BASI hivyo ndivyo alivyoandika Neema na kutuma meseji ile kwa
Cliff aliyejibu kwa kifupi; "mh.."
Neema sasa akatoka taratibu mle chumbani gauni la bluu, kiremba
cheupe, mawani ya kusomea yakiwa yameegeshwa vyema juu ya mianzi ya pua yake
nyembamba; soksi ndefu zilizotokomea chini ya skuna za chini kabisa. Akafanana
tikatika na picha ya kitambulisho chake cha utawa kutoka monasteri ya Italia
jiji la Rome palepale mji wa mtakatifu Petro.
Hakika Neema sasa alikuwa ni sista Anne kama ambavyo jina lake
la utawani lilipaswa kuwa. Akashuka kutoka mle hotelini na kutembea kama mfuasi
thabiti wa Yesu Kristu, unadhifu na mabadiliko hayo hakika hakuna aliyeweza
kusema kuwa huyo ndiye Neema aliyekuwa na Cliff.
Utofauti wake ukaufanya ukumbi mzima umtazame, naye macho ya
watu akayakinga na ufito wa shaba ye pembeni ya miwani yake aibu ikavumilika.
Naye Neema alikwishatarajia hilo kutoka kwa watu maana wakati wengine wakianza
kukurupuliwa mahotelini na maaskari na kupimwa kwa shuruti, yeye akasalimiwa
kwa heshima na viongozi.
"Tumsifu Yesu Kristu, sista, wewe ni mgeni wetu pia?"
aliuliza Meneja wa Hoteli akiwa na wasiwasi na lugha yake maana rangi ya Neema
ilikuwa na hatihati kuwa ni msauzi au mbrazili, wazo la kuwa ni mtanzania
lilikuwa dogo mno kichwani mwa meneja huyo.
"milele amina, ndiyo ni mgeni nimefika jana kutokea Roma.
nilisikia simu ikiita lakini nilikuwa kwenye sala ya asubuhi. tafadhali hapa
tunaelekea wapi samahani sifahamu utaratibu," alisema Neema mikono yake
ikiwa inazungusha tufe za rozali kubwa mkononi mwake.
"ooh nadhani utakuwa umemiss maelekezo ya mheshimiwa mkuu
wa mkoa, ni hivi wageni waliotokea Italia wataenda upande ule pale. Utakuwa na
passport size yako hapo ili nikushughulikie haraka?" alisema meneja, Neema
akampatia passport yake, haraka Meneja akamuomba Neema aongozane naye, basi
wakavunja utaratibu na sista akapishwa kupima yeye kwanza.
Vipimo vikaonesha hakuwa na chochote, wakati huo Cliff alikuwa
akiduwaa huyoo, akaamini aliyoyasema Neema kuwa atatoka tofauti kabisa.
"Sista Anne, natumai hii dhalura ya leo haitakufanya
uichukie hoteli yetu," alisema Meneja aliyejitenga kusimama na sista
mahala,
Mikono yake ikionesha heshima na adabu, lakini kwa jicho la
ndani kabisaalikuwa akidadisi kitu na Neema aligundua hilo.
"hapana, hii ipo kila mahali, fikiria hata Papa ameruhusu
turudi na shughuli za kanisa zimesitishwa sasa hivi huko Roma, kwa hapa
Tanzania hii hatua imechelewa lakini nashukuru kuna jitihada za kuzuia huu
ugonjwa," alisema Neema kisomi akajibu.
"Aisee Mungu atunusuru," alisema Meneja.
"Ni mitihani tu na tutaushinda, Mungu daima ni mwema,"
"hivi samahani, ulifikia chumba gani? nataka nihakikishe unapata huduma
zote stahiki," aliamua kusema Meneja akifungua kile kitabu cha register ya
wageni.
Neema akakenua meno maana alikuwa ameshalijua hili kabla,
akasema sasa ule uongo kuwa eti kutokana na ndege yake kughairishwa mara kadhaa
akafanyiwa booking na dereva wa parokia ambaye ndiye Cliff, loh meneja akaomba
hata Cliff pia apimwe haraka na kuheshimiwa.
Na ndiyo hapo sasa Neema akafanya kumpelemba meneja aweze
kufanya iwezekanavyo apate kuondoka hotelini hapo siku hiyohiyo.
"Dah sista hapa kutoka ni ngumu, mwambie tu askofu
atakuelewa maana hata mimi mwenyewe nipo kwenye lockdown sitakiwi kuondoka na
wenye mamlaka ni mkuu wa mkoa na askari wake. Nakupa siri tu hapa mpaka sasa
kuna wagonjwa watatu wamegundulika na sisi wengine tunaweza kuwa tumeambukizwa
kifo njenje sista," alisema Meneja akihamisha macho yake kutoka kwa Neema
hadi kwa Cliff kisha akauliza.
"sasa braza jana usiku ulivyomleta sista kutokea airport
ulilala wapi? si ungetuambia tungekupa chumba kingine?"
Swali hilo lilikuwa kama vile mwiba kwa Cliff akashtuka
akamtazama Neema huku kichwa chake kikiwaza kwa haraka mno.
"Nililala kwenye gari yangu maana ratiba zilionesha leo
mchana tutaondoka kuelekea parokiani," alijibu Cliff akiunganisha uongo
wake vizuri. Sista Anne ama Neema kama tumjuavyo akapumua taratibu chinichini
maana alizuia hofu yake asiheme kwa muda;lakini wakati huo yule meneja alikuwa
akipekuwa kiregister na kumuita pembeni Cliff.
"Niliambiwa na wahudumu wangu kuwa ulipanga hapa tangu
majuzi na ulikuwa na binti fulani mkilala mle ndani kabla ya sista kuja; kwa
sababu wewe ni mfanyakazi wa kanisa ninakukaushia sijamwambia sista uovu wako
na jambo baya kabisa ilibidi hadi huyo msichana awepo hapa leo karantini,"
alisema meneja akikenua meno yake hadi mwisho.
Japokuwa Cliff alichukia lakini akazuga kujifanya anashukuru
sana kwa meneja kumfichia siri yake na akacheka kimoyomoyo kuwa laiti kama meneja
angefahamu kuwa huyo msichana anayemzungumzia ndiyo sista Anne sijui
angefanyaje.
"Niliteleza tu meneja si unajua tena, sisi wote
wanaume," alisema kwa aibu Cliff. Meneja akacheka na pamoja wakacheka kwa
kuviziana.
"Sasa leo jioni nitafute nitakupa chumba kingine,"
alisema meneja na Cliff akashukuru. Meneja akaondoka zake kuelekea na majukumu
yake na Cliff akarudi kwa Neema kijasho kikimtiririka.
"Alikuwa anasemaje?" aliuliza Neema kwa sauti ya
wasiwasi ya chinichini huku akilinda haiba yake ya usista isiharibike.
Cliff akajitia naye kuwa na adabu akamhadithia sista Anne
alivyoulizwa na meneja na namna alivyotumia akili kujibu maswali yake.
"Dah! hili limeisha,pia nitamdanganya baba nilifika hapa
jana na kuzuiwa karantini; kwangu nitakuwa nimemaliza cha msingi tusubiri tu
hizo siku kumi na tano za karantini," alisema Neema tabasamu likianza
kumrejea.
"So..!?"" aliuliza Cliff akiulizia mpango wa
kupata punino la Neema maana aliona kama kutenganishwa chumba na Neema ndiyo
kunamkosesha masijala.
"we Cliff hebu kuwa na adabu kwanza bado tu unataka?"
"ndiyo.." alilalamika Cliff.
"tutaona itakuwaje, hebu kwanza tutulie tusikilize
utaratibu," alisema Neema ikawa kwa vazi lake la kitawa Cliff mwenyewe
akaona haya kuendelea kubembeleza zaidi.
Basi baada ya kupimwa pale, ikatangazwa wagonjwa wenye corona ni
wanne, na waliokuwa wanatiliwa mashaka kwakuwa walikuwa karibu na wagonjwa hao
ni watu kumi; wakati huo wengine wakatakiwa kuendelea kubakia kwa siku kumi na
tano zilezile.
hofu sasa ikazuka kwa kila mtu kuwa hatihati ya kifo ilikuwa
ikiwakabili lakini si kwa Cliff wala Neema. Wakaelekezwa jinsi ya kuziba nyuso
zao na kusalimiana, wakaelekezwa jinsi ya kunawa kwa sanitizer na kutakiwa
kubakia kwenye vyumba vyao wakiwasiliana na ndugu na jamaa zao kuwatoa
wasiwasi.
Wakarudi mavyumbani mwao, wakati huo hoteli nzima ikawa
inapuliziwa madawa ili kuondoa virusi watakaokuwa wamezagaa sehemu mbalimbali
bila kujulikana.
Mbaya zaidi Cliff akapatiwa chumba magharibi kabisa mwa hoteli,
Neema akawa mashariki kabisa. huku agizo la kila mtu kubakia chumbani kwake
likitangazwa na askari wakilinda korido na varanda; asitoke mtu. ubaya wa
tangazo hilo aliyekuwa singo alibakia singo chumbani mwake asitoke, aliyekuwa
na mtu wake akatakiwa kujifungia na mtu wake hivyohivyo; Loh Cliff na Neema
wakagundua japokuwa kujidhihirisha utawa kwa Neema kulisaidia kuondoa wasiwasi
wa kushtukiwa kwa Neema lakini iliharibu mpango wao wa kuwa pamoja doh!
Cliff akapiga ukuta kwa hasira akiwaza ni siku kumi na tano
mbele hadi waonane na Neema tena, kwa hiyo kwa mara nyingine anakosa penzi loh!
ghafla wakati akiwaza hivyo simu yake iliita, ni mpenzi wake
polisi Grace kwa hasira akashindwa kupokea, lakini ikaingia meseji.
"sorry dia, nakukumbusha kesho kutwa ndiyo ile birthday
yangu, nimeshaandaa kila kitu, miss you!" i
lOh! hiyo meseji ikamshtua Cliff ilionekana alikua bize mno na
kuwaza penzi la Neema kiasi kwamba akasahau kabisa kuhusu ya demu wake, huyo
Afisa wa jeshi la polisi Mwanza.
Kwa taarifa yako gari,utanashati na fedha alizokuwa nazo Cliff
jeuri yote ilitoka kwa Grace, na ndiyo eti asionekane Marioo kwenye familia ya
Grace akapachikwa kwa muda kwenye kiofisi cha bima hapo Arusha kwa koneksheni
ya Grace pasina mshahara. Maana yake hata akitambulishwa kwenye familia ya Grace
apate kuonekana ana kazi fulani kwasababu Grace kwao kuanzia bibi yake mpaka
marehemu babu yake ni wanausalama tu, huyu kikosi cha magereza, yule afisa
jeshi la kujenga Taifa na hata asiye na kazi kwao alikuwa ni afisa wa jeshi la
zima moto.
Kwa tafsiri hiyo kwao ni watu wakubwa tu na baba yake sasa ndiye
huyo Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, RPC Harlod Mabula; mtu mwenye
manyota na wadhifa naye akamfanya hata mwanaye katika umri wake mdogo wa miaka
26 tayari alikuwa afisa.
Kusema za kweli sio kwamba Grace ni mzuri, hapana ila
ukichanganya na fedha zake na cheo chake hata kama sio mweupe ataonekana
mweupe; hata kama hana tako, tako litaonekana tu na atavumilika; huo ndiyo
msimamo wa wanaume na ndio uliomfanya Grace akawa kipusa kwa Cliff.
Sasa nikupe tu siri msomaji wangu, ni kwamba huyo CLiff alikuwa
ameshajipenyeza kwenye familia ya mzee Harlod na alikuwa ameshatambulishwa kwa
mama yake Grace, lakini rasmi kabisa utambulisho wa Cliff kwa familia nzima
ulipaswa kuwa ni hiyo siku ya tarehe 10 ambayo ndiyo birthday ya Grace,
waliyopanga kupeleka posa na Mungu akibariki wavalishane pete hapohapo
ukumbini.
kwahiyo basi meseji ya Grace kumkumbusha Cliff ilikuwa na maana
kwamba kila kitu kwa upande wake kulikuwa shwari ni yeye tu kwenda ukumbini na
pete yake.
Cliff akaisoma ile meseji na kutetemeka hadi utumbo, akapata
homa yabisi mifupa ikamkakamaa. Akawaza cha kufanya. Akaona asikurupuke kujibu
ile meseji; akashusha pumzi na kufumba kope zake alipofumbua macho akasogea
kwenye droo akachukua notebook mpya aliyoiona juu ya meza ikiwa na peni;
nadhani kila chumba cha hoteli hiyo kilikuwa na hizo notebook.
ITAENDELEA

0 Comments