetu”
“Umeshamaliziwa?” Mama akaniuliza.
“Tayari”
Mama akamuga mwenzake kisha akaingia kwenye kile chumba alichokuwemo mganga akaagana naye kisha akatoka.
Tulitoka nje tukapanda pikipiki na kuondoka.
“Dawa inanuka kweli!” nikamwambia mama.
“Dawa za kufukuza mashetani ndivyo zilivyo, vumilia tu”
Nilipomfikisha mama nyumbani kwake, nikaenda Msambweni nilikokuwa nikiishi.
Licha ya kuwa na hofu sikuona tatizo lolote usiku ule. Nikalala hadi asubuhi.
Wakati naamka, shuka za kitanda na ile niliyojifinika zilikuwa zikinuka ile harufu ya dawa za mganga. Niliziondoa kitandani nikatandika zingine kisha nikaenda kuoga. Licha ya kujisugua kwa sabauni zaidi ya mara moja, ile harufu bado nilikuwa nikiisikia mwilini mwangu.
Nilikwenda mkahawani nikanywa chai kisha nikapanda pikipiki yangu na kuelekea Chuda kwa kaka yangu.
Nilipofika nilimueleza nilivyoshughulikiwa na yule mganga na alivyonieleza kuwa niende tena siku ile.
“Jana usiku yule mwanamke hakukufuata?” akaniuliza.
“Sikumuona lakini nadhani kama nisingekwenda kwa yule mganga wa Amboni, angenifuata. Naamini zile dawa ndizo zilizomzuia”
“Sasa leo utaakwenda na mama au utakwenda peke yako?”
“Nitakwenda kumsikiliza mama, kama atasema twende tutakwenda”
“Hata kama atakwambia uende peke yako wewe nenda tu, ukirudi utakuja kunieleza”
“Sawa kaka”
Nyumbani kwa mama nilimkuta mama akinisubiri. Nilipomuuliza kuhusu safari ya Amboni akaniambia tutakwenda sote. Mama yangu alikuwa na huruma sana. Nikampakia kwenye pikipiki tukaenda Amboni.
Tulipofika tulimkuta mganga akiwa kwenye chumba chake cha uganga akishughulika. Tulisalimiana naye akatuambia tumsubiri nje. Baada ya muda kidogo alitoka nje. Uso wake ulikuwa umefadhaika sana. Akatuambia.
“Jana niliwambia mje lakini usiku nilipolala yule jini wako alinifuata na kuniletea vitisho vikali sana. Aliniambia kuwa kama nitaendelea kukushughulikia kitanikuta kile kilichomkuta mganga wa Mnyanjani. Kwa kweli nilipata hofu sana”
“Lakini jana si ulituambia kuwa huyo jini unaweza hata kumpiga makofi?”
“Baba! Ni kweli nilisema lakini sikujua kama jini mwenyewe ni yule aliyenifuata. Yule jini ni mkali. Alipokuja, majini yangu yalinywea”
Maneno ya mganga huyo yalinifanya nimtazame mama. Mama naye akanitazama kwa mshangao.
Kama ambaye aligundua kuwa maneno yake yalikuwa yamemdhalilisha mwenyewe mganga huyo aliendelea kutuambia.
“Sidhani kama utaweza kuepukana na jini yule. Ameniambia kuwa hakuna atakayeweza kuwatenganisha, atakuwa na wewe mpaka kufa”
“Yaani ameshajihakikishia ushindi?” Mama akamuuliza kwa mshangao.
“Yeye mwenzetu ni jini, sisi ni binaadamu. Anatuona lakini sisi hatumuoni mpaka anapotaka mwenyewe” Mganga akasema.
“Sasa unatushauri nini?”
“Lakini huyu jini hana matatizo kama mnavyomdhania, tena ni jini tajiri na kisha ni mganga, kwanini hutaki kuwa naye?” Mganga akaniuliza.
“Siwezi kuwa na mke jini wakati mimi mwenyewe ni binaadamu. Nitaishi naye vipi?” Nikamuuliza mganga.
“Sasa utafanyaje wakati ameshakuchunuka?”
“Nitajitahidi kuhangaika kwa waganga wengine”
“Ukibahatika kwenda Pemba naamini unaweza kupata waganga ambao wataweza kukusaidia. Wapemba ni hodari sana kwa majini”
“Kama hakuna budi nitafika hata huko Pemba”
“Kama utaweza kwenda naamini utafanikiwa”
Tuliondoka kwa yule mganga tukiwa tumenywea. Mategemeo yangu yote yalififia ghafla. Suala lile sasa lilianza kunipa changamoto kali.
“Maneno ya yule mganga yamenitisha sana” Nilimwambia mama wakati namuendesha.
“Hakuna lisilo na mwisho, jini si Mungu, usitishike mwanangu. Endelea kumuamini Mungu. Jini ni kiumbe kama wewe naye ameumbwa na Mungu. Mungu ndiye wa kumuogopa”
Maneno ya mama yalinipa matumaini kidogo. Nilipomfikisha nyumbani kwake aliendelea kuniambia.
“Makosa yetu ndiyo yanayotuponza. Imani za watu zimekuwa ndogo sana katika dini. Watu wanapenda dunia zaidi. Sasa vile vitu ambavyo vilipaswa kuwa chini yetu vinakuwa juu yetu. Mwanaadamu ndiye aliyetakiwa kutawala dunia hii lakini baada ya watu kupunguza kumcha Mungu, sasa majini yanataka kututawala sisi”
“Leo mama umeniambia maneno ya akili na ya kufikirisha sana” nikamwambia mama.
“Rudi nyumbani na muamini Mungu wako, jini hatakufuata”
“Asante mama”
Nikaondoka na pikipiki yangu kurudi nyumbani nikiwa na imani tele. Nilijiambia kama mimi ndiye niliyepaswa kuwa mtawala wa dunia hii sitakubali jini anitawale wala kunitia hofu.
Ni kweli imani ina nguvu, nilikaa wiki nzima bila kuona kitisho chochote. Nikaona kama vile tatizo langu lilikuwa limekwisha.
Wiki iliyofuata nikiwa kazini kwangu, tuliendelea kufanya biashara hadi saa kumi jioni, yaani siku ile kulitokea biashara ya ajabu. Tulipata wateja wengi kutoka vijijini kwa vile ulikuwa msimu wa kuuza mazao.
Nikajikuta nilikuwa na pesa nyingi kwenye dawati langu. Muda huo sikuweza kuzifikisha pesa hizo benki kwa sababu benki zilikuwa zimeshafungwa.
Nilizihesabu pesa hizo, zilikuwa shilingi milioni kumi. Hizo zilikuwa za mauzo ya jioni tu, za mauzo ya asubuhi na mchana zilishapelekwa benki.
Nikaamua kuziacha pesa hizo kwenye dawati langu kwa vile nilifunga kitasa kwa funguo. Tukafunga duka na kuondoka.
Asubuhi ya siku ya pili yake nilikwenda kazini kama kawaida. Nilipofika kitu cha kwanza nilitaka nizitoe zile pesa ili zipelekwe benki. Nilipofungua dawati sikuona kitu.
Nikashituka na kutumbua macho yangu. Sikutosheka kutazama kwa macho, nilitia mkono wangu na kupapasa. Hakukuwa na kitu. Dawati lilikuwa tupu kama mkono uliorambwa!
“Pesa za watu zimewenda wapi jamani?” nikajiuliza kwa fadhaa.
Meza yangu ilikuwa na madawati matatu. Pesa niliziweka katika dawati la juu. Baada ya kuzikosa pesa katika dawati hilo nilianza kuzitafuta katika madawati ya chini yake japouwa nilikuwa na hakika kuwa pesa hizo niliziweka katika dawati la juu.
Nilikuwa kama niliyerukwa na akili. Licha ya kupekua kwenye madawati yote matatu, pesa sikuziona. Akili yangu ilikuwa haiamini kama pesa hizo hazikuwemo kwa sababu niliziweka mwenyewe na dawati nililifunga kwa funguo.
Nikarudi tena kwenye dawati la juu kutazama tena. Nikaja kwenye dawati la pili na la tatu. Lakini hakukuwa na pesa.
Ule mchezo wangu wa kufungua madawati kuanzia la juu hadi la chini na kisha kurudia tena, uliwashitua wafanyakazi wenzangu wakaanza kuniuliza ninachotafuta.
“Amour mbona umeshughulika sana, unatafuta nini?” Mfanyakazi mmoja akaniuliza.
“Natafuta pesa. Jana tulipoondoka niliacha shilingi milioni kumi katika dawati hili la juu, sasa sizioni!” nikamwambia.
“Zimekwenda wapi?”
“Sijui!”
“Kwani ulipoondoka hukulifunga?”
“Nililifunga na funguo niliondoka nazo, sasa nashangaa pesa sizioni!”
“Haiwezekani! Hebu tazama vizuri”
“Nimetafuta sana, pesa hazimo. Sijui nani amezichukua!”
“Na haiwezeani zichuuliwe na mtu wa sababu funguo uliondoka nazo mwenyewe”
Nikanyamaza kimya huku macho yangu yakitanga tanga kwenye meza.
Wafanyakazi wengine waliposikia mazungumzo yetu wakasogea karibu.
“Umepoteza nini, pesa?” mfanyakazi mmoja akaniuliza.
“Ndio pesa”
“Uliziweka wapi?”
“Nilizizifungia kwenye dawati hili hapa jana jioni tulipotoka kazini, sasa nashangaa pesa sizioni”
“Ulifunga kwa funguo?” Mhasibu aliniuliza.
“Nilifunga kwa funguo na funguo niliondoka nazo”
“Sasa nani atazichukua kama dawati ulilifunga?”
Katika maswali yote niliyokuwa nikiulizwa, swali hilo ndilo lililonikera kwa sababu sikuwa na jibu nalo na lilinifanya nionekane mzushi na mpumbavu.
“Hilo ndilo jambo la ajabu” nilijikuta ninatoa jibu hilo.
Baada ya muda mfupi nikawa nimezungukwa na wafanyakazi wenzangu waliokuwa wakilishangaa tukio hilo.
“Hebu jaribu kukumbuka kama uliziweka sehemu nyingine” Mhasibu akaniambia.
“Sikuweka sehemu nyingine, niliziweka kwenye dawati hili hapa” nilimuonesha lile dawati la kwanza.
“Sasa zitakuwa zimekwenda wapi?”
“Sijui bosi”
“Na ni kwanini hizo pesa hazikupelewa benki tangu jana ?”
“Ni pesa za mauzo ya jioni, benki zilikuwa zimeshafungwa bosi”
“Mara ngapi umeshalaza pesa kwenye droo lako?”
“Mara nyingi tu lakini leo ndio nimekomolewa”
“Sasa umekomolewa na nani? Mhasibu akaniuliza.
“Siwezi kujua”
“Bado sikuelewi Amour, pesa uliziweka mwenyewe na hakuna aliyejua isipokuwa wewe mwenyewe. Sasa utasema umekomolewa, umekomolewa na nani?”
Nikabaki kimya. Sikuwa na jibu
Msibu akanitazama.
“Umehakikisha kuwa hizo pesa hazipo?” akaniuliza.
“Sizioni” nikamjibu kwa sauti iliyonywea
“Sasa njoo ofisini kwangu”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Moyo wangu ukashituka lakini nilijikaza kiume. Nikamfuata mhasibu ofisini kwake. Kwa pembeni mwa macho yangu niiwaona wafanyakazi wenzangu wakinitazama. Kuna niliowaona wakinihurumia na kuna waliokuwa wakiona nilikuwa nimefanya ulaghai wa kuiba pesa za shirika.
Nilipoingia ofisini mwa mhasibu, mhasibu aliniambia.
“Kaa hapa” alinionesha kiti.
Yeye mwenyewe alizunguka nyuma ya meza yake, naye akaketi.
“Nataka nikwambie kitu” akaniambia. Sauti yake na uso wake haukuonesha urafiki hata chembe.
“Ndiyo” nikamuitikia nikiwa sijui anataka kuniambia nini.
“Umekuwa mfanya kazi muaminifu kwa muda mrefu sana lakini hii haitufanyi tusikuchukulie hatua kutokana na wizi huu wa pesa za shirika. Ninachokuomba ni kuwa nakupa siku mbili tu utupatie zile pesa” Alipofika hapo alinikazia macho kisha akaniuliza.
“Sijui umenielewa?”
“Nimekuelewa” Sikuwa na jibu jingine zaidi ya hilo.
“Sasa nenda katuletee zile pesa”
“Si kwamba hizo pesa ninazo, pesa zimeibiwa”
“Sasa nenda katutafutie pesa za watu uzilete”
“Nitakwenda kuzitafuta wapi bosi?”
Nilijua kwamba niliuliza swali la kipumbavu lakini lilitokana na hoja ya kipumbavu.
“Popote utakapojua utazipata, sisi shida yetu ni pesa tu”
Nikageuza uso wangu pembeni kutafakari.
“Nimekupa siku mbili uje na hizo pesa, vinginevyo itabidi suala hilo nilifikishe polisi”
Nilihisi kijasho chembamba kikinitiririka kwenye mfereji wa uti wa mgongo wangu.
“Tumeelewana?” Bosi akaniuliza alipoona nipo kimya.
“Sawa bosi” nikamjibu kisha nikainuka kwenye kiti.
Nilikwenda kwenye mlango. Wakati naufungua mlango huo nikaisikia sauti ya mhasibu akiniambia.
“Kumbuka kwamba nimekupa siku mbili”
Nikageuza uso na kumtazama.
“Nimekuelewa” nikamjibu kisha nikafungua mlango na kutoka.
Wakati natoka, macho ya wafanyakazi wenzangu yaligeuka kwangu. Sikuwapatiliza wala kuwajali. Nilihisi walikuwa miongoni mwa walionikomoa. Mimi nimeshapewa onyo la kusulubiwa, wao wanafurahia milioni kumi za bure.
Nilitoka nje ya duka letu bila kuzungumza na mfanyakazi yeyote. Nilikuwa nimefadhaika kweli. Nilipanda pikipiki yangu nikaiwasha na kuondoka.
Sikujua nilikuwa naenda wapi, nikaona niende kwa mama nikamueleza kuwa nimefikwa na mitihani. Wakati naendesha nilikuwa najiuliza nitazipata wapi shilingi milioni kumi ili nirudishe pesa za watu.
Pale nilipomkubalia bosi, aliponiambia niende nikazitafute pesa hizo nilimkubalia tu ili niweze kuondoka kwani nilijua kuwa sitazipata.
Nilipofika kwa mama yangu nilimueleza mkasa ulionitokea, mama alitaharuki sana.
“Imekuwaje tena mwanangu?” akaniuliza.
“Kwa kweli sielewi kitu mama. Huyo mtu aliyenichezea mchezo huu amenikomoa kweli”
“hilo dawati ulikuta limevunjwa?”
“Halikuvunjwa. Watu wana mbinu nyingi za wizi. Inawezekana kuna ufunguo mwingine uliotumika”
“Kwanini usiwaeleze hivyo wakubwa wako wa kazi?”
“Nani atanisikiliza. Unapotoa malalamiko unatakiwa utoe na ushahidi, ushahidi uko wapi kwamba kuna mfanyakazi mwenzagu amefungua dawati langu kwa ufunguo mwingine na kuiba hizo pesa!”
“Sasa wewe utazipata wapi milioni kumi?”
“Hiki ni kifungo mama!”
“Umekwenda kumueleza kaka yako?”
“Sijakwenda bado”
“Hebu nenda kamueleze usikie atakupa ushauri gani?”
“Sawa. Acha niende nikamsikilize”
Nilipofika nyumbani kwa kaka Chuda, ilikuwa ikikaribia kuwa saa sita mchana.
“Leo hukwenda kazini?” kaka akaniuliza.
“Nimekwenda lakini kumetokea matatizo”
“Matatizo gani?”
“Kuna pesa zimeibiwa kwenye dawati langu”
“Lini?”
“Leo hii”
“Kiasi gani?”
“Shilingi milioni kumi”
Kaka akashituka. Enzi hizo pesa hizo zilikuwa nyingi sana.
“Zimeibiwaje?”
Nikamueleza kaka jinsi wizi huo ulivyotokea.
“Inawezekana huyo jamaa alikuwa na ufunguo mwingine ambao aliutumia kufungua dawati lako akaiba hizo pesa”
“Ndio hivyo lakini sasa dhima imeniangukia mimi”
“Kwa hiyo umeambiwa nini”
Nitoke nikatafute pesa za shirika nizirudishe, nimepewa siku mbii tu”
“Kama hukuzipata itakuwaje?”Kaka akaniuliza.
“Suala hilo litapelekwa polisi”
“Ukisikia balaa ndio hilo, wadhani utazipata wapi milioni kumi?”
“Hiki ni kifungo kinaningoja”
Kaka akatikisa kichwa kusikitika.
“Nakuhurumia sana mdogo wangu sijui nitakusaidiaje?”
“Msaada ni kupata hizo pesa na pesa hazipo”
“Umekwenda kumueleza mama?”
“Nimekwenda, nimemueleza”
“Amesemaje?”
“Hakuwa na usemi, amesikitika tu”
Wakati ninasema hivyo nilimuona kaka amezama katika fikira. Nikajua lile tatizo lilikuwa limeugusa moyo wake.
“Sasa itabidi tusubiri tuone uamuzi wa wakuu wako” Kaka akaniambia baada ya kimya kifupi.
“Uamuzi! Kuna uamuzi gani tena kaka zaidi ya kufunguliwa kesi ya wizi. Kwani si nimeshaambiwa kama pesa hazitapatikana baada ya siku mbili, hili suala linafikishwa polisi!” Nikamwambia kaka.
Kaka alikuwa amejishika kichwa akisikitika.
“Kilichobaki sasa ni kuomba Mungu hizo pesa zipatikane”
Wakati kaka akisema hivyo mimi nilikuwa kimya.
“Mungu amtie imani huyo aliyeziiba azirudishe kabla ya hizo siku mbili” Kaka aliendelea kuniombea.
Hakuna mwizi au jambazi anayerudisha kile alichokiiba lakini kwa vile kaka yangu alikuwa akiniombea ilibidi nimsikilize.
Siku ile nilishinda bila furaha na kusema kweli nilishindwa hata kula chakula. Nilikwenda nyumbani kulala tu.
Siku ya pili yake nilikwenda kazini. Mhasibu aliponiona akaniita ofisini kwake. Nilipokwenda aliniuliza kama nimefanikiwa kupata zile pesa.
“Sijazipata bosi” nikamwambia.
Uso wa mhasibu ukaonesha kuhamaki.
“Unajua kuwa zile ni pesa za shirika?” akaniuliza kwa ukali kidogo.
“Ninajua bosi”
“Na unajua kuwa nilikupa siku mbili urudishe zile pesa?”
“Ninajua”
“Kama unajua hivyo sawa. Kesho uje na hizo pesa vinginevyo sitakuelewa”
Sikuwa na jingine la kumjibu zaidi ya kumuitikia. Nilishajua kuwa nisipokuja na pesa hizo atanifikisha polisi. Na mimi nilikuwa nimeshajitolea kwenda jela.
Siku ile nilishinda kazini hadi muda wa kutoka kazini nikatoka na wenzangu. Tulipokuwa nje baadhi ya wafanyakazi wenzangu waliniuliza kuhusu upotevu wa zile pesa. Kila mtu alionekana kushangaa jinsi pesa hizo zilivyoibiwa.
“Nimepewa siku mbili nizirudishe hizo pesa vinginevyo suala litafikishwa polisi kwa hatua zaidi” nikawambia.
Kila mtu aling’aka na kunihurumia.
“Sasa ni nani aliyefanya mchezo huo. Hapa kazini kweli hakuna mchezo wa kuibiana pesa” Mfanyakazi mmoja akaniambia.
“Hata mimi nashindwa kuelewa”
Baadhi ya wafanyakazi wenzangu walikuwa wamenizunguka wakinisikiliza na kunihoji. Baadaye tulichangukana tukarudi majumbani.
Lakini mimi sikurudi nyumbani. Nilikwenda nyumbani kwa mama. Ukiwa na mama, hata ukiwa mtu mzima utamdekea tu. Pale kwa mama ndipo nilipopaona mahali muafaka wa kupeleka kilio changu ingawa hakuwa na uwezo wowote lakini alikuwa ni mama.
Nikamueleza mama yaliyojiri huko kazini kwangu. Nikamwambia kwamba kesho ndio natakiwa kupeleka hizo pesa vinginevyo ninafikishwa polisi.
“Itabidi hapo kesho uende kazini na kaka yako ili litakalotokea aweze kulijua” Mama akaniambia.
Jioni ile ile nilikwenda kwa kaka nikamueleza na tukakubaliana kwamba nimpitie asuhuhi anisindikize kazini.
Siku ile nilipanga vizuri vitu vya nyumbani nikijua kwamba kesho yake ninakwenda jela. Usiku wake sikupata usingizi kwa mawazo.
Nakumbuka nilipata usingizi majira ya saa kumi alfajiri nikaota ndoto ya kutisha. Niliota nimesimamishwa kizimbani nikihukumiwa kwa kosa la wazi wa fedha za shirika.
Hakimu aliniambia. “Ushahidi uliotolewa hapa mahakamani umeonesha na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba umeiba shilingi milioni kumi fedha za shirika ukiwa mfanyakazi wa shirika hilo. Hivyo mahakama hii imekutia hatiani”
Hakimu akainua uso wake na kunitazama kisha akaniuliza.
“Una lolote la kuiambia mahakama hii kwanini isikupe adhabu kali?”
“Mheshimiwa hakimu ninaiomba mahakama yako tukufu isinipe adhabu kali kwa kuzingatia kuwa fedha zenyewe sikuziiba mimi na kwa kweli sijui zimeibiwa na nani” nikasema.
inaendlea....

0 Comments