Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Mwanamke jini sehemu ya tisa (09)



 “Umekuja kutembea tu huku Pemba?” Zena akaniuliza kwa sauti iliyoonesha kuwa hakuyaamini maneno yangu.

“Ndio” nikamjibu.
“Sasa umeshatembea na kuuona mji?”
“Ndio”
“Umeuonaje?”
“Ni mji mzuri”
“Kumbe unatembea hadi huku Pemba?’
“Ni leo tu”
“Umepanga kurudi lini?”
“Nitarudi leo”
“Si ulale uondoke kesho?”
Nikatikisa kichwa.
“Nitaondoka leo leo”
“Nisubiri basi tuondoke sote”
Zena akainuka. Aliingia kwenye chumba kimojawapo ambacho mlango wake ulikuwa wazi. Nikamuona anavaa baibui. Akachukua mkoba wake na kutoka.
“Twendezetu” akaniambia kama vile tulikuja safari moja.
Nikainuka na kumfuata. Tulitoka kwenye ile nyumba tukashika njia ya kuelekea bandarini.
Wakati wote nilikuwa nikijiuliza kwanini nilimkuta Zena pale nyumbani. Huyo mganga mwenyewe alikuwa wapi?
Ile ilikuwa ni miujiza ya ajabu ambayo sikuwahi kuiona katika maisha yangu.
Matarajio yangu ya kumpata mganga wa kuliondoa tatizo langu yalififia kabisa moyoni mwangu. Huyu jini alikuwa amenizingira kila pembe.
Tulipofika bandarini Zena alikata tikiti mbili za boti inayokwenda kasi. Boti hiyo ilikuwa inakwenda Dar. Siku ile hakukuwa na chombo chohote kinachokwenda Tanga.
Tulipojipakia kwenye boti nilikaa na Zena siti zilizokuwa zimepakana. Tulisubiri kwa muda wa saa nzima kabla ya safari kuanza.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kweli kupambana na jini aina ya Zena ni kazi! Sasa alikuwa akinirudisha Dar. Niliamini kuwa alikuwa akijua kilichonipeleka Pemba ingawa hakuniambia. Kitu ambacho nilishindwa kuelewa ni jinsi nilivyomkuta yeye pale nyumbani kama vile ni kwake.
Wakati boti iko katikati ya safari nilimuona Zena amelala usingizi kabisa. Nikawa namtazama. Alikuwa na weupe uliochanganyika na wekundu. Uso wake ulikuwa na pozi la kiarabu ingawa alionekana kuchanganya damu ya Kiafrika. Sikujua kama majini nao wanakuwa machotara kama binaadamu.
Kwa uzuri alikuwa mzuri sana, sikuwahi kuona msichana mwenye mvuto wa sura na umbile kama yeye. Tatizo lake ni kwamba alikuwa jini tena jini mbaya mwenye vituko vilivyoshindikana.
Hadi pale nilikuwa nimesalimu amri. Nilishasema kuwa Zena sitamuweza tena na hakukuwa na mganga yeyote atakayemuweza.
Ghafla tuliona boti ikikata moto. Ikawa inasuasua juu ya bahari. Muda si muda ikapigwa na wimbi kubwa. Sote tulitikiswa. Hapo ndipo watu walipoanza kwenda mbio na kuifanya boti ilale upande mmoja.
Baadhi ya abiria wakaanza kujitosa baharini. Nikaona sasa hali ilikuwa mbaya. Nilijikuta nikimuamsha Zena bila kupenda. Zena akaamka.
“Nini. Mbona kuna hekaheka?” akaniuliza.
“Boti inazama” nikamwambia.
“Boti inazama?” akaniuliza kwa fadhaa.
Kabla sijamjibu, ule upande wa boti uliokuwa unazama ukazidi kulala.
“Duh ni kweli, twende tukaruke, tutakufa humu!” akaniambia huku akiinuka kwenye siti.
Tulikwenda kwenye mlango wa boti tukatoka. Watu walikuwa wakiendelea kuchupa baharini.
“Chupa!” Zena akaniambia.
Laiti angejua jinsi ambavyo sikuwa nikijua kuogelea asingeniambia chupa.
Upande wa pili wa boti nao ikaanza kuzama.
“Chupa, boti inazama!” akaniambia tena.
Sikuthubutu. Nilibaki kuitazama bahari.
“Amour unasubiri kufa humu ndani ya boti?” Zena akaniuliza kwa hasira.
Nikatikisa kichwa.
“Siwezi kuogelea, nikiruka ndio nimekwisha!”
“Mwanaume mzima unasema huwezi kuogelea, mimi mwanamke nisemeje?” akaniuliza.
Sikuwa na jibu. Nikaendelea kutikisa kichwa changu.
Sikujua ilikuwaje. Zena alinishika mkanda wa suruali yangu kwa nyuma kisha akanirusha baharini. Hadi leo nashindwa kujua alinirushaje.
Kabla ya kutumbukia baharini, nilijiambia ule ulikuwa ndio mwisho wangu.
Nilitanguliza mikono na kichwa, Nikazama chini kabisa.

kisha nikarudishwa tena juu. Wakati natokeza juu nilimuona Zena akijirusha baharini. Alichupa kama samaki. Akawahi kunishika kabla sijazama kwa mara ya pili.
Nilivamia mwili wake ili nijiokoe kwani pumzi zilikuwa zimeniishia.
“Usinivamie, tutazama sote. Tuliza akili yako” akaniambia huku akielea juu ya maji.
Niliendelea kumg’ang’ania.
“Usining’ang’anie, tutazama sote. Shika miguu yangu. Usishike mwili wangu!” Zena alinipigia kelele. Sasa nilikuwa kama hayawani nisiyejielewa.
Zena alipoona bado simsikilizi alinipiga ngumi ya shavu, nikamuachia na kuzama chini. Wakati niko ndani ya maji nikipelekwa chini, Zena alipiga mbizi akaniwekea mgongo wake kwenye kifua changu kisha akaibuka na mimi juu ya maji.
”Tulia kwenye mgongo wangu, ukifurukuta nakuacha. Nishike mabega yangu” akaniambia.
Nikafanya vile alivyotaka.
Zena akaanza kuogelea huku nikiwa kwenye mgongo wake. Yule msichana alikuwa hodari sana.
Aliweza kuogelea kwa mwendo mrefu akiwa na mimi bila kunidondosha na bila kuonesha kuchoka.
Ile boti iliyokuwa inazama tuliiacha mbali kabisa.
Zena aliendelea kuogelea tu kama vile alikuwa na mashine iliyokuwa inampa nguvu. Nikakumbuka maneno ya watu wanaosema kwamba majini huzaliwa baharini. Nikahisi kuwa hiyo ndio sababu akawa na uzoevu mkubwa wa kuogelea.
Hatimaye ile boti sikuiona tena. Sasa nikawa najiuliza tunaelekea wapi. Sikupata jibu. Jua lilikuwa linakuchwa kwa haraka upande wa magharibi na tayari lilionekana likitoa mionzi ya kimanjano iliyoashiria kuwa wakati wa magharibi ulikuwa unakaribia.
Mbele yangu nikaona kitu kimejitokeza. Baadaye niligundua kuwa tulikuwa tunatokea kwenye kisiwa. Kilikuwa bado kiko mbali na sisi. Kwanza nilianza kuona majani ya miti yaliounda shada kubwa la rangi ya kijani. Halafu nilianza kuona msitu mkubwa.
Kadiri tulivyokuwa tunakikaribia kisiwa hicho ndivyo nilivyoweza kukiona vizuri. Naam kilikuwa ni kisiwa. Sasa ardhi yake ilionekana waziwazi. Kilikuwa kisiwa kidogo kilichokuwa na msitu mkubwa wa miti.
Tulipofika maji madogo Zena aliniambia niondoke mgongoni kwake.
Sikumsikia vizuri, nilikuwa nimeendelea kumshikilia. Ile harufu ya udi wa mawaridi niliyokuwa nikisikia mgongoni mwake ilikuwa imenilewesha.
“Ondoka bwana, mwenzako nimechoka!” akaniambia kwa sauti ya ukali.
Nikajaribu kuishusha miguu yangu taratibu, taratibu, nikaona ninakanyaga mchanga lakini maji yalikuwa yakinifika kwenye kifua. Nikaanza kutembea kwa miguu nikiwa bado nimemshikilia Zena. Ilibidi nipate kitu cha kushika, vinginevyo maji yangeweza kunikupua.
Niliendelea kutembea hadi maji yaliponifikia kiunoni ndipo nilipomuacha Zena. Sasa tulikuwa tukitembea pamoja. Nguo zetu zilitota chapa. Maji ya chumvi yalikuwa yakitutiririka mwilini.
Tulifika ufukweni mwa kisiwa hicho. Fukwe yake ilikuwa nzuri yenye mchanga mweupe.
“Hapa ni wapi?” nikamuuliza Zena.
Zena aliyeonesha wazi kuwa alikuwa amechoka hakunijibu chochote, aliendelea kwenda hadi tukaingia kwenye ule msitu.
Zena alitafuta sehemu iliyokuwa juu akapanda na kujilaza chini.
“Oh leo nimechoka sana. Sijaogelea mwendo mrefu kama leo” Zena akajisemea peke yake akiwa amejilaza kichali chali.
Baibui alilokuwa amevaa lililoa maji na kuonya kama kioo. Nguo aliokuwa amevaa ndani nayo ilikuwa ikionya kwa sababu ya kutota maji. Ngozi nyeupe ya mwili wa Zena iliyokuwa na malaika marefu ilikuwa ikionekana wazi wazi.
Mimi nilikuwa nimeketi nikihema huku nikiyatembeza macho yangu kila upande wa kile kisiwa. Sikujua tulikuwa katika kisiwa gani na kilikuwa wapi.
Pia sikujua tungeondokaje katika kisiwa hicho ambacho hakikuonesha dalili yoyote ya kuishi watu. Nilikuwa nikijiambia kama kutakuwa na wanayama wakali wanaweza kutudhuru.
“Unangoja hizo nguo zako zikaukie mwilini mwako?” Zena akaniuliza.
“Sasa nizifanye nini?”
“Si uzivue?”
“Nizivue nikae uchi?”
“Kwani huna chupi?”
“Acha tu, zitakauka humu humu”
“Mimi nguo zangu ni nyepezi, zitakauka mara moja”
Niliyapuuza yale maneno ya Zena. Akili yangu ilikuwa kwingine. Nilikuwa nikijiuliza jinsi tutakavyoondoka kwenye kisiwa kile.
“Tutaondokaje hapa?” nikamuuliza Zena.
Kabla ya Zena kunijibu nikaona kitu kikitokeza kwenye miti mbele yetu. Nilishituka nilipogundua kuwa lilikuwa joka kubwa na refu. Lingeweza hata kutumeza mimi na Zena kwa wakati mmoja.
“Zena! Zena!” nikamuita Zena.
Zena akainua kichwa na kunitazama.
“Nini?’ akaniuliza.
“Angalia kule!” nikamwambia huku nikimuonesha lile joka kwa kidole.
Zena akapeleka macho yake na kuliona.
“Sijakwambia lakini sasa nakwambia, hiki kisiwa ni cha majini. Lile si joka kama unavyoliona ni jini limejigeuza joka. Wako wengi tu hapa”
Maneno yake yalizidi kunitisha.
“Sasa kwanini tumekuja hapa?” nikamuuliza kwa taharuki.
“Unawaogopa? Si majini wakubwa kama sisi, ni visubiani vya ovyo ovyo tu. Ngoja nitamfukuza”
Lile joka lilikuwa limetusogelea, likitaka kupandisha kichwa chake juu ya ile sehemu tuliyokuwa.
Zena akaanza kulifokea kwa lugha ya kikwao. Mimi nilisogea nyuma ya Zena kwa hofu. Zena akanyanyuka na kulifuata kabisa huku akiendelea kulifokea.
Lile joka lilibaki pale pale likinitazama mimi.
Zena akavua kiatu chake akakishika na kulipiga kichwani. Joka hilo likatoweka hapo hapo.
“Shika” alinipa kile kiatu. Akaniambia.
“Ukiona joka linakufuata lipige na hiki kiatu changu, litatokomea”
“Halitanimeza?” nikamuuliza huku nikipokea kile kiatu.
“Hapana”
“Kumbe hapa mahali ni pa hatari namna hii?”
“Wewe ndio umetaka tufike hapa”
“Nimetaka mimi?”
“Ndio”
“Nilikwambia kuwa tuje hapa?”
“Kwani wewe siku zote unajua mimi nataka nini kwako?”
Hapo nikagwaya.
Zena akaendelea kuniuliza.
“Ulifuata nini Pemba?”
Sikuwa na la kumjibu.
“Sasa niambie utanioa niwe mke wako au bado hutaki?”
“Nikishakuoa tutakwenda kuishi wapi?’ nikamuuliza.
“Kule kule unakoishi wewe”
“Turudi kule kwanza ndio tupange mipango ya ndoa, si hapa”
“Nataka tukirudi niwe tayari ni mke wako”
“Kwani tutakwenda kuoana wapi?” nikamuuliza Zena.
“Mtu huolewa kwao na mimi utakwenda kunioa kwetu”
“Kwenu wapi?”
“Kwetu hukujui?”
“Sikujui”
“Kwetu ni ujinini”
“Yaani tutakwenda kuoana kwenu ujinini?”
“Ndio”
“Sasa ungeacha kwanza nirudi nyumbani nikajiandae. Hatuwezi kuoana ghafla”
“Wewe umekuwa mkaidi mara nyingi. Siwezi kukupa nafasi hiyo. Madhumuni yangu ya kukuleta hapa ni kuwa twende tukaoane. Muda umeshafika”
Nikanyamaza kimya.
Zena alikuwa akiendelea kuniambia.
“Ile boti niliizamisha mimi kusudi ili nikulete hapa. Ninajua tukiwa hapa hutakuwa na ujanja wowote”
Ndipo nilipogundua kuwa Zena alikuwa amenizunguka! Kumbe ile boti aliizamisha yeye ili anipate mimi…
Kufika Kwetu pale kisiwani nilidhani nilikuwa nimesalimika na kifo, kumbe nilikuwa ninasubiriwa na matatizo mengine.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kama alivyoniambia Zena, ni kweli pale kisiwani nisingekuwa na ujanja wowote zaidi ya kusalimu amri.
Lakini akili yangu bado ilikuwa haikubaliani na mawazo ya Zena. Kumuoa jini lilikuwa jambo ambalo sikuwa tayari nalo.
“Sikiliza Zena, naona sasa unatumia jazba ambayo si nzuri” nikamwambia Zena. Lakini hataka kabla sijamaliza sentensi yangu au alinikatiza.
“Kumbe ulitaka nifanye nini?”
Sasa sauti yake ilikuwa ya hamaki.
“Nilitaka unisikilize ninachokwambia”
“Kipi?”
“Turudi Tanga ili nijiandae kwa jambo hilo, kwanini wewe unachukulia nguvu?”
“Nachukulia nguvu kwa sababu nimeshaakuona kuwa huko tayari kunioa”
“Niko tayari, nani kakwambia kama siko tayari. Ninachotaka mimi unipe muda tu wa kujiandaa”
“Amour usinidanganye, huko tayari. Kama ungekuwa tayari usingekwenda kumuoa yule mwanamke wako niliyemfukuza pale nyumbani”
“Yule nilimuoa kwa sababu ndugu zangu walimtaka yeye lakini sasa nitawaambia kuwa nataka kuoana na wewe”
“Usiniambie habari ya ndugu zako, nyote nyinyi ni kitu kimoja”
“Mbona hutaki kunisikiliza Zena!”
“Sitakusikiliza. Wewe ni muongo ingawa sipendi kukuita hivyo. Wewe hunitaki mimi wakati mimi nimekusaidia sana. Kwanza niambie ulifuata nini Pemba?”
“Si nimekwambia kwamba nilikwenda kutembea”
“Usinidanganye. Usinifanye mimi sina akili. Wewe ulikwenda Pe,mba baada ya kuambiwa kuna mganga ambaye ataweza kupambana na mimi”
Nikajikuta natikisa kichwa changu kwa fadhaa.
“Si kweli” nikamwambia lakini uso wangu ulikuwa umetahayari.
“Unaona aibu mwenyewe kutokana na hila zako, Unadhani kuna mganga ataniweza mimi?”
Nikabaki kimya. La kusema nilikuwa sina.
“Sasa usinipotezee muda wangu, nataka jibu lako. Tutakwenda ujinini kuoana au hatutakwenda?” Zena akaniuliza.
Nilikuwa nimeinamisha kichwa changu nikiwaza. Sikuwa na jibu la kumpa, nikabaki kutikisa kichwa kuashiria kutokukubaliana naye.
“Amour nakuuliza tena, tutakwenda ujinini tukaoane au hatutakwenda?”
Niliendelea kutikisa kichwa.
“Una maana huko tayari siyo?”
Sikumjibu.
“Sasa mimi nakwenda zangu, nakuacha hapa hapa. Hutaniona tena”
Nikainua uso wangu haraka ili nimwambie asiniache pale lakini Zena alitoweka ghafla kama upepo. Kama alivyoniambia sitamuona tena na kweli sikumuona tena!
Nikatazama huku na huku, Zena hakuweko. Nikabaki peke yangu kwenye kisiwa kile cha majoka!

Kile kiatu chake alichokivua na kulipiga lile joka nikabaki nacho. Mwenyewe amekwenda na kiatu kimoja.
Nilipata hofu kweli kweli.
Jua lilikuwa limeshakuchwa na kiza kilikuwa kinaingia. Nikajiuliza “nitafanyaje Amour?”
Zena alikuwa ameshaniacha peke yangu. Nikawa nahisabu dakika zangu za kufa au kuliwa na majoka.
Nikaondoka mahali pale nilipokuwa nakwenda kupanda juu ya mti nikiwa na kile kiatu. Nilikaa kwenye tawi moja nikawa naitazama bahari. Hakukuwa na mtumbwi wala ngarawa iliyokuwa ikipita. Bahari ilikuwa nyeupe.
Kusema kweli nilijuta kufunga safari ile ya kwenda Pemba kufuata mganga. Na kama niliamua kwenda ningekwenda na ndugu yangu na si peke yangu kama nilivyofanya.
Nilianza kusikia baridi mwilini, sikujua itakapofika usiku ingekuwaje.
Nilitamani Zena anionee huruma aje anichukue. Lakini mawazo yangu yalikuwa sawa na dua la kuku. Hakuna aliyelisikia.
Wakati nimekaa kwenye tawi nikiendelea kuwaza nikasikia majani yakichakachika juu ya ule mti kama vile kulikuwa na kitu kinatambaa.
Nikainua uso wangu juu kutazama kulikuwa na nini.
Nikashituka. Niliona kichwa cha joka kikiwa karibu yangu kabisa. Kumbe katika ule mti niliokuwa nimeupanda kulikuwa na joka ambalo sikuliona.
Kile kiatu cha Zena nilikuwa nacho mkononi, nikakipiga kile kichwa. Nikadhani lile joka lingeniangukia lakini pale pale lilitoweka. Sikuliona tena.
Nikagundua kuwa licha ya Zena kunikimbia alikuwa ameniachia silaha ya maana sana.
Nikaangaza angaza juu ya ule mti kuona kama kulikuwa na joka jingine. Sikuona joka.
Hata hivyo sikuamini. Kila wakati nilikuwa natazama tena.
Kiza kiliendelea kushamiri na baridi ilizidi kuwa kali lakini sikuwa na la kufanya. Nilibaki kutetemeka tu.
Nilijiambia kama nitakufa pale kisiwani maiti yangu haitapatikana. Mama yangu na kaka yangu hawatajua nimepotelea wapi na hawatajua kuwa mwenzao ni marehemu.
Eti wakati nawaza vile nikapitiwa na usingizi ghafla. Nikalala pale pale juu ya mti bila kujitambua.
Nikaota nimelala chumbani kwangu, mara nikaona mwanamke ametokea kwenye dirisha langu lakini alikuwa kama kivuli. Sikuweza kumuona sura yake. Akaniambia.
“Ni mpaka uirithi pete ya Sulaiman Dauud na hutairithi mpaka uishuhudie damu ya kaka yako ikimwagika”
Hapo hapo nikazinduka. Ile ndoto haikuwa ngeni kwangu nakumbuka katika kipindi cha mwaka mmoja nilishaiota zaidi ya mara tatu. Lakini sikujua maana yake.
Wakati nazinduka niliona mawingu yakianza kun’gaa. Kumbe kulikuwa kunanaanza kupambazuka. Nikatambua kuwa nililala usiku kucha pale juu ya mti ingawa niliona nililala kwa muda mfupi.
Wakati naangaza macho baharini nikaona boti moja kubwa inakuja kwa kasi. Nikashukuru ingawa sikujua ilikuwa boti ya kina nani.
Boti ile ilikuja hadi maji madogo ikatia nanga. Nikaona watu watano wanashuka na kutembea kuelekea ufukweni. Walikuwa wamesega suruali zao ili zisitote.
Mmoja wa watu hao alikuwa amebeba tenga kubwa kichwani. Nikasikia sauti kama ya mlio wa mbuzi.
Watu hao walipofika ufukweni walitembea hadi kwenye ule msitu. Yule aliyebeba tenga akalitua chini. Ule mlio wa mbuzi uliendelea kusikika.
Nikaona mbuzi mweusi anatolewa kwenye tenga hilo. Sikuweza kuona vizuri kilichokuwa kinaendelea isipokuwa niliona kama walikuwa wanamchinja yule mbuzi na kumuacha pale chini.
Nikapata hisia kwamba watu hao walikuwa wanafanya kafara lakini ghafla nikaona wanaingia katika ule msitu.
Baada ya muda wa kama nusu saa hivi wakaanza kutoka mmoja mmoja lakini kila aliyetoka alikuwa amebeba pembe nne za ndovu.
Walikwenda nazo kwenye ile boti wakazipakia kisha wakarudia zingine.
Walirudia mara kumi, zilikuwa pembe nyingi sana. Ile mara ya kumi waliobeba pembe walikuwa watu wawili. Nikahisi walikuwa wamemaliza pembe zao na kwamba walikuwa wanakwenda zao.
Nikadhania tu kuwa wale watu walikuwa wafanya magendo na walikuwa wakificha pembe zao katika kisiwa kile.
Nikaona nisiipoteze ile nafasi ingawa sikujua watu wale walikuwa wanaelekea wapi.
Nikashuka haraka kwenye ule mti na kuwakimbilia.
“Jamani naomba mnichukue!” nikawa nawapigia kelele.
Watu hao walipoona ninawafuata huku nikiwaomba msaada wakasimama na kunisubiri.
Nilipowafikia, mtu mmoja mfupi aliyekuwa amevaa pama jeusi akaniuliza.
“Wewe nani na umetokea wapi?”
“Mimi ni mwananchi niliyekuwa natokea Pemba nikielekea Dar kwa boti inayokwenda kasi ambayo ilizama jana” nikamwambia.
“Boti ilizama jana mbona wewe upo hadi leo”
“Nilinusurika baada ya kuogelea….”
Kabla sijamaliza kile nilichotaka kumueleza akanikatiza.
“Ulifuata nini kwenye kisiwa hiki?”
“Niliogelea hadi nikafika hapa”
“Tangu jana ulikuwa unafanya nini hapa?”
“Nilikuwa nimekaa tu nikisubiri msaada”
“Wewe ni muongo sana!”
“Hapana. Ninachokieleza ni ukweli mtupu”
“Wewe ni mpelelezi siyo, umekuja kutupeleleza sisi?”
“Hapana, hapana. Mimi siwajui, nimewaona tu hapa. Ninachoomba ni msaada wenu tu”
“Haya twende tukaingie kwenye boti”
“Asante bwana, nakushukuru sana kwa maana nilikuwa sijui ningefikaje Tanga”
Nilifuatana na wale watu hadi kwenye boti yao nikajipakia. Yule mtu aliyekuwa akinihoji ambaye alionekana kama mwenye mali alikuwa akiamrisha kila kitu ndani ya ile boti.
Safari ikaanza. Nikadhani kwamba nilikuwa nimenusurika. Sikujua tulikuwa tunaelekea wapi na jinsi nilivyowaona watu wenyewe ni wakali nilishindwa kuwauliza.
Nilikuwa nimeshaamua popote watakaponifikisha patatosha. Kama watanirudisha Pemba au kama watakwenda Unguja au Dar itakuwa sawa.
Boti iliendelea na safari kwa kasi. Kitu kilichonishitua ni kwamba baada ya kukiacha kile kisiwa, yule mtu aliyekuwa amevaa pama jeusi alikwenda kukaa peke yake akatoa bangi na kuanza kuvuta.
Moshi wa bangi ulienea kwenye boti ukawa unaniumiza kichwa lakini yule mtu hakujali kabisa. Alikuwa akiendelea kuvuta tu.
Baada ya kwenda mwendo wa karibu kilometa thelathini tukaona boti nyingine inatufuata. Wale watu walipoiona ile boti walishituka.
Yule mtu aliyevaa pama akakitupa kipisi cha bangi baharini kisha akanitazama na kuniambia.
“Polisi wenzako wanatufuata, mimi nilishajua kuwa wewe ni mpelelezi!”
“Polisi gani?” nikamuuliza.
CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Utawaona sasa hivi”
Mazungumzo ya polisi yakaanza ndani ya boti huku wale watu wakinishutumu mimi kuwa ni mpelelezi niliyekuwa nimetumwa katika kile kisiwa kuwachunguza.
Kumbe ile boti iliyokuwa inatufuata ilikuwa boti ya polisi wanamaji iliyokuwa kwenye doria.
Upande mmoja wa moyo wangu nilipata hofu lakini kwa upande mwingine nilipata matumaini. Nilipata hofu kutokana na zile shutuma nilizokuwa ninazipata kutoka kwa wale watu kuwa mimi ni mpelelezi. Na nilipata matumaini kujua kuwa kulikuwa na polisi wanatufuata.
Sikuwa na hofu na polisi hao kwa sababu sikuhusika na wafanya magendo hao ambao hata sikujua walikuwa wanaelekea wapi.
Kadiri ile boti ilivyokuwa inatukaribia wale watu walikuwa wakihaha huku wakitukana.
Boti ya polisi ilipotufikia polisi wanne waliingia kwenye ile boti. Polisi mmoja alikuwa ameshika bunduki.
“Mnakwenda wapi?” Polisi aliyeshika bunduki akatuuliza.
Polisi hao hawakupata jibu. Jamaa wote walikuwa kimya.
Katika kukagua kagua ndani ya ile boti, polisi hao wakaziona zile pembe za tembo.
“Kuna meno ya tembo mengi sana wanayasafirisha!” Polisi mmoja akawapigia kelele polisi wengine waliokuwa kwenye boti ya pili.
Yule mtu aliyevaa pama aliingia kwenye kijichumba kilichokuwa ndani ya boti hiyo. Muda ule ule alitoka akiwa ameshika kitu kama chupa kubwa iliyokuwa na utambi uliokuwa ikiwaka moto, akairusha ile chupa kuelekea kwenye boti ya polisi. Ile chupa ilipotua chini ililipuaka kama bomu.
Kitendo kile kilinishitua. Mara moja ile boti ya polisi ililipuka moto. Wale polisi walioingia kwenye boti niliyokuwemo walikuwa wameduwaa. Hapo hapo wakavamiwa na wale watu, wakapigwa na kufungwa kamba. Yule polisi aliyekuwa na bunduki alinyanganywa bunduki yake.
Jambo lililonishitua zaidi ni kuwa hata mimi nilikamatwa nikafungwa pamoja na polisi hao.
“Tutakwenda kuwatosa huko mbele ya safari” aliyekuwa amevaa pama akatuambia.
“Lakini mimi ninahusikaje, mimi niliwaomba msaada tu kwanini mnataka kwenda kunitosa?” nikawalalamikia.
“Wewe ndio mpelelezi uliyekuwa ukitoa taarifa kwa wenzako. Pale nilipokuwa nakupakia nilishakupangia kwenda kukutosa” Mwenye pama akaniambia.
“Balaa gani hili jamani linalonikuta. Jana nilikaribia kufa, leo tena balaa jingine linaningoja. Nimekosa nini jamani!” nikalalamika peke yangu.
Wakati huo ile boti ya polisi tulishaiacha mbali ikiendelea kuwaka.
Mpaka jua linafika utosini ikiashiria ilikuwa saa sita mchana, boti ya watu hao ambao sasa niliwahisi walikuwa majambazi ilikuwa ikiendelea kukata maji.
Nilikuwa nimeshafuta mawazo kwamba tulikuwa tunaelekea katika miji iliyokuwa karibu kama Pemba au Unguja. Nilihisi kwamba tulikuwa tunaelekea mahali kwingine kusikojulikana.
Hofu ya kuuawa ilikuwa imenitawala. Wakati wote moyo wangu ulikuwa ukienda mbio. Sikujua kwamba tungeuawa au tungetoswa baharini saa ngapi.
Mara nikamuona yule mtu aliyekuwa amevaa pama akitoka kwenye kile chumba kilichokuwamo ndani ya boti, akawambia wenzake.
“Eneo hili lina papa wengi, tuwatose hapa hapa”
Kauli yake ile ilinishitua. Ilikuwa kama nyundo ya moto iliyopigwa kwenye moyo wangu.
Mapama aliposema hivyo aliwaagiza watu watatu wamuinue polisi mmoja na kumtosa. Polisi huyo alilalamika kuomba asitoswe lakini hakukuwa na aliyekuwa akimsikiza. Jamaa hao walimbeba na kumtosa baharini akiwa amefungwa kamba miguu na mikono.
Mara moja tukaona damu kwenye eneo lile la bahari. Kipande kimoja cha mwili wa polisi huyo kiliibuka juu na kwenda na maji. Bila shaka kipande kingine kilikuwa kimeshamezwa na papa.
Hapo hapo tukamuona papa upanga akibuka kutoka chini ya bahari na kuking’ata kipande kingine cha ule mwili na kuzama nacho baharini.
Tayari jamaa hao walikuwa wameshambeba polisi wa pili ambaye kama mwenzake alikuwa akilalamika bila kusikilizwa, naye akatoswa.
Polisi wa tatu naye akatoswa. Nikabaki mimi na polisi mmoja. Nilikuwa nikiomba toba kimoyomoyo ili nipate msamaha huko ahera ninakokwenda.
Machozi yalikuwa yametosa kifua changu na yalikuwa yakiendelea kunitoka hasa nilivyoona vipande vya miili ya wale polisi ilivyokuwa ikidakwa na papa.
Wale jamaa wakatufuata tena.
Sikujua ilikuwa zamu ya nani, mimi au yule polisi?
Jibu nililipata baada ya nusu dakika. Watu hao wakamshika mwenzangu. Bila shaka mimi waliniweka mwisho. Polisi huyo alibebwa juu juu. Ingawa alikuwa akipiga kelele, hakukuwa na aliyemjali. Kiasi cha kufumba na kufumbua tu akawa ametoswa baharini. Kwa vile alikuwa mnene na mzito kuliko wenzake waliokuwa wametoswa, alisababisha kishindo kukubwa, maji ya bahari yakaruka na kuingia kwenye boti!
Wakati wote nilikuwa na matumaini kuwa wangewatosa wale polisi kwa kuamini kuwa mimi sikuwa mwenzao na ndio maana waliniacha.
Lakini matumaini yangu yaliyayuka mara tu nilipowaona wale watu wakinifuata mimi baada ya kumtosa yule polisi wa mwisho,
Nilipoona wananishika nikawambia.
“Jamani, jamani mimi nina kosa gani. Kuwaomba msaada ndio kosa, mnataka mniue”
Hawakunijibu na hawakuonesha kama walihitaji kunijibu, Walinibeba kama walivyowabeba wenzangu. Vile ambavyo mwili wangu haukuwa mzito walinichota kama takataka. Wakanipeleka kwenye ukingo wa boti.
Kufika hapo waliniinua juu wakahesabu moja...mbili…
Kabla hawajafika tatu, kuliibuka kitu kilichotokea baharini. Kiliibuka kwa nguvu na kwa kishindo huku kikitoa mlio uliofanana na mlio wa fataki iliyorushwa.
Yale maji yaliyorushwa juu na kitu hicho yalitutosa wote. Ghafla kitu hicho kikatuvamia. Mimi niliachiwa nikaangukia ndani ya boti. Wale watu pia walianguka na kulaliwa na kitu hicho kizito kilichotua ndani ya boti.
Nilikuwa nimefungwa kamba mikono na miguu. Nilipoanguka sikuweza kusimama ila niliweza kujigeuza ili nikione kitu hicho kilichoibuka kutoka baharini na kuvamia ndani ya boti ile.
Nilishindwa kuamini macho yangu! Lilikuwa dude kubwa kama joka lililokuwa na mikono yenye vidole vyenye kucha ndefu. Urefu wake ulikuwa kama guzo la umeme. Lilipokuwa ndani ya ile boti lilikuwa limejikunja. Mwili wake ulikuwa na magamba makubwa kama ya samaki.
Kwa kutumia kucha zake lilimvamia mtu mmoja na kuruka naye juu kisha likajitosa baharini likiwa na mtu huyo.
Sote tulikuwa tumetaharuki na hatukujua ni jambo gani lilitaka kutokea. Wakati wale watu wanajiinua pale chini, joka hilo likaibuka tena likiwa halina mtu. Likavamia mtu mwingine na kuruka naye kisha likajitosa baharini.
Watu hao wakawa wanapigana vikumbo ndani ya boti kutafuta pa kujificha. Kutahamaki joka hilo likatokea tena, likamnyakua mtu mwingine na kuzama naye chini ya bahari. Watu wote wakamalizwa nikabaki mimi na Mapama
Mapama alikuwa akihangaika akijua kwamba joka hilo litaibuka tena na kumchukua yeye.lakini dakika zikapita hatukuliona. Kwa sababu ya hofu na kujiona amebaki peke yake mtu huyo alikuja kunifungua zile kamba.
“Njoo huku” akiniambia akitangulia kuingia katika kile kijichumba kilichokuwa ndani ya ile boti.
Nikainuka na kumfuata. Mikono yangu ilikuwa imekufa ganzi kutoka na kufungwa kamba kwa muda mrefu. Nikawa ninainyooshanyoosha.
Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kioo cha kutazamia mbele. Pia kulikuwa na sukani na mitambo ya boti.
“Samahani bwana, naona tumebaki sisi wawili tu. Sijui lile lilikuwa joka gani na limetokea wapi?” Mapama akaniambia kwa hofu.

ITAENDELEA

Post a Comment

0 Comments