“Yaani nikafukue kaburi?’
“Ndio”
“Si nitaonekana na watu”
“Huendi mchana, unakwenda usiku”
“Mh!” nikaguna nilipofikiria kwenda usiku makaburini na kufukua kaburi.
“kama hutaweza basi, tutakuwa tumeshindwa”
“Nitakupa jibu hapo kesho kama nitaweza au la”
“Kumbuka kwamba nitakuwa hapa Tanga kwa siku tatu. Nikitoka hapa ninakwenda Arusha”
“Nimekuelewa, acha niende. Nitakuja tena kesho”
Nikaagana na yule mganga na kutoka, Nilipanda pikipiki yangu nikaenda nyumani kwa kaka. Kaka mwenyewe sikumkuta, mke wake aliniambia kaka aliondoka tangu saa tisa na hakumwambia anakwenda wapi.
Nikaona niende kwa mama. Nilipofika nilimueleza kwamba kaka alinipeleka kwa mganga aliyetoka Pemba na mganga akanieleza kwamba nimpelekee kucha za maiti.
“Kucha za maiti utazipata wapi?” mama akaniuliza kwa mshangao.
“Tena anataka maiti aliyekwishazikwa”
“Sasa utampataje huyo maiti aliyezikwa ukate kucha zake?”
“Sijui”
“Mh! Hayo ni makubwa”
“Maana yake niende nikafukue kaburi”
“Kaburi gani utakalokwenda kulifukua?”
“Kaburi lolote tu”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mh! Si utaonekana ni mchawi!”
“Labda niende usiku”
SASA ENDELEA
“Utaweza kufukua kaburi mpaka uipate maiti kisha uikate kucha?” Mama aliniuliza kwa mshangao.
“Nitajaribu, nikishindwa nitaacha”
“Mh!”
“Sasa nitafanyaje mama?”
“Najua kuwa huna la kufanya”
“Basi ngoja nijaribu”
Nilipoondoka kwa mama nikaanza zoezi la kuzungukia makaburi niliyokuwa nayafahamu. Pale jirani na nyumba niliyokuwa nikiishi paliwa na makaburi lakini yalikuwa karibu na makazi ya watu, ningeweza kuonekana.
Nilikwenda katika eneo la Usagara ambako pia kulikuwa na makaburi. Nikaangalia angalia kisha niliondoka tena nikaenda Gofu. Kulikuwa na makaburi yaliyokuwa kando ya barabara. Mahali hapo ndipo paliponiridhisha.
Laiti ningejua ni balaa gani ambalo ningekutana nalo usiku kwenye makaburi hayo, nisingekwenda na mpango huo ningeuacha kabisa!
Baada ya kupata uamuzi kuwa niende katika makaburi yale wakati wa usiku, nilikwenda katika duka moja la vifaa vya ujenzi nikanunua shepe, viatu vya mvua na mipira ya kuvaa mikononi. Nikavifunga nyuma ya pikipiki yangu kisha nikarudi nyumbani kwangu.
Nilikuwa nimepanga nitoke saa nane usiku ambapo hakutakuwa na watu mitaani na hivyo nisingeweza kuonekana na mtu.
Wakati nimekaa sebuleni nikiwaza nikasikia mlango wa mbele ukigongwa.
Nilisubiri, ulipogongwa tena ndipo nilipoinuka na kwenda kunako mlango huo.
“Nani?” nikauliza.
“Ni mimi Marijani”Sauti ya kaka yangu ikajibu kutoka nje.
Nikafungua mlango.
“Karibu kaka” nikamkaribisha ndani huku nikimpisha kwenye mlango.
Kaka aliingia ndani, nikafunga mlango.
“Umenishitua kidogo” nikamwambia.
“Kwanini?”
“Nilivyokuona umekuja kwangu huu usiku moyo wangu umeshituka”
“Nimekuja na wazo”
“Kaa kwenye sofa” nikamwambia kwa shauku ya kutaka kulisikia wazo alilokuwa amekuja nalo.
“Sitakaa. Nimekuja mara moja tu. Nataka niwahi kurudi”
“Pikipiki ipo nitakurudisha kaka”
“Usijali Amour tunaweza kuzungumza tukiwa tumesimama, sisi bado ni vijana. Tusiogope kusimama”
“Sawa kaka, nieleze hilo wazo ulilokuja nalo”
“Kwanza nilipata salamu kutoka kwa mke wangu kwamba ulikuja nyumbani ulipotoka kwa yule mganga”
“Ndio nilikuja lakini nikaambiwa na shemeji kuwa ulitoka”
“Ni kweli nilitoka, niliporudi ndio nilipata hizo salamu. Nikaenda kumuuliza mama kama ulifika kwake akaniambia ulifika na akanieleza ulivyoelezwa na yule mganga”
“Umeona kuwa mganga wako amenipa mtihani mkubwa”
“Ni mtihani mkubwa. Mama ameniambia ametaka umpelekee kucha za maiti”
“Tena maiti aliyezikwa, yaani niende nikafukue kaburi”
“Sasa mimi nilikuwa na wazo”
“Ndio”
“Kwanini usiwatumie vijana?’
“Kuwatumia kivipi?”
“Yaani unamtafuta kijana wa maskani unampa pesa kisha unamtuma hiyo kazi na unamuahidi kuwa akikuletea hizo kucha za maiti utampa pesa nyingine”
“Ni wazo zuri, sikuwahi kulifikiria wazo hilo”
“Yaani badala ya wewe kupata kazi ya kufukua kaburi, kazi hiyo unampa yeye. Hawa vijana ukiwapa elfu ishirini tu ya kunywea gongo na bangi wanaweza kukupatia hizo kucha”
“Ni kweli. Nitawatafuta huu usiku”
“Tena makaburi yako pale karibu tu. Kuna vijana wanaovutavuta bangi pale”
“Nashukuru kaka kwa wazo lako, umenisaidia sana”
Baada ya kunipa wazo lake hilo nilimrudisha kaka nyumbani kwake kwa pikipiki yangu.
Wakati narudi nyumbani nikawa nalitafakari lile wazo alilonipa kuona kama lilikuwa la busara.
Kwa upande mmoja wa akili yangu niliona lilikuwa wazo la busara kwa sababu lingenigharimu pesa lakini lingenirahisishia kazi. Badala ya mimi kwenda kufukua kaburi, ningempa pesa mtu mwinginne akanifanyie kazi hiyo.
Wahuni walikuwa wengi tu katika mtaa niliokuwa nikiishi, ningeweza kumtuma mmojawapo na akanifanyia kazi hiyo bila wasiwasi.
Lakini kwa upande mwingine niliona halikuwa wazo zuri. Halikuwa wazo zuri kwa sababu huyo mtu nitakayemtuma hiyo kazi nitamuaminije. Atakaponiletea hizo kucha akaniambia kuwa ni za maiti, nitaaminije kuwa ni kucha za maiti kweli?
Je kama atakwenda kukata kucha zake mwenyewe na kuniletea, nitajuaje?
Muhuni ni muhuni tu, anaweza kuona kazi ya kufukua kaburi ni ngumu na pesa haiachiki hivyo akaenda kujikata kucha zake mwenyewe na kuniletea. Sitaweza kujua kama kucha hizo si za maiti au ni zake mwenyewe.
Hivyo nikajiambia, si vizuri kufanya jambo la kubahatisha. Ni vizuri nifanye jambo la uhakika. Na nitakuwa na uhakika wa kucha hizo endapo nitakwenda mimi mwenyewe kufukua hilo kaburi na kukata kucha hizo.
Nilipofika nyumbani niliingiza pikipiki yangu nikasubiri saa nane ifike. Wakati nimeketi sebuleni nikiendelea kusubiri muda, nikapitiwa na usingizi.
Katika usingizi huo eti nikaota nimekwenda kufukua kaburi. Nikakuta mtoto mchanga aliyezikwa, hana hata kucha, Nikalifukia na kufukua kaburi jingine, hilo nalo nilikuta mtu aliyekuwa amekatwa mikono na miguu. Alikuwa amefariki kwenye ajali ya gari.
Nikalifukia tena na kutafuta kaburi jingine ambalo nilianza kulifukua. Wakati nakaribia kulifikia sanduku mvua ikanyesha kwa kishindo. Kaburi likawa linajaa maji. Kazi ikanishinda! Kutahamaki kulikuwa kunaanza kupambazuka.
Ikabidi niondoke nikiwa nimechukia. Hapo hapo nikazinduka.
Nilitazama saa yangu na kuona ilikuwa saa saba ikielekea kuwa na nusu. Nikaona wakati huo pia ulikuwa muafaka kuondoka. Nikaenda kunawa uso kisha nikarudi sebuleni na kuvaa vile viatu vya mvua kwa ajili ya kujikinga na tope wakati wa kufukua kaburi.
Ile mipira ya mikononi sikuivaa kabisa. Nikatoa pikipiki yangu. Lile shepe nilikuwa nimeshalifunga katika siti ya nyuma ya pikipiki.
Kifaa cha kukatia kucha nilikuwa nimeshakitayarisha. Ulikuwa wembe mpya.
Nikaondoka.
Niliendesha piki piki yangu taratibu hadi nikafika Gofu. Usiku huo kulikuwa kimya. Hakukuwa na gari wala watu waliokuwa wakipita. Nilikuwa na hakika kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye angeniona.
Nilifika katika lile eneo la makaburi. Nikaiingiza pikipiki yangu ndani ya eneo hilo lililokuwa na mti pamoja na vichaka vidogo vidogo.
Nikaiegesha pikipiki chini ya mti huku nikiangaza macho huku na huku. Mbalamwezi ililiangaza vizuri eneo hilo kiasi kwamba sikupata taabu kuyaona makaburi hayo.
Nilianza kuvaa mipira ya mikononi kisha nikalifungua lile shepe. Nililishika mkononi nikaanza kutafuta kaburi la kuchimba.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Makaburi mengi yalikuwa yamewekewa zege, nikaenda mbele zaidi. Nikakuta kaburi moja ambalo halikuwa limewekewa zege na lilionesha lilikuwa jipya. Huenda kulikuwa na mtu aliyekuwa
amezikwa siku iliyopita.
Nikaanza kulichimba. Kwa vile mchnaga wake ulikuwa laini nililichimba haraka harka huku nikirundika mchanga upande mmoja juu ya kaburi hilo. Shimo lilipokuwa kubwa niliweza kuingia ndani nikaendelea kuchimba.
Baada ya kama nusu saa tu nikawa nimelifikia sanduku lililokuwemo ndani. Nilipofanikiwa kuuondoa mchanga wote uliokuwa juu ya sanduku hilo nikaufungua mlango wa sanduku na kuuacha wazi. Ndani ya sanduku hilo niliona maiti ya mwanamke.
Nikatia mkono mfukoni mwangu na kutoa ule wembe. Niliufungua kwenye karatasi yake nikaushika kisha nikaushika mkono wa ile maiti ya mwanamke. Hapo hapo nikaona mwanga wa tochi unanimulika kutoka juu ya kaburi kisha sauti nzito ikaniuliza.
“Wewe nani na unafanya nini hapa?”
Kwa kweli nilishituka sana. Wembe uliniponyoka. Miguu ikanitepeta. Nikainua uso wangu haraka na kutazama juu ya kaburi hilo.
Nilijuta!
Nilimuona mtu aliyekuwa akinimulika tochi akiwa juu ya kaburi lakini sikuweza kumuona vizuri kwa sababu ule mwanga wa tochi ulikuwa unapiga kwenye macho yangu.
“Ulikuwa unafanya nini?’ Mtu huyo aliendelea kuniuliza kwa ukali.
Sikumjibu. Yeye alikuwa amesimama upande mmoja wa kaburi. Na mimi nilikurupuka kuelekea upande mwingine wa kaburi nikapanda juu haraka.
Wakati ninainuka ili nikimbie, alinirushia rungu. Nikainama na kulikwepa. Wakati nainama niliona kitu kikiruka kutoka mfuko wa shati langu na kuanguka chini. Sikujua kilikuwa kitu gani. Na sikuwa na muda wa kukitazama vizuri.
Yule mtu nilimuona. Kwa jinsi alivyovaa niligundua alikuwa mlinzi. Nikahisi alikuwa mlinzi wa eneo lile.
Nikatimua mbio kuelekea nilikoiacha pikipiki yangu. Wakati nakimbia nilijiuliza kama kulikuwa na mlinzi, alikuwa wapi wakati nafika na kufukua lile kaburi?
Nilitazama nyuma na kumuona alikuwa ananikimbiza.
“Simama wewe, utakufa!” aliniambia.
Lakini sikugeuka wala sikusimama. Niliendelea kukimbia hadi nikaifikia pikipiki yangu, yeye bado akiwa mbali. Niliiwasha haraka haraka. Pikipiki ilikubali mara moja. Nikaipanda na kuondoka kwa kasi.
“Wewe…bahati yako!” aliniambia baada ya kunikosa.
Alikuwa amesimama akinielekeza rungu lake. Niligeuza uso mara moja tu nikamtazama.
Alipoona namtazama aliniambia kwa hasira.
“Usije tena hapa mchawi mkubwa. Ningekuua leo!”
Niligeuza uso wangu nikatazama mbele ninakoelekea. Kimoyomoyo nilikuwa nikijiambia.
“Ningekufa leo!”
Nilikuwa nimekaa kwenye pikipiki huku nikijihisi wazi kuwa nilikuwa natetemeka. Sikuwa nimezoea mapambano hivyo tukio lile la kufumwa na kutimuliwa kwa sime lilitosha kunifanya nitetemeke.
Nilikuwa nikijiambia laiti yule mtu angenishika angeniua kwa vile mwenzngu alikuwa na silaha, mimi niko mikono mitupu.
Nilirudi nyumbani nikiwa nimeacha shepe langu ndani ya lile kaburi.
Lakini halikuwa mali kuliko uhai wangu. Kucha za maiti zilitaka kunitoa roho yangu!
Nilipofika nyumbani nillikuwa nahema kama vile nilikimbia njia nzima kurudi nyumbani. Niliingiza pikipiki yangu. Nikavua vile viatu nilivyovaa kuzuia tope pamoja na mipira ya mikononi kisha nikaingia bafuni kuoga.
Nilipotoka bafuni niliona afadhali kidogo. Nikaenda kulala. Hata usingizi wenyewe sikuupata. Nilianndamwa na njozi za ajabu ajabu hadi kunakucha. Moja ya ndoto iliyonitisha ilikuwa ile maiti niliyoifukua imegeuka mzuka na kunifuata nyumbani ikiwa imetoka kucha ndefu vidoleni.
Kucha hizo ndizo zilizokuwa zinatoboa mlango wa chumbani kwangu. Wakati nashituka mlango wa chumbani kwangu ulikuwa umeshafunguka.
Laiti nisingewahi kuamka sijui ingekuwaje?
Ilikuwa miujiza mitupu!
Baada ya kuoga na kuvaa nilitoa pikipiki yangu. Hapo ndipo nilipogundua kuwa leseni yangu sikuwa nayo mfukoni. Usiku uliopita niliiweka kwenye mfuko wa shati langu na kwa muda ule sikuwa nayo.
Nikahisi ndio iliyonianguka kule makaburini usiku wakati yule mlinzi akinikurupusha.
Nikawa nimegwaya. Nilijiambia kama yule mlinzi ataiona ile leseni yangu ambayo ilikuwa na picha yangu anaweza kuipeleka polisi. Kwa vile tayari nilikuwa na rikodi mbaya polisi, kugunduliwa kwangu kungekuwa rahisi sana.
Polisi watakapoiona picha yangu watanifuata kazini kwangu na kunikamata.
Imeshakuwa balaa!
Licha ya kupatwa na fadhaa kiasi hicho nilipanda pikipiki yangu. Kwanza nilikwenda Chuda kumueleza kaka yangu mkasa mzima.
“Amour umefanya uzembe mwenyewe!” kaka akaniambia baada ya kunisikiliza.
Uso wake ulionesha wazi kuwa hakufurahishwa na kitendo changu.
“Nimefanya uzembe kivipi kaka?” nikamuuliza.
“Jana nilikwambia nini?”
“Hebu nikumbushe pengine nimesahau”
“Si nilikwambia kwamba tuma mtu”
“Kaka kutuma mtu kunaweza kuleta matatizo”
“Matatizo gani?’
“Sitakuwa na uhakika kama hizo kucha atakazoniletea ni za maiti kweli. Anaweza kwenda kujikata kucha zake mwenyewe akaniletea”
“Ungetafuta mtu unayemuamini”
“Wahuni hawaaminiki kaka. Wangechukua pesa zangu halafu wakaniletea kucha zao wenyewe”
Kaka yangu akanywea.
“Saasa umeshajitia kwenye balaa jingine!”
“Kwa kweli ni balaa, sasa sijui itakuwaje!”
“Kwani hivi sasa unakwenda wapi?”
“Ninakwenda kazini”
“Ukitoka kazini nenda ukamueleze yule mganga”
“Nitakwenda”
“Basi wewe nenda kazini kwako, punguza wasiwasi”
Nikaondoka kwa kaka na kwenda kazini. Lakini njia nzima nilikuwa nawaza tu.
Nilipofika niliingia kazini kama kawaida. Baadaye kidogo mhasibu alifika na kuingia ofisini kwake. Haukupita muda mrefu mhasibu alitufuata akatueleza kisa kilichonishitua.
“Jana tulikwenda kuzika kule Gofu, shemeji yangu alikuwa amefariki. Hivi sasa napigiwa simu naelezwa kwamba kuna mtu alikwenda kulifukua lile kaburi usiku. Sijui alitaka kuichukua ile maiti?”
“Labda ni wachawi, lakini hakuwahi kuichukua?” Mfanya kazi mmoja akamuuliza.
“Hakuwahi, alikurupushwa na mlinzi. Lile eneo linalindwa kwa ajili yakuzuia watu kama hao”
“Angemkamata ingekuwa vizuri kwa sababu angefahamika” Mfanyakazi mwingine alidakia.
“Alikimbia na pikipiki. Mlinzi amesema huyo mtu alikuja na pikipiki”
Niliposikia hivyo moyo wangu ulishituka. Kama namba za pikipiki yangu nazo zimeonekana nimekwisha!
Sikujua kama ile maiti ilikuwa ni ya shemeji yake mhasibu wetu. Nikaona nimejiingiza katika matatizo mengine ambayo sikuyatarajia.
“Hivi sasa nimeitwa polisi nikatoe maelezo, ile maiti imepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi kujua kama ilibakwa. Kuna watu wanabaka maiti” Mhasibu aliendelea kutueleza.
“Inawezekana. Ni vizuri kama amepelekwa hospitali kufanyiwa uchunguzi. Binaadamu hivi sasa hawaaminiki kabisa” nikajidai kusema ili nisionekane nimefadhaika.
“Kumbe yule mlinzi alikwenda kuripoti polisi” Mwenzetu mwingine akauliza.
“Alikwenda polisi asubuhi. Ndio maana ninaitwa polisi” Mhasibu akamjibu kisha akatuaga na kuondoka.
Niliwaza kwamba kama mlinzi alikwenda kuripoti polisi, ile leseni yangu pia aliipeleka baada ya kuiokota pale ilipoanguka. Polisi watakuwa wameshaiona picha yangu. Bila shaka mhasibu wetu ameitwa ili kuoneshwa ile leseni ili athibitishe kama ndiye mimi.
Sasa sijui nikimbie kuepusha aibu, au niwangoje polisi waje wanikamate hapa hapa?
Kwa kweli nilikuwa nimechanganyikiwa.
Kwa dakika kadhaa sikuweza kujua nifanye nini. Wafanyakazi wenzangu walikuwa wakilizungumzia lile tukio la kufukuliwa kaburi, mimi nilikuwa kimya. Moyo wangu ulikuwa ukihangaika. Lakini hakukuwa na yeyote aliyeweza kunigundua.
Wasiwasi uliponizidi nilitoka nje ya duka letu. Kilichonitoa ni ule wasiwasi kwamba polisi wakitokea niweze kuwaona mapema. Nilikuwa nimeshapanga kuwakimbia.
Ilikuwa bora kupotea kuliko kupatwa na fedheha kama ile mbele ya wafanyakazi wenzangu.
Nilisimama nje ya duka letu kwa karibu nusu saa, nilipoona hakukuwa na polisi wowote waliokuwa wanakuja nikarudi ndani. Baadaye nikatoka tena. Nikaangalia pande zote za barabara kisha nikarudi.
Wakati nimekaa nikiendelea na mawazo yangu nilishituka nilipomuona mhasibu akiingia. Nilijua kuwa alikuwa amefuatana na polisi waliokuja kunikamata.
Lakini sikuona polisi. Alikuwa peke yake. Nikamkodolea macho ya tashiwishi. Nilikuwa na hisia kwamba alikuwa ameoneshwa leseni yangu na kunitambua.
Mfanyakazi mwenzetu mmoja akamuuliza kilichotokea huko polisi alikokwenda.
“Nimekwenda kutoa maelezo yangu” akasema na kuongeza.
“Ule mwili bado uko hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi”
“Huyo mtu aliyefukua hilo kaburi hakufahamika?’ nikauliza ili kuondoa dukuduku nililokuwa nalo.
“Si rahisi kufahamika. Mtu mwenyewe alikimbia na pikipiki” Mhasibu akanijibu.
Hapo wasiwasi ukanipungua kidogo.
Baada ya mhasibu kuzungumza na sisi kwa dakika chache akaingia ofisini kwake.
Haukupita muda mrefu, simu tuliyokuwa tunaitumia ikaita. Ilikuwa inapokelewa na mtu yeyote aliye karibu nayo. Akaipokea mfanyakazi mmoja akasikiliza kisha akaniita.
“Amour ni simu yako”
Moyo ukanipasuka.
Ni nani tena?CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikaenda na kukipokea chombo cha kuzungumzia. Nikakiweka sikioni na kusema.
“Hello!”
“Naongea na bwana Amour?” Sauti nzito tena inayokwaruza ikauliza kutoka simu ya upande wa pili.
Moyoni mwangu nilikuwa nikijiuliza ni nani mwenye sauti hii? Akilini mwangu sikuweza kukumbuka mtu yeyote ninayemfahamu mwenye sauti inayolingana na ile.
Nikashuku kwamba anaweza kuwa afisa wa polisi ananipigia kuniita kituo cha olisi.
“Ndio. Wewe nani?”
“Hebu njoo hapa Tropicana, utanijua tu”
Tropicana ulikuwa mkahawa uliokuwa mtaa wa pili ambao wafanyakai wengi hupenda kunywa chai wakati wa saa nne na hata kula chakula cha mchana.
“Ni vizuri unifahamishe wewe nani?”
“Usiwe na wasiwasi. Ukifika hapa utaniona na utanijua”
Nikaurudisha mkono wa simu kisha nikatoka. Niliwaaga wenzangu kuwa ninakwenda kunywa chai.
Nilipotoka nje ya duka letu nilizunguka mtaa wa pili ambako kulikuwa na huo mkahawa wa Tropicana. Wakati natembea nilikuwa nikiwaza huyo mtu aliyeniita atakuwa nani kama si afisa wa polisi.
Nilikuwa na hakika kwamba sikuwa nikifahamiana na mtu aliyekuwa na sauti kavu kama ile.
Nilipofika kwenye mkahawa huo nikaingia. Nilisita kidogo kando ya mlango nikawatupia macho watu waliokuwamo ndani. Nikaona mtu mmoja aliyekuwa amekaa katika meza ya pembeni akinipungia mkono kuniita.
Sikuweza kumfahamu mpaka nilipofika karibu yake.
“Ah Mgosingwa!” nikasema mara tu sura yake iliponijia akilini mwangu.
Alikuwa mlinzi wetu ambaye alifukuzwa kazi kwa tabia yake ya ulevi wa kupita kiasi. Tulikuwa tunamuita Mgosingwa, neno la kabila la kizigua linalotokana na neno mgosi, yaani mwanamme.
Kwa vile yeye mwenyewe alikuwa mzigua, alikuwa akimuita kila mtu “mgosingwa” hasa pale anapotaka kumkopa mtu pesa ya kwenda kulewea. Na sisi tukampa jina hilo la mgosingwa. Nilizoea kumuita hivyo na jina lake halisi nilikuwa silijui.
“Vipi Mgosingwa?” akaniambia huku akinipa mkono kunisalimia.
“Salama tu Mgosingwa. Wewe ndio uliyenipigia simu kuniita?’
“Ndiye mimi Mgosingwa. Karibu ukae”
Nikakaa kwenye kiti.
“Ulikuwa unasemaje Mgosingwa?” nikamuuliza nikiwa na shauku ya kutaka kujua alichoniitia.
“Mgosingwa unatakiwa polisi!”
Kusema kweli nilishituka aliponiambia hivyo. Moyo wangu ukawa unadunda pu!pu!pu!
Nikajidai natabasamu.
“Nimefanya kosa gani Mgosingwa?”
Mgosingwa alitia mkono kwenye mfuko wa shati lake akatoa ganda kama la kitambulisho akaniwekea mezani.
“hii si leseni yako Mgosingwa?’ akaniuliza.
Nikalichukua lile ganda na kulifungua. Naam. Ilikuwa ni leseni yangu niliyokuwa nimeitupa kule makaburini. Pale pale uso wangu ulibadilika rangi kwa hofu iliyochanganyika na fadhaa. Nikamtazama mgosingwa huku nikijiuliza ameipata wapi leseni yangu.
“Huku nikiendelea na tabasamu langu la kulazimisha nilimuuliza.
“Mgosingwa umeipata wapi hii leseni yangu?’
“Si nimekwambia unatakiwa polisi?”
Jibu lake hilo lilizidi kunichanganya na kunifadhaisha. Midomo yangu niliyokuwa ninailazimisha kutabasamu huku nikiwa na fadhaa ilianza kutatizika na kutetemeka. Sasa haikuweza tena kutabasamu.
“Mgosingwa unanichanganya. Sasa nani kakupa hii leseni na kakupa kwa madhumuni gani?” nikamuuliza huku nikiizuia modomo yangu isitetemeke wakati nikimuuliza hivyo.
Mgosingwa aligundua kuwa nilikuwa nimetaharuki. Akacheka. Hata hivyo kwa vile uso wake ulikuwa umekunjana kutokana na kuendeleza kilevi, kicheko chake hakikuufanya uso wake upendeze, bali ulionekana kama anataka kulia.
“Mgosingwa hukumbuki uliiacha wapi leseni yako?” akaniuliza.
Nikatikisa kichwa.
“Sikumbuki” Nilimjibu hivyo ili nijue ataniambia nini.
“Mgosingwa jana usiku si ulikuja kule makaburi ukafukua lile kaburi nikakukurupusha”
Aliponiambia hivyo nikanywea na kumtazama. Alipoona nipo kimya aliendelea kunieleza.
“Wakati unakimbia mgosingwa uliiangusha hii leseni yako”
“Kumbe wewe ndiye unayelinda pale?” nikamuuliza.
“Nilipoacha kazi STC niliajiriwa na kanisa kulinda yale makaburi. Sasa jana usiku niliondoka kidogo kwenda kupata ulabu (kilevi), niliporudi nikakuta mtu amechimba kaburi na kuingia ndani. Hii leseni niliiokota asubuhi ndio nikagundua kuwa ulikuwa wewe”
“Sasa Mgosingwa umeshakwenda kutoa ripoti polisi?”
Polisi nimeshakwenda lakini nilipoona hii leseni yako sikuwapa. Niliwambia huyo mtu sikumuona vizuri”
Hapo hapo nilitia mkono mfukoni nakutoa pochi yangu. Niliifungua na kuchomoa noti za shilingi elfu ishirini, nikampa.
“Asante sana Mgosingwa, umenisaidia sana”
SASA ENDELEA
“Tunajuana Mgosingwa , hatuwezi kusalitiana” Mgosingwa aliniambia wakati akipokea zile pesa.
“Unajua lile kaburi ni la shemeji yake mhasibu wetu. Mimi sikujua kabisa”
“Kwani ulikuwa unataka nini Mgosingwa?”
“Kuna kitu nilikuwa nataka”
“Kitu gani?”
Kwanza nilisita kumwambia nilikuwa nataka nini lakini nikaona ni vizuri nimwambie.
“Nilikuwa nataka kucha za maiti”
“Mgosingwa unataka kwenda kuroga au kuua mtu?”
“Hapana. Ni kwa mambo yangu binafsi”
“Mgosingwa ungeniambia, ningekupatia. Mimi Ndio nalinda yale makaburi”
“Bado ninazihitaji Mgosingwa, nifanyie huo mpango”
“Utanipa shilingi ngapi?”
“Ukiniletea hizo kucha nitakuongezea kumi nyingine”
“Fanya ishirini Mgosingwa, kumi ndogo sana”
“Si kitu, nitakupa hizo ishirini”
“Sasa Mgosingwa nitafutie shepe na kiwembe. Niletee pale saa nne usiku. Mimi nitafukua kaburi, asubuhi nitakuletea hizo kucha nyumbani kwako”
“Hakuna tatizo. Nitakuletea hilo shepe. Kiwembe utanunua mwenyewe”
“Sasa Mgosingwa fanya kitu kimoja, nipatie kianzio cha shilingi elfu kumi, hiyo kumi nyingine utanipa asubuhi”
Nilitaka kucheka lakini nilisita kwa sababu tulikuwa katika suala nyeti sana kwa upande wangu.
“Kwanini usisubiri hadi hiyo asubuhi nikupe zote?” nikamuuliza.
“Ninahitaji hiyo pesa kwa sasa”
“Mgosingwa si nimekupa elfu ishirini za bure?”
“Mgosingwa si za bure, polisi ungetoa ngapi ili wakuachie”
“Sawa. Sasa si hizo nimekupa”
“Hazitoshi Mgosingwa”
“Wewe unataka kwenda kulewa tu” nikamwambia huku nikitia mkono kwenye mfuko wa suruali yangu.
Nilitoa pochi yangu nikaifungua na kumpa shilingi elfu kumi alizotaka.
“Umeridhika?” nikamuuliza.
“Hapa Mgosingwa umeniokoa sana”
“Utapata chupa ngapi”
“Acha mzaha Mgosingwa. Mimi siendi kulewa. Mke wangu amekwenda kwao kujifungua. Nilitaka kumtumia hzi pesa”
“Sawa Mgosingwa mtumie, nilikutania tu”
“Sasa Mgosingwa niletee shepe saa nne usiku pale pale”
“Sawa, nitakuletea”
Nikaagana na Mgosingwa na kuondoka.
Nilipotoka kazini jioni nilikwenda kununua shepe jingine nikaenda nalo nyumbani. Nikawa nasubiri saa nne usiku ifike nimpelekee Mgosingwa.
Kwa mara ya kwanza niligundua hata mlevi anaweza kuwa na manufaa yake. Sikutarajia kuwa Mgosingwa mlevu wa gongo na pombe ya mnazi angeweza kunisaidia. Licha ya msaada wa kucha za maiti alioniahidi, kile kitendo chake cha kuiokota leseni yangu na kuja kunipa mwenyewe bila kuipeleka polisi ulikuwa msaada mkubwa kwangu.
Nilimshukuru sana nikijua kama si yeye ningeumbuka. Pengine muda ule ningekuwa niko mahabusi.
Ilipofika saa nne usiku nililifunga lile shepe sehemu ya nyuma ya siti ya pikipiki yangu nikatoka.
Nilikwenda katika lile eneo la makaburi analolinda Mgosingwa. Niliposimamisha tu pikipiki, Mgosingwa akajitokeza. Alitazama kila upande, alipoona kuko kimya akasogea kwenye pikipiki yangu na kunisaidia kulifungua lile shepe.
Ile hewa yake ya mwilini tu ingetosha kumlewesha mtu. Alikuwa akinuka pombe aina ya gongo kama vile alikuwa mtambo wa kuitengenezea. Muda ule tayari alikuwa ameshalewa.
Sikumlaumu. Kulinda makaburi wakati wa usiku ilikuwa kazi ya kutisha. Alihitaji kupata kitu cha kutuliza akili yake, vinginevyo anaweza kuota ndoto za maiti waliozikwa usiku kucha.
Hatukuungumza chochote. Alipochukua lile shepe, alinionesha ishara kuwa tukutane asubuhi akatokomea makaburini.
Nikapanda pikipiki yangu na kuondoka. Nilipofika nyumbani nilifikia kuoga na kulala.
Kulikuwa kunaanza kupambazuka nilipoamshwa usingizini kwa kishindo cha mlango wa mbele uliokuwa unabishwa. Nikatazama saa yangu na kuona ilikuwa saa kumi na mbili kasorobo. Nikajiuliza ni nani abishae mlango? Sikupata jibu.
Nikashuka kitandani na kuvaa suruali yangu kisha nikafungua mlango wa chumbani mwangu na kutoka ukumbini. Nilikwenda kwenye mlango wa mbele na kuuliza.
“Nani abishaye?”
“Ni mimi Mgosingwa!” nikaisikia sauti ya Mgosingwa ikisikika kwa nje.
“Ahaa ni wewe!” nikasema huku nikifungua mlango.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nikamuona mgosingwa amesimama mbele ya mlango. Kando ya baraza ya nyumba niliyokuwa naishi kulikuwa na baskeli iliyoegeshwa. Katika kiti chake cha nyuma ilikuwa imefungwa shepe.
“Kumekucha mgosingwa. Habari ya leo?” Mgosingwa akaniambia kwa uchangamfu.
“Nzuri Mgosingwa, je umefanikiwa?”
“Nisifanikiwe kwanini?” akaniuliza huku akitia mkono kwenye mfuko wa shati lake na kutoa kibiriti.
Nilidhani alikuwa anataka kuwasha sigara lakini alipokifungua alikielekeza mbele ya macho yangu. Nikaona alikuwa ameweka kucha nyeupe.
“Ndio hizo Mgosingwa?” nikamuuliza.
“Si ulitaka kucha za maiti?”
“Ndiyo”
“Ndio hizo nimekuletea”
“Ulifukua kaburi?”
“Kulikuwa na kaburi moja la maiti iliyozikwa jana, nililifukua usiku nikaikata kucha ile maiti kisha nikalifukia kama nilivyolikuta. Kucha zenyewe ndio hizo”
Nilizitazama vizuri zile kucha alizoziweka ndani ya kibiriti kisha nikakifunga.
“Asante sana Mgosingwa” nikamwambia Mgosingwa kisha nikamtazama.
“Mgosingwa fanya basi hayo makwarukwaru” Mgosingwa akaniambia huku akinitazama kwa jicho la tamaa.
Makwarukwaru ni lugha ya mitaani. Mgosingwa alikuwa akimaanisha nimpe pesa.
“Makwarukwaru yapi Mgosingwa?”
“Si tuliongea jana, nikikuletea hizo kucha utanipa shilingi elfu ishirini”
“Mgosingwa si nilikupa kumi?’
“Ndio, ikabaki kumi”
Nikatia mkono kwenye mfuko wa suruali yangu na kutoa noti za shilingi elfu kumi nikampa.
“Asante Mgosingwa, wewe hata kama utataka mguu wa maiti niambie nitakupatia”
“Sawa bwana”
Mgosingwa akachukua baskeli yake na kuniaga. Na mimi nikarudi ndani.
Nilipoingia ndani nilikwenda kuoga nikavaa na kutoka na pikipiki yangu. Nikaenda kwa yule mganga wa kipemba. Kwa vile ilikuwa bado mapema nilisubiri nje ya gesti hadi mlango wa gesti ulipofunguliwa, nikaingia.
Nilibisha mlango wa chumba cha mganga. Baada ya muda kidogo mlango ulifunguliwa. Mganga aliponiona tu akanikumbuka.
“Oh karibu, wewe si ndiye yule jamaa uliyekuja juzi?” akaniuliza.
“Ndiye mimi”
“Karibu ndani”
Alinipisha kwenye mlango nikaingia mle chumbani.
“Kaa kwenye kiti” akaniambia na kuongeza.
“Bahati yako umenikuta, leo ndio siku yangu ya kuondoka. Naenda Arusha. Nilikutazamia jana sikukuona”
“Jana sikufanikia kupata zile kucha”
“Sasa leo umezipata?”
“Nimezipata”
“Ni kucha za maiti khaswa?”
“Ni kucha za maiti. Kuna mtu alifukua kaburi jana usiku akamkata kucha maiti”
Nilitia mkono kwenye mfuko wangu wa shati nilikoweka kile kibiriti alichonipa mgosingwa.
“Kama umezipata hizo kucha nitaahirisha safari yangu ili nikufanyie kazi yako” Mganga alinaimbia.
Nilikitoa kile kibiriti.
“Ni hizi hapa” nikamwambia na kukifungua kile kibiriti na kumuonesha.
“Ziko wapi. Mbona sioni kitu” Mganga akaniuliza.
Nikashituka na kuangalia ndani ya kile kibiriti.
Hamkuwa na kitu. Kibiriti kilikuwa kitupu kama mkono uliorambwa!
Mbali ya kukichomoa kabisa kwenye ganda lake sikuona chochote.
“Jamani zile kucha zimekwenda wapi?” nikajiuliza kwa mshangao.
“Ulikuwa umezitia humu?” Mganga akaniuliza.
“Ndio, nilizitia humu. Wakati naondoka nyumbani zilikuwamo!”
“Sasa zimekwenda wapi?”
“Sijui”
“Au umezimwaga bila kujua?’
“Sijazimwaga. Nilipoondoka nyumbani kucha zilikuwemo. Nikakitia hiki kibiriti mfukoni na sijakitoa mpaka muda huu”
“Basi itakuwa ni miujiza”
“Sasa miujiza hii inatokea wapi?”
Mganga akawa anafungasha vitu vyake kwenye begi lake alilokuwa ameliweka kitandani. Niliona kama amenipuuza.
“Sasa miujiza hii imetokea wapi?’ nikamuuliza tena.
“Hilo jini limekutawala sana, itakuwa vigumu kuliepuka” Mganga akaniambia huku akiendelea kupanga nguo zake.
“Limenitawala kivipi?’
“Wauliza jibu, wewe huoni mambo yako yanakwenda ovyo unadhani ni kwa sababu ya nini?’
Sikumpinga, mambo yangu yanaenda ovyo kweli.
“Ndio sababu hizi kucha zimepotea?” nikamuuliza.
Mganga hakunijibu. Badala yake aliniambia.
“Kazi kama hizo sizitaki kabisa, zitaniletea nuksi bure”
“Wewe ndiye mtaalamu nilitegemea kuwa utanisaidia”
“Sitaweza kukusaidia, naomba uende zako. Nina safari ya arusha nisije nikachelewa gari” Mganga aliniambia akionesha wazi kukasirika.
Sikuwa na jingine isipokuwa kuinuka kwenye kiti. Nikamuga na kuondoka zangu. Nilivyomuaga hata hakunijibu kitu. Sijui nilimkosea nini. Alikuwa amehamaki mara moja.
Wakati natoka mle chumbani yale maneno yake kwamba hilo jini limenitawala sana na kwamba itakuwa vigumu kuliepuka, yalikuwa yakinirudia akilini mwangu.
Kusema kweli niliondoka pale gesti nikiwa na fadhaa sana. Nilipanda pikipiki yangu. Sikutaka kwenda kwa kaka ingawa hapakuwa mbali na pale gesti, nikaenda kazini kwangu.
Nilifanya kazi huku nikiwaza jinsi zile kucha zilivyopotea kwenye kibiriti. Kwa kuzingatia maneno ya yule mganga iliwezekana kwamba zile kucha zilipotezwa na Zainush.
Lakini kubwa ambalo lilinitia fadhaa ni yale maneno ya yule mganga kwamba hilo jini limenitawala sana na itakuwa vigumu kuliepuka.
Kama mganga wa majini amesema hivyo, je juhudi zangu za kumuondoa zainush zitafanikiwa kweli, nikajiuliza kwa fadhaa.
Mganga mwenyewe amenifukuza, nikaendelea kuwaza, bila shaka na yeye alikuwa amepata hofu baada ya kuona jinsi zile kucha zilivyotoweka kwenye kibiriti.
“Una nini leo Amour?” Wafanya kai wenzangu walikuwa wakiniuliza.
“Nikoje?’
“Leo unaonekana una mawazo sana” Mfanyakazi mmoja akaniambia.
“Kawaida tu”
“Tuambie kama kuna kitu kimekukwaza”
“Kwa hapa kazini?”
“Popote tu”
“Hakuna kitu. Binaadamu kuwaza ni kawaida”
“Mwenzetu leo umezidi sana”
“Basi nitapunguza” nikasema kwa utani kisha nikacheka ili kukatisha yale mazungumzo yake.
Nilipomwambia hivyo naye akacheka, akaniambia.
“Sawa bwana”
Maneno yakaishia hapo hapo. Sikujua kama wafanyakazi wenzangu walikuwa wananiona nilikuwa na mawazo. Baada ya hapo nikajitia kufanya kazi ili nionekane wa kawaida. Sikutaka mtu yeyote ajue lililokuwa moyoni mwangu.
Jioni nilipotoka kazini nikaenda Chuda kwa kaka. Nilimueleza juhudi nilizozifanya jana yake hadi nikafanikiwa kupata zile kucha na hatimaye zikatoweka zikiwa ndani ya kibiriti wakati nikiwa kwa yule mganga.
“Mganga alipata hasira akanifukuza. Aliniambia niondoke na kwamba yule jini ameshanitawala, itakuwa vigumu kumuondoa” nikamwambia.
“Sasa kwanini alikufukuza?’
“Sijui”
“Na hizo kucha zilitoweka vipi?’
“Sijui. Mgosingwa aliniletea asubuhi zikiwa ndani ya kibiriti. Sasa nafika kwa mganga nafungua kibiriti, kucha hazimo!”
INAENDELEA

0 Comments