Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

Simulizi: Mwanamke jini sehemu ya nane (08)



 “Na wewe ulihakikisha ulipopewa hicho kibiriti kucha zilikuwemo?”

“Ndio. Mgosingwa aliponipa hicho kibiriti alinifungulia akanionesha. Kucha zilikuwemo”
“Mganga alikwambia hizo kucha zimnmekwenda wapi?’
“Aliniambia huyo jini ndiye anayeniharibia mambo yangu”
“Kwa hiyo huyo jini ndiye aliyezipoteza?’
“Itakuwa ni yeye”
Kaka alifikiri kisha akaniuliza.
“Hizo kucha zilikuwa ndogo sana?”
“Ndio zilikuwa ndogo”
“Inawezekana zilichomoka moja moja kwenye kibiriti bila wewe kujua. Siamini kwamba huyo jini amezichukua yeye”
“Unafikiria hivyo?’
“Acha wasiwasi. Kwanza huyo jini kuna muda mrefu hajakutokea. Mimi nafikiri ameshakata tamaa”
“Sawa kaka, nimekuelewa”
Sikuwa na uhakika kwamba kaka alikuwa akiniambia ukweli kutoka ndani ya moyo wake au alikuwa akinituliza tu.
Baada ya mazungumzo yetu mafupi nikamuaga na kuondoka.
Baada ya wiki moja kaka yangu aliniita na kunishauri nioe.
“Umeshakuwa mkubwa sasa, unatakiwa uwe na mke wako” aliniambia.
“Ni kweli kaka. Haya mambo ya huyu jini aliyekuwa akiniandama ndio yaliyonizubaisha”
“Mimi naamini akikuona una mke hatakufuata tena. Atakwenda kutafuta mtu mwingine. Kama atakubali, awe mke mwenza” Kaka akanichekesha.
Tukacheka sote.
“Nadhani hawezi kukubali kuwa mke mwenza” nikamwambia.
“Ndio atakuacha sasa”
“Ni kweli kaka, ni bora niwe na mke”
“Sasa unaye msichana unayemfikiria kwamba anafaa kuwa mke wako ili tukakuposee”
“Nitakujibu”
“Lini?”
“Nipe siku mbili tu”
“Sawa”
Lile wazo la kuoa alilonipa kaka nilikwenda kulitafakari nyumbani na kuona lilikuwa wazo la busara sana. Mbali ya kwamba nilishafikia umriwa kuwa na mke pia niliona nitakuwa na mwenzangu wa kunifariji kutokana na matatizo yaliyokuwa yananikabili.
Pia nilizingatia kauli ya kaka kwamba nikioa, huenda yule jini akaacha kuniandama.
Kulikuwa na msichana mmoja aliyekuwa akiishi mtaa wa pili na ule niliokuwa nikiishi mimi. Alikuwa akiitwa Salma.
Salama nilikuwa nikimfahamu tangu alipokuwa anasoma shule ya sekondari ya Usagara. Alipomaliza kidato cha nne niliwahi kumtamkia kuwa ninampenda.
Akaniuliza. “Unanipenda kweli au unanidanganya?’
“Ninakupenda kweli” nikamjibu.
“Sasa kama unanipenda kweli, waone wazazi wangu. Mimi nimeshakukubalia”
Kwa vile muda ule sikuwa na mawazo ya kuoa, sikumpatiliza tena ila kila tulipoonana nilimtania kwa kumwambia, “Nitakuja kwa wazazi wako”
Na yeye hucheka na kunijibu. “Njoo tu, njia nyeupe”
Alikuwa mzuri mwenye heshima na alikuwa na sifa zote zinazostahili kuwa mke wangu.
Yeye ndiye niliyemfikiria.
Hata hivyo wakati ule wazazi wake walikuwa wameshahama katika mtaa waliokuwa wakiishi. Mwenyewe aliniambia walihamia Chumbageni.
Kwa wakati ule Salama alikuwa akifanya kazi Shirika la Posta. Nikapanga nimfuate nizungumze naye ili nimueleze nia yangu ya kupeleka posa yangu kwa wazazi wake.
Siku iliyofuata nikaenda kazini. Saa nne wakati wa kwenda kunywa chai nikaenda posta. Nikamkuta.
Nilisubiri watu wawili aliokuwa akiwahudumia walipoondoka nikamsalimia.
“Hujambo mrembo?”
“Sijambo, sijui wewe”
“Mimi ni mzima tu kama unavyoniona, hivi kule Chumbageni unaishi mtaa gani?” nikamuuliza.
Salama akanielekeza mtaa anaoishi. Kwa vile na mimi nilikuwa mwenyeji wa mitaa ya Chumbageni niliifahamu mpaka nyumba waliyokuwa wanaishi.
“Si ile inayotazamana na Cumbageni Guest House?” nikamuuliza.
“Ndiyo hiyo hiyo”
“Natarajia kutuma mshenga kwenu” nikamdokeza.
Salama hakunijibu kitu. Nikaridhika. Kuwa kimya inachukuliwa na masheikh wa kiislamu kuwa ni ishara ya kukubali, kwa vile suala hilo tulishalizungumza.
Nilipotoka kazini jioni nilikwenda kwa kaka nikamueleza kuhusu msichana huyo.
“Umeshazungumza naye” akaniuliza.
“Niliwahi kuzungumza naye siku nyingi lakini ilikuwa kama mzaha, leo ndio nilimfuta kazini kwake nikamwambia kuwa nitatuma mshenga kwao akanyamaza. Nimechukulia ishara kwamba amekubali”
“Sasa tujaribu kupeleka ujumbe kwao?”
“Ndio hivyo”

“Kwa hiyo utaandika barua utaniletea hapa, halafu mimi nitatafuta mzee mmoja niende naye. Unasema anaishi wapi?’
“Anaishi chumbageni lakini usiku tutakwenda kama tunapita njia ili nikuoneshe nyumba yao”
“Sawa, utanifuata saa ngapi?’
“Saa mbili usiku”
“Nitakusubiri”
Baada ya mazungumzo yetu na kaka nikarudi nyumbani. Saa mbili usiku nikamfuata tena na pikipiki yangu. Nilimpakia na kwenda kumuonesha ile nyumba aliyonielekeza Salama. Nilipata uhakika kwamba sikuikosea kwani tulimkuta baba yake ambaye namfahamu, ameketi barazani kwenye kiti cha uvivu akivuta mtemba wake.
Tukapita na pikipiki yetu.
Wakati tunarudi kaka alinaimabia.
“Kama nyumba ni ile nimeshaiona”
“Na yule mtu uliyemuona ameketi barazani kwenye kiti cha uvivu ni baba yake”
“Kumbe baba yake ni yule mzee?”
“Ndio yule”
“Basi tutamuona hapo kesho”
Nikamrudisha kaka nyumbani kwake, akanisisitizia tu nisisahau kuandika barua ya posa.
Nilipofika nyumbani niliiandika barua hiyo usiku ule ule nikaitia ndani ya bahasha. Kwa kawaida barua za posa kama zile huwekwa kitu kidogo. Nikatia shilingi elfu hamsini.
Asubuhi wakati naenda kazini nikaipeleka ile barua kwa kaka. Kaka aliifungua kwa vile sikuwa nimeifunga kabisa. Aliisoma kisha akaniambia.
“Umeiandika vizuri”
“Nimeweka na shilingi elfu hamsini, sijui zinatosha”
“Zinatosha, hizi huwekwa kama ada tu”
“Sawa, sasa mimi naenda kazini utatafuta mtu wa kwenda naye”
“Barua yako itafika leo leo”
Nikaenda zangu kazini.
Saa nne nikaenda posta kwa Salama. Baada ya kusalimiana naye nilimwambia.
“Ujumbe wangu utaupata leo”
Salama akatabasamu.
“Naungojea” akaniambia. Nilikuwa na hakika kwamba alijua ni mzaha wangu.
Jioni nilipotoka kazini nilikwenda kwa kaka. Akaniambia.
“Barua yako imefika”
“Umeshaipeleka?” nikamuuliza kwa tashiwishi.
“Tuliipeleka mchana. Mzee ameniambia nifuatie majibu kesho”
“Hakukuwa na maswali yoyote aliyokuuliza?”
“Kuuliza ni lazima. Aliniuliza ile posa ilikuwa ni ya nani wangu. Nikamjibu ni ya mdogo wangu. Akaniuliza anafanya kazi wapi nikamueleza. Akataka pia kujua unaishi wapi nikamueleza”
“Yule mzee hatufahamiani isipokuwa nafahamiana na binti yake”
“Aliuliza pia kama wewe ulishamueleza binti yake kuhusu nia yako”
“Ukamjibu nini?”
“Nilimwambia mlishazungumza na mlikubaliana. Akaniambia kwamba atazungumza naye na kwamba nifuatie majibu kesho”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa hiyo mtaenda tena hapo kesho?”
“Tutakwenda”
“Sawa kaka”
Jioni yake niliporudi kazini nikapitia kwa kaka kupata majibu.
Akaniambia. “Kazi imekamilika”
“Kivipi?” nikamuuliza.
“Posa yetu imekubaliwa. Mzee ameniambia wanataka mahari ya shilingi laki tano”
“Mahari yake ni shilingi laki tano?” nikamuuliza kwa mkazo.
“Inaelekea yule mzee msomi. Amesemi yeye hana mambo ya Kiswahili. Hakutaka kututajia gharama kubwa. Mimi naona laki tano si nyingi”
“Sawa”
“Mimi mchango wangu nitakusaidia shilingi laki moja”
“Mimi mwenyewe nitatoa laki nne”
“Lini zitapatikana hizo laki nne”
“Hata kesho zinaweza kupatikana”
“Utaniletea asubuhi?”
“Nitakuletea jioni, wewe utazipeleka kesho kutwa”
“Sasa tupange harusi, sipendi uchumba wenu uchukue muda mrefu sana”
“Tukishalipa hizo pesa tutakaa na mama tupange harusi itakavyokuwa”
“Sawa jitahidi upate jiko lako”
“Nitajitahidi kaka”
Nikaagana na kaka na kwenda nyumbani kwa mama. Nilimueleza ile habari. Akaniambia ameshaelezwa na mwanawe, yaani kaka yangu.
“Ni jambo zuri” akasema.
“Kesho kutwa tutakuja kufanya kikao cha harusi hapa kwako”
“Kwani mambo tayari?’
“kaka atapeleka mahari kesho kutwa”
“Hizo shilingi laki tano?”
“Ndio”
“Umeshampa?”
“Nimemwambia nitampa kesho”
“Yeye atakusaidia shilingi ngapi?’
“Ameniambia atanitolea shilingi laki moja, mimi mwenyewe nitatoa laki nne”
“Kwa hiyo mnasubiri mmpeleke mahari ndio tufanye kikao”
“Ndiyo”
“Mimi nawaunga mkono. Nilitaka sana wewe uwe na mke. Hilo wazo nililitoa mimi”
“Lilikuwa wazo zuri na natumaini nikiwa na mke matatizo yangu yatapungua’
“Utakuwa vizuri mwanangu”
“Sawa mama, basi mimi narudi nyumbani”
Nikaagana na mama na kuondoka.

Siku iliyofuata nilikwenda benki, nikatoa shilingi laki tano kutoka katika akaunti yangu. Jioni nilipotoka kazini nikampelekea kaka shilingi laki nne kama tulivyokubaliana.
Nilipotoka kwa kaka nikaenda kwa mama. Nikamueleza kuwa nimeshampa kaka shilingi laki nne.
Mama akafurahi.
“Nawatakia heri na mafanikio” akaniambia na kuniuliza.
“Zitapelekwa kesho?”
“Kaka ameniambia atazipeleka kesho na kesho hiyo hiyo tutakuwa na kikao hapa kwako”
“Saa ngapi?’
“Nadhani itakuwa usiku”
“Sawa wanangu, nawasubiri”
Siku iliyofuata ilikuwa jumapili, sikwenda kazini. Nilibaki nyumbani kufanya usafi na kufua nguo zangu zilizochafuka.
Saa saba ndipo nilipotoka. Nilikwenda kwenye mkahawa mmoja kula chakula. Nilipotoka hapo nikaenda kwa kaka. Aliniambia ndio kwanza amerudi kutoka chumbageni.
“Mzee ameniambia baada ya kupata mahari anachosubiri ni kutajiwa siku ya harusi” kaka akaniambia.
“Sasa tujiandae, tupeleke siku”
“Kwani tutakutana saa ngapi kwa mama?’
“Nimemwambia tutakutana usiku”
“Usiku saa ngapi?’
“Tukutane kuanzia saa moja”
“Sawa”
“Naona mambo yanakwenda vizuri”
“Yanakwenda vizuri sana”
Saa mbili usiku tulikutna nyumbani kwa mama. Mimi nilifika mapema zaidi kabla ya kaka. Ilibidi niwahi kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa na shughuli, ilikuwa vyema mwenzangu anikute pale nyumbani na sio nimkute yeye.
Kaka alipofika tukaanza mazungumzo. Mazungumzo yetu yalikuwa marefu na yaliishia saa nne usiku. Tulipanga kila
kitu. Kwa vile mimi nilikuwa na akiba yangu ambayo nilipanga niitumie kwa ajili ya harusi yangu, tulikubaliana kwamba harusi ifanyike haraka, baada ya wiki mbili.
“Hizi wiki mbili ndio za kufanya maandalizi, mnaonaje zinatosha au tuongeze siku?” kaka alituuliza wakati tunaendelea na kikao chetu.
Nikamtazama mama, nikaona mama naye ananitazama mimi.
“Mimi naona zinatosha, hakuna haja ya kuongeza siku zaidi” nikasema.
“Mama unasemaje?” Kaka akamuuliza mama aliyekuwa kimya.
“Mimi sina usemi, nawasikiliza nyinyi”
“Na wewe unaafiki kwamba wiki mbili zinatosha kwa maandalizi?” Kaka akamuuliza.
“Kama Amour mwenyewe amesema zinatosha na mimi nasema hivyo hivyo zinatosha”
“Sawa. Naona tumeafikiana kwa hilo. Sasa tupange siku yenyewe ya kufunga ndoa” kaka akatuambia.
“Tuweke siku ya ijumaa baada ya mshuko. Muda huo ni mzursana kufunga ndoa” nikasema.
“Mimi pia naafikiana na muda huo. Kwa hiyo hatuhitaji kwenda kutazamia siku wala saa?’
“Enzi zetu tulikuwa tunatazamia siku lakini siku hizi mambo yamebadilika” mama akasema.
“Mama unajua kutazamia siku ni kuleta ushirikina. Siku zote zinafaa kuoa na saa zote mtu unaweza kuoa. Mtume ametuambia saa nzuri ni baada ya mshuko wa ijumaa” nikamwambia mama.
“Swadakta Amour, umesema sawa. Umekuwa answar sunna” Kaka akanikubalia.
“Si lazima niwe answaar sunna. Hivi ndivyo tulivyofundishwa na mtume wetu. Kufanya vinginevyo ni ushirikina”
“Wanasema kwamba usipotazamia siku unaweza kuoa siku mbaya na maisha yako ya ndoa yakawa ya mikosi na vifo” kaka akayuambia.
“Uongo mtupu. Ni imani tu za watu” nikasema.
“Sawa. Tumeshakubaliana kwamba ndoa itafanyika baada ya mshuko wa ijumaa. Kutahitajika tende kidogo na kahawa au siyo”
“Ndiyo”
“Ndoa itafanyika wapi?”
“Msikiti wa ijumaa”
“Msikiti ule ni mkubwa, siku za ijumaa unakuwa na watu wengi, haluwa haitatosha. Tuchague msikiti mwingine” kaka akashauri.
“Basi tutatafuta msikiti mwingine kule kule Chumbageni”
“Hilo tumelimaza. Sasa tayarisha kadi mapema uzitoe kwa wafanyakazi na rafiki zako. Na mimi nitachukua kiasi. Baada ya wiki moja tukutane tena tuone tumepata kiasi gain”
“Sawa kaka”
Tulimaliza mazungumzo yetu. Nikampakia kaka kwenye pikipiki yake kumrudisha nyumbani kwake. Na mimi nikarudi nyumbani kwangu.
Usiku wa siku ile ndoto zangu zote zilikuwa za harusi. Niliota ninamuoa Salma aliyekuwa akingara kama mwezi. Ingawa mwenyewe nilipanga kumuoa mchana, niliota ninamuoa usiku wa manane.
Ndoa yenyewe ilifanyika kwenye kisiwa kisicho na watu. Tulikuwa mimi na yeye na muozeshaji wetu..
Baada ya kuota ninaona na salama nikaota Salama amepata mtoto wa kiume, mzuri ajabu.
Nilipoamka asubuhi na kiondoka nyumbani nilikwenda kazini kwangu. Siku ile ile nikashughulikia mpango wa kuchapisha kadi za harusi ambazo nilizipata siku ile ile.
Wakati tunatoka kazini jioni nilimkabidhi kiasi kikubwa cha kadi msichana mmoja ambaye ni mfanya kazi mwenzangu ili anichangie kwa marafiki zake na kwa wafanyakazi wenzetu. Nikawataarifu baadhi ya wafanyakazi wenzangu kuhusu ndoa yangu.
Nilipotoka kazini nilikwenda nyumbani kwa kaka. Naye nikampa kiasi cha kadi ili azigawe kwa marafiki zake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mimi mwenyewe nilibaki na kiasi kidogo cha kadi hizo kwa ajili ya kuwagaia marafiki zangu.
Nilishukuru kwa jinsi nilivyoungwa mkono. Kadi zote ziligaiwa kwa watu na kila aliyepewa kadi aliahidi kunichangia baada ya wiki moja.
Kweli, baada ya wiki moja nilipata mchango wa kutosha sana ambao ulinipa matumaini kuwa ndoa yangu itafanikiwa. Ile wiki tuliyopanga nifunge ndoa, kaka alipeleka taarifa ukweni kuwa ndoa itafanyika siku ya ijumaa. Tulikuwa tumewapa siku saba tu za maandalizi lakini walikubaliana na sisi.
Naam siku ikawadia. Niliwekwa ndani kama mwari, nikasingwa kwa msio na mafuta ya nazi. Walionisinga walikuwa ni binamu zangu. Ilikuwa raha asana.
Ndoa ilifungwa katika msikiti mmoja uliokuwa maeneo ya Chumbageni.
Nakumbuka hadi leo jinsi sheikh mmoja alivyonifungisha ile ndoa.
Aliniita jina langu kisha akaniambia nimuitikie “Labaika”
“Labaika” nikamuitikia.
Akaniita tena.
“Amour Amrani”
“Labaika” nikamuitikia.
“Ninakuozesha Salama binti Riyami kwa mahari mliyokubaliana, umekubali?”
“Ndiyo” nikamuitikia huku midomo yangu ikitetemeka. Sikujua ilitetemeka kwa sababu gani.
“Hapana. Hilo silo jibu linalotakiwa ujibu. Unatakiwa useme nimekubali kumuoa Salama binti Riyami kwa mahari tuliyokubaliana”
“Sawa”
“Amour binti Amraani” Sheikh akaniita tena.
“Labaika”
“Ninakuozesha Salama binti Riyami kwa mahari mliyokubaliana, umekubali?”
Nikayakumbuka yale maneno aliyonifundisha.
“Nimekubali kumuoa Salama binti Riyami kwa mahari tuliyokubaliana” nikajibu.
Sheikh alirudia tena kuniambia hivyo mara tatu na mimi nilijibu mara tatu. Baada ya hapo ikasomwa hutuba ya ndoa iliyochukua karibu nusu saa.

Baada ya ndoa kufungwa nilipewa mawaidha. Niliambiwa siku ile nimeoana na Salama kwa wema, kwa hiyo niishi naye kwa wema na kumpa huduma zote zinazopaswa kutolewa kwa mke.
Sheikh aliendelea kuniambia kuwa kama itabidi kuachana, pia tuachane kwa wema kwani hivyo ndivyo ambavyo tumeusiwa na mtume wetu.
Baada ya hapo halua na tende pamoja na visheti ziikagaiwa. Watu wakala na kufurahi.
Baada ya shughuli kumalizika tukaenda nyumbani kwa mke. Nilikuwa nimekodi magari matano. Tulipofika tulikuta shamra shamra zikiendelea. Tuliingia chumbani kwa mke wangu aliyekuwa amepambwa vilivyo.
Nikampa mkono. Hapo hapo sheikh akatuombea dua na kututakia afya njema na maisha mema ya ndoa. Tulipiga picha za kumbukumbu zikiwemo za mnato na za video.
Ikafuatia pilau. Mimi na mke wangu tuliletewa sahani ya pamoja na jagi la juisi.
Tulishindwa kula sana kwa sababu ya zile hekaheka. Si unajua siku ya ndoa mtu unapata fadhaa kidogo.
Baada ya shughuli zote kumalizika, mtu aliyekuwa amesimamia ndoa upande wangu alitaka tuondoke. Wenyeji wetu wakapinga na kutaka tuendelee kuwepo kwa vile sherehe ilikuwa ikiendelea.
“Hapana, sisi hatukufuata sherehe hapa. Tumekuja kuoa” Msimamizi wangu alisema.
“Na ndoa ni sherehe, kama mtaondoka mapema hakutakuwa na sherehe tena” alijibiwa na msemaji wa upande wa mke wangu.
“Tatizo ni nini? Kama tumeshaoa tunachukua mke wetu tunaondoka” Msimamizi wangu akachachamaa.
“Msiondoke jamani, sherehe bado zinaendelea. Mkiondoka nyinyi mtatukatisha”
Msimamizi wangu akanishika mkono na kuniinua.
“Sisi tunaondoka. Nyinyi endeleeni na sherehe zenu. Na sisi huko tuna sherehe zetu”
Tukatoka.
“Jamani mnaondoka!” Wenyeji wetu wakalalamika.
“Waswahili bwana, wanataka tuendelee kukaa hapa, tufanye nini? Kwani sisi hatuna kwetu?” Msimamizi wangu alisikika akisema peke yake.
Tulitoka nje, gari zilikuwa zikitusubiri. Tukajipakia. Mimi nilipanda gari moja na mke wangu pamoja na wapambe wetu.
Gari nyingine mbili zikapanda watu wengine.
Tukaelekea Msambweni ilikokuwa nyumba yangu.
Nyumbani kwangu pia kulikuwa na sherehe. Tulipokewa kwa vifijo na hoihoi. Tulipoingia chumbani. Wapambe wetu wakatuacha.
Sherehe ziliendelea hadi saa sita usiku. Sisi tulikuwa chumbani tumelala.
Nilikuwa nimeomba ruhusa ya siku tatu kazini kwangu. Kwa hiyo nilikaa siku tatu bila kwenda kazini. Katika siku hizo tatu sikuchezea mbali. Muda wote nilikuwa chumbani na mke wangu Salma. Mara chache nilitoka peke yangu na kukaa sebuleni.
Baada ya siku hizo tatu kwisha nilikwenda kazini. Huko nilipata pongezi nyingi sana kwa kupata jiko (kuoa).
Sasa nikawa nimefungua ukurasa mpya wa maisha yangu. Siku za mwanzo mwanzo nilipotoka kazini tu nilirudi nyumbani haraka. Siku za jumapili sikuondoka nyumbani.
Ile tabia ya kula kwenye mikahawa ikaisha, nikawa nakula nyumbani tena chakula kizuri kilichopikwa na laazizi wangu. Naam. Maisha yalikuwa matamu sana!
Ilikuwa imepita miezi mitatu. Usiku mmoja wakati tumelala na Salma, Salama alianza kuweweseka akiwa
usingizini. Nilimuamsha na kumuuliza alikuwa na nini, akaniambia alikuwa anaota kuna msichana mmoja anamuamrisha aondoke pale nyumbani.
“Ananiambia hapa si kwangu, ni kwake yeye” Salma aliniambia.
Nikashituka na kumuuliza.
“Huyo msichana yukoje?”
“Umbo lake ni kama mimi ila yeye ni mweupe sana na ana sura kama muarabu”
Mara moja nikamkumbuka Zena ambaye nilikuwa nimeshamsahau.
“Anakwambia uondoke hapa nyumbani?”
“Ndio. Tena amenishikia bakora, anataka kunichapa”
Ili kumtoa hofu Salama nikajaribu kuzuga.
“Unajua ulikuwa umelala kichali chali halafu ulishiba sana. Lazima uote ndoto zisizoeleweka”
“Nilaleje sasa?” Salma akaniuliza kwa hofu.
“Lala kiubavu ubavu, elekea huku kwangu” nikamwambia”
Salma alipoelekea upande wangu akaniambia.
“Nikumbatie naogopa”
Nikamkumbatia. Salma hakuchelewa kupata usingizi. Akalala fofo. Mawazo yakabaki kwangu.
Asubuhi tulipoamka nilimuuliza.
“Uliota tena”
“Hapana, sikuota” akaniambia.
Nikashukuru aliponiambia hivyo. Nikajitayarisha kwenda kazini. Muda wangu wa kutoka ulipowadia nikatoka.
Nilichapa kazi hadi saa kumi jioni nikarudi nyumbani. Nilikuta nyumba ilikuwa imefungwa. Funguo nilipewa na mpangaji mwenzangu wa upande wa pili.
“Mke wako aliondoka, akaniachia hizi funguo. Amesema ukija nikupe”
“Amekwambia amekwenda wapi?”
“Hakuniambia”
Nikazichukua zile funguo na kufungua mlango huku nikiwa na mawazo. Nilipoingia chumbani nilikuta karatasi ya barua iliyokuwa imeachwa kitandani. Nikaichukua na kuisoma.
Mwandiko ulikuwa wa mke wangu Salma. Iliandikwa.
“Nimelazimika kuondoka hapa nyumbani ili kuokoa maisha yangu. Ile ndoto ilinijia tena mchana. Nilimuota tena yule msichana. Aliniuliza kwanini sijaondoka. Akaanza kunitandika bakora. Ngozi yangu ya mgongo imeharibika kwa jinsi alivyonichapa. Hali yangu ni mbaya. Ninakwenda hospitali na nikitoka hospitali narudi kwetu. Naomba uniletee talaka yangu. Huyo msichana ninayemuota ameniambia kama nitaendelea kukaa ataniua”
Salama alimaliza barua yake kwa kuweka jina lake.
Kusema kweli maneno ya Salma aliyokuwa ameniandikia yalinishitua sana. Nilipomaliza kusoma barua ile niliona miguu ikininyong’onyea na kuishiwa na nguvu.

Nikakaa kitandani na kuanza kutafakari. Tayari nilihisi presha yangu ikiwa juu na moyo ukienda mbio.
Nilirudia kuisoma tena ile barua. Nikaona kama uso wa Salma umetokeza katikati ya ile karatasi ukitamka yale maneno aliyoandika.
Nikaisikia waziwazi sauti yake ikimalizia kusoma barua hiyo kwa kuniambia.
“Naomba uniletee talaka yangu. Huyo msichana ninayemuota ameniambia kama nitaendelea kukaa ataniua…”
Nilihisi sasa mwili mzima ukipoteza nguvu. Tukio lile lilikuwa limenichoma mithili ya mkuki wa moto moyoni mwangu. Picha ya kuachana na Salama haikukubalika akilini mwangu. Si tu nilikuwa nampenda bali alikuwa ni kila kitu kwangu.
Tukio lile liliniashiria kwamba sitaweza tena kuishi na mke yeyote.
Zena amemtandika bakora Salma kama alivyowatandika wale vijana waliomuibia pochi.
Nilijua kuwa kama Salma asingeondoka na yeye angeuawa. Kuondoka kwake ulikuwa uamuzi wa maana ingawa sikuupenda.
Pia nilijua huo ulikuwa ndio mwisho wangu na Salma. Salama singeweza kurudi tena pale nyumbani na asingetaka tena kuishi na mimi.
Yale mawazo niliyokuwa nayo kwamba nikioa mke zena atakuwa mbali na mimi hayakuwa sahihi. Sikuweza kutambua huyu jini alikuwa na nia gani na mimi.
Kusema kweli nilisikia uchungu sana. Nikatikisa kichwa changu kusikitika. Nilishindwa kuvumilia machungu niliyokuwa nikiyasikia moyoni mwangu, nikaona machozi yakinitiririka.
Wakati nimeinamisha kichwa changu, nilihisi kama Zena amesimama mbele yangu akinicheka. Nikashituka na kudhani alikuwa Zena kweli. Kumbe yalikuwa ni mawazo yangu tu.
Nikajiuliza niende kwa kina salma nizungumze naye, lakini nikajiuliza tena ningekwenda kuzungumza naye nini wakati Salama ameshaamua kuondoka kusalimisha roho yake?
Nikajiambia kuwa si ajabu ameshagundua kuwa nina jini mwanamke ambaye hataki niwe na mke. Kama itakuwa hivyo nikifika kwao Salama anaweza kukataa nisizungumze naye zaidi ya kudai talaka yake kama alivyoniandikia kwenye barua.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Nilijihisi nilikuwa nimekabiliwa na uamuzi mgumu sana. Baada ya kuwaza kwa dakika kadhaa bila kupata ufumbuzi niliamua kutoka na kwenda kumueleza kaka kilichonitokea.
Kaka akapatwa na mshangao hasa nilipomueleza kuwa Salama ametandikwa bakora na Zena na ameshaondoka nyumbani.
“Sasa tufanye nini?” Kaka akaniuliza. Swali lake lilinikatisha tamaa. Nilichotarajia ni kupata ushauri kutoka kwake na sio mimi nimueleze yeye la kufanya.
Ilionesha mpaka kufikia kuniuliza tufanye nini ni kwamba alikuwa amekwama.
“Mimi sijui la kufanya. Nimekuja kwako ili nipate ushauri” nikamwambia.
“Mmh!” kaka aliguna kwanza kabla ya kuniambia.
“Sijui nikupe ushauri gani. Nikikwambia umbembeleze mke wako arudi ni kwamba atatandikwa tena na nikikwambia muache huko huko kwao, unyumba wenu utakuwa haupo tena!”
“Yaani tangu sasa unyumba wetu hauko tena, anadai nimpe talaka yake!”
“Ndio hapo sasa!”
“Mimi siwezi kumpa talaka. Nataka nipambane na hili tatizo kwa nguvu zote”
“Utapambana nalo kivipi?”
Swali hilo likanifanya nihamaki. Niliona kama vile kaka hakuwa pamoja na mimi.
“Kaka kwa mara ya kwanza naona una maswali ya kunikatisha tamaa” nikamwambia huku nikitikisa kichwa kusikitika.
“Hapana Amour, usinifikirie hivyo. Mimi niko pamoja na wewe. Nimekuuliza ili unieleze jinsi tutakavyopambana na hilo tatizo”
Nilikuwa nimeshahamaki. Nikaondoka kwenye kiti.
“Sasa unakwenda wapi?” Kaka akaniuliza.
“Niache kwanza” nilimwambia na kufungua mlango ili nitoke.
Kaka akanyanyuka.
“Hebu subiri Amour…!”
Nikatoka haraka. Nilipanda pikipiki yangu nikaiwasha na kwenda kwa mama.
Mama alivyouona uso wangu alijua kulikuwa na jambo lisilo la kawaida. Akaniuliza.
“Kulikoni?”
“Kuna matatizo yametokea” nikamwambia na kumueleza tatizo la kutandikwa bakora kwa mke wangu na kuondoka nyumbani.
“Nimekwenda kwa kaka, kaka ameshindwa kunisaidia kimawazo. Sasa mimi naondoka nyumbani nitakwenda kokote ambako naona nitapata msaada. Kama itashindikana, basi bora nife huko huko!”
Nilipomwambia hivyo mama nilitoka na kupanda pikipiki yangu. Mama alikuwa ametoka nje akinisemesha lakini sikujua alikuwa akiniambia nini na sikutaka kumsikiliza. Nikaondoka.
Nilirudi nyumbani, nikapanga baadhi ya nguo zangu kwenye begi. Nilikuwa na akiba ya pesa nilizokuwa nimeziweka kwenye kabati. Nikazichukua.
Kwa vile kichwa kilikuwa kimenichafuka, nilimuachia funguo mwenzangu wa upande wa pili nikaenda kulala gesti.
Kitu ambacho kilinikera sana, niliota Zena amesimama kwenye jangwa akinicheka. Alikuwa akinicheka hadi anayumba kama mlevi.
Asubuhi kulipokucha nilitoka nikaenda kituo cha mabasi. Nilipanda basi la kuelekea Dar. Nilifika Dar saa sita mchana nikaenda kutafuta gesti. Nilipopata gesti niliacha begi langu na kwenda kwenye mkahawa uliokuwa karibu kupata chakula kwani sikuwa nimekula chochote tangu subuhi.
Baada ya kula chakula nilirudi pale gesti. Kulikuwa na mgeni mmoja wa kipemba aliyekuwa amepangisha chumba. Tulikutana ukumbini. Nikamsalimia na kumuuliza kama alikuwa anatoka Zanzibar.
“Natoka Mwanza, ndio niko safarini kuelekea Zanzibar” akaniambia.
“Unakwenda Unguja au Pemba?”
“Mimi naenda Pemba”
“Unatarajia kwenda lini?”
“Kesho asubuhi Mungu akipenda”
“Basi tutaondoka sote, nilikuwa na tatizo linalohusu huko Pemba na nitakueleza”
“Ni tatizo gani?”
“Hebu njoo huku chumbani kwangu nikueleze”
Yule mtu alikubali kuingia chumbani kwangu. Nikamueleza yale matatizo yangu.

“Sasa shida yangu ni kupata mganga ambaye ataliondoa hili tatizo” nikamwambia.
Mpemba alinyamaza kimya akafikiri kisha akaniambia.
“Yuko mama mmoja pale Pemba ni mganga anayetegemewa sana kwa matatizo ya majini. Kama yeye atashindwa ujue hutapata tena mganga ambaye atamuweza huyo jini wako”
“Ningekuomba unipeleke kwa huyo mwanamke”
“Nitakuelekeza na hutapotea”
“Lakini wewe pia si unakwenda huko huko”
“Ndio, mimi nakwenda Pemba lakini ninakokwenda ni kwingine na huyo mganga yuko kwingine. Yaani hata tukienda sote tutaachana bandarini”
“Si kitu, wewe nielekeze tu, nitafika”
Kwa vile mji wenyewe nilikuwa siujui, yule mtu alinichorea ramani ikianzia bandari ya Pemba hadi ulikokuwa mtaa huo. Akaniambia nyumba ya mganga huyo iko kwenye kona. Ni nyumba kubwa lakini ni ya kizamani sana na imepakwa chokaa nyeupe.
“Alama yake ni kuwa mlango wa mbele wa nyumba hiyo umechorwa picha ya nyota na mwezi” akaniambia.
“Nitapaelewa tu” nikamwambia.
Asubuhi ya siku iliyofuata tukasafiri sote kwenye boti. Tulipofika Pemba akanielekeza tena. Nikaenda mwenyewe katika huo mtaa.
Kwa vile nilikwenda kwa miguu ili nisipotee nilitembea sana
Mara kwa mara nilikuw a nawauliza watu niliokutana nao njiani kama wanamfahamu mganga huyo. Baadhi ya watu hao walikuwa wanamfahamu na wakanielekeza zaidi mtaa aliokuwa anaishi.
Baada ya mwendo mrefu nikafika katika mtaa huo, nikawa naitafuta ile nyumba. Baada ya kuhangaika sana nikaiona. Ilikuwa kwenye kona na ilipakwa chokaa nyeupe.
Alama kubwa iliyonipa moyo ni picha ya nyota na mwezi niliyoikuta kwenye mlango.
Kama alivyonieleza yule mtu niliyesafiri naye, nyumba hiyo ilikuwa ya kizamani sana na ilikuwa kwenye hatari ya kuanguka kwani ilikuwa ni nyumba iliyojengwa kwa mawe na udongo ingawa ilipauliwa kwa bati. Bati hilo lilikuwa limeota kutu na kuchakaa.
Nikaenda kwenye mlango na kubisha. Nilibisha mara mbili bila kupata jibu. Nilipobisha mara ya tatu nikajibiwa.
“Karibu” Ilikuwa sauti ya mwanamke. Nilishaambiwa kuwa mgaga mwenyewe ni mwanamke.
Baada ya sekunde chache mlango ukafunguliwa. Ndani kulikuwa kiza. Hata mtu aliyenifungulia mlango sikuweza kumuona vizuri.
“Karibu ndani” Sauti ya mwanamke ikaniambia.
Nikaingia. Kulikuwa na ukumbi mpana uliokuwa umetandikwa jamvi.
“Karibu ukae kwenye jamvi”
Nikakaa. Yule mwanamke naye akakaa kando yangu.
“Pole kwa safari, naona umetoka mbali” akaniambia huku akinitazama. Sasa pale ndipo nilipomuona vizuri. Kumbe alikuwa Zena!
Nilishituka sana nilipogundua kuwa mwanamke mwenyewe alikuwa Zena.
Nilishindwa kuelewa kwanini amekuwa Zena wakati niliambiwa kulikuwa na mwanamke ambaye ni mganga.
“Habari za huko?” Zena aliniuliza alipoona nimepigwa na butwaa.
Niligeza haraka uso wangu nisitazamane naye. Nikawa natazama chini.
“Nzuri” nikamjibu. Sauti yangu ilikuwa nzito ya mtu aliyetahayari.
“Mbona umekuja huku, una shida gani?” akaniuliza huku akinitazama kwa makini. Nilikuwa nimeinamisha uso wangu lakini nilikuwa namuona kwa pembeni mwa macho yangu.
Nilishindwa kujibu Swali lake kwa sababu sikujua ningemjibu nini. Nimjibu kuwa nimekwenda Pemba kufuata mganga na badala yake nakutana na yeye? Hapana.
“Nimekuja kutembea tu” nikamwambia
baada ya kushindwa kumueleza ukweli.

INAENDELEA

Post a Comment

0 Comments