“Poleni sana jamani,” Dokta akawaambia wale watu waliompeleka Mariam hospitalini.
“Tunashukuru sana Dokta.”
“Nani anayehusika zaidi na huyu mgonjwa, nataka kufanya naye mazungumzo kidogo!”
“Kwakweli hakuna!”
“Hakuna?!”
“Ndiyo hakuna daktari!”
“Unamaanisha nini kusema hivyo, kwahiyo kati ya ninyi nyote hakuna ndugu wa huyu mgonjwa?”
“Hakuna!”
“Kivipi?!”
“Sisi ni wasamaria wema tu, ambao tumeamua kumsaidia baada ya kumuona ameanguka na kupoteza fahamu!”
“Ilikuwaje?”
“Kwakweli hatujui, lakini ilikuwa ni mbele ya meza ya magazeti!”
“Basi hakuna tabu, lakini mnaweza kujitolea pia kumsaidia malipo ya matibabu yake!”
“Hilo halina tabu.”
“Mungu akubariki kwa hilo, acha sisi tuendelee!”
“Sawa, sijui wewe ni dokta nani?”
“Naitwa Dk. Ringo, tena nilisahau kukufahamisha, sijui na wewe mwenzangu nani?”
“Naitwa Ramsey Muhando.”
“Nashukuru sana kukufahamu.”
“Nami pia.”
Kazi ya kumtibu Mariam ikaanza, huku gharama zote zikilipwa na Ramsey ambaye alijitolea.
******
“Sikiliza shoga yangu, mimi sijazoea mambo ya nuksi nyumbani kwangu, kama nilivyokuambia, mama yake Tom amefariki na sitaki kujihusisha na jambo lolote linalomuhusu yeye!” Mayasa alikuwa akimwambia Rukia katika kikao chao kilichofanyika usiku, ndani ya hoteli moja ya kifahari katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Kwahiyo sasa utafanyaje?”
“Nawaachia watu wa Halmashauri ya Jiji wazike!”
“Lakini huoni kwamba mambo yanaweza kushtukiwa?”
“Kwanini?”
“Magazeti yameshaandika, halafu nyumbani hakuna msiba, unadhani utaelewekaje?”
“Kila kitu nimeshakamilisha, nimeshauza vitu vyote, fedha zilizokuwa benki pia nimekomba zote tena kwenye akaunti zake zote, kuna madini aliyokuwa akiyahifadhi ndani nayo nimeyachukua. Sina kinachonifanya niendelee kubaki kwenye ile nyumba, waache wenye moyo mwema watamzika, wakikosekana basi, bahati mbaya!”
“Safi sana, sasa vipi kuhusu mimi, naambulia nini?” Rukia akamwuliza Mayasa akiwa anamtizama kwa macho yenye kusubiria jambo fulani.
Mayasa hakumjibu kitu, zaidi ya kumwangalia kuanzia chini hadi juu, ni kama alikuwa akimchambua!
“Twende!” Mayasa akasema.
“Wapi? Mi’ nataka kujua changu!”
“Ndiyo maana nimekuambia twende!”
“Wapi sasa?”
“Nikakupe chako!”
“Ni nini?”
“Surprise!”
“Okay!” Wote kwa pamoja wakaondoka na kushuka chini ambapo walipanda kwenye gari la Mayasa na safari ya kwenda kusipojulikana ikaanza.
Rukia alikuwa kimya muda wote wa safari, akiwa hajui ni wapi hasa walipokuwa wakielekea, maswali tele kichwani mwake yalibaki yanazunguka. Baadaye gari likasimama nje ya geti jeusi, lenye nyumba moja nzuri sana. Mayasa akapiga honi mfululizo, mlango ukafunguliwa.
Wakaegesha gari kisha Mayasa akamshika mkono Rukia na kumtembeza kila kona ya nyumba ile. Ilikuwa nyumba ya kisasa iliyokuwa na kila kitu ndani, bwawa la kuogelea, gari ndogo ya kutembelea, samani ndani na bustani nzuri sana iliyokuwa nje.
“Sikiliza rafiki yangu...wewe ni rafiki yangu mpenzi, nakupenda na ninaheshimu sana msaada wako katika kufanikisha zoezi hili, kuanzia leo hii ni nyumba yako na kila kitu kilichomo ndani.
“Kwa bahati nzuri, hii nyumba nilijengewa na Tom mwenyewe, na hati zote zina majina yangu, kwahiyo usiwe na wasiwasi kabisa, hapa ni kwako na kila kilichomo ndani, kuanzia gari na samani zote, kuishi hapa au kuuza ni hiyari yako!” Mayasa akamwambia Rukia.
Rukia hakutegemea kama angepewa zawadi kubwa kiasi kile, kwanza alitumia muda mwingi kuwa kimya akijaribu kutafakari kama ni kweli kilichokuwa mbele yake kilikuwa yakini, Mayasa akampatia hati zote na kumtoa wasiwasi kwamba pale palikuwa ni nyumbani kwake na alikuwa na uhuru wa kufanya jambo lolote apendalo.
“Ahsante sana Mayasa shoga yangu, huu ndiyo urafiki wa kweli, ni wachache sana wanaweza kuwa kama wewe!”
“Usijali...sasa sijui utaishi hapa au utauza?”
“Nitauza, siwezi kuishi hapa!”
Ndivyo ilivyokuwa, siku iliyofuata nyumba ilitafutiwa mteja wa chapchap, ikauzwa kwa bei ya kutupwa! Jioni ya siku hiyo hiyo, Mayasa akaondoka kwenda zake Uingereza. Hakutaka kuendelea kuishi Tanzania tena, haikuwa sehemu salama kwake!
Hadi wiki moja baada ya mama yake Tom kufariki bila kutokea kwa ndugu yeyote, mwili huo ulichukuliwa na Halmashauri ya Jiji na kwenda kuzikwa. Kama kawaida, magazeti yaliripoti kila kitu, haikueleweka ni wapi Mayasa, mwanamke aliyekuwa akiishi naye baada ya Tom kumuacha mkewe Mariam, alipokwenda.
Kwakuwa hapakuwa na ndugu mwingine yeyote, mambo yaliendelea kuwa giza nene, mwenye majibu alikuwa ni Tom ambaye kwa wakati huo ni kama alikuwa nusu-mfu!
*******
“Toooom....Toom...Tooom, usife, bado nakupenda, bado nakuhitaji Tom wangu usife...” Ndiyo maneno aliyozungumza Mariam baada ya kuzinduka siku tatu baadaye katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro alipokuwa amelazwa.
“Vipi dada yangu, naomba utulie kwanza...tulia...” Ilikuwa sauti ya muuguzi ambaye alimwita mwenzake mara moja, ambapo alimuagiza akamwite dokta haraka.
“Afadhali amezinduka, vipi dada unaendeleaje sasa?” Dokta akamwuliza akiwa anamtizama usoni.
Mariam hakuwa na la kuongea, alianza kushangaa hadi aliporudisha fahamu vizuri, hapo ndipo Daktari alipomsimulia kila kitu. Bahati nzuri, Ramsey mmoja wa watu walioshuhudia tukio la yeye kuanguka, ambaye ndiye aliyekuwa akigharamia matibabu yake, akatokea. Alifurahi sana kumkuta katika hali nzuri. Akamsimulia kila kitu kilichotokea, Mariam naye hakuficha chochote kuhusu Papaa Bill ‘Tom’. Alizungumza kila ukweli unaohusu uhusiano wake na Tom. Historia yake ilihuzunisha sana, haikuwa rahisi kuamini kama msichana mdogo kama yeye aliwahi kupitia historia ngumu kiasi kile.
“Pole sana dada yangu, sasa nafikiri ni vyema nikurudishe nyumbani ukapumzike kwanza!” Ramsey akasema.
“Wapi?”
“Matombo, kwa bibi yako.”
“Haiwezekani!”
“Kwanini?”
“Sitaki!”
“Unataka kwenda wapi?’
“Kama ni kweli unataka kunisaidia, kwasasa nataka kwenda Muhimbili kuonana na Tom, pili kushughulikia mazishi ya mama mkwe wangu! Nampenda sana mama...nampenda, najua alikuwa akitamani sana niishi na mwanaye, lakini Tom alimpuuza mama yake. Lazima nionyeshe mapenzi yangu kwake hata kama amekufa!”
“Sawa nitakusaidia, lakini lazima hali yako itengemae kidogo!”
“Sawa!”
Siku tatu baadaye, hali ya Mariam ilipokuwa nzuri akaruhusiwa kutoka Hospitalini. Kama Ramsey alivyoahidi ndivyo alivyofanya, alifika Hospitalini akiwa amemnunulia nguo mpya na viatu. Mariam akaoga na kubadili nguo zake kisha wakaondoka na kwenda Msamvu ambapo walipanda basi la Hood kwa safari ya kwenda Dar es Salaam.
Safari ilikuwa ndefu sana kwa Mariam, lakini hatimaye walifika Ubungo, Ramsey akakodi teksi iliyowafikisha Muhimbili. Kutokana na umaarufu wa Tom ‘Papaa Bill’, haikuwa kazi kubwa kufahamu wodi aliyokuwa amelazwa. Ramsey na Mariam wakaongozana hadi kwenye kitanda cha Tom.
Mariam hakuamini macho yake, Tom alikuwa amelala kimya kitandani huku akipumua kwa kutumia mashine. Tom alikuwa hajitambui! Mariam akaanza kulia, hadi muuguzi alipofika eneo hilo na kumwita ofisini kwake.
“Vipi dada, wewe ni ndugu yake na Papaa Bill?”
“Ndiyo!”
“Nani wake?”
“Mume wangu.”
“Mumeo?
“Ndiyo!”
“Wewe ndiye Mariam, tunayekusoma kwenye magazeti?”
“Ndiyo!”
‘Pole sana mdogo wangu, una moyo wa peke yako kwakweli!”
“Ahsante sana sister, vipi maiti ya mama Tom? Nataka kushughulikia taratibu za mazishi!”
“Pole sana, ni juzi tu alizikwa na Halmashauri ya Jiji baada ya ndugu zake kutoonekana!”
“What?!” Mariam alitamka maneno hayo, macho yakimtoka.
Hakuwa tayari kuamini alichosikia.
Marehemu mama Tom alikuwa akimpenda sana Mariam, alimpenda kwa mapenzi yake yote. Alimfahamu vizuri sana Mariam, wema wake ulikuwa mkubwa sana, alikumbuka kila kitu alichokuwa akikifanya kwa ajili ya marehemu mume wake.
Alijua yote hayo yalifanyika kutokana na mapenzi ya kweli aliyokuwa nayo kwa mwanaye! Hilo pekee lilimfanya ajitahidi kumshauri mwanaye kwa kila hali aachane na wazo la kutoishi na Mariam. Alishazungumza sana, alionyesha kila dalili ya kuchukizwa na vitendo vya Tom, lakini kijana wake hakubadilika!
Pamoja na kwamba Mariam aliamua kwenda kujificha kijijini Matombo kwa ajili ya kukaa mbali na Tom, lakini hakuwa akimchukia mama yake! Siku alipoona habari kwenye gazeti la Ijumaa kuwa amefariki dunia, aliona fadhila aliyokuwa akitakiwa kufanya ni kumzika mama huyo kwa heshima!
Pengine angeumia sana baada ya kukuta amezikwa na jambo pekee ambalo lingefuata ingekuwa ni kwenda kutizama kaburi lake na kusoma dua pembeni ya kaburi lake, lakini sasa ndoto hizo zimezimika kama mshumaa!
Mama Tom amezikwa na Halmashauri ya Jiji, ni jambo ambalo lilimuumiza sana moyo wake. Machozi kama maji yakazidi kumiminika machoni mwake.
“Nyamaza Mariam, huna sababu ya kulia dada yangu, shukuru kwa kila jambo!” Ramsey, msamaria mwema aliyemsadia kuanzia Morogoro alimwambia.
“Siyo rahisi Ramsey, ni vigumu sana kaka yangu!”
“Kwanini....kubali kilichotokea, unajua hakuna kitakachobadilishwa na machozi yako!”
“Najua, lakini naamini machozi yangu yatakuwa yanaonyesha kujali kwangu!”
“Kwa mtu aliyekufa?”
“Ndiyo!”
“Ndiyo nasikia kwako...lakini Mariam, nyamaza kulia, huna sababu ya kulia kiasi hicho, utakuwa unajiumiza tu mdogo wangu!” Nesi naye akamwambia Mariam.
“Ahsante!”
“Pole sana!”
“Nashukuru!” Sasa Mariam akatulia kidogo.
Ramsey akamwangalia Mariam aliyekuwa akiendelea kutokwa na machozi mepesi, akachukua kitambaa chake na kumfuta machozi.
“Kwahiyo Sister ni nani anayemuuguza Tom kwa sasa?”
“Papaa Bill?”
“Ndiyo!”
“Hakuna mtu yeyote anayemhudumia, yupo peke yake!”
“Hali yake?”
“Kama ulivyomuona, hali yake siyo nzuri na amepoteza fahamu tangu siku aliyoletwa hapa!”
“Nini zaidi kinachomsumbua?”
“Kwani Mariam ulikuwa wapi hadi usijue yote hayo?”
“Acha tu dada’ngu, ni stori ndefu lakini fahamu kwamba sijui chochote kinachoendelea, nitakusimulia baadaye, lakini nafikiri ni vyema ukanieleza.”
“Alivamiwa na majambazi na kumpiga risasi, kwa bahati mbaya amepooza kuanzia shingoni kushuka chini, mbaya zaidi hajapata fahamu na anapumua kwa msaada wa mashine!”
“Mungu wangu!”
“Usijali Mariam, maadam unajua kuna Mungu, basi huyo ndiye msaada pekee uliobakia kwa sasa!”
“Nitaendelea kumuomba yeye siku zote!”
“Amen!”
“Sasa Mariam, kwahiyo utakuwa ukimuuguza Tom siyo?”
“Ndiyo, lazima nifanye hivyo!”
“Vizuri sana!”
Baada ya hayo, Ramsey na Mariam wakarudi tena wodini kumuangalia Tom, bado hakuwa amefumbua macho, hali yake ilikuwa mbaya sana. Mariam akamsogelea na kumbusu mashavuni mwake, kisha akamshika Ramsey mkono na kuondoka naye.
“Tunakwenda wapi?” Mariam akamwuliza Ramsey.
“Unamaanisha nini?”
“Namaanisha tunapokwenda!”
“Mariam kwani hujui nyumbani kwangu ni Morogoro?”
“Najua!”
“Sasa?”
“Nilikuwa nataka kujua kama unakwenda huko!”
“Ndiyo jibu lake!”
“Ramsey nashukuru sana kwa msaada wako, napenda kukuambia wazi kwamba wewe ni binadamu kamili, mwenye utu na unayetambua thamani ya ubinadamu. Mungu akubariki sana kwa hilo, lakini nilikuwa na ombi lingine!”
“Nini?”
“Sitaki kwenda nyumbani leo, nahitaji kulala hotelini kwa wiki nzima, unaweza kunisaidia fedha za kulipia pango na chakula kwa muda huo?”
“Hilo linawezekana, lakini kwanini hutaki kwenda nyumbani?”
“Nataka akili yangu ipumzike kidogo kwanza, nina mawazo mengi sana Ramsey!”
“Usijali lakini sioni kama ni busara kukuacha peke yako katika kipindi hiki kigumu, nafikiri tutafute hoteli kisha nitalipia vyumba viwili, niendelee kukupa kampani zaidi au unaonaje?”
“Sawa!” Ndivyo ilivyokuwa, wakaongozana hadi katika hoteli moja nzuri iliyopo Magomeni, wakalipia na kuingia ndani.
*****
Magazeti yote ya siku iliyofuata yalikuwa yamepambwa na habari ya Mariam kuonekana Muhimbili. Yaliandika habari ile kwa undani sana tena yakiwa na picha mbalimbali zinazomwonyesha Mariam akilia wodini na nyingine akimbusu Tom aliyekuwa amelala hoi kitandani!
Walielezea kitendo kile kuwa ni cha kijasiri na kwamba Mariam alikuwa na penzi la kweli. Habari hizo ziliwafikia wazazi wa Mariam ambao walikasirika sana. Kwanza walishindwa kuelewa ni kwanini mtoto wao alikuwa anaendelea kumsaidia Tom, mwanaume ambaye alimtesa, mbaya zaidi aliwatukana hata wao!
“Unaona mama Mariam, huyu mtoto ana akili kweli?”
“Sijui amempa nini mwanangu huyu Tom? Huyo mwanamke aliyemuona anafaa, amemkimbia na nasikia ameuza kila kitu, sasa kipindi cha matatizo ndiyo Mariam awe msaada kwake, haiwezekani!”
“Haiwezekani kabisa!”
“Sasa tutafanyaje?”
“Kilichopo hapa ni kwenda Muhimbili hadi kwenye wodi aliyolazwa, lazima tutamwona Mariam!” Wazo hilo liliungwa mkono na wote wawili ambapo waliingia kwenye gari na kwenda moja kwa moja Muhimbili.
Walipofika wakaingia katika wodi aliyolazwa Tom, kama walivyokuwa wakitarajia ndivyo ilivyokuwa. Walimkuta Mariam akimhudumia Tom, machozi mengi yakimtoka. Mama yake Mariam alipomuona mwanaye alikuwa na hasira sana, akamfuata na kumvuta pembeni uso wake ukiwa na makunyazi.
“Hivi we’ mtoto umelogwa? Una akili kweli? Kwani huyu hana ndugu, hana marafiki? Mabaya yote aliyokufanyia huyaoni? Matusi aliyotutukana sisi wazazi wako hayakuuma?
“Umelazwa mara ngapi kwa ajili yake, lakini leo wewe ndiyo unakuwa wa kumsaidia..sasa sisi kama wazazi wako, tunakuambia toka haraka sana hapo, unatakiwa tuongozane pamoja nyumbani!”
“Najua nyie ni wazazi wangu, najua kuwa mnanipenda, lakini lazima mzifahamu na kuheshimu hisia zangu. Mimi nampenda Tom kwa mapenzi yangu yote, siwezi kwenda na nyie nyumbani nikaamuacha Tom katika hali hii!”
“Unasemaje wewe mtoto, hivi una akili kweli wewe?” Baba yake Mariam akamwuliza kwa hasira sana.
“Akili ninazo tena nyingi sana, lakini penzi langu kwa Tom litaendelea kudumu siku zote za maisha yangu!”
“Sasa kama hujatoka kwenye tumbo langu mimi mama yako, endelea kubaki hapa hospitalini, lakini kama mimi ni mama yako, niliyekuzaa, urudi mwenyewe nyumbani!” Mama Mariam akasema kwa sauti ya ukali sana, kisha akamshika mumewe mkono na kutoka nje.
Baba Mariam alikuwa na hasira sana, hakuweza kuongea neno lolote zaidi ya kuwa msikilizaji! Baadaye Mariam naye alitoka kwa hasira, akachukua taxi na kwenda hotelini.
******
Mariam alipofika hotelini, aliingia chumbani kwake akiwa amechanganyikiwa sana. Kila alichokifanya aliona kama anakosea! Mawazo mengi yalimchanya kichwani.
Zaidi ya kufikiria kuhusu wazazi wake ambao walikuwa wanamzuia kumhudumia Tom, lakini pia aliumizwa na wema wa Ramsey. Hakutaka maumivu tena baadaye, alianza kuhisi kwamba Ramsey angehitaji kulipwa fadhila.
Hapo ndipo alipoamua kumpigia simu Ramsey, hakutaka kubaki na mawazo kichwani mwake. Akachukua mkonge wa simu, kisha akabonyeza namba za chumbani kwa Ramsey, simu ikaanza kuita, baadaye ikapokelewa na sauti tulivu sana ya Ramsey.
“Yes, Mariam hapa, naomba uje chumbani kwangu Ramsey!”
“Chumbani kwako?” Ramsey akauliza kwa mshangao.
“Ndiyo!”
“Kuna nini?”
“Njoo tu!” Dakika mbili baadaye Ramsey alikuwa chumbani kwa Mariam akiwa amevaa bukta na fulana nyepesi, uso wake ukionyesha wazi wasiwasi aliokuwa nao.
“Kuna nini dada Mariam?”
“Nataka kujua kwanini unanifanyia yote haya?”
Ramsey hakuwa na jibu la haraka. Aliangalia juu, kisha akarudisha macho yake chini kabla ya kuyatuliza usoni mwa Mariam.
“Unasema?” Ramsey akauliza.
“Kwanini umekuwa mwema kwangu kwa kiasi kikubwa namna hii?”
Ramsey alikuwa kimya.
Ramsey aliendelea kuwa kimya, katika siku ambazo alishangazwa sana na Mariam basi ni pamoja na siku ile. Swali aliloulizwa lilikuwa gumu sana, gumu kwa sababu hata mazingira ya swali lenyewe yalikuwa tata! Kuna wakati alianza kuwaza kwamba, inawezekana Mariam alikuwa akimtaka ndiyo maana akamwuliza swali lile kama mtego.
Macho ya Ramsey yalibaki usoni mwa Mariam kwa muda mrefu, akimtizama kwa makini na kumsoma uso wake kama ulifanana na aliyokuwa anayazungumza. Kwa kiasi kikubwa hakuweza kujua nia hasa ya Mariam ilikluwa nini kwani katika uso wake hapakuwa na kitu hata kimoja kilichoonekana kushabihiana na maneno yake.
Hakujua kama alikuwa anamtania au alikuwa anamwekea mitego! Ramsey akabaki anamwangalia Mariam bila kufungua kinywa chake kusema neno lolote. Sasa Ramsey akaamua kumwangalia Mariam kwa umakini zaidi, macho yake yalishuka hadi miguuni mwa Mariam, akaikagua.
Akayapandisha taratibu hadi kiunoni, hapo akakubali kwamba kweli Mariam alikuwa mwanamke mwenye mvuto wa kike! Akamwangalia macho yake ya mviringo ambayo yalikuwa pambo tosha katika chumba kile. Ramsey akahema kwa kasi, kisha akatizama “lips” za Mariam, hakika zilipendeza sana.
Lakini alikuwa na maswali yaliyomchanganya kichwani mwake, anaweza kuonekana mwenye tabasamu wakati alikuwa kwenye kipindi kigumu cha matatizo? Hilo lilizunguka ubongoni mwake bila kuwa na majibu ya moja kwa moja.
Kila kitu kilikuwa gizani. Maswali yote hayakuwa na majibu. Mariam ambaye muda wote alionekana kuwa kimya, sasa alifungua kinywa chake akionekana kuwa na jambo la msingi sana la kuzungumza naye. Akayatoa macho yake kwa kasi, kama alikuwa haoni vizuri, akameza fundo moja la mate ambayo bila shaka aliyakusanya kwa muda mrefu sana mdomoni mwake.
Akawa mtulivu sana, akaanza kuzungumza: “Nimekuuliza swali Ramsey!”
“Swali?”
“Ndiyo!”
“Mh!”
“Mbona unaguna?”
“Naguna sababu ya maneno yako Mariam!”
“Yanachekesha au hayana maana?”
“Siyo kwamba yanachekesha na wala siyo kwamba hayana maana.”
“Bali?”
“Nina wasiwasi na wewe.”
“Juu ya nini?”
“Ya ulipotoka, sijui kama umetoka sehemu salama.”
“Nini maana yako?”
“Siyo kawaida yako kuwa hivi Mariam, nahisi kuna tabia nyingine ambazo unazifanya ambazo mimi nilikuwa sizijui.”
“Kwanini unasema hivyo Ramsey?”
“Naweza kukuuliza kitu?”
“Uliza tu!”
“Unakunywa pombe?”
“Hapana.”
“Kweli?”
“Nakuhakikishia, kwani naonekana nimekunywa?”
“Hapana ila yanayotoka kinywani mwako ndiyo yanayosababisha nihisi hivyo.”
“Anyway...nisikilize Ramsey, tufanye hivi, mimi ni mnywaji wa pombe na leo nimekunywa. Halafu baada ya hapo jibu maswali yangu hata kama ni ya mlevi sawa?”
“Usiseme hivyo...”
“Sasa niseme nini? Inawezekana umesahau swali, nitakukumbusha...wewe ni kijana mzuri sana, ambaye roho yako inafanana na tabia yako! Nashukuru kwa hilo, lakini naamini una kazi nyingi za kufanya umeziacha na kuamua kunisaidia mimi katika kipindi hiki kigumu, je kwanini umeamua kufanya hivyo?” Mariam aliongea maneno hayo huku machozi yakimlengalenga machoni mwake.
“Mariam acha kulia, naomba ufahamu kitu kimoja, nimefanya yote hayo kwa sababu ya mapenzi tu, sina kitu kingine chochote ambacho kimenifanya nikaamua kukusaidia!”
“Unanipenda?”
“Ndiyo...kama dada yangu, rafiki yangu wa karibu lakini kubwa zaidi natimiza moja ya amri muhimu tulizopewa na Mungu, tuliagizwa tupendane Mariam, kwanini nisikusaidie kwa upendo huo?”
“Kweli?”
“Niamini!”
“Hakuna lingine?”
“Lipi tena?”
“Basi nashukuru sana kama ni kweli hakuna lingine zaidi ya hilo, umenifurahisha sana Ramsey.”
“Usijali.”
Wakaendelea kuzungumzia mambo mengine, hadi baadaye Ramsey alipoaga na kurudi chumbani mwake. Hata hivyo Ramsey aligundua kwamba lazima Mariam alikuwa na kitu kilichomchanganya hasa kutokana na maswali aliyokuwa akiuliza.
Jioni walikutana kwa ajili ya chakula cha jioni, baada ya kula Ramsey alishindwa kuvumilia kubaki na maswali mengi kichwani mwake, akaamua kumuuliza Mariam ili kupata ukweli. Mariam hakuona sababu ya kuficha jambo, akamweleza ukweli jinsi alivyokwaruzana na wazazi wake hadi kufikia hatua ya kuondoka wodini bila kuwepo kwa maelewano.
“Lakini wale ni wazazi wako Mariam, lazima uwasikilize!”
“Hujakosea Ramsey, lakini na wao hawawezi kunichangulia mtu nitakayeishi naye.”
“Ungewapa nafasi kwanza, hata kama unampenda huyo Tom kiasi gani lakini waliyokuambia yana maana, unampenda vipi mtu ambaye alikufukuza na kuwatukana wazazi wako?”
“Najua siyo yeye, ni yule shetani Mayasa niliyekupa habari zake.”
“Hata kama, lakini wazazi wako walikuwa na hoja ya msingi.”
“Sasa naona unataka kuniudhi,” Mariam akasema akionyesha hasira.
“Basi Mariam yaishe,” Ramsey akaamua kuwa mpole.
*******
Mariam akaendelea kumhudumia Tom kwa karibu sana, kila siku alikuwa akishinda Muhimbili na kurudi hotelini usiku. Hakutaka mpenzi wake apate shida, alikiri wazi kwamba hatatokea mwanaume ambaye atampenda kama alivyompenda Tom.
Tom alikuwa kila kitu kwake, alimkabidhi maisha yake yote, hakujali mateso na manyanyaso yote aliyompa. Imani kubwa aliyokuwa nayo moyoni mwake ni siku moja Tom angeamka na kuwa naye kama mke na mume maana Mayasa ambaye kwake alikuwa ni shetani alikuwa ameshatoroka.
INAENDELEA...
0 Comments