Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Mwanamke jini sehemu ya sita (06)

 


Hakimu akaandika maelezo yangu kisha akainua tena uso wake na kuniambia.

“Maelezo yako hayawezi kuizuia mahakama hii isikupe adhabu kali. Ninakuhukumu kifungo cha miaka thelathini jela ili iwe fundisho kwa wengine”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hapo hapo nikaacha mdomo wazi kwa mshangao kama ambaye sikuamini kuwa nilihukumiwa kifungo hicho. Uso wangu ukiwa umenywea nilimtazama mama yangu na kaka yangu waliokuwa wamekaa katika safu za mbele.
Nikamuona mama yangu anaangua kilio akinililia…
Sauti yake ya kizee ndio iliyoniamsha usingizi. Wakati nazinduka moyo ulikuwa ukinienda mbio na mwili wote ulikuwa umenitota jasho. Nilijiinua kitandani nikaketi.
Nikajiuliza, je ndoto ile ndio inanitabiria hatima yangu, kwamba nitahukumiwa kifungo cha miaka thelathini kama jambazi?
Kama ni hivyo, niliendelea kujiambia, nitafia jela. Sitamuona tena mama yangu, sitamuona tena kaka yangu.
Wazo la kufungwa miaka thelathini lilinifanya nitaharuki. Nikajiambia “…sijui nikimbie nisiende tena kazini…”
Lakini nikajiuliza nitakimbilia wapi katika Tanzania hii ambapo mkono wa serikali hautakuwepo?
Kukimbia ni kama kujidanganya na kuonesha kuwa zile pesa niliiba mimi wakati sivyo, nikajiambia, la msingi ni kwenda kazini, litakalotokea na litokee. Kama ni kufungwa au kuachiwa, ingawa tegemeo la kuachiwa sikuwa nalo.
Mpaka inafika saa moja kamili asubuhi nilikuwa nimeshafika nyumbani kwa kaka. Nilitangulia kwenda kwa mama nikaagana naye. Mama aliniombea Mungu kile ‘kikombe’ kiniepuke.
Nilisubiri kaka ajitayarishe hadi saa moja na nusu ndipo tulipoondoka.
Tulifika kazini saa mbili kama na robo hivi nikaingia ndani na kaka. Tulikwenda katika ofisi ya mhasibu. Mhasibu aliponiona tu akaniuliza.
“Umekuja na pesa?”
Nikatikisa kichwa taratibu.
“Sikufanikiwa bosi”
“Mimi ni kaka yake” Kaka yangu akajitambulisha na kumuuliza mhasibu.
“Mheshimiwa kwani hiwezekani kumkata katika mshahara wake wa kila mwezi hadi hizo pesa zikaisha?”
Mhasibu akakasirika.
“Nyinyi mnaleta utani na kazi. Huu ni wizi, huyu hakukopa pesa hapa hadi tumkate kila mwezi. Shilingi milioni kumi tutamkata kwa miaka mingapi wakati pesa za shirika zinahitajika? Nimeshamwambia kama hakuja na pesa leo atakwenda kujieleza polisi” Mhasibu alifoka na kuinuka kwenye kiti, akaniambia.
“Twende!”
Tukatoka mle ofisini na akawaambia wafanyakazi wengine kuwa tunakwenda kituo cha polisi. Tulikuwa tuna magari mawili ya shirika yenye madereva wake. Tukapanda kwenye gari mojawapo. Kaka yangu tulimuacha pale pale.
Wakati napelekwa polisi na nikijua kuwa ninakwenda kufungwa nilimlaani sana yule aliyeiba zile pesa. Nilipata uchungu nilipowaza kwamba mimi ninakwenda kufungwa, yeye yuko ofisini akiwa ameficha shilingi milioni kumi nyumbani kwake.
Tulikwenda kituo cha polisi cha Chumbageni. Tulipoingia katika kituo hicho mhasibu akatoa maelezo yote kuhusiana na wizi huo.

Baada ya kumaliza kutoa maelezo yake na mimi nikatakiwa nijieleze.
Nikaeleze hali iliyotokea ambapo fedha hizo zilichukuliwa ndani ya ndroo yangu wakati ndroo hiyo niliifunga kwa funguo.
Baada ya maelezo yangu nikaanza kukabiliwa na maswali ya polisi.
“Baada ya kufungia hizo pesa kwenye droo yako, asubuhi ulipokwenda kazini kwako ulikuta droo imevunjwa?”
“Ndroo haikuvunjwa”
“Untaka utuambie huyo aliyeziiba pesa hizo alizichukuaje bila kuvunja droo?”
“Pengine alikuwa na ufunguo mwingine”
“Funguo za droo yako ziko ngapi?”
“Ni mbili na zote ninazo mimi”
“Unaona sasa unajiingiza mwenyewe, huo ufunguo wa tatu alioutumia huyo mtu umetokea wapi wakati funguo ni mbili na unazo mwenyewe?”
“Unaweza kuwa ufunguo wa kuchongesha. Kuna mafundi wa kuchonga funguo”
“Tunajua kuwa wapo lakini hata wao ni mpaka uwapelekee ufunguo wa sampuli ndio wanaweza kukuchongea”
“Wezi wana mbinu nyingi. Kama mtu alishapanga kufanya uwizi anaweza kuvizia hizi funguo ninapoziacha juu ya meza yangu wakati sipo, akaukandamiza ufunguo mmoja kwenye sabuni ili kupata meno yake halafu sabuni ile anaipeleka kwa fundi. Fundi anaweza kuchonga ufunguo kama ule”
“Unaweza kuzungumza mengi lakini hayana ushahidi. Hebu twendeni tukaione hiyo droo yako”
Huo ndio ukawa mwisho wa maswali.
Tulitoka na polisi. Mimi nilipakiwa kwenye gari la polisi, mhasibu akaondoka na gari la shirika.
Wakati tunaondoka ndio kaka yangu alikuwa anafika pale kituoni. Akatuona tunaondoka. Siku ile nilimsumbua sana kaka kwa sababu alikuwa akitembea kwa miguu.
Tulipofika kazini kwetu tuliingia ndani, mhasibu akawapeleka polisi kwenye meza yangu.
“Pesa ziliibiwa kwenye meza hii” Mhasibu aliwambia polisi.
“Hebu toa hizo funguo tuzione” Polisi mmoja akaniambia.
Nikazitoa funguo zangu kutoka mfukoni na kuwaonesha
Polisi walizitazama kisha polisi mmoja akaniambia nifungue ile droo. Nikaifungua.
Sote tuliokuwa tunashuhudia, mimi mhasibu na wale polisi pamoja na baadhi ya wafanyakazi, tuling'aka baada ya kuziona zile pesa zilizokuwa zimetoweka zikiwa ndani ya droo.
“Na hizo ni pesa zipi?” Polisi mmoja akaniuliza kwa mshangao.
“Sijui, ndio naziona sasa. Zilikuwa hazimo” nikamjibu.
“Hapo mwanzzo mlihakikisha kwa makini kuwa hizo pesa hazikuwemo?”
“Mimi nilihakikisha na mhasibu pia alihakikisha”
“Hebu zitoe”
“Nikazitoa na kuziweka juu ya meza
“Ni kiasi gani?” Mhasibu akaniuliza
Nikazihesabu na kuona zilikuwa shilingi milioni kumi.
“Sasa nani amezitia hizo pesa?” Mhasibu akauliza kwa mshangao.
Hakukuwa na jibu
“Asubuhi uliangalia kwenye hii droo?” akaniuliza tena
“Sikuangalia”
Mhasibu alipowauliza wafanya kazi wenzangu kuhusu zile pesa hakukuwa na yeyote aliyeeleza kuwa alijua chochote kuhusu pesa hizo.
“Mimi naamini kuwa hizi pesa zimerudishwa kwa sababu mimi mwenyewe niliangalia kwenye hii droo juzi, sikukuta kitu” Mhasibu akatuambia.
“Hapa pana mchezo umepita, mimi nimechezewa na wenzangu” nikasema kwa hasira. Sasa nilikuwa na nguvu baada ya zile pesa kuonekana.
“Sasa ni nani aliyefanya mchezo huu? Tunataka tumjue” Mhasibu akauliza.
“Huu ni wizi ulikuwa umefanyika. Huyo aliyeiba alipoona suala hili limefika polisi ndio aliamua kuzirudisha pesa hizi” Polisi mmoja akasema.
“Tunashukuru kwa vile amezirudisha lakini tunaomba mchezo huu usirudiwe tena” Mhasibu akaonya
“Basi sisi tunakwenda zetu” polisi wakatuambia.
“Mimi naona mwende kwa sababu tatizo lilikuwa ni kwenye hizi pesa ambazo zimeshaonekana” Mhasibu akawambia polisi
Polisi hao wakatuaga na kuondoka.
Mhasibu akachukua zile pesa na kuniambia nimfuate ofisini kwake.
Tulipokuwa ofisini aliniambia.
“Usirudie tena kuacha pesa kwenye droo, sasa hivi sina imani tena na wafanyakazi wa shirika hili”
“Kutokana na msukosuko huu ulionipata, sitarajii kulaza pesa tena kwenye droo yangu”
“Shukuru kwamba hizi pesa zimepatikana, vinginevyo ungelala ndani leo”
“Ni kweli. Hilo nilikwishalijua”
“Kuwa makini sana na wenzako”
“Nitakuwa makini”
Mhasibu akawa anahesabu zile pesa. Alipohakikisha kuwa zilikuwa shilingi milioni kumi taslim nilimuomba anipe mapumziko ya siku moja ili niende nikatulize presha yangu nyumbani.
Mhasibu akaniruhusu, nikaondoka. Wakati natoka mlangoni nikakutana na kaka akitokea kituo cha polisi. Alikuwa amechoka kwa mwendo.
“Imekuwaje?” akaniuliza huku akinitazama kwa uso wa sintofaham.
“Twenzetu” nikamwambia
Akanifuata. Tukashuka baraza.
“Tunakwenda wapi?” akaniuliza akionesha kuwa na wasiwasi
“Nyumbani”
Nikaona uso wake unachanua tabasamu.
“Kwani imekuwaje?”
“Zile pesa zimeonekana”
Kaka akashituka.
“Zimeonekana wapi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwenye droo”
“Droo ya nani?”
“Droo yangu”
“Zimeonekana kivipi?”
“Ni tukio la ajabu sana” nikamwambia kisha nikamueleza jinsi tulivyozikuta pesa hizo kwenye droo yangu.
“Una maana huyo aliyeiba ameamua kuzirudisha?”
“Itakuwa ndio hivyo”
“Kwa hiyo zile pesa alikuwa amezificha sehemu nyingine, alipoona unapelekwa polisi akaamua kuzirudisha”
“Bila shaka. Lakini sasa nimepata fundisho sitaacha pesa tena kwenye droo yangu kwa maana wanataka kunitoa kafara”
“Ni tukio ambalo sikulitarajia”
“Naona dua za mama zinafanya kazi. Mama aliniombea sana”
“Wakati tunavuka barabara tukapishana na msichana mmoja ambaye naye alikuwa anavuka kutoka upande ule tuliokuwa tunakwenda sisi. Alinitupia jicho mara moja ili kujua kama nimemuona.
Nukta ile ile nikamtambua.
Alikuwa Zena!

Niliendelea kuvuka barabara huku uso wangu nimeugeuza nyuma nikimtazama yule msichana.
Baada ya yeye kunitupia macho mara moja tu, aliugeuza mbele uso wake akaendelea na safari yake. Mimi ndiye niliyekuwa nikiendelea kumtazama.
Kaka yangu alikuwa akinisemesha bila kujua kwamba akili yangu ilikuwa imeshughulishwa na kitu kingine.
Tulipomaliza kuvuka barabara nilimuona Zena akikata kona kwenye jengo lililokuwa na ofisi yetu na kupotea
Hapo ndipo nilipomshitua kaka.
“Nimemuona zena!” nikamwambia.
“Zena….Zena yupi?” akaniuliza.
“Yule msichana wa kijini”
Kaka akageuka kwa hamaki.
“Yuko wapi?”
“Wakati sisi tunavuka barabara na yeye alikuwa anavuka kutoka huku kwenda kule upande wa pili. Tulipishana katikati ya barabara. Nimemuona na yeye ameniona lakini hakunisemesha kitu”
Kaka alikuwa akigeuza uso huku na huku kumtafuta.
“Yuko wapi sasa?”
“Ameshakata kona kwenye hili jengo, hebu njoo tumuangalie”
Tukasogea kwenye ile barabara aliyoelekea Zena na kumchungulia.
Hatukumuona tena.
“Ameshapotea”
“Ungenishitua pale pale ulipomuona” Kaka akaniambia
“Sijui anatoka wapi na anakwenda wapi?”
“Labda ana safari zake mwenyewe”
“Unajua tangu nilipokwenda kwa mganga wa Amboni sjakutana naye hadi hii leo!”
“Lakini yule mganga si alisema asingeweza kumuondoa”
“Alituambia hivyo lakini mama alinipa moyo. Niliamini Mungu”
Baada ya kutomuona yule msichana tukawa tunatembea kurudi nyumbani.
“Sasa ni kwanini unarudi nyumbani?” Kaka akaniuliza.
“Nimeomba mapumziko ya siku moja, unajua ule msukosuko ulikuwa mkubwa”
“Ni kweli inabidi upumzike”
Tulitangulia kwenda kwa mama. Aliponiona nikiwa na uso wa tabasamu alishangaa.
“Imekuwaje wanangu?” akatuuliza.
“Kesi imekwisha mama, dua zako zimesaidia” nikamwambia huku nikiendelea kutabasamu
“Imekwisha kivipi?”
“Zile pesa zimeonekana” Kaka ndiye aliyejibu.
“Zimeonekana!” mama akauliza kwa mshangao.
“Kuna mchezo walinichezea pale kazini” nikamwambia mama.
“Hebu nielezeni vizuri Nataka kujua hizo pesa zimeonekana wapi?”
Nikamueleza tukio lilivyotokea.
“Wenzako unaofanya kazi nao si wazuri” mama akaniambia na kuongeza.
“Jihadhari nao”
“Nimemwambia hivyo hivyo, kesho na kesho kutwa wanaweza kukufanyia tena” Kaka akasema.
“Nimepata fundisho. Sitaacha tena pesa kwenye droo, hata iweje”
“Usiache mwanangu, utajitafutia matatizo ya bure”
Tuliongea mengi na kaka yangu pamoja na mama yangu. Baadaye mimi na kaka tukaondoka kwa mama. Nilimpeleka kaka Chuda kisha nikarudi nyumbani kwangu.
Nilipofika nilipanda kitandani nikajilaza. Wakati nawaza hili na hili usingizi ukanipitia nikalala. Wakati niko usingizini nikaota ilikuwa ni siku ile niliyoweka pesa kwenye droo yangu. Usiku wake Zena akafika kwenye mlango wa duka letu.
Alisimama mbele ya mlango wa duka hilo, milango ukafunguka yenyewe. Akaingia ndani.
Alikwenda hadi ilipokuwa meza yangu akavuta ndroo ambayo ilifunguka. Akachukua zile pesa nilizokuwa nimeziweka akazitia kwenye pochi yake. Wakati akifanya hivyo nilimsikia akisema. “Akijifanya anajua vile na mimi najua hivi, atakoma!”
Alipozitia zile pesa kwenye mkoba wake akatoka. Alipotoka ile milango ya duka ikajifunga yenyewe.
Wakati ule nahangaika kutafuta zile pesa Zena alikuwa yuko mle ofisini lakini alikuwa haonekani. Mpaka siku ile ambayo nilipelekwa polisi alikuwa amekwenda tena usiku kwenye duka letu akazirudisha zile pesa alizokuwa amezichukua kwenye droo yangu kisha akafunga ndroo na kutoka.
Vile nilivyokuwa napelekwa polisi Zena alikuwa ameketi kando yangu kwenye gari lakini tulikuwa hatumuoni. Wakati ule nahojiwa na polisi na yeye alikuwa akisikiliza.
Niliporupi ofisini na polisi Zena alikuwa yuko sambamba na mimi hadi zile pesa zipoonekana.
Sasa wakati ule navuka barabara nikiwa na kaka alijipitisha kusudi ili nimuone kisha akapotea.
Nikazinduka usingizini. Wakati nazinduka niliisikia sauti ya Zena ikiniambia.
“Hilo ni onyo!”
Nikadhani kwamba zena alikuwa mule chumbani. Nilipofumbua macho nikainuka na kuketi, nikaanza kutazama huku na huku kwa hofu kwamba ningemuona Zena mle chumbani. Lakini sikumuona.
Nikashuka kitandani na kutoka sebuleni ambako nilikaa kwenye kochi na kuifikiria ile ndoto.
Hapo ndipo nilipoanza kufahamu kuwa zile pesa zilikuwa zimechukuliwa na Zena ili kunikomoa. Nikajiambia kama asingezirudisha ndio ningekiona cha moto.
“Huyu msichana ataendelea kuniamndama hadi lini?” nikajiuliza.
Nilihisi kwamba kama sitachukua hatua thabiti za kuhakikisha kwamba ninaepukana naye, mwisho wake anaweza kunitia katika matatizo makubwa.
Baada ya kufikiri sana nilitoa pikipiki yangu nikaenda kumueleza mama kuhusu ile ndoto. Mama naye alistaajabu.
“Kumbe bado anakufuatilia!” akaniambia
“Huyu jini atakuja kunitia kwenye matatizo makubwa hapo baadaye” nikamwambia mama.
“Sasa fanya mpango wa kwenda huko Pemba”
“Inabidi nipate mwenyeji au mtu wa kufuatana naye ndio nitaweza kufika”

“Ulizia kwa marafiki zako unaweza kupata mtu anayekwenda. Hapa Tanga watu wa Pemba wako wengi” Mama akaniambia.
“Nitaanza kuuliza uliza kwa watu. Nikipata mwenyeji au mtu anayekwenda huko itabidi niende”
Baadaya kuzungumza na mama nilikwenda kwa kaka, naye nikamueleza kuhusu ile ndoto.
“Mimi naamini majini wana matatizo sana na huyo jini hawezi kukuachia kirahisi lakini kwa vile humuhitaji nitakusaidia kukuulizia waganga kwa wenyeji wa Pemba” Kaka akaniambia.
“Na mimi mwenyewe pia nitakuwa naulizia ulizia kwa jamaa”
Ikapita wiki moja. Siku moja ya jumapili kaka yangu akaja nyumbani. Hakuwa na kawaida ya kufika kwangu, hivyo nilipomuona nilishituka.
Akaniambia kulikuwa na mganga aliyetoka Pemba amefikia katika gesti moja pale Chuda. Katika matangazo yake ameeleza pia kuwa anafukuza majini wabaya.
“Nataka twende umueleze matatizo yako anaweza kukusaidia” Kaka akaniambia.
Nilipopata habari zile nilimwambia kaka anisubiri. Baada ya dakika chache tukawa njiani tukielekea Chuda. Nilikuwa nimempakia nyuma ya pikipiki yangu.
Tulipofika Chuda alinipeleka katika gesti alikofikia huyo mganga aliyeniambia. Ilikuwa mtaa wa pili na ule aliokuwa akiishi yeye.
Wale watu niliowakuta hapo nje wakisubiri zamu ya kuingia kwa mganga huyo walinipa matumaini kwamba huyo mganga alikuwa mganga kweli.
Alikuwa ameweka tangazo lake mbele ya gesti lililoandikwa matatizo aliyokuwa akiyashughulikia likiwemo tatizo la majini.
“Ninafukuza majini mabaya katika mwili au nyumba. Pia ninatuliza wale majini wa kichwa wanoleta maradhi na matatizo mengine” Ilisema sehemu ya tangazo hilo.
Mwisho wa tangazo lake aliandika.
“Njoo ujaribu kwani wengi wamefanikiwa. Nitakuwa Tanga kwa siku tatu”
Kutokana na wale watu niliowakuta kuwa wengi nilitaka kumwambia kaka turudi baadaye, watu watakuwa wamepungua lakini nilivyoona pameandikwa kuwa mganga atakuwa Tanga kwa siku tatu nikaamua nisubri hapo hapo.
Siku tatu ni chache sana. Kama ningemkosa siku ile na pengine siku inayofuata, uwezekano wa kumpata tena ungekuwa mdogo sana. Nilijiambia.
Watu tuliowakuta walifikia arobaini. Nilimwambia kaka kama hatakuwa na muda wa kusubiri hapo aende zake.
“Niache niendelee kusubiri hata kama itafika jioni” nilimwambia.
“Sawa, basi wewe subiri ikifika zamu yako utaingia na utamueleza tatizo lako. Ukitoka hapa utakuja nyumbani kuniambia”
Tulipokubaliana na kaka aliondoka akaniacha pale. Mpaka inafika saa nane mchana walikuwa wamebaki watu kumi nikiwemo mimi. Nikaendelea kusubiri hadi saa kumi jioni ndio ikafika zamu yangu.
Nikaingia.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Chumba cha mganga kilikuwa cha kwanza cha mkono wa kushoto. Niliingia katika chumba hicho nikamkuta mganga aliyekuwa amekaa chini kwenye mswala. Kando yake alikuwa amechoma udi wa kijiti uliokuwa unafuka moshi.
Mbele yake kulikuwa na vitabu kadhaa vya kiarabu pamoja na chupa za dawa za kiasili.
Alikuwa amevaa kofia ya darize aliyoiweka katika muundo wa jahazi. Pia alikuwa amevaa shati jeupe na shuka nyeupe. Hakuwa amevaa suruali.
“Karibu” akaniambia alipoona nimesita baada ya kuingia humo chumbani.
“Asante” nikamjibu.
“Kaa kwenye kiti”
Kulikuwa na kiti kilichokuwa kando ya ukuta kushotoni kwake. Nikaenda kuketi.
“Niambie shida yako” akaniambia.
Nikamueleza matatizo yangu mwanzo hadi mwisho.
“Umepata bahati sana. Kule kwetu ukiwa na jini kama huyo tayari unajihesabu kuwa ni tajiri” Mganga akaniambia baada ya kunisikiliza.
“Huko kwenu kuna watu waliooa majini”
“Enhe! Wapo”
“Mimi simuhitaji huyu jini”
“kama wewe umuhitaji ndipo anapokutia kwenye matatizo”
“Ndio nimekuja kwako unisaidie”
“Unataka nikusaidieje?”
“Umuondoe”
“Una uhakika kuwa umuhitaji kabisa, usije ukajuta baadaye”
“Hapana, siwezi kujuta”
“Kwangu mimi si kazi kubwa kama utanipatia vitu ninavyotaka”
“Unataka vitu gani?”
“Ninahitaji kucha zako na kucha za maiti aliyezikwa. Unaweza kuzipata kucha za maiti?”
“Mh! Itakuwa ngumu!”
“Bila kupata kucha za maiti kazi itakuwa ngumu. Nenda kanitafutie kucha za maiti. Ukizipata niletee nitamuondoa huyo jini siku hiyo hiyo. Mimi nikalipo (nitakuwepo) hadi kesho kutwa. Ukiniletea kesho itakuwa bora”
“Bila hizo kucha haitawekana?” nikamuuliza”
Mganga akatikisa kichwa.
“Itakuwa vigumu”
Nikawaza kidogo kisha nikamwambia.
“Basi acha niende nikafikirie nitakavyoweza kuzipata hizo kucha halafu nitakuja hapo kesho”
“Sikiliza. Kucha zenyewe ni lazima ziwe za maiti aliyezikwa si za maiti ambaye hajazikwa”
“Sasa maiti ambaye amezikwa nitampata wapi?”
“Kaburini”
“Yaani nikafukue kaburi?’
“Ndio”
“Si nitaonekana na watu”
“Huendi mchana, unakwenda usiku”
“Mh!” nikaguna nilipofikiria kwenda usiku makaburini na kufukua kaburi.
“kama hutaweza basi, tutakuwa tumeshindwa”
“Nitakupa jibu hapo kesho kama nitaweza au la”
“Kumbuka kwamba nitakuwa hapa Tanga kwa siku tatu. Nikitoka hapa ninakwenda Arusha”
“Nimekuelewa, acha niende. Nitakuja tena kesho”
Nikaagana na yule mganga na kutoka, Nilipanda pikipiki yangu nikaenda nyumani kwa kaka. Kaka mwenyewe sikumkuta, mke wake aliniambia kaka aliondoka tangu saa tisa na hakumwambia anakwenda wapi.
Nikaona niende kwa mama. Nilipofika nilimueleza kwamba kaka alinipeleka kwa mganga aliyetoka Pemba na mganga akanieleza kwamba nimpelekee kucha za maiti.
“Kucha za maiti utazipata wapi?” mama akaniuliza kwa mshangao.
“Tena anataka maiti aliyekwishazikwa”
“Sasa utampataje huyo maiti aliyezikwa ukate kucha zake?”
“Sijui”
“Mh! Hayo ni makubwa”
“Maana yake niende nikafukue kaburi”
“Kaburi gani utakalokwenda kulifukua?”
“Kaburi lolote tu”
“Mh! Si utaonekana ni mchawi!”
“Labda niende usiku”

MAKUBWA! MAMBO SASA NI YA KUFUKUA ,MAKABURI! MMH! KAZI IPO JAMANI!

ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments